UHAKIKI WA USHAIRI
UHAKIKI WA USHAIRI
FANI
1. Muundo
Muundo katika ushairi hujumuisha umbo la ubeti na shairi zima. Ili kuchambua muundo katika ushairi mhakiki unapaswa kueleza idadi ya mistari (mishororo) katika kila ubeti uliomo kwenye shairi husika.
Mfano, ikiwa shairi limeundwa na beti:
(a) Mstari mmoja (1) muundo huu huitwa TAMOLITHA
(b) Mistari miwili (2) muundo huu huitwa TATHNIA
(c) Mistari mitatu (3) muundo huu huitwa TATHLITHA
(d) Mistari mine (4) muundo huu huitwa TARBIA
(e) Mistari mitano na kuendelea muundo huu huitwa SABILIA au TAKHMISA.
(f) Ikiwa shairi halina mpangilio maalumu wa mistari na beti, shairi hilo huitwa shairi huru na kitupekee kinachotegemewa katika kujadili muundo wa shairi huru ni MUWALA au nmtiririko wa mawazo katika shairi zima.
2. Mtindo
Tunaweza kueleza mtindo katika ushairi kwa kuangalia urari wa vina na mizani.
Vina, ni silabi zinazofanana katika nusu mstari na mwisho mwa mstari katika kila mstari wa kila ubeti.
Mfano,
Mume wangu nakupenda, josefu amenikuna,
Nimekula naye tunda, nampenda sana,
Ila usifanye inda, mimi ni wako kimwana,
Nitaishi kwa mpango, kwako na kwake josefu.
Katika ubeti huu, vina vya kati ni nda na vina vya mwisho ni na.
Mizani, ni idadi ya silabi katika mstari kwenye ubeti.
Mfano,
Mu–me-wa-ngu-na-ku-pe-nda (8), jo-se-fu-a-me-ni-ku-na (8)
Kwa kawaida, ushairi wa kimapokeo huwa na mizani nane (8) kwa kila kipande na hivyo kufanya idadi ya mizani kuwa kumi na sita (16).
Mstari au Mshororo, mshororo ni kila mstari uliohusika katika ujenzi wa shairi,
Mfano,
Mume wangu nakupenda, josefu amenikuna,
mshororo
Nimekula naye tunda, nampenda sana,
mshororo
Ila usifanye inda, mimi ni wako kimwana,
mshororo
Nitaishi kwa mpango, kwako na kwake josefu.
Kiitikio au kibwagizo
Kipande, mshororo mmoja huweza kuwa na idadi mbili au tatu ya vipande.
Mfano, kwenye mshororo wa (Mume wangu nakupenda, josefu amenikuna) kuna vipende viwili.
1 2
3. Matumizi ya lugha
Mshairi anauhuru mkubwa katika kutumia lugha, uhuru huo hutokana na uwalali wake katika kukiuka baadhia ya kanuni za matumizi ya lugha ilimradi shairi lilete maana. Pia uhuru mwingine hujitokeza katika uteuzi wake wa msamiati, ubunifu wake, kubuni msamiati wake na kuyaendeleza maneno kwa njia tofauti.
Katika ushairi, vipengele muhimu vya lugha vinavyochunguzwa na mhakiki ni:
(a) Uteuzi wa msamiati au maneno
(b) Matumizi ya semi. Mfano, misemo, nahau, methali, misimu na mafumbo.
(c) Matumizi ya tamathali za semi. Mfano, tashbiha, sitiari, tashihisi na tafsida.
(d) Matumizi ya mbinu nyingine za kisanaa. Mfano, takriri, mdokezo na onomatopea.
(e) Matumizi ya takriri na ridhimu
(f) Matumizi ya usambamba
(g) Matumizi ya ishara na taswira mbalimbali (Jazanda)
4. Jina la kitabu na jalada lake
Mhakiki wa ushairi pia anatakiwa aangalie uhusiano uliopo kati ya jina la kitabu na maudhui yake na jalada na picha zilizopo kwenye jalada na maudhui yake.
