UCHMBUZI WA DIWANI CHUNGU TAMU, MWANDISHI: THEOBALD MVUNGI
KITABU: CHUNGU TAMU
MWANDISHI: THEOBALD MVUNGI
WACHAPISHAJI: TPH
MWAKA: 1985
UTANGULIZI
Chungu Tamu
ni diwani iliyoandikwa na Theobald
Mvungi miaka ya 1980. Katika diwani hii mwandishi
anaimulika jamii na kuichunguza kwa makini. Anakosoa na kutoa mapendekezo ili
wananchi waondokane na machungu yanayowaandama na kuonja utamu ambao
utawafikisha kwenye kheri. Katika diwani hii mwandishi ameonesha dhahiri jinsi
Uchungu na Utamu vinayotangamana katika harakati zote za maisha ya mwanadamu.
Kwa ufupi, tunaweza kusema kuwa diwani hii ni kipaza sauti kinacholia kwa sauti kali kuujulisha ulimwengu
juu ya uchungu unaoiandama jamii yetu ya Tanzania .
MAUDHUI
DHAMIRA KUU; UJENZI YA JAMII MPYA
Suala la ujenzi wa jamii mpya limezishughulisha fikra za wanafasihi wengi hapa Tanzania . Jamii endelevu ni jamii mpya
ambayo haina ubaguzi, matabaka, uongozi mbaya, yenye kufuata misingi ya haki na
usawa. Jamii iliyojikomboa katika Nyanja zote yaani kiuchumi,
kisiasa, kiutamaduni na kifikra.
Wanafasihi wa Afrika wanaitaka jamii hiyo ijengwe kwa kufuata misingi ya haki
na usawa kwa kila mtu. Wameonesha dhahiri kuwa jamii iliyoachwa na wakoloni
ilikua imeoza na hivyo zinahitajika juhudi kubwa ili kuondoa uozo huo.
Nchini Tanzania
suala la jamii endelevu lilianza mara tu baada ya kupata uhuru na
kuimarishwa zaidi wakati wa Azaimio la Arusha. Watanzania walitaka wajenge
jamii yenye kufuata misingi ya haki na utu, jamii isiyokuwa na matabaka, jamii
yenye viongozi waliotakasika, jamii yenye demokrasia ya kweli, jamii isiyo na
unyonyaji wa aina yoyote ile, jamii
ambayo hatamu za uongozi zingekuwa mikononi mwa wakulima na wafanyakazi, jamii
isiyo na dhuluma ya aina yoyote, n.k.
Hadi mwandishia
anaandika diani hii anaonyesha kuwa
jamii bado haijafanikiwa kuifikia
lengo la kujenga jamii mpya.
Mwandishi
ameonesha vikwazo mbali mbali vinavyokwamisha ujenzi wa jamii mpya
na endelevu hapa nchini na mbinu za kujikwamua kutoka kwenye vikwazo hivyo.Mwandishi ametoa mapendekezo ambayo anaamini kuwa endapo
jamii itayafuata itafanikiwa kuijenga
jamii mpya na endelevu. Mbinu hizo ndizo dhamira ndogo ndogo
za diwani hii kama ifuatavyo;
1. KUPINGA DHULUMA
Dhuluma ni tendo lisilo la haki, tendo la uonevu,
ukatili au uovu. Dhuluma hupingana na haki. Suala la dhuluma hurudisha nyuma
maendeleo ya jamii na hivyo ni kikwazo kikubwa cha ujenzi wa jamii endelevu.
Suala la dhuluma limemshughulisha sana mwandishi wa diwani hii,katika shairi la “ Chatu na kuku” ubeti wa mwisho mwandishi anasema;
Basi
babu akatua akatua,
Funda akajimezea,
Mimi tama imejishikia,
Huzuni imenisaliti,
Kwa chatu kukosa dhati,
Ndipo nikapanga hizi beti,
Ziwe kama ndiyo hati
Ukumbusho wa huyu dhulumati .
Katika shiri la “Chatu na Kuku”, mwandishi amelijenga kitaswira
kuonesha jinsi wakoloni (chatu) walivyoingia Afrika na kuendeleza dhuluma.
Chatu amewakilisha wakoloni na kuku anawakilisha wananchi (Waafrika)
walioonyonywa na kudhulumiwa na wakoloni. Mayai ya kuku yanawakilisha mali
ghafi waliyodhulumu wakoloni kutoka hapa Afrika.
Katika shairi la “Chanzo ni Wenye Kauli”, mwandishi
anaonesha jinsi ulanguzi unavyosababisha dhuluma katika jamii. Ameonesha kuwa
chanzo cha ulanguzi ni upungufu wa bidhaa muhimu, tamaa, pamoja na uzembe toka
kwenye vyombo vya dola. Ulanguzi husababisha rushwa, magendo na hivyo haki haitendeki
katika jamii.
Mwandishi
anasema;
“Mianzo tukiijua,
Mipango tujipangia,
Kmwe pasiwe na njia,
Ulanguzi kurudia,
Iwe tu twahadithia,
Mithili historia”.
Katika
shairi la “Kademokrasia Katoweka”mwandishi anasema;
Ya msiba atayetamka,
Udikteta waja haraka,
Mtemi na walomzunguka,
Wawatia raia mashaka,
Dhuluma yatangazwa fanaka.
Mwandishi anaonesha jinsi wananchi wanavyodhulumiwa demokrasia yao ya kutoa
maoni yao hadharani. Demokrasia inapokosekana, dhuluma ya kutawala kwa mabavu
huendelezwa.
