Hekaheka: Madereva wa mabasi wagoma kwa saa tisa, nchi yatikisika
Baadhi ya madereva na wapigadebe wakiwashusha abiria kwenye gari aina ya Town Hiace iliyokuwa imebeba abiri eneo la Ubungo, wakati madereva wa daladala walipokuwa kwenye mgomo, Dar es Salaam.
POSTED SATURDAY, APRIL 11, 2015 | BY- JULIUS MATHIAS NA RAYMOND KAMINYOGe
Dar es Salaam. Hali ya taharuki, hekaheka na tafrani ilitanda kwenye Kituo cha Mabasi cha Ubungo (UBT) na sehemu nyingine jijini Dar es Salaam na mikoani wakati madereva wa mabasi walipofanya mgomo wa takriban saa tisa kuishinikiza Serikali kufuta matumizi ya kanuni mpya za udhibiti wa safari na usalama.
Barabara mbalimbali zilifungwa, mabomu ya machozi kulipuliwa, madereva wa magari madogo kupigwa na viongozi wa Jeshi la Polisi kupuuzwa wakati wakijaribu kutuliza madereva wa magari ya mikoani kuachana na mgomo huo kwa maelezo kuwa madai yao yanashughulikiwa.
Wakati hali ikiwa tete kwenye kituo cha mabasi ya mikoani cha Ubungo, hali ilikuwa mbaya zaidi kwenye vituo vya daladala ambako hakukuwa na mabasi na kulazimisha wananchi wengi kutembea kuelekea makazini.
Hali ilikuwa tofauti kwenye barabara nyingi za jijini Dar es Salaam kutokana na kutokuwapo kwa misululu ya magari kama ilivyo kawaida, huku mabasi ya daladala yakionekana kwa nadra.
Hali hiyo, iliyoanza tangu saa 11:00 alfajiri, ilitulia na kubadilika kuwa shangwe saa 7:30 mchana baada ya Waziri wa Kazi, Ajira na maendeleo ya Vijana, Gaudensia Kabaka kutangaza kufutwa kwa matumizi ya kanuni hizo mpya, huku kamanda wa Polisi wa Kanda ya Dar es Salaam, Suleiman Kova akitangaza kusitishwa kwa tochi maalum za kung’amua mwendo wa mabasi na kuondolewa kwa vituo vya ukaguzi.
Mgomo huo ulitokana na Serikali kuifanyia marekebisho Sheria ya Usalama Barabarani kwa kuingiza kipengele kinachowataka madereva kwenda Chuo cha Usafirishaji (NIT) kwa mafunzo ya muda mfupi mara kila wakati leseni zao zinapoisha ili kupata sifa ya kupata leseni nyingine.
Utaratibu huo uliotangazwa Machi 30, mwaka huu, ulipingwa vikali huku madereva wakidai kuwa hawakushirikishwa katika kuiandaa.
Madai hayo ni pamoja na kuondolewa kwa ulazima wa kusoma kila baada ya miaka mitatu na kujilipia gharama za mafunzo ambazo walidai ni Sh560,000 kwa magari ya kawaida na Sh200,000 kwa magari ya abiria.
Madereva hao pia wanadai kuwa hawawezi kuhudhuria mafunzo hayo wakati hawana mikataba ya ajira inayoweza kuwahakikishia kazi zao zinalindwa hadi wanapomaliza mafunzo.
Madai mengine ni kuondolewa kwa faini ya Sh300,000 kwa kila kosa la barabarani, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchikavu (Sumatra) kuhakiki uhalisi wa dereva anayeandikishwa na mmiliki wa chombo husika.
Waziri Kabaka
Jana wakati hali ilipozidi kuwa mbaya, waziri Kabaka alilazimika kwenda UBT saa 6:15 mchana akiwa ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk Shaaban Mwinjaka, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda.
Kabaka alipokelewa na Kamanda wa Operesheni wa Jeshi la Polisi, Simon Sirro na Kamanda Kova waliokuwa wakimsubiri pamoja na viongozi wa vyama vya madereva nchini.
Baada ya kusikiliza kero zao, Kabaka alisema Serikali inawaagiza wamiliki wa magari kupeleka mikataba Sumatra wakiwa wameongozana na madereva wenyewe.
