Tahadhari zachukuliwa hofu ya ugaidi

Kamanda Kova
ADVERTISEMENT
Dar, Mikoani. Ulinzi umeimarishwa kwenye maeneo mbalimbali nchini ikiwamo vyuoni, ofisi za umma na kwenye migahawa mikubwa baada ya kuwapo kwa hofu ya shambulizi la kigaidi katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Mwanza.
Hofu hiyo imekuja baada ya hivi karibuni Chuo Kikuu cha Garissa, cha nchini Kenya kushambuliwa na kusababisha vifo vya wanafunzi 148.
Baada ya shambulizi hilo, kumekuwa na ujumbe mfupi wa simu unaoendelea kusambazwa ukionya kuwapo kwa shambulizi katika mikoa ya Mwanza, Arusha na Dar es Salaam.
Akizungumzia hali ya usalama Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo alisema wamejipanga kukabiliana na kundi hilo.
Vyuo Vikuu vyaimarisha ulinzi
Februari 10, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kiliweka tangazo la kuwataka wanachuo kuchukua tahadhari baada ya kuwapo kwa matukio yenye taswira ya ugaidi.
Habari zilizopatikana zinasema polisi imejipanga kikanda kukabiliana na ugaidi katika mikoa ya Temeke, Ilala na Kinondoni.
Mkoani Mbeya, vyuo vikuu mkoani humo vimeimarisha ulinzi kwa wanafunzi na wafanyakazi wake.
Mratibu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), tawi la Mbeya, Dionise Lwanga alisema tukio la ugaidi la Kenya ni la aina yake kimataifa na limewashtua wasomi wengi duniani.
ADVERTISEMENT
Lwanga alisema pamoja na kwamba ugaidi ni tishio kwa mataifa mbalimbali, CBE imetoa maelekezo ya kujihami kwa wanachuo na wafanyakazi na pia imeagiza kila mwanafunzi awe amevaa kitambulisho awapo eneo la chuo.
Hali kama hiyo pia ilionekana kwenye Chuo cha Teofilo Kisanji (Teku), ambako walinzi wameamua kusimama langoni kukagua vitambulisho tofauti na siku zilizopita.
Mkoani Singida, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Thobias Sedoyeka aliwataka wakazi wa mkoa huo kutoa taarifa juu ya vituo vya mafunzo yasiyo rasmi, ili hatua zichukuliwe mapema.
Akizungumzia suala la ugaidi, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda aliagiza wamiliki wa hoteli za kitalii kufunga mitambo ya ukaguzi na usalama.
Ntibenda alisema Arusha kwa sasa ipo shwari na hakuna matukio ya ugaidi, lakini ni lazima kuchukua tahadhari.
Jana polisi imetoa taarifa na kuwakanya wale wanaosambaza ujumbe mfupi wa simu ukiwatia hofu ya kuwapo kwa shambulizi la kigaidi katika miji ya Mwanza, Dar es Salaam na Arusha katika baadhi ya vyuo vikuu nchini.
Msemaji wa jeshi hilo, Advera Senso alisema pamoja na hayo, bado watafanyia kazi taarifa zozote zinazohusu usalama wa nchi.
Wakati huohuo, habari zilizopatikana jana jioni zinaeleza kuwa mwanafunzi mwenye asili ya Kisomali anayesoma Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut) cha Mwanza, alizua tafrani chuoni humo baada ya kuhisiwa kufanya tukio la kigaidi.
Msemaji wa Saut, Livin Komu alisema tahadhari zimechukuliwa ili kuimarisha ulinzi chuoni hapo.
POSTED SATURDAY, APRIL 11, 2015 | BY- WAANDISHI WETU, MWANANCH
Powered by Blogger.