UHAKIKI WA USHAIRI KITABU: FUNGATE YA UHURU
UHAKIKI WA USHAIRI
KITABU: FUNGATE YA UHURU
MWANDISHI: MOHAMED S. KHATIBU
WACHAPISHAJI: DUP
MWAKA: 1988
UTANGULIZI
Fungate ni kipindi cha siku saba baada ya
harusi..Ni kipindi ambacho Bwana na bibi harusi hula na kunywa tena milo ya
kuchagua wakati wote wa fungate.Fedha na vifaa vitumiwavyo na maharusi huwa ni
vya kuazima au kuchangiwa(si lazima viwe vyao) Wanapewa kutoka kwa ndugu na jamaa na hata na vijana wa
kuwahudumia.Wachangaji hufanya hivyo kwa sababu wanajua kuwa fungate ni ya muda
mfupi(siku saba tu),hivyo huvumilia.
Fungate ni
lazima iwe na kikomo.Ikizidisha kikomo hicho ibadili jina labda iitwe
unyang’anyi,ulimbwende,uvivu,uzembe au jina lolote lenye kashfa hasa unafiki au
usaliti.Mwandishi wa diwani hii ameimwaga ghadhabu hiyo kwa hao maharusi
waliohesabu ukarimu wao kuwa ni upumbavu.
Uhuru:Uhuru
ni neno linalopendwa sana na wanasiasa wa ubepari au ujamaa.Hekaheka za
uhuru(kudai,kuomba au kupigania) zinaweza kufananishwa na shughuli za kutafuta
mchumba,kupeleka posa kulipa mahari,na kufunga ndoa.
Katika
kipindi chote cha uhuru, watu, hususani viongozi,hufurahi na kufanya sherehe
ambazo huwagharimu raia-mali na vitu mbalimbali.Lakini kwa kuwa uhuru ni kitu
cha thamani kama maharusi,raia hukubali kugharimia sherehe hizo.Lakini pia
sherehe za uhuru kama fungate hutazamiwa iwe ya muda mfupi –labda mwezi mmoja au miwili.
Raia wanchi
zilizopata uhuru barani Afrika walikuwa na shauku ya kupata maendeleo lakini
hawajafikia lengo lao hadi sasa kwa sababu viongozi wetu wanaendeleza Fungate ya
Uhuru.Hivyo viongozi wanchi za Afrika wamewasaliti wananchi wao
waliowachagua.Katika utangulizi mwandishi anasema ;
Nikate tama,
Kwani tuendavyo,hatufiki,
Vile ipasavyo,hayakamiliki,
Mambo yalivyo,ni unafiki,
Tumesalitiwa!
MAUDHUI
Fungate ya Uhuru ni diwani inayojdili kwa
mapana sana juu ya matatizo mbalimbali yanayokwamisha ujenzi wa jamii mpya hapa
Tanzania.Matatizo hayo ni kama vile usaliti,unafiki,wizi,hujuma,udanganyifu,rushwa
pamoja na uongozi mbaya.
Dhamira Kuu: Ujenzi wa jamii mpya.
Mwandishi
anajadili kwa kiasi kikubwa suala la ujenzi wa jamii mpya.Mwandishi
anaitaka jamii itupilie mbali unyonyaji , uonevu, dhuruma,
udanganyifu, wizi, unafiki, umasikini,
uongozi mbaya na ukandamizaji wa watu wa tabaka la chini ili kuijenga jamii kwa
upya.Jamii ambayo hatamu zote za uongozi (utawala,siasa na uchumi) zitakuwa
mikononi mwa wakulima na wafanyakazi kwa misingi ya haki na usawa.
