TAHAKIKI TAMTHILIYA YA KILIO CHETU KIDATO CHA 3&4
JINA LA TAMTHILIYA: Kilio Chetu
MWANDISHI: MEDICAL AID FOUNDATION
MCHAPISHAJI: TANZANIA PUBLISHING HOUSE (TPH) MWAKA 1995
UTANGULIZI
Kilio Chetu ni
tamthiliya inayojikita kuzungumzia umuhimu wa elimu ya jinsia na ukimwi
kwa vijana, Tamthiliya hii inaonesha namna ukosefu wa elimu ya jinsia
na ukimwi kwa jamii hususani vijana inavyochangia mimba za utotoni au
mimba zisizotarajiwa na maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa vijana.
Katika
tamthiliya hii, mwandishi anaonesha namna ambavyo jamii ikiangaika
kujielimisha kuhusu elimu hii ya jinsia na ukimwa na kuwaacha vijana
wakiangamia kwa kukosa elimu hiyo, hali hii inaifanya jamii kugawanyika,
wapo wanaoona kuwa suluhisho la janga hili la Ukimwi, ni jamii nzima
wakiwemo na vijana kupewa elimu hii lakini wapo wazazi wanaopinga
wakiamini vijana umri wao wakupewa elimu hii haujafika bado. Je ni nini
hatima ya vijana hawa? Basi tafuta kitabu hiki cha Kilio chetu kisome
utajifunza mambo mengi sana ni kitabu kinachotakiwa kusomwa na watu wa
rika lolote.
WAHUSIKA
Katika
kazi ya fasihi wahusika wanaweza kuwa watu, wanyama au vitu, na
wahusika ndiyo wanaobeba dhamira za msanii, na katika kazi ya fasihi
wahusika tunawagawa katika makundi mawili, wahusika wakuu na wahusika
wasaidizi/ wahusika wadogowdogo
(a) Wahusika Wakuu
Katika tamthiliya hii, ina wahusika wakuu wawili, ambao ni Suzi na Joti.
1. SUZI
ü Ni binti anayesoma shule ya msingi
ü Ni
binti asiyekuwa na elimu ya jinsia na ukimwi, Mama yake anashindwa
kumpa elimu hiyo akiamini kuwa umri wa Suzi haujafikia kupewa elimu
hiyo.
ü Anajiingiza katika mapenzi akiwa mdogo.
ü Anakuwa na mahusiano ya kingono na mwanafunzi mwenzake anayeitwa Joti.
ü Ni binti wa pekee wa Mama Suzi.
ü Anapata mimba akiwa mwanafunzi na anafikiria kuiotoa mimba hiyo.
2. JOTI
ü Ni kijana wa kiume anayesoma shule ya msingi.
ü Ni
kijana asiyekuwa na elimu ya jinsia na ukimwi, baba yake anashindwa
kumpa elimu hiyo akiamini kuwa umri wa joti haujafikia kupewa elimu
hiyo.
ü Anajiingiza katika mahusiano ya kingono akiwa mdogo huku akiwa mwanafunzi.
ü Anajihusisha na mahusiano ya kingono na wasichana wengi, akiwemo Suzi, Chausiku, Gelda n.k.
ü Ni mvulana mlaghai, anawalaghai wasichana ili tu kutimiza haja zake za kingono.
ü Anaambukizwa virusi vya ukimwi
ü Anafariki kwa ugonjwa wa ukimwi.
(b) Wahusika wadogo wadogo
1. MAMA SUZI
ü Huyu ni mama yake Suzi
ü Anamlea Suzi bila baba
ü Anajishughulisha na biashara ndogondogo kama vile kuuza vitumbua ili kujipatia kipato.
ü Anaamini kuwa mtoto mdogo hawezi kuambukizwa virusi vya ukimwi.
ü Anakumbatia mila na desturi zililozipitwa na wakati zinazokataza watoto/vijana kupewa elimu ya jinsia na ukimwi.
ü Anakataa
katakata mtoto wake, Suzi kupewa elimu ya jinsia na ukimwi akiamini
kuwa umri wake ni mdogo, na kufanya hivyo ni sawa na kumfundisha
umalaya.
ü Anamwadhibu mtoto wake (Suzi) baada ya kukuta vidonge vya kuzuia mimba katika mfuko wa sketi yake.
2. BABA JOTI
ü Ni baba yake na Joti.
ü Anaamini kuwa ukali wa mzazi na viboko ndiyo suluhisho la kuwazuia watoto kujiingiza katika mambo mabaya.
ü Anakataa katakata elimu ya jinsia na ukimwi kutolewa kwa watoto/vijana.
ü Anaangaika kuokoa uhai wa mtoto wake, Joti, kwa kutafuta tiba yake kila mahali.
ü Anampoteza mtoto wake(joti) baada ya kufariki kutokana na ukimwi.
3. MAMA JOTI
ü Huyu ni mama yake Joti.
ü Mke wa Baba Joti
ü Rafiki yake Mama Suzi
ü Anahisi
mume wake ana uhusiano wa kimapenzi na wanawake wengine, hali
inayomlazimu kuwanunulia kanga zenye maandishi ya mafumbo ili kuwapasha
wezi wake.
ü Yeye na mumu wake (Baba Joti) wanashindwa kumpa Joti elimu ya jinsia na ukimwi.
4. BABA ANNA
ü Huyu ni baba yake Anna.
ü Anaamini kuwa elimu ya jinsia na ukimwi ni muhimu kwa vijana ili kuwanusuru na janga la ukimwi.
ü Kwa
kushirikiana na mke wake wanafanikiwa kuwapa watoto wao elimu ya jinsia
na ukimwi, elimu inayowasaidia kupambana na vishawishi.
5. MAMA ANNA
ü Huyu ni mama yake Anna.
ü Ni mke wa Baba Anna
ü Kwa
kushirikiana na mume wake wanafanikiwa kuwapa watoto wao elimu ya
jinsia na ukimwi, elimu inayowasaidia kupambana na vishawishi.
6. ANNA
ü Mtoto wa kike wa Baba Anna na Mama Anna
ü Ni mwanafunzi wa Shule ya msingi.
ü Amepewa
elimu ya jinsia na ukimwi, elimu inayomsaidia kupambana na vishawishi
vya kujiingiza katika mahusiano ya kimapenzi akiwa mdogo
ü Ana mkatalia Mwarami kuwa naye kimapenzi
7. MJOMBA
ü Huyu ni kaka yake na Mama Suzi
ü Mjomba wake na Suzi
ü Anasisitiza elimu ya jinsia itolewe kwa vijana wote ili kuwanusuru na maambukizi ya virusi vya ukimwi na mimba zisizotarajiwa.
ü Anamshauri
Baba Joti kutoangaika kwenda kwa waganga na kumaliza rasilimali zake
kwa ajili ya kutafuta tiba ya UKIMWI kwa mtoto wake Joti kwani ukimwi hauna dawa
8. JIRANI
ü Huyu ni jirani yake na Baba Joti.
ü Anamshawishi Baba Joti kwenda kwa mganga wa kienyeji kutibiwa ukimwi.
