FORM 3-KISWAHILI-UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI ANDISHI

UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI ANDISHI
Fasihi andishi ni tawi la fasihi linalotumia sanaa ya maneno kufikisha ujumbe kwa hadhira kwa njia ya maandishi. Zipo aina nyingi za fasihi andishi, miongoni mwa hizo ni pamoja na hadithi fupi, riwaya, tamthiliya na mashairi.
Uhakiki wa Fani katika riwaya ya Takadini
Hakiki fani katika riwaya ya Takadini
MWANDISHI: BEN J. HANSON
WACHAPISHAJI: MATHEWS BOOKSTORE AND STATIONARIES
MWAKA: 2004
JINA LA KITABU
Jina la kitabu TAKADINI lina maana ya “Sisi tumefanya nini”. Hili ni jina ambalo Sekai alimpa mwanae mara baada ya kumzaa. Jina hili lilitokana na majonzi aliyokuwa nayo juu ya kutaka kuuawa kwa mwanae na yeye ilihali hawakuwa na hatia, ila tu kwa sababu ya mila za jamii yake zilivyotaka. Jina hili la kitabu ni sadifu kwani linasawiri vyema maudhui yaliyomo katika kitabu hiki. “Sisi tumefanya nini?’ ni swali ambalo linatokana na ukosefu wa haki ya kuishi, kubaguliwa kutopendwa, na hata kutengwa kwa watu wenye matatizo katika jamii. Swali hili linawalelekea wanajamii ambao bado wanashikilia mila potofu zinazowakandamiza na kuwanyanyasa watu wenye matatizo mfano, ulemavu wa ngozi, wagonjwa nk. Jina hili pia ni sadifu kwa maisha ya jamii yetu ya watanzania kwani watu bado wanashikilia mila potofu ambazo si nzuri. Mwandishi ametumia jina hili makusudi ili kutaka kuionesha jamii hali halisi ya vilio vya albino, wasichana wadogo wanaolazimishwa kuolewa nk. Kuwa huu sasa ni muda mwafaka wa jamii kuyaacha na kutupilia mbali mambo hayo.
MUUNDO
Muundo alioutumia mwandishi wa riwaya hii ni muundo wa msago au kwa jina lingine muundo wa moja kwa moja. Ameyapanga matukio katika mtiririko sahili kwani ameanza kutuonesha toka mwanzo mpaka mwisho wa maisha ya kijana Takadini “Msope”.Toka kutungwa kwa mimba yake, kuzaliwa kwake na kuishi kwake, matatizo na changamoto zinazomkumba na jinsi anavyokabiliana nazo na hatma ya maisha yake.
Mgawanyo wa visa na mtukio umepangwa katika sura ambapo visa vimejengwa kwa ufundi na kuvifanya vijengane na kukamilishana kuelekea kilele cha masimulizi. Matukio haya yamewekwa katika sura kumi na tatu.
  • Sura ya Kwanza:Sura hii inaanza kutuelezea kuhusu mwanamke Sekai anavotunga mimba, pia tunaelezwa kuhusu mtazamo mbaya wa wake wenzie juu ya mimba hiyo baada ya Sekai kukaa kwa muda mrefu bila ya kujaliwa mtoto.
  • Sura ya Pili:Hapa tunasimuliwa jinsi Sekai anavyofanikiwa kujifungua salama. Lakini kwa bahati mbaya kwa kawaida ya jamii yao anajifungua mtoto Zeruzeru ambaye kwa mila zao mtoto huyo ni laana. Hivyo alipaswa kutupwa mara moja ama kuuawa. Hakuna ambaye alikuwa tayari kumpokea mtoto yule kwani si baba yake wala jamii yake ila mama yake pekee.
  • Sura ya Tatu:Jamii bado haipo tayari kumpokea mtoto Sope, wanawake wenza wa Sekai wanasubiri kwa hamu kuona tukio la kutupwa kwa Takadini litakavokuwa, kwani ndio jinsi mila na taratibu za mababu zilivyotaka. Kutokana na hali hii ndipo Sekai anapata wazo la kutoroka. Anaamua kuondoka kwenda mbali ili kukinusuru kichanga kisicho na hatia kwani alisubiri kwa hamu na uchu wa muda mrefu kupata mtoto.
  • Sura ya Nne:Sekai anafanikiwa kutoroka na mwanae Takadini ili kumuepusha na kifo, jamii na Mtemi wanapata habari ya kutoroka kwake. Upelelezi unafanyika lakini juhudi hazikuzaa matunda kumpata Sekai na mwanae mchanga waliotakiwa kuuawa. Sekai anasafiri mbali na kufikia kijiji kingine na kupokelewa na mzee Chivero.