UHAKIKI WA MAUDHUI
Maudhui ni neon linalotumiwa kujumuisha yaliyomo katika kazi ya fasihi. Katika ushairi uchambuzi wa maudhui, mhakiki anapaswa kuangalia:
(a) Dhamira kuu na ndogo
(b) Ujumbe wa mwandishi
(c) Falsafa ya mwandishi
(d) Msimamo wa mwandishi
(e) Mtazamo wa mwandishi
(f) Migogoro (Kama ipo)
(g) Kufaulu au kutofaulu kwa mshairi
UHAKIKI WA DIWANI YA FUNGATE YA UHURU
Jina la kitabu: FUNGATE YA UHURU
Jina la mwandishi: MOHAMED S. KHATIBU
Wachapishaji: DAR ES SALAAM UNIVERSITY PRESS (DUP)
Mwaka: 1988
Jina la mhakiki: MWALIMU MAJUMBENI
UTANGULIZI
Fungate ya Uhuru ni diwani inayoeleza kwa kina juu ya changamoto mbalimbali zinazokwamisha juhudi za ujenzi wa jamii mpya na bora hapa nchini.
Fungate maana yake ni kipindi cha siku saba baada ya harusi. Katika kipindi hiki maharusi hula na kustaree bila kufanyakazi. Maisha ya fungate ni ya gharama kubwa, maharusi hula wanachotaka na kwenda kutalii wanapotaka. Gharama za harusi na fungate huchangiwa na watu, wengi wao huwa ni watu wa kawaida tu. Watu ambao wakati mwingine hawajui hatima ya milo mitatu ndani ya jamii, watu waliobatizwa majina mengi ndani ya jamii, mafukara wao, makabwela, walalahoi, chokambaya na makapuku.
Maana ya Uhuru, ni hali ya kuwajitawala pasipo kuingiliwa na mtu au hali ya taifa moja kujitawala pasi kuingiliwa na taifa lingine.
Katika nchi nyingi za kiafrika viongozi wengi hupenda kusherehekea siku ya uhuru, katika siku hiyo bajeti kubwa hutengwa kwaajili ya kugharamikia shughuli nzima ya kumbukumbu hiyo.
Dhana hii inajitokeza vizuri katika diwani hii ya Fungate ya Uhuru. Wakati kumbukumbu za uhuru zikiendelea kuadhimisha karibu kila mwaka kwenye nchi nyingi za kiafrika wananchi waliowengi bado wamenasa katika tope zito la umasikini. Wanaonufaika na uhuru huu ni wachache. Vigogo walioshika nyazifa nyeti ndani ya serikali ndio wenye kutumbua fungate la uhuru, bado wanakula na kunywa kwa michango ya walalahoi.
UCHAMBUZI WA MAUDHUI
A: Dhamira
Dhamira kuu ndani ya diwani hii ni ujenzi wa jamii mpya
Dr. Khatibu anachora kwa ufundi mkubwa changamoto zinazokwamisha ujenzi wa jamii mpya na namna yakuzikabili changamoto hizo. Baadhi ya changamoto zinazokwamisha ujenzi wa jamii mpya nipamoja na unyonyaji, wizi na ufisadi, uonevu, dhuluma, uhaini, udanganyifu, unafiki, umasikini, uongozi mbaya na ukandamizwaji kwa watu wa tabaka la chini.
Katika nchi yetu itikadi ya ujenzi wa jamii mpya ilianza punde baada ya kutagazwa kwa Azimio la Arusha hadi mwaka 1988. Chini ya uongozi wa baba wa taifa, jamii ilijitahidi kujenda mazingira ya kuondoa ukandamizwaji na matabaka kwa wananchi.
Katika ujenzi wa jamii mpya, mwandishi wa diwani hii anasema bado kuna dhuluma, usaliti, unyonyaji na wizi wa mali za umma. Mfano shairi la Wingumwandishi anasema:
Nguvu,
Zimeangamia,
Angamia,
Mmetusaliti.
Katika shairi la Waja wa Mungu, katika shairi hili mwandishi anaonyesha jinsi watu wa tabaka la chini wanaoishi maisha ya ufukara wa hali ya juu na sababu ya ufukara wao ni usaliti uliotokana na kusalitiwa na viongozi wao hasa baada ya kupata madaraka. Ufukara uliojadiliwa hapa ni pamoja na ule wa kula kwa shida, kulala kwa shida, kuvaa kwa shida hawapati elimu na huduma nzuri za afya.
