Ajali zinapunguzika, wadau wanena

Moja ya ajali zilizotokea hapa nchini
ADVERTISEMENT
Dar es Salaam. Wakati ajali za barabarani zikiendelea kukithiri nchini na kugharimu maisha ya mamia ya watu na wengine kubakia na ulemavu, wadau wanaamini kuwa janga hilo linaweza kupunguzwa ikiwa hatua kadhaa zitachukuliwa.
Kumekuwa na ajali nyingi katika miezi ya karibuni, hasa zinazohusisha mabasi ya masafa marefu, na juhudi za Serikali kuzipunguza, ikiwa ni pamoja na kutaka madereva warudi mafunzoni kila baada ya miaka mitatu, hazijafanikiwa.
Kwa mujibu wa takwimu za ajali zilizotolewa juzi na mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamanda Mohamed Mpinga, kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu ajali zilikuwa 2,116 ambazo zilisababisha vifo 866 na kujeruhi watu 2,363.
Ajali hizo zimetokea katika kipindi tofauti na miaka iliyopita ambayo ajali nyingi zilikuwa zikitokea mwishoni mwa mwaka, kipindi ambacho mwaka jana kikosi hicho cha usalama barabarani kilisema kiliweka mkakati madhubuti wa kupunguza matukio hayo na hivyo kufanikiwa.
Wakati Kamanda Mpinga akitoa taarifa hizo, Jeshi la Polisi, Kanda ya Dar es Salaam limesema kuanzia Machi Mosi, kulikuwa na makosa 34,641 kwenye mkoa mmoja pekee na hivyo kulifanya Jeshi la Polisi kuvuna Sh1.04 bilioni zinazotokana na faini.
Wakizungumza na Mwananchi jana, wadau kadhaa walipendekeza mambo kadhaa ambayo walisema yanaweza kupunguza ajali, ikiwa ni pamoja na kutungwa kwa sheria kali na kuwapo kwa elimu ya mara kwa mara kwa madereva.
“Sheria zikibadilishwa na kufanywa kuwa kali zaidi, lazima tutaona mabadiliko,” alisema makamu mkuu wa Chuo cha Usafirisaji (NIT), Dk Simon Lushakuzi.
Mkuu huyo alisema sheria za usalama barabarani zinazotumika sasa ni lazima ziboreshwe.
“Dereva anaweza kusababisha ajali na kuua mtu, lakini faini anayotakiwa kulipa ni Sh20,000. Ndiyo maana wanakuwa wazembe barabarani,” alisema mkuu huyo.
Hata hivyo, katika kuboresha sheria hizo, Serikali iliunda kanuni zinazotaka madereva wapate mafunzo ya muda mfupi kabla ya kupewa leseni mpya.
Kanuni hizo pia ziliweka adhabu kali kwa madereva ambao magari yao yanahusika kwenye ajali, ikiwa ni pamoja na kunyang’anywa leseni na kuwekwa mahabusu, lakini madereva wakafanya mgomo mkubwa nchi nzima uliosababisha Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka kutangaza kutengua kuanza kutumika kwa kanuni hizo.
Tangu kuzimwa kwa mgomo huo Jumapili iliyopita, ajali zimekuwa zikitokea takriban kila siku na jana basi la Air Jordan lilipata ajali wilayani Nzega, Tabora na kuua mtu mmoja na kujeruhi wengine 28.
Dk Lushakuzi, ambaye chuo chake ni moja ya taasisi mbili ambazo Serikali iliziteua kwa ajili ya kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa madereva kila mara leseni zao zinapoisha, alisema mafunzo ya mara kwa mara kwa madereva pia ni muhimu.
“Miji inakua kwa kasi kwa hivyo ni lazima madereva wapate mafunzo ili waende sambamba na mabadiliko hayo… dereva aliyewahi kuendesha gari jijini hapa miaka mitatu iliyopita na kuondoka ukimleta hawezi kuendesha gari vizuri kama zamani lazima apate mafunzo.”
Mmiliki wa mabasi ya Mrindoko, Hussein Mrindoko aliungana na Dk Lushakuzi kuhusu umuhimu wa elimu.
“Elimu ni kila kitu. Tukielimishana vizuri namna ya kufuata miongozo na kanuni za barabarani bila kusukumana, tutafika mbali na siyo kutegemea Polisi kwa kila kitu,” alisema Mrindoko.
Mmiliki wa mabasi ya Ngorika, George Temba alipingana na dhana kuwa chanzo cha ajali ni madereva kuchoka kutokana na kutokuwa na wasaidizi, badala yake akaelekeza lawama kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchikavu (Sumatra).