  • Sura ya Tano:Sekai anapokelewa katika kijiji cha mzee Chivero, jamii na wazee wanashitushwa sana na ujio huo lakini wanalazimika kumpokea tu baada ya malumbano ya muda mrefu. Kwani mila ziliwataka kutowatelekeza wageni katika kijiji chao, na hiyo ndiyo inakuwa mwanzo wa matumaini ya Sekai kuhusu kuishi kwa mwanae ambaye alionekana kuwa ni laana ya mababu na hakupaswa kuishi.
  • Sura ya sita:Baada ya Sekai kupokelewa katika kijiji cha mtemi Masasa, habari za ujio wake zinaenea kwa wanakijiji wote na wanaonekana kushtushwa sana, si hivo tu bali pia wanajiapiza katu kutomsogelea Sope kwani waliamini amelaaniwa. Lakini kwa juhudi za mzee Chivero baba mpya mlezi wa Takadini Sekai anapata rafiki. Tendai mke wa mtemi Masasa. Anajengewa kibanda cha kuishi yeye na mwanae na maisha yanaanza.
  • Sura ya saba:Sekai anaanza kujishughulisha na shughuli za kawaida kama mama na mwanamke, analima bustani na kufanya kazi ndogo za nyumbani. Siku moja katika safari ya kurudi nyumbani kwa bahati mbaya wanavamiwa na nyuki na kujeruhiwa vibaya yeye na mwanae, anaamua kumtupia mwanae kichakani ili kumuokoa na yeye kujitumbukiza mtoni. Wote wawili wanafanikiwa kutibiwa na kupona majeraha.
  • Sura ya nane:Taratibu Takadini anaanza kukua lakini anagundulika kuwa hawezi kutembea vyema kwa mguu mmoja, hii ilitokana na kuvunjika Mguu baada ya kurushwa kichakani na mamaye kama juhudi za kumwokoa. Hali hii inamhuzunisha zaidi Sekai na Chivero kwani walimpenda sana. Hapa ndipo mapenzi ya Chivero yalianza kudhihirika rasmi kwa Takadini kwani alijenga urafiki naye na kumpenda kama mwanae. Alimfundisha utabibu wa dawa za kienyeji na mambo mengine mengi. Pia tunaona watoto jinsi walivyombagua Takadini kutokana na hali yake, kwani waliambiwa na wazazi wao wasicheze naye amelaaniwa hivo hawakuthubutu.
  • Sura ya tisa:Katika sura hii, Mzee Masasi anafariki dunia na kumuacha mzee Chivero katika majonzi makuu. Hali ya mzee Chivero nayo inaanza kuzorota kwa uzee. Anampa Takadini usia mbalimbali na kumfunza. Pia tunaelezwa juu ya fikra mpya za Takadini za kupiga “mbira” kifaa cha muziki cha kijadi, hii baada ya kuvutiwa na sanaa hiyo aliposhiriki sherehe za mavuno za mwaka. Jamii bado ilimtenga Takadini na kumbagua, walimwona si binadamu bali mzuka tu! Na kwa bahati mbaya mzee Chivero naye aliaga dunia na kuacha simanzi kuu kwa Sekai na Takadini mbao alikuwa ni tegemeo na faraja kwao.
  • Sura ya kumi:Baada ya kifo cha mzee Chivero, Takadini anapata mwalimu maarufu mpiga mbira mzee Kutukwa, anamfundisha kupiga mbira, Takadini anaonesha juhudi kuu na kufanikiwa. Pia anmsaidia kifaa cha kumsaidia kutembea kutokana na mguu wake mbovu, hii inakuwa ni faraja kubwa kwa Takadini na mamaye.
  • Sura ya kumi na moja:Hapa tunaelezwa juu ya kijana Nhamo adui mkuu wa Takadini kwani hakumpenda na alimdhihaki na kumdhalilisha mara kwa mara. Kijana huyu anaonekana kuwa ni shujaa katika jamii yake kwa kitendo cha kumuua simba mla mifugo. Hiyo inamletea sifa kubwa na majivuno mengi hivo wasichana wengi kumtamani awaoe, hali ni tofauti kwa Shingai ambaye anaonesha hisia za mapenzi kwa Takadini pamoja na hali yake ya “Usope”. Chemchemi za mapenzi ya Takadini kwa Sekai zinaanza kumea jambo ambalo linamkera sana Nhamo na kuzidisha chuki kwa Takadini kwani pia alitamani kuwa na Shengai binti mrembo. Jamii inafanya kikao kujadili suala la Shengai kumpenda Takadini na wanalipinga vikali suala hilo.
