Rais akabidhiwa ripoti ya Operesheni Tokomeza Ujangili
Rais Jakaya Kikwete
Dar es Salaam. Tume iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete Mei Mosi mwaka jana kuchunguza vitendo vilivyotokana na uendeshaji wa Operesheni ya Tokomeza Ujangili ambayo iliwang’oa mawaziri wanne, imemaliza kazi jana na kukabidhi ripoti kwa Rais Jakaya Kikwete, Ikulu, Dar es Salaam.
Mawaziri waliojiuzulu ni; aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo.
Operesheni hiyo ilianza Oktoba 2013 na kusitishwa na Bunge Novemba 4 mwaka jana kutokana na ukiukwaji wa sheria na haki za binadamu wakati wa utekelezaji wake.
Baada ya kupokea ripoti kutoka kwa mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji na Balozi mstaafu Hamisi Msumi, Rais Kikwete aliishukuru kwa kufanya kazi nzuri.
Pia alisisitiza kwa sasa suala hilo limefika mwisho wake.
“Serikali itaisoma Ripoti hii na katika wiki mbili itatoa maelezo ya jinsi itakavyoshughulikiwa,” ilieleza sehemu ya taarifa ya Ikulu ikimnukuu Rais Kikwete.
Tume hiyo iliundwa kuchunguza tuhuma mbalimbali za uvunjifu wa sheria, kanuni, taratibu na hadidu za rejea za utekelezaji wa operesheni hiyo.
Rais Kikwete aliipa tume hiyo jukumu la kupendekeza hatua stahiki za kisheria za kuchukua dhidi ya watakaobainika kuhusika na uvunjifu wa sheria na taratibu na kushauri namna bora ya utekelezaji wa operesheni kama hiyo hapo baadaye.
Tume hiyo ilichunguza namna operesheni hiyo ilivyotekelezwa na maofisa kama walizingatia sheria, kanuni, taratibu na hadidu za rejea walizopewa.
Katika maelezo yake, Jaji Msumi alisema tume ilitembelea mikoa 20 na wilaya 38 na kupokea malalamiko mbalimbali kutoka kwa viongozi wa Serikali, mawaziri wanne waliojiuzulu, walalamikaji, waathirika wa operesheni.