SANAA ZA MAONYESHO
Kuna aina kuu tatu za sanaa. Kwanza ni
sanaa ambazo uzuri wake hujitokeza katika umbo la kudumu, umbo ambalo
linaweza kuhifadhiwa na uzuri wake kuonyeshwa wakati wowote. Hizi ni
sanaa za uonyesho.
Nazo ni kama vile uchoraji, uchongaji, ufinyanzi na utarizi.
Uzuri wa sanaa za vitendo umo katika umbo la vitendo, na ili kuupata uzuri huu yampasa mtu kutazama vitendo vikifanyika.
Umbo hili linalazimisha kuwepo kwa msanii na mtazamaji wa sanaa mahali pamoja kwa wakati mmoja ama sivyo sanaa haikamiliki.
Hali hii ndiyo iliyosababisha sanaa
za vitendo kuitwa sanaa za maonyesho, kwa sababu lazima wakati
zinapotendeka awepo mtu wa kuonyeshwa, maana uzuri wake umo katika
vitendo vyenyewe.
Kwa hiyo sanaa za maonyesho ni
kitendo chochote kinachohitimishwa na dhana inayotendeka, mtendaji,
uwanja wa kutendea na watazamaji. Zipo nadharia tatu zinazoelezea
chimbuko na asili ya sanaa za maonyesho.
MICHEZO YA KUIGIZA
Sanaa za maonyesho ni michezo ya
kuigiza, ama ni michezo inayoonyeshwa kwenye jukwaa lenye pazia na taa
nyingi za jadi. Huu ni mtazamo mmojawapo ambao unaaminiwa na baadhi ya
wataalamu kwa kuwa unasisitiza kwamba sanaa za maonyesho lazima zichezwe
jukwaani, kuwepo na pazia na taa nyingi.
Nadharia hii inatuaminisha kuwa sanaa za maonyesho ni tamthilia tu, jambo ambalo linaleta shaka kidogo.
Tamthilia ni utanzu ulioletwa na
Wakoloni kwa hiyo, kuamini nadharia hii ni sawa na kusema kuwa hakuna
sanaa za maonyesho zenye asili ya hapa Afrika Mashariki.
Ni sawa na kusema kuwa kabla ya ujio
wa Wakoloni sisi tulikuwa hatuna sanaa zetu wenyewe. Wazo hili si kweli
na ni potoshi. (Mhando & Balisidya 1976).
Mtazamo huu unatokana na fasili ya
sanaa za maonyesho inayodai kuwa sanaa za maonyesho ni kitendo chochote
chenye sifa za mchezo, mchezaji, uwanja wa kuchezea na watazamaji.
Dosari kubwa katika ufafanuzi huu
imo katika neno mchezo (play). Neno hili lina maana duni likilinganishwa
na hali na umuhimu wa sanaa za maonyesho zenye asili ya Kiafrika.
Tukichukua kwa mfano unyago, jando,
kusalia mizimu au masimulizi ya hadithi, ambayo ni mifano ya sanaa za
maonyesho zenye asili ya Kiafrika, tunakuta zile sifa zote zipo.
Isipokuwa tunajua kuwa shughuli zote
hizi si mchezo na umuhimu wazo hauruhusu hata kidogo kuingiza neno
mchezo. Shughuli hizi zina maana muhimu ambayo inahusu maisha ya
binadamu katika jamii yake.
Ni shughuli zinazobeba wazo maalum
lenye lengo la kujenga utu wa mwanajamii na kubainisha taratibu za
maisha yake. Basi vipi tuseme shughuli hizi zina sifa ya mchezo?
Wazungu wanaridhika na neno hili kwa sababu sanaa za maonyesho za utamaduni wao aghalabu zinafanywa kwa masihara tu.
Sanaa za maonyesho zao zaidi ni kwa madhumuni ya kujiburudisha au pengine kutafuta kipato.
Lakini kila aina ya sanaa za
maonyesho ya Kiafrika ina dhana fulani ndani yake, kwa mfano kuhusu
maana ya maisha, utekelezaji wa madaraka ya kiutu uzima, ushujaa,
maadili au mafunzo ya historia ya jamii.
Kwa hiyo basi sanaa za maonyesho za
Kiafrika ni dhana zilizo kwenye umbo linalotendeka na katu si mchezo.
Kutokana na utamaduni wa Kiafrika, tunaweza kusema kuwa sanaa za
maonyesho ni dhana inayotendeka.
Na ili dhana hii itendeke
anahitajika mtu wa kuitenda. Mtendaji huyu huhutaji uwanja wa kutendea
hiyo dhana na wakati akiitenda wanakuwapo watazamaji.
VICHEKESHO
Wakati Mkoloni alituletea sanaa ya
maonyesho ya kikwao, sisi tulishiriki katika tamthilia za Shakespeare
kama washiriki au watazamaji tu.
Tamthilia hizi hazikuwa na maana
yoyote kwetu kutokana na kuwa zilibeba na ziliongelea utamaduni wa
Kizungu. Tulifurahishwa na vile vitendo vilivyofanywa kwenye jukwaa
katika tamthilia hizi na hivyo vitendo hivi vilituchekesha tu.
Basi jambo kubwa kwa Mwafrika ikawa
ni vile vichekesho na hivyo kudhani kuwa jambo muhimu katika tamthilia
ni kule kuchekesha kwake.
MAIGIZO
Wazo hili limetokana na tafsiri
mbovu ya neno “play” ambalo lina maana ya mchezo wa kuigiza. Inawezekana
aliyetafsiri neno hili alifuata nadharia za zamani sana za drama,
ambapo ilidhaniwa kuwa uigizaji (imitation) ndio kiini cha drama.
Hata hivyo nadharia hii ilitupiliwa
mbali kwa vile haikudhihirisha kiini hasa cha drama. Wengi wamepotoshwa
na wazo kuwa uigizaji ndio kiini cha sanaa za maonyesho kama vile neno
michezo ya kuigiza linavyoonyesha.
Hivyo, hata katika kutazama sanaa za maonyesho za asili wengi wamekuwa wakitazama iwapo kuna uigizaji.
Na hapa wengi wanakwama kwani katika
unyago, jando, kusalia miungu n.k hakuna uigizaji bali wanaoshiriki
wanashika nafasi fulani fulani. Hivyo ni bora kutumia neno tamthilia
pale tunaporejelea “play.”
Ingawa zote ni sanaa za maonyesho, zina misingi tofauti kutokana na tofauti za utamaduni wa jamii husika.