Itikadi ya kujenga jamii mpya ilijengeka
juu ya siasa ya ujamaa na kujitegemea ambayo ilitangazwa mwaka 1967 baada ya
kutangazwa kwa Azimio la Arusha.Hadi
1988,mwandishi anaandika kitabu hiki anaonesha kuwa bado hatujafanikiwa kujenga
jamii mpya hapa Tanzania.Hii inatokana na sababu zifuatazo;
Kwanza,bado kuna dhuruma, usaliti,unyonyaji
na wizi wa mali za umma.katika shairi la
“Wingu’’ mwandishi anasema;
Bado:
Wingu limetanda,
Limetanda,
Na kutughubika ghubi,
Mvua:
Lakini hainyeshi,
Hainyeshi,
Ukame umetanda waa!
Mimea:
Tulipanda kwa miongo,
Kwa miongo,
Yote imekauka!
Pia katika
shairi la “Wizi”mwandishi ameonesha
dhahiri kuwa wizi umo ikuluni, bomani, kanisani, misikitini, na
hekaluni.Mwandishi ameonesha kuwa dini zawabariki wezi, polisi hulinda wezi, na
majeshi huhalalisha wizi.katika ubeti wa 1 mwandishi anasema;
Wizi
umo;
Kanisani,
Msikitini,
Kasirini,
Na
bomani,
Wanyang’anywao
ni waumini.
Pili,
mwandishi ameonesha kuwa bado kuna matabaka katika jamii zetu.Ameonesha kuwa
kuna tabaka la wenye nacho na tabaka la wasionacho.Tabaka la juu (utawala)
unaolinyonya tabaka la chini(tawaliwa).Mfano katika shairi la “Fungate”
mwandishi ameonesha jinsi tabaka tawala linavyofurahia maisha kwa kuishi katika
majumba mazuri, kutembelea magari ya faharin, n.k.
Katika
shairi la”Waja wa Mungu”mwandishi
anaonesha jinsi tabaka la chini linavyoishi kwa shida.Kwa mfano, kula kwa
shida, kulala kwa shida, kuvaa kwa shida, hawapati elimu na huduma nzuri za
afya.
Tatu, mwandishi ameonesha kuwa, bado kuna uongozi mbovu
katika jamii zetu.Mfano katika shairi la “Viongozi
wa Afrika” mwandishi anashutumu vikali viongozi wanaotumia madaraka
yao vibaya na kugandamiza watawaliwa.Anasema;
“Viongozi wa Afrika,
Wanaotawala kwa mabavu,
Kujifanya ni washupavu,
Wao wachache na werevu,
Na umma wote ni mpumbavu,
Wanafiki,
Wazandiki”.
Pia shairi
la “Njama” mwandishi anaonesha jinsi viongozi wanavyotumia njama mbalimbali
kulinyonya tabaka tawaliwa.Viongozi wanatumia njama mbalimbali ili kuhakikisha
kuwa hakuna anayewapinga wala kuhoji hata kidogo.
Nne, mwandishi anaonesha kuwa, kuna
unyonyaji wanaofanyiwa wakulima katika kuuza mazao yao.Ameonesha kuwa wakulima
hunyonywa na kudhurumiwa na kupewa bei kidogo wakati kuuza mazao yao.Shairi la
“Naona”mwandishi linadhihirisha haya katika ubeti wa 6,ansema;
Naona
Wanakwenda gulioni
Mazao kuyazabuni
Wanapata bei duni
Na kubaki maskini
Unyonge ulele.
Ni kutokana na matatizo hayo ya wizi,
rushwa, uongozi mbovu, dhuruma, uonevu
na unyonyaji ndiyo maana tumeshindwa kujenga jamii mpya.