  • Sura ya kumi na mbili:Nhamo anakata shauri na kwenda kumposa Shengai, wazazi wa pande zote mbili wanaliunga suala hilo mkono asilimia zote. Kwani hilo lingewanusuru aibu ya mwanao kuolewa na Sope, kwani walijua fika Shingai alimpenda Takadini na hakumtaka Nhoma. Nhoma anamuonya vikali Takadini kuwa asiendelee na lolote kwa Shengai. Pia hapa zinafanyika sherehe ya kijadi ya kumkaribisha hayati mzee Chivero tena nyumbani.
  • Sura ya kumi na Tatu:Wakati wa sherehe ya mavuno, binti Shengai anashindwa kuvumilia na kuamua kumfuata Takadini kibandani kwake. Anaamua kuvunja mila za kwao kwani alimpenda kwa dhati Takadini, pamoja na dharau, kejeli, kubaguliwa, ulemavu wake na kuonekana kuwa ni mtu aliyelaaniwa. Wazazi wake wanamtenga na kutomtambua kama ni mtoto wao tena. Suala hilo linatikisa jamii ya watu wa kijiji kile na hata kutaka kuwafukuza Sekai na mwanae lakini wanaokolewa na maamuzi ya busara ya wazee kwa kuwacha Shengai na mpenziwe Takadini waishi hali wakisubiri matokeo! Kuwa je mtoto atazaliwa sope? Na kuongeza ukoo wa masope na kijiji chao kuwa cha masope? Hapa ndio inapojulikana hatma ya Takadini na mkewe kwani anapata ujauzito na kufanikiwa kujifungua mtoto salama asiye Sope. Ilikuwa furaha kuu kwa mama na mtoto na wote pia. Wanaamua kurudi kijijini kwao walikotoroka ili kwenda kuwadhihirishia kuwa hata sope anaweza kuishi hapaswi kubaguliwa na kutengwa
MTINDO
Mwandishi ametumia mitindo kadha wa kadha ili kuipamba kazi yake na kuifanya ivutie wasomaji; mfano matumizi ya nafsi mbalimbali, matumizi ya nyimbo nk.
Matumizi ya nafsi
Kwa kiasi kikubwa yametawala matumizi ya nafsi ya tatu umoja na wingi katika sura zote.Mfano.uk. 30. “ aliingia ndani na kuanza kazi.”Piauk.3 “ Sekai alikoka moto nje ya kibanda, akaketi na kuzungumza na Pindai”.
Matumizi ya nafsi ya pili au dayalojia
Mfano uk 29 - 30. Mazungumzo kati ya Chivero na Sekai:“je umelala salama?je umelala salama?Sijambo mwanangu, sijui wewe?Sijambo Sekuru,Na mwanao je?Naye hajambo.”
Matumizi ya nafsi ya kwanza. Mfano uk. 82 na 83
“lakini ghafla nilipata nguvu mpya”;“nilikuwa na nguvu kama kijana….”
Pia mwandishi ametumia nyimbo katika baadhi ya sura ili kuwaburudisha na kuliwaza wasomaji. Mfano uk. 2 wimbo aliouimba mke mwenza wa Sekai Rumbdzai.
“Mashamba yetu yamelimwa mbegu nazo zimepandwa zimechipua na kumea, sisi watatu tumepanda mavuno yetu; mheshimiwa wetu amemiliki mavuno kwa mikono yake halisi kutoka mashamba yetu yote lakini ni kipi alichoambulia kutoka ardhi ile isiyomea kitu?”pia ametumia wimbo uk. 34, 57, 85.
Matumizi ya hadithi ndani ya hadithi pia ni mtindo mwingine wa usimulizi alioutumia mwandishi.Mfanouk82Kutukwa alisimulia vijana hadithi enzi ya ujana wake na jinsi alivopambana na maadui vitani.
Matumizi ya Lugha
Lugha aliyotumia mwandishi ni lugha fasaha na rahisi inayoeleweka kwa wasomaji wake. Ametumia pia lugha nyinginezo kama vile lugha za kikabila.Maneno kama vile“Amai”,lenye maana yamama, “Sope”lenye maana yazeruzeru, “shumba”- simba, “mbira” – chombo cha asili cha muziki, “gudza” – blanketi lililotengenezwa kwa nyuzi za magome ya miti.nk.Hivyo mwandishi ametumia lugha hii ili kuwaleta wasomaji kwenye mazingira halisi ya kiutamaduni ya jamii ile.
Matumizi ya tamathali za Semi
  • Tashibiha:Mfanouk. 6 “ muda huenda polepole mithili ya mwendo wa kakakuona Uk.15 “ habari njema huchechemea kwa mguu mmoja lakina mbaya hukimbia kama Sungura”Uk.16 “….. alibaki kama kinyago cha mpingo”.Uk.28 “ sio kufurika kama Chura”Uk.33 “aligeuza shingo yake sawa na Mbuni”Uk.42 “ nywele kama vinyweleo vya mahindi yaliyokaribia kukomaa”Uk.82 “muziki ulikuwa kama chemchemi ya maji mwilini mwake”
  • Tashihisi:Mfanouk. 5 “ndege mbalimbali wakiimba kuikaribisha siku mpya”Uk. 7 “vivuli vya jioni viliongezeka urefu”Uk. 18 “maneno yananila mifupa yangu”Uk 25 “kifo kilinukia”
  • Tafsida:Mfano, uk. 83 “sehemu zake za siri”
  • Sitiari:Mfano, uk. 88 “Tapfumaneyialigeukambogo” Uk.97“mwana Mbwa hakuiba mfupa”, Tawanda mfupa ulikwenda wenyewe kuchezanaye.” Hapa mfupa umefananishwa na Shingai na Takadini ndio mwanambwa
Matumizi ya Semi
  • Methali:Uk. 45 “ kipofu huwa hachagui shimo la kutegea wanyama”uk.33 “ moyo mwema utakufanya uuwawe”
  • Misemo:Mfano.Uk. 12 “kufikiri katika siri ni sawa na safari ya mbwa”Uk. 100 “kanga hawezi kutua juu ya bua la mtama”Uk.101 “kibuyu kikubwa hakikosi mbegu ndani”Uk. 125 “fuvu la nyanilimekuwa kijiko kwa mlo wa mahindi”
  • Nahau:uk. 27 “ penzi langu kwake halikufua dafu”Uk. 88 “kutiana moyo wa ari”
Matumizi ya mbinu nyinginezo za kisanaa
  • Nidaa:Mfano,Uk.4 “Ha!” , “Ha! Atimuliwe tena? Mchawi?” Uk.16 “Mai, Wee!” Uk.39. “Ha! Iwe! Ha!”
  • Mdokezo:MfanoUk.3 “ndiyo Pindai, ninaogopa……….” Uk.42 “mtu mzima kama watu wenine ameamua………”
  • Takriri:Mfano,uk 57 “ mwanangu, mwanangu, mwanangu, wamekufanya nini?”
Wahusika
Sekai
  • Ni mke wa Makwati wa kwanza.
  • Ni mwanamke jasiri.
  • Anapinga mila potofu na mbaya za jamii yake.
  • Ni mvumilivu.
  • Ni mchapakazi mzuri.
  • Anajifungua mtoto zeruzeru ambaye ni laana kwa jamii yake.
  • Ni mtiifu na mwenye adabu.
  • Ana huruma na mnyenyekevu.
  • Ana mapenzi ya dhati.
  • Anafaaa kuigwa na jamii.
Takadini
  • Ni mtoto anayezaliwa na ulemavu wa ngozi( albino)
  • Anasadikika kuwa ni laana kwa jamii yake hivyo kupaswa kuuawa au kutupwa mbali.
  • Anaokolewa na mama yake kwa kutoroshewa katika kijiji kingine.
  • Anapokua anakua kijana jasiri.
  • Hapendwi na jamii.
  • Anabaguliwa na jamii, hana rafiki.
  • Ni mvumilivu na msikivu mwenye heshima.
  • Alimpenda Chivero sana.
  • Alikuwa mpiga mbira (chombo cha muziki cha kijadi) maarufu.
  • Alimuoa Shingai na kupata mtoto asiye Sope.
Makwati
  • Mume wa Sekai.
  • Ameoa ndoa ya mitara ana wake wanne.
  • Anashikilia mila na desturi potofu.
  • Hana mapenzi ya dhati kwa mwanae.
  • Hafai kuigwa na jamii.
Dadirai na Rumbidzai
  • Wake wengine wa mzee Makwati.
  • Wana wivu.
  • Hawampendi Sekai.
  • Wana roho mbaya kwani wanamwombea Sekai mabaya.
  • Ni katili kwani wanashinikiza Sekai na mwanae wauawe bila huruma.
  • Wasengenyaji.
  • Hawafai kuigwa na jamiii.
Pindai
  • Mke wa pili wa Makwati.
  • Ana upendo wa dhati kwa Sekai.
  • Ni mkweli.
  • Hana wivu.
  • Ni mshauri mzuri.
  • Anafaa kuigwa na jamii.
Chivero
  • Ni mzee wa kijiji cha mzee Masasa.
  • Anawapokea Sekai na mwanae baada ya kutoroka kwao kwa ukarimu mkubwa.
  • Ni mwenye roho nzuri.
  • Ana huruma sana.
  • Ni mganga wa tiba za asili.
  • Ana mapenzi ya dhati kwa Takadini na Sekai.
  • Anamrithisha Takadini uganga.
  • Ana busara na hekima.
  • Ni mshauri mkuu wa Mtemi Masasa.
  • Anafaa kuigwa na jamii.
Mtemi Masasa
  • Ana busara na hekima.
  • Ana huruma.
  • Anafuata mila na desturi ya jamii yake.
