Sababu za Al-Shabaab kuishambulia Kenya

Wanafunzi wakiwa katika majonzi baada ya kunusurika shambulizi la kigaidi mjini Garissa, Picha na AFP.    
ADVERTISEMENT
Eneo la Afrika Mashariki liko katika taharuki kubwa kutokana na tetesi za kuwepo uwezekano wa kufanyika mashambulizi zaidi kutoka kwa kundi la Al Shabaab ambalo tayari limeleta maafa makubwa kwa wananchi wa Kenya.
Katika makala haya, mwandishi wetu wa masuala ya kimataifa George Njogopa anajaribu kudadisi baadhi ya mambo yanayosababisha kundi hilo kuendelea kuishambulia Kenya.
Kenya iko katika wakati mgumu kutokana na wimbi la mashambulizi ya kigaidi yanayoendeshwa na makundi ya kigaidi. Kundi hilo sasa limepanua wigo kwa mashambulizi yake kutoka ule wa awali wa kuwalenga watalii wa kigeni hadi kufikia maeneo ya raia wa kawaida.
Tukio la hivi karibuni la kundi la kigaidi, Al-Shabaab kushambulia Chuo Kikuu cha Garissa, ambalo limesababisha vifo vya watu 148 linatajwa kuwa ni moja ya matukio mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya taifa la Kenya.
Serikali imeliita shambulizi hilo la wiki iliyopita kuwa ni lenye nia ya kuwataka kuwatia woga wananchi. Imeahidi kutolegeza kamba katika harakati zake za kukabiliana na vitendo vya kigaidi. Kumekuwa na hoja mbalimbali zinazoendelea kutolewa kuhusiana na sababu zinazolifanya kundi hilo kuendelea kuilenga zaidi Kenya.
Pamoja na hoja zinazoendelea kuibuliwa, lakini jambo kuu linalojitokeza ni lile linalotajwa kuwa ni hatua ya kulipa kisasi.
Kundi la Al-Shabaab linaendesha mapambano ya ulipizaji kisasi dhidi ya Jeshi la Kenya ambalo katika miaka michache iliyopita lilijiunga na Vikosi vya Umoja wa Afrika (AMISON) kwa lengo la kuwaondoa wapiganaji wa kundi hilo katika miji mikubwa na midogo nchini Somalia.
Ikumbukwe kuwa mwaka 2011, kundi hilo la Al Shabaab liliwateka nyara watalii kadhaa waliokuwa katika shughuli zao kaskazini mwa Kenya.
Kitendo hicho kilizusha hofu na wasiwasi kuhusu usalama wa watalii wanaoitembelea kwa wingi Kenya.
Wengi waliona kuwa hatua ya Al Shabaab kuwavizia watalii wa kigeni na kisha kuwateka ingehatarisha sekta ya utalii inayochangia asilimia 12 katika uchumi wa jumla wa Kenya.
Baadaye Jeshi la Kenya lilituma vikosi vyake nchini Somalia kupambana na waasi kwa lengo la kulinda maeneo yake ya utalii dhidi ya mashambulizi ya kundi hilo.
Jeshi hilo liliendesha operesheni kali na kufanikiwa kuingia katika miji muhimu iliyokuwa ikidhibitiwa na kundi hilo.
Kundi hilo lilipoteza mwelekeo hasa baada ya ngome zake ikiwamo mji wa Kisimayu kudhibitiwa na vikosi vya Kenya.
Vikosi vyake vya anga vilikoleza mashambulizi na baadaye kusonga mbele katika maeneo ya mashariki na kaskazini mwa Somalia maeneo ambayo yalitumika kama maficho ya wapiganaji hao.
Wengi walihisi kuwa ushawishi wa kundi hilo ulikuwa umepotea na kwamba hali ya amani na usalama ingerejea upya katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
Kutokana na kuzidiwa nguvu, wapiganaji wa Al-Shabaab walilazimika kuweka kambi katika maeneo ya vijijini na kuanzisha mkakati mpya wa mashambulizi kwa njia ya kuvizia tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
Likiwa limejichimbia katika maeneo hayo, kundi hilo liliibuka upya na kuanza kupanga mashambulizi ya kulipa kisasi katika nchi za Somalia na Kenya.
Shambulizi lililolenga jengo la maduka la Westgate na kuua zaidi ya watu 66 liliamsha hisia na mshtuko mkubwa kwa Serikali ya Kenya.
Mashambulizi dhidi ya raia yanayoendelea kufanywa na kundi hilo katika maeneo yanye mkusanyiko mkubwa watu yamesababisha kuwepo haja ya kuimarishwa kwa ulinzi na usalama.
Serikali ya Kenya imeapa kutorudi nyuma katika kukabiliana na tishio la ugaidi na tayari imeanzisha tena operesheni za kijeshi kushambulia sehemu ambazo kundi hilo limeweka ngome yake.
Hivi karibuni, Serikali ya Kenya ilipitisha sheria kali inayolenga kukabiliana na makundi ya kigaidi huku akitaka ushirikiano zaidi kutoka jumuiya ya kimataifa.
Wachambuzi wengi wa mambo wanasema kuwa kuongezeka kwa migogoro ya kijamii na ile yenye sura ya kidini kumetoa mwanya kwa kundi hilo kuwashawishi vijana kirahisi na kuingia kwenye matukio ya kigaidi.
Vitisho vya kundi hilo sasa vimevuka mipaka na kusambaa katika nchi nyingine za Afrika Mashariki hali ambayo imefanya raia wengi kuishi kwa hofu na wasiwasi mkubwa.
POSTED SATURDAY, APRIL 11, 2015
Powered by Blogger.