3. FANI NA MAUDHUI YA HADITHI FUPI ZA KISWAHILI
Sura ya Tatu
KANUNI kubwa ya kuipima kazi ya sanaa na fasihi kwa ujumla ni
kuangalia uwiano uliopo kati ya fani na maudhui katika kazi inayohusika. Kanuni
hii ndiyo uti wa mgongo na roho ya kazi ya sanaa, hususan hadithi fupi ya
Kiswahili.
Suala la fani na maudhui katika fasihi ni pana na limeleta utata
mwingi miongoni mwa wanataaluma mbalimbali. Kwa sababu hii, ni muhinu kupambanua
vipengele hivyo vya kisanaa. Katika sura hii tutajaribu kueleza maana ya fani na
maudhui katika ngazi tatu. Kwanza tutajadili maana ya fani kama inavyoelezwa na
wanataaluma ama wanafasihi mbalimbali. Pili tutaangalia maana ya maudhui kama
inavyoelezwa pia na wanataaluma hao. Tatu, tutaona uhusiano na uwiano ulioko
kati ya fani na maudhui katika kazi ya sanaa. Mwisho tutaangalia kwa kifupi wapi
waandishi wa hadithi hizo wanaweza kuchota dhamira na aina za dhamira hizo.
Maana ya Fani
Cleanth Brooks na Robert Penn Warren wanaelezea maana ya fani
kuwa ni "vipengele mbalimbali katika kazi ya fasihi. Ni jinsi kazi hiyo
inavyojengwa ili kuipata maana yake."1 Halafu wanaendelea kusisitiza
kuwa "vitu hivyo ni lazima vihusiane vyenyewe, na pia vihusiane na kile
kinachosemwa ili kujenga kazi bora na yenye kuleta maana ya
kifasihi."2 Babette Deutsch naye anaelekea kukubaliana na wazo hilo
anaposema, fani ya ushairi ni "mpangilio wa mizani, beti..."3 n.k.
Akijadili maana hiyohiyo ya fani, Walter Blair na wenzake
anasema kuwa, "katika fasihi, fani ina maana ya tawi ama aina ya kazi ya sanaa
inayohusika."4 Halafu anaendelea kutoa mifano ya matawi au aina yake
kama vile hadithi, ushairi, na tamthiliya. Hii ni maana ya kwanza anayoitoa
mwanafasihi huyo. Maana yake ya pili anayoitoa ni ile inayohusu mpangilio au
umbo la kazi ya sanaa. "Ni jinsi kazi ya fasihi ilivyojengwa, bila ya kujali
maudhui yake."5
Dhana hii ya pili anayoitoa Blair na wenzake inatenganisha fani
na maudhui ya kazi ya sanaa. Jambo hili lina dosari kwa sababu sivyo ilivyo
katika kazi za sanaa za kifasihi. Kimsingi, fani na maudhui ni vitu ambavyo
vinatazamwa katika umoja na wala haviwezi kutenganishwa. Swala hili tutalijadili
baadaye.
Kwa upande mwmgine, maelezo yaliyotolewa hapa juu yanatupa dhana
mbili. Kwanza, kuna wazo linaloieleza maana ya fani kwa dhana ya tawi na pili,
kwa dhana ya umbo.
Dhana ya umbo inahusu uwezo wa msanii wa kusanifu kazi yake,
yaani kuunganisha vipengele mbalimbali vinavyoijenga kazi ya kisanaa
anayoishughu-likia.
Katika ushairi kwa mfano, fani ya ushairi huo itakuwa imepimwa
kwa kuangaliwa vipengele vyake kama vile miundo, mtindo, lugha, wahusika n.k.
Katika tamthiliya, licha ya kuangalia vipengele vilivyotajwa
hapojuu, vitu kama mandhari, wahusika, vifaa, lugha n.k. vitaangaliwa kama
vipengele muhimu vya fani ambavyo katika ujumla wake, vitatoa maana ya kazi
nzima.
Kwa upande wa hadithi, fani yake itajumuisha mambo kama vile
wahusika walivyojengwa, lugha ilivyotumika, mandhari, muundo na mtindo, n.k., na
Batimaye jinsi vipengele hivyo vinavyoleta na kuathiri maana ya kazi nzima.
