UCHAMBUZI WA DIWANI YA KIMBUNGA
UHAKIKI WA USHAIRI
KITABU: KIMBUNGA
MWANDISHI: HAJI GORA HAJI
WACHAPISHAJI: TUKI
MWAKA: 1995
UTANGULIZI
Kimbunga ni diwani inayozungumziwa juu ya
mawaidha mbali mbali katika maisha pamoja na suala zima la ujenzi wa jamii
mpya. Katika diwani hii, mwandishi ametoa maadili na maonyo mbali mbali pamoja
na mbinu mbalimbali za kufuata ili kufanikisha suala la ujenzi wa jamii hapa
nchini.
Maudhui
Dhamira Kuu- Ujenzi wa jamii mpya
Mwandishi amejadili dhamira ya ujenzi wa
jamii mpya katika kazi yake. Katika diwani hii mwandishi ameonesha vikwazo
mbali mbali vinavyokwamisha ujenzi wa jamii mpya hapa nchini. Vikwazo hivyo ni
kama vile uongozi mbaya, rushwa, tamaa,
ukosefu wa elimu, ukoloni mamboleo, n.k.
Katika
kujadili dhamira hii mwandishi ameonesha mbinu/njia mbalimbali ambazo jamii inapaswa kuzitumia katika zoezi zima la ujenzi wa jamii mpya
hapa nchini.
1.
Uongozi Bora
Mwandishi ameonesha kuwa Uongozi bora unahitajika kwa jamii yoyote ile ili kuleta
ufanisi mzuri katika utendaji na utekelezaji wa
majukumu mbalimbali kwani Uongozi
mbaya unasababisha kushindwa kufikia malengo. Kutokana na uongozi mbaya ndiyo
maana jamii hufikia kufanya mpinduzi ili kuuondoa uongozi uliopo na kusimika
uongozi mpya ili kuijenga jamii kwa upya.
Katika
shairi la “Kimbunga” (uk 1) mwandishi
anaongelea juu ya mapinduzi yanayofanywa
na tabaka la chini dhidi ya tabaka tawala.mwandishi anasema;
‘’kimbunga mji wa siyu,kilichowahi
kufika,
Si kwa yule wal huyu,ilikua
patashika,
Kimeing’owa mibuyu,minazi kunusurika,
Nyoyo zilifadhaika.
Ametumia mji wa Siyu kama kielelezo kizuri kwa jamii yoyote inayotaka kufanya mapinduzi ili kuondoa viongozi wabovu na kuleta
viongozi bora. Katika mapinduzi hayo mwandishi amefafanua kuwa wengi ndio
wanaoathirika na wachache hunusurika.
Shairi la “Madanganyo” linazungumzia jinsi uongozi mbaya
unavyowadanganya wananchi, unavyowaathiri na kuwakera wananchi. Wananchi
hushiriki katika shughuli za uzalishaji mali (miradi mbli mbali) lakini matunda
ya jasho lao hufidiwa na wachache. Wachache hao husahau wale waliosulubika
katika uzalishaji na mtokeo yake wnanchi wanaishia kuishi maisha ya taabu.
Ubeti wa 6, msanii/mwandishi ansema;
“Mlitupigia mbiu, tulimeni ushirika,
Tukakatana miguu, kwa mapanga na
mshoka,
Manufaa kwa wakuu, wadogo yetu
mashaka,
Wezeni kutukumbuka, mjue nasi
wenzenu.”
Shairi la “Wenye Vyao Watubana” (uk 8) mwandishi
amejadili namna matajiri au vitu jinsi
wanavyowagandamiza, kuwanyonya na kuwabana wale wasio na chochote. Mwandishi
anawaomba viongozi wawatetee ili kuepukana na hali hii. Hii ni kutokana na
uongozi mbaya ndiyo maana hali kama hii ipo nchini lakini viongozi hawachukui
tahadhari.Ubeti wa 7, mwandishi anasema;
“Maji yamezidi unga, kwa lochi wa
darajani,
Kujitole mhanga, kwa bei hiwezekani,
Mvao wake wa kanga, ni shilingi
elifeni,
Wakubwa tuteteeni, wenye vyao
watubana.”