“Tunapitia mikataba yote ya madereva ili kukagua kama kuna upungufu wowote wa kimaslahi. Chochote kilichopungua tutakiingiza. Hii itaenda pamoja na utekelezaji wa mfuko wa uchangiaji kwa wamiliki wa magari ili kuwahudumia madereva wanaopata ajali wawapo safarini,” alisema.
Kabaka alisema hayo na kueleza kuwa barua zao za kuwataka mawaziri waje kuwasikiliza hana uhakika kama zimewafikia walengwa wote kwani wengi walikuwa katika likizo ndefu ya sikukuu ya Pasaka na kwamba atafanya kila awezalo kuwafikishia ujumbe.
“Serikali haina nia ya kuwatesa madereva wala abiria ndiyo maana tumekuja kuwasikiliza ili kutatua kero mlizonazo. Nitafikisha madai yenu kwa mawaziri wasiokuwepo. Nawaombeni muendelee na kazi ya kusafirisha abiria tutaonana katika mkutano utakaofanyika Jumamosi ijayo,” alisema.
Lakini alipingwa vikali na madereva hao ambao walisema hawakuja kusikiliza siasa.
“Haturudi kazini huna majibu wewe, hatutaki…hatutaki hadi kero zetu zitakapotatuliwa,” alisema mmoja wao kwa sauti kubwa.
Kauli kama hiyo ilirudiwa na makamu mwenyekiti wa Chama cha Madereva wa Malori Tanzania (Chamamata), Shaaban Mdemu ambaye alisema: “Hatutaki siasa hapa mheshimiwa waziri, tunataka uamuzi kuhusu kero tulizokueleza.”
Alisema madereva waliopo wameacha shughuli zao ili kumsikiliza waziri mwenye dhamana, na wanachotaka ni kero zao kumalizwa na si kusikiliza siasa.
Baaadaye Kamanda Kova alichukua kipaza sauti na kutangaza kuondoa matumizi ya tochi za kudhibiti mwendo barabarani.
“Kuanzia sasa hakuna tochi wala check point (vituo vya ukaguzi) za ajabu ajabu. Check point zitakazotumika ni zilizopo katika mizani,” alisema Kova.
Baada ya kupata nafasi nyingine ya kuzungumza, Waziri Kabaka alisema kuanzia sasa Serikali inalifuta sharti la madereva kwenda kusoma kila baada ya miezi mitatu.
“Serikali inakifuta kipengele cha madereva kwenda kusoma kila baada ya miaka mitatu,” alisema Kabaka na kushangiliwa na umati wa madareva ambao walianza kurukaruka wakimshangilia kwa kuimba: “Mama! mama! mama!”
Kabaka alitoa kauli hiyo saa 7:20 mchana na viongozi wa vyama wa madereva wakaamuru madareva hao kuanza safari kwenda mikoani.
Mabasi yalianza kutoka kituoni kuelelekea mikoa mbalimbali nchini kuanzia muda huo na kivutio cha pekee kilikuwa ni kufungwa kwa barabara za Mandela, Sam Nujoma na Morogoro kwa magari yanayotoka katikati ya jiji, ili kuruhusu mabasi hayo kutoka kituo cha Ubungo kuingia barabara ya Morogoro hadi yalipomalizika saa 8:20 mchana.
Wananchi waliokuwa kituoni hapo na abiria walikuwa wakishangilia kwa nguvu wakati mabasi hayo yakiondoka kwa mwendo wa kasi.
Ilivyokuwa
Kuanzia saa 11:05 asubuhi, watu waliokuwa wakitarajia kusafiri kwenda mikoa mbalimbali, walianza kuwasili kituo cha Ubungo ili kupakia mizigo yao yao kwenye mabasi.
Hali hiyo iliendelea kwa utulivu huku wakata tiketi wakiendelea kupokea fedha kutoka kwa wasafiri na makondakta wakipanga mizigo ya abiria kwenye mabasi.
Ilipotimu saa 11:30 asubuhi kila dereva alikuwa nyuma ya usukani wa basi lake, lakini dakika chache baadaye hali ya sintofahamu ilianza kujitokeza baada ya minong’ono kusambaa kuwa mgomo umeanza.
Minong’ono hiyo ilieleza kuwa madereva wa mabasi wameanza mgomo, hivyo hakuna basi litakaloruhusiwa kuondoka ili kuunga mkono mgomo huo unaohusisha vyombo vyote vya usafiri wa nchikavu.
