UCHAMBUZI WA TAMTHILIYA-MORANI
UHAKIKI WA TAMTHILIYA
TAMTHILIYA: MORANI
MWANDISHI : E. MBOGO
WACHAPISHAJI : DUP
MWAKA : 1993
UTANGULIZI
Morani ni tamthiliya inayoelezea juu ya matatizo yaliyoikumba nchi yetu mwaka
1980 na kusababisha hali ngumu ya uchumi kwa tabaka la chini.Matatizo haya ni
kama uhujumu uchumi, wizi wa mali ya umma, ulanguzi, rushwa na kukosekana kwa haki,
unafiki wa viongozi wetu, matabaka,n.k.Mwandishi wa tamthiliya hii, E.Mbogo
anaonesha kuwa, kukithiri huko kunakwamisha maendeleo hapa nchini.
MAUDHUI
Dhamira Kuu: Ujenzi wa
jamii mpya
Ujenzi wa jamii mpya ndiyo
dhamira kuu ya tamthiliya hii ya Morani.
Katika kujadili dhamira hii mwandishi anapendekeza kuwa jamii mpya itakayojengwa
iwe jamii inayopinga aina yoyote ya unyonyaji,ukoloni mamboleo pamoja na wahujumu
uchumi wa nchi, msanii anasema,
‘’ Tuandike risala itakayoamsha chuki dhidi ya ubeberu, ukoloni mamboleo,
risala yenye mishale ya sumu.Sumu itakayounguza maini na mapafu ya wahujumu
uchumi,mabepari uchwara na vibaraka popote walipo’’ (uk 41)
Msanii
anaonesha wazi nia yake ya kupinga unyonyaji na uhujumu katika jamii
itakayojengwa ili kuleta haki na usawa kwa kila mtu.Vile vile msanii
anapendekeza kuwa, katika jamii hiyo mpya,lazima njia kuu za kuzalisha mali
zimilikiwe na umma.Msanii anasema,
‘’ Tena risala hii iwakumbushe wananchi sherehe za harusi – matanga :
sherehe za kutaifisha viwanda,mabenki,majumba,mashamba,hospitali na maduka kila
kitu mali ya umma’’ (uk 4)
Hapa msanii anakumbusha
kuwa ili umma umiliki njia hizi ni lazima zitaifishwe toka kwa watu binafsi na
ziwekwe mikononi mwa umma ambapo zitatumika kwa faida ya umma.Katika kujadili
dhamira hii, mwandishi anaona kuwa ili tujenge jamii mpya ni lazima jamii iungane
kuwa kitu kimoja, kwani umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu, msanii anasema,
‘’Risala itoe mwito kwa
Morani wote,Morani waungane ili kuendeleza safari ya kuitafutanguzo ya uswezi’’
(uk 41)
Pili,msanii anaonesha
kuwa, ili tujenge jamii lazima tujitoe mhanga,Tuwe na ujasiri na ushujaa ili
tusiogope upinzani wa watu wanaonyonya.Vile vile msanii anawahimiza wanajamii
kushika silaha ili kuweza kujenga jamii mpya. Hivyo anasema,
‘’Enyi Morani nyakueni
sime na ngao ili kulitetea dongo’’ (uk 44)
Dongo na Jalia ni mfano
mzuri wa watu waliojitoa mhanga kupigania ujenzi wa jamii mpya. Hawa hawajali
upinzani wa aina yoyote wakisaidiwa na Mapoto,Malongo na Hadikwa. Hawa wapo
mstari wa mbele katika ujenzi wa jamii mpya ambayo itafutilia mbali ukoloni
mamboleo na aina zote za unyonyaji (uk 40-42)
Vile vile msanii
anatahadharisha kuwa katika ujenzi wa jamii mpya kuna wasiliti wasiopenda
mafanikio ya umma. Yusufu na Mlemeta ni mfano wa waliopewa jukumu la kuliongoza
gurudumu la ujenzi wa jamii mpya, lakini kutokana na ubinafsi pamoja na
kushirikiana na wahujumu,wanakwamisha zoezi zima la ujenzi wa jamii mpya
(sehemu ya pili, tatu na nne).