9. MWARAMI
ü Huyu ni rafiki yake Joti, Choggo na Jumbe
ü Ni mwanafunzi wa shule ya msingi
ü Hana elimu ya jinsia na Ukimwi anaamini ukimwi unawapata wakubwa tu
ü Wenzake
wanamshawishi kujiingiza katika mahusiano ya kimapenzi na hata
kumtishia asipofanya hivyo watamfukuza katika kundi lao la urafiki
ü Anashindwa kumshawishi Anna
10. CHOGGO
ü Huyu ni rafiki yake Joti, Mwarami na Choggo
ü Ni mwanafunzi wa shule ya msingi
ü Anajiingiza katika mahusiano ya kimapenzi akiwa mtoto mdogo tena mwanafunzi
ü Yeye na rafiki zake wana tabia ya kwenda katika vibanda vinavyoonesha video za ngono (sinema za X) kuangalia
11. JUMBE
ü Huyu ni rafiki yake Joti, Mwarami na Choggo
ü Ni mwanafunzi wa shule ya msingi
ü Anajiingiza katika mahusiano ya kimapenzi akiwa mtoto mdogo tena mwanafunzi
ü Yeye na rafiki zake wana tabia ya kwenda katika vibanda vinavyoonesha video za ngono (X) kuangalia
12. CHAUSIKU
ü Huyu ni mwanamke mtu mzima jirani na akina Joti.
ü Anajishughulisha na biashara ndogondogo hususani biashara ya vitumbua ili kujipatia kipato.
ü Anakuwa na mahusiano ya kimapenzi na kijana mdogo tena mwanafunzi (Joti)
ü Ana mahusiano ya kimapenzi na Mpemba muuza duka.
13. FAUSTA
ü Huyu ni msichana anayesoma darasa la tano
ü Anafariki kwa ukimwi
14. MPEMBA
ü Huyu ni mfanyabiashara wa duka
ü Anakuwa na mahusiano ya kimapenzi na Chausiku
Mfano wa maswali unayoweza kuulizwa sehemu hii
1. Wahusika na hasa mhusika mkuu katika tamthiliya ndiye anayeifikishia jamii ujumbe uliokusudiwa. Tumia tamthiliya mbili kutetea hoja yako.
2. Chagua
wahusika watatu wa kike kutoka kila tamthiliya kati ya tamthiliya mbili
ulizosoma, kasha onesha kukubalika kwao kama kielelezo cha maisha
katika jamii.
DHAMIRA
Hili ni wazo kuu au mawazo mbalimbali yanayojitokeza katika kazi ya fasihi. Na katika tamthiliya hii kuna dhamira kuu na dhamira ndogondogo ambazo zimejitokeza, kwa kuanza tunaanza na;
(a) Dhamira Kuu
Dhamira
kuu katika tamthiliya ni umuhimu wa elimu ya jinsia na ukimwi,
mwandishi anaamini kuwa, ili jamii iweze kunusurika na matatizo
yatokanayo na kujamiana kama vile mimba za utotoni (mimba
zisizotarajiwa) magonjwa ya zinaa kama vile kasendwe, kisonono gono na
ukimwi, sharti vijana wapewe elimu ya jinsia na ukimwi, mwandishi
anathibitisha hili akimtumia muhusika Mjomba anaposema, “Upepo
umebadilika sasa. Hawa vijana wetu wapewe elimu ya familia ikiwepo ya
jinsia. Watoto waambiwe wazi juu ya mambo haya ya mapenzi na hatima
yake.” Uk. 9
Vilevile,
mwandishi anaonesha namna ambavyo vijana wanapukutika, wanaangamia na
ukimwi kwa sababu ya kukosa elimu hii ya jinsia na ukimwi, hali hii
inasababisha vijana kuwa gizani kabisa wanashindwa namna ya kujikinga na
wengine hata kushindwa kutofautisha kati ya puto na kondomu , rejea
ukurasa wa 13, Mwandishi akimtumia muhusika Mtambaji anaposema, “Kisiwa kizima kipo gizani. Watoto ndio kabisa. Wapo katika giza nene. Wanashindwa kutofautisha kati ya puto na kondomu.”
Si
hivyo tu, mwandishi anaendelea kutuonesha kuwa, ukosefu wa elimu hii ya
jinsia na ukimwi kwa vijana/watoto inawafanya watoto/vijana kujitenga
na mapambano dhidi ya ukimwi kwakuwa wao wanaamini kuwa ugonjwa huu wa
ukimwi ni wa wakubwa tu kwani watoto hawawezi kuambukizwa virusi vya
UKIMWI kama mwandishi anavyosema akimtumia muhusika Mwarami anapomwabia
Anna, “Ukimwi unawapata wakubwa, Anna.” Uk. 25
Si
watoto tu, wapo hata wazazi, watu wazima ambao nao wanaamini kuwa
watoto wadogo hawawezi kuambukizwa virusi vya ukimwi, kama anavyoamini
Mama Suzi, rejea ukurasa wa 4, muhusika Mama Suzi anaposema, “...Lakini shoga, watu wanatafuta laana ya marehemu. Kitoto kama kile; kife kwa ukimwi! Ungeingilia kona gani?” {Uk.4}
Mwandishi
anaendelea kutuonesha kuwa, hata mimba za utotoni, mimba zisizotarajiwa
kwa vijana husababishwa na ukosefu wa elimu hii ya jinsia, kwa mfano
mwandishi anamtumia muhusika Suzi ambaye anaamini kuwa, kwa kufanya
ngono mara moja hakuwezi kusababisha mtu akapata mimba, hili tunaliona
ukurasa wa 28, Suzi anapomwambia Anna, “Wala sina mimba, kwanza mimi nimefanya mara moja tu na joti.” {Uk.28}
Vilevile,
mwandishi anaonesha kuwa, wapo watoto/vijana ambao kutokana na kukosa
elimu hii ya jinsia, wanaamini kuwa wao kama watoto hawawezi kupata
mimba, mwandishi anamtumia muhusika Joti anapowaambia rafiki zake, “Mara moja tu, hakuna mimba sisi watoto.” {Uk. 16}
Mwandishi
hakuishia tu kuonesha madhara ya kukosa elimu hii ya jinsia, kwa upande
mwingine ameonesha faida za elimu hii ya jinsia na ukimwi kwa vijana,
mwandishi anaonesha kuwa, vijana waliopata elimu hii, huwasaidia sana
kupambana na kujizuia na vishawishi vya kingono kutokana na uelewa
waliokuwa nao, kwa mfano mwandishi anamtumia muhusika Anna, ambaye
kutokana na mafunzo aliyopewa na wazazi wake yanamsaidia sana kupambana
na kujizuia na vishawishi hivyo kutokana na kufahamu madhara ya
kushiriki ngono kabla ya wakati, hili mwandishi analithibitisha
akimtumia muhusika Anna anaposema, “...Hujui
kama kuna madhara mengine. Hujui magonjwa ya zinaa wewe: hujui
kisonono, kaswende na mengine kedekede. Haya hata UKIMWI hujui?” {Uk. 25}
Hivyo
mwandishi anashauri, elimu hii ya jinsia na UKIMWI, isitolewa
kiubaguzi, itolewe kwa watu wote kwani kila mtu yuko katika hatari ya
kuambukizwa virusi vya UKIMWI, mwandishi anaonesha namna ambavyo vijana
wanateketea kwa kubaguliwa kwao kupewa elimu hii, rejea ukurasa wa 1-2,
Mtambaji anaposimulia, “Wakubwa
wakaandika mabuku kupeana habari. Wakabandika mabango kupeana tahadhari,
lakini watoto wakateketea kwa kukosa habari zozote za kuwaokoa.”
Mwandishi
anaonesha kuwa, kama vijana wangeelimishwa kuhusu madhara ya kufanya
mapenzi kabla ya wakati, namna ya kujilinda, basi wasingetummbukia
katika janga hili, mwandishi anathibitisha kwa kumtumia muhusika Suzi anaposema, “Naapa kwa Mungu wangu, mimi na Joti tungepata bahati ya kuelimishwa, tusingetumbu...tusi...(Anaanguka chini.)” {Uk. 36}
(b) Dhamira ndogo ndogo
1. Ukosefu wa elimu
Dhamira
hii inajitokeza katika tamthiliya, mwandishi anaonesha kuwa ukosefu wa
elimu ya namna ya kupambana na Ukimwi unaifanya jamii kushindwa
kulikabili gonjwa hili, ukosefu wa elimu unawafanya wengine kuamini
ugonjwa huu ni wa kurogwa, wengine wanaamini ni ugonjwa unaletwa na
mizimu na hata wengine kudhani ni majini.
2. Mapenzi na ndoa
Suala
la mapenzi na ndoa pia limepewa nafasi katika tamthiliya hii, tukianza
na suala la mapenzi, mwandishi anajadili mapenzi ya namna mbili, mapenzi
ya dhati na mapenzi ya ulaghai.
(a) Mapenzi ya dhati
ü Baba Anna kwa familia yake
ü Mjomba kwa Suzi
ü Anna kwa wazazi wake
ü Anna kwa Suzi
ü Suzi kwa Joti
(b) Mapenzi ya ulaghai
ü Joti kwa Suzi
ü Joti kwa Chausiku
ü Chausiku kwa Joti
3. Malezi kwa vijana
ü Mwandishi
pia amegusia suala la malezi kwa watoto, mwandishi anaonesha kuwa,
malezi bora kwa mtoto ni malezi ya wazazi wote wawili, yaani baba na
mama, na anapokosekana mzazi mmoja huweza kumuathiri mtoto, katika
tamthiliya hii tunamuona Suzi akilelewa na mama peke yake bila baba hali
hii inachangia mtoto kuingia katika matatizo, hili linathibitishwa na
mwandishi akimtumia muhusika Mama Suzi anaposema, “Kila
siku ninasema mwanangu mdogo, mwanangu ni mtoto mzuri, leo Suzi
unanifanyia hivi? Hivi baba yako angekuwepo ungefanya hivi? Ah Suzi,
ungefanya?” {Uk.31}
ü Katika
suala hili la malezi, mwandishi anatuambia kuwa kuwa, mzazi ndiyo
mwalimu bora kwa malezi mema ya mtoto,rejea ukurasa wa 11, Mjomba na
Baba ANNA wanaposema, “Mzazi ndiye mwalimu wa kwanza...Na ndiye bora.”
{Uk. 11} hivyo wazazi wawafundishe vema watoto wao, lakini wazazi
wasipofanya hivyo, walimwengu watawafundisha na kwa kawaida walimwengu
hufundisha katika upotofu, rejea ukurasa wa 10-11, Baba Anna anaposema, “Dunia imeharibika bwana. Mzazi usipomfunza, walimwengu watamfundisha tena sasa si maadili mema bali njia potofu.” {Uk.10-11}
ü Mwandishi
pia anaonesha kuwa, ili watoto/vijana wawe na maadili mema, wazazi
wanatakiwa kukaa na watoto wao kuwaelimisha mambo mbalimbali ambayo
yanaweza kuwa na madhara kwao kama alivyofanya Baba Anna na mke wake,
rejea ukurasa wa 10 Baba Anna anapowaambia wenzake, “Hilo
ndilo mie nililofanikiwa mwenzenu. Nimemwambia mama Anna akae na
mabinti zake name nikae na vijana wangu wa kiume. Tumefanya kazi hiyo
kwa makini sana. Tumewaelimisha juu ya madhara ya tabia hiyo kwao
binafsi na kwetu sote. Hatukubakiza kitu.” {Uk. 10}
4. Usaliti
Usaliti
ni dhamira nyingine inayojitokeza katika tamthiliya hii, kwa mfano
mwandishi anaonesha usaliti unaofanywa na Baba Joti kwa mke wake, Baba
Joti anaisaliti ndoa yake kwa kuanzisha uhusiano wa kimapenzi na
mwanamke mwingine, hili linathibitishwa na Mama Anna anaposema, “Lakini leo nimefika kikomo. Ndiyo mwisho wa kumvumilia huyu nguru anayeichimba ndoa yangu.” {Uk. 7}
Usaliti
mwingine, tunaona kwa Joti, pamoja na kwamba Joti anakuwa na mahusiano
ya kimapenzi na Suzi anaamua kumsaliti na kuanzisha mahusiano na
wanawake wengine, mwandishi analithibitisha hili akimtumia muhusika Suzi
anaposema, “Ndiyo maana mie nilikuwa nakataa Joti. Nishaambiwa kwamba unawasichana wengi shuleni na mtaani kwetu.” {Uk. 21}
Usaliti
mwingine unajitokeza kwa Joti na Chausiku, mwandishi anaonesha kuwa
Joti pamoja na kuwa na mahusiano na Chausiku anamsaliti Chausiku kwa
kuwa na mahusiano na wasichana wengine, Joti anapewa vitu na Chausiku
naye anawapa wanawake wengine, rejea ukurasa wa 22, Chausiku anaposema, “Toka
hapa. Nimesikia habari zako. Kila msichana unamtaka tu. Mie nakununulia
fulana ya mazoezi wewe unahonga kinyago chako kile. Bisha...Nikikupa
hela ya kununua peni we unanunulia bazooka visichana vyako.” {Uk.
22} lakini si Joti tu ndiye anamsaliti mwenzake, mwanandishi anatuonesha
kuwa, hata Chausiku pia, anamsaliti Joti kwa kuwa na mahusiano na
wanaume wengine, rejea ukurasa wa 22-23, Mwarami anapomwambia Joti,
“Sasa ndiyo kuparamia mpaka wasichana wakubwa wa mtaani? Fikiri juu ya
Chausiku, Yule msichana mjuvi wa mji ambaye pia anachukuliwa na Yule
mpemba muuza duka.” {Uk. 22-23}
Tukigeukia
katika uhalisia wake, suala la usaliti katika ndoa au mapenzi bado ni
tatizo kubwa sana katika jamii yetu, wanandoa wanasalitiana, wapenzi
wanasalitiana tabia hii ya usaliti huwa ni kichochea kikubwa sana kwa
watu kuambukizana virusi vya ukimwi, kama tunavyoona kwa Joti. Hivyo
jamii iache usaliti.
5. Athari za utandawazi
Mwandishi
pia amejadili suala la utandawazi na athari zake, mwandishi anaonesha
namna utandawazi unavyochangia kwa kiasi kikubwa kuharibu tabia na
maadili ya watoto na vijana, kwa mfano tunawaona akina Joti, Jumbe,
Choggo na Mwarami wanajiingiza katika mahusiano ya kingono wakiwa watoto
wadogo kutokana na kuathiriwa na video za ngono (sinema za X)
wanazozitazama mtaani, mikanda hii ya ngono imekuwa rahisi sana
kupatikana kutokana na utandawazi.
