UCHAMBUZI WA RIWAYA YA MFADHILI
UHAKIKI WA RIWAYA
KITABU: MFADHILI
MWANDISHI: HUSSEIN TUWA
WACHAPISHAJI: MACMILLAN
MWAKA: 2007
UTANGULIZI
Mfadhili ni riwaya
inayoelezea suala la mapenzi na ndoa, ikionesha matatizo mbalimbali
yanayotokana na mapenzi na ndoa na athari zake kwa jamii. Ni riwaya
inayoongelea juu ya penzi zito baina ya Gaddi Bullah na Dania Theobald na jinsi
ambavyo penzi hilo lilivyoingiliwa na mitihani pamoja na majaribu makubwa.Riwaya
hii imejadili kwa mapana suala ya
mapenzi na ndoa na athari zake kwa jamii.
MAUDHUI
Dhamira kuu: Mapenzi na
ndoa
Msanii
ameainisha aina mbili za mapenzi na ndoa;
v Mapenzi ya kweli
v Mapenzi ya uongo
Mwandishi amejadili mapenzi ya kweli kama
ifuatavyo;
Mosi, mapenzi ya kweli,kati ya Gaddi Bullah
na dada yake Bi Hanuna.Hawa
walipendana kwelikweli na ndio maana mmoja alikua akiwa na tatizo lina kuwa ni
tatizo la wote wawili,mtu akimuudhi Gaddi amemuudhi na dada yake Bi Hanuna pia na walisaidiana katika shida zao zote.
Pili,Mapenzi ya kweli kati ya Gaddi Bullah na Dania,
mwanzoni walipendana hasa mchana walikua wakienda kula chakula pamoja na hata
walifika hatua ya kutembeleana. Gaddi katika kuonesha mapenzi ya dhati kwa
Dania alimsaidia kwa kila hali wakati wa shida raha na (UK 101-106)
Hata baada
ya Dania kumsaliti Gaddi bullahh, bado Gaddi bullah aliendelea kumpenda Dania na hata alimfadhili baada ya kusalitiwa
na Jerry kwa mara ya pili.Alikubali kutoa ini lake ili Dania aendelee kuishi.
(UK 137-139).
Tatu,Mapenzi ya kweli kati ya Gaddi Bullah na Junior mtoto wa Dania.
Pamoja na kwamba Junior hakuwa mtoto wake.Gaddi alimpenda sana na ndio maana
baada ya Junior kuumia mkono aliyempeleka hospital ni Gaddi Bullah na wala si
baba yake Jerry (UK 146)
Nne,Mapenzi
ya kweli kati ya Mama Mlole (Fausta) kwa wafanyakazi wa chini yake
kama vile Gaddi Bullah na Dania. Pamoja na Gaddi Bullah kuharibu kazi,
Mama Mlole alimtetea sana asifukuzwe kazi bali aangaliwe upya (UK 69-71).
Vilevile alimtetea sana Dania asifutwe kazi kipindi anaumwa .Mama Mlole ni
mfano wa viongozi wenye mapenzi ya kweli kwa wale anaowaongoza .
Tano,Mapenzi ya dhati kati ya Nunu na Dania,Nunu
alimsaidia sana Dania kulea mtoto wake
Junior wakati Dania yuko kituo cha kuponya walevi (UK 115). Pia Nunu alikua
bega kwa bega na wazazi wake Dania
wakati wa magonjwa yote yake yaliyomkumba na alimsaidia kumtafuta Gaddi Bullah na Bi Hanuna ili awaombe msamaha kwa
yote aliyowatendea.
Sita,Mapenzi ya dhati kati ya Nunu na Boazi;
Hawa walipendana kwa dhati na ndio maana
shida ya Nunu ilikua shida ya Boazi pia. Nunu na Boazi walisaidana kwa hali na
mali katika kumtafuta Gaddi Bullah aliyekuwa anatafutwa na Dania. Hata
wakafikia hatua ya kuhatarisha maisha yao kumteka nyara Bi Hanuna kwa lengo la
kumsaidia Dania (UK 36-56).