Katika shairi la “Wengine Wabaki Taabuni”, mwandishi anajadili juu ya
dhuluma wanayoiendesha wakubwa dhidi ya watu wa tabaka la chini. Ameonesha kuwa
majambazi wanayo idhini ya kufanya kila jambo kwa wanyonge, kwani hayo majambazi
hulindwa na wakubwa. Anaendelea kueleza kuwa dhuluma inayoendeshwa na
majambazi hapa nchini ni njama za
walinzi (vyombo vya dola).
Anasema;
“Majabazi wanayo idhini,
Kufanya lijalo akilini,
Na hawataingia nguvuni,
Maana walinzi wamo njamani,
Tabu yaanzia kileleni.”
Mwandishi
anaeleza kuwa tabu inaanzia kileleni
maana yake ni tabu au dhuluma inaanzia kwa wakubwa. Hivyo ili tufanikishe
suala la ujenzi wa jamii mpya ni lazima
tujitoe mhanga kupambana na kila aina ya dhuluma katika jamii.
2. KUFANYA KAZI KWA BIDII
Uzembe na
kutowajibika ni kikwazo kikubwa kinachokwamisha maendeleo ya jamii yoyote sile.
Jamii yoyote ile yenye viongozi wazembe, viongozi wasiowajibika au wananchi
wasiojua wajibu wao daima itabaki nyuma kimaendeleo. Mwandishi anaitaka jamii
yetu ijue umuhimu wa kazi na kuwajibika katika suala zima la maendeleo.
Mashairi kadhaa katika diwani hii yanasisitiza kuhusu umuhimu wa kufanya kazi
ili kuleta maendeleo ya jamii. Mashairi haya ni kama vile “Daktari Askari” (UK
11-24), “Chanzo ni Wenye Kauli” (UK 27-28), “Wimbo Wake Hotubani” (UK 28-29)
pamoja na lile la “Wengine Wabaki Taabuni” (UK 32-32).
Katika shairi
la “Daktari Askari”, mwandishi anaonesha jinsi waganga wanavyojua umuhimu wa
kuwajibika katika kazi yao ya utabibu. Ameonesha kuwa wale waganga
waliwahudumia majeruhi kwa bidii wakati wa vita. Hivyo kila mtu anatakiwa
kuwajibika kama wale waganga ndipo tutaweza kulisukuma mbele gurudumu letu la
ujenzi wa jamii endelevu.
Katika
shairi la “Chanzo ni Wenye Kauli” mwandishi anaonesha utekelezaji na
uwajibikaji mbovu unavyosababisha rushwa, magendo na ulanguzi katika jamii
yetu. Katika shairi hili mwandishi ameonesha dhahiri kuwa uzembe toka kwenye
vyombo vya dola ndio umechangia uwajibikaji kuwa mbovu. Anasema;
“Chombo hiki
kuzembea,
Chanzo
kilichozidia,
Magendo
kuyatetea,
Watu
kuwasaidia,
Chombo
kilididimia.”
Katika
shairi la “Wimbo Wake Hotubani” mwandishi anaonesha utekelezaji mbaya wa maazimio unavyochangia kuzorota kwa
maendeleo ya jamii yetu. Katika shairi hili, mwandishi ameonesha kuwa viongozi
wetu wametuna ofisini na shambani hawingii, wanatumia madaraka vibaya, maagizo
ni midomoni bila utekelezaji, kila siku-mchana kutwa wanakunywa na kulewa, n.k.
Utekeleaji wao uko kwenye hotuba! Mwandishi anasema;
“Cheo kiko
mkononi,
Agizo li
mdomoni,
Mchana kutwa
ndotoni,
Wimbo wake
hotubani,
Raia kazi
fanyeni.”
Katika shiri
la “Wengine Wabaki Taabuni”, mwandishi anaonesha jinsi uzembe kazini,
kutowajibika ipasavyo, usaliti pamoja n rushwa unavyorudisha nyuma utekelezaji
mzuri wa maazimio tunayojiwekea. Kwa ujumla mshairi anaitaka jamii ifahamu na kutambua umuhimu wa kazi na wajibu
wa kila mmoja katika jamii ndipo tutaweza kufanikisha kuijenga jamii mpya.
I.
KUWA
KIONGOZI MZURI
Suala la
uongozi mbaya linaonekana kuwashughulisha sana waandishi wengi wa Afrika.
Waandishi wengi wameonesha jinsi ambavyo viongozi wengi walioshika madaraka
baada ya mkoloni kuondoka walivyoteka nyara uhuru uliopatikana, kwa hiyo
mabadiliko yakawa rangi ya ngozi tu, kwani wananchiwengi waliendelea kuteseka
katika umasikini wao.
Nchini
Tanzania, pia waandishiwa ushairi kama vile E. Kezilahabi ( Karibu Ndani), T.
Mvungi (Raha Karaha na Mashairi ya Cheka Cheka), M.S.Khatibu (Fungateya Uhuru),
M.M.Mulokozina K.K.Kahingi (Malenga wa Bara), n.k. wamelijdili suala hili la
uongozi kwa mapama sana.