Dhana nymgine ya fani m ile ya tawi ama utanzu. C. Hugh
Holmann6 anasema kuwa utanzu ni istilahi inayosimamia aina ya kazi ya
kisanaa kufuatana na umbo ama fani yake, yaani kufuatana na mbinu za uumbi ama
ujenzi wake. Ziko namna mbalimbali za kugawanya tanzu hizo. Kwa mfano, katika
fasihi simulizi na fasihi andishi tuna tanzu kama vile ushairi, hadithi na
tamthiliya. Lakini pia katika tanzu hizo tunaweza kupata matawi mengine
yanayogawanywa kwa kutumia misingi maalumu na ambayo bado yataitwa tanzu. Matawi
hayo, kwa mfano, katika hadithi tuna riwaya (hadithi ndefu) na hadithi fupi.
Katika ushairi tuna tanzu ama matawi mengineyo kama tarbia, tathlitha n.k. Na
katika sanaa za maonyesho tuna tamthiliya, vichekesho, n.k. Pengine tanzu hizo
zinaweza kugawanywa kidhamira.
Mgawanyo wa kitanzu una maana kuwa kuna makundi ya kazi za sanaa
zenye sifa maalumu katika aina moja ya utanzu, k.v. ushairi, au aina mbalimbali
ya kazi za sanaa k.v. ushairi na tamthiliya, na mbinu za ujenzi wake bila kujali
wakati na mahali pa uandishi wake, dhamira n.k. na kwamba vipengele hivyo vya
kifani ni vya msingi katika kuainisha kazi ya sanaa inayohusika. Tanzu za
kifasihi, kwa mujibu wa Rene Wellek na Austin Warren zinabadilika kufuatana na
kazi mbalimbali za kifasihi zinazoandikwa.
Tukizingatia maelezo ya fani ya awali na fani ya pili tunaona
kuna haja ya kuzipambanua vyema istilahi hizo ili kuondoa utata wa matumizi
uliopo miongoni mwa wanafasihi.
Kutokana na hoja hiyo, tutatumia istilahi ya FANI kwa maana ya
UMBO la kazi ya sanaa ya kifasihi. Dhana ya pili ambayo inahusu TAWI la kazi ya
sanaa tutatumia istilahi ya UTANZU.
Maana ya Maudhui
Kwa upande wa maudhui imekuwepo mikinzani na mikanganyiko
nuongoni mwa wanataaluma wa kazi za fasihi juu ya maana yake. Wengi wa
wananadharia hao wanajadili fani na maudhui pamoja, japo pengine mitazamo yao
haiwi sahihi.
Baadhi ya wanataaluma wa kazi za fasihi wanasema kwamba fani na
maudhui ni vipengele ambavyo havina uhusiano wowote na kwamba vinaweza
vikatenganishwa. F.V. Nkwera7 analinganisha fani na maudhui na
kikombe na maji. Kikombe kinachukuliwa kama ndiyo fani, na upande mwingine maji
ndiyo maudhui. Mnywaji wa maji hayo analinganishwa na msomaji wa kazi ya fasihi.
S.D.Kiango na T.S.Y.Sengo8 wanafafanua fani na
maudhui kwa kulinganishwa na chungwa ambalo lina sehemu ya nje na ndani. Maudhui
ya kazi ya sanaa yanalinganishwa na nyamanyama za chungwa na fani ni ile sehemu
ya nje.
Mawazo mengine juu ya fani na maudhui yanatolewa na Penina
Muhando na Ndyanao Balisidya ambao wanaelekea nao kuukubali mtazamo huu
ulioelezwa hapo juu wakati wanapoelezea hadithi kuwa na "umbo la nje" wakati
lugha inapotumiwa na kujenga hilo umbo la ndani (maudhui) ambalo huhusika na
wazo kuu analolitaka fanani, (dhamira) ujumbe wake, maadili, na falsafa zake
(kama zipo) za maisha."9
Nadharia hizo zote zilizojadiliwa hapo juu kwa ujumla
zinaonyesha kupwaya na zinaweza kuwakanganya wasomaji. Nadharia hizo hazionyeshi
ama kuwakilisha ukweli wa mambo ulivyt) juu ya uwiano uliopo kati ya fani na
maudhui katika kazi ya sanaa kwani zinaonyesha kuwa fani na maudhui ni vitu
viwili vinavyoweza kutazamwa katika utengano, jambo ambalo si la kweli. Ukweli
ni kwamba vitu hivi viwili vinategemeana na kukamilishana, na wala havitazamwi
katika utengano.
Ufafanuzi wa kuiona fani na maudhui kama kitu kisichoweza
kutenganishwa umefanywa na Henri Arvon10, Avner Zis11 na
wanataaluma wengine wengi walio na mtazamo wa kisayansi ama kiyakinifu.
Kwa upande wa fasihi ya Kiswahili, M.M. Mulokozi na K.K. Kahigi
wamekuwa na mtazamo wa aina hiyo pia. Wanafasihi hao wanasisitiza kuwa "fani na
maudhui huathiriana na kutegemeana ... Maudbui ni maana ya shairi (kazi ya
sanaa), ni yale mawazo yanayozungumzwa (dhamira, falsafa, maoni), pamoja na
mtazamo wa mtunzi juu ya mawazo hayo... wazo kuu (dhamira) na mtazamo wa msanii
hutupa ujumbe."12
Akiungana na mtazamo huu, Senkoro naye anasema kuwa "maudhui ni
jumla ya mawazo, mafunzo yapatikanayo katika kazi ya fasihi... Maudhui huunda
lengo kwa mwaudishi. Kutokana na lengo, mawazo na mafunzo ya mwandishi ndipo
tunapata falsafa. Mawazo, mafunzo, lengo na falsafa au mtazamo wa mwandishi
kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii huunda msimamo."13
Mawazo hayo aghalabu yanajaribu kufafanua nini hasa ni maudhui.
Lakini dhana ya kutotenganishwa kwa vitu hivi viwili haijawekwa waziwazi. Ndipo
Senkoro anapotumia mfano wa "sarafu" kwa kufananisha fani na maudhui ya kazi ya
sanaa na "sura mbili za sarafu moja."14 Mfano huu unajaribu
kusisitiza dhana ya kutotenganishwa kwa fani na maudhui katika kazi za sanaa za
kifasihi. Mfano huu wa sarafu unajaribu kuonyesha dhana ya ukamilifu ya fani na
maudhui kama kitu kimoja cha kazi ya sanaa kwa kutumia mfano wa sarafu yenye
sura mbili, lakini umuhimu wake kama sarafu moja unategemea tuweko kwa sura hizo
mbili. Sura moja ya sarafu ikikosekana, basi, sarafu hiyo haiwezi kuwa na hadhi
yake ya kisarafu. Jambo la muhimu ni kuona jinsi kitu kimoja (fani) kinavyoweza
kukikamilisha kingine (maudhui).
Kwa kuzingatia nadharia hizo, tunakubaliana na
Senkoro15 au Mulokozi na Kahigi16 wanaosema kuwa "fani na
maudhui huwiana, hutegemeana na hatimaye kuathiriana." Uhusiano huu ndio
unaojenga kazi bora ya fasihi. Aidha ni vizuri kutoa tahadhari hapa kuwa uwiano
wa fani na maudhui wa kazi ya sanaa huwa ni lengo la msanii. Maudhui iliyotawala
kuumbwa kwa kazi ya sanaa inatakiwa kujitokeza katika fani inayohusu. Ili
maudhui yatawale fani, sharti yajitokeze kama kazi ya sanaa na si kama hotuba ya
mwanasiasa. Ni wajibu wa msanii kuchagua fani inayomruhusu kutumia maudhui
anayotaka kuyafikisha kwa hadhira yake.
Uhusiano wa Fani na Maudhui
Mwandishi wa hadithi fupi anatakiwa autazame uhusiano huu muhimu
uliojadiliwa hapa kwa makini sana. Kama hatakuwa mwangalifu anaweza kujikuta
katika hali ya utata wakati wa uandishi wake.
Tatizo kubwa linalowakabili waandishi wengi wa hadithi fupi na
fasihi kwa ujumla ni lile la kipi kipewe uzito wa kwanza katika uandishi.
Wasanii wenyewe wanagawanyika katika makundi mbalimbali. Kuna ambao
wanaian-galiajanui kama kitu kinachobadilika kulingana na mfumo wa kihistoria
kwa wakati na mahali maalumu na kuna wale wanaoona kuwa kila jambo linalotendeka
katikajamii ni kudra ya Mwenyezi Mungu. Yawezekana kuna wasanii wenye mtazamo
ulio nje na hii tuliyoitaja. Kisanaa, wako wale wanaoona kazi ya sanaa kama
chombo maalumu kinachobeba maudhui muhimu kwa ajili ya jamii na kuna wate
wanaoiona kazi ya jamii ya sanaa ikiwa na kazi ya kufurahisha ambayo haipaswi
kuambatana na itikadi ama mfumo wowote ule wa maisha ya jamii. Sanaa, walidai
wataalamu hao isihusighwe na maisha bali itazamwe kama sanaa tu.
Tukianza na mtazamo tulioutaja kwanza tutaona msisitizo huwekwa
kwenye maudhui (maana) ya kazi ya sanaa. Lakini fani pia hawajaiacha katika
mtazamo huo. Wanataaluma hao huiona fani kuwa inategemeana na maudhui katika
sanaa nzima. A. Lunarchasky, mwanafasihi mwenye mtazamo wa kiyakinifu anasema:
Mhakiki (msanii) wa Ki-Marx atachukua kwanza maudhui (maana) kama ndilo lengo la uhakiki (usanii) wake. Atatafuta uhusiano wake na jamii, pia atazingatia matokeo ya kazi yake katika jamii hiyo. Baada ya hapo atarudi kwenye fani na kuona imetosheleza vipi lengo lake la kuieleza kazi hiyo na kuvutia wasomaji17
Tunaweza kuifikiria kauli hii kwa kuihusisha na hadithi fupi ya Kiswahili. Mwandishi wa hadithi fupi akitaka kazi yake iwe na manufaa kwa jamii anayoiandikia lazima awe mwangalifu Katika kuchagua dhamira zile ambazo zinafundisha na kujenga msimamo wa kimaendeleo katika kuikwamua jamii kutoka katika minyororo ya utumwa na ukandamizwaji. Itabidi msanii huyo afanye utafiti juu ya matakwa na mategemeo ya jamii yake. Dhamira hizo lazima zielezwe kifundi ili kufanya watu wapende kusoma kazi za sanaa hizo. Kama kazi ya sanaa itakuwa na fani duni lakini maudhui yake ni mazuri, basi, hata maudhui yaliyokusudiwa hayatatoa ujumbe unaokusudiwa inavyopasa. Au ikitokea maudhui ni duni na fani ni bora, pia jamii itapata hasara ya kufikiwa na maudhui yasiyo na maana katika jamii hiyo kwa kupitia fani iliyo bora. Wana-Marx walilazimika kurekebisha mtazamo wao wa kutoa uzito kwa maudhui peke yake kwa sababu iligundulika kuwa maudhui hayawafikii wasomaji bila kutumia kiungo cha fani.
Mtazamo mwingine tulioutaja hapa juu ni ule unaoiona sanaa kama
kitu cha kufurahisha tu. Mtazamo huu kimsingi hujali sana fani zaidi kuliko
maudhui. Maudhui kwao sio kitu cha muhimu sana, kwa hiyo wasanii wa aina hii
hujali na kuchunguza maneno, jinsi yanavyofanya kazi yakiwa katika msisitizo,
urefu wa msitari (kama ni ushairi) na kadhalika. T.S.Eliot na Allan Poe ni kati
ya wanataaluma waliosisitiza mtazamo huu. Jambo la muhimu kutamka hapa ni kuwa
mazingira ni muhimu katika kufanya uamuzi huu. Katika itikadi nyingine mtazamo
kama wa Eliot na Poe ni sahihi lakini kwa itikadi ya kimaendeleo ionayo fasihi
kama chombo muhimu kinachohitajika katika kusaidia jamii katika mapambano yake,
mtazamo huu si sahihi. Lile linalosemwa haliko katika fani, bali fani ni njia ya
kusemea. Kwa hali hii, suala la wasanii pia kuwa na msimamo fulani linafuata
udhamini na itikadi inayotawala na kutetea maslahi maalumu. Kwa vyovyote, msanii
hawezi kusaliti tabaka linalomlea na kumtunza. Ni wasanii wachache wanaweza
kukemea utawala wao kama unawasaliti umma wa wakulima na wafanyakazi. Nao
wakifanya hivyo, wana- jikuta katika matatizo makubwa kama tulivyokwisha ona
hapo mapema katika sura iliyotangulia.
Ikiwa mwandishi wa hadithi fupi atajali "maneno" tu kama mtazamo
huu unavyodai, itakuwa ameshindwa kabisa kuijengajamii yake. Atakuwa
ameian-gusha fasihi na kufanya ishindwe kufanya kazi yake. Kwa kuzingatia hali
halisi, mtazamo sahihi utakuwa ule unaoihusisha kazi ya sanaa ya fasihi na
maisha ya jamii ambayo imeandikiwa kazi ya fasihi inayohusika. Maisha ya jamii
yana matatizo na furaha. Mtazamo sahihi utakuwa unawahudumia watu kwa kadiri
inavyowezekana. Mwandishi wa hadithi fupi anategemewa awe na mtazamo wa
kisayansi wa aina hii kwa janui yake. Ni juu ya mwandishi wa hadithi fupi kuwa
mwangalifu wakati wa usanii wake kama atataka kazi. yake iwafae kwa kiwango cha
kuridhisha umma wa wakulima na wafanyakazi. Uhusiano muhimu juu ya vipengele
vinavyoijenga hadithi fupi umeonyeshwa katika Kielelezo Na. 2.
Kielelezo 2: Vipengele vya Fani na Maudhui ya Kazi ya Fasihi (Hadithi Fupi)
Kielelezo hiki kimezingatia ukweli na msimamo kuwa maudhui kama
kile kinachosemwa ndicho kitu muhimu katika kazi ya sanaa ya kifasihi. Kitu hiki
muhimu kinasaidiwa na fani kuwafikia wanaohusika inavyopasa. Aidha, msi- mamo
huu kimsingi unatofautiana, na ule unaothamini fani tu katika kazi ya sanaa ya
kifasihi. Suala la kuzingatia ni mazingira ya uandishi na mtazamo wa jamii
inayoandikiwa. Mwandishi anaandika nim na wapi? Anamwandikia nani na kwa lengo
gani? Hali hii itamsaidia kuamua jinsi au njia ya kuwasilisha alilonalo kwa
hadhira aliyoikusudia.
Chimbuko la Dhamira
Baada ya kuangalia maana ya fani na maudhui, na kuona uhusiano
na uwiano kati ya fani na maudhui, tuangalie sasa wapi waandishi wa kazi za
hadithi za kifasihi, hususan hadithi fupi, hupata dhamira zao. Katika mjadala
wetu, tutajaribu kuangalia pia jinsi dhamira inavyoweza kuunganika na fani
katika kutoa maudhui kwa hadhira iliyokusudiwa.
Dhamira m mawazo yanayoelezwa katika kazi ya sanaa Ziko dhamira
za aina nyingi ambazo mwandishi anaweza kuchagua.
Wakati mwingine, waandishi wanaweza kuwa katika mazingira
yaleyale, na wakaandikajuu yajambo moja, labda la mapenzi. Kwa vile watu hawa
wanayatazama mambo tofauti, maelezo yao yanaweza. kutofautiana. Tunaweza
kujadili hoja hiyo'kwa kutoa mifano tuliyo nayo katika kitabu hiki.
Katika sehemu ya pili ya kitabu hiki, kuna hadithi kadhaa ambazo
zinajadili dhamira mbalimbali. Miongoni mwa dhamira zinazojadiliwa sana ni
siasa, mapenzi na utamaduni kwa ujumla.
Tunaweza kuanza na dhamira ya siasa katika kujadili suala hili.
Tunapenda kujadili suala hili kwa kutumia hadithi mbili: Siri ya Bwanyenye
(M.M.Mulokozi) * na Cha Mnyonge Utakitapika Hadharani (E.
Kezilahabi).
* Hadithi zote zinazojadiliwa kama mifano ziko katika sehemu ya pili ya kitabu hiki.
Hadithi ya Siri ya Bwanyenye kimsingi inajadili masuala
mengi yanayoihusu jaimii ya Tanzania ya wakati. wa TANU na nchi zinazoweza kuwa
na mazingira ya aina hii. Mwandishi ametumia mazingira aliyomo, na wakati uliopo
katika kuandika badithi yake. Kuna masuala ya watu kushangilia "Azimio la
Arusha" kwa unafiki - kwamba watu wengine wamekuwa wakiimba uzuri wa "Azimio la
Arusha," wakati huo huo wanalisaliti. Kwa hiyo mambo kama uongozi bora, haki,
uhuru wa kweli na kadhalika, yanajadiliwa kwa mapana.