Mwandishi
ameonesha mbinu mbalimbali ambazo jamii inapaswa kuzitumia ili kuijenga
jamii mpya na hizo ndizo dhamira ndogo ndogo za diwani hii kama
zifuatazo;
1.Kuwa na uongozi bora
Uongozi mbaya ni kikwazo kikubwa katika ujenzi wa jamii mpya.Shairi la”Fungate” Mwandishi ameonesha jinsi viongozi
wanavyotumia madaraka yao vibaya kwa kuwanyonya wananchi wa kawaida.katika
ubeti wa 1 mwandishi anasema;
Fungate ya uhuru,bado inaendelea,
“Harusi” wana nuru,wazuri wanavutia,
Wengi inawadhuru,na tena wanaumia
Mwandishi
anaeleza kuwa tangu tupate uhuru hadi leo bado viongozi wetu wapo Fungate
wakila na kunywa huku wananchi wakiendelea kuteseka na maisha magumu,hivyo
mwandishi anaitaka jamii kuung’oa
uongozi mbaya na kusimika uongozi uliobora unaowajali wananchi wake .
Shairi la “Viongozi wa Afrika”mwandishi anakemea
viongozi wanaotumia madaraka yao vibaya kwa kujinufaisha wao wenyewe, wenye
hisa katika viwanda, mabenki, makampuni au mashamba ya mabepari kuwa ni
wasaliti.Anawakemea wale viongozi wenye upendeleo, wanaotumia pesa za umma kwa
kuendeshea sherehe.Mwisho anawakemea viongozi wanaopokea rushwa na amewaita
magaidi au mafisadi.
Shairi la “Utawala” mwandishi amehimiza kuuangusha utawala wa kibepari ambao
unawanufaisha wachache na walio wengi hunyonywa, hugandamizwa, huonewa na
kunyanyaswa na hao wachache.
Shairi la “Kinyang’anyiro” mwandishi anaonesha
jinsi viongozi walivyokimbilia kushika madaraka (hasa enzi za uhuru) lakini
wanashindwa kuleta maendeleo hapa nchini.
Kwa ujumla mwandishi anapendekeza kuwa, ili
tujenge jamii mpya lazima tuwe na uongozi bora .
2. Kuwa na umoja na
ushirikiano
Mwandishi
anaona kuwa ili tujenge jamii mpya ni muhimu tuungane sote tuwe kitu kimoja “Katika shairi la “Unganeni” mwandishi anawataka wananchi
wote wa Afrika kuungana ili kuendeleza mapambano ya kuleta haki na usawa.
Anasema:-
“Wafanyakazi wa Afrika, tuungane,
Na wakulima kadhalika, tushikamane,
Makabwela mnaosumbuka, tukutaneni,
Tujiandae kwa mapambano, yalo marefu,
Ushindi ni wetu”.
Mwandishi anaitaka jamii hasa tabaka la
chini kuungana na kuendeleza mapambano dhidi ya viongozi wanafiki, mabepari,
mamwinyi wanaonyonya, wanaonyanyasa, wanaowatesa, wanaowadhurumu na
kuwagandamiza watu wa tabaka la chini.
Mwandishi
katika shairi la “Nikizipata Bunduki
‘’anapendekeza matumizi ya silaha ili
kuondokana na matatizo hayo yote. Hivyo ili tujenge jamii mpya ni lazima
tuungane tuwe kitu kimoja kwani ‘’Umoja
ni nguvu na utengano ni udhaifu’’.
3. Ujasiri na kujitoa
mhanga
Mwandishi anaona ili kuijenga jamii kwa upya ni muhimu kuwa na ujasiri,kutoogopa
vitisho. Katika shairi la “Gorila”
ubeti wa 1 mwandishi anasema;
Gorila,jasiri!
Wa Afrika ,shujaa,mshupavu,umevinjari,
Mtutu shika,mevaa,ukakamavu,uko tayari,
Gorila,ruwaza,wa kizazi kipya
Mwandishi anaitaka
jamii hasa vijana kuwa majasiri na mashujaa katika harakati za kuleta mapinduzi.
Pia wanamapinduzi wanatakiwa wawe wavumilivu kwa sababu ujenzi wa jamii mpya
sio lelemama, ni safari ndefu.