6. Athali za ukoloni na ukoloni mambo leo
Suala la ukoloni na ukoloni mambo leo pia limepewa nafasi katika tamthiliya hii, mwandishi anaonesha namna wakoloni
walivyoharibu utamaduni wetu kwa kuuita ushenzi na hata tulivyopata
uhuru, viongoni wetu wakaendelea kushikilia mawazo hayo potofu ya
kikoloni ambayo kwa kiasi kikubwa tunaangamia wenyewe, hili mwandishi
analithibisha akimtumia Mtambaji anaposema, “Mila
zetu hazikukataza kutoa mafunzo ya elimu ya jinsia...Wakoloni na
vibaraka wao ndio wanaostahili kulaumiwa wakoloni walipiga vita jando na
unyago wakidai eti ni ushenzi.” Mtambaji anaendelea kutuambia tena, “Viongozi wetu nao wakaendeleza mawazo hayo hata baada uhuru bila kutambua kuwa wanajiua wenyewe.” {Uk. 13-14}
7. Nafasi ya mwanamke katika jamii
ü Mwanamke
amechorwa kama mlezi wa familia, mwandishi anatuonesha namna ambavyo
mwanamke anakuwa mlezi mzuri wa familia, anaangaika hapa na pale
kuhakikisha mtoto au watoto wake wanapata mahitaji yote muhimu kama vile
chakula, mavazi na hata elimu, rejea ukurasa 30, Mama Suzi anaposema, “Mimi ninahangaika kukusomesha, wewe unanifanya hivi...Mama yako nimeungua viganja kwa kupika vitumbu ili mwanangu usome.” {Uk. 30}
ü Mwanamke amechorwa kama mtu mwenyemsimamo,
mwandishi anamtumia muhusika Anna kumuonesha mwanamke kama mtu mwenye
msimamo katika maamuzi yake, tunamuona Anna pamoja na kusumbuliwa mara
kwa mara na Mwarami kumtaka kimapenzi bado anashikilia msimamo wake ule
ule wa kumkatalia, hata watu wazima wenye uwezo kipesa wanapomtaka Anna
bado Anna anaonesha kutoyumba kimimamo kwa kuwakatalia. Rejea wimbo
anaoimba Anna ukurasa wa 27,
“Anna Anna Anna mie niacheni mie x2
Msichana mdogo bado nasoma niacheni mie.
Muda wangu kufanya hayo haujafika mie.
Pesa zenu, na lifti zenu niacheni mie.
Anna Anna Anna mie niacheni x2”
ü Mwanamke amechorwa kama mtu anayepinga mabadiliko katika jamii,
mwandishi anatuonesha kuwa mwanamke ni mtu asiyependa mabadiliko katika
jamii, asiyependa kwenda na wakati, dunia inabadilika jamii inatakiwa
kuwaelimisha vijana wao kuhusu elimu ya jinsia na mahusiano ,Mama Suzi
anapinga, rejea Mama Suzi anaposema, “Tena ishia hapo hapo kaka! Huko si kunifundishia mwanangu umalaya? Umfunze mwanangu habari za ngono ilitoka wapi hiyo? {Uk. 9}
ü Mwanamke amechorwa kama mtu asiye na msimamo,
mwandishi anatuonesha kuwa, mwanamke ni mtu asiye na msimamo katika
maamuzi yake, mwandishi anamtumia Suzi, kuijadili nafasi hii, richa ya
Suzi kuamua kuachana na Joti na hata anapogundua kuwa Joti anamahusiano
na wanawake wengine bado anakubali kuendelea naye. (Rejea uk. 17 na 21)
ü Vile vile, mwandishi amemchora mwanamke kama chombo cha starehe,
anamtumia muhusika Joti ambaye anawatumia wanawake ili kujistarehesha
kingono, lakini pia tunaona namna watu wanavyotumia pesa na vitu vya
thamani ili kuwarubuni wasichana wapate kukidhi mahitaji yao ya kingono.
{rejea ukurasa 27}
ü Mwanamke amechorwa kama mtu asiye na elimu juu ya mambo ya jinsia na ukimwi,
katika kuilezea nafasi hii, mwandishi anamtumia muhusika Mama Suzi,
ambaye anaoneka kutokuwa na ufahamu mzuri juu ya masuala ya UKIMWI, kwa
mawazo yake anaamini kuwa ugonjwa wa UKIMWI ni ugonjwa unaowahusu watu
wakubwa tu, na watoto hawawezi kuambukizwa jambo ambalo si sahihi. Hata
katika jamii yetu, wapo watu wanaoamini kuwa ugonjwa huu wa UKIMWI
huwakumba watu wazima watoto na watu walio katika ndoa hawawezi
kuambukizwa virusi vya ukimwi jambo ambalo si kweli. Hivyo jamii
inatakiwa kuelimishwa sana kuhusu ugonjwa huu.
Mfano wa maswali unayoweza kuulizwa sehemu hii
1. Taja maadui sita na fafanua jinsi waandishi wa tamthiliya mbili kati ya ulizosoma walivyojitokeza kupambana na maadui hao.
2. Waandishi
wa tamthiliya wamemchora mwanamke katika sura tofauti. Thibitisha kauli
hii kwa kutumia waandishi wawili (2) wa tamthiliya mbili (2)ulizosoma.
MIGOGORO
Migogoro
ni hali ya kutoelewana baina ya pande mbili, unaweza kuwa mgogoro kati
ya mtu na mtu, mtu na kikundi cha watu, kikundi kimoja na kikundi
kingine cha watu au unaweza kuwa mgogoro wa mtu na nafsi yake.
Katika tamthiliya hii, mwandishi ameweza kuibua na kuonesha migogoro
mbalimbali ambayo kwa kiasi kikubwa migogoro hiyo imeweza kusaidia
katika ujenzi wa dhamira mbalimbali zilizoweza kujitokeza katika kazi
hii, migogoro iliyojitokeza katika tamthiliya hii ni:
ü Mgogoro kati ya Mama suzi na mwanaye,(Suzi)
chanzo cha mgogoro ni Mama Suzi kukuta kasha la vidonge vya kuzuia
mimba kwenye mfuko wa sketi ya Suzi, mgogoro unakua zaidi Mama Suzi
kuamua kumuadhibu kwa kumchapa Suzi hadi anapotokea Mjomba na Baba Anna,
kuamulia mgogoro huo na kushauri jambo la msingi ni kumpa elimu ya
jinsia na si kutumia ukali na viboko, kama ambavyo Baba Anna anasema, “Watoto
wajazwe elimu, waone uchafu na hatari ya kufanya haya. Siyo kuwatia
hofu tu. Je leo ukifa ama kulazimika kuwa mbali nawe? Si atafanya tu
maana mtia hofu hayupo?” {Uk. 13}
ü Mgogoro kati ya Mjomba na Mama Suzi,
chanzo cha mgogoro ni kitendo cha Mjomba kumshauri Mama Suzi kuacha
kumuadhibu Suzi na badala yake apewe elimu ya jinsia na mahusiano ya
kimapenzi jambo linalopingwa na Mama Suzi na hivyo kuibua mgogoro.
{Rejea ukurasa wa 8-14}
ü Mgogoro kati ya Suzi na Joti,
mgogoro huu unaibuka baada ya Suzi kupigwa na mama yake sababu ya
vidonge vya kuzuia mimba alivyopewa na Joti, mgogoro huu unafikia hatua
ya Suzi kuamua kuachana na Joti, suluhisho la mgogoro huu, wanaamua
kurudiana na kuendelea na uhusiano wao. (Rejea uk. 17 na 21)
ü Mgogoro kati ya Mwarami na rafiki zake yaani Jumbe, Joti na Choggo.
Chanzo cha mgogoro ni kitendo cha Mwarami kutokuwa na uhusiano wa
kimapenzi na wasichana, hatua inayosababisha kumtishia kumfukuza katika
kundi lao, rejea ukurasa wa 24, Jumbe anapomwambia Mwarami, “Sasa bwana hapa kwenye grupu letu hatutaki tabia hiyo ya ushamba. La sivyotutakutoa umemba.” Suluhisho la mgogoro huu ni Mwarami kuamua kumshawishi Anna kimapenzi hata hivyo juhudi zake zinagonga mwamba.
ü Mgogoro kati ya Mama Joti na Mwanamke anayedhani anaingilia ndoa yake,
Mama Joti anaona suluhisho la mgogoro huu ni kununua kanga zenye maneno
ya vijembe ili kumpasha na kumuumiza roho, Rejea Mama Joti anaposema, “Lakini
leo nimefika kikomo. Ndiyo mwisho wa kumvumilia huyu nguru anayeichimba
ndoa yangu...Ngoja kwanza nimpashe najua litamuuma tu.” {Uk. 7}
ü Mgogoro mwingine ni kati ya Chausiku na Joti,
chanzo cha mgogoro huu ni baada ya kugundua kuwa Joti anamahusiano ya
kimapenzi na wasichana wengine, mgogoro unafikia hatua ya Chausiku
kumtishia kumdhuru Joti, kama anavyosema, “We
usinifanye mie bwege mwenzio...wewe ndiyo unajigonga gonga. Wewe na
visichana vyako hivyo nitawachoma moto mie! Nyie hamnijui, ohoooo!” {Uk. 22}
ü Mgogoro kati ya ukale na usasa,
huu ni mgogoro mwingine unaojitokeza katika tamthiliya, mwandishi
anaonesha mgogoro kati ya watu wanaokumbatia mambo ya kale, mambo
yaliyopitwa na wakati na wale wanaotaka mabadiliko katika jamii,
mwandishi anawatumia wahusika, Mama Suzi na Baba Joti kama watu
wanaokumbatia mambo ya kale na kwa upande mwingine anawatumia wahusika,
Mjomba, Baba Anna na Mama Anna kama watu wanaotaka mabadiliko katika
jamii, wanataka ukuta unaowatenga watoto na wazazi wao wasipate elimu ya
jinsia ubomolewa, mwandishi anaonesha kuwa, kukumbatia mambo ya kale
kunaweza kuleta madhara kwa vijana kama madhara ya kupata mimba kwa
Suzi, rejea Suzi anaposema, “Mama
hakuwa radhi kuachana na utamaduni wa kale wa kuweka ukuta baina ya
wazazi na watoto katika kujadili mambo haya. Haya ndiyo madhara yake.” {Uk. 36}
ü Mgogoro wa Suzi na nafsi yake,
chanzo cha mgogoro huu ni kitendo cha kuambiwa na mama yake kuwa
shangazi yake ataenda kumpima mimba, Suzi anaona suluhisho la mgogoro
huu ni kutokubali kwenda kupimwa mimba na shangazi yake na badala yake
kumtafuta mwanaume anayehusika na mimba hiyo (Joti) kuzungumza naye, rejea Suzi anaposema, “Oh
Mungu wangu! Nifanye nini sasa? Siwezi kumruhusu shangazi
akanipime...oh, nifanye nini mie! Nimtafute Joti, lazima niongee naye.” {Uk. 31}
ü Mgogoro mwingine unaojitokeza ni mgogoro wa Suzi na nafasi yake
kama ameambukizwa virusi vya Ukimwi au la, chanzo cha mgogoro huu ni
baada ya Suzi kugundua kuwa ana mimba na kijana aliyempa hiyo mimba
ameathirika na virusi vya ukimwi, rejea Suzi anaposema, “Na mie Suzi nina mimba, mimba ya Joti. Kasha ina maana na mie nina ukimwi?” {Uk. 36}
UJUMBE
Ujumbe
ni funzo analolipata fanani anaposoma ama kusikiliza kazi za fasihi,
pamoja na ujumbe pia kuna maadili mbalimbali hupatikana, katika
tamthiliya hii kuna mafunzo mbalimbali ambayo msomaji wa kazi hii
anaweza kuyapata, mafunzo hayo ni kama:
ü Elimu
ya jinsia na ukimwi ni muhimu kwa vijana ili kuwanusuru vijana na mimba
za utotoni(mimba zisizotarajiwa) na maambukizi ya virusi vya ukimwi.
ü Ukimwi hauchagui rika, mwandishi anatupa ujumbe kuwa gonjwa hili la UKIMWI hauchagui mtu,
kila mtu anaweza kuupata, kama tunavyoona kwa Fausta na Joti, ni watoto
wadogo lakini wanaathirika na virusi vya ukimwi na kusababisha vifo
vyao.
ü Asiyefunzwa na mama yake, hufunzwa na ulimwengu,
hili ni funzo linguine tunalilipata katika tamthiliya, mwandishi
anatufundisha umuhimu wa wazazi kuwafundishi watoto wao maadili mema na
si kuwaacha watoto wakajifunza wenyewe mtaani, wakiwaacha hivyo, huko
hujifunza mambo yasiyofaa, tunaona kwa Suzi, Joti, Mwarami, Choggo,
Jumbe, wazazi wao hawakuwafundisha elimu ya jinsia na mahusiano watoto
wakajifunza wenyewe mambo machafu na hataimaye yakawaletea madhara.
ü Wazazi ndiyo walimu bora kwa malezi bora na maadili mema kwa watoto wao.
Mwandishi anaendelea kutufundisha kuwa, ili vijana wetu wawe na tabia
njema, mzazi ni mwalimu bora kabisa anayeweza kumfundisha mtoto wake
vema, rejea mwandishi akimtumia muhusika Baba Anna anaposema, “Dunia imeharibika bwana. Mzazi usipomfunza, walimwengu watamfundisha tena sasa si maadili mema bali njia potofu.”
ü Kinga ni bora kuliko tiba.
Ni vizuri jamii ikajikinga na magonjwa mbalimbali, kuliko kutojikinga
na baadaye kuanza kutafuta tiba, tiba huwa gharama sana kuliko
kujikinga, tunamuona Baba Joti akitumia gharama kubwa kutafuta tiba ya mtoto wake, kama ambavyo mwandisha anasema, “Mtani ushauza rasilimali zako kuuguza mtoto. Ushajitia umskini kwa kuhangaika...”
{Uk. 34} Hivyo basi ni vema jamii ikaamua kujikinga dhidi ya matatizo
mbalimbali kwani matatizo hayo pindi yanapokukumba huwa ni gharama sana
kuyatatua na wakati mwingine matatizo mengine huwa hayana tiba kama
tunavyoona katika ugonjwa wa UKIMWI.
ü Ngono zembe ni chanzo cha maambukizi ya virusi vya ukimwi na mimba zisizotarajiwa,
Tunamuona Joti akiambukizwa virusi vya ukimwi kutokana na kushiriki
ngono zemba, vilevile tunamuona Suzi akipata mimba na hata kuwa katika
wasiwasi wa kuambukizwa virusi vya UKIMWI kutokana na kushiriki ngono
zemba. (Rejea ukurasa wa 4 na 34)
Mafunzo mengine tunayoyapata katika tamthiliya hii ni pamoja na:
ü Jamii inatakiwa kubadilika ili kwendana na mabadiliko katika jamii.
ü Mila na desturi zilizopitwa na wakati hatuna mudi kuachana nazo
ü Huwezi kumtambua mtu aliyeathirika na virusi vya ukimwi kwa kumtazama kwa macho tu. Uk. 4-5
ü Vijana waelimishwe namna ya kukabiliana na changamoto za utandawazi.
ü Utandawazi ni chanzo cha mmong’onyoko wa maadili ya vijana.
ü Malezi bora ni muhimu kwa watoto/vijana ili kuwa na maisha bora baadaye.
ü Majuto ni mjukuu, tunamuona Suzi akijuta kutokana na kutopata elimu ya jinsia na hivyo kujikuta akitumbukia katika matatizo.
MATUMIZI YA LUGHA
Mwandishi
ametumia lugha ya kawaida, sentensi fupifupi na inayoeleweka kwa
urahisi,pamoja na hayo mwandishi pia ametumia lugha ya kisanaa yenye
mbinu mbalimbali za kisanaa kama vile nahau na tamathari za semi.
(a) Matumizi ya methali
ü “Mzazi usipomfunza, walimwengu watamfundisha.” Uk.
ü “Shukrani ya punda mateke.” {Uk. 19}
(b) Matumizi ya misemo na nahau
ü Shoga, mtakatifu wa kwenye mwanga si lazima awe mtakatifu gizani. {Uk. 4}
ü “Kakanyaga nyaya.” {Uk. 4}
ü “Potelea kwao...” uk. 9
ü “Makapera kibao, mume wangu wa nini. Uk. 7
ü “Wembamba wa reli treni inapita, uk 6
ü Kifua simkingii, maana siwi naye. Uk 6
ü “Kwa mashairi nimekuvulia kofia siku nyingi.” Uk.6
ü “We pita juu mie nipite chini...”uk 19
ü Mbona umetuanika juani. Uk 16
ü “Hakikisha ndege mjanja ananasa katika tundu bovu.” Uk. 24
(c) Matumizi ya taswira/lugha ya picha
ü Dubwana, Manaa yake ni kitu au mtu mwenye umbo kubwa lisilo la kawaida au la hovyo hovyo, mwandishi ametumia neno dubwana kitaswira kuufananisha ugonjwa wa Ukimwi sawa na jambo linalotisha, kuogopesha. (Rejea ukurasa wa 1-2)
ü Gizani,
gizani ni mahali pasipokuwa na mwanga, hivyo mwandishi ametumia neno
giza, akimaanisha kukosa maarifa au kutokuwa na ufahamu ya jambo fulani,
kwa kifupi kukosa elimu, Rejea mtambaji anaposema, “Kisiwa kizima kipo gizani...watoto ndio kabisa. Wapo katika giza nene.” {Uk. 13}
(d) Matumizi ya tamathali za semi.
(i) Tashibiha, hizi
ni tamathari ambazo hulinganisha vitu kwa kutumia viunganishi kama,
mfano wa, sawa na, mithili ya, kama vile. N.k. baadhi ya tashibiha
zinazojitokeza katika tamthiliya hii ni:
ü “Wewe nawe unakuwa nyuma nyuma kama koti.” Uk. 4
ü “Shoga mbona unakuwa mgumu kama mpingo?” uk. 5
ü “Watu walipukutika, wakapukutika kama majani ya kiangazi.” Uk.1
ü “Lile Dubwana limetanda kama utando wa buibui.” {Uk.13}
ü “Miti inayoungua kama mabua.” Uk. 6
(i) Sitiari, hizi ni tamathari za semi ambazo hulinganisha vitu bila kutumia viunganishi, mfano wa tamathali zilizotumika ni pamoja na:
ü “We mbwa mweusi.” Uk. 8
ü “Nyoka wee.” Uk.9
(ii) Mjalizo, hii
ni aina ya tamathali za semi ambazo msanii/mwandishi huitumia kutaja
vitu au mambo yaliyo katika orodha bila kutumia viunganishi. Mfano:
ü “...Lakini soma maneno yake. Yamejaa kejeli, ushari, uchimvi, kusengenyana na kufumbiana mafumbo ya kila aina.” Uk. 6
(iii) Nidaa, hizi ni tamathali za semi, zinazoonesha hali ya kushangaa au kushangazwa na jambo Fulani, mfano wa tamathali hizi ni:
ü “Ai, ai, lahaula lakwata...weye, hiki kitoto?” {uk. 9}
ü “Oi, oi, oi, toba! Kile si kitoto kama cha kwangu...” {uk.10}
(iv) Takriri,
hii ni hali ya kurudiarudia maneno, neno, silabi au sauti zinazolingana
katika kazi ya fasihi ili kusisitiza au kutia mkazo jambo fulani. Mfano
wa takriri zinazojitokeza katika tamthiliya hii ni:
ü “Watu walipukutika, wakapukutika kama majani ya kiangazi. Wakapukutika.” Uk. 1
ü “Waongo! Waongo wakubwa.” Uk. 3
ü “ Vifo vikawazoa, vikawazoa...vikawazoa.” uk. 2
ü “Piga domo, piga doma, nikashinda.” Uk. 16
(v) Tanakali sauti
Hii ni aina ya tamathali ambayo sauti ya kitu fulani huigwa ili kwa
lengo la kuburudisha au kuipa dhamira uzito falani. Mfano wa tanakali
sauti zilizotumika katika tamthiliya hii ni:
ü “Wacha moyo unipwite pwi,pwi,pwi...” uk.16
(vi) Tashititi Hii
ni aina ya tamathari ya semi ambayo mtu huuliza swali huku jibu lake
akilifahamu, mfano wa tashititi zinazojitokea katika tamthiliya hii ni:
ü “Huyu ni Suzi kweli au nani?” uk.15
Mfano wa maswali unayoweza kuulizwa sehemu hii
1. Lugha
ni kipengele muhimu sana kwa mwandishi katika kufikisha ujumbe wake kwa
jamii. Jadili kauli hii kwa mifano toka katika tamthiliya mbili
ulizosoma.
MTINDO NA MUUNDO
(a) Mtindo
Mtindo
ni jinsi msanii anavyotumia ufundi, umahiri na hisia zake katika
kutenda au kueleza jambo fulani katika kazi ya fasihi, na mtindo ndiyo
huweza kumtofautisha msanii/mwandishi mmoja na mwandishi mwingine.
Mtindo hutumika kuipamba kazi ya fasihi, baadhi ya mitindo nayotumika
katika kazi hii ni pamoja na:
ü Matumizi ya hadithi ndani ya tamthiliya
Mwandishi
ametumia mtindo wa hadithi ambao ni utanzu wa fasihi simulizi ndani ya
tamthiliya, mtindo huu unajidhihirisha ukurasa wa kwanza, Mtambaji
anapoanza kusimulia hadithi anaposema, “Paukwa” na hadhira inaitikia “Pakawaaaaaaa” na Mtambaji anaendelea, “Hapo zamani za kale paliondokea kisiwa kimoja...” {Uk. 1} Ni utanzu wa hadithi pekee ndiyo huwa na mwanzo wa namna hiyo.
ü Matumizi ya wimbo/shairi ndani ya tamthiliya
Mwandishi
pia ametumia wimbo kuipamba kazi yake, wimbo unajitokeza ukurasa wa 27
Anna anaimba wimbo unaowataka wanaume wanaomtaka kimapenzi kuacha
kumfuatafuata, muda wake wa kujihusisha na mahusiano ya kimapenzi
haujafika bado mwanafunzi.
“Anna Anna Anna mie niacheni mie x2
Msichana mdogo bado nasoma niacheni mie.
Muda wangu kufanya hayo haujafika mie.
Pesa zenu, na lifti zenu niacheni mie.
Anna Anna Anna mie niacheni x2”
ü Matumizi ya lugha ya majibizano/dialojia na masilmulizi
Kama
ilivyo ada, mtindo wa lugha unaotumika katika tamthiliya, kwa asilimia
huwa ni mtindo wa majibizano, yaani dialojia. Hivyo basi hata katika
tamthiliya hii, mwandishi kwa kiasi kikubwa ametumia mtindo wa
majibizano na kidogo ametumia masimulizi, (Rejea masimulizi ya Mtambaji
ukurasa wa 1-2, 3-4, na 36)
ü Matumizi ya nafsi zote tatu
Pia nafsi zote tatu zinajitokeza katika tamthiliya hii,
ü Nafsi ya kwanza, mfano,Mimi nawashangaa... {Uk. 6} Najua litamuuma tu (uk.7), Tumebomoa ghala imara...” {Uk. 6}
ü Nafsi ya pili, mfano, “Utamaliza kanga zilizoandikwa kila aina ya maneno...”
Wewe unamwona Fausta alikuwa mdogo?
ü Nafsi ya tatu, mfano, ...alikufa kwa ukimwi” uk. 9, atakutafuta tu mwenyewe.” (uk 17), “Wanashindwa kutofautisha kati ya puto na kondomu.” (Uk. 13)
ü Matumizi ya picha,
mwandishi pia ametumia michoro mbalimbali inayoonesha matendo/matukio
mbalimbali ya wahusika, picha hizi zimesaidia sana kuipamba na
kuipendezesha kazi yake, picha hizo zinapatikana ukurasa wa
3,5,8,11,17,20,23,27, 29 na 35.
(a) Muundo
Muundo
ni mfuatano wa masimulizi au visa katika kazi ya sanaa ya fasihi, hivyo
basi.muundo wa tamthiliya hii ni wa moja kwa moja, yaani visa vyake
vimepangwa kuanzia kisa cha kwanza , kati hadi mwisho, katika kuvipanga
visa vyake, mwandishi ameigawa kazi yake katika sehemu sita, ambazo
amezipa majina, Sehemu ya kwanza, Sehemu ya Pili, ya Tatu, ya Nne, Tano
na Sehemu ya Sita.
Sehemu ya kwanza.
Mtambaji anasimulia habari za Dubwana(Ukimwi),
anasimulia namna wakubwa wanavyoelimishana namna ya kujilinda na
ugonjwa huo, huku wakiwaacha watoto wakiangamia kwa kukosa elimu ya
jinsia na ukimwi.
Sehemu ya Pili
Hapa
mwandishi anatuonesha nyumbani kwa Mama Suzi, Mama Suzi na Mama Joti
wanapeana habari za kifo cha Fausta kilichosababishwa na ukimwi, Mama
Suzi anakuta kasha la vidonge kwenye mfuko wa sketi ya Suzi wakati
akifua jambo linalozua mgogoro kati ya Suzi na mama yake, Mjomba na Baba
Anna wanamshauri Mama Suzi kuacha kutumia ukali na badala yake
anatakiwa kumpa elimu ya jinsia binti yake ili ajitambue jambo
linalopingwa vikali na Mama Suzi.
Sehemu ya Tatu
Hapa
mwandishi anatuonesha mtaani, Joti anakutana na Suzi, Suzi anaamua
kuachana na Joti kwa sababu ya vidonge vya kuzia mimba alivyopewa na
Joti kumsababishia kupigwa na mama yake. Joti anawasimulia wenzake namna
alivyofanikiwa kumpata Suzi, Joti, Jumbe, Choggo na Mwarami wanaenda
mtaani kuangalia sinema za X.
Sehemu ya Nne
Tukio
linatendeka njiani, Joti na Suzi wanakutana, Suzi anamlaumu Joti kwa
kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wasichana wengine, wanaamua kurudisha
uhusiano wao, Joti anaanza kujisikia vibaya, Jumbe anaamua kumpeleka
nyumbani, Mwarami anaonekana akimshawishi Anna amkubalie ombi lake la
kuanzisha mahusiano ya kimapenzi, Anna anaonesha msimamo anamkatalia,
mwandishi pia anatuonesha namna Anna anavyoshinda vishawishi vya
kingono.
Sehemu ya Tano
Tukio
linatendeka chumbani kwa Suzi akiwa na Anna, Suzi anajisikia vibaya,
anahisi huenda ana mimba, anataka kuitoa, rafiki yake Anna anamshauri
kuachana na mpango huo kwani ni hatari, anaamua kwenda kwa Joti
kuzungumza naye suala hilo.
Sehemu ya Sita
Hii
ni sehemu ya mwisho, mwandishi anatuonesha nyumbani kwa Baba Joti,
tunaona namna Baba Joti alivyoangaika kwa waganga mbalimbali kutafuta
tiba ya Joti bila mafanikio, mwisho wanaamua kumpeleka hospitali, huko
wanapata wajibu kuwa Joti amethirika na virusi vya ukimwi, Jirani
anamshauri Baba Joti kumpeleka Joti kwa mganga mwingine, Mjomba
anamshauri Baba Joti kuachana na mpango huo kwani ugonjwa alionao Joti
hauna tiba wala dawa. Suzi anawasili kwa akina Joti anagundua Joti ana
ukimwi, Joti anafariki dunia, Suzi anakuwa na wasiwasi kama naye atakuwa
ameambukizwa virusi vya ukimwi, anabaki akijutia kwa kukosa elimu ya
jinsia na ukimwi. Na mchezo unaishia hapo.
MANDHARI
Mandhari
ni sehemu au eneo ambalo visa na matukio hutendeka katika kazi ya
fasihi, katika kazi ya fasihi mandhari huweza kuwa mandhari halisi au ya
kubuni, katika tamthiliya mwandishi ametumia mandhari ya kubuni, hivyo
basi, mandhari ya tamthiliya hii yanaweza kuwa sehemu yoyote ile katika
nchi za Kiafrika. Pia mwandishi anatuonesha visa na matukio yakitendeka
mandhari ya nyumbani, mtaani, njiani n.k.
Mandhari ya nyumba
Katika
mandhari ya nyumbani, tunaona nyumbani kwa Mama Suzi na Nyumbani kwa
Baba Joti, kwa Mama Suzi tunaona ukuta uliowekwa kati ya mzazi na mtoto
kuhusu elimu ya jinsia kwa mtoto, Mama Suzi anamuadhibu Suzi kwa kukuta
vidonge vya kuzuia mimba kwenye mfuko wa sketi ya Suzi, Suzi anaanza
kujisikia vibaya, anafikiria kuitoa mimba. Nyumbani kwa Baba Joti,
tunaona kuumwa kwa Joti, kugundulika kuwa ana ukimwi na kufariki kwake.
Hivyo
mwandishi ametumia mandhari hii, ili kufikisha dhamira ya umuhimu wa
elimu ya jinsia kwa watoto, malezi bora ya mtoto, tatizo la ugonjwa wa
ukimwi na athari zake katika familia, n.k.
Mandhari ya Mtaani
Katika
mandhari haya, mwandishi, anatuonesha Joti na Suzi wakiwa katika
mazungumzo ya uhusiano wao wa kimapenzi, pia tunaoneshwa kuwa ni mahali
ambapo Joti na wenzake hukutana na kupanga mambo yao ya mapenzi.
Mwandishi anatumia mandhari haya, kuonesha namna watoto
wanavyoharibikiwa kitabia mtaani, mandhari ya njiani inatuonesha namna
watoto wakike wanavyosumbuliwa na wanaume wasiokuwa waadilifu ambao
huwataka kimapenzi.
Mfano wa maswali unayoweza kuulizwa sehemu hii
1. Jadili jinsi fani ilivyotumika kukamilisha kazi za waandishi wawili wa tamthiliya ulizosoma ukizingatia mtindo na mandhari.
FALSAFA, MTAZAMO NA MSIMAMO WA MWANDISHI
(a) Falsafa ya mwandishi
Falsafa
ni mchujo wa mawazo ya mwandishi kuhusu maisha na jamii yake. Falsafa
ya mwandishi wa tamthilia hii anaamini kuwa, ili jamii yoyote ile iweze
kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii husika, elimu
ni nyenzo muhimu sana ya kupambana na changamoto hizo. Na elimu hiyo
isitolewe kimatabaka.