Pia kwenye shairi la Njama, mwandishi anaonesha jinsi viongozi wanavyotumia njama mbalimbali kulinyonya tabaka tawaliwa. Viongozi wanatumia njama mbalimbali ili kuhakikisha kuwa hakuna anayekwenda nje ya mipango yao uchu wa madaraka. Hapa mwandishi anasema:
Tongotongo,
Zimegubika mboni,
Umma umeshapofuka,
Nuru imeshaondoka,
Ni Njama.
Hayo ni baadhi ya matatizo yaliyochambuliwa na mwandishi wa diwani hii. Matatatizo haya na mengine lukuki ndio yanayokwamisha ujenzi wa jamii mpya.
1. umoja na mshikamano
Ili jamii yeyote ijengwe kwa umakini mwandishi anapendekeza kuwepo kwa umoja na mshikamano. Katika shairi la Unganeni, mwandishi anawataka wananchi wote wa Afrika kuungana ili kuendeleza mapambano ya kuleta haki na usawa: Anasema:
Wafanyakazi wa Afrika, tuunganeni,
Na wakulima kadhalika, tushikamaneni,
Makabwela mnaosumbuka, tukutaneni,
Tujiandae kwa mapambano, yalo marefu,
Ushindi ni wetu.
Mwandishi anawataka wanajamii kuungana na kushirikiana kwa lengo la kuwaondoa viongozi wanyonyaji madarakani.
2. Mapinduzi
Mapinduzi katika diwani hii yanaelezwa kama mageuzi. Kutokana na maoni ya mwandishi anaitaka jamii kufanya mageuzi hasa ya kiuongozi kwa kuwaondoa madarakani hata kwa kutumia nguvu viongozi wote wabadhilifu wa mali za umma. Maoni haya yameelezwa hasa katika shairi la Unganeni. Hapa mwandishi anasema:
Itikadi ya mapinduzi, ni sukani,
Nayo Tuifanyie kazi, vitendoni,
Kwa wanafiki viongozi, tutumieni,
Tusiajizi, kwa madhalimu, wanodhulumu,
Haraka tuanze
Mashairi mengine yanayojadili dhana hii ya mapinduzi ni pamoja na Utawala, siku Itafika, Nikizipata Bunduki, Mjamzito, Ni vita si Lelemama, Maendeleo ya Umma na Joka La Mdimu.
3. Ujasiri na kujitoa mhanga
Katika kuleta mapinduzi ya jamii mpya ni wazi mwandishi anatawaliwa na itikadi ya ujasiri na kujitoa mhanga kama moja ya funguo muhimu katika kufungulia mlango utakaoleta haki na usawa katika jamii ya kitanzania. Katika shairi la Gorila mwandishi anaitanabaisha wazi itikadi hii:
Gorila, Jasiri!
Wa Afrika, shujaa, mshupavu, umevinjari,
Mtutu shika, mevaa, ukakamavu, uko tayari.
Gorila, ruwaza, wa kizazi kipya.
Kushika mtutu na ukakamavu ni ishara ya jeshi lililovitani au linalojiandaa kuingia vitani na kuwa tayari ni wazi mwandishi anahamasisha watu wa kizazi kipya ambao bila shaka ni vijana kuwatayari kwa mapambano.
4. Uzalendo
Uzalendo ni kitendo cha kuipenda hasa nchi na hata kuwa tayari kuifia. Mwandishi anaihasa jamii kuwa wazalendo kwa nchi yao. Uzalendo umejidhihirisha wazi katika shairi la Nchi Yangu. Hapa mwandishi anasema:
Naipenda nchi yangu,
Naipenda, naipenda nitakufa naipenda,
Tailinda nguvu zangu, tailinda.........
Niwazi mwandishi anaamini kuwa tukiwa wazalendo kwa nchi yetu tutaweza kuijenga jamii yetu kirahisi sana.
5. Mapambano dhidi ya ukoloni mamboleo
Ukoloni mambo leo ni ile hali ya nchi kupata uhuru wa maneno na wakwenye makaratasi lakini nchi hiyo ikakosa uhuru wa kuamua mambo yao binafsi. Mwandishi wa diwani hii pia amelijadili suala hili la ukoloni mambo leo kwa kuitaka jamii yake kupambana na tabia hii ya nchi zilizoendelea kutawala nchi maskini kimaamuzi. Katika shairi la Ruya mwandishi anaeleza kuwa wazungu japokuwa wameondoka Afrika lakini wamerudi kwa mlango wa misaada na wanaitawala Afrika na kuinyonya zaidi ya walivyokuwa wanainyonya zamani.
Pia katika shairi la Kunguru mwandishi anawataja kunguru kwa lugha ya picha kama wakoloni. Kunguru hawa wameondoka Afrika na sasa wamerudi Afrika, wanaleta bidhaa na kuziuza huku. Bidhaa zao zinasababisha maradhi ya hali ya juu kwa waafrika.
6. Mapambano dhidi ya ubadhilifu wa mali za umma
Mwandishi ametaja bila kificho maeneo ambayo ubadhilifu unafanyika, baadhi ya maeneo hayo ni pamoja na makanisani, miskitini, Ikulu na bomani. Katika shairi la Wizi, mwandishi anasema:
Wizi umo:
Kanisani,
Msikitini,
Hekaluni,
Wanyang’anywao ni waumini
Wezi na wabadhilifu wengine wa mali za umma waliojadiliwa na mwandishi ni wazungu wanaorudi Afrika kwa mlango wa ukoloni mambo leo ambapo wamejadiliwa sana katika shairi la Kunguru na Joka la Mdimu.
Vilevile katika shairi la Naona mwandishi anaweka wazi mateso wanayopata wakulima wanaonyonywa na machuuzi kwa kununua mazao yao kwa bei ya chini sana. Katika shairi hili la Naona, mwandishi anasema:
Naona
Ni fukara wakulima,
Wamepigwa alitima
Kwa wengine ni neema
Kwao wao ni na kama
Wanakosa haki!
Kwa ujuma mwandishi anaihasa jamii kuwa tayari kupambana na ubadhilivu na unyonyaji wa mali za umma wa namna yeyote ile.
7. Kupiga vita uongozi mbaya
Katika kujadili suala hili la uongozi mbaya mwandishi anakemea tabia ya baadhi ya viongozi kuwa na tabia ya ukasuku. Mwandishi anaifananisha tabia hii ya ukasuku na ugonjwa hatari unaohitaji tiba. Mwandishi anasema ugonjwa huu hudumaza sana akili kwa kuwa kiongozi huwa hanamuda wa kufikiri bali huchukua maneno ya mabepari na wanyonyaji kama yalivyo na kuwaeleza wananchi. Mwandishi anayasema haya katika shairi lake la Ukasuku. Katika moja ya mabeti ya shairi hili anasema:
Kupea kwa ukasuku,
Rais huhubiri
Wabune hukariri
Wasomi huhariri
Na Taifa husimama.
Mwandishi pia hakuacha kuzungumzia tabia ya viongozi wengi wa kiafrika, kuwa ni viongozi wenye chembechembe za ubepari, udikteta, wakabila, wabadhilifu wa mali za umma na wapenda rushwa.
8. Mapenzi
Mwandishi wa diwani hii ameichora dhana ya mapenzi kwenye pande mbili.
Kwanza, mapenzi ya mtu kwa nchi yake (uzalendo) na mapenzi ya mtu kwa mtu mwingine.
Katika kujadili mapenzi ya mtu kwa nchi yake mwandishi andika shairi la Nchi Yangu. Katika kujadili mapenzi ya mtu na mtu mwandishi ameandaa mashairi kama vile Wewe peke yako, nia yangu sigeuzi, uwapi uzuri wako, ua si ruwaza njema na kantu sauti ya kiza.
B. UJUMBE
(a) Uongozi mbaya, rushwa na ubadhilifu wa mali za umma ni baadhi ya vikwazo vinavyokwamisha
ujenzi wa jamii mpya.
(b) umoja na mshikamano ni funguo katika kufungua lango litakalo ruhusu mamia ya watu kushiriki
katika ujenzi wa jamii mpya.
(c) Ili tujenge jamii mpya ni lazima tuwe na ujasiri wa kujitoa mhanga, tuwe wazalendo na nchi yetu na
tufanye mapinduzi katika jamii.
(d) Ukoloni mamboleo ni kikwazo cha ujenzi wa jamii mpya hapa nchini.
(e) Mapenzi ya kweli ni yale yasiyojali fedha au hali ya mtu.
C. FALSAFA
Mwandishi anatetea waziwazi itikadi ya ujamaa yenye kuleta haki na uswa kwa kila mtu. Pia kwa lugha ya ukali analaani dhuluma, wizi na ubadhilifu wa mali za umma na anatoa suluhisho la matatizo haya.
D. MSIMAMO
Mwandishi anamsimamo wa kimapinduzi kwakuwa ameyafunua matatizo mbalimbali yanayozikumba jamii zetu na mbinu za kuondokana na matatizo hayo. Miongoni mwa matatizo hayo ni uongozi mbaya, wizi wa mali ya umma, rushwa na dhuluma.
FANI
(a) Muundo
Kwenye diwani hii mwandishi ametumia muundo changamano. Kuna muundo wa tathnia (mistari 2) mfano shairi la Mjamzito, muundo wa tathlitha (mistari mitatu 3) mfano shairi la Fungate na Nataka Kusema. Muundo wa tarbia (mistari mine 4) mfano shairi la Nahodha Mtwesi, Gorila, Afrika na Kunguru. Pia ametumia muundo wa sabilia au takhmisa (mistari mitano 5), mfano shairi la Utawala, Ladha ya Maji Katani, Joka la Mdimu na Mkata.
(b) Mtindo
Mtindo changamani pia umejitokeza ndani ya diwani hii kwani kuna mashairi yanayofuata kanuni za ushairi wa kimapokeo nay ale yanayofuata kanuni za mashairi ya kisasa. Huu ni shaidi tosha kwamba mwandishi Dr. Khatibu ni mfuasi wa aina zote mbili za mashairi.
(c) Matumizi ya Lugha
Katika matumizi ya lugha, mwandishi ametumia lugha sanifu yenye lahaja ya Kiunguja. Lugha hii imejaa misemo mbalimbali, tamathali za semi na taswira.
Misemo
Misemo iliyotumiwa katika diwani hii ni pamoja na:
Mfano:
i. Joka la mdimu (uk. 24)
ii. Utakiona cha mtema kunu (uk. 31)
iii. Paka shume (uk.20)
Tamathali za semi
Mfano:
Tashibiha
Katika shairi la Mkata (uk.15), tashibia zifuatazo zimejitokeza:
i. Kitandani nilalapo kama dema la samaki....
ii. Mbu ndani kama ndege wa vita....
iii. Matopeni hujazika mithili nimo karoni
Sitiari
Katika shairi la Uwapi Uzuri Wako (uk. 35), sitiari zifuatazo zimejitokeza:
i. Sasa ni chano cha mji, watu wajichanyatiya
ii. Bao la mkahawani, kila mtu akaliya
iii. Sasa jamvi la wageni, wajapo huwapokeya
Kejeli
Kejeli zimejitokeza kama ifuatavyo:
i. Shairi la Fungate (uk. 1) linakejeli. Neon fungate ni kejeli kwa baadhi ya viongozi ambao wanaendelea kuinyonya jamii tangu enzi na enzi. Ingawa kodi zinakusanywa kwa watu wa hali ya chini kama ilivyo kwenye michango ya harusi lakini wao wanazitumia katika kujinufaisha wao na familia zao.
ii. Shairi la Kantu Sauti ya Kiza, mwandishi anawatumia nyuki kukejeli baadhi ya tabia chafu za watu.
Tafsida
Mwandishi ametumia mbinu hii ya kupunguza ukali wa maneno. Mfano kwenye shairi la Paka Shume, linamwelezea Paka anayemendea vitu vya watu na bila shaka paka huyo ni mtu mwenye kutaka kutapeli au kupora vitu vya watu.
Pia tafsida imetumika katika kuelezea maana ya fungate kwenye shairi la Fungate, linaeleza namna viongozi wanavyoendelea kufuja kodi, mapato na mali za umma bila huruma.