Mashairi yanayojadili dhana ya
uongozi mbaya katika diwani hii ni kama:- “Tishio la Binadamu”, “Chini ya Mti
Mkavu”, “Wanajua Kuvumilia”, “Chanzo ni Wenye Kauli”, “Wimbo Wake Hotubani”
pamoja na “Shairi la Udongoni”
Katika
shairila “Tishio la Binadamu” mwandishi anakemea juu ya uongozi unaotumia
mabavu. Mfano mzuri mwandishi anakemea nchi za Urusina Marekani ambazo ni
wanachama wenye VETOkwenye umoja wa Mataifa zinavyotumia mabavu kuzikandamiza
nchi zisizo na nguvu kisilaha. Mwandish anasema;-
“Kuyasudu
mabavu, mwadai tusilotaka,
Maoni yetu
chakavu, sawa nguo yamiaka,
Ni pengi
penye makovu, nchi zilivyopasuka,
Mabomu
yateketeza, waundaji mwafurahi!”
Shairi la
“Chini ya Mti Mkavu”mwandishi analaani uongozi unaoendeleza dhuluma katika
jamii. Anakemea juu ya uongozi mbaya usiojali maslahi ya wengi, uongozi
usiopiga vitaumaskini hapa nchini, n.k.
Shairi la
“Wanajua Kuvumilia”, mwndishi analaaniahadi za uongo zinazotolewa na viongozi
wetu. Ameonesha kuwa viongozi wetu hawasemi ukweli bali uongo ndio umetawala
midomo yao. Sauti ya mshairi inayosikika katika shairi hili lina laani vibaya
viongozi ambao hawafiki vijijini kwa wananchi waliowachagua kwa kishindo ili
kujionea hali halisi ya maisha wanayoshi. Mwandishi anasema:-
“Afadhali
kuimba ukweli,
Wimbo mchomo
mkali,
Wimbo,
unalilia hali,
Ya vijiji
vilivyo mbali,
Kwa wale
wasio kauli.”
Katika
shairi la “Chanzo ni Wenye Kauli”, mwandishi anajadili juu ya madhara yaletwayo
na uongozi mbaya. Ni dhahiri kuwa chanzo cha ulanguzi, rushwa, uzembe, na kila
aina ya uovu ni uongozi mbaya.
Shairi la
“Wimbo Wake Hotubani” linjadili na kuonesha jinsi ungozi mbaya unavyochangia
utekelezaji mbaya wa maazimio na mipango tunayojiwekea.
Katika
shairi la “Kademokrasi Katoweka”, mwandishianaonesha jinsi uongozi mbaya
unavyozorotesha demokrasia katika bara la Afrka. Demokrasia inapokosekana
udikteta, dhuluma, usaliti, rushwa na kukosekana kwa haki hutawala katika
jamii.
“Shairi la
Udongoni” lawakumbusha viongozi wajibu
waokatika jamii. Mwandishi anasema:-
“Lanikumbusha
wajibu,
Kujenga si
kuharibu,
Naahidi
kujaribu,
Kulinda
tulichojenga.”
Hivyo, ili
tujenge jamii mpya ni lazima tuwe na uongozi bora. Uongozi mbaya ni kikwazo
kikubwa cha ujenziendelevu hapa nchini.
II.
KUWEPO
NA DEMOKRASIA YA KWELI
Demokrasia
ni mfumo wa kuendesha serikali iliyochaguliwa na watu kwa manufaa ya watu.
Demokrasia inahitajika sehemu yoyote ile ili kuwaruhusu wananchi kutoa maoni
yao kwa uhuru bila wasi wasi au kikwazo chochote. Mashairi yanayoongelea suala
la demokrasia ni “M janja yu Mashakani”, (UK 25-26), na lile la “Kademokrasi
Katoweka”, (UK 30-31)
Katika
shairi la “Mjanja yu Mashakani” mwandishi anajadili juu ya mfumo wa demokrasia
ambao umejitokeza miaka ya 1980 kote ulimwenguni. Mfumo huu ni ule wa kupiga
sera a chma kimoja na kuingia katika mfumo wa vyama vingi (mageuzi). Katika
shairi hili mwandishi anaonesha kuwa mfumo wa vyama vingi umewaamsha wananchi
wengi kutoka usingizini na kuanza kutetea haki zao. Hata hivyo, mwandishi
anaonesha kuwa wale viongozi waliojilimbikizia madaraka na vyeo mbali mbali
wamehofia sana mfumo huu na hivyo hufanya kila mbinu ili kuudididmiza. Viongozi
wanaong’ang’ania madaraka ndio wanaohofia mfumo huu. Mwandishi anaonesha jinsi
wananchi walivyougomea mfumo wa chama kimoja:-
“Barani
migomo baridi, kuugomea mfumo,
Mgomo
usokaidi wenye kufumba midomo,
Mfumo uso
shahidi , vikao wala misemo,
Ni migomo ya
kisiasa, modeli ya kote kote.”
Shairi la
“Kademokrasi Kametoweka” linapinga uongozi mbaya barani Afrika.ika shairi hili
mwandishi ameonesha kuwa demokrasia inapopokonywa na viongozi wachache,
udikteta huota mizizi na kuung’oa huchukua muda mrefu. Hali hii inasababisha
vita vya wenyewe kwa wenyewe katika baadhi ya nchi barani Afrika. Mfano wa nchi
hizo ni Jamuhuri ya Watu wa Kongo, Uganda, Burundi, Sierra Leone, n.k. Utawala
wa nguvu hurudisha nyuma maendeleo ya bara la Afrika nan chi nyingine za
ulimwengu wa tatu ambako hakuna demokrsia ya kweli. Mwandishi anasema:-
“Barani
mabavu yatumika,
Dikteta
asijeanguka,
Na majungu
pia ayapika,
Udikteta
pasi shufaka,
Nasimulia ya
Afrika.”
