Sekta ya Viwanda: Kiini cha maendeleo Tanzania
Kwa mujibu wa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda, sekta ya viwanda ndiyo hasa inayoshikilia ufunguo wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini kutokana na uwezo wake wa kutengeneza ajira nyingi.
Akizungumza katika uzinduzi wa ripoti ya sekta ya viwanda katika ukanda wa mashariki mwa Afrika mwezi uliopita, Waziri Kigoda anasema sekta hiyo siyo tu injini ya taifa katika kukuza uchumi bali pia katika kubadili maisha ya Watanzania.
Ripoti hiyo ilikuwa inasisitiza kuchochea matumizi ya teknolojia, uvumbuzi, uzalishaji pamoja na kuunganisha viwanda na sekta nyingine za uchumi.
Ripoti hiyo iliyozihusisha nchi za Tanzania, Burundi, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Shelisheli na Uganda, ni sehemu ya utafiti wa sekta ya viwanda uliyodhaminiwa na Kituo cha Rasilimali Ukanda wa Mashariki mwa Afrika cha Benki ya Maendeleo ya Africa.
“Kunaweza kuwa na nguzo nyingine za maendeleo lakini hakuna hata moja yao inayoweza kushinda nguvu ya viwanda. Viwanda siyo tu vinakuza uchumi kwa kuongezea bidhaa thamani bali pia vinatengeneza ajira nyingi ambazo huongeza uzalishaji,” anasema Waziri Kigoda.
mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) Godfrey Simbeye aliliambia gazeti hili katika mahojiano kwa njia ya simu kwamba nchi yoyote inayotaka kujitegemea kwenye bajeti yake, lazima kwanza iimarishwe uuzaji wa bidhaa zake zilizoongezewa thamani nje ya nchi.
“Nchi inayotumia bidhaa za nje kwa wingi kama Tanzania isitarajiwe kujitegemea kibajeti. Ili nchi yoyote iepuke misaada ya kibajeti kutoka kwa wahisani basi lazima iimarishe mauzo ya nje,” anasema Simbeye.
Pamoja na umuhimu huo kwa uchumi na maisha bora ya jamii, sekta ya viwanda Tanzania bado inakabiliwa na changamoto nyingi kiasi cha kuchelewesha kufikia malengo yaliyokusudiwa. Kwa mujibu wa Simbeye, Tanzania haina sera madhubuti zinazolenga kuboresha na kuendeleza sekta ya viwanda. Sera zilizopo, anasema, zinawaruhusu wawekezaji kuja kufungua maduka nchini ili wauze bidhaa za nje badala ya kuzalisha hapahapa.
“Kama serikali yetu ingekuwa makini, ingewaruhusu hawa wawekezaji wa maduka makubwa kuingiza bidhaa za nje kwa muda fulani kisha waanzishe viwanda,” anasema Simbeye.
Wakati ripoti hiyo ikionyesha kwamba sekta ya viwanda Tanzania imekuwa ikikua kwa asilimia tisa kwa mwaka, bado kiwango hicho ni kidogo ikilinganishwa na malengo yaliyopo katika Dira ya Maendeleo-2025.
Dira hiyo inataka kuona mchango wa sekta ya viwanda katika uchumi wa Tanzania unafikia asilimia 25, kama ilivyo katika nchi za Kusini Mashariki ya bara la Asia ambazo zipo nusu ya kufikia uchumi wa viwanda.
Ripoti hiyo inaonesha kwamba kiwango kidogo cha biashara ya nje ya nchi pamoja na masuala kadhaa yanayohusiana na uanzishwaji na ufungaji wa kampuni kama sababu kubwa zinazokwamisha ukuaji wa sekta ya viwanda nchini.
“Kwa kuzingatia umuhimu wa biashara ya nje ya nchi ambayo hutengeneza mazingira ya kujifunza na kuongeza ujuzi, kudorora kwa biashara hiyo huchelewesha maendeleo ya haraka ya viwanda,” inasomeka ripoti hiyo.
“Kwa kuzingatia umuhimu wa mwingiliano wa uzalishaji wa viwanda na sekta zingine, ugumu katika uanzishwaji wa taasisi za biashara ni kikwazo kikubwa katika usambazaji wa bidhaa za viwandani,” kwa mujibu wa ripoti hiyo.