  • Ni msikivu.
  • Ni rafiki mkubwa wa Chivero.
  • Ni kiongozi bora.
  • Anafaa kuigwa na jamii
Nhamo
  • Ni kijana katika kijiji cha mtemi Masasa.
  • Ana majivuno na jeuri.
  • Hampendi Takadini kwani alimbagua kumpiga na hata kumdhalilisha.
  • Hafai kuigwa n ajamii.
Tendai
  • Mke mdogo wa mwisho wa mtemi Masasa.
  • Aliolewa bila kupenda, hakumpenda mtemi Masasa kwani alimzidi umri.
  • Alikuwa rafiki mzuri wa Sekai.
  • Ana mapenzi ya dhati kwa Takadini.
  • Ana bidii na mvumilivu.
  • Anafaa kuigwa na jamii
Nhariswa na mkewe
  • Ni wazazi wa Shingai
  • Wanashikilia mila desturi potofu
  • Hawakupenda kabisa kitendo cha mtoto wao kumpenda Takadini
  • Walimlazimisha kuolewa na Nhamo kwani walitaka sifa na maujiko
  • Walimtenga Shingai baada ya kutoroka na kuolewa na Takadini
  • Si wazazi wazuri
  • Hawafai kuigwa na jamii
Kutukwa
  • Ni mzee katika kijiji cha mtemi Masasa
  • Ni mpigaji mbira maarufu
  • Alimfundisha Takadini kupiga mbira
  • Alitoa mtazamo mbaya kwa wanakijiji wenzake kwa kuwaeleza sifa nzuri za Takadini
  • Alimpenda Takadini. Anafaa kuigwa na jamii
Mandhari
Mandhari aliyotumia Ben J Hanson ni mandhari ya kijijini kwani maisha ya watu na mazingira yanayoelezwa ni ya kijijini, masuala kama ya kilimo, ufugaji, sherehe za mavuno, makazi ya watu kukaa katika jumuiya ya pamoja kijamaa inayoongozwa na mtemi mmoja. Mfano mtemi Masasa, yote haya ni viashiria kuwa mandhari ni ya kijini. Mandahari ambayo mwandishi ameijengea mawazo yake na kuyaibua ni sadifu na halisi. Kwani maeneo ya vijijini ndiko kulikokithiri mambo ya imani potofu na za kishirikina kama vile kuwaua watoto Sope au albino.
Fani katika Riwaya ya Joka la Mdimu
Hakiki fani katika Riwaya ya Joka la Mdimu
MWANDISHI: ABDALLAH J. SAFARI
MCHAPISHAJI: HUDA PUBLISHERS
MWAKA: 2007
UTANGULIZI WA KITABU
Joka la mdimu ni riwaya iliyojengwa kwa visa tofautitofauti vinavojengana kukamilisha masimulizi. Ni riwaya inayosawiri au kuakisi mambo yaliyopita ya nyakati za nyuma ambapo kulikuwa na shida kama vile za mafuta ya petroli, Nguo, vyakula nk. Pamoja na hayo zipo pia dhamira au mawazo ambayo yanasawiri maisha ya Mtanzania wa leo kama vile masuala ya rushwa na uhujumu uchumi.
Kwa upande wa fani ni riwaya ambayo mwandishi amewaumba vyema wahusika wake kwa kuwavika uhalisia vyema, amepanga visa vyake na amejitahidi kutumia lugha yenye mvuto na vionjo vya kisanaa huku akiwaburudisha wasomaji kwa mtindo wa kipekee.
JINA LAKITABU
Jina la kitabu limewekwa katika lugha ya picha, JOKA LA MDIMU ni nyoka anayeishi katika miti ya kijani. Nyoka huyu hupendelea kuishi katika miti ya Minyaa na Midimu inayofanana na rangi yake. Nyoka huyu awapo kwenye miti hiyo si rahisi kumtambua kutokana na rangi yake kufanana sana na miti hiyo. Hivyo ni nyoka hatari sana kwa binadamu.
Mwandishi anatumia taswira ya Joka la Mdimu kufananisha na viongozi ambao ni wananchi wenzetu, wanafanana na sisi, ni ndugu zetu damu yetu. Lakini ni hatari mno kwani hutugeuka na kuwa mafisadi, wala rushwa, hawatimizi majukumu yao, ni walaghai nk. Badala ya kusaidia wananchi wao hujali maslahi yao kwanza na hivyo kusababisha mifumo ya kiuchumi kuendelea kuwa migumu kwa wananchi na kupelekea kuongezeka kwa kiasi kikubwa cha watu walio maskini au hohehahe. Hivyo jina la kitabu linasawiri yaliyomo ndani ya kitabu na katika jamii.