Katika
shairi mwandishi anaonesha kuwa mabovu yanatumika ili kumlinda dikteta asije
akaangushwa kwa kufuata mfumo wa demokrasia ya kweli. Madikteta hao hutumia
vyombo vya dola kama vile polisi, jeshi, magereza na mahakama ili kutetea
maslahi yao. Kwa ujumla anatoa pendekezo kuwa, ili tuweze kufanikisha kuijenga
jaii endelevu hatuna budi kujenga na kudumisha demokrasia ya kweli katika
harakati zetu za maisha.
III.
KUPIGA
VITA MATABAKA
Katika
kushughulikia suala la mgawanyiko wa jamii katika matabaka ya watu kufuatana na
madaraka walionayoya uchumi na siasa, msanii ametumia vielelezo halisi
kufikisha ujumbe. Mashairi yanayojadili mgawanyiko wa watu kulingana na hali
zao ni kama vile “Chatu na Kuku” (UK 2),
“Wengine wabaki Taabuni”,”Thomasi na Doto” (UK 38), “Wimbo wake Hotubani” (UK 28), pamoja na lile la “Manzese Mpaka Ostabei” (UK 43).
Shairi la
“Chatu na Kuku” limejengwa kitaswira kuonesha tabaka la wadhulumaji (chatu) na
tabaka la wadhulumiwa (kuku). Pia shairi la “Wimbowake Hotubani”linadhihirisha
mataaka yaliyopo nchini mwetu. Magavana wanawakilisha tabaka la juu (viongozi)
na punda na ngamia wamechorwa kitaswira kuwakilisha wananchi wanyonge
wanaoteswa na kunyanyasika. Shairi la “Wengi Wabaki Taabuni” linaonesha kuwa,
kuna matabaka ya aina mbili katika jamii- tabaka la wachache wanaofurahia
maisha na tabaka la wengi wanaoteseka taabuni. Shairi la “Thomas na Doto” linaonyesha
jinsi tabaka la wazungu (watu weupe)
wanavyolibagua tabaka la watu weusi (waafrika), hata katika suala la mapenzi na
ndoa. Na shairi la “Manzese mpaka Ostabei” linadhihirisha jinsi mgawanyo wa
watu katika matabaka unavyoleta tofauti za maisha katika jamii. Watu wa tabaka
la juu huishi sehemu za starehe kama vile Ostabei lakini watu wa tabaka la
chini (mafakiri) huishi sehemu duni zenye msongamano wa watu kam vile Manzese,
jijini Dar es saam.
Kwa ujumla
mwandishi ameonesha kuwa mgawanyiko wa watu katika matabaka huleta utengano
katika jamii. Ili tuweze kufaulu kuijenga jamii mpya (endelevu) hatuna budi
kupiga vita matabaka yaliyoshamiri katika jamii. Lengo liwe kuijenga jamii .
Yenye kufuata misingi ya haki na usawa.
IV.
KUEPUKA
VITA (UHASAMA)
Vita husababisha
uhasama katika jamii. Huleta ugomvi na kutokuelewana kwa watu. Vita hurudisha
nyuma maendeleo ya jamii. Vita huleta athari mbaya katika jamii. Mfano vifo,
umasikini, ughali wa maisha, n.k. Mshairi yanayopingana na suala la vita katika
diwani hii ni “Tishio la binadamu” na lile la “Daktari Askari.”
Katika
shairi la “Tishio la Binadamu”, mwandishi anaitahadharisha dunia kuwa vita kuu
vyanukia. Hii ni kutokana na uhasama uliopo kati ya nchi na nchi pamoja na
utengenezaji wa silaha kali kutoka Urusi na Marekani. Kutokana na hali hii
dunia nzima sasa iko mashakani juu ya vita. Mwandishi anaendelea kueleza kuwa
mashindano ya silahayamekuwa ni mchezo nan chi kubwa zinaona fahari
kuzitengeneza. Anasema:-
“Mashindano
ya silaha, yamekuwa ni mchezo,
Wakubwa wanaona
raha, kwa silaha waziundazo,
Mabomu yaso
na silaha, ndiyo yanawapa uwezo,
Urusi na
Marekani, dunia mwaipa adha?”
Katka shairi
la “Daktari Askari”, mwandishi anaelezea na kusimulia habari za vita kati ya
Tanzania na Uganda mwishoni mwa miaka ya 1970. Katika vita hii, Tanzania
ilipata hasara kubwa sana kwani uhalifu, ulanguzi, maendo, rushwa vilishamiri
wakati wa vita na baada ya vita. Hivyo katika mashairi haya yote mwandishi
anaitaka jamii itakayojengwa iepukane daima na suala la vita.
DHAMIRA
NYINGINE
I.
SUALA
LA MAPENZI
Mwandishi
amejadili aina mbali mbali za mapenzi katika diwani hii. Aina ya kwanza ya
mapenzi aliyoyajadili ni yale ya mtu nan chi yake. Haya mapenzi tunayaona
katika shairi la “Daktari Askari” ambapo tunona kuwa, wakati wa vita kati ya Uganda
na Tanzania raia, wanajeshi, manesi, n.k.walijitolea kwa moyo wa dhati kwenda
kupigana ili kuikomboa nchi yao. Mapenzi haya ni ya kweli na dhati. Mapenzi ya
Iddi Amina Dada kwa nchi yake hayakuwa ya dhati ndiyo maana alitumia mabavu
kuiongoza nchi yake.