Alisema mamlaka hiyo imeweka utaratibu wa mabasi ya mikoani kutoka kwa vituo vya mabasi asubuhi saa 12:00.
“Mabasi yanaporuhusiwa kuondoka kituoni, madereva huwa wanakimbizana ili kuwahi abiria kituo kinachofuata,” alisema Temba.
“Sumatra wanatakiwa kubadilisha huo utaratibu. Kama inawezekana magari yawe yanaruhusiwa kutoka kituoni kwa kupishana hata kwa dakika kumi na tano.”
Temba, ambaye magari yake hufanya safari kati ya Dar es Salaam na Kilimanjaro, alisema njia nyingine ni kutoa vibali kwa wamiliki wa mabasi kutumia barabara mpya.
“Si sawa magari zaidi ya 60 kutumia ruti moja wakati kuna barabara mpya ambazo wamiliki wapya wa mabasi wanaweza kupewa kibali cha kuzitumia kuliko kulundika magari kwenye barabara moja,”alisema na kutoa mfano wa barabara kutoka Dodoma kwenda Mbeya kupitia Mtera ambayo haina mabasi mengi.
Nassoro Sanga, dereva wa malori ya mizigo yanayofanya safari za Zambia, alisema ili kupunguza ajali madereva wanatakiwa kuzingatia alama za barabarani.
“Uzembe wa kutozingatia alama hizo umekuwa ukisababisha ajali… hata mwendo kasi pia. Kuna madereva wanakimbiza sana magari wakati mwendo unaotakiwa unafahamika,” alisema Sanga.
Alisema, madereva wanatakiwa kuacha kunywa pombe.
“Huwezi kuamini alfajiri tukiwa tunaanza safari unakuta mtu ‘anabugia kiroba’ cha pombe halafu anaendesha gari. Huko barabarani uendeshaji wake ni hovyo sana. Unategemea asisababishe ajali? Hakuna.”
Dereva wa lori linalosafirisha mizigo kwenda Congo, Jerry George alisema endapo kipato cha madereva kikiongezeka na kukidhi mahitaji yao, itasaidia kupunguza ajali za barabarani.
“Madereva wanalazimika kwenda mwendo kasi ili wawahi kule wanakokwenda na kurudi haraka kwa sababu ya maslahi yao. Lakini kama mtu analipwa hela ya kutosha kukidhi mahitaji yake, haraka ya nini?” alihoji.
Alisema, akienda safari ya wiki moja analipwa Sh 200,000, fedha ambazo alisema hazitoshi.
Kaimu katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika alieleza kusikitishwa kwake na kuongezeka kwa vifo vinavyotokana na ajali za barabarani.
“Mara nyingi serikali imekuwa ikitoa salamu za rambirambi kwa wahanga wa ajali hizo. Kama si Rais mwenyewe, basi wasemaji wake lakini hatuambiwi ni mikakati gani ipo mezani ili kukabiliana nazo,” alisema Mnyika.
Mnyika aliiomba jamii kwa ujumla kutumia nguvu kama ile inayotumika kupambana na mauaji ya albino na kueleza kuwa ajali hizo zimekuwa ni janga la Taifa kutokana na kupoteza maisha ya wananchi wengi ndani ya muda mfupi.
Neema Fanuel, mkazi wa Mwanza alisema: “Watu wakiacha kutoa na kupokea rushwa, nadhani tutapunguza ajali,” alisema.
“Unakuta mtu amevunja sheria halafu anatoa kitu kidogo na kuachiwa.”
Wakati huohuo, Mustapha Kapalata anaripoti kutoka Tabora kuwa jinamizi la ajali limeendelea baada ya basi la Air Jordan lililokuwa likitoka Mwanza kwenda Arusha kupata ajali katika Kijiji cha Ngonho, Kata ya Kitangili wilayani Nzega na kusababisha kifo cha mtu mmoja na kujeruhi wengine 28 wakijeruhiwa.
Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Jackline Liana alisema mtu huyo aliyefariki ambaye alikuwa fundi wa gari hilo, ametambuliwa kwa jina mmoja la Emmanuel na uchunguzi wa awali unaonyesha chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi. Dereva wa basi hilo alitoweka.
Mganga mkuu mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Nzega, Dk Erick Mbuguye alisema walipokea majeruhi 28, akisema hali ya majeruhi wanne ni mbaya.
POSTED THURSDAY, APRIL 16, 2015 | BY- SUZAN MWILLO, MWANANCHI
Powered by Blogger.