Suala la kisiasa linavyojitokeza katika Cha Mnyonge
Utakitapike Hadharani linatofautiana na Siri ya Bwanyenye. Wakati
Siri ya Bwanyenye hazungumzii matatizo ya utabaka moja kwa moja, Cha
Mnyonye Utakitapika Hadharani analiweka suala hili wazi zaidi anapotenga
watu katika "bwana," "ukubwa" ama "uwezo" na "unyonge", "umaskini" na kadhalika.
Si hilo tu, mwandishi wa hadithi ya Cha Mnyonge Utakitapika Hadharani
ametu-mia mapenzi kama kitu cha kubebea dhamira kuu ya utabaka. Hayo ni baadhi
tu ya maoni yanayojitokeza kwa upande wa siasa katika hadithi hizo mbili.
Japokuwa hadithi hizo ni za kisiasa, na ingawa wote wameandikia katika mazingira
wanamoishi, kuna utofauti uliojionyesha tayari.
Kwa upande wa dhamira ya mapenzi, tutazigusia hadithi za
Kiumbe Mzito (M.Msokile), Kijana Yule (M.Mohamed) na Ndumila
Kuwili (J. Rutayisingwa).
Ukiangalia kijuujuu, hadithi ya Kiumbe Mzito ni ya
mapenzi. Lakini ikichunguzwa kwa undani sana, hadithi hii imetumia dhamira ya
mapenzi katika kuelezea mambo mengine zaidi ya kijamii. Suala linalojadiiwa sana
linahusu elimu ya malezi kwa vijana hasa wasichana - na matatizo yanayowapata
wasichana wanaosoma shule za mijini, hususan Dar es Salaam.
Kwa upande mwingine, haditbi ya Kijana Yule nayo inahusu
mapenzi pia. Lakini mwandishi alivyoyajenga mapenzi katika hadithi hiyo, ni
tofauti na ilivyo katika Kiumhe Mzito Mapenzi ya Kijana Yule ni
mazito, yanawahusu wanawake wasio na matarajio ya Kusoma shule kama katika
Kiumbe Mzito. Tamaa ya wanawake wa Kijana Yvle ni kukidhi matakwa
ya mapenzi yao, lakini katika Kiumbe Mzito, mwandishi anawasawiri
wasichana wenye pupa ya kukidhi kiu yao ya pesa kwa kutumia mapenzi. Ni vipofu
wanaotazama!
Ndumila Kuwili inatuonyeeha upande wa pili wa mapenzi.
Hadithi hii inaelezea maisha ya ndoa yaliyokosa uaminifu na hasara ya kukosa
jambo hilo. Si hilo tu, hadithi inaonyesha pia nafasi ya uaminifu katika kulinda
unyumba na hata marafiki na ujirani mwema. Pamoja na mapenzi, masuala ya chuki,
haki na uonezi yanajitokeza pia.
Dhamira zote hizi zimetokana na mzingira wanayoyaishi waandishi
hao kila siku. Lakini je, kwa nini dhamira hizo zimeelezwa kwa viini
vinavyoto-fautiana kati ya mwandishi na mwandishi? Kwa nini mapenzi yameelezwa
tofauti miongoni mwao? Kwa nini suaia la siasa nalo limepewa uzito tofauti kati
ya waandishi wanaohusika?
Maswali haya yanajibika kwa kuzingatia msimamo wa mwandishi,
mtazamo, falsafa na uwezo wa jumla wa kisaaaa alionao msanii anayehusika.
Falsafa, Mtasamo, na Msimamo waa Mwandishi
Katika kazi yoyote ya kifasihi mambo hayo lazima yawepo. Aidha,
kila msanii ana nafasi na uwezo wake katilca kuyakabili na kuyawasiIisha katika
mazingira yanayohusika. Tutavijadili vipengele hivyo kimoja kimoja hapa chini.
Pengine tuanze na dhana ya mtazamo kwa msanii m nini? Kimsingi,
tunasema kuwa mtazamo m jinsi ya kuona mambo katika maisha. Tunaweza pia kusema
kuwa kila mtu ana namna najinsi ya kuyatazama mambo yanay-omzunguka katika
maisha yake.
Wasanii wana mitazamo au maono ya aina mbili. Kwanza, huutazama
ulimwengu au mazingira yanayomzunguka binadamu kiyakinifu - kisayansi. Msanii wa
aina h» huuona ulimwengu kuwa ni kitu kinachobadilika kufu-atana na mfumo
wa kihistoria. Mtazamo huu humfanya msanii kuutazama ulimwengu kama kitu dhahiri
- kitu katika uhalisia wake.
Kinyume cha mtazamo huu, kuna mtazamo wa kidhanifu.
Mtazamo huu huuchukulia ulimwengu kama kitu kinachobadilika kulingana na matakwa
ya Mungu. Msanii mwenye mtazamo huu, atauwasilisha hivyo katika kazi yake ya
sanaa.
Vilevile falsafa inahusiana sana na mtazamo. Kwa mujibu wa
kamusi ya Kiingereza ya Concise Gxford Dictionary, falsafa imeelezwa kuwa
"ni busara au elimu inayoshughulikia ukweli - chanzo cha jumla cha mambo na
mawazo, welewa wa binadamu na maisha. (Falsafa) m msingi muhimu wa
maisha."18
Kwa kuzingatia kauli hii, falsafa ya kazi ya kifasihi inatakiwa
ichambuliwe kwa kuzingatia jinsi kazi hiyo ilivyoutazama ulimwengu unayoihusu.
na kuueleza ukweli juu ya mambo mbalimbali. Ukweli huo lazima uhusishwe na
binadamu. Kwa hiyo falsafa ya kazi ya kifasihi inahusiana na mtazamo, na
uyakinifu au udhanifu huunda falsafa.
Mtazamo na falsafa ni vitu vya msingi katika kujenga msimamo wa
msanii. Msimamo wa msanii ndio unaosababisha kazi ya sanaa iwe na mwelekeo
maalumu na hata kutofautiana na kazi za wasanii wengine.
Katika fasihi ya Kiswahili kwa mfano, kuwa baadhi ya wasanii
wanaosema kuwa ushairi lazima uwe na kanuni ya vina, mizani, mistari, na
kadhalika. Huu ni msimamo wao, na wako katika kutokubaliana na wale wanaosema
vitu hivi si vya lazima kama yalivyo maudhui.
Katika kusoma kazi hizo, mtu anaweza kupata ujumbe, maadili,
mafunzo na kadhalika, kwa kuzingatia mtazamo, msimamo na falsafa.
Aidha, msanii huwajenga wahusika kwa kuwapa lugha na tabia
zinazolingana na dhamira zinazoelozwa. Lugha mara zote ni kiungo muhimu katika
kutoa maudhui yanayostahili kwai hadhira iliyokusudiwa.
Tunahitimisha hapa kwa kusema kuwa maudhui ya kazi ya sanaa ya
kifasihi, lazima yajumuishe dhamira zinazoelezwa, msimamo, matazamo falsafa,
ujumbe, maadili na kadhalika.
Maelezo
1. C- Brooks na R.P. Warren, Understanding Fiction, F.S.
Crofts & Co., Inc. 1943.
2. Kama Na. 1.
3. B. Deutsch, Poetry Handbook, Jonathan Cape, Thirty
Bedford Square, 1965.
4. W. Blair (na wenzake), Literature, Scott, Foresman and
Company, New York: 1966.
5. C.H. Holman, A Handbook to Literature, The
Odysey Press, New York, 1936.
6. R. Wellek na A. Warren, Theory of Literature, A
Harvest/HBJ Book London 1975.
7. F-V. Nkwera, Sarufi na Fasihi: Vyuo na
Sekondari, TPH, 1978
8. S.D- Kiango na T.S.Y. Sengo, Hisi Zetu - I . TUKI,
1973.
9. P. Muhando na N. Balisidya, Fasihi na Sanaa za
Maonyesho, TPH, 1976
10. H. Arvon, Marxist Aesthetics Cornell University Pres,
1973.
11. A. Zis, Foundations of Marxist Aesthetics, Progress
Publishers, Moscow, 1977.
12. M.Mulokozi, na K-K- Kahigi, Kunya. za Ushairi na Diwani
Yetu", TPH, Dar es Salaam: 1979.
13. F.E.M.K Senkoro, Fasihi, Press and Publicity Centre,
Dares Salaam: 1979.
14 Kama Na. 18.
15. Kama Na. 13.
16. Kama Na. 12.
17. A. Lunacharsky, On Literature and Art, Progress
Publishers, Moscow,
1973.