Miili minane ya waliofariki dunia kwa radi yaagwa

Majeneza yenye miili ya waliopoteza maisha baada ya kupigwa na radi juzi, yakiwa katika viwanja vya Shule ya Msingi Kibirizi Manispaa ya Kigoma kwa ajili ya kutolewa heshima ya mwisho kabla ya kuzikwa jana. Picha na Anthony Kayanda    
ADVERTISEMENT
Kigoma. Vilio na simanzi jana vilitawala katika Manispaa ya Kigoma Ujiji wakati salamu za mwisho zikitolewa kwa miili ya watu wanane waliofariki dunia juzi kwa kupigwa na radi.
Miili hiyo iliwasili kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Kibirizi, saa 4.05 asubuhi na kusababisha zaidi ya wanafunzi 500 waliokuwapo kuangua vilio.
Wengine waliokuwapo ni viongozi mbalimbali wa Serikali, vyama vya siasa na taasisi za dini.
Wanafunzi waliofariki dunia ni Yusufu Athumani, Fatuma Slay, Zamda Seif, Shukurani Yohana na Walupe Kapupa wote wa darasa la kwanza pamoja na Hassan Ally anayesoma darasa la tatu.
Wengine ni Mwalimu Elieza Mbwambo na Focus Ntahamba mkazi wa Bangwe mjini Kigoma.
Awali, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Kigoma, Maweni, Dk Fadhili Kibaya alisema walipokea maiti wanane.
Alisema majeruhi 16 waliopokewa, kumi wameruhusiwa na wengine sita bado wamelazwa na hali zao zinaendelea vizuri.
“Tunaendelea kuwahudumia vizuri majeruhi wote ili warudi katika hali zao za kawaida, ikizingatiwa wengine ni wanafunzi.
“Kama kuna mtu mwingine alijeruhiwa lakini hakuweza kufika hospitali, namuomba aje ili achunguzwe afya yake,” alisema Dk Kibaya.
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Saveli Maketa alisema Serikali imeandaa utaratibu wa kusafirisha mwili wa Mwalimu Mbwambo kwenda nyumbani kwao Same mkoani Kilimanjaro kwa mazishi.
Maketa aliwataka wananchi kutambua kwamba tukio hilo ni la kawaida ambao limetokana na janga la kiasili. Alisema majanga ya namna hiyo yanaweza kutokea wakati wowote, huku akiyataja mengine kuwa ni kimbunga, mafuriko na tetemeko la ardhi.
Balozi Mdogo wa Burundi mjini Kigoma, Johnbosco Ntayikengurukiye alisema amepokea taarifa za ajali hiyo kwa masikitiko.
Alisema kwa niaba ya wananchi wa Burundi ametoa rambirambi ya Sh200,000 kwa wafiwa.
Baadhi ya wakazi wa Kigoma walisema tukio la kwanza kutokea eneo la Kibirizi na kuua watu wengi.
Mmoja wa wakazi hao, Kalikela Shaaban alisema tukio hilo limeacha majonzi kwa familia zilizondokewa na wapendwa wao.
Baada ya salamu za mwisho kutolewa kila familia iliruhusiwa kuchukua mwili wa ndugu zao kwenda kuzika.
Mvua iliyosababisha radi ilinyesha juzi saa tano asubuhi.
POSTED THURSDAY, APRIL 16, 2015 | BY- ANTHONY KAYANDA NA DIANA RUBANGUKA, MWANANCH
Powered by Blogger.