Mpaka saa 12:00 asubuhi tayari ilikuwa dhahiri kuwa kusingekuwa na safari kulingana na ratiba ya kila siku.
Punde magari kadhaa ya Jeshi la Polisi yalianza kuwasili yakiwa yamejaa askari ambao walitapakaa ndani ya stendi hiyo. Walikuwepo trafiki, wapelelezi na wale wa kazi za jumla.
Kila dereva alikuwa ndani ya gari yake likiwa linaunguruma bila kusogea na abiria wakiwa katika viti vyao wakingoja safari ianze. Hata hivyo haikuanza na muda ukazidi kwenda. Ilikuwa hivyo mpaka saa 1:00 asubuhi.
Kamanda Sirro aachwa solemba
Saa 1:45 asubuhi Kamanda Sirro aliwasiri UBT na kuelekea ilipo ofisi ya Umoja wa Madereva wa Mabasi Tanzania (Umamata) kwa lengo la kuzungumza na viongozi ili kuwashawishi madereva hao kuendelea na kazi.
Alifuatwa na watu kadhaa wakati akielekea katika ofisi hizo. Wengi hawakumfahamu. Alipofika kwenye eneo lilikuwa na mkusanyiko mkubwa wa madereva na watu wengine wakiwemo waandishi wa habari alianza kuongea. Lakini baada ya madereva hao kumtambua, waliondoka wakisema kuwa hawataki kuongea chochote na polisi.
Madereva hao walimueleza kuwa hawataki kumsikiliza mpaka atakapokuja na viongozi wao wanaoshikiliwa na jeshi lake pamoja na madereva wengine waliokamatwa.
Kamanda Sirro aliwaambia waandishi wa habari akisema: “Najua kuwa tunawashikilia viongozi wao, lakini hatuwezi kuwaachia kutokana na vurugu hizi. Huwezi kutatua kosa kwa kufanya kosa jingine. Hata viongozi wanalitambua hili linaloendelea hapa.”
Baada ya kutokuwa na njia ya mbadala ya kubadili msimamo ulioonyeshwa na madereva hao, kamanda huyo aliondoka.
Vibaka watumia fursa
Wakati askari polisi wengi wakiwa ndani ya stendi, hali ilikuwa tete kwa watumiaji wa barabara ya Morogoro. Makundi ya vijana walitanda barabarani na kuanza kuwashambulia madereva na magari ya abiria waliokuwa katika mabasi madogo aina ya Toyota Hiace, Noah, Canter, teksi, bajaj na pikipiki.
Vijana hao ambao hakufahamika, walianza kuyasimamisha magari yote ambayo hayakuwa ya serikali au binafsi. Waliomba leseni kwa madereva husika na hata walipopewa waliwashambulia wao pamoja na abiria walikuwa nao.
“Unaona madereva wote wamegoma kwani wewe unataka kurudi chuo na kusoma tena utakapoenda ku-renew leseni yako? Mbona husemi? Baadaye mvua ya makonde ilianza kuporomoshwa kwa dereva pamoja na abiria aliokuwa nao,” alisimulia mmoja wa vijana walioongea na gazeti hili.
Alisema wapo walioshushwa na kupigwa. Wanawake walishikwashikwa hovyo huku magari yakipekuliwa bila ridhaa ya wenye nayo. Waliporwa pia lakini hawakuwa na namna, nguvu ya umma ilikuwa mikononi mwa vibaka hao.
Waliokuwa kwenye pikipiki au bajaji walishushwa wakapigwa. Walisukumwa bila kujali wanaangukia wapi. Akina mama waliathirika zaidi kwani wapo walioshushwa na kulazimishwa kubeba mizigo yao. Wengine waliumia baada ya kusukumwa au kuvutwa na kuanguka.
Walifanya oparesheni hiyo kwa madereva wote waliokatiza; ama lango la kutokea au kuingilia stendi hiyo. Baada ya kupata taarifa za vurugu hizo, gari za Jeshi la Polisi aina ya Land Rover Defender ziliwasili na kutawanya makundi ya watu waliokuwa wamekusanyika hovyo.
Ubungo uwanja wa vita
Kuanzia saa 3:05 hadi 5.00 asubuhi, Kituo cha Mabasi Ubungo kiligeuka uwanja wa vita baada Polisi, kwa kushirikiana na Kikosi cha Kuzuia Ghasia (FFU), kulipua mabomu ovyo ili kuwatawanya vijana waliokuwa wakipiga magari kwa mawe.