MUUNDO
Riwaya ya Joka la Mdimu imetumia muundo changamani yaani kwa kiasi fulani ametumia rejea au rukia pia ametumia muundo sahili au msago.
Mfano ametumia muundo warejeakatika sura ya Mindule ambapo anaanza kutueleza juu ya habari za Amani dereva wa taxi na adha anazopata kutokana na ukosefu wa mafuta na jinsi anavyoiendesha biashara yake hiyo. Lakini ndani ya sura hiyohiyo anaturudisha nyuma na kuanza kutuelezea namna Amani alivyopata kazi ya udereva Taxi na kutueleza juu ya mmiliki wa Taxi hiyo ambaye ni Shiraz Bhanj. Pia katika sura ya Boko anatueleza juu ya Safari ya Tino kwenda kumuona mwanae mgonjwa uk.73 ila hatuelezi inavyoendelea lakini anarukia kisa kingine cha Brown Kwacha na sura ya Kwale halafu badae anaturudisha nyuma na kuendelea kutuelezea juu ya habari za kuuguliwa kwa Cheche na Tino anapofika kumuona katika sura ya Dakta Makwati. Pia ametumia muundo wa moja kwa moja katika sura zingine kwani ameyapanga matukio yake katika usahili bila kuruka.
Pia mwandishi amegawanya visa na mtukio katika sura kumi ambapo kila sura ameipa jina kwa kutumia majina ya wahusika.
  • Sura ya kwanza, MINDULE:Hapa mwandishi anatueleza kuhusu habari za Amani dereva Taxi, masaibu anayopata katika kazi yake kutokana na uhaba wa mafuta katika vituo vya mafuta.
  • Sura ya pili, TINO:Hapa tunaelezwa kuhusu maisha ya Tino na kazi anazofanya ya kuvuta kwama. Tunaambiwa kuhusu hali ngumu ya maisha ya Tino na wakazi wengine wa Sega, hapa tunaelezwa pia kuhusu masuala ya uongozi jinsi ulivyo mbovu na ugawanywaji mbovu wa vyanzo vya uchumi na bidhaa.
  • Sura ya tatu, JINJA MALONI:Katika sura hii tunaelezwa kuhusu maisha ya Jinja Maloni, hapa anaibua dhamira kama vile za uvamizi, uhalifu na mauaji pia anaendela kutueleza kuhusu hali ngumu ya maisha.
  • Sura ya nne SEGA:Maisha ya wakazi wa Sega yanaelezewa hapa jinsi yalivyo ya dhiki, pia tunaelezwa kuhusu Tino na mkewe maisha yao yalivyo na familia yao, anaibua dhamira ya mapenzi ya dhati na upendo kwa familia.
  • Sura ya tano, BOKO:Hapa tunaelezwa kuhusu adha ya usafiri kwa watu, shida ya mafuta, ubovu wa miuondmbinu kama vile barabara, vinasemwa hapa.
  • Sura ya sita, BROWN KWACHA:Sura hii inaeleza habari za Brown maisha yake na tabia zake, anaibua dhamira kama vile uhujumu uchumi, biashara za magendo, suala la kutowajibika kwa watumishi, suala la kukosekana kwa uaminifu katika ndoa na mapenzi ya pesa ambapo sifa zote hizi alizibeba Kwacha.
  • Sura ya saba, KWALE:Hapa yanaelezwa mambo kuhusu hifadhi ya Kwale, safari ya Brown na Leila kwenda kutembea kwale. Hapa yanatajwa mambo ya udhalimu wa kuharibu mali za umma (maliasili za taifa) mfano pembe za ndovu, vipusa pia mapenzi yasiyo ya kweli.
  • Sura ya nane, DAKTA MIKWALA:Dakta Mikwala ndiye mhusika mkuu anayeelezwa hapa, tunalezwa juu ya ugumu wa upatikanaji wa huduma za afya kwani Cheche anashindwa kutibiwa kutokana na ukosefu wa fedha za kigeni.
  • Sura ya tisa, CHECHE:Tunaelezwa juu ya juhudi za Amani na Tino ili kumsaidia Cheche aweze kwenda kutibiwa Uingereza. Wanafanikiwa kupora benki na kupata pesa za kumtibu Cheche.
  • Sura ya kumi, MOTO:Hapa hatma ya visa vidogo vidogo imeelezwa kwa kutolewa hatma ya maisha ya Cheche na Brown Kwacha. Cheche alipata matibabu na kupona na Browna anafanikiwa kuirubuni serikali kwa kuipanga mahesabu ya uongo.
MTINDO
Mwandishi ametumia mitindo ya aina tofautitofauti ili kuweza kuipamba kazi yake ivutie.