MBINU
ZA UJENZI WA JAMII MPYA
1.
KUPIGA VITA UHUJUMU UCHUMI
WA NCHI
Msanii anaonesha kuwa uhujumu uchumi ni kikwazo cha
ujenzi wa jamii mpya.Katika tamthiliya hii,msanii anaonesha kuwa
wafanyabiashara wengine pamoja na viongozi wa juu ndio wahujumu uchumi wakubwa,
kwani wanavusha mazao kwenda nchi za
nje. Nungunungu ni mfano wa watu matajiri wahujumu uchumi wanchi.Msanii anasema,
‘’ Ufahamu kuwa Nungunungu anavusha kahawa na
karafuu katika nchi ya jirani kwa
magendo?Husemi? Sawa! Mlemeta unajua kuwa Nungunungu ana hoteli kubwa Marekani?
Ana akaunti ya fedha Uswisi, Eee’’ (uk 12)
Msanii anaonesha kuwa vitendo kama hivyo vinalikosesha taifa kupata
fedha ambazo zingetumika kuendeleza nchi na badala yake pesa hizo zinaingia
mikononi mwa watu binafsi kwa faida yao binafsi.Kana kwamba haitoshi ,Nungunungu
pia anaingilia kuvusha madini nje kwa magendo kama anavyosema jalia;
‘’Ninyi ndio mnaotuvurugia nchi,Mbona husemi chochote kuhusu kahawa na
Tanzanite mnazovusha nje kwa magendo? Mbona husemi lolote kuhusu madola yenu
mnayolundika ughaibuni? Hata ufunike
mavi kwa bakuli haitakusaidia kitu’’ (uk 29)
Msanii anaonesha kuwa uhujumu uchumi unakwamisha maendeleo na watu wanaohujumu ni watu wa juu wala sio wa
chini,msanii asema;‘’Katikati hakuna wahujumu, wahujumu wako juu’’ (uk 13)
Katika harakati za kutokomeza uhujumu uchumi
unakwamisha maendeleo, na watu wanaohujumu ni watu wa juu wala sio wa chini,
msanii asema;
‘’ Hatuwezi kuacha mapapa tukavuna pelege’’ (uk 13)
Hapa mapapa huwakilisha watu wa tabaka la juu
wanaohujumu uchumi wanchi ambao huvusha mazao nchi za jirani.Wana akaunti,mahoteli
nchi za nje na kulikosesha taifa pesa na Pelege ni watu wa kawaida wanaohujumu
uchumi wanchi. Hivyo msanii anapendekeza kuwa vita dhidi ya wahujumu uchumi
lazima vianze kwa mapapa na sio pelege.
Uhujumu uchumi,magendo na ulanguzi
vinapokithiri katika nchi husababisha
uadimu wa bidhaa muhimu.Bidhaa zinapoadimika zile chache zinazopatikana
huwa ghali sana kiasi kwamba,watu wa tabaka la chini hushindwa kuzinunua na
kubaki kuwa za watu wa juu tu.Msanii anasema;
‘’Vitu vimepanda bei
chumvi,mchele,sukari,unga kila kitu.Ninyi tu mnaolalia magodoro ya manoti ndio
mnaozimudu hizo bei,makabwela na watoto wao wakale wapi? (uk 29)
Hapo msanii anaonesha hali halisi iliyopo kwenye jamii;
wakati wengine wanalalia manoti ya fedha watu wa chini wanashindwa hata pesa ya
kununulia chumvi kwa sababu ya bei yake kuwa juu.Hii inasababisha hali ngumu ya
maisha kwa tabaka la chini.Hivyo kujaa vitu madukani hakusaidii lolote kutatua
shida za maskini.Kwani vitu vinauzwa kwa bei ghali kiasi kwamba wanakosa hela
ya kununulia.
Msanii anasema;
‘’Tena risala hii ieleze jinsi maisha yalivyo magumu kwa watu wa chini,ieleze
jinsi maduka yalivyojaa vitu, vitu vyenye bei ya kutisha makabwela na watoto wao
wakiendelea kuandamwa na utapiamlo.’’(uk 41)
Pia msanii anasema fedha kidogo zinazopatikana badala
ya kuendeleza uchumi zinatumika kununua vitu vya anasa ili kuwanufaisha wenye
hela kama Nungunungu (uk 41)
Msanii anaeleza kwa masikitiko makubwa kuwa nchi yetu
ni tajiri, lakini ni kutokana na kuhujumiwa na wachache ndiyo maana uchumi wetu
uko chini ukilinganisha na nchi nyingine.Msanii anasema;
‘’Tena risala hii ieleze jinsi nchi ilivyotajiri, ardhi tele, maji,
maziwa, mamilioni ya ng’ombe, mbuzi, kondoo, samaki na kwamba kusingizia hali
ya hewa na opeki ni uzandiki-dhambi nyekundu pyu isiyofutika wala kusameheka’’
(uk 42)
Hivyo msanii anasema, ilikujenga jamii mpya ni lazima
tupige vita wahujumu uchumi wanchi.Kwa upande mwingine vita iliyoanzishwa dhidi
ya uhujumu uchumi ilionekana kama ni kuwaonea wahujumu uchumi hao. Wao
walifikiri vita hii imeanzishwa na wachache wenye wivu dhidi yao. Nungunungu
mmoja wa wenye mawazo hayo anasema;
‘’Hii kampeni mmeivaa kama koti la kutungua. Akina Fulani
wachache wameibua hii vurugu isiyokuwa na mbele wala nyuma’’ (uk 29)
Kwa upande wa wahujumu uchumi wao wanaona hizi kampeni
kama vurugu za kuwavurugia maslahi yao kama anavyosema Nungunungu;
‘’Ukifungua duka unaambiwa hujuma, mtu akinunua lori hujuma?,Ukijenga
kajumba ka ghorofa moja hujuma, ukiweka vielfu vichache benki hujuma.Baadae mtasema
mtu akioa wake wawili au watatu pia ni hujuma? Uyai huo? Mnataka kutuvurugia
nchi’’ (uk 29)
Mawazo kama haya anayosema Nungunungu ni potofu, kwani
haelezi waziwazi hizo pesa kapata wapi, labda kama tungekubaliana naye. Katika Morani msanii anasema ili tujenge jamii
mpya lazima tupige vita wahujumu,kwani wanakwamisha zoezi hilo.
2. KUPIGA VITA UNAFIKI NA
USALITI
Unafiki ni hali ya mtu kutokuwa
mkweli au hali ya kujifanya mkweli huku sivyo.Katika Morani msanii anasema wazi kuwa zoezi la kupiga vita uhujumu uchumi
nchini lilikwama kutokana na wasimamizi kuwa wanafiki.Yusufu na Mlemeta ni
mfano wa watu wanaowakilisha suala hili.Hii ni kwasababu walinunuliwa na
Nungunungu kama asemavyo Jalia:
‘’ Mlemeta kama wewe umenunuliwa siyo
mimi’’ (uk 13).
Kutokana na kununuliwa huko wanashindwa kumuweka
Nungunungu kwenye orodha ya wahujumu uchumi na hivyo kukwamisha zoezi zima.
Licha ya hiyo Yusufu na Mlemeta wako mstari wa mbele kutetea hujuma.Wanawazuia
askari ili wasimkamate Nungunungu.Mlemeta
anasema;
‘’Na wewe mzee umeponea chupuchupu kama
tusingetumia mbinu ya kuzuia askari wa Jalia, basi sa hii tungekuwa
tunazungumza hadithi nyingine’’ (uk 23).
Wakati wahujumu wengi wamekamatwa na mali zao
kufilisiwa, Nungunungu analindwa na watekelezaji wa kampeni hiyo. Kana kwamba
hiyo haitoshi,Mlemeta na Yusufu wamepewa jukumu la kumtafutia Nungunungu wakili
pindi akamatwapo,kama msanii asemavyo;
Nungunungu: ‘’ Itabidi mwende
mkamuone…..advocate mpange kila kitu tayari. Lazima ahakikishe nikiwekwa ndani,
nishinde kesi’’.
Mlemeta: Sawa mzee’’ (uk 24).
Kutokana na Yusufu na Mlemeta kutetea hujuma,
wanakwamisha zoezi la ujenzi kwa jamii mpya na ili tujenge jamii mpya lazima
tuwaondoe watu kama hao. Msanii hakuishia hapo tu, anasema pia utaona
wanaopinga maendeleao ya nchi ndio kwanza wanapandishwa vyeo na kuwa mabalozi
Uchina, na kuwa mkuu wa jimbo. Hapo msanii anakejeli tabia za nchi yetu ya
kuwapandisha madarakani watenda maovu na kuacha wale watimizao vema wajibu wao. (uk 37).
3.
KUPIGA VITA MATABAKA
Ni hali kuishi
kutokana na kipato,cheo n.k. Msanii ameonesha matabaka ya aina mbili. Kwanza,kuna
tabaka la juu yaani la wenye pesa.Tabaka hili humiliki njia kuu za
uzalishaji mali, vyombo vya dola, ili kulinda maslahi yao kama vile; pesa na vitega uchumi nchi za nje
(uk 12). Pia tabaka hili hupata hudumu muhimu kama matibabu bila matatizo
yoyote (uk 38). Msanii anaonesha kuwa tabaka hili pia hupendelewa kwenye sheria
pindi wapelekwapo.Kwa kuelezea kesi ya Nungunungu msanii anadhihirisha hayo;
‘’Basi unajua yule Jaji alifungua mbuku wake
mweusi wa sheria akasoma ….kamati na mahakama imechunguza na kuona kuwa hakuna
ushahidi wowote kuwa ndugu Nungunungu amejihusisha na biashara haramu. Mahakama
inaridhika na bila mashaka kuwa ushahidi uliotolewa dhidi ya Nungunungu ni
majungu matupu yenye nia ya kumpaka matope. Hivyo mahakama inamwachilia Nungunungu
huru’’ (uk 34)
Kwa upande mwingine tabaka hili wapo mstari wa mbele
kufanya biashara haramu inayohujumu uchumi wetu.Tabaka la pili ni la chini,
kwanza maisha yao ni duni ukilinganisha na tabaka la juu (uk 41).Hufanyishwa
kazi ngumu na tabaka la juu yaani mizuke (uk 2) na pia hunyanyaswa na vyombo
vya sharia kama vile mahakama ukilinganisha na tabaka la juu.Msanii anasema;
‘’Juzi juzi kasimama msulupwete,yule mbele ya mahakama.Hakimu
wala hakujisumbua kufungua ule mbuku wake wa sharia.Hakupoteza muda.Hakupoteza
muda. Aliegesha miwani yake katika ncha ya pua jicho kali la hakimu lilimtambaa
kabwela toka vidoleni hadi utosini.Mvua saba, kazi ngumu!....Mvua saba!!
Muhujumu uchumi mkubwa!Eti kakutwa nyumbani kwake na tenga mbili za kisamvu na
dawa tatu za kolgeti.Dawa tu za mswaki.Maskini haokoti,akiokota – mwizi’’ (uk
35)
Msanii
anaonesha jinsi vyombo vya sheria vinavyowatendea watu wa tabaka la chini
kutokana na kutokuwa na sauti yoyote katika jamii. Tabaka hili linanyonywa, kunyanyaswa,kuonewa
na kugandamizwa.Ili tujenge jamii mpya lazima tuondoe
matabaka haya katika jamii zetu.
4. KUJITOA MHANGA
Msanii anaonesha kuwa,ili tujenge jamii mpya ni lazima
tujitoe mhanga katika kuondoa unyonyaji na uonevu wa kila
aina.Dongo,Jalia,Mapoto,Malongo na Hadikwa ni mfano mzuri wa wahusika waliopo
mbele katika kupiga vita hujuma.Mzee,Malongo na Mapoto walijitoa mhanga kwa
safari ya mbali kufuata nguzo ya uswezi,ingawa safari yao ilikuwa ya shida sana
lakini hawakukata tamaa (uk 7-8).
Pia Jalia alionesha ujasiri bila woga kwenda kwa Nungunungu
kumpiga (uk 28-30) na kuongoza harakati za kupiga vita hujuma (uk 40-45).Pia
aliwakemea Yusufu na Mlemeta kuwa wamenunuliwa na Nungunungu bila woga,hata
walipotaka kumpiga,alimpiga Yusufu na wala hakujali lolote (uk 12-14)
Kwa upande mwingine, tunamwona Dongo akipambana na
wahujumu uchumi ili kuwaendeleza na
kuwasaidia wanyonywaji bila kuogopa kitu chochote.Na ni kutokana na msimamo
wake wa kutoteteleka anauwawa na wahujumu (uk 43-45).
Ili tujenge jamii mpya ni lazima tuwe na ujasiri na
ushujaa kwani bila ya vitu hivi hatuwezi kujenga jamii mpya.
5. KUWA NA UMOJA NA
MSHIKAMANO
Msanii anaonesha kuwa, ili tujenge jamii mpya lazima
tuwe na umoja kwani umoja ninguvu na utengano ni udhaifu.Msanii anawahimiza wana
Morani waungane ili waweze kupiga vita hujuma nchini. Msanii anasema;
‘’ Morani waungane na umma.Waungane
kuiendeleza kutafuta nguzo za uswezi’’ (uk 41)
Pia katika kauli mbalimbali za Dongo naye anawahimiza
wana Morani ili kupiga vita hujuma.Ni kutokana na utengano uliokuwepo katika
jamii ndio maana zoezi la kupiga vita wahujumu lilishindwa na matokeo yake
kushindwa kujenga jamii mpya.
Mfano mzuri tunauona kupitia Yusufu na Mlemeta
waliokuwa viongozi wa kusimamia zoezi hili walitofautiana na wenzao kwa ajilia
ya ubinafsi,hivyo zoezi zima likakosa mshikamano miongoni mwa watekelezaji (uk
8-25).Msanii anapendekeza kuwa ili tujenge jamii mpya lazima umoja na
mshikamano viwepo,kwani bila hivyo hatuwezi kufanikisha zoezi hilo.
6.
NAFASI YA MWANAMKE KATIKA
JAMII
Msanii amemchora mwanamke katika sura mbalimbali kama ifutavyo:,
kwanza kama mwanamapinduzi aliyeko mstari wa
mbele katika kupiga vita hujumu. Jalia ni mfano wa mwanamke mwanamapinduzi katika
kutokomeza hujuma akishirikiana na Dongo, Mapoto, Malongo na Hadikwa (uk
39-42).
Pili
kama jasiri,jalia aliwambia waziwazi kina Mlemeta na Yusufu kuwa, wamenunuliwa na Nungunungu ndio maana
wakawa wanakwamisha zoezi zima la kuwakamata wahujumu (uk 13-18).
Pia Jalia ndiye aliongoza kikosi cha kwenda kumkamata
Nungunungualiyeogopwa na watu wote kwa ajili ya umaarufu wake.Licha ya
kumkamata alimwambia wazi madhambi yake aliyoyafanya (uk 28-30). Kama hiyo haitoshi
Jalia alimpiga Nungunungu bila kuogopa vitisho vyake atoavyo kwa wengine tena
bila wasiwasi (uk 38). Katika kuandaa mipango ya kupinga hujuma,Jalia alifanya
kazi bega kwa bega na akina Mapoto bila kujali vitisho alivyopewa na Nungunungu
(uk 40). Kwa upande mwingine mwanamke amechorwa kama chombo cha kustarehesha
wanaume. Rejea Aisha alivyomstarehesha Nungunungu (uk 26-27).
7.