Mapenzi
mengine kati ya mtu na nchi yake yanapatikana katika shairi la “Ngulu Wapaona”
(UK 33-36). Katika shairi hili msanii anaonesha umuhimu wa kuwa na mapenzi na kwenu (nchi yako) hata kama ni
porini. Msaanii anamtaka kila mtu kuthamini kwao ahata kama kuna karaha.
Anaonesha kuwa kwenu ni kwenu na
ukuthamini na kukuheshimu kwa raha na Baraka.
Pia kuna
mapenzi kati ya mwanamme na mwanamke. Mapenzi haya mwandishi ameyagawa ktika
makundi makuu mawili ya mapenzi ya dhati
na yale ya udanganyifu. Mashairi yanayoongelea mapenzi ya dhati ni yale ya
“Daktari Askari”, “Thomas na Doto”, “Manzese Mpaka Ostabei” pamoja na lile la
“Takumbuka Daima.” Mashairi
yanayoongelea mapenzi ya udanganyifu ni kama vile “Usiwe Mwonja Asali”, “Fikra
za Waungwana”.
Mapenzi ya dhati
ni ya kuheshimiana. Mapenzi yasiojali
hali au kipato cha mtu. Mapenzi ya uaminifu. Mapenzi kati ya Daktari Adam na
Eva katika shairi la “DaktariAskari” yalikua ya dhati, bila kujali kwao au
taifa. Hali kadhalika mapenzi kati ya Thomas na Doto yalikua ya dhati bila
kujali rangi au taifa. Na mapenzi kati ya Mashaka na Dorothy yalikua ya dhati
bila kujali pesa au utajiri. Mapenzi ya dhati husababisha uvumilivu katika
maisha. Mapenzi ya dhati huzaa matunda mema katika ndoa, yaani hujenga ndoa za
uaminifu. Hivyo mapenzi ya dhati huzaa ndoa za kudumu, ndoa zisizojali rangi,
utajiri, utaifa au hali ya mtu. Ndoa za uaminifu zilizotokana na mapenzi ya
dhati katika diwani hii ni zile kati ya dakitari Adam na Eva, pamoja na ile ya
Mashaka na Dorothy.
Mapenzi ya udanganyifu
nayo pia huzaa ndoa za udanganyifu na mara nyingi ndoa hizo huwa hazidumu.
Katika shairi la “Usiwe Mwonja Asali”, msanii anaonesha jinsi mapenzi ya
udanganyifu yanavyosababish uchumba wa udanganyifu. Pia katika shairi hili
msanii anaishauri jamii kuwa ukiwa na mchumba msiwe na tabia za kujamiiana
ovyo, bali mpaka mtakapooana. Shairi la “Fikra za Waungwana” linadhihirisha
wazi jinsi mapenzi ya udanganyifu yanavyosababisha ndoa za ulaghai. Mwandishi
anasema:-
“Mume wangu
nakupenda, Joseph amenikuna,
Nimekula
naye tunda, ninampenda sana,
Na usifanye
inda, mimi ni wako kimwana,
Nitaishi kwa
mpango, kwako na kwake Joseph.”
Katika
shairi la “Mfereji Maringo” (UK 57), msanii anawashauri wanajamiikuwa
wajiheshimukatika suala zima la mapenzi na wawe waaminifu au wasafi na wasiwe
Malaya. Kwa ujumla, katika mashairi haya yote, mwandishianaitaka jamii yetu
idumishe mapenzi na ndoa za dhati.
II.
NAFASI
YA MWANAMKE PAMOJA NA UHURU WAKE KATIKA JAMII.
Mwandishi wa
diwani hii amemchora mwanamke katika nafasi mbali mbali. Kwanza amemchora kama
mwanamapinduzi na jasiri. Katika shairi la “Daktari Askari” mwanamke ameoneshwa
akifanya kazi za kimapinduzi sawa na zile za mwanamme. Mwanamke anpigana vita
ili aikomboe nchi yake.
Pili,
mwanamke amechorwa kama mtu mwenye mapenzi dhati katika jamii. Katika shairi la
“Mapenzi Mpaka Ostabei” linamwonesha Dorothy akiwa na mapenzi ya dhati kwa
Mashaka . Hali kadhalika katika shairi la “Daktari Askari linamwonesha Eva
akionesha mapenzi ya dhati kwa Daktari Adam.
Tatu,
mwanamke amechorwa kama kiumbe laghai, asiye mwaminifu hususani katika suala a
mapenzi na ndoa. Haya yote tuayoyaona katika shairi la “Fikra za Waungwana”.
Mwisho,
mwanamke amechorwa kama mzazi na ezi katika jamii. Katika shairi la “Manzese
mpaka Ostabei”, mwanamke amechorwa kama mzazi na mlezi na hii nafasi
inawakilishwa na Dorothy ambaye alimzaa motto na kumlea baada ya kuolewa na
Mashaka.
Kuhusu uhuru
wa mwanamke, msanii ameleta mjadala juu ya uhuru wa mwanamke, uhuru wa kuolewa
na wanaume wawili kama afanyavyo mwanaume kwa kuoa wake wawili au zaidi.
Katika
shairi la “Fikra za Waungwana” (UK55-57), msanii anajadili dhamira hii kupitia
Anna. Katika shairi hili, Anna ana mume wake (Nania) lakini kwa upande mwingine
anampenda Joseph mume wake wa pili. Anna haoni sababu ya kutokuwa na wanaume
wawili. Kama asemavyo ubeti wa 11:-
“Mume wangu
nakupenda, Joseph amenikuna
Nimekula
tunda naye, nampendelea sana,
Ila usifanye
inda, mimi ni wako kimwana,
Nitaishi kwa
mpango, kwako na kwake Joseph.”