Saba,Mapenzi ya kweli
kati ya daktari Virani na Gaddi Bullah; Hawa walipendana sana na ndio maana
Virani alimsaidia Gaddi Bullah katika matatizo mbalimbali kwa mfano; kumtibu
mpenzi wake Dania.Vilevile daktari Virani alihangaika sana kuokoa maisha
ya Gaddi Bullah kutokana na ugonjwa
aliokuwa anaumwa ingawa hakufanikiwa.
Haya yote aliyafanya kwasababu alimpenda Gaddi Bullah kwa dhati na Gaddi Bullah vilevile
alimpenda Virani.
Nane,Mapenzi mengine ya dhati ni kati ya
Nunu na Gaddi Bullah; Nunu alimpenda sana Gaddi Bullahkwa dhati ndio maana alimshauri
sana Dania asimwache Gaddi na kurudiana na Jerry . Si kwasababu alimsaliti,
bali awe na Gaddi Bullah aliyemsaidia wakati wa shida (UK 114-115).
Vilevile Gaddi alimpenda pia Nunu kama
rafiki mzuri anasema (UK 146).
“…..Nunu
….”A…..bee! Nunu alitikia kwa upole huku akitiririkwa na machozi wewe….ni
rafiki… mzuri….”Gaddi alimwambia……”
Tisa,Mapenzi ya dhati kati ya wazazi wa
Dania kwa mtoto wao Dania. Wazazi hawa walimpenda sana mtoto wao ndio
maana walimsaidia kwa hali na mali hadi wakampeleka Afrika ya kusini kutibiwa
ugonjwa wake wa ulevi. Pia wakati wa ugonjwa wake wa ini ,wazazi wake
walimsaidia sana mpaka hatua ya kuweka matangazo radioni ili kumsaidia mtoto wao kwa mtu ambaye
angejitolea ini. Hayo ni mapenzi ya dhati ya wazazi kwa binti yao.
Pia mwandishi amejadili kwa kina mapenzi
ya uongo kama ifuatavyo;
Mosi,Mapenzi ya uongo kati ya Jerry na Dania. Inaonyesha Jerry hakumpenda kwa
dhati Dania na ndio maana alimsaliti wakati wa harusi yao. Jerry alipenda sana
masomo kuliko kufunga ndoa na Dania. Jerry alitakiwa kutolewa ini moja ili
waponye maisha ya Dania, lakini siku ilipofika hakufika hospitali bali
alitokomea kusikojulikana(UK 133-135).
Pili,Mapenzi
ya uongo ni kati ya rafiki yake Gaddi na
Gaddi. Huyu hakuwa rafiki wa kweli kwani alimshauri vibaya Gaddi Bullah
pale ambapo Gaddi alipomuomba ushauri kuhusu uwepo wa mabadiliko mabaya ya
kimahusiano kati yake na mkewe rafiki yake alimshauri atafute nyumba ndogo. Pia
alimtorosha mke wa Gaddi Bullah na kumuoa na akawa mkewe (UK 64-67).
Tatu,mapenzi ya uongo kati ya Gaddi na Nyambuja. Gaddi alimpenda
sana mkewe alimjali kwa kila kitu Lakini
mke wake Nyambuya hakuwa na mapenzi ya dhati katika ndoa yake. Baada ya mwaka
mmoja tu wa ndoa yao, Nyambuja alianza kumsaliti mume wake kwa kuchelewa kurudi
nyumbani, kusafiri bila taarifa kwa mume wake na mwisho akamwacha nakwenda
kuolewa na rafiki yake Gaddi Bullah (UK 60-67).
DHAMIRA NDOGO NDOGO
1. USALITI
Ni hali ya
kufanya jmbo kinyume na makubaliano.Mwandishi ameonyesha namna wahusika
walivyosalitiana pamoja na athari zake kama ifuatavyo;
Mosi,Mwandishi ameonesha jinsi Nyambuja alivyomsaliti
mumewe Gaddi Bullah kwa kufanya mapenzi nje ya ndoa na aliamua kumwacha Gaddi Bullah na kwenda kuolewa na rafiki yake Gaddi Bullah.
Pili,Mwandishi
ameonesha jinsi Rafiki yake Gaddi Bullah
alivyomsaliti Gaddi Bullah kwa kumnyang’anya mkewe Nyambuja.
Matokeo ya usaliti huo yalimpelekea Gaddi bullah kushindwa kufanya kwa ufanisi pamoja kasi ya itendaji wake kupungua.
Hatimye akaandaliwa barua ya kumuonya na kutokana na mawazo mengi aliyokuwa
nayo akasaini cheki feki za wizi (UK 62-63)
Tatu,Mwandishi ameonesha
namna Afisa usafirishaji alivyomsaliti Gaddi Bullah kazini.
Huyu aliandaa vocha ya malipo hewa ili
Gaddi Bullah aisaini . Matokeo yake Gaddi Bullah alishushwa cheo na
kuhamishwa kituo chake cha Arusha na
kuja kufanya kazi Dar-es-salaam kwa uangalizi wa makao makubwa (UK 71-72).
Nne,Mwandishi ameonesha namna Dania alivyomsaliti Gaddi
Bullah.Kwanza
Dania alimsaliti Gaddi kwa kutoandaa ripoti aliyotakiwa kuandaa kwa ajili ya
kwenda kusoma kwenye kikao cha wakuu wa vitengo. Dania hakuandaa ripoti hiyo na
siku ya kikao hakuonekana kazini hadi muda wa kikao ulipoanza saa mbili na nusu
asubuhi (UK 77-79) na matokeo yake Gaddi Bullah alimwandikia barua ya onyo na
kumtaka ajieleze ,lakini kwa busara ya mama Mlole alisuluhisha mgogoro huo.
Tano,Mwandishi
ameonesha namna Dania alivyomsaliti Gaddi Bullah kwa kumwacha wakiwa katika
mapenzi mazito na wakati huo huo wajindaa kufunga ndoa. Dania alimwacha Gaddi na kurudiana na Jerry ambaye alimsaliti
siku ya harusi yake. Matokeo yake Gaddi Bullah alipata shinikizo la moyo, kupigana na
Jerry na dada yake Bi Hanuna kuwekwa ndani (Lupango).
Sita,Mwandishi
ameonesha namna Jerry alivyomsaliti Dania,kwanza alimsaliti wakati wa harusi yao kwani Jerry
kwani alikuwa Marekani na wakati huo aliahidi angerudi ili wafunge ndoa. Na
kutokana na usaliti huo harusi ilivunjwa na Dania alikonda sana hali chakula
na akawa mlevi wa kupindukia wa pombe kali na ikapelekea kupata ugonjwa wa ini (uk 83-87).
Saba,Mwandishi
ameonesha namna Jerry alivyomsaliti Dania akiwa mgonjwa mahututi hospitalini kwa kuahidi kutoa ini
lake moja ili amuokoe mpenzi wake Dania lakini hakufanya hivyo bali alimtoroka
akiwa kitandani hospitalini (UK 133-134)
2.
NAFASI YA MWANAMKE KATIKA JAMII
Mwandishi wa riwaya hii amemchora mwanamke
katika nafasi au sura mbali mbali kama ifuatavyo;
v Mosi,Mwandishi amemchora
mwanamke kama kiumbe asiyekuwa na msimamo katika kufanya maamuzi.
Mfano, Dania anaonekana kuwa na maamuzi
yasiyofaa kwa kutokuwa na msimamo na kuamua tena kumrudia Jerry ambaye
alimuumiza mwanzoni.
v Pili,Mwandishi amemchora mwanamke kama mtu mwenye huruma na mshauri mzuri. Mfano Nunu alimhurumia
rafiki yake Dania na kumhangaikia kwa hali na mali wakati anaumwa.Pia alikuwa
mshauri mzuri wa Dania.
v Tatu,Mwandishi amemchora Mwanamke kama
mtu jasiri. Mfano Nunu ambaye alifanya kazi
kubwa sana ya kumpatanisha Dania na Gaddi Bullah hata akafikia hatua ya kumteka
kwa nguvu dada yake Gaddi Bullah Bi
Hanuna ili aweze kuwasaidia kumpata Gaddi Bullah.
v Nne,Mwandishi amemchora mwanamke kama
mtu katili na msaliti. Mwandishi amewaonesha
Nunu,Nyambuja na Dania walivyomsaliti Gaddi Bullah na hatimaye kwenda kuolewa kwa wanaume wengine.
v Tano,Mwandishi amemchora kama mtu mwenye
upedo,moyo wa huruma
na moyo wa kusaidia.Mwandishi amemuonesha mhusika Mama Mlole alivyokuwa na upendo na
wafanyakazi wa chini yake.
3.
CHUKI
Mwandishi
ameonesha namna baadhi ya wahusika walivyona chukiana au kuwa na chuki kwa
wenzao kma ifuatavyo;
Mosi,Bi Hanuna alikuwa na chuki na Nunu kwasababu ya Dania. Dania alimuacha kaka yake
Gaddi Bullah wakati wako katika mapenzi
ya raha na furaha,kitendo hichi kilimuudhi sana Bi Hanuna. Hata Nunu
alipokwenda kwake mkuranga kuomba msaada wa kusaidiwa kuonana na Gaddi Bullah Bi Hanuna alikataa kumsikiliza
kutokana na chuki aliyokuwa nayo (UK 25).
Pili,Bi Hanuna alikuwa na chuki kwa Dania .Hii ilitokea baada ya kumuacha kaka
yake Gaddi Bullah na kumuweka ndani (Gerezani) Bi Hanuna.Mwandishi anaendelea
kuonesha kuwa jinsi Bi Hanuna alivyokuwa anamuona mdogo wake akiteseka ndivyo
alivyozidi kumchukia Dania (UK 125-126).
Na kutokana na
chuki aliyokuwa nayo Bi Hanuna kwa Dania ndiyo maana alikataa kuwaeleza Nunu na
Boazi ailikokuwa Gaddi Bullah. Vile vile alikataa hata kuwapelekea barua kwa
Gaddi Bullah iliyotoka kwa Dania kwaajili ya kuomba msamaha (UK 24-56). Pia
Dania alionesha chuki za waziwazi kwa
Gaddi Bullah kwa kumuacha na kumuona kama mtu aliyemnyang’anya cheo chake.
Tatu,Dania alikuwa na chuki kwa Gaddi Bullah,
Hii ilipelekea Dania kuharibu kazi ili Gaddi Bullah aonekani hafai. Matokeo
yake Dania akaandikiwa barua kali na Gaddi na kumuonya na kutaka ajielezee
kwanini asifukuzwe kazi (UK 75-79).
Nne,Dania naye alikua
na chuki na Jerry hasa baada ya kumuacha au kumtelekeza wakati wa maandalizi yote ya harusi yao yamekamilika.
Hata Jerry aliporudi kutoka Marekani alimfukuza kama mbwa nyumbani kwake (UK
107).
Tano,Nunu alikuwa na chuki kwa Jerry
kwasababu ya Jerry kumuacha rafiki yake Dania, hata Jerry
alipokwenda kuomba msaada wa kumsaidia kumshawishi Dania alimfukuza na kumtaka
asirudi tena nyumbani kwake (UK 109).
Sita,Wazazi wake Dania nao walikua na chuki
na Jerry kwasababu ya kumsaliti motto wao (UK 109-110).
Mwandishi anaonesha kuwa wenye chuki ipo siku
watasameheana na anaonyesha Bi Hanuna
anamsamehe Nunu, halafu Dania anamsamehe Jerry ingawa msamaha huo ulileta
matatizo kwa Gaddi Bullah na Bi Hanuna. Hivyo msanii anaonesha kuwa ni muhimu kumsamehe
mtu aliyekufanyia makosa.
4.
UMUHIMU WA UONGOZI BORA
Msanii
amemtumia mhusika mama Mlole ambaye alikua kiongozi mzuri ambaye aliwajali wale
aliowasimamia.
Gaddi Bullah
alipata matatizo kazin yaliyotokana na athari za kuacwa na mkewe , mama Mlole
aimtetea sana asifukuzwe kazi baada ya kumwelezea matatizo yake (UK 70). Pia
alipendekeza Gaddi ahamishiwe DSM ili
aangaliwe zaidi badala ya kufukuzwa kazi.
Pia mama
Mlole alimtetea Dania asifukuzwe kazi baada yakuachwa na Jerry. Baada ya ndoa
kuvunjika, utendaji wake wa kazi uliathirika sana. Alifikia hatua anakwenda
ofisini amelewa (UK 88) na hatua aliyofikia ilikua aachishwe kazi lakini mama
Mlole kama Afisautumishi wakapuni alimtetea sana na akapendekeza apewe likizo
bila malipo kwa muda wote akaokua kwenye matibabu ya ulevi wake (UK 88)
Msanii
anataka kuifundisha jamii kuwa cheo ni dhamana lazima kukitumia kwa faida ya
watu wote na sio kuwanyanyasa.
DHARAU
Msanii
amemtumia Nyambuya kama mtu mtu mwenye dharau kwa mume wake,hata akiulizwa
swali na mume wake majibu aliyokua akiyatoa yalikua yamejaa dharautupu (UK 60).
Pia kitendo cha Nyambuya kusafiri safari za gafla na kumtaarifu mume wake kwa
simu ni sehemu ya dharau. (UK 61)
Kitendo cha
Nyambuja kufanya mapenzi na rafiki wa Gaddi na kumwacha Gaddi na kwenda kuolewa
na rafiki yake Gaddi hiyo nayo ni dharau kwa mume wake. Hata barua aliyoiandika
kwa Gaddi (UK 65) ilijaa dharau ya Nyambuja kwa Gaddi.
Dania pia
alimdharau Gaddi siku ya kwanza tu alipomkuta ofsini kwake. Kitendo cha Dania
kumuita Gddi kwamba wewe ni “Gaddi Bullah” (UK 73) ni sehemu ya dharau
alioionyesha kwa Gaddi. Pia kitendo cha Dania kumfukuza Gaddi kwenye meza
aliyokuwa amekaa na motto wake Junior kwenye bar ni sehemu ya dharau. Dania
alimfukuza Gaddi kwenye meza kama mbwa mwizi.
Pia Dania
alionesha dharau ya hali ya juu baada ya kumwacha Gaddi na kurudi kwa Jerry,
majibu aliyokua anamjibu Gaddi yalikua majibu ya kijeuri na dharau tupu (UK
120-123).
Lakini msanii anaitaadharisha jamii kuwa mtu
anayemdharau baadae anaweza kukufaa. Dania alimwacha Gaddi , alimdharau lakini baadae akawa mfadhiliwake baada ya
kutelekezwa na Jerry kwa mara ya pili akiwa mgonjwa mahututi hospitalini,hivyo
tuepuke dharau.
BIDII KATIKA KAZI
Msanii
amemtumia Gaddi Bullah ambaye alionesha kuwa kijana mdogo lakini mchapa kazi
mzur,alipendwa na wafanyakazi wote waliokuwa chini yake na hata wakuu wake wa
kazi huko makao makuu (UK 59).
Pia Dania
ambaye alikua mmoja kati ya wafanyakazi wenye nidhamu, bidii na ushirikianao.
Pia aliwaheshimu wafanyakazi wote na wala hakuruhusu utajiri wa wazazi wake
umpe kichwa.
Pia msanii
anaonesha matatizo ya mtu binafsi au ya kifamilia yanaweza kupunguza bidii na
ufanisi wa mtu katika kazi yake. (UK 63)
Kwa ufupi
msanii anaonyesha kuwa bidii katika kazi ni kichocheo cha maendeleo ya jamii.
Pia matatizo yanaweza kumfanya mtu achanganyikiwe, aache kazi na pia yanaweza
kupunguza ufanisi katika kazi , kufukuzwa kazi au kushushwa cheo.
UJUMBE
Ø Rafiki wa kweli ni Yule anayekusaidia
au kukujali wakati wa shida.
Ø Si kila king’aacho nidhahabu
Ø Bidii na ufanisi katika kazi ni
chanzo cha maendeleo katika jamii
Ø Ni vigumu kumpata mtu mwenye mapenzi
ya kweli au atakayekupenda kama unavyopenda wewe
Ø Matatizo, majaribu, chuki na dharau
ni vitu visivyoepukika katika mapenzi na ndoa
Ø Mtu anapotenda kosa, lazima akubali
kutubu kosa
FALSAFA
Msanii
anaamini kuwa katika suala la mapenzi kuna kupenda na kutokupendwa, kunakuoa na
kuachwa, hivyo ni vigumu kupata mtu mwenye mapenzi ya dhati.
MSIMAMO
Mwandishi
ana msimamo wa kimapinduzi kwani anaonesha wazi kuwa katika suala la mapenzi na
ndoa kuna matatizo yake. Watu lazima tukubali kusameheana kwani hujui ni yupi
atakayekusaidia wakati wa shida.
MIGOGORO
Mgogoro kati ya Gaddi na Nyambuja
Mogoro kati ya Gaddi na Dania
Mgogoro kati ya Gaddi na Jerry
Mgogoro kati ya Nunu, Boaz na Bi
Hanuna
Mgogoro kati ya Dania na Jerry
Mgogoro kati ya Jerry na wazazi wa
Dania
Mgogoro kati ya Nunu na Jerry
Mgogoro wa nafsi
FANI
Muundo
Msanii
ametumia miundo mitatu ambayo ni muundo changamano,muundo rejea na Muundo wa moja
kwa moja. Sura ya kwanza ametumia muundo Rejea
na kuanzia sura ya pili na kuendelea ametumia muundo wa moja kwa moja
mpaka mwisho wa riwaya.
MTINDO
Ø Msanii ametumia kwa kiasi kikubwa
mtindo wa masimulizi na kiasi kidogo mtindo wa dayalojia, nafsi zote tatu
zimetumika. Vilevile kuna matumizi ya barua. (UK 65)
MATUMIZI YA LUGHA
Ø Ametumia lugha rahisi yenye misemo,
methali, tamathali za semi na mbinu nyingiezo za kisanaa.
Misemo/ Nahau
Jibu lile
lilimkata maini (UK 36)
Methali
Ø Ukistaajabu ya Musa utayaona ya
firauni (UK 27)
Ø Hakuna marefu yasiyo na ncha (UK 17)
Ø Ni bora nusu shari kuliko shari
kamili (UK 127)
Ø Mkaidi hafaidi mpaka siku ya Iddi (
UK 135)
TAMATHALI ZA SEMI
Tashbiha
Ø Paa lake lililokuwa limeengwa kwa
mithili yam domo kwa lile dege aina ya concord. (UK 11)
Ø Gari iliruka mbele kama jiwe na
kutimua vumbi. (UK 41)
Ø Kamfukuza kama mbwa kutoka kwenye nyumba ya marehemu
mumewe.
Onomatopea
Ø Vilitilia mkazo uharaka kwa binti
yule kwa kutoa sauti za ko! Ko! Ko! (UK 1)
Ø Aaaaah! Ni -niche! Uuuuuuuuwiiii! Yallaaaaah! (UK 37)
Takriri
Ø Toka hapa! Ondoka! Na usirudi tena!
(UK 32)
Ø Nimesema sitaki! Sitaki! Sitaki! (UK
35)
Ø Sikubali! Sikubali!nawaambia nitawashitaki
kwa hili! (UK 43)
Mdokezo
Ø Oh, Mungu wangu, sasa itakuwaje
jamani………(UK 12)
Ø Ah! Ni kweli anti……lakin………..(UK 12)
WAHUSIKA
1. Gaddi
Bullah
·
Mhusika
mkuu, alikuwa meneja wa kampuni
·
Mchangamfu
na mwenye huruma
·
Mkarimu
na mchapakazi mzuri
·
Alikuwa
na upendo wa dhati
·
Mume
wa kwanza wa Nyambuja na mpenzi wa Dania
·
Alikuwa
msamehefu na alizitawala vyema hisia zake
·
Anafaa
kuigwa na jamii
2. Dania
·
Mwanamke
aliyezaliwa katika familia ya kitajiri
·
Mtu
mwenye hasira anapokuwa amechukizwa na mwenye chuki
·
Mtu
asiye na msimamo na anadanganyika kirahisi
·
Mfanyakazi
mwenye nidhamu , bidii na ushirikiano
·
Alikuwa
mlevi wa kutupwa baada ya kuachwa na Jerry
·
Anafaa
kuigwa kwa baadhi ya mambo na hafai kuigwa kwa baadhi ya mambo
3. Bi Hanuna
·
Dada
yake Gaddi Bullah,
·
Alimpenda
mdogo wake kiasi cha kukataa kumsaliti
·
Alikua
na chuki na mtu yeyote aliyemuudhi mdogo wake Gaddi, Dana na Nunu
·
Bi
Hanuna anafaa kuigwa na jamii kutokana na mapenzi aliyokuwa nayo kwa mdogo wake
Gaddi Bullah
4. Jerry
·
Alikuwa
mpenzi wake Dania na mtaalamu wa kompyuta
·
Mcheshi,
mtanashati na mwenye mvuto mkubwa kwa kina dada
·
Katili
na msaliti mkubwa
·
Hakua
na mapenzi ya kweli
·
Hafai
kuigwa na jamii
5.Nunu
·
Rafiki
yake Dania
·
Alikua
na mapenzi ya kweli kwa watu, aliwasaidia sana wakati wa shida.
·
Anafaa
kuigwa na jamii
Ø Wahusika wengine ni Boazi, mama
Mlole, Marry, Aisha, Agness, Junior na wengineo kama daktari Virani.
MANDHARI
v Mandhari ya riwaya hii ni ya Arusha,
Dar-es-salaam na Pemba katika sehemu hizo zote kuna mandhari ya ofisini,
nyumbani, baa, barabarani, hospitalini.
JINA LA KITABU
Mfadhili ni
mtu anayemdhamini mtu katika kugharamia kitu fulani. Katika riwaya hiimwandishi
ameonesha ufadhili wa aina mbalimbali kama ifuatavyo;
Mosi,Mama Mlole
anamfadhili Gaddi Bullah baada ya kukumbwa na kashfa ofisini kwake asifukuzwe kazi.
Mama Mlole ndiye aliyemtetea Gaddi Bullah hata kumhamishia Dar es salaam kwa uangalizi
zaidi.
Pili, Mama Mlole
alimfadhili Dania
asifukuzwe kazi kutokana na kuwa mlevi sugu baada ya kuachwa na mpenzi wake
Jerry.
Tatu,Mama Mlole
alimfadhili Gaddi na Dania kwa kuwapatanisha kutokana na uhasama wao pale ofisini kwao.
Bila yeye ugomvi ungeendelea.
Nne,Gaddi Bullah alimfadhili Dania baada y kuachwa na Jerry. Dania
mpenzi wake wa kwanza baada ya kuachwa na Jerry alichukuliwa na Gaddi ambaye
alimpenda sana hali iliyopelekea Dania asimkumbuke Jerry. Gaddi Bullah alimfadhili
Dania kwa kumpa ini lake moja wakati anaumwa baada ya kusalitiwa mara ya pili
na Jerry, bila Gaddi, Dania angekufa. Vile vile Gaddi alimfadhili Junior kwa kumpeleka
hospitalini baada ya kuumia mkono. Asingekua Gaddi,Junior angepata matatizo
makubwa.
KUFAULU NA KUTOKUFAULU KWA MSANII
KUFAULU
v Kimaudhui msanii amefaulu kuonesha matatizo
mbalimbali yanayoikumba jamii yetu hasa
katika suala la mapenzi na ndoa na kuonesha suluhisho la matatizo hayo.
v Kifani amefaulu kutumia lugha rahisi na
inayoeleweka na ujengaji mzuri wa wahusika wake.
KUTOKUFAULU
v Kutumia viswahili badala ya Kiswahili
sanifu (UK 15-16)
v Matumizi ya kiingereza kwa mtu ambaye
hajui kiingereza atashindwa kupata ujumbe.