  • Matumizi ya nafsi ya tatu Umoja. Imetawala: Mfanouk.5“Amani aliangalia…….” Uk.25 “Amani alijizuia” .Nafsi ya tatuwingi;mfano uk. 63“ wote walitoka nje kuelekea klabuni”.Piauk.53 “wale wanaume walimvamia”
  • Matumizi ya nafsi ya pili: Mfanouk.106 “ mmechoka kuangalia video?” “aa tumeshaziona mara nyingi tunaombaainanyingine.” Mazungumzo baina ya mke wa Brown na wanae.Pia mazungumzo baina ya Brown na Leila.Uk.113. “habari za asubuhi”“ Nzuri sijui wewe” alijibu“Uliota njozi njema?”"Wapi?""Kwa nini?"
  • Matumizi ya nafsi ya kwanza: Mfanouk. 39 “mimi nimemaliza” “….kuiba nimeiba sana….”
  • Matumizi ya nyimbo.Uk.70. wimbo wa Chaupele: “Chaupele mpenzi, haya usemayoKama ni maradhi, yapeleke kwa DaktariWanambia niache rumba,na mimi sikuzoeaSitaweza kuliacha rumba, kwa sababu yakoKama wanipenda, nenda kwa baba”Piauk.58 “sega! Sega! Sega!, usioogope” wimbo waliouimba washabiki wa michezo.
  • Masimulizi ya hadithi ndani ya hadithi: Hapa mwandishi amemtumia muhusika kusimulia kisa kingine kidogo ndani ya kisa kikuu. Mfanouk.39mhusika Tino anamsimulia mteja wake maisha yake ya mwanzo kabla hajaanza kazi ya kuvuta kwama.
MATUMIZI YA LUGHA
Mwandishi A. Safari ametumia lugha fasaha na inayoeleweka kwa wasomaji wake. Kuna matumizi ya lugha nyinginezo kama vile kiingereza.Uk.55 “city devils” uk.155 “I miss my family”, uk.24 “Hey man you will pay extra money”, uk.99 consignment”.Pia kuna matumizi ya lugha ya kiarabu, mfanouk.45 “Salaam aleikum mayitun” uk.42 “Inna Ilayhi Raajiunna!”, uk.13, “Insha Allah!”. Vilevile kuna matumizi ya lugha ya mtaaniuk.39 “msela”, “ndito”, “kashkash”.
Matumizi ya tamathali za semi.
  • Tashibiha:Uk.117 “ngozi yake nyeusi kama udongo wa mfinyanzi”Uk.122 “mweusi kama sizi la chungu”Uk.9 “Zepher 6 ile iliunguruma kama simba dume”Uk.10 “mteuzi mithili ya Mbega”Uk.35 “……miguu yake ikakazana mithili ya upinde uliotaka kufyatuliwa”
  • Sitiari:Uk.91 “Brown Kwacha alikuwa kinyonga”Uk.15 “sarahange wetu mboga kweli siku hizi”Uk.40 “huku twakaa vinyama vya mwitu”Uk.72 “sote ni kobe”
  • Tashihisi:Uk.109 “……gari lile zuri lilioondoka kwa madaha” Uk.143 “ kuta nyeusi za nyumba zaidi ya kumi zilisimama twe!kuomboleza” Uk.91 “pua zake zikalakiwa na riha na ashrafu ya manukato”;Uk.12 “utumbo ulimlaumu”; Uk.27 “mvua ikapiga kwa kiburi na kuviadhibu vibati vibovu”.
  • Tafsida:Uk. 49 “isijekuwa nimekukatiza haja!”,piauk.hohuo“kinyesi”.
Mbinu nyingine za kisanaa.
  • Takriri:Uk.151 “mwizi! Mwizi! Jambazi! Jambazi!”Uk.57 “shinda! Shinda! Shinda!”Uk.33 “karibu baba, kariibu kaka, karibu mkwe” Uk.72 “uhuru upi? Uhuru gani? Uhuru wa nini na nani?”
  • Mdokezo:Uk.149 “lakini……..”
  • Onomatopea au tanakali sauti:Uk. 1 “saa mezani niliendelea kugonga taratibu ta! ta! ta!”; Uk.10 “ikatoka sauti kali tupu ta nye nye”;Uk.67 “upepo wa stova uliolia shshsh”;
  • Tashtiti:Uk.113. leila anamuuliza Brown maswali ambayo anayajua majibu yake. Brown:“uliota njozi njema? Leila: Wapi?” Leila:Kwanini? Brown:Mwenywe unajua”
  • Nidaa:Uk.39 “Aaa! Limbukeni wa jiji anataka kunitia kashkash”: Uk 30 “nguo zangu Mungu wee!” Uk.42 “Inna Lillah wa Inna Ilayhi Raajiunna!” Uk.92 “Ah! Leila kwacha alimsalimia kwa furaha” Uk. 105 “Lahaula”
Matumizi ya Semi.