Katika
diwani hii, msanii anaonesha kuwa uhuru anaoutaka Anna ni wa kuishi au kuwa na
wanaume wawili na huo ndio msimamo wa Anna.
Hata baada
ya kesi yake kupelekwa mahakamani, Anna alibaki na msimamo huo huo. Hali kadhalika majaji walishindwa
kutoa hukumu, kwani hakuna sharia inayozui mwanamke kuwa na wanaume wenginkama
walivyo wanaume ambao huwa na wanawake wengi.
Lakini swali
la kujiuliza ni kuwa, je, mwanamke ana haki ya kuwa na wanaume wawili katika
jamii? Hakuna sharia inayomzuia mwanamke kuwa na wanaumewawili lakini mila na
desturi ndiyo zinazomzuia mwanamke kuwa na waume wawili. Hivyo ni kutokana na
ksoro hizo ndiyo maana anapinga kasoro hizo, kudai uhuru wake wa kuolewa na
wanaume wawili kwa wakati mmoja kama mwanaume anavyooa wake wawili au zaidi kwa
wakati mmoja. Hivyo anaishauri jamii kuona inaweka wazi sharia zinazohusiana na
suala hili. Majaji walishindwa kuhukumu kesi ya Nania- hii ni kwasababu hakuna
kifungu cha sharia kinachomzuia mwanamke kuolewa na wanaume wawili kwa wakati
mmoja.
III.
UMUHIMU
WAKUTOA WOSIA
Msanii
katika diwani hii anaishauri jamii kutoa wosia kwa familia zao kabla ya mauti
kufika. Katika shairi la “Wosia” (UK58-59), msanii anasema kuwa siku yako
ikifika, yaani mauti yanapokufikia ni muhimu kutoa wosia kwa familia yako
kuhusu mambo ambayo ungetka wakufanyie.
Msanii
anatoa wosia wake kuwa yeye akifa jamii inatakiwa imfanyie mambo yafuatayo:-
Kwisha
kuniweka chini,
Udongo kasha
funika,
Na nyimbo
niimbie,
Katoliki
yangu dini,
Halafu
nawaambia,
Sheree
kafanyeni,
Kawaida ya
Tanzia (ubeti 2)
Kwa hali hii
anaitadharisha jamii kuwa wosia ni kitu cha muhimu kutoa kabla hujafa n sio
wosia wa namna watakavyokufanyia, bali hata kuhusu mali zako na namna ya
kumilikiwa baada ya kifo chako.
UJUMBE WA
MWANDISHI
I.
Ni
lazima tujitoe mhanga ili kutetea wanyonge
II.
Dhuluma,
unyonyaji, kutowajibika pamoja na uongozi mbaya ni baadhi ya vikwazo
vinavyokwamisha ujenzi wa jamii mpya.
III.
Mshindano
ya kutengeneza silaha kwa mataifa makubwa huhatarisha amani uniani.
IV.
Demokrasia
ya kweli ndiyo njia pekee ya kuendeleza mfumo wa mageuzi hapa nchini na katika
nchi nyingine za ulimwengu wa tatu.
V.
Mgawanyiko
wa watu katika matabaka husababisha kukosekana kwa umoja na mshikamano katika
jamii.
VI.
Mapenzi
ya dhati yanhitajika katika jamii nan i lazima yadumishwe. Mapenzi ya ulaghai
yapigwe vita kwa hali zote.
VII.
Suala
la mapenzi na ndoa waachiwe wawili wanaopendana na si maamuzi ya wazazi.
FALSAFA YA
MWANDISHI
Mwandishi
anaamini itikadi itakavyowatetea wanyonge, yenye kuleta haki na usawa kwa kila
mtu. Analaani wizi, dhuluma, udikteta,unyonyaji na kila aina ya uovu. Vile vile
anatetea uhuru katika mapenzi na ndoa.
Mwandishi wa
diwani hii ana msimamo wa kimapinduzi kwani ameonesha matatizo mali mbali
yanazikumba jamii zetu na mbinu za kuondokna na matatizo hyo. Miongoni mwa
matatizo hayo ni uongozi mbaya, ulanguzi, dhuluma,rushwa, n.k.
FANI
MUUNDO
Katika
ushairi, muundo ni umbo, ploti pamoja na mjengo wa ushairi.Muundo hupatikana
kwa kuangalia idadi ya mistari kwa kila ubeti wa shairi linalohusika. Katika
diwani hii msanii ametumia miundo changamano. Miundo mikuu iliyotumiwa na
mwandishi ni ile ya tarbia (mistari mine kwa kila beti) pamoja na sabilia
(mistari mitanona kuendelea kwa kila ubeti).