Jina la Kitabu
Jina la diwani hii ni Fungate ya Uhuru, jinaili linasadifu kwa uwazi mambo yaliyojadiliwa ndani. Mwandishi kwa kutumia shairi la Fungate na mashairi mengine ameonyesha, kuonya na kukemea tabia ya baadhi ya viongozi waumma kujilimbikizia mali na kuwaacha wananchi wengi wakiumia na wananchi hao kubebeshwa adhabu za ubadhilifu wao.
Kufaulu na kutofaulu kwa mwandishi
Kufaulu, kimaudhui
Mwandishi amefaulu kimaudhui kwani amejadili matatizo sugu yanayoikabili jamii yetu yakiwemo masuala ya rushwa, tabia ya viongozi kufanya kazi kwa mazoea, mapenzi ya ulaghai na athari za ukoloni mamboleo. Pia mwandishi amejaribu kutoa baadhi ya suluhisho kwa matatizo kadhaa ikiwemo kuwahamasisha watu kuwa na umoja na mshikamano katika kutetea haki zao na katika ujenzi wa jamii mpya.
Kufaulu, kifani
Kwaupande wa fani mwandishi wa diwani hii amefaulu kutumia aina zote mbili za mashiri yaani mashairi ya kimapokeo na mashairi ya kisasa. Pia ametumia lugha rahisi inayoeleweka kwa msomaji.
Kutofaulu kwa mwandishi
Kutofaulu , kimaudhui
Mwandishi amejadili maudhui yake kwa kujikita zaidi kwenye siasa, bilashaka kwakuwa na yeye ni mwanasiasa tunaweza kusema ameathiriwa sana na mwenendo wa siasa za nchi yetu na wakati mwingine anaweza kufanya hivi kwa chuki za kuwachukia wanasiasa wenzake walio madarakani.
Kutofaulu, kifani
Mwandishi ametumia taswira na tafsida ya hali ya juu, uhakiki huu unaamini kuwa amefanya hivi
ili kukwepe mkono wa sheria kwa kuwasema viongozi
UHAKIKI WA RIWAYA YA ROSA MISTIKA
Jina la mhakiki: Henry Mapunda
Riwaya ya Rosa Mistika iliyoandikwa na E. Kezilahabi mwaka 1971, ni moja kati ya riwaya zinazotumika katika utafiti huu kama data ya msingi. Kwa kiasi kikubwa, masimulizi ya riwaya hii yamejikita katika kueleza maisha ya mhusika, Rosa, tangu akiwa mtoto mpaka kifo chake na maisha baada ya kifo. Masimulizi yamehusisha maisha ya wahusika wengine ambao kimsingi ndio ambao wamemjenga mhusika mkuu Rosa. Hivyo, katika utafiti huu, wahusika, Regina ambaye ni mama yake Rosa, Zakaria baba yake Rosa, Flora mdogo wake Rosa, Charles mpenzi wa Rosa na Padre anayetaka kuokoa nafsi ya Rosa, wamechambuliwa.
Kwanza tunaona wasifu wa Rosa akiwa mtoto mdogo. Mwandishi anamchora Rosa kama kifungua mimba cha familia ya Zakaria na Regina kati ya wasichana watano na mvulana mmoja. Rosa akiwa mtoto mdogo anaonekana ni msichana mrembo na mwenye aibu, mrefu kiasi, mnyenyekevu na mkakamavu.
Rosa anakua chini ya malezi ya baba yake aliye na mtazamo hasi juu ya wanawake. Zakaria akiwa kama mwalimu aliyeachishwa kazi kwa sababu ya ulevi, anamtesa mke wake kwa kumpiga na kutomjali pamoja na familia yake kwa sababu ya kuzaa watoto wa kike wengi. Kama riwaya isemavyo (uk.3):
…..Regina tangu aolewe hakuwa na raha: alikuwa akisumbuliwa na kuteswa na mumewe kwa kosa lisilo lake. Katika kijiji chote cha Namagondo hapakuwa na mwanamke aliyekua akipigwa karibia kila juma kama Regina.