Shairi la “Kibwangai” linajadili dhana ya usaliti wa viongozi wetu
kwa wananchi wanaowaongoza. Mwandishi ameonesha jinsi wananchi wanavyowachagua
viongozi wao lakini viongozi hao wakishapata madaraka au wakishashika nyazfa wanageuka
na kuwasaliti wananchi waliowachagua. Msanii
anathibitisha hayo kwenye ubeti wa 7;
“Kibwangai alipoona, ni mtu kakamilika,
Akaanza kujivuna, na dharau kuzidiya,
Wala hakujali tena, wenzake
waliwambiya,
Akahisi hawi nyani, umbo lile
litadumu.”
Shairi hili, limetumia taswira ya Kibwangai kuwakilisha
viongozi wasaliti na nyani kuwakilisha
wananchi wanaoongozwa na akina Kibwangai
yaani watawaliwa.
Katika shairi la “Hili
Mnatutakiya” , mwandishi anaonesha jinsi vyombo vya dola kama vile polisi
,jeshi namna vinavyoshindwa kutekeleza
wajibu wake wa kuwalinda raia na kuwashughulikia wahalifu..Ubeti wa 1msanii anasema;
Twasema kinaganaga,tumechoka vumiliya,
Wenzetu
mkatubwaga,hasa ukiangaliya,
Hao wezi
mwafuga,wazidi kutuibiya,
Msanii ameonesha kuwa vyombo hivyo
ndivyo vinavyowalinda wezi,majambazi na
matapeli.Kwa ujumla msanii wa diwani hii anaona kuwa ili tujenge jamii mpya
lazima tuwe na uongozi bora unaowajali wananchi wake.
2.
Kupiga vita rushwa
Rushwa ni
kikwazo kimojawapo kinachokwamisha kujenga jamii kwa upya. Kutokana na rushwa kuota
mizizi katika jamii haki hupotea,
wachache wanafaidi matunda ya nchi na
wengine wanaendelea kuumia. Shairi la “Rushwa”
mwandishi anasema;
“Rushwa kajenga kambi, na kuondoka hataki,
Afanya kila vitimbi, mkaidi hashindiki,
Tumzushieni wimbi, isiwe kutahiliki,
Tumchimbie handaki, rushwa
tukamzikeni.”
Katika ubeti huu, mwandishi anatuonesha kuwa
lazima jamii yetu ipinge rushwa ili haki na usawa vitawale.Kupiga vita rushwa
ni njia pekee itakayoisaidia kujenga jamii mpya ambayo mwandishi ameipendekeza.
3. Umuhimu wa Elimu
Ili tuijenge jamii mpya ni lazima watu wapate elimu na
waelimike bila kujali umri. Mwandishi anawahimiza wazee kujiunga na kisomo
chenye manufaa ili wafute ujinga wa kutojua kusoma na kuandika. Mwandishi anathibitisha haya katika shairi la
“Kisomo cha Maarifa” Msanii ansema;
Kisomo chenye manufaa,tusomeni kwa
haraka,
Isiwe tunakataa,kwa kuwa tumekongeka,
katika
shairi hili mwandishi anawahimiza wazee wajiunge na kisomo cha elimu ya watu
wazima kwa sababu wakishaelimika watakuwa na uwezo wa kupanga mipango yao ya
maendeleo. mwandishi anaonesha kuwa elimu ni silaha madhubuti katika kufanikisha
zoezi zima la ujenzi wa jamii mpya kwani
bila kuwa na wasomi katika jamii
kama hii yetu zoezi la ujenzi wa jamii mpya halitaweza kufanikiwa.
4. Kupiga vita ukoloni mamboleo
Ukoloni mamboleo ni kitendo cha nchi kuwa na uhuru wa bendera
lakini kimaamuzi inatawaliwa na nchi nyingine.Ukoloni mamboleo ni kikwazo
kikubwa kinachokwamisha maendeleo ya uchumi hapa nchini. Na ili tuweze
kufanikisha ujenzi wa jamii mpya hapa nchini hatuna budi kupiga vita ukoloni
mamboleo . Katika shairi la “Chuwi” Mwandishi
anaonesha jinsi ukoloni mamboleo unavyoathiri maendeleo ya uchumi hapa chini.
Ukoloni mamboleo unawaathiri watu wa tabaka la chini wasio nachochote na
kuwasetiri matajiri au tabaka la juu. Katika ubeti wa 6 mwandishi anasema:-
“Ambao ni matajiri, kwao anapowafikiya,
Huweza kujisitiri, salama kujipatiya,
Walokuwa mafakiri, huzidi kuwaoneya
Huyu ndiye Chuwi gani?
Mwandishi
ameeleza kuwa ukoloni mamboleo huingia kwa njia mbali mbali katika nchi
zinazoendelea. Hivyo mwandishi anatahadharisha kuwa tuepukane na mbinu (njia)
hizo na tuupinge ukoloni mambo leo kwa nguvu zote ndipo tutaweza kujenga jamii
mpya.
5. Umuhimu wa kujitawala
Ili tuweze
kujenga jamii mpya ni lazima tujitawale katika Nyanja zote za kifikra, kisiasa, kiutamaduni pamoja
na kiuchumi. Katika shairi la “Afrika “
Mwandishi anaeleza kuwa ili tuweze
kujitawala ni lazima tuepukane na unafiki, vibaraka (wasaliti), tusikate tama na tudumishe amani. Katika ubeti wa 3 msanii ansema:-
“Wasaliti wazikishe, wasio wenye
kuzuzuka,
Tamaa uwakalishe, yasiwe unayotaka,
Katu wasiwawezeshe, wabakie kuzuzuka,
Katu washindike mahusuda, wasiopenda
bara letu.”
Katika
shairi la “Kujitawala” Mwandishi anaeleza umuhimu wa
kujitawala kwa jamii yoyote ile. Mwandishi anaonesha kuwa, kujitawala ni
pale umma unapokuwa na mamlaka ya kuamua mambo yao wenyewe bila kuingiliwa au
kuwekewa vikwazo vyovyote.Katika Ubeti wa 1 Msanii anasema:-
“Kujitawala ni kwema, kuliko kutawaliwa,
“Kujitawala ni umma, kila yao kuamua…”
Katika
shairi hili la kujitawala mwandishi
anonesha faida mbalimbali za kujitawala kama vile demokrasia, kuwepo umoja
naushirikiano, kuwepo haki na usawa, amani hudumishwa, vile vile mila na
desturiza nchi zinadumishwa. Hivyo mwandishi anatuasa kuwa ili tujenge jamii
mpya ni lazima tujitawale kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kifikra.
6. Umuhimu wa kazi na kuwajibika
Kazi ni
nguzo muhimu sana ya ujenzi wa jamii
mpya. Mwandishi amesisitiza umuhimu wa kazi na kuwajibika katika shairi la “Kazi” Mwandishi anatuonesha kuwa kzi ndio msingi wa
maendeleo. Anasisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii na tuepukane na uvivu.
Ubeti wa 1, mwandishi anasema;-
“Pesa huletwa na kazi, ni njia
zipitiayo….”
Katika shairi la “Uokolewe”, mwandishi anasisitiza umuhimu wa kudumisha umoja na
mshikamano ili kuuinua uchumi wetu. Anasisitiza umuhimu wa kufanya kazi
kwa bidii kutumia vyema rasilimali zetu za kuinua uchumi wetu.
Hivyo msanii aniasa jamii kujihusisha na
ukulima, uvuvi, utalii na viwanda ili kujenga jamii kwa upya.
Katika shairi la “Dumizi” mwandishi anakemea tabia ya baadhi ya watu kukaa bila kazi
(uvivu) na kuanza maisha ya kunyonya.
Hivyo mwandishi anapiga vita unyonyajiwa watu waishio kwa jasho la wenzao.
7.
Mapenzi na ndoa
Katika diwani hii, mwandishi ameonesha kuwa
mapenzi yamegawanyika katika pande kuu mbili ambayo Kuna mapenzi ya kweli na
udanganyifu.
Katika shairi la “Usimpige Mkeo “ mwandishi anasema kuwa haifai mwanaume kumpiga mke
wake na vile vile mwanaume hatakiwi
kumwekea mkewe masharti magumu.
Shairi la “Hongera” mwandishi
anaendelea kujadili suala la mapenzi na ndoa katika jamii zetu. Anawaonya
wanandoa(bibi na bwana) wasiwe na tabia ya kufukuzana wawapo nyumbani. Amewapa kila
mmoja maadili yake kwa mwenzake. Beti za
(4-5) mwandishi anasema:-
4- “Bi arusi yangu shika, uyatie akilini.
