Mgomo wa maderva: Kizazaa mikoa yote
Kituo Kikuu cha mabasi yaendayo nje ya Manispaa ya Morogoro kikiwa bila daladala kufuatia mgomo wa madereva wa mabasi ya abiria mkoani humo jana. Picha na Juma Mtanda
Mikoani. Wananchi waliokuwa wamepanga kusafiri kutoka mikoa mbalimbali, jana walijikuta kwenye hali ngumu baada ya mabasi kushindwa kuondoka kama ilivyokuwa imepangwa kutokana na mgomo wa madereva ulioendeshwa nchi nzima kwa takriban saa tisa kabla ya Serikali kuingilia kati.
Baadhi ya wasafiri wa masafa marefu walijikuta wakishindwa kuendelea na safari zao jana asubuhi baada ya madereva kutelekeza mabasi, huku wengine wakikwama vituoni ambako walitarajia kupata usafiri kwenda mikoa mingine kwa ajili ya shughuli mbalimbali, zikiwamo za kibiashara, matibabu na ajira.
“Nimeshindwa kwenda Dar es Salaam kwenye matibabu kwa sababu ya mgomo huu,” alisema msafiri aliyejitambulisha kwa jina la Halima Haule ambaye alitakiwa kufanyiwa upasuaji wa uvimbe wa uzazi kesho kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Haule alikuwa kwenye kituo cha mabasi cha mjini Songea hadi saa 7:00 mchana lakini hakuweza kuondoka na basi la New Force ambalo alishakata tiketi.
Licha ya Chama cha wamiliki wa Mabasi ya Abiria (Taboa) kukanusha kuwapo kwa mgomo huo, madereva wa mabasi walitekeleza azma yao ya kugoma kuanzia jana alfajiri wakiishinikiza Serikali kusitisha utekelezaji wa kanuni mpya za leseni na ratiba za usafiri.
Kwa mujibu wa kanuni hizo mpya, madereva ambao leseni zao zitaisha, watatakiwa kwenda Chuo cha Usafirishaji (NIT) kwa mafunzo ya wiki mbili na kwa gharama zao, huku wale ambao mabasi yao yatahusika kwenye ajali wakitakiwa kuwekwa mahabusu na kufutiwa leseni zao hata kama hawakusababisha ajali hizo.
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) lilitoa ratiba inayotaka mabasi hayo yaende kwa mwendo wa kilomita 80 kwa saa na yale ya masafa marefu kusimama wakati jua linapozama na kuendelea na safari kunapokucha.
Hali ilivyokuwa Mbeya
Mkoani Mbeya, zaidi ya watua 300 waliokuwa wakitaka kuelekea jijini Dar es Salaam walikwama kwenye kituo cha mabasi cha Tunduma.
Watu hao hawakupata usafiri hadi ilipotimu saa 5:00 asubuhi wakati mabasi hayo yalipoanza safari.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya abiria, walionyesha kushtushwa na mgomo huo kwani walikuwa tayari wamekata tiketi bila ya kuwa na taarifa zozote za mgomo.
Kampuni za mabasi ambayo hayakuondoka asubuhi kama ilivyo kawaida ni Colar Star, New Force, Abood, Ilasi, Sai Baba, na Princes Muro.
Mfanyakazi wa kampuni ya Abood, Godfrey Mjenda alisema mabasi yaliyoondoka ni yale yanayoanzia Stendi Kuu ya Mbeya mjini, lakini ya Tunduma hayakuondoka kama ilivyopangwa.
Kamanda wa polisi wa mkoani hapa, Ahmed Msangi alisema suala hilo lilikuwa gumu kulidhibiti kwa vile linaratibiwa na watu walioko Dar es Salaam.
Ruvuma
Mjini Songea, wasafiri walisota katika kituo cha mabasi cha Msamala baada ya madereva kutelekeza mabasi na kuzima simu zao za mkononi. Hali hiyo iliwalazimu baadhi ya wasafiri hao kuomba msaada kwa Jeshi la Polisi wakitaka warudishiwe nauli zao.
Akizungumza na Mwananchi, Flora Kambi aliyedai kuwa alikuwa akitarajia kuelekea Dodoma kwenye usaili wa kazi, alisema alishindwa kusafiri.
“Mimi nauomba uongozi wa polisi na makampuni ya mabasi kutusaidia tuweze kupata haki zetu kwani wametuchanganya… wangesema ukweli kuliko kututelekeza,” alisema.
Mwanza
Jijini Mwanza madereva wa mabasi ya mikoani yanayoegeshwa vituo vya Buzurugwa na Nyegezi nao walikwamisha safari za abiria wao.
Katika stendi ya Buzurugwa ambako mabasi yaendayo mkoani Mara na Simiyu huanzia safari zake, hali ilikuwa tete.
Mwananchi lilifika kituoni hapo saa12:00 alfajiri na kushuhudia mabasi mengi yakiwa yameegeshwa bila madereva.
“Tupo hapa tangu saa 12:00 alfajiri, mabasi yapo mengi kama unavyoona, lakini madereva hakuna. Tunashindwa jinsi ya kufanya, tunapata shida, tunaomba mamlaka husika zitatue mgogoro huu haraka, kwani unatuathiri,” alisema abiria aliyejitambulisha kwa jina la Joseph Wambura.
Kwenye stendi ya Nyegezi ambako mabasi yaendayo mikoani huanzia safari zake hali ilikuwa tete na kumlazimisha Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Baraka Konisaga kuingilia kati bila mafanikio.
Baadhi ya madereva waliiambia Mwananchi kuwa tamko la Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga kuwataka madereva kupunguza kasi na kwamba, atakayekiuka awekwe mahabusu siku 14 na kufutiwa leseni, ni chanzo cha mgomo huo.
Dereva wa basi la kampuni ya Bunda Express, Victor Gervas alisema mgogoro uliopo unatokana na waajiri wao kukubali kufuata sheria ambazo zimeweka na Kamanda Mpinga.
Kahama
Wilayani Kahama, mabasi yaendayo Dar es Salaam na nchi jirani za Rwanda, Burundi na Uganda abiria wa masafa marefu hawakuweza kuendelea na safari.
Makamu mwenyekiti wa mawakala wa mabasi wa kituo cha mjini Kahama, Abdi Mohamed alisema licha ya madai ya madereva kuwa ya msingi, tatizo ni wale wa masafa marefu ambao wametoka Dar es Salaam na abiria huku wakijua kuna mgomo kisha kuwatelekeza stendi.
Mohamed alisema wao ni mawakala wanaotaka mabasi yasafiri ili wapate fedha na kwamba, Serikali inatakiwa kuyapatia ufumbuzi madai ya madereva.
Dereva wa basi la kampuni ya Leina, Said Sultan alisema hawapo tayari kuendelea na safari kama Serikali haitaondoa masharti ya dereva kwenda mafunzo ya udereva wakati leseni yake inapoisha na kulipa gharama kubwa za mafunzo.
Shinyanga na Tabora
Hali ilikuwa kama hiyo kwenye mikoa ya Shinyanga na Tabora ambako mabasi yaendayo Dar es Salaam yalisimama eneo la Kigwa, takriban kilomita 40 kutoka Tabora na kurudi stendi. Mabasi ya Mwanza nayo yaliishia njiani huku yale yaliyokuwa yaondoke kuanzia saa 1:00 asubuhi yakishindwa kufanya hivyo.
Mabasi ya Kigoma yaliondoka lakini moja lilisimama eneo la Usoke, zaidi ya kilomita 50 kutoka Tabora, kusubiri maelekezo na jingine la kampuni tofauti likisimama karibu na Urambo.
Ofisa wa Sumatra mkoani Tabora, Joseph Michael alisema wanasubiri majadiliano kati ya Serikali na wanaoratibu mgomo huo, hivyo waliwataka abiria kusuburi hadi saa 7:00 mchana kujua hatma ya safari yao. “Tumewataka abiria wawe na subira hadi saa 7:00 mchana tutakapowaeleza hatua iliyofikiwa,” alisema.
Kagera
Mkoani Kagera, mgomo ulianza kimyakimya kituo cha mabasi mjini Bukoba ambako hadi saa 6:00 mchana, hakuna gari la abiria lililokuwa limewasili kutoka wilayani Muleba.
Madereva katika kituo cha Muleba waligoma kupakia abiria waliokuwa wanaelekea mjini Bukoba, huku madereva wakisema wasingerudi kama ilivyo kawaida.
Mmoja wa madereva hao, Dominick Festus anayeendesha gari la abiria kuelekea Muleba, alisema anapeleka abiria wilayani humo baadaye atajiunga na mgomo kama walivyofanya wenzao wa maeneo mengine.
Geita
Mkoani Geita, mgomo huo umewaathiri wauzaji na wasomaji wa magazeti kutokana na kutofika kwa mabasi yanayotoka Mwanza ambayo husafirisha magazeti.
Mmoja wa wauzaji wa magazeti mkoani hapa, Fidelis Kanani alisema alisubiri kwa zaidi ya saa mbili kupokea magazeti, lakini hakuna basi lililofika kwa muda na baadaye alipokea taarifa kuwa kuna mgomo.
“Huwa napokea magazeti kuanzia saa 2:00 asubuhi, lakini hivi sasa ni saa 4:00 hakuna basi lolote lililofika. Hili ni tatizo kwangu kwa maana leo mauzo yangu yatashuka,” alisema Kanani. Baadhi ya madereva wa mabasi yanayofanya safari za Mwanza na Kahama, walisema waliogoma ni wenzao wa masafa marefu.
Hali kama hiyo ilikuwa wilayani Musoma baada ya madereva wa magari ya abiria kuungana na wenzao nchini kugoma.
Dereva wa basi la kampuni ya Super Sami, Alphonce Samwel alisema ili madereva wakubaliane na hoja hiyo ni vyema Serikali ikawaeleza wanachotakiwa kwenda kusomea.
Kigoma wajipanga zaidi
Mkoani Kigoma, dereva wa basi la Adventure, Eddy Mande alisema kitendo cha kukamatwa kwa viongozi wa kitaifa wa chama cha madereva, kiliwachochea mgomo huo.
“Hadi asubuhi hatukuwa na taarifa kwamba tutagoma, lakini tulipata meseji za simu kutoka kwa wenzetu kwamba tugome ili viongozi wetu waachiwe huru. Lakini tuna malalamiko yanayohusu haki zetu za msingi na lazima yapatiwe ufumbuzi,” alisema Mande.
Katika kudhibiti magari, bajaji na pikipiki ambazo zilikaidi mgomo huo, baadhi ya madereva na wapigadebe walijikusanya na kuweka vizuizi barabarani kuzuia wenzao wasiendelee na kazi hadi polisi wa wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) walipofika na kuwatawanya.
Vizuizi hivyo viliwekwa eneo maarufu la Darajani lililopo Ujiji, Mlole jirani na Shule ya Sekondari ya Ujiji ambako bajaji moja ilivunjwa kioo katika harakati za kupambana na wazuiaji.
Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva Mkoa wa Kigoma (Umaki), Kasongo Kashushu alisema licha ya kwamba mgomo huo utamalizika mapema, wanafikiria kuandaa mwingine mkubwa zaidi utakaodumu kwa zaidi ya siku moja kushinikiza kushughulikiwa kwa madai yao.
Dodoma hali shwari
Hata hivyo, mkoani Dodoma safari za mikoani ziliendelea kama kawaida tofauti na miji mingine. Katika stendi ya mabasi, huduma za usafiri ziliendelea kama kawaida na mabasi yalikuwa yakiondoka kwa zamu kama ilivyo siku zote.
Mmoja wa mawakala wa mabasi ya Mohamed Trans, Msafiri Sadala alisema kuwa hawajatangaza mgomo.
Sadala alisema viongozi wao waliwaambia jana kuwa huduma za mabasi ziendelee kama kawaida hadi hapo watakapowajulisha
POSTED SATURDAY, APRIL 11, 2015 | BY- WAANDISHI WETU, MWANANCHi