Vijana hao ambao inadaiwa si madereva, walikuwa wakizuia magari yasipite katika barabara hiyo wakitaka madereva waungane na mgomo huo. Vijana hao wanaofikia 25 walikamatwa na polisi. Zaidi ya milio 50 ya mabomu ya machozi ilisikika na kusababisha eneo hilo kuwa lenye moshi mithili ya nyumba inayoungua.
Wakati mabomu hayo yakilipuliwa, wananchi, wakiwamo wanawake na watoto, walikimbia huku na kule ili kunusuru maisha yao.
Wapo baadhi ya abiria waliojeruhiwa na kupoteza fahamu wakati wakikimbia, akiwamo Abdallah Kassim aliyekuwa na tiketi za basi la Kibinyiko linalofanya safari kati ya Dar es Salaam na Dodoma.
Baada ya kuzinduka, Abdallah hakuwa na uwezo wa kuongea kutokana na kupumua kwa tabu wakati akiwa ametelekezwa nje ya kituo cha polisi kilichopo UBT.
Wakati mabomu hayo yakiendelea, baadhi ya vijana walikimbia huku na kule na wengine walionekana wakiwa wamejeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao.
Kabla ya mabomu hayo hayajalipuliwa, vijana hao walichoma matairi katikati ya barabara ya Morogoro karibu na kituo hicho na kusababisha magari yashindwe kupita.
Biashara Ubungo
Biashara ya chakula katika eneo la kituo hicho ilikuwa yenye mafanikio makubwa kutokana na uwingi wa abiria na wananchi wengine.
Mmoja wa wauzaji wa chakula, maarufu kwa jina la mamalishe, Anna Temu alisema mgomo huo umemfanya auze chakula kingi ikilinganishwa na siku nyingine.
“Wafanyabiashara wengi wanaombea mgomo huu ungedumu hata kwa siku tatu kwa sababu kwa saa nane wamepata fedha nyingi ikilinganishwa na siku nyingine,” alisema.
Mmoja wa wauza soda kituoni hapo, Sudi Suleiman alisema ilibidi afuate soda Manzese baada ya kreti sita alizokuwa nazo kumalizika ilipofika saa 5:30 asubuhi.
“Kwa kawaida nauza kreti tatu kwa siku lakini jana ilikuwa nzuri kibiashara, bidhaa zote maji na vitafunio vingine vilinunuliwa kwa wingi,” alisema.
Abiria wazungumza
Baadhi ya abiria walisema mgomo huo wa abiria umetokana na viongozi wa serikali wasio na weledi wa kazi.
Neema Mwamfupe, aliyekuwa akisafiri kwenda Tanga kwa basi ya Raha Leo, alisema mgomo huo ulijulikana tangu wiki iliyopita.
“ Kama tungekuwa na viongozi wa Serikali wanaofanya kazi hii kwa weledi, mgomo wa leo usingekuwepo na usingesababisha madhara kwa wasafiri,” alisema.
Alisema lengo la safari yake lilikuwa ni kumsindikiza mgonjwa ambaye anayekwenda kwao Pangani na kwamba itambidi alale Tanga kwa kuwa atachelewa mabasi ya kuunganisha.
“Kulala njiani ni kuongeza gharama na usumbufu mkubwa. Ninawachukia viongozi hawa wasiojali maisha ya wenzao,” alisema. Abiria mwingine, Husna Abdallah aliyekuwa akisafiri na basi la Shabiby kwenda Bahi, alisema kwa kuwa anasafiri kwenda Bahi itabidi alale Dodoma.
“Kama tungeondoka asubuhi, ningeweza kufika nyumbani Bahi lakini kwa kuwa tutafika usiku Dodoma sitawahi mabasi ya kwenda huko,” alisema.
Kamanda Kova
Baada ya muda Kamanda Sirro alirudi akiwa na Kova na kwa pamoja walijaribu kuwatuliza madereva hao bila mafanikio. Kutokana na hali kutokuwa shwari hasa nje ya stendi, walisindikizwa na magari kumi ya polisi likiwemo la maji ya kuwasha.