Changamoto nyingine inatokana na kuwepo kwa miundombinu dhaifu ya kiuchumi ambayo ipo chini ya viwango vya kimataifa na hata vile vya bara la Afrika.
Umeme usiotosha ni mojawapo ya matatizo makubwa kabisa ya kimiundombinu Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Ripoti hiyo pia inaonesha kuwa ukanda wa mashariki wa Afrika ndio una kiwango kidogo kabisa cha uzalishaji wa nishati na wadau wanasema kukatika ovyo kwa umeme pamoja na kuwepo kwa mitambo ghali ya kuzalishia ndiyo vitu vinavyowaongezea gharama.
“Ukanda huu wa mashariki wa Afrika unazo barabara zinazoungana lakini ni duni, hali ambayo huongeza gharama za usafirishaji ukijumuisha mwendo kasi na umbali uliopo. Kukosekana kwa usafiri wa reli madhubuti kunaongezea matatizo ya usafirishaji wanchi kavu. Na mwisho, suala la usimamizi wa usafishaji wa bidhaa huenda likabakia kama tatizo kubwa katika miundombinu linalokwamisha uendelezaji wa viwanda,” inasema ripoti hiyo.
Bandari za ukanda huu nazo bado zinafanya kazi chini ya viwango ikilinganishwa na washindani wao katika sehemu zingine.
Changamoto hizi ambazo zimetajwa katika ripoti, zinakwamisha maendeleo ya sekta ya viwanda nchini na iwapo hazitatatuliwa, wadau wanasema, hata malengo ya kufikia asilimia 15 ifikapo mwaka 2020 yatakuwa safari ngumu. Inatajiwa kwamba serikali pamoja na wadau wengine watatatua changamoto hizi za kibiashara ili kuendeleza sekta ya viwanda ambayo mauzo ya bidhaa zake nje ya nchi yamekua kwa asilimia 31 kati ya mwaka 2000 na 2010.
Katika uzinduzi wa mpango wa Matokeo Makubwa Sasa unaohusu uboreshaji wa mazingira ya kibiashara mwaka jana, Rais Jakaya Kikwete anasema Serikali itafanyia kazi kwa makini ripoti ya Benki ya Dunia kuhusu ufanyaji biashara ya mwaka 2014 kwa kuboresha maeneo yaliyotajwa ili kuboresha mazingira ya biashara nchini. “Bila shaka, ripoti hii haina habari njema kwetu. Nakiri kwamba tuna matatizo ya ufanisi katika kutoa huduma ambazo ni muhimu kwa maendeleo ya sekta binafsi. Habari njema ni kwamba tumedhamiria kuziondoa changamoto zote hizi,” anasema Rais Kikwete. “Nawahimiza sekta ya umma na ile ya binafsi kufanya kazi kwa pamoja kwa misingi ya uzalendo katika uchambuzi wa matatizo tuliyonayo pamoja na kutafuta suluhisho la kudumu,” anasema.
Rais Kikwete pia anasema kwamba ili uboreshaji wa mazingira ya kibiashara uwe na maana, lazima uende pamoja na uboreshaji wa Serikali katika kutoa huduma.
“Mitazamo ya taasisi za umma pamoja na wale wanaozisimamia lazima ibadilike. Kinachoisibu sekta binafsi kinatakiwa kuihusu pia hata serikali,” anasema.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa hivi karibuni na Profesa Samwel Wangwe na wenzake “changamoto za kiteknolojia, kifedha, kisera na kiutawala bado hazijatatuliwa na hivyo kukwamisha maendeleo ya haraka katika viwanda na mabadiliko ya kijamii.”
Kila Alhamisi katika gazeti la Mwananchi. Kwa mrejesho tutumie ujumbe mfupi wa maneno kupitia 0786240172. Washiriki wanne, watapewa muda wa maongezi wa Sh10,000.
Ukurasa wa Urahisi wa Kufanya Biashara umerudi katika jarida la Uchumi, gazeti la Mwananchi kila Alhamisi. Lengo lake ni kusaidia juhudi za kuboresha mazingira ya ufanyaji wa biashara Tanzania.
POSTED THURSDAY, APRIL 16, 2015 | BY- VENERANDA SUMILA