UZURUFU
Katika tamthiliya hii
msanii ameonesha jinsi wazee wanavyofanya
mapenzi na watoto wadogo.Mfano mmoja wapo ni Nungunungu ambaye anafanya mapenzi
na Aisha ambaye ni mwanafunzi.Kutokana na hali hiyo,Aisha anasahau hata kwenda
shule na matokeo yake anafukuzwa shule.Msanii
anasema (uk 26);
Nungu: Nini Aisha!!!
Aisha: Wamenifukuza shule
Nungu: (Anagutuka) Ee! Umefanya nini?
Aisha: Nakueleza mie!
Kitendo cha watu wazima kufanya mapenzi na watoto wa
shule kina madhara yake kwa jamii kama tulivyooneshwa hapo juu, mtoto anaweza
kufukuzwa shule au anaweza kupata mimba au magonjwa ya zinaa.
Aisha alifukuzwa shule kwa sababu hakwenda siku
nyingi; na hakwenda shule kwa sababu ya starehe alizokuwa anapewa na Nungunungu
usiku kucha. Msanii anasema (uk 26);
Aisha: Siku nyingi sijaenda shule mie
mwezi.Walimu wamemletea barua mzee. Wamenifuta….utanisamehe mpenzi Nungu.
Nungu: (Anamsukuma) mpumbavu mkubwa. Hutaki
shule halafu unakuja kunililia mimi? Mpumbavu mkubwa?
Aisha:Mpumbavu! Mpumbavu mimi? Mimi
mpumbavu?Siku zote narudi saa nne usiku nyumbani baada ya hekaheka za
night-club mimi na wewe. Ulitegemea nini?Ee?
Matukio kama haya yapo katika
jamii yetu. Akina Nungunungu wako wengi na akina Aisha nao wapo wengi. Jambo la
muhimu ni kupiga vita vitendo kama hivyo.Vitendo vya kurubuni watoto wa shule
kwa hela zao nyingi halafu wanawaharibia maisha yao ya baadaye,ni kinyume na
maadili ya jamii.Nungunungu alimfundisha Aisha umalaya, ulevi na kuvuta sigara
kitu ambacho ni kinyume na maadili ya jamii.Waswahilii husema mshika
mawili mmoja humponyoka,na ukweli Aisha alifukuzwa shule,kwani
aliendekeza starehe.Starehe hizo zikamfanya asahau shule na matokeo yake
alifukuzwa shule.
MIGOGORO
v Mgogoro wa wahujumu uchumi
na wale wapiga vita wahujumuuchumi.
v Mgogoro kati ya Jalia na
Mlemeta pamoja na Yusufu.
v Mgogoro kati ya Malongo na
Yusufu kwenye baa.
v Mgogoro kati ya Jalia na
Nungunungu.
v Mgogoro kati ya Aisha na
Nungunungu.
UJUMBE
Ø Hujuma,unafiki na kuwepo
kwa matabaka katika jamii ni kikwazo cha ujenzi wa jamii mpya.
Ø Umoja na mshikamano,
ujasiri na ushujaa na kujitolea mhanga
ni mbinu za kujenga jamii mpya.
Ø Kikulacho ki-nguoni mwako,
yule anayekwamisha maendeleo ya nchi ni mwananchi mwenyewe – Nungunungu,
Mlemeta na Yusufu.
Ø Kupiga vita ukoloni,ukoloni
mamboleo na aina yoyote ile ya unyonyaji ni mbinu muhimu za ujenzi wa jamii
mpya.
FALSAFA
Msanii anaamini kuwa wahujumu uchumi wetu ndio wanaokwamisha
ujenzi wa jamii mpya.Msanii anasema lazima tuwaondoe wahujumu hao,tupige vita
aina zote za unyonyaji.
MSIMAMO
Msimamo wa msanii ni wa kimapinduzi,kwani ameonesha
waziwazi matatizo yanayoikabili jamii yetu na kuonesha kuwa matatizo haya ni
pamoja na hujuma,unafiki, rushwa,matabaka na kupeana kazi kwa kujuana (uk 27).
FANI
MUUNDO
Mwandishi ametumia muundo wa moja kwa moja.Mchezo
unaanza kuonesha kifo cha Dongo na utata uliojitokeza kwa wananchi juu ya kifo
chake,Mchezo unaendelea kwa kueleza vita dhidi ya wahujumu uchumi na matokeo
yake.Mchezo umegawanyika katika sehemu nne.
MTINDO
Msanii ametumia dayolojia ilivyo kawaida kwa
tamthiliya – maelezo ya majibizano baina ya wahusika. Pia msanii ametumia nafsi
zote tatu (yaani I, II, III)
Pia msanii ametumia nyimbo katika mchezo huu (uk 42).
MATUMIZI YA LUGHA
Lugha aliyotumia msanii ni ya kawaida inaeleweka na
imejaa misemo,methali, tamathali za semi na mbinu nyingine za kisanaa.
MISEMO / NAHAU
v Ndumi la kuwili (uk 13)
v Anatuchomea utambi ( uk
15).
v Paka shume (uk 17).
v Kuwapaka watu matope (uk
29).
v Umeota meno jana (uk 8).
METHALI
v Penye nia pana njia na
subira yavuta heri (uk 4)
v Siri ya kaburi aijua maiti
na siri ya maiti aijua kaburi
v Fimbo ya mbali haiuwi
nyoka (uk 23)
v Mfuga punda fadhila
hukujambia mashuzi (uk 23)
v Mwosha huoshwa (uk 24)
v Bandu bandu unataka
kumaliza gogo? (uk 31)
v Usimsifu sana lasivyo
tembo atalitia maji (uk 23)
v Mwenzako akinyolewa wewe
tia maji (uk 23)
TAMATHALI ZA SEMI
TASHIBIHA
v Kesho tutawasambaza kama
punje za mtama.
v Nungunungu na Mlemeta ni
kama kupe na mkia wa ng’ombe.
v Watu wengi kama sisimizi
(uk 39).
v Hii kampeni mmevaa tu kama
koti la kutungua (uk 29).
TASHIHISI
v Jicho kali la hakimu
lilimtambaa Kabwela Yule toka vidoleni hadi utosini.
v Jua lilipo tabasamu na
kutandaza mbawa zake.
TAFSIDA
v Nikakumbatie blanketi
mwenyewe? (uk 27)
v Tutaenda umana au
wasiwasi? (uk 27).
MBINU NYINGINE ZA KISANAA
TANAKALI SAUTI
v Uuuuu!Uuuuuu!Dongo! Dongo
jamaa.............(uk 1)
v
TAKRIRI
v Mpumbavu mimi? Mimi mpumbavu? (UK 26).
v Nimekosa nimekosa niseme
hivi niseme (uk 22).
v Mnachuja, mnachuja
mnachuja hadi lini? Mlemeta.
MDOKEZO
v Hallo bado tunaendelea na
kazi .......mambo magumu mzee.....lakini nadhani tutayamudu......yaa saa
ngapi.....sawa (uk 15)
v Lakini mzee.........(uk
18).
PICHA /TASWIRA
Msanii pia katumia lugha ya picha (uk 2), kuna picha ya
mizuka inayolima shamba la tajiri – hiyo huwakilisha tabaka la wanyonge,watu
wanaofanya kazi kubwa kwa kuwatajirisha matajiri wakati wao wenyewe
wananyonywa.
Pili,kuna nguzo ya uswezi hii inaashiria mali za azimio la Arusha.Dongo
anaashiria wanamapinduzi wanaotaka kuleta mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na
utamaduni.Mti uliokuwa karibu na ofisi pamoja na wachawi hizi zote mbili
huashiria wahujumu uchumi wetu.
Morani inaashiria vijana wanaotakiwa kuungana ili kuleta
mabadiliko katika jamii.
WAHUSIKA
1.