Mpaka saa 10:00 asubuhi hapakuwa na dalili ya mafaniko, hivyo kuwalazimu kuondoka na kuwaacha vijana wao wakiimarisha ulinzi katika eneo hilo.
Madereva waliendelea kushinikiza kuachiwa kwa viongozi wao, madereva 25 waliokamatwa mkoani Morogoro pamoja na mwenyekiti wa madereva mkoani Njombe. Waliporejea, walikuwa na viongozi hao.
Wakiwa na makamanda hao, viongozi hao walisimulia kilichojiri tangu walipokamatwa na makubaliano waliyoyafanya na Serikali. Walieleza kuwa viongozi wamesema watatatua kero hizo kabla ya Jumamosi ijayo.
Kauli hiyo ilizusha kelele na madereva hao kupaza sauti zao wakisema wanawataka viongozi hao jana la sivyo wataendelea kuwasubiri mpaka watakapokuwa tayari kuzungumza nao.
Makumbusho
Abiria walianza kuchanganyikiwa kutokana na kukosekana kwa mabasi ya kuwapeleka maeneo mbalimbali ya jiji.
Mwananchi iliyokuwa kituo cha Makumbusho saa 12:15 ilishuhudia abiria kufurika huku daladala zikiwa chache na zaidi zilikuwa zikishusha abiria na kuondoka tupu kituoni.
Gongo la Mboto
Katika kituo cha Gongo la Mboto, wananchi walifunga barabara wakizuia magari binafsi kwenda mjini baada ya kukosa usafiri kwa muda mrefu.
Mwananchi ilishuhudia wananchi wakiwa wametanda barabarani na baadhi ya magari yaliyojaribu kupita yalizuiwa na kusababisha taharuki.
Mwandishi wa Mwananchi aliyejaribu kupita na gari ndogo, alifuatwa kwa kasi na kundi la vijana na kulazimika kugeuza gari na kurudi hadi barabara ya kuelekea kambi ya Jeshi la Wananchi ya kikosi cha 511 ambako vijana hao walishindwa kuingia.
Magari madogo yalilazimika kupita barabara ya kuelekea Kipunguni na kutokea Mombasa kuendelea na safari.
Hadi kufikia saa 11:45 alfajiri ni daladala chache zilikuwa barabarani na zaidi ni zilizokuwa zinatoka Kisarawe, Masaki na Chanika hadi Buguruni. Katika hatua nyingine, makamu mkuu wa NIT, Dk Simon Lushakuzi amesema mgomo huo haukuwa na mashiko yoyote na kwamba hauna uhusiano na kanuni mpya zilizoandaliwa kwa madereva nchini.
Kabla ya kuandaliwa kwa kanuni hizo, uongozi wa NIT uliwahi pia kunukuliwa kwamba asilimia kubwa ya madereva hawana vyeti vyenye ubora. Kanuni hizo zilitakiwa kuanza rasmi kutumika Aprili Mosi.
Dk Lushakuzi, ambaye pia ni mkuu wa Kitengo cha Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi alisema kanuni hizo bado zilikuwa kwenye hatua za mwisho katika maandalizi yake hivyo hakukuwa na sababu za msingi kuanzisha mgomo kwa kuwa hazijatangazwa rasmi.
“Kwanza kanuni hizo haziwezi kutumika mpaka wadau wote tujulishwe, hata sisi hatujapata barua, lakini pia madereva hao walikuwa ni miongoni mwa wadau walioshiriki kujadiliana juu ya kanuni hizo, ninachofahamu mchakato umefikia hatua za mwisho ila bado kanuni hazijaanza kutumika,” alisema Dk Lushakuzi.
“Kuhusu, hoja ya gharama na muda wa kusoma kozi ya udereva, si kweli ada itakuwa Sh560,000 kwani kozi hiyo itakuwa ya muda mfupi. Kozi ya muda mrefu (siku 10) tunatoza Sh200,000 sasa hiyo fupi ya siku nne au tatu itakuwa chini zaidi ya hapo.”
Habari zaidi na Tausi Ally, Kalunde Jamal, Goodluck Eliona, Emma Kalalu, Lilian Timbuka, Beatrice Moses, Hadija Jumanne, Suzan Mwilo, Imani Makongoro na Kelvin Matandiko
POSTED SATURDAY, APRIL 11, 2015 | BY- JULIUS MATHIAS NA RAYMOND KAMINYOGe