Baba Ahukumiwa Kifungo cha Maisha Jela Kwa Kosa la Kumbaka Mtoto wake Wa Miaka 9 na Kumsababishia Ujauzito
Mahakama ya Hakimu Mkazi wilaya ya Shinyanga imemhukumu kifungo cha maisha jela mkazi wa mtaa wa Kitangili katika manispaa ya Shinyanga baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka na kumpa ujauzito mtoto wake wa kambo, mwanafunzi wa darasa la tatu.
Alimbaka mtoto huyo kutimiza masharti ya mganga ili kutoa tiba kwa mkewe.
Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi mwandamizi wa wilaya, Thomson Mtani alisema mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka ukiongozwa na wakili wa serikali, Judith Tuka.
Mtuhumiwa Osward Charles (45) mkazi wa Kitangili alifikishwa mahakamani kwa tuhuma mbili. Kosa la kwanza likiwa ni kumbaka mtoto wake mwenye umri chini ya miaka kumi ambaye ni mwanafunzi kinyume na kifungu namba 130, kifungu kidogo cha kwanza na cha pili na kifungu namba 131 kifungu kidogo cha pili cha sura ya 16 cha kanuni ya adhabu.
Kosa la pili ni kumwingilia kimwili mtoto wake ambaye ni mwanafunzi wa shule na kumpa ujauzito kinyume na kanuni ya tano ya sheria ya elimu ya mwaka 2003 inayotoa adhabu kwa watu wanaowaoa na kuwapa mimba wanafunzi wa shule kama ilivyo katika kifungu cha 35 kifungu kidogo cha tatu cha sheria ya elimu ya 353.
Ilidaiwa na mwendesha mashtaka mwanasheria wa serikali Judith Tukakuwa, kati ya Novemba 12 mwaka 2012 na Septemba katika eneo la mtaa wa Kitangili manispaa ya Shinyanga mshitakiwa alimbaka mtoto wake wa kambo ambaye ni mwanafunzi mwenye umri wa miaka tisa na kumsababishia ujauzito.
Awali mshitakiwa katika mwenendo wa kesi alikana kutenda makosa hayo lakini katika utetezi wake mbele ya mahakama kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo ili mahakama impunguzie adhabu alikiri kumbaka mtoto wake mbele ya mama yake mzazi kwenye kitanda kimoja baada ya kupewa maagizo ya mganga wa jadi kama sehemu ya tiba ya mke wake aliyekuwa akisumbuliwa na maradhi.