DONGO
v Huyu ni mhusika mkuu wa
tamthiliya hii anayepambana na hujuma ili kuwaendeleza na kuwasaidia wanyonge.
v Dongo alikuwa mstari wa
mbele katika kupiga vita hujuma akisaidiwa na
Mapoto, Jalia, Malongo, Hadikwa. Dongo ni mfano wa viongozi
wanamapinduzi anayefaa kuigwa na jamii.
2.
JALIA
v Ni mhusika mwanamke
aliyejitoa mhanga kuongoza kampeni ya kutokomeza hujuma.
v Jalia aliongoza askari
kumkamata Nungunungu bila woga.
v Pia katika maandalizi ya
maandamano Jalia alishirikiana na
Mapoto, Malongo na Hadikwa katika kufanikisha maandamano hayo.
v Vilevile alimpiga Yusufu na Nungunungu bila woga wala
wasiwasi. Hivyo Jalia ni mwanamke anayefaa kuigwa na jamii kutokana na matendo
yake.
3. MAPOTO NA MALONGO
Hawa ni wahusika wadogo wa tamthiliya hii.
v Hawa wako pia mstari wa
mbele kupiga vita rushwa, ukoloni, ubepari na hujuma
v Walishitikiana bega kwa
bega na Jalia katika vita hiyo.
v Ni mfano mzuri wa kuigwa na watu katika jamii
yetu.
4. NUNGUNUNGU
v Huyu anawakilisha wahujumu
uchumi.
v Alikuwa anavusha kahawa na
karafuu nchi za nje kwa magendo.
v Ana hoteli Marekani na akaunti Uswisi.
v Ni mfano wa watu
wanaolikosesha taifa letu fedha za kigeni kwa kufanya magendo yao, na ni mfano
wa mtu mbaya asiyehitajika kuigwa na yeyote.
5. YUSUFU NA MLEMETA
v Hawa ni viongozi wanafiki
walioko mstari wa mbele katika kukwamisha shughuli zote za maendeleo.
v Wanashirikiana na Nungunungu kuihujumu nchi
yetu.
v Wakati wa kampeni za kutokomeza
hujuma, walileta wahujumu mfano Nungunungu,hivyo hawafai kuigwa na jamii.
Ø Wahusika wengine ni Mzee, Aisha, Dala
Bongi, Okashi n.k.
MANDHARI
Mandhari yake ni ya Kitanzania kutokana na matukio
yanayoelezwa katika tamthiliya hii, yalijitokeza wazi katika jamii yetu ya
Kitanzania.Matukio haya ni kama vile hali ngumu ya maisha,hujuma na vita dhidi
yake.Matukio haya ndiyo yaliyotawala Tanzania kuanzia miaka ya 1980 na kuendelea.Vile
vile kuna mandhari ya nyumbani, ofisini,
porini, baa, kumbi za tarehe, mitaani, hospitalini, n.k.
JINA LA KITABU
Kwa ujumla jina
la kitabulinasadifu yale yaliyomo ndani ya kitabu,msanii anatoa wito kwa vijana
– Morani ili waweze kuungana na umma katika kupiga vita hujuma nchini.
KUFAULU KWA MWANDISHI
Mwandishi amefaulu kwa
kiasi kikubwa kwa kuionesha jamiiyetu matatizo yanayoikabili kama vile
umaskini, hujuma, hali ngumu ya maisha,matabaka, na unafiki wa viongozi wetu na
ametoa wito kwa vijana kushirikiana katika kupiga vita matatizo hayo.
Pia msanii amefaulu katika kuwachora wahusika wake
wanamapinduzi. Kwa upande mwingine msanii amefanikiwa katika kuoanisha jina la
kitabu na yaliyomo. Morani ni vijana wa Kimasai wenye jukumu la kulinda jamii
yao. Katika kitabu hiki msanii anatoa wito kwa morani(vijana) wote kupiga vita
hujuma hapa nchini.
KUTOFAULU
Msanii ametumia taswira nyingi mno si rahisi kwa mtu
wa elimu ya chini kupata maana zake na hivyo hushindwa kupata ujumbe
uliokusudiwa na mwandishi.