Mashairi
yaliyotumia muundo wa tarbia ni Chungu Tamu” (UK 1), “Tishio la Binadamu”
(UK1-2), “Chini ya Mti Mkavu’ (UK 10), “Mjanja yu Mashakani” (UK 25), “Radi ya
Kiangazi” (UK32-33), “Shairi la Udongoni”(UK36-37), “Fikra za Waungwana”
(UK55-57), “Mfereji wa Maringo” (UK57) pamoja na lile la “Takumbuka Daima”
(UK57-58)
Mashairi
yaliyotumia muundo wa sabilia ni kama vile:- “Daktari Askari” (UK11-25),
“Chanzo ni Wenye Kauli” (UK27-28), “Wimbo Wake Hotubani” (UK28-29), “Wengine
Wabaki Taabuni” (UK31-32), “Ngulu Wapaona” (UK33-34), “Chungu na Tamu”
(UK34-35), “Usiwe Mwnja Asali” (UK37-38), “Thomas na Doto” (UK38-43), “Manzese
Mpaka Ostabei” (UK43-54), pamoja na shairi la “Wosia” (UK58-59). Mashairi
mengine yaliyobakia yemetumia muundo wa tarbia kwa baadhi ya beti na nyingine
muundo wa sabilia.
MTINDO
Mtindo
katika kazi ya fasihi ni mbinu au njia pekee inayotumiwa na waandishi ambayo
huweza kumtofautisha mwandishi mmoja na mwandishi mwingine. Katika ushairi,
kuna aina mbali mbali za mitindo kama vile mtindo unaofuata kanuni za ushairi
wa kimapokeo na mtindo unaofuata kanuni za usasa. Mtindo unaofuata kanuni za
ushairi wa kimapokeo hutawaliwa na urari wa vina na mizani, muwala, mara nyingi
kuna mfanano kwa kila kituo, huweza kuimbika, n.k. Mtindo unaofuata kanun za
ushairi wa kisasa haufuati au haufungwifungwi na kanuni za ushairi wa
kimapokeo. Hakuna urari wa vina, mizani, ufanano wa kituo, kuimbika, n.k.
Diwani ya
Chungu Tamu ina mashairi yaliyotumia mtindo changamano, yaani mtindo unaofuata
kanuni za ushairi wa kimapokeo na ule unaofuata kanuni za ushairi wa kisasa. Hii ina maana kwamba,
mshairi anyakubali mashairi ya in azote mbili (kimapokeo na kisasa).
Vile vile
mwandishi ametumia mtindo wa masimulizi kwa baadhi ya mashairi. Katika mashairi
ya “Chatu na Kuku”, “Daktari Askri” “Thomas na Doto” na “Manzese Mpaka
Ostabei”, Mwandishi metumia mtindo huu ili kufikisha ujumbe kwa jamii aliyokusudia.
MATUMIZI YA
LUGHA
Aina ya
lugha iliyotumika ni sanifu yenye misemo, nahau na methali, tamathali za semi,
mbinu nyingine za kisanaa pamoja na ujenzi wa taswira. Lugha ya kishairi yenye
uchaguzi maalum wa maneno (diction) imetumika.
MISEMO,
NAHAU NA METHALI
Imetumiwa na
mwandishi kwa lengo la kuwasilisha ujumbe kwa jamii husika. Mfano:-
a/ Sasa
mwaleta shari (msemo) – uk 7
b/ Umoja ni
nguvu (methali) –uk 6
c/ Kuvaa
masulupwete (msemo) – uk 48
d/ Ndoa ni
fumbo (msemo) – uk 42
e/ Usinawe
kwa ulimbo (msemo) – uk 42
f/ Mapenzi
hayana mipaka (msemo) – uk 40
g/
Utajichimbia kaburi (msemo) – uk 9
h/ Lakini
haikutiwa chumvi mitaani (msemo) – uk 12
TAMATHALI ZA
SEMI
TASHIBIHA
i.Maoni yetu
chakavu, sawa nguo ya miaka (uk 2)
ii.Macho yao
mekundu mithili wvuta bangi (uk 6)
iii.Kwa
msikilizaji husisimua mithili filamu za wachunga ng’ombe
iv.Shaba
kama maji (uk 12)
v.Kichwa
chake kama cha kifutu (uk 38)
vi.Mwili
ukamjaa harara kama jinni lililokosa mbuyu (uk 41)
vii.Tumbo
lake kubwa kama pipa (uk 50)
viii.Kichwa
kidogo kama cha chatu (uk 50)
ix.Mweusi
kama kiatu cha jeshi (uk 50)
x.Utaonekana
kama kinyago cha kuchonga (uk 12),n.k.
TASHIHISI
- Kifo
kimeniita (uk 4)
-Njaa
inawasaliti (uk 6)
-Kicheche
pia ameapa (uk 7)
-Huzuni
imenisaliti (uk 10)
-Katika ile
baridi kali, mabomu ya mikono, yakatubusu miguuni (uk 16)
-Vichaka
vikawakaribisha (uk 38)
-Taa zawaka
kwa maringo (uk 44)
-Jiji lasema
hali ngumu (uk 44)
-Mapenzi
hayana mpango, yakikanywa zaidi, hayana akili ati (uk53)
-Mioto
ikapasuka anga (uk 11), n.k.
SITIARI
=Ushairi ni
sukari tamu (uk 1)
=Utoto ni
kito (uk 2)
=Yeye
alisema dunia ni raha na tabu (uk 2)
=Umaskini ni
mzigo (uk 11)
=Wote weusi
awa mkaa (uk 45)
TAFSIDA
+Usiwe
mwonja asali (uk 37)
+Walipenda
faragha (uk 51)
+Dora ana
kitu tumboni (uk 54)
+Nimekula
naye tunda (uk 56)
TABAINA
-Kuwaza na
kuwazua
-Lakini
usikubali raha tu, kumbuka na karaha (uk 13)
-Aponya
aua (uk 17)
KEJELI
-Nyie
yawafalia, mfanyakazi ya kuchoma na kuuza mkaa (uk 45)
-Wa Manzese
atakulisha taka (uk 52)
-Jina lenye
ugonjwa wa kaka (uk 52)
-Iweje binti
shibe aende kwa omba omba (uk 52)
DHIHAKA
-Ati
mchumba, mchumba siye Baraka (uk 52)
MBINU
NYINGINE ZA KISASA
TAKRIRI
-Mateka,
mateka wapenzi (uk 22), Adamu, machozi (uk 20)
-Je je,
je….je nyingi (uk 43), Mateka, Mateka, wapewa (uk 22)
-Mama Dora
akaasa akaasa (uk 53)
-Tukanyata,
tukanyata tukakaribia Mbarara (uk 16)
MDOKEZO
-Je je je…je
nyingi (uk 43)
-Si mganga
wa tunguli…(uk 14)
-Sijui yaah
yaah…(uk 44)
-Sijui
Mashaka…(uk 53)
-Kati yao
huyu…!(uk 51)
-Profesa Idd
Amin…(uk 19)
-Ikawa
nakupenda lakini…
NIDAA
-Ati mie
mzee1!
-Ghafla
mwewe huyu!
-Umeshituka!
-Mwauzunika
nini!
-Kwa hamu ya
umoja!
TASHTITI
-Hujisikia
wezi wakiomba Mungu kabla ya kwenda huko waendako? (uk 13)
-Wewe mwana
–kibarua, hujioni? (uk 49)
MJAZIO
-Yule naam,
sio huyo, sijui Mashaka…(uk 53)
-Wawaona
wanaopelekewa chai, mikate, karanga, mayai…(uk 13)
-Ndugu
mwenyekiti nadhani, labda, pengine, ningependekeza, kwa maoni yangu, kwa mfano
tungeliweza….(uk 15)
ONOMATOPEA(TANAKALI
SAUTI)
-Lo! (uk 4)
-Loooo! (uk
19)
LUGHA YA
KIINGEREZA
-Movement
order (uk 14)
-Surrender
(uk 17)
-Doctor
where College? (uk 18)
-Life
President? (uk 19)
-Good Doctor
(uk 19)
-My first
fiancé (uk 20)
-But this is
war sir (uk 20)
-Look Adam.
My parents are dead. I am alone (uk 23)
-Sir is that
a request or an order? (uk 24)
-Two doctors
fighting for no reason (uk 25) n.k.
TAFASIRI YA MOJA KWA MOJA
=Fomu wani
(uk 48)
UJENZI WA
TASWIRA
Mwandishi
ametumia baadhi ya taswira ili kufikisha ujumbe kwa jamii aliyoiandika. Baadhi
ya taswira hizo ni kama vile:-
-Chatu (uk
2)…..Inawakilisha wadhulumaji (wakoloni)
-Kuku
(uk2)……Inawakilisha wadhulumiwa (Waafrika)
-Vifaranga
(uk 9)….Inawakilisha mali ghafi
-Mjanja (uk
25)….Viongozi wanaoshikilia mfumo wa chama kimoja
-Watwana (uk
25)….Wananchi wanaotaka mabadiliko au uongozi mbovu
-Nuglu (uk
33)….Vijiji, sehemu isiyo na maendeleo, sehemu iliyosahaulika
-Zabibu (uk
42)…..Msichana au mwanamke
MANDHARI
Kitbu hiki
kiliandaliwa miaka ya 1980. Na matukio yanayosimuliwa katika kitabu hiki
yanazungukia nchi za Afrika ya Mashariki hususani Tanzania na Uganda. Hata
hivyo, maudhui ya kitabu hiki yanasadifu huu wa sasa katika nchi yoyote ile
ulimwengu wa tatu.
JINA LA
KITABU
Jina la
diwani hii Chungu Tamu linasadifu yaliyomo ndani ya kitabu. Msanii ameonesha
kuwa, baada ya kupita katika machungu na kuamua kupambana nayo ndipo utamu
utafuata. Anaitaka jamii itumie kila mbinu kupambana na vikwazo vinavyokwamisha
jamii siweze kuupata utamu (ujenzi wa jamii mpya endelevu). Aidha msanii
anaonesha kuwa katika maisha, uchungu na utamu havitengamani. Vile vile msanii
ameonesha dhahiri kuwa, wananchi wa kawaida ambao ndio wazalishaji wanakula
“Chungu” lakini viongozi ambao si wazalishaji wanakula “Tamu”.
KUFAULU KWA MWANDISHI
KIMAUDHUI
·
Ameongelea
masuala ambayo yanaisakama jamii yetu katika wakati huu tulio nao. Ameonesha
mbinu mbalimbali za kufuata ili kufanikisha suala zima la ujenzi wa jamii mpya.
KIFANI
Amefaulu
kutumia miundo changamano, mitindo changamano, lugha ya kishairi pamoja na
ujenzi wa taswira.
KUTOFAULU KWA MWANDISHI
·
Lugha
imejaa taswira kwa kiasi kikubwa na hivyo msomaji wa kawaida hawezi kuambulia
ujumbe wowote. Hivyo amewanyima baadhi ya wasomaji uhondo wa kazi yake.
·
Msanii
ametumia lugha ya Kiingereza (kigeni) katika baadhi ya mashairi. Huu ni udhaifu
wa mwandishi, kwani anakinyima Kiswahili sanifu nafasi ya kuenea. Vile vile kwa
mtu asiyefahamu Kiingereza atashindwa kupata ujumbe.