Mumeo akifika, anapotoka kazini,
Mpe mema mamlaka, aliwazike moyo,
Hongera.”
5- “Bwana arusi sikia, ukiwa kwako
nyumbani,
Maneno ya kutupia, hayafai asilani,
Kauli njem tumia, na lugha iwe laini,
Hongera”
Katika
shairi la “Sifa ya Mke” Msanii anaonesha kuwa sifa kubwa ya mwanamke ni tabia
na wala si sura. Sifa ya tabia njema
humpa mwanamke taadhima, huruma, utiifu na hata uhodari. Anaeleza kuwa mwanamke anapaswa kuwa mtulivu, asiwe kiruka njia, asiwe na ufedhuli
wa aina yoyote, uovu, n.k.
Katika
shairi la “Sitaki” Mwandishi anakemea mapenzi ya udanganyifu
yaliyoshamiri katika jamii zetu kwa wakati huu. Anasema:-
“Rabi simpe mapenzi, hakuna wa kuamini,
Wapendwa wenye ujuzi, ni wachache
duniani,
Mapenzi yamepotea, sasa ni adimu sana,”
Ni kweli
mapenzi ya siku hizi hutawaliwa na pesa na yamejaa ulaghai wa kila aina pamoja
na udanganyifu.
8. Maonyo na maadili mema katika maisha
Mwandishi amekuwa mwalimu mzuri wa walimwengu kuhusiana
na harakati mbali mbali za maisha. Mawaidha aliyoyatoa mwandishi ni kielelezo
kizuri kinachofaa kufuatwa na kizazi hiki. Maadili na maonyo haya ni ya muhimu
sana katika maisha. Maadili hayo ni kama vile:-
(a)Malezi bora katika
jamii ni njia pekee ya kuiweka jamii katika msingi bora wa maisha. Katika shairi la “Vijana wa Zanzibar” Mwandishi ameonesha
kuwa matendo ambayo vijana wa siku hizi
wanayatenda si mazuri, ni ya kusikitisha. vijana wa siku hizi hawana utii, ni wajeuri,
ni wadanganyifu, ni majambazi na pia hudharau mila na desturi zetu za asili a
kukimbilia tamaduniza kigeni. Katika ubeti wa 2 msanii anasema:-
“Mwawacha yenu ya hapa, ambayo yako mazuri,
Kutii na kuogopa, mwaona haina heri,
Mwayavamia kwa pupa, kwa kedi na
jeuri,
Mila zetu za fakhari, wacheni
kuzipotosha.”
Kulingana na ubeti huu,mwandishi anaonesha
kuwa suala la malezi bora ni muhimu sana katika jamii ili kuwaandaa vijana wetu
kuendana na mazingira wanamoishi.
.
Kwa ujumla,
katik suala la malezi mwandishi anaifundisha jamii kuwa, samaki mkunje angali
mbichi.
b)Umuhimu wa
kuwathamini wazazi
Mwandishi
ameonesha kuwa kuna umuhimu wa kuwaheshimu na kuwathamini wazazi. Katika shairi
l “Wazazi” ameonesha kuwa wazazi ndiyo ngao ya mtoto;
mtoto hatakiwi kuwakasirikia, kuwaudhi wala kuwachikiza bali anatakiwa kuwa na
mapenzi nao. Wajibu wa wazazi kwa mtoto ni
kumpa chakula, mavazi, malezi mema pamoja na elimu. Katika ubeti wa 4:-
“Wakatafuta walimu, kukupatia ujuzi,
Wakakufunza elimu, pamoja na
matumizi,
Sasa ni mtu timamu, waendelea na
kazi,
Usiwaudhi wazazi, hiyo ndiyo yako
ngao”
Katika
shairi la “Ulezi Kazi” Mwandishi
ameonesha jinsi mama (wazazi) wanavyohangaika kubeba mimba hatimye kuzaa na
kuanza kazi ya ulezi wa mtoto hadi anapofikia umri wa kujitegemea. Anaonesha
kuwa wazazi hupata taabu na shida mbalimbali katika ulezi wao. Hivyo mwandishi
anashauri wazazi wathaminiwe napewe heshima zote.
c)Kuepukana na umbea
Umbea ni ile
tabia ya kutoa maneno au habari bila kutumwa. Mwandishi anaona tabia hii si
nzuri, kwani huweza kutenganisha marafiki au ndugu kwa njia ya uchonganishi.
Katika
shairi la “Wacha Hayo” mwandishi anaishauri jamii iepukane na umbea na badala
yake ijishughulishe katika shughuli za uzalishaji mali. Madhara ya umbea ni
kama vile majungu, uchochezi, n.k. Umbea
pia husababisha utengano. Ubeti wa 1 mwandishi anasema;
“Wacha kupika majungu, na kuleta uchochezi,
Kuwajaza walimwengu, kasumba zile na
hizi,
Hicho kimoja kifungu, huletesha
ubaguzi,
Tuacheni ubaguzi, huvunja mafanikio.”
Katika
shairi la “Hayafai Mitaani” mwandishi anaionya jamii kuwa si jambo la
busara au zuri kusambaza au kupeleka taarifa ya jambo fulani sehemu ambayo
haihusiki. Anaona kuwa ni busara sana endapo jambo fulani limefanyikia sehemu
fulani liishie huko huko lilikotokea na haifai kulipeleka sehemu isiyohusika.
Si tabia nzuri kupeleka mitaani kwa watu wasiohusika. Ubeti wa 2 unasema:-
“Yanayosemwa kunini, huko huwa yamekisha,
Haifai asilani, mitaani kufikisha,
Kwani siri ya mwituni, si vyema
kuelewesha,
Ya kunini huishia kunini.”
Hivyo mwandishi
anatushauri kuwa jambo mojalikitendeka sehemu moja ni bora liishie katika
sehemu hiyo na hakuna haja ya kulipeleka sehemu nyingine.
(d)Kuepukana na udokozi
(tabia ya wizi)
Udokozi ni
ile hali ya kunyemelea vitu visivyo vyako kwa lengo la kuiba au kunyang’anya.
Mwandishi anakemea tabii hii kwani si
nzuri. Tabia hii ipo miongoni mwa wanajamii. Mwandishi anaonya kuwa tabia hii
huhatarisha maisha ya wahusika yaani wenye tabia hii. Mwandishi amemtumia paka kuwakilisha watu wenye tabia hiyo.
Aidha mwandishi anaendelea anaelezea kuwa tabia hii husababisha uchokozi, ugomvi pamoja na chuki katika maisha.
(e)Umuhimu wa shukrani
katika maisha
Mwandishi
anaieleza jamii umuhimu wa kutoa shukrani pale mtu anapofanyiwa hisani na mtu
mwingine. Katika shiri la “Punda” mwandishi ameonesha jinsi baadhi ya watu wasivyo
na shukrani katika maisha . Ameonesha kuwa mwandamu asiye na shukrani hata
umfanyie wema kiasi gani hawezi kutoa shukrani. Ameelezea kuwa mtu asiye na
shukrani ni kuachana naye au kumtenga (kutengana naye) kabisa. Anasema;
“Punda hakumbuki wema, hta kwa mchunga wake,
Humpa mwingi mtama, na majianufaike,
Katu hawi salama, shukrani zake
mateke,
Ndiyo tabia ya punda, kurusha rusha
matee,
Kuchunga akikushinda, mwacheaende
zake.”
Katika ubeti
huu, mwandishi anasisitiza umuhimu wa kutoa shukrani pale tunapofanyiwa
fadhila.
UJUMBE
Ø Dhana potofu ya kudhani bila ya kuwa
na uhakika wa mambo haifai katika jamii kwa sababu hupotosha ukweli wa mambo.
Ø Mapenzi na ndoa ya dhati ni muhimu
katika jamii zetu
Ø Ukoloni mamboleo, uongozi, mbaya,
rushwa na ukosefu wa elimu ni baadhi ya vikwazo vya ujenzi wa jamii mpya hapa
nchini.
Ø Maadili mema na maonyo ni njia pekee
ya kuiweka jamii katika misingi ya haki na usawa.
FALSAFA
Mwandishi
anaamini kuwa maadili mema na maonyo ni njia pekee ya kuiweka jamii katika
msimamo na mwendo bora wa maisha na
anatetea misingi ya haki na utu katika jamii.
MSIMAMO
Msimamo wa
mwandishi una hali ya udhanifu kwani amejadili baadhi ya mambo katika jamii kwa
kudhani tu bila kuwa na misingi ya kisayansi.
FANI
a)Muundo
Mwandisha ametumia
miundo tofauti katika diwani hii kma vile;Tarbia (mistari 4), Tathlitha
(mistari 3) katika shairi la “Kujitawala”
(uk 7-8).
Pia ametumia muundo wa takhimisa (sabilia) – mistari 5 na kuendelea katika
shairi la “Punda” (uk 21-22), shairi
la “Bahati” (uk 36).
b)Mtindo
Mtindo
uliotumika ni ule unaofuata kanuni za mapokeo za urari wa vina na mizani pamoja
na mpangilio wa beti. Karibu mashairi yote yana vina vya kati na mwisho
isipokuwa katika mashairi ya “Kimbunga”
(uk 1), “Dumuzi” (uk 41), “Madereva” (uk 43), “Chuwi” (uk 42) yana nusu mstari katika kituo.
c)Matumizi ya Lugha
Mwandishi
ametumia lugha rahisi iliyoshehenezwa lahaja ya Kiunguja yenye mafumbo na taswira mbali mbali na
tamathali za semi kidogo na misemo kwa kiasi.
d)TAMATHALI ZA SEMI
Tashibiha
-Kwenye
shairi la “Sifa ya Mke” (uk 40)
-Ufedhuli na
uovu kama yake mazoea.
-Awe kama
malaika mzuri kupindukiya
Tafsida
Mwandishi
ametumia mbinu ya kufumba kwa kusema maneno makali, machafu, matusi kw kutumia
tafsida. Mfano shairi la “Nyang’au”
(uk 44) linahusu tamaa, “Paka” (uk
22) linahusu wizi, shairi la “Dumuzi”
(uk 41) linakemea uvivu, n.k.
Mbinu Nyingine za
Kisanaa
Takriri
Mwandishi
ametumia takriri ili kuweka msisitizo mfano shairi la “Kujitawala” (uk 7-8) neno
kujitawala limerudiwarudiwa.
Matumizi ya Taswira
Mwandishi
ametumia taswira nyingi kama vile;
Mfano:
Kimbunga …(uk 1)…..Kuashiria mapinduzi
Kibwangai…(uk 9)….Kuashiria viongozi
wasaliti
Nyani…..(uk 9)…….Kuashiria wananchi
waliosalitiwa
Chuwi…..(uk 42)…..Kuashiria ukoloni
mamboleo, n.k.
Jina la Kitabu
Jina la
Kitabu Kimbunga halisadifu yale yaliyomo
ndani ya kitabu kwa sababu hatuyaoni mageuzi yoyote ambayo anayajadili katika
kitabu hiki zaidi ya mashairi ya maadili mema na maonyo ya kimaisha. Asilimia
kubwa ya mashairi katika diwani hii yamejadili juu ya maonyo na maadili katika
maisha.
Kufaulu kwa Mwandishi
Kimaudhui
Mwandishi amefaulu ;
Ø Kutoa maadili mema na maonyo katika
jamii
Ø Kujadili dhamira ya ujenzi wa jamii
mpya
Ø Ameonesha mbinu mbalimbali za kufuata
ili tufanikiwe katika ujenzi wa jamii mpya
Kifani
Ø Ametumia lugha rahisi, mafumbo, taswira,
n.k.
KUTOFAULU KWA MWANDISHI
Kimaudhui
Ø Baadhi ya maadili aliyoyajadili
katika kitabu hiki ameyajadili kidhanifu, ni sawa na yale tunayoyapata
makanisani, ambayo yana nafasi ndogo sana katika ujenzi wa jamii mpya
Ø Vile vile amejadili masuala
mbalimbali kidhanifu hasa anapomhusisha Mungu. Kama vile maswala ya kipaji (uk
38-39), bahati (uk 36), umaskini (uk 35).
Kifani
v Mwandishi ametumia lahaja ya Unguja badala ya Kiswahili sanifu
ivyo ni vigumu kueleweka kwa watu wote.
v Diwani hii ni ya hali ya chini sana
katika muundo, mtindo na baadhi ya vipengele vingine vya kisanaa.