  • Methali:Uk.78 “asilojua mtu ni usiku wa kiza”Uk.83 “ukiona mwenzako anyolewa zako tia maji”Uk.98 “mtaka waridi sharti avumilie miiba”Uk. 99 “biashara haigombi”Uk.43 “ajizi nuksani huzaa mwana kisirani”
  • Misemo:Uk.10 “asiye na bahati habahatishi”Uk.47. “asiyezika hazikwi”Uk.64 “mmetupa Jongoo na mtiwe”Uk.98 “asali haichomvwi umoja”Uk.111 “ajali haina kinga”Uk.115 “mwenye macho haambiwi tazama”Uk.120 “matendo hushinda maneno”Uk.47. “asiyezika hazikwi”
  • Nahau:Uk.11 “sio unanilalia kila mara” –kunidhulumuUk.107 “alikonda akajipa moyo” –kujifariji moyo
Matumizi ya taswira
Taswira mwonekano imetumika, ambayo inatujengea picha kutokana na vitu tunavyovifahamu. Mfanouk.76 “alisema kijana mmoja wa kiume kavaa sketi, blauzi na sidiria iliyopachikwa juu yake. Kichwani alifunga kilemba.”Hii inatupa picha halisi ya huyo kaka kwani tunaposoma ni kama kweli tunamuona kutokana na jinsi mwandishi alivyoelezea. Piauk.135 “mwambie yule jamaa pale atayarishe kuku mzuri wa kukaanga”……… na kachumbari yenye pilipili”hii inamfanya msomaji ahisi ladha ya kuku na hiyo pilipili kwa maneno ambayo mwandishi ameyajengea taswira na hii ni taswira hisi.
Joka lamdimuni taswira ya nyoka mbaya ambaye amefananishwa na viongozi wabaya.
WAHUSIKA
AMANI
  • Ni dereva taxi
  • Ana upendo wa dhati
  • Ni mchapakazi
  • Ana hekima na busara
  • Ana huruma
  • Ni rafiki wa kweli wa Tino
  • Kutokana na hizo sifa amani ni mhusika bapa
  • Anafaa kuigwa na jamii
TINO (mhusikabapa)
  • Ni mchapakzi
  • Mlezi bora wa familia
  • Baba wa Cheche
  • Ana huruma
  • Ana upendo wa dhati
  • Ni makini
  • Ni jasiri
  • Ni mwanamichezo
  • Anafaa kuigwa na jamii
BROWN KWACHA
  • Ni mkurugenzi wa idara ya fedha za kigeni
  • Ni muhuni na Malaya
  • Fisadi na mla rushwa
  • Anafanya biashara haramu
  • Hana mapenzi kwa familia yake
  • Anapenda anasa
  • Si muaminifu kwa mkewe
  • Si muadilifu
  • Hafai kuigwa na jamii
  • Ni mhusika bapa
JINJA MALONI
  • Ni jasiri na mwenye nguvu
  • Ana huruma na upendo
  • Mchapakzi
  • Mlevi
  • Maskini
  • Ni mhusika duara
DAKTARI MIKWALA
  • Ni daktari bingwa wa mifupa
  • Anapenda rushwa
  • Si muwajibikaji katika kazi yake
  • Ni mlevi
  • Hafai kuigwa na jamii
  • Ni mhusika bapa
SHIRAZ BHANJ
  • Ni mfanyabiashara
  • Ni mtoa rushwa
  • Ana biashara za magendo
  • Rafiki wa Brown
  • Hafai kuigwa na jamii
  • Ni mhusika bapa
ZITTO
  • Ni mfanyakazi bandarini
  • Ni mwanamichezo
  • Ni jasiri ana kipato duni
  • Rafiki wa Tino na Aman
CHECHE
  • Ni mtoto wa Tino
  • Ana nidhamu na bidii
  • Ni mwanamichezo
  • Ana upendo kwa wazazi wake
  • Ni mtiifu na msikivu
  • Mcheshi na mudadisi
  • Alivunjika kiuno michezoni
  • Ni mhusika bapa
MWEMA
  • Ni mke wa Tino
  • Mvumilivu
  • Ana mapendo ya dhati kwa familia yake
  • Ni mchapakazi
  • Ni mhusika bapa
JOSEPHINE NA LEILA
  • Wasichana wahuni waliojiuza kwa Brown Kwacha
  • Hawafai kuigwa na jamii
MANDHARI
Mandhari aliyoitumia mwandishi ni ya mjini, anataja baadhi ya maeneo ya nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam kama vile Boko, Sega, Mindule. Mandhari hii ni sadifu kwa yale ambayo mwandishi ameyaeleza kwani masuala ya rushwa, upotevu wa haki, hali ngumu ya uchumi na maisha kwa ujumla, ni matatizo halisi ya jamii ya Tanzania.
Powered by Blogger.