Zakaria alizoea kumlaumu Regina kwa kuzaa watoto wa kike na kudai amemletea matatizo katika nyumba yake. Ingawa Regina alipigwa na mumewe kwa lakini hakutaka kuachana na mumewe sababu ya mategemeo yake juu ya maisha ya baadae ya watoto wake. Ndiyo maana katika ukurasa wa 3 twaambiwa kuwa mawazo yake yalikua juu ya furaha ya watoto wake katika maisha yao ya baadae.
Kutokana na kuwa na watoto wa kike wengi katika nyumba yake, Zakaria anatumia ukali kama silaha ya kuwalinda dhidi ya wanaume. Ingawa Zakaria anawapenda watoto wake lakini mfumo wa kijamii unamkandamiza. Hajui lipi ni jema kwake kutenda kama mwanaume katika familia iliyojaa wanawake. Mawazo na imani ya wanajamii ni kwamba ili familia iheshimike ni lazima kuwepo na mtoto wa kiume. Kukiwa na mtoto wa kiume hata ndege na wanyama wanaiheshimu na kuiogopa. Lakini nyumba iliyojaa wanawake haiheshimiki. Hili tunaliona katika (uk 15-16):
…….Vilikuwa kumi, sasa vimebaki vitatu!” Flora alishangaa. Rosa alikaa chini tena kunyolewa. Muda si mrefu mwewe alirudi. Safari hii Honorata alikuwa wa kwanza kumwona.
“Swa! Swa! Swa!” alitupa mikono juu, “swa!”Mwewe alikuwa amekwisha chukua kifaranga kingine. Zamu hii hakwenda mbali. Alitua juu ya mti karibu na mji. Wasichana walianza kumtupia mawe lakini hayakumfikia. Mwewe alikula kifaranga bila ya kujali.Alipomaliza aliruka kwa raha ya shibe. Vifaranga vilibaki viwili. Ilionekana kana kwamba hata mwewe alifahamu kwamba huu ulikua mji wa wanawake.
Mtazamo kama huu ndio unaomkandamiza Zakaria, anashindwa kutafuta njia iliyo sahihi katika kuwalea binti zake. Hajui jinsi ya kukabiliana na Rosa aliye katika hatua muhimu katika makuzi yake. Tunaona Zakaria hana muda wa kuzungumza na binti zake juu ya hisia zao. Pia hawaelezi ni nini wanakabiliana nacho katika hatua hiyo ya makuzi. Wala hawajulishi nini wafanye ili kuyazima matamanio yao.Tunaona jinsi anavyompiga Rosa akiwa nusu-uchi sababu ametumiwa barua na pesa toka kwa mwanaume. Mwanaume mwenyewe aliyetuma barua hiyo ni Charles, kijana aliyekuwa rafiki yake Rosa kwa muda mrefu na wazazi wote walijua juu ya urafiki huo. Urafiki wao ulikuwa umeunganishwa zaidi na masomo. Rosa na Charles wanakatazwa kuwasiliana tena baada ya Zakaria kujua juu ya barua aliyopokea Rosa. Tunaona baada ya kitendo hicho Zakaria anajisifia na kujitakia amani, “amani Duniani kwa watu wenye malezi mema”.
Tunaona mtazamo wa mwandishi kuhusu malezi ya namna hii, malezi ya baba kwa binti yake, hususani katika kipindi cha makuzi ya hatua ya kingono (uk.9):
Hivyo ndivyo Rosa alivyolelewa, hivi ndivyo alivyotunzwa, hivi ndivyo alivyochungwa na baba yake. Tangu siku hiyo alikoma kutembea na mvulana yeyote. ….. hakufahamu kwamba Rosa alikuwa katika rika baya, na kwamba ukali ulikuwa haufai; hakufahamu kwamba mabinti wanahitaji uhuru fulani kutoka kwa baba zao; hakufahamu kwamba kumpiga binti yake alikuwa anaingilia utawala usio wake, na kwamba katika masuala ya ndoa yeye alifaa kidogo sana, na hakufahamu kwamba Rosa alihitaji kuwafahamu wanaume. Kwa hiyo kutokana na malezi ya namna hii, Rosa alianza kuwatazama wanaume kama watu asiopaswa kuandamana nao na hata kuzungumza nao. Alianza kufikiri kwamba alitakiwa kujitosheleza.
Kwa upande wa mama yake Rosa, yeye alitumia muda wake mwingi wa kuwafundisha binti zake namna ya kuenenda vizuri kama wanawake. Alitumia muda wa usiku wakiwa wanakula chakula cha usiku kuwaonya na kuwafundisha jinsi ya kuishi na mambo gani ya kuepukana nayo na mambo ya kuyaacha. Alifanya hivyo kwa kila mtoto kulingana na umri wake.
Rosa alikuwa amevunja ungo na amefaulu kwenda kusoma mbali na nyumbani. Jambo kubwa alilousiwa na mama yake ni kutowasahau wazazi wake na kukaa mbali na wanaume.
Mwanangu, wewe sasa umeshakua mtu mzima. Karibu utakwenda huko ng’ambo Usukumani. Usitusahau sisi wazee wako - tuandikie barua mara kwa mara. Jambo moja ningependa hasa kukuhadharisha: wavulana wakorofi. Huenda wakakutaka kimapenzi, nia yao ikiwa tu kukupa mimba itakayokukatisha masomo yako. Daima wakwepe hao. Na ikiwa utakuwa mpumbavu ukapata mimba usiitoe. Tunasikia kwamba siku hizi wasichana wengi wanaosoma wanafanya hivyo ili wapate kuendelea na masomo yao. Wanapenda masomo zaidi kuliko watoto.
Mawazo ya Regina sio mabaya. Jambo kubwa analopigania ni kutafuta maisha bora kwa ajili ya binti zake wakiwa watu wazima, na kujaribu kuwapatia ukombozi ambao yeye hakuupata. Lakini Regina anashindwa katika kumalizia maonyo, anamuonyesha Rosa ubaya wa wanaume tu hamuambii inakuaje mpaka ndoa inatokea. Hatujui kwa nini haongelei juu ya furaha inayoweza kupatikana kati ya mwanamke na mwanaume isiyoleta maumivu kwa upande wowote na bila kuwaumiza watu wengine. Inawezekana Regina haoni kama kuna umuhimu wa uhusiano kati ya mwanaume na mwanamke kwa sababu ya mateso anayoyapata toka kwa mume wake Zakaria. Kutokuwa wazi kwa Regina juu ya maisha ya mapenzi kwa binti zake kunasababisha wabaki katika kitendawili, hawajui uhakika wa mambo hayo ni upi, wakizingatia jinsi wanavyojisikia na jinsi ambavyo watu wanaowazunguka wanafanya.
Regina na mumewe Zakaria, kama wazazi wengine, wana wasiwasi na maisha ya baadae ya watoto wao hususani baada ya kufikia kipindi cha kubalehe. Hawajui jinsi ya kukabiliana na hali inayowakumba binti zao. Tofauti na jamii zingine za Watanzania wanaopeleka watoto katika umri huu jandoni au unyagoni, Kama Senkoro (1997:100) anavyosema:
Mpito toka utotoni mpaka utu uzima ni kikwazo au wakati mwingine tatizo kwa wazazi walio wengi katika jamii yetu. Muunganiko sawia wa kibaiolojia au mabadiliko ya kihomoni za kisaikolojia na majukumu ya kijamii katika balehe inatengeneza tabia tofauti tofauti ambazo sio lazima zilingane na nini wazazi au watu wazima katika jamii kwa ujumla wangetaka. Aina hii ya tatizo linashughulikiwa na jamii nyingi za Kiafrika kwa njia ya kufundwa katika jando na unyago.
Kulingana na jinsi mwandishi alivyoichora jamii ya Wakerewe, watoto wanapokua hawapewi mafunzo yoyote yanayohusu mambo watakayokabiliana nayo watakapokuwa watu wazima. Inawezekana kutokuwepo kwa mafunzo haya ndiko kunakoleta matatizo, kwani Regina anashindwa kuwafundisha binti zake kwa mapana zaidi hususani kuhusu mambo yanayohusu mahusiano; mafunzo ambayo wangeyapata kama kungekuwapo na jando na unyago. Kwa kawaida katika jamii nyingi za Kiafrika, mambo haya hayafundishwi na wazazi; badala yake mashangazi, makungwi au somo ndio wanaohusika kuwafundisha mabinti kuhusu masuala ya mahusiano wanapovunja ungo.