Vile vile katika shairi la “Umma” mwandishi anahimiza ujasiri katika kuleta
mapinduzi katika jamii. Mwandishi nasema:-
“Umma,
Uliovinjari, kuangamiza mtabaka,
Hima,
Uwe tayari na usiwena shaka,
Ongoza mapambano,ya wafanyakazi, hadi
ushindi.
Hivyo mwandishi anaitaka jamii ijitoe
mhanga ili kufanikisha suala la ujenzi wa jamii mpya.
4. Kufanya mageuzi
(mapinduzi)
Mwandishi
anapendekeza mbinu ya kufanya mageuzi ili kufanikiwa katika suala zima la
ujenzi wa jamii mpya. Katika shairi la “Umma”
mwandishi anawaasa wanajamii wajiandae kuangamiza matabaka yaliyokithiri katika
jamii.
Mwandishi
anapendekeza mbinu mbalimbali za kufanya mageuzi (mapinduzi), kwanza, jamii
hasa watu wa tabaka la chini waungane ii kuondoa viongozi wanaotumia madaraka
waliyopewa kwa manufaa yao binafsi. Katika shairi la “Ungameni”
mwandishi anasema;
Msimamo wa kitabaka,tuwekeni,
Bepari wote kuwashika,wawe ndani,
Na mamwinyi bila ya shaka,wambaroni,
Tusizubae,kazi ianze,twangoja nini?
Wakati ni huu.
Pili,mwandishi
anapendekeza kutumia silaha katika mageuzi hayo ikiwa unyonyaji hautaondoka kwa
amani. Mfano shairi la “Siku Itafika” na
“Nikizipata Bunduki” .Pia Katika
shairi la “Utawala” mwandishi
anapendekeza yafanyike mgeuzi ili
kuuangusha utawala unaojinufaisha na kuendeleza matabaka katika jamii. Katika
shairi la “Mjamzito” mwandishi
anaonesha jinsi watu wanavyoogopa harakati za mapinduzi katika jamii zetu.
Katika mashairi ya “Ni vita si Lelemama”
na “Maendeleo ya Umma” mwandishi
anaonesha jinsi suala la mageuzi lilivyo gumu, ingawa ana matumaini kuwa umoja
na ushirikiano wetu utatufanya tushinde. Pia anaamini kuwa unyonyaji na uonevu
hautadumu milele, kwani kuna siku, saa, dakika na nukta itafika uovu wote
utaondolewa kwa nguvu.
Katika
shairi la “Joka La Mdimu” mwandishi anatoa mfano wa tawala dhalimu
zilizoondolewa kwa nguvu kwa ushirikiano wa tabaka la chini. Katika shairi hili
mwandishi anaonesha jinsi wananchi walivyoshirikiana katika kuutokomeza ukoloni
hapa nchini.
Hivyo ili
nasi tufanikiwe kujenga jamii mpya hatuna budi kufanya mapinduzi (mageuzi).
5. Kuwa na uzalendo
katika nchi
Uzalendo ni
ile hali ya kuipenda nchi kwa dhati na hata kuifia. Msimamo wa mwandishi ni
kuwa hataihama nchi yake hata kwa kutishiwa njaa, maafa au umaskini. Pia
ataipigania nchi yake ili iwe salama. Hivyo hata sisi hatuna budi kuipigania
nchi yetu kwa hali na mali ili kuondoa udhalimu uliopo. Katika shairi la “Nchi
Yangu” mwandishi anasema;
Naipenda nchi yangu,
Naipenda,naipenda nitakufa naipenda.
Tailinda nguvu zangu,tailinda,
Tailinda kwa maafa tailinda,
Sitakwenda kwa wenzangu,
Sitakwenda,sitakwenda hata sifa
sitakwenda,
Nitakwenda hku kwangu,nitaganda,
Nitaganda kwa ulofa nitaganda.
Mwandishi anaona kuwa, tukiwa na uzalendo na
nchi yetu tutafanikiwa kujenga jamii mpya, kwani usaliti wa viongozi wetu
utaanguka na kila mmoja ataipenda nchi yake kwa dhati.
6. Kupiga vita ukoloni
mamboleo
Ukoloni
mamboleo ni ile hali ya nchi kupata uhuru wa bandia (kisiasa) lakini njia zote
za uchumi hutawaliwa au hubaki mikononi mwa mabepari au watu wa nchi nyingine.Katika
shairila “Ruya” mwandishi anasema;
Ruya,menitoa shamba,mji kuuramba niwe
utumwani?
chini umwinyini,
nimo kifungoni!
Ni ‘’huru’’ machoni!
Ruya,hivyo wanitimba,kunifunga kamba,za
ukoloni,
Njozi niondokee!
Mwandishi anaona kuwa wazungu ndio
walioondoka katika ardhi ya Afrika lakini unyonyaji bado upon a unaendelea.
Viongozi waliochukua madaraka baada ya uhuru bado wanaendeleza zile taratibu
zilizoachwa na wakoloni.
Katika shairi
la “Kunguru” mwandishi anaonyesha pia athari za ukoloni mamboleo hapa nchini.
Katika shairi hili mwandishi anazungumzia juu ya kuondoka kwa ukoloni mamboleo.
Hivyo mwandishi anaonesha kuwa ili tujenge jamii mpya ni lazima tupige vita
ukoloni mamboleo ili tuwe na uhuru wa kuamua mambo y etu wenyewe.
7. Kupiga vita wizi wa
maliya umma
Mwandihi wa
diwani hii ameshindwa kuficha hasira yake dhidi ya wizi. Ameutaja wazi kuwa umo
kanisani, msikitini, ikuluni na bomani. Waandishi wengi kukwepa kutaja ukweli kama
huu. Asemacho mwandishi ni kwamba, sehemu zote za jamii zimeoza. Zamani watu
wengi waliamini kuwa viongozi wa dini wana maadili wasiyoweza kuyakiuka. Kwa
hiyo, maovu hayo yasingetokea huko. Lakini sasa viongozi hao na wale wa Ikulu
wamejiunga na wahalifu. Lililo baya zaidi ni kuwapo kwa “Walinzi” wanaolinda
hao wezi.. Shairi hili la “wizi” mwandishi
anasema;
Wizi umo;
Kanisani,
Msikitini,
Hekaluni,
Wanyang’anywao ni waumini.
Kwa kifupi
wizi umehalalishwa na kubarikiwa .
Mwandishi hasemi tufanyeje Lakini kwa mtiririko na mantiki ya mashairi
yake mengine, mwandishi anashauri ufumuaji na usafishaji wa jamii nzima.Katika shairi la“Kunguru”
mwandishi pia anajadili Suala la wizi .
Japo amefumba lakini anawaelimisha
wasomaji kuhusu wezi waliotimuliwa na kutawanywa. Baada ya muda wezi
wakajitayarisha kwa mbinu tofauti na kuendeleza wizi wao. Mwandishi anatanabaisha raia kuhusu kuwapo kwa wezi hawa
na marafiki zao. Katika shairi la “Joka
la Mdimuni” mwandishi anatanabaisha watu kuhusu uwezekano wa wakoloni
kurudi kwa umbo tofauti lakini kwa athari zile zile. Katika shairi la “Naona “
Mwandishi anaonesha taabu wanazopata wakulima na malipo duni wanayopewa
kwa mzao yao. Anamaliza kwa msimamo huu;
”Naona
Ni fukara wakulima
Wamepigwa alitima
Kwa wengine ni neema
Kwao wao ni nakama
Wamekosa haki!
8. Kupiga
vita ukasuku wa viongozi wetu
Mwandishi amekemea tabia za viongozi na
watendaji wengine kukubali kila lisemwalo bila kufikiri au kwa hofu tu, si
nzuri. Tabia hii ya ukasuku anauita ugonjwa unaohitaji tiba (tiba yenyewe hakuitaja). Ugonjwa huu
hudunisha akili. Mwandishi anaonyesha chanzo na athari zake.Katika shairi la
“Ukasuku” mwandishi anasema;
“Kupea kwa ukasuku
Rais huhubiri
Wabunge hukariri
Wasomi huhariri
Na taifa husimama” .
Mwandishi anawachunguza viongozi wa bara la Afrik na
kuwaona kuwa ni mabepari, madikteta, wenye ukabila, wabadhirifu wasiojali raia
wao wapenda hongo. Wote amewakemea na kuwakanya wasitende hivyo. Amewapa majina
yanayowafaa- wahaini, wasaliti, majasusi n.k. Mwandishi anastahili pongezi kwa
kuweza kuwakemea, badhi ya waandishi huwasifu.
UJUMBE
v Uongozi mbaya, wizi wa mali ya umma,
rushwa na kukosekana kwa haki, ukasuku na matumizi mabaya ya mali ya umma ni
vikwazo ujenzi wa jamii mpya hapa
nchini.
v Umoja na ushirikiano ni njia moja
wapo ya ujenzi wa jamii mpya hapa nchini.
v Mfumo wa ujamaa ni mfumo pekee
utakaomkomboa mtu mnyonge, yaani ndiyo utakaoleta hali nzuri kwa wakulima au
wafanyakazi.
v Ili tujenge jamii mpya ni lazima tuwe
na ujasiri wa kujitoa mhanga, tuwe wazalendo na nchi yetu na tufanye mapinduzi
(mageuzi ya kweli) katika jamii.
v Ukoloni mamboleo ni kikwazo cha
ujenzi wa jamii mpya hapa nchini.
v Mapenzi ya kweli ni yale yasiyojali
fedha au hali ya mtu.
FALSAFA
Mwandishi
anatetea itikadi ya ujamaa yenye kuleta haki na usawa kwa kila mtu. Analaani
wizi, dhuluma na majivuno ya kirasimu. Mwandishi angependa nchi iongozwe kwa
haki na usawa. Vile vile anatetea mapenzi ya kweli katika maisha.
MSIMAMO
Mwandisi ana msimamo wa kimapinduzi, kwani ameonesha matatizo
mbali mbali yanayozikumba jamii zetu na mbinu za kuondokana na matatizo hayo.
Miongoni mwa matatizo hayo ni uongozi mbaya, wizi wa mali ya umma, rushwa na
dhuluma, n.k.
Fani
a)Muundo
Mwandishi
ametumia muundo changamano. Kuna muundo wa tathnia (mistari 2) mfano shairi la
“Mjamzito” (uk 5-6), Muundo wa
tathlitha (mistari mitatu) mfano shairi
la “Fungate” (uk 1), “Nataka Kusema” (uk 14), Muundo wa tarbia
(mistari minne) mfano shairi la “Nahodha
Mtwesi” (uk 5), “Gorila” (uk 11),
“Afrika” (uk 17) , “Kunguru” (uk 19), n.k.
Vile vile ametumia muundo wa sabilia au
takhimisa (mistari mitano na kuendelea) mfano mshairi ya “Utawala” (uk 21), “Ladha ya
Maji Katani”(uk 27), “Joka la Mdimuni”
(uk 31), “Mkata “ (uk 15) n.k.
b)Mtindo
Diwani hii
ina mashairi yanayofuata kanuni za ushairi wa kimapokeo na yale yanayofuata
kanuni za mashairi ya kisasa. Hii ina maana kwamba, mwandishi anayakubali
mashairi ya aina mbili (kimapokeo na kisasa)
c)Matumizi ya Lugha
Mwandishi
ametumia lugha sanifu yenye lahaja ya Kiunguja. Lugha hii imejaa misemo mbali
mbali, tamathali za semi na taswira.
Misemo
Imetumika
kwawingi.
Mfano:
i)Nahodha
mtwesi chombo chenda joshi (uk 5)
ii)Waja wa
Mungu (uk 20)
iii)Paka
shume (uk 34)
iv)Utakiona
cha mtema kuni (uk 24)
v)Joka la
mdimuni (uk 31) n.k.
Tamathali za semi
Tashibiha
Mfano shairi
la “Mkata” (uk 15):-
i)Kitandani
nilalapo kama dema la samaki…
ii)Mbu ndani
kama ndege wa vitani…
iii)Matopeni
hujazika mithili nimo karoni…
iv)Nimekoni
kama ndizi natokota na kufoka
Sitiari
Mfano shairi
la “Uwapi Uzuri Wako” (uk 35)
-Sasa ni
chano cha maji, watu wajichanyatia
-Baola
mkahawani, kila mtu akaliya
-Sasa jamvi
la wageni, wajapo huwapokeya.
Kejeli
-Shairi la “Fungate” (uk 1) linakejeli tabia za
baadhi ya viongozi wetu wanaoendelea kuifaidi Fungate ya Uhuru.
-Shairi la
“Kantu Sauti ya Kiza” mwandishi anatumia
nyuki kukejeli baadhi ya tabia chafu za watu.
Tafsida
Mwandishi
ametumia Tafsida kuyasema maneno makali, machafu, matusi. Mfano shairi la “Paka Shume” linajadili suala la
kumendea vitu vya watu kwa njia isiyo halali. Hata neno lenyewe fungate ni
tafsida.
Mbinu nyingine za
kisanaa
Takriri
Katika
shairi la “Mkata” (uk 15), “Dafina” pamoja na shairi la “Nchi Yangu”
Mjalizo
Katika
shairi la “Mkata” (uk 15).
Mdokezo
Katika
shairi la “Mwinyi Mpe Ndiyo”
Ujenzi wa Taswira
Neno Fungate
linaleta taswira ya ulimbwende wa maharusi au viongozi. Shairi la “Mjamzito” (uk 5) linajenga taswira ya
viongozi waoga katika jamii. Viongozi wasioweza kutatua matatizo ya wananchi.
Shairi la “Paka Shume” (uk 34)
linajenga taswira ya udokozi. Shairi la “Viongozi
wa Afrika” (uk 15) linajenga taswira ya viongozi wanaotumia madaraka vibaya.
Jina la Kitabu
Kwa ujumla
jina la kitabu Fungate ya Uhuru
linasadifu yale yaliyomo ndani ya
kitabu. Mwandishi ameonesha jinsi
viongozi wetu walivyo kwenye fungate ya Uhuru. Hali kadhalika wananchi bado
wanaendelea kugharamia sherehe mbali mbali za viongozi kwa njia ya michango
kama vile kodi, mchango wa mwenge, n.k.
KUFAULU KWA MWANDISHI
Kimaudhui
v Mwandishi amefaulu Kuonesha matatizo
mbali mbali ya jamii zetu na mbinu za kuyaondoa.
Kutofaulu kwa Mwandishi
v Mashairi mengi kyanahusu siasa na hivyo kuwa kama mahubiri ya kisiasa.
v Kusisitiza mfumo wa chama kimoja
badala ya mfumo wa mageuzi na kitabu
kiliandikwa wakati mfumo wa mageuzi
umepamba moto dunia nzima.
v Kumfanyia Mwinyi kampeni ni udhaifu,
hii ni kutokana na ukweli kuwa Rais Mwinyi hakuweza kuondoa matatizo
aliyoyajadili na ndiyo maana hadi sasa yapo.
v Amekemea uongozi mbaya, lakini
hakuonesha chanzo cha uongozi mbaya na mbinu mbali mbali za kuwapata viongozi
bora hapa nchini.
v Kutumia lahaja ya Kiunguja ni udhaifu
mwingine wa mwandishi, kwani anakinyima Kiswahili sanifu uwanja wa kukua na kuenea.