(b) Mtazamo wa mwandishi
Mwandishi
ana mtazamo wa kiyakinifu, ana mtazamo kuwa, matatizo yote yanayotokea
katika jamii chanzo ni jamii yenyewe na jamii yenyewe ndiyo inayotakiwa
kukabiliana na matatizo hayo, na ndiyo maana anaitaka jamii yake
ibadilike.
(c) Msimamo wa mwandishi
Mwandishi
ana msimamo wa kimapinduzi, kwani anaitaka jamii yake ibadilike ili
kuendana na wakati, na anaitaka jamii kuachana na mila na desturi
zilizopitwa na wakati ili kukabiliana na changamoto zinazoikabili jamii.
JINA LA KITABU
Jina la kitabu au tamthiliya hii ni Kilio Chetu,kilio
chetu ina maana ya tatizo, balaa au janga linapoingia katika jamii ni
letu sisi sote. Hivyo basi, jina la kitabu Kilio Chetu linasadifu sana
yaliyomo katika tamthiliya hii. Tukianza na:
Tatizo la ukimwi
Mwandishi anajadili ukimwi kuwa ni ugonjwa hatari sana, ni ugonjwa usiobagua mkubwa wala mtoto, kama mwandishi anavyosema, “Ukimwi hauchagui mkuwa wala mdogo.”
{Uk. 25} hii inathibitisha kuwa tatizo hili la ukimwi ni letu sote
tunatakiwa wote kupambana nalo, na hapa ndipo linapokuja suala la Kilio Chetu.
Elimu ya jinsia
Mwandishi
pia anaonesha kuwa suala la watoto/vijana kupewa elimu ya jinsia na
ukimwi ni kilio cha jamii, jamii inasisitiza na kupigia kelele suala la
vijana kupewa elimu ya jinsia na ukimwi, kwa mfano, mwandishi anamtumia
muhusika Baba Anna anaposema, “Mimi bwana nitaendelea kusisitiza juu ya
elimu hii.” Mwandishi anaendelea kwa kusema akimtumia muhusika Mjomba,
“Tutaendelea kuwaelimisha wazazi umuhimu wa elimu hii.” {Uk.12} Hivyo tunaona kuwa Baba Anna na Mjomba wanatoa kilio chao cha kutaka watoto kuelimishwa elimu ya jinsia.
Si
vivyo tu, hata vijana wenyewe, wanapaza sauti, wanatoa kilio chao
kutaka kupewa elimu hii ya jinsia na ukimwi, mwandishi anatuonesha kuwa
kama vijana wangepata elimu hii wasingeatwa na matatizo, kama anavyosema
Suzi, ““Naapa kwa Mungu wangu, mimi na Joti tungepata bahati ya kuelimishwa, tusingetumbu...” {Uk. 36} Pia rejea Mtambaji anaposema, “Watoto hawana uwezo wa kukabiliana nalo...Sikieni kilio chetu!” {Uk. 15}
Hivyo
basi, kwa ushahidi huu ni wazi kuwa, jina la kitabu linasadifu yale
yote yanayozungumzwa katika tamthiliya hii, na kwa hili mwandishi
amefanikiwa sana.
KUFAULU NA KUTOFAULU KWA MWANDISHI
(a) Kufaulu kwa mwandishi.
Hapa tunaangalia kufanikiwa kwa mwandishi katika vipengele vya fani na maudhui, Kifani mwandishi amefanikiwa sana, tukianza na:
Wahusika
Mwandishi
amefanikiwa kuwajenga wahusika wake vizuri, amewajenga wahusika katika
rika tofauti tofauti na kila rika amefanikiwa kuwavisha uhusika
unaendana na rika husika, na amafanikiwa kuonesha namna kila rika
linavyoweza kuathiliwa na UKIMWI na kuitaka jamii kutoa elimu ya jinsia
kwa kila rika.
Lugha
Mwandishi
amefanikiwa kuifanyanga lugha yake kiufundi, amefanikiwa kutumia lugha
nyepesi inayoeleweka na kila mtu inayoambatana na matumizi ya methali,
misemo/nahau na tamathali za semi, matumizi yote haya ya lugha
yamesaidia kwa kiasi kikubwa kufikisha ujumbe uliokusudiwa na kuipamba
kazi husika. (Rejea kipengele cha Matumizi ya lugha)
Mtindo,
katika suala la mtindo, mwandishi amefanikiwa kwa kiasi kikubwa sana,
kwani amefanikiwa kutumia utanzu wa hadithi na wimbo kuipamba kazi yake
na ikawa kazi ya kuvutia na inayovuta hisia za msomaji kupenda kuendelea
kukisoma kitabu hiki zaidi na zaidi. (Rejea kipengele cha Mtindo)
Muundo
Mwandishi
ametumia muundo rahisi, muundo unaeleweka kwa urahisi na hivyo
kumsaidia mwandishi kufikisha ujumbe alioukusudia kwa jamii husika, visa
vyake amevipangalia vizuri hali inayomfanya msomaji apende kuendelea
kukisoma kitabu hiki ukurasa mmoja hadi mwingine hadi anakimaliza kitabu
hiki.
Kwa upande wa maudhui, mwandishi amefanikiwa kuonesha dhamira mbalimbali ambazo kwa kiasi kikubwa zina uhalisia katika jamii yetu. (Rejea dhamira)
Vilevile, kwa upande wa ujumbe, mwandishi amefanikiwa
kutupa ujumbe au mafunzo muhimu sana ambayo kama jamii itayazingatia
basi mafunzo haya yanaweza kuwasaidia sana. (Rejea Kipengele cha ujumbe)
Migogoro,
mwandishi amefanikiwa kuibua migogoro, kuonesha chanzo, upeo na hata
baadhi ya migogoro amefanikiwa kuitolea suluhisho. (rejea kipengele cha
Migogoro)
(b) Kutofaulu kwa mwandishi
Kutofaulu
kwa mwandishi tunaangalia mapungufu tunayokutana nayo katika kazi ya
fasihi, hivyo basi, kama ilivyo kawaida huwa hakuna kizuri kisichokuwa
na kasoro, hivyo hivyo katika tamthiliya hii, tunakutana na baadhi ya
kasoro ambazo si nyingi, baadhi ya kasoro hizo au mapungufu ni pamoja
na,
ü Mwandishi ameshindwa kutuonesha mwanamke aliyemuambukiza Joti virusi vya UKIMWI.
ü Mwandishi
pia ameshindwa kutuonesha hatima ya akina Jumbe na Choggo kama nao
waliathirika na UKIMWI au la, maana hawa wote matendo yao alikuwa
yanafanana tu na Joti.
ü Mwandishi ameshindwa kutuambia alipo baba yake, kama amesafiri au amefariki.
ü Mwandishinpia
ameshindwa kuonesha umuhimu wa watu kujitokeza kupima afya zao, kwa
mfano Suzi anaoenesha kuwa na wasiwasi kama naye ameambukizwa au la,
mwandishi alitakiwa aoneshe Suzi anaamua kwenda kupima afya yake.
Mfano wa maswali unayoweza kuulizwa sehemu hii
1. Ukitumia vitabu viwili vya tamthiliya, jadili jinsi waandishi wa vitabu hivyo walivyofanikiwa kifani na kimaudhui.
Mwandishi ni Mwalimu Shule ya Sekondari Mwanzi-Manyoni (Singida) anapatikana kwa namba zifuatazo: