KISWAHILI -2-MADA 1 : FASIHI KWA UJUMLA
MADA NDOGO -1; NADHARIA
YA FASIHI
Nadharia ni Imani au kanuni
zinazofuatwa na watu Fulani au jamii katika kushughulikia jambo Fulani mahsusi.
Nadharia za fasihi ni muongozo au
kanuni zinazofuatwa na wataalamu (wanazuoni) mbalimbali katika kuteua fasili/maana
halisi ya fasihi.
Fasihi ni nini?
Wataalamu mbalimbali wamefasili/Maana ya dhana ya fasihi,
maana hizo ni kama zifuatazo:-
1. Fasihi ni kioo cha jamii (maisha),Kwa
maana kwamba mtu anaweza akajitazama akaona taswira yake na akajirekebisha .
Fasihi hii ina udhaifu kwani kioo hakiwezi kumweleza mtu jambo la kufanya ili hali yake iwe bora zaidi
. Pia si sehemu zote takazojiona kwenye kioo(F.Mkwera , 1978)
2.
Fasihi ni hisi,Fasili ina maana kuwa
lazima pawe na mguso fulani wa wahusika ndipo mtu aweze kuandika na kueleza
jambo fulani,’Sengo na kiango Wanasema “hisi
ni kama kuona njaa, baridi, joto, uchovu pengine kuumwa. Hapa swali la
kujiuliza ni kwamba, je fasihi ina maana moja kati ya hiyo? Uamuzi wa kutenda
jambo huja wakati umeguswa?. Je hizo hisia ziko wapi? Je mtu ambaye
haguswi sana moyoni hawezi kuwa mwanafasihi
mashuhuri? Je mwanamuziki ambaye huusifu
uzuri wa mwanamke anaguswa moyoni? Je mwandishi kama Shaban Robert, E. Kazilahabi wameguswa mara ngapi? Vile vile
kivipi waguswe Zaidi ya wengine? (Sengo
na Kiango) hivyo bado fasili hii ina udhaifu
3. Fasihi
ni mwamvuli wa mtu na jamii na utu na maisha ya hadhi na taadhima.Fasihi hii ina maana kwamba mwamvuli humkinga mtu
katika mvua na jua na fasihi huhifadhi na kukinga amali za jamii zisiharibike
maana hii ni nzuri kwani inasisitiza utunzaji wa kile kizuri kwa maana kuwa
jamii inachambua kuwa makini na kuona amali za jamii zinazohifadhiwa. Lakini
swali la kujiuliza ni kwamba jamii
itasaidiwa?
Jamii haitulii kama maji katika mtungi bali hubadilika mara kwa mara kutokana na
nguvu za migongano, hivyo kitu kipya huzaliwa na cha zamani hufa kwasababu
jamii haitulii, hivyo hakuna haja ya kuhifadhi amali za jamii chini ya
mwamvuli. Zipo mila na desturi zilizohifadhiwa na makabila mengi ambazo hazina
nafasi leo. Hali ya mabadiliko ya jamii kutokana na siasa, utawala, uchumi,
elimu, sayansi na teknolojia vyote hivi katika maendeleo vitatoboa mwamvuli na
kuziharibu amali zilizohifadhiwa (Sengo na Kiango 1973)
4.
Fasihi ni sanaa ya uchambuzi wa lugha yoyote
kadri inavyosemwa,inavyoandikwa na kusomwa,Hii ni kweli kuwa fasihi
lazima itumie lugha kwani lugha ndicho chombo muhimu kitumiwacho na fasihi na
si fasihi tu bali taaluma zote hutumia
lugha.Udhaifu wa fasili hii ni kwamba maana hii imejikita katika uchambuzi wa
Lugha kana kwamba hakuna vipengele vingine vinavyochambuliwa katika fasihi
zaidi ya lugha na hii ni sawa na kusema umeme ni waya wa shaba kwa vile umeme umepita
kwenye waya huo.Na hii ni si kweli kwani Hisabati,fizikia au historia si fasihi
ingawa hutumia lugha.
5.Fasihi ni kielelezo cha hisia
za mwandishi juu ya mambo yanayomwathiri yeye,kikundi au jamii nzima anamoishi
na kwamba lengo lake ni kustarehesha au kufunza wasomaji.Fasili(maana)
hii ni nzuri kwa ujumla lakini mapungufu yake ni kwamba imemuwekea mwandishi
kama chanzo pekee cha uumbaji wa Sanaa na hasa akili yake pia maana hii
imetokana na falsafa ya kidhaanifu kwa
kuhusisha uchambuzi wa mambo katika fikra bila
kutazama hali halisi ya maisha ya watu na vitu.
6. Fasihi ni chombo cha utetezi wa maslahi ya
tabaka moja au jingine na kwamba mwandishi ni mtumishi wake anayejijua au
asiyejijua atake asitake mwandishi huyu analengo au dhamira fulani anayotaka
kuionesha.Wasomaji wanaweza kuyakubali au kuyakataa maudhui ya kazi
yake na pengine jamii kufuatana na msimamo juu ya itikadi ya siasa (napengine
amali za jamii) inayotawala kwa kipindi kile
na jinsi mwandishi anavyooanisha maandishi yake na itikadi hiyo.Fasili
au maana hii ni nzuri sana kwani kwa kifupi ni kwamba fasihi ni mojawapo ya silaha
nyingi zinazotumiwa na tabaka moja kutetea maslahi yake katika mapambano ya
kudumu dhidi ya matabaka mengine.
Hitimisho kwa ufupi fasihi ni taaluma inayotumia Sanaa
maalumu ya lugha ili kufikisha ujumbe kwa jamii inayohusika.Fasihi hutueleza
uzuri wa maandishi au mazungumzo ambayo huonekana katika mashairi ,historia za
maisha ya watu ,tenzi,hadithi za kusisimua na insha mbali mbali.
DHIMA YA MWANAFASIHI KATIKA JAMII
Maana ya mwanafasihi/mtunzi wa
kazi ya fasihi
Ni mtu yeyote anayejishughulisha
na uandishi au utungaji wa kazi za fasihi yaani fasihi andishi na fasihi
simulizi.
DHIMA ZA MWANAFASIHI
1. .Kuelimisha jamii,Katika kuelimisha jamii mwanafasihi ;
(a)Huchambua
na kuchochea umma kuwafumbua macho,hufichua wazo au uchafu uliomo
katika jamii,wagandamizaji hufichuliwa na wagandamizwao hupewa muongozo sahihi
ili waitambue hali yao dhaifu.Mfano”Duka la Kaya”imechambua na kuchochea jamii
ili iweze kupambana na hali mbaya ya maisha.
(b).Kupiga vita kwa hali na mali mazingira yote ya ujinga,maradhi,njaa
na umaskini,Mfano mwandishi wa tamthiliya ya Hawala ya fedha
anapambana na maovu kama vile ujinga na uvivu na Ngoswe Penzi Kitovu cha Uzembe
anajadili na kupiga vita uzembe na
mengineyo.
(c).Kukosoa jamii,Mwanafasihi anaikosoa jamii katika vipengele
mbalimbali vya maisha.Mfano riwaya ya “ Vuta n’kuvute”inakosoa mila na desturi
zilizopitwa na wakati “Raha karaha na Mashairi ya Chekacheka”mwandishi wa
diwani hizi anaikosoa jamii ya Tanzania kwa mapana kama vile Uongozi
mbaya,kukithiri kwa rushwa n.k.
(d).Kutia hamasa na kumfanya mtu asikate tamaa,Mfano S.Kandoro
anaeleza hamasa ya wananchi waliokuwa wameungana kama “Siafu ili kumtoa nyoka
pangoni katika shairi liitwalo ‘Siafu wamekazana’’.Mwandishi kwa hamasa
amewaita waafrika njooni “au” kwetu ni kwa nini’.Hivyo ni wazi kuwa kazi hizi
zinajitahidi kuendeleza mapambano dhidi ya ukoloni mambo leo.
(e)Mwandisi anadhima kujenga misingi na fikra za usawa na demokrasia
miongoni mwa umma wa wakulima na wafanyakazi,Mwanafasihi huyu
huwatukuza wakulima na wafanyakazi pamoja na amali zao.
(f) Mwanafasihi hueneza mawazo na falsafa za jamii,Kwa mfano
katika shairi na ngonjera za Mathias Mnyapala ametangaza sana siasa ya ujamaa
na kujitegemea kwa kutumia ngonjera za UKUTA 1 & 2 vile vile riwaya kama
vile mfaa na utu,njozi za usiku,ndoto yandaria ,jero si kitu n.k zimetangaza
sana siasa ya ujamaa na kujitegemea hapa nchini Shaban Robert aliwahi kueneza
falsafa juu ya kweli kwa kiasi kikubwa katika mashairi yake.
(g)Mwanafasihi hutoa mwongozo kwa kuikomboa jamii kutoka fikra mbovu za
kugandamizwa,kunyonywa na kuonewa na kujikomboa ili iweze kupata haki na usawa,Mfano
Riwaya ya kiimbila “Ubeberu Utashindwa” na tamthiliya ya E.Mbogo “Tone la
Mwisho” G Husseni “Kinjekitile”
2.Kuburudisha,zipo kazi mbalimbali za fasihi
zinazoburudisha.Msomaji au msikilizaji wa fasihi huburudisha yaani husisimsha
mwili na akili na huvutiwa kihisia na kazi ya fasihi anayoisoma au
kusikiliza.Tabia ya msomaji au msikilizaji huweza kujengwa kutokana na mafunzo
na mifano bora ya matendo ya kuigwa anayoyapata katika fasihi.
3.Kuhifadhi na kurithisha amali za jamii,Amali za jamii ni
pamoja na mila na desturi mtindo wa maisha,Imani, historia jiografia,visasili
na visakale ni urithi wa maarifa ya kijadi kwa mfano tiba, sayansi ya
kilimo,mbinu za uwindaji,ufundi wa aina zote n.k.Amali hizo huweza kuhifadhiwa
na kuendelezwa na mwanafasihi na hivyo kurithishwa kwa vizazi vijavyo.
Kwa mfano tamthiliya ya Kinjikitile inahifadhi mengi kuhusu
hali ya maisha wