UHAKIKI-RIWAYA KITABU-USIKU UTAKAPOKWISHA MWANDISHI-MBUNDA MSOKILE MWAKA-1990 WACHAPISHAJI-DUP
UHAKIKI-RIWAYA
KITABU-USIKU UTAKAPOKWISHA
MWANDISHI-MBUNDA MSOKILE
MWAKA-1990
WACHAPISHAJI-DUP
UTANGULIZI
Riwaya ya Usiku
Utakapokwisha imejadili kwa kina masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii
katika jamii ya Tanzania baada ya miaka
ishirini na mitatu ya Azimio la Arusha.Mwandishi ameyaangalia baadhi ya kwa
jicho pevu matatizo yanayoikumbaTanzania katika juhudi zake za kujenga jamii
mpya ya kijamaa. Riwaya hii imekitwa kwa wahusika watatu: Chioko, Gonza na
Nelli.
Nelli ni mchumba
wake Chioko na wanaishi kwa Gonza ambaye ana chumba kimoja tu,Gonza anaishi kwa kutegemea kuuza karanga na kufanya
shughuli nyingine ambazo Chioko hazifahamu. Katika msako unaofanyika mjini ili
kutafuta wazururaji, Nelli anakamatwa na kupelekwa kijii cha mapinduzi. Chioko
hafanikiwi katika juhudi zake za kutafuta kazi: Gonza anamshauri Chioko waende
Zambia amabako watapata kazi. Chioko anatilia mashaka mpango huo; lakini
anapopata barua kwa Nelli kumweleza kwamba,anakuja kumtembelea na hali yeye
hana pesa anashawishika na mpango huo.
Mwandishi Kupitia wahusika hawa watatu anaichambua
jamii ya Tanzania na hali nzima ya mfumo wa kiuchumi na kijamii, na kuonesha
uozo uliomo katika jamii hii ambayo inatarajia kujenga mfumo wa Ujamaa. Suala
la rushwa, na utumiaji mbaya wa madaraka kwa viongozi, matabaka, dhiki za Walalahoi/makabwela
na masuala mengine mengi yanayohusiana na hali halisi ya kiuchumi,kisiasa na
kijamii Mwandishi ameyapa nafasi kubwa
na kuyajadili kwa kina katika riwaya hii.
MAUDHUI
DHAMIRA
KUU;UMASKINI AU HALI NGUMU YA MAISHA
Hali ngumu ya maisha au umaskini kwa makabwela umemshughulisha sana Mwandishi
katika riwaya hii ya Usiku Utakapokwisha. Katika riwaya hii, mwandishi anaonesha
kuwa umasikini umewatawala sana watu wa tabaka la chini kiasi kwamba, hata
mahitaji muhimu hukosa na kusababisha vifo vyao, kama asemavyo msanii (uk.7);
“Kifo kilichotokea kati
ya mama na watoto wake wawili uko Buguruni kinasikitisha. Ukweli ni kwamba haya
ni madhara ya ufukara na umasikini, watu hawa hawakua na kazi kwa muda mrefu na
maisha yao yamekuwa yakitegemea mno chakula kilichotokana na kuuzwa kwa vifaa
na vyombo vyao vya nyumbani. Lakini vifaa na vyombo hivyo vimeuzwa hadi
vikaisha. Mwishoni wakafa kutokana na kukosa chakula”.
Ugonjwa wa ufukara ulikuwa umewasonga sana watu wa tabaka la
chini. Kila wakijaribu kuutibu kwa kufanya kazi walishindwa (uk.11). Matatizo
ya maisha yaliwakumba wengi.Walijitahidi kupambana na shida usiku kucha, mchana
kutwa lakini mafanikio yao yakazidi kuwa duni. Mtatizo haya hayakuwakumba watu
wa tabaka la chini tu, yaliwakumba hata vijana wa shule.Katika uk. 16 mwandishi
anasema;
“Kwa watoto wa shule,
hasa wasichana walipita mitaani huku wakiwa wamebeba vyeti vya maisha yao. Kwa
upande wao, mtu aliyempa chai ni ‘mpendwa’. Aliyetoa pilau ni mfadhili na yule
aliyetoa lifti wakati wa jua kali lililokausha midomo yao na kuwatoa jasho
alikuwamungu mtu”.
Kutokana na umasikini vijana wengine walipoona hawana fedha,
walivuta bangi ili kutoa woga. Kisha wakawa wanauza bangi kwa siri,
walifanikiwa na walioshindwa walijiingiza kwenye vitendo vya wizi (uk.17).
Mwandishi ameonyesha namna makazi ya makabwela yanavyokatisha
tamaa. Waliishi sehemu duni ambazo hazina miundo mbinu kama Manzese. Manzese ni
sehemu muhimu ya mji wa Dar-es-salaam na ina mambo mengi. Huko ndiko wanakoishi
makabwela na makapera wa jiji hili, sehemu ambayo ni chafu na haitamaniki.Katika
uk.1 mwandishi anasema;
“Sehemu ya jiji ambayo inafukuta harufu ya uozo wa aina aina; sehemu
ambayo ina mashimo na makaro yanayobwabwaja maji machafu ya mji, sehemu ambayo
ina mabanda mbavu za mbwa yenye kushika tama kwa unyonge! Manzese
inahuzunisha!”.
Mwandishi ameonyesha namna makabwela/maskini wanavyoishi
maisha ya taabu sana, nyumba zao si salama, chakula chao cha taabu daima
wanaishi na wadudu kama vile nzi, mbu, panya, kama rafiki zao. Maisha ya mtu
masikini hayakudhaminiwa ndio maana hata wakipeleka malalamiko yao serikalini
hawashughulikiwi (uk.7).
Hali ngumu ya maisha au Umaskini imesababisha
makabwela kutegemea majaa ya takataka kupata chakula chao.Hawa waliokota vile
vyakula vilivyotupwa na wenye pesa ili kuokoa maisha yao ya kila siku. Katika
uk.25 mwandishi anasema;
“Wengine walikua wamejaa kwenye jaa moja la
takataka, karibu na barabara wakiokota punje ndogo ndogo za mchele zilizokuwa zimetupwa
huko.Pengine ilibidi wapepete makapi ya mchele zilizokuwa zimetupwa huko.Pengine
ilibidi wapepete makapi ya mchele kwa saa nyingi huku jua kali likiwachoma.Hakika
lilikuwa tatizo”.
Hali ya umasikini ina madhara yake kwa jamii.Kutokana na
umasikini makabwela wanapoteza utu wao. Mfano mtu yuko tayari kufungwa kwa
niaba ya mwenye pesa ya kununulia chakula kama asemavyomsanii (uk. 40);
“Mtu mmoja, mheshimiwa,
mwenye pesa alikuwa amepatikana katika kosa, akahukumiwa kifungo. Lakini yeye
liamua kulinda hadhi yake kwa kumtafuta mtu wa hali ya chini akafungwe ili
alipwe pesa”.
Maisha ya masikini yalitegmea kuzunguka mitaani na kuuza
karanga, na njugu huku wakifukuzwa na mgambo kila sehemu. Maisha yao niya
kukimbizana na mgambo kila sehemu; masikini akipata matako hulia mbwata. Kwa
ujumla, msanii anaonesha kuwa watu masikini kula kwao ni kwa taabu, kulala kwa
kwa taabu, kunywa kwao kwa taabu, kila kitu ni taabu kwao, hawana nafuu yoyote.
Mwandishi
anaonyesha kuwa kwenye hoteli za
makabwela vyakula vinavyouzwa navyo ni vya hali ya chini sana ukilinganisha na
mahoteli makubwa wanaokula viongozi na watu wengine wenye pesa.Katika uk.37
mwandishi anasema;
“Akapita mbele ya jingo
moja, akaona kibao kimeandikwa bei mbalimbali za vyakula. Maandishi yake
yalikuwa yakisomeka wazi.
NKom Ba hoTeLI
BEI: MAkonGolo……………………………………………………………………Shs
25.00
BatA La kUchoMA………………………………………….Shs 20.00
PUA
ya nguluwe…………………………………………...Shs 15.00
MBavu YamBuZI…………………………………………Shs 20.00
SuPu Ya kicHwa CHA kuku…………………….…….Shs 3.00
UtumBo wa KUKU………………………………………Shs 4.00
KichWA chA KuKu…………………………………………Shs 6.00
UGAli……………………………………………………………Shs 5.00
fIrIGIsi la BAtA ……………………………………………Shs
10.00
Fika JioNEE mWENYEWE: nDunGu:
ChAKula
Ni uZIMA: NKomBa end GampaNi
Sehemu hii ilikuwa maarufu kwa watu wa tabaka la chini,
lakini wa hali ya juu haikuwa sehemu maarufu kwao, kwani hoteli yenyewe haikuwa
ya hadhi yao. Pua ya nguruwe, supu ya kichwa cha kuku, utumbo wa kuku, na
filigisi za bata ni vyakula vya makabwela.
Katika kuondokana
na tatizo hili la umasikini. Gonza anasema lazima itafutiwe sababu ili tuweze
kuondokana na umasikini. Gonza anasema (uk.8);
“Panapowezekana pawezekane! Panaposhindikana pashindikane;na
sababu itafutwe na kutolewa hadharani”.
Mwandishi anaona kuwa ili tuondoe
umasikini, lazima tutafute kwanza chanzo cha umasikini huo.Chanzo kikipatikana,
hata hatua zakuchukua dhidi ya umasikini itakuwa rahisi kupatikana.Mwandishi
anapendekeza kuwa, kufanya kazi kwa bidii ni njia mojawapo ya kuondoa umasikini.(uk.
11);
Mwandishi anaonesha kuwa kufanya kazi kwa bidii kutaondoa
ugonjwa huu wa ufukara kwa makabwela. Bila kufanya kazi kwa bidii;itakuwa ndoto
kuondokana na huu umaskini.
Mwandishi anaona kuwa kurudi shamba si suluhisho
la umasikini kwani hata huko shamba kuna matatizo yake kama ilivyo mjini.
Mwandishi anasisitiza kuwa sio makabwela tu walazimishwe kwenda shamba
mabadiliko ya nchi lazima yawe ya watu wote na sio makabwela tu (uk. 19).
Mwandishi anaonesha kuwa lazima huduma zote muhimu zipelekwe huko kijijini ili
ziwavutie watu kwenda huko (uk. 19).
Mwandishi anaona kuwa ili kuondokana na umasikini ni muhimu kuanzisha
miradi mjini. Lakini kwanza lazima tuwe na nia, kama hatutakuwa na nia miradi
hiyo itakufa. Miradi anayopendekeza mwandishi ni kama vile maduka ya ushirika.
Kwa upande wa Gonza na Nyundo wanaona njia pekee ya kuondokana na umasikini ni
kupambana na wenye pesa kwa nguvu na kugawana kile wanachomiliki: Gonza na
Nyundo wanaona wenye vyeo ndio wamesababisha umasikini, kwahiyo tunapotaka
kuondoa umasikini lazima tupambane nao (uk. 74);
“Leo jioni kuna
kazi………leo usiku tutakwenda nyumbani kwa yule meneja wa kampuni ya mabomba……
Tanzania frendi; hatuwezi kulala njaa wakati watu wengine wanachezea mifwedha……
wanasaza mifedha……”
Mapambano ya Gonza dhidi ya wenye
navyo yanaangamiza maisha yake kabla usiku haujaisha. Mwandishi anatuonesha
kuwa mapambano dhidi ya umaskini si lelemama bali yanahitaji umoja na
mshikamano wa makabwela, kwani umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu (uk. 39).
Mwandishi wa riwaya hii ameonesha matatizo mbalimbali yanayoikumba
Tanzania ya leo kama vile umaskini,uongozi mbaya na rushwa,matabaka,wizi
na ujambazi,umalaya na matatizo mengine mengi na hizo ndizo dhamira ndogo ndogo.
1. SUALA LA UONGOZI NA RUSHWA
Azimio la
Arusha lilianzishwa mwaka 1967 hapa
Tanzania lilikusudia kujenga mfumo wa
Ujamaa.Katika Azimio hilo suala la uongozi bora lilijadiliwa kwa kina hasa
misingi yake.Mwandishi anaonyesha kuwa licha ya kulipa kipaumbele suala la
kujenga ujamaa lakini bado kuna viongozi ambao wanakiuka misingi ya kujenga jamii yenye
haki na usawa.Mwandishi ameonesha kuwa
viongozi wetu wako mstari wa mbele kupokea rushwa ili watoe huduma .Katika uk
13 mwandishi anasema;
“Natafuta kazi”
“Kazi?”
“Ndiyo kazi”
“Je una chochote?”
“Kama
nini?”
“Ma-dalla
kadhaa!”
“Ya kazi gani?”
“Ili tumlainisha meneja. Unajua
meneja ni mzee wa nyumbani, lakini habari hii ya dalla anaipenda sana. Hii ni silaha kubwa tukitaka
kufanikiwa mambo ya siku hizi magumu”
Akameza mate na kuendelea kusema
“Isitoshe, kila mtu tutakamopita
kabla ya kufika kwa mzee itabidi kutoa dalla kadhaa. Iko kazi”
Pia Suala hilo linajitokeza tena katika uk.21 pale Gonza
anapomtaka Chioko amshawishi mpenzi wake Nelli ahonge mwili wake ili apate
kazi, mwandishi anasema;
“Mwambie shemeji ahonge bwana.Kama hana pesa kama sisi anaweza kutumia
njia nyingine. Kama ujuavyo yeye ni msichana bwana. Anao uwezo mkubwa sana wa
kuwaweka sawa maofisa wa aina yoyote ile. Usiwaone wasichana wengine wamevalia
wakipita mitaan ukadhani ni hivihivi tuu”
Watu walioshika
nafasi za uongozi kwenye taasisi mblimbali wanaajiri watu baada ya kupata hongo
au rushwa na Iwapo mwombaji kazi ni mwanamke basi wanatarajia kulala nae kwanza
kabla ya kumpatia kazi. Lakini wakati mwingine msichana anayehusika anakuwa
kama mcheza kamari kwani anaweza kutoa penzi na kazi hapati kama anavyosema
mwandishi (uk. 21);
Kuna
vijana ambao pengine wanahonga lakini kazi yenyewe wasipate, na kuna wasichana
ambao pamoja na kuyakubali matakwa ya wakubwa, lakini hawafanikiwi katika matumaini
yao ya kupata kazi; wakubwa waliowaahidi kuwapa kazi wanawapa mimba na
kuwatelekeza. Hivyo basi, mwandishi anaona kuwa wanasichana hawanabudi kuepuka
rushwa kwani katika hali kama hii msichana anaweza kuwa Malaya.
Mwandishi anaitaka jamii kuwainga viongozi wanaotumia vibaya madaraka
waliokabidhiwa. Badala ya kuwaajiri watu kufuatana na kanuni zinazofahamika
katika masuala ya ajira, wao wanafuata kanuni zao wenyewe ambazo zinawaletea
maslahi binafsi.Mwandishi anaonyesha kuwa Matokeo ya msichana kutafuta kazi
yanakuwa kupata mimba (uk. 42-43). Msichana wa namna hii, ambaye anapata mtoto
na hana uwezo wa kumhudumia,kuna uwezekano mkubwa wa, kama hakufikiria kutoa
mimba kabla ya kujifungua au kumtupa mtoto baada ya kuzaa.
Suala la uongozi mbaya, wizi na njia
mbaya ambao watu wenye nyadhifa wanazitumia ili kupata pesa za kutumia kwa
ajili ya starehe zao ni kinyume na misingi ya Azimio la Arusha. Gonza anasema
kwamba, watu wengi ambao wana fedha nyingi wamepata fedha hizo kutokana na njia ya dhuluma au za wizi. (uk 43);
“Wewe sikiliza, Chioko uawaona wale
wenye mifedha hapa mjini”? Wengi wao wamedhulumu walishikwa? Hawakushikwa.
Walioshikwa n bahati mbaya na hawana raha”.
Katika hali
kama hii maskini au walalahoi au makabwela hawafurahii matunda ya uhuru yaani kana
kwamba uhuru umetekwa nyara na watu wachache ambao wananufaika kutokana na
uhuru huo.
Wakulima na wafanyakazi sio wanaonufaika na
jasho lao, bali vibepari uchwara ambavyo vimepata bahati ya kujipachika katika
sehemu za uongozi. Wao ni wanyonyaji wa jasho la wakulima na wafanyakazi.
Wakati wakulima na wafanyakazi wanatoa jasho lao kufanya kazi, viongozi hao
ndio wanaolifaidi jasho hilo. Matokeo yake ni kuwa, matunda ambayo mkulima na
mfanyakazi wanayahangaikia usiku na mchana hawayaoni. Hawaoni jinsi ambavyo
serikali inajitahidi kuondoa matatizo yao yanayowakabili. Wameshindwa kujikimu
walau kwa mahitaji yao ya lazima.
2.
UJENZI WA VIJIJI VYA UJAMAA (Operesheni sogeza)
Miaka ya
1974 Tanzania ilifanya ikifanya jitihada ya kujenga vijiji.Kumekuwa na juhudi
mbalimbali za kujenga vijiji .Katika
kujenga vijiji vya ujamaa hapa Tanzania njia mbili zilitumika ambazo ni:
Ø Kuwaweka pamoja watu ambao nyumba zao zilikua
mbalimbali
Ø Kuwasaka watu wasio na kazi mjini na kuwapeleka vijijini.
Dar-es-salaam,kama miji mingine ya
Tanzania umewahi kukumbwa na msako wa watu wasio na kazi ambao wamekamatwa na kupelekwa kijiji cha
mapinduzi.Riwaya ya Usiku Utakapokwisha
inalishughulikia tatizo hili.Watu wasiokua na kazi wanakamatwa na kupelekwa
kwenye kijiji cha ujamaa cha mapinduzi, miongoni mwa wanaokamatwa ni wauza
karanga,maji ya barafu,korosho kama asemavyo msanii(uk. 48);
“Walishikwa wa aina aina.Wauza
kashata,Njugu na karanga,walikuweko wauza pombemwenye mabaa,walikuweko walevi
pia,walikuweko wale waliofikiriwa pia kuwa ni wezi walikuwepo.Tulipofika huko
tulikua watu wengi, huko tulikuta pia wachawi waliokuwa wamekamatwa na
kupelekwa huko kama adhabu. Tulikutana wengi……………………”
Watu hawa
wote walishukiwa kwamba,wao ndio wezi ambao usiku wanabomoa majumba. Iwapo ni
hivyo, basi kitu ambacho kinafanyika ni kama kuusafisha mji, watu ambao
hawatakiwi kuwepo mjini na kuwapeleka vijijini.
Je,ndiyo kusema kwamba vijiji ndio vimekuwa
ngao ya kuhimili mishale inayorushwa?Je, pengine kusingeweza kupatikana na
uwezekano mwingine wa kuwashirikisha watu hawa katika shughuli za kijamii
wakiwa hukohuko mijini badala ya kuwasukumizia vijijini ambako hawakai bali
wanatafuta mbinu za kutoroka na kurejea tena mjini? Aidha, kuwapeleka watu kama wezi na
wanyang’anyi vijijini kunatoa picha ya kwamba vijijini ni mahali pa kuishi watu
wa aina iyo. Hivyo basi, kitendo hiki kinaweza kufisha juhudi zote za kujarbu
kuviimarisha vijiji na kuvifanya mahali pazuri pa kuishi.
Katika maongezi yake, Nelli anakisifu mno
kijiji cha Helela.Anatoa picha ya kwamba hapo ni mahali ambapo hakuna matatizo
(uk. 49);
“Kijiji hiki kina wakazi wapata elfu saba. Kina umeme, kina maji, kina
chakula kingi na cha kutosha kuwalisha majirani wa vijiji vikubwa visivyopungua
kumi. Helela imesonga mbele, kijiji cha Helela kina mashamba mengi ya mahindi
na ngano, mashamba ya maharage, ndizi na smatunda mengineyo. Naikumbuka Helela,
naipenda Helela. Helela imesonga mbele”.
Picha
anayoitoa Nelli kuhusu Helela ni ishara ya maendeleo ya kuridhisha kwa vijiji
vya ujamaa vilivyoanzishwa na serikali, na vijiji lazima viige maendeleo ya
kijiji cha Helela.
Baada ya
kukamatwa Nelli na kupelekwa kijiji cha mapinduzi, kulitokea matatizo
mbalimbali. Kwanza kulitokea fujo, mkusanyiko wa waovu mbalimbali hauwezi
kujenga jambo la maana. Kutokana na kuwepo kwa wachawi, wezi, wahuni ikatokea
vita vya kugombea wasichana (uk. 48).
Baada ya
zile vurugu za kijiji cha mapinduzi, watu wengi sana walifanikiwa kutoroka na
kurudi tena mjini. Kurudi kwao mjini kunaonesha kwamba, katika mfumo kuna jambo
Fulani ambalo linakosekana. Je, jambo hilo ni lipi? Nelli (uk.50) anasema; “Utaratibu
wake si mzuri”.
Katika mfumo
wetu wa kijamii kuna tofauti kubwa kati ya mfumo wa mji na kijiji, mfumo wa
kiuchumi na kijamii umeipendelea zaidi niji kuliko vijiji. Katika masualaya
mawasaliano na huduma nyingine za kijamii hakuna uwiano kati ya miji na vijiji.
Vitu hivi vimeshughulikiwa mjini lakini vijiji vimeachwa nyuma. Huu upendeleo
wa miji dhidi ya vijiji ndio unaowafanya watu wakapendelea zaidi kuishi mijini
kuliko vijijini. Na ndio maana watu waliosakwa na kupelekwa kijiji cha
Mapinduzi wanaamua kutoroka kutoka huko na kurudi mjini ambako kuna starehe
ambazo huko vijijini hazipatikani.
Kwa upande wa Gonza, yeye hana sababu ya
kwenda kijiji cha mapinduzi. Gonza amezaliwa mjini, amekulia mjini na
ataendelea kuishi mjini kama alivyosema(uk. 50);
“Mimi binafsi sipendelei “Alijibu
Gonza haraka haraka”.
“Kwa nini?
“Nimezaliwa mjini, nimekulia mjini;
na sasa makazi yangu ni mjini; shamba nimfuate nani na nikafanye nini?”
Kwa upande
wa Nelli, amejifunza maisha ya kijijini na baada ya kurudi mjini anatamani
kurudi tena kijijinimradi tuu ahakikishwe usalama wake, anasema (uk. 51);
“Niko tayari kurudi tena huko
nikihakikishiwa usalama wangu”.
Gonza
anashangaa kusikia tamko la Nelli la kutaka kurudi kijijini. Kwa ujumla, msanii
anaonesha kuwa kuwasaka watu na kuwapeleka vijijini si suluhisho la msingi. La
muhimu ni kutafuta suluhisho la matatizo hayo mjini hukohuko.
3. SUALA LA MAPENZI
Ni hali ya kupenda na
kuvutiwa sana inayojengeka baina ya mtu mzima mmoja na mwingine.Mwandihi
ameainisha aina mbili ambazo;
Ø mapenzi ya kweli na mapenzi ya uongo
(pesa).
Ø Mapenzi ya kweli
Kwa upande
mwandisi ameainisha kama ifuatvyo;
Mosi,mapenzi ya kweli kati
ya Chioko na Nelli; hawa walipendana hasa katika shida na raha,katika uk.2-3 Chioko anasema;
“Barua hiyo ilikuwa imetoka kwa
mpenzi wake Nelli. Nelli alikuwa tumaini la maisha yake ……Nelli……Nelli alikuwa
waridi la moyo wake.Nelli alikuwa kioo cha maisha yake…..Nelli alijazwa katka
kilakona ya maisha yake”.
Pia katika
uk.6 Chioko anaendelea kusisitiza kuwa ;
“Nelli ndiye ua langu…Nelli ndiye
waridi la moyo wangu mchanga ……….Nelli wangu “
Maneno ya Chioko
dhidi ya Nelli ni ishara tosha kuwa ,hawa watu walipendana kwa dhati na mapenzi
yao hakuna wa kuyatenganisha labda kifo tu.
Pili,mapenzi ya kweli
kati ya Chioko na Gonza, Chioko na Gonza walikuwa marafiki hasa na wasiri wakubwa. Walikuwa
wamesoma wote huko Iringa,ingawa kiini chao kilikuwa tofauti.Wazazi wao
walikuwa wakifanya kazi huko Iringa. Na huko ndiko walikokutana vijana hawa
wakashibana.Walielewana sana.Walikuwa wameelewana hata wakawa wanazungumza kwa
kutumia viungo vya miili yao na sasa walikuwa wamekutana tena hapa jijini na
waliishi pamoja kwa kusaidiana hadi kifo cha Gonza.
Kwa upande wa mapenzi
ya uongo ambayo msingi wake ni pesa mwandishi anaonyesha
kuwa Wanawake wengi waliwapenda wanaume tofauti kwa sababu ya pesa. Wanafunzi
nao walikua kwenye mkumbo huohuo,wa kupenda wanaume kwa sababu ya pesa,kama
asemavyo msanii (uk 17);
“Utanipa nini nawe katika kipindi
hiki cha dhiki”? Alidharau msichana
mmoja alipokuwa ametupiwa kombora la penzi na kivulana kitanashati kilichokua kinasoma hapa jijini”.
Mwandishi wa
riwaya hii anaonesha kuwa mapenzi ya
pesa kwa kiasi kikubwa yanatokana na hali ngumu ya maisha inayowakabili watu wa
tabaka la chini. Nakutokana na hali hiyo ndiyo maana linajitokeza tatizo la
umalaya jijini.
4. TATIZO LA USAFIRI
Mwandishi
anaonesha kuwa katika jiji la Dar-es-salaam kuna tatizo kubwa la usafiri kwa
watu wa tabaka la chini.Usafiri pekee unaotumiwa na watu wa tabaka la chini ni
UDA ambapo mtu unakaa kituoni kwa muda mrefu Kutokana na uchache wa mabasi ya
UDA.Katika uk. 27 mwandishi anasema;
“Walifika kituoni, hapa walikuta umma
wa watu, utadhani kulikuwa na sherehe ya kumtoa mwali na ambaye leo hii
amefunga ndoa”
Mwandishi anaoneshak kuwa Licha ya watu kukaa
sana vituoni kusubiri usafiri pia kuna tatizo la msongamano wa watu kwenye
vyombo hivyo vya usafiri. Watu wanasukumana, kila mmoja akigombea nafasi.Hasara
za kusukumana huko ni kuibiana na kupata vilema ambavyo havikutegemewa (uk. 29).
Mwandishi naonesha
kuwa kwenye vyombo hivyo vya usafiri, kuna matusi ya kila aina.Mtoto anamtukana
mtu mkubwa, konda anamtukana abiria,abiria wanamtukana konda na dereva, matokeo
yake ni matusi mtindo mmoja. Kutukana matusi kwenye vyombo vya usafiri ni kinyume
na utaratibu wa jamii, kwani kwenye vyombo hivyo kuna watoto.Hivyo matusi hayo
yanawakomaza watoto kabla ya umri wao (uk. 29-34).
Kutokana na tatizo hili la usafiri kwa watu wa
tabaka la chini; wengi wao wanachelewa makazini na kwenye shughuli nyingine za
kujenga taifa. Mwandishi ameongelea tatizo hilo miaka ya 1990, na bado tatizo
hili linaendelea, leo hii watu wanapitia madirishani kutokana na tatizo la
usafiri.
5. UTOAJI MIMBA NA UTUPAJI WA WATOTO
Suala la utoaji mimba linaonekana kuota mizizi katika jamii
ya sasa.Mwandishi amejadili suala hili kwa mapana.Kwa kuangalia suala hili kwa
mapana zaidi inaonekana kwamba, ukiacha wanafunzi wa vyuo vikuu, wanafunzi
wengine wote wanafukuzwa shule wanapopata mimba. Tatizo hili pia linapelekea
utoaji mimba au utupaji wa watoto (uk. 56).
Mwandishi wa
riwaya hii anaonesha kuwa suala la utoaji mimba na utupaji wa watoto ni tatizo
sugu, na hili kwa kiasi kikubwa linasababishwa na umasikini .Katika uk. 42-43
mwandishi anasema;
“…… Mara ngapi watu huimba jijini juu
y wasichana wanaoitwa Malaya ‘ na wale wanaotupa watoto mapipani………
wanawalaumu…… eti Malaya! Ati wahuni! Ni kweli wanauza miili; sawa lakini tumekaa na kufikiri kwa
nini? Nani anapenda mwili wake? Ni mwanake gani angependa
kumridhisha kila mwanaume? Hakuna!Nani anapenda kutupa watoto? Hakuna lakini
kuna maana gani kutunza mtoto wakati huna chakula cha
kumlisha? Uhai wa mtoto huyu ni nini kama
si chakula? Kwa msichana anayetafuta fedha akipata mimba ni suala la bahati
mbaya yeye anataka chakula …… matokeo ya mtoto hayakutarajiwa wala hayaheshimu”
Suala hili
linafungamana na suala zima la mfumo wa kiuchumi na kijamii. Wasichana wanatoa
mimba au kutupa watoto kwasababu hawawezi kuwakimu kimaisha. Mkabala wa jamii
dhidi yao ni wa kikatili. Kupata kwao mimba kunaangaliwa kama mtu ambaye
amefanya dhambi isiyosameheka.Kuogopa hali ngumu ya jamii kunawasukuma
wasichana hawa ama kutoa mimba au kutupa watoto.
Katika
kutatua tatizo hili mwandishi anapendekeza kwamba, lazima tuchunguze kwanza
mfumo wa uchumi na kijamii. Mfumo mzima wa kiuchumi na kijamii hauna budi
kuchunguzwa. Na katika mambo hayo ndimo ambamo jawabu la tatizo hili linaweza
kupatikana.
6.
NAFASI YA MWANAMKE
Katika riwaya hii mwanamke amechorwa katika
nafasi mbalimbali.
Kwanza mwanamke amechorwa kama chombo cha
starehe kwa wanaume.Viongozi na mameneja wengi wanawatumia wanawake
kukidhi haja zao za kimwili pindi wanawake hao wanapokwenda kutafuta kazi ili
apate kazi lazima amstareheshe kwanza mwajiri wake (uk. 23).
Pili,mwanamke amechorwa kama kitega uchumi
na ndiyo maana Gonza alimshawishi rafiki yake Chioko amshawishi mchumba wake
Nelli akahonge penzi apate kazi ili wapate hela ya kwaajili kukidhi mahitaji
yao muhimu ya nyumbani.
Tatu, mwanamke amechorwa kama kiumbe duni
asiye na maamuzi yoyote katika jamii zaidi ya kumtegemea mwanaume,
katika uk 56 mwandishi anasema;
“Mwanamke …kwani mwanamke nani? Kila
cha maana hubebwa na mwanaume.Haki zote anazo mwanaume. Ndio mwamuzi na hakimu
nyumbani.Kazi ya mwanamke? Kuzaa, kupika na kumtumikia mume. Mwanamke!”
Nne,
mwanamke amechorwa kama mshauri mzuri wa mwanaume,mwandishi anaonesha kuwa Nelli
kama mshauri mzuri. Kwanza aliwashauri Gonza na Chioko kurudi kijijini na pia
aliwashauri kuanzisha miradi na shughuli mbalimbali za kibiashara zinazoweza
kuwafanya waishi na ndugu na wote wanaowahusu hapa mjini (uk. 51).
kwa ujumla Mwandishi anawalakini juu ya nafasi ya mwanamke
katika jamii.Mwandishi anaona mwanamke hana mchango wowote katika jamii zaidi
ya kumtegemea mwanaume tu.Mwanamke pia ananafasi yake katika kuleta maendeleo
ya jamii kama alivyo mwanaume.
DHAMIRA NYINGINE
8.UGUMU WA AJIRA
UJUMBE
Ø Ili tuweze kujenga jamii mpya lazima
tupige vita uongozi mbaya na rushwa.
Ø Mfumo wa elimu unaotolewa haumjengi
mwanafunzi kujitegemea, bali kutafuta kazi za ofisini.
Ø Umoja na mshikamano kwa watu wa
tabaka la chini ni njia mojawapo ya kupambana na umasikini.
Ø Kufanya kazi kwa bidii ni njia
mojawapo ya kuondokana na umasikini.
Ø Kutoa mimba au kutupa watoto chanzo kikubwa
sni hali ngumu ya maisha kwa wale wanaohusika.
Ø Tatizo la usafiri litatatuliwa iwapo
tu serikali itajenga miundo mbinu zaidi ili kuwezesha kununuliwa kwa magari
mengi.
MGOGORO
v Kuna mgogoro kati ya wenye navyo
(matajiri) na wasio navyo (masikini).
v Mgogoro kati ya tabaka tawala na
tabaka tawaliwa.
v Mgogoro kati ya mgambo na walalahoi
(masikini).
MSIMAMO
Msimamo wa
mwandishi ni wa kimapinduzi kwani ameonesha matatizo mbalimbali yaliyoko katika
jamii na baadhi ya suluhisho la hayo matatizo.
FALSAFA
Mwandishi
anaamini kuwa umasikini utaisha iwapo masikini watafanya kazi kwa bidii na
kuanzisha miradi mbalimbali ya biashara ambayo itawaingizia kipato cha kuweza
kujikimu. Vilevile anaona kuwa mfumo wa kiuchumi na kijamii lazima ubadilishwe.
FANI
MUUNDO
Mwandishi
ametumia muundo wa rejea katika riwaya yake. Ameigawanya riwaya yake katika
sura tisa na matukio kutoka sura moja kwenda sura nyingine ni changamano.
Mtindo
Msanii
ametumia mtindo wa masimulizi na Nafasi
zote tatu amezitumia. Vilevile ametumia mbinu mbalimbali za kifasihi simulizi.
Kwanza kuna matumizi ya
nyimbo,mfano katika
ukurasa wa 23;
KILINDWACHO
Ajabu ya kilindwacho,
kwa upeo wa kulinda,
kilindwacho hutokea.
Na kwa mwizi kikanenda
Jizi likatoa macho
na kikanena kilindwa,
mwizi ni’ be hima hima,
ili nende nikalindwe.
Pili mwandishi ametumia hadithi ndani ya
hadithi. Hii inapatikana katika kurasa za 19, 24 na 42.
Tatu,matumizi ya barua,Barua mojawapo ni ile anayoandakiwa
Gonza na Chuchu kutoka Zambia inayomtaka Gonza aende Zambia, huko kuna maisha
mazuri.
MATUMIZI YA LUGHA
Lugha
aliyotumia mwandishi ni lugha rahisi iliyojaa misemo, methali, tamathali za
semi, mbinu nyingine za kisanaa na taswira mbalimbali.
v Misemo/ Nahau
·
Mtu
anayelala mbavu za mbwa – (uk.1).
·
Mtu
anayelala na mgonjwa ndiye anayejua miugulio yake (uk. 7).
·
Hatukupata
kiamsha kinywa (uk.10).
·
Jitu
hili la miraba mitano (uk. 29).
·
Hawamziki
mama yao akafika chini (uk. 39).
v Methali
·
Ukishindwa
kupata kwale mawindoni rudi na bundi (uk. 43).
·
Nguo
ya kuazima haisetiri matako (uk. 36).
·
Jino
la pembe si dawa ya pengo (uk. 36).
·
Alipo
kilema usikunje kidole (uk. 3).
·
Usipochomwa
mwiba hujui kiatu (uk.5).
TAMATHALI ZA SEMI
v Tashibiha
§ Hata majengo yaliyokuwa yamesimama
kama askari jela wa kikoloni yalikuwa shwari (uk.4).
§ Lakini iliyobeta kdogo mithili ya
mdomo wa bata (uk. 5).
§ Yalikuwa katika siri ya moyo wake
mithili ya kaburi lifichayo maiti (uk. 5).
§ Jogoo kama mfalme wa nyumba alifunza
vifaranga kunya tunduni (uk. 33).
v Tashihisi
§ Alichukuliwa na usingizi haraka
haraka, guu moja kalipinda na kuligandisha ukutani bila yeye mwenyewe kujijua
(uk. 1).
v Sitiari
§ Sehemu ambayo ina mabanda mbavu za
mbwa yenye kushika tama kwa wanyonge (uk. 1).
§ Nelli alikuwa waridi la moyo wake;
Nelli alikuwa kioo cha maisha yake (uk. 3).
§ Nelli ndiye waridi la moyo wangu
mchanga (uk. 6).
MBINU NYINGINE ZA KISANAA
v Tanakali sauti (Onomatopea)
§ “Myaau! myaau!myaau!Sauti kali ya paka
ilisikika juu ya paa (uk. 1).
§ Haa! Haa! Mwanaume mzima unaogopa
(uk. 9).
§ Baada ya muda kidogo nasikia sauti
kali pyaaaaa.
v Takriri
Ø Kila kitu kilikuwa kimya! Kimya
kushoto, kimya kulia …… Hata mbele kulikuwa kimya (uk.3).
Ø Alikuwa na kiu, Kiu kubwa! ….. Alijua
miugulio ya kiu (uk. 7).
Ø Nimeporwa a-a-a, nimeporwa jamani? Watu hawakujali (uk.
29).
TASWIRA
Katika
riwaya hii mwandishi ametumia taswira mbalimbali kama ifuatavo;
Kwanza ametumia taswira
zionekanazo za wadudu/wanyama kama vile nzi, kunguni, mende, viroboto, panya,
paka, n.k kuashiria makazi duni ya watu wa hali ya chini huko Manzese.
Pili, sehemu nyingine katika riwaya hii
giza limetumika
kuashiria matumaini finyu ya makabwela kuweza kupata nafuu katika maisha yao ya
kila siku.
WAHUSIKA
Mwandishi
ametumia wahusika watatu ambao ndio washiriki katika riwaya hii. Wahusika hao
ni Chioko, Gonza na Nelli: kuna wahusika wengine kama vile Chuchu, Nyundo,
Matiko, Kazimoto, Priscilla, Titos, n.k.
1.
CHIOKO
- Amemaliza darasa la saba na anatafuta
kazi ya ofisini. Yeye ni kiwakilishi cha vijana ambao baada ya kumaliza masomo
yao wanakimbilia mjini ambako wana mategemeo ya kupata kazi ya kuajiriwa.
-Chioko anakaa kwa rafiki yake Gonza,
Manzese.
-Alikuwa rafiki yake Gonza na msiri
wake na kabila lake ni Mngoni.
-Chioko hakubahatika kwenda sekondari
kutokana na kifo cha babake aliyetakiwa ampe vifaa vya shule.
- Alikuwa mpenzi wake Nelli na alikuwa
tegemezi kwa kila kitu.
2.
GONZA
- Huyu ni rafiki yake Chioko na kabila
lake ni Mgogo na alisoma mpaka kidato cha nne.
- Anaishi Manzese ambako anaendesha
maisha yake kwa kuuza karanga. Ni kutokana na hizo karanga ndio anaweza
kutosheleza kwa kiasi fulani maisha yake naya Chioko pamoja na Nelli.
-Anaishi maisha ya kikabwela katika
chumba kimoja.
- Anayaelewa maisha na mbinu za namna
ya kuyaishi. Gonza ndiye anayemfafanulia Chioko ambavyo wanawake kwa wanaume
wanavyotumia mbinu mbalimbali kupata kazi.
- Anawakilisha mawazo na malalamiko ya
tabaka linalokandamizwa. Anaona jinsi mfumo wa uchumi unavyowapendelea baadhi
ya watu ambao wanafanikiwa kimaisha kutokana na wizi au udanganyifu, pamoja na
kutofuata maadili ambayo jamii imekubaliana.
-Malalamiko aliyonayo ni ya kimsingi,
ndiyo yanayomsukuma kuwa mwizi.
- Anataka kuyakimbia maisha kwa kwenda Zambia
KWANI akifika huko atapata kazi.
3.
NELLI
- Huyu ni mpenzi wake Chioko na katika
harakati zake za kutafuta maisha anakamatwa na kupelekwa kijiji cha Mapinduzi;
ambako katika muda mfupi tu wa kuishi huko kunakuwa na athari katika maisha
yake.
-Anataka kurudi katika kijiji cha
Helela au Mapinduzi kama watamhakikishia usalama wake.
- Ni muhusika ambaye amechaguliwa
kuwakilisha mawazo ya kijiji. Kutokana na kuishi kwake kijiji cha Mapinduzi
amebadilika kabisa kimaendeleo, na hana analoongelea kuhusu kijiji cha Helela
isipokuwa sifa tu. Hivyo anafaa kuigwa na jamii.
MANDHARI
Mandhari ya
riwaya hii ni ya jijini Dar-es-salaam,hasa sehemu za Manzese, Kariakoo,Posta,Tandika
na Buguruni.Vilevile kuna mandhari ya nyumbani, barabarani, kwenye vyombo vya
usafiri, kwenye mabaa,mitaani, n.k.
JINA LA KITABU
Jina la
kitabu Usiku Utakapokwisha linasadifu
yale yaliyomo ndani ya kitabu hiki kwa kuwa Neno Usiku linamaanisha Giza.Giza
linaloongelewa na mwandishi ni matatizo wanayokabiliana nayo watu wa tabaka la
chini kama vile; Umaskini,Hali ngumu ya maisha,Ukosefu wa ajira,Tatizo la
usafiri n.k Je lini matatizo haya yatakapokwisha? Matatizo haya yamefananishwa
na Giza kulingana na utatuzi wa matatizo
hayo.
KUFAULU NA KUTOFAULU KWA MWANDISHI
KUFAULU
Mwandishi
amefaulu kwa kiasi kikubwa;
-Kuonesha matatizo mbalimbali yanayowakabili mafukara na
makabwela hapa nchini.
-Kuonesha chanzo cha matatizo hayo.
-Kutumia lugha rahisi inayoeleweka na amewachora
vizuri wahusika kuwakilisha hali halisi ya jamii.
KUTOFAULU
Suluhisho
la matatizo ya makabwela halijapatikana mpaka mwisho wa riwaya, tunachoona ni
wahusika kuandika kwenye mikokoteni yao “Iko siku” (uk.36). Hili ni suluhisho
la kukatisha tamaa, hiyo siku ni lini na kwa nini isiwe sasa. Kwa hapa
mwandishi hajatuonesha wazi suluhisho la matatizo aliyoyajadili.
Na Mwl GODLOVE J GWIVAHA
+255 764 745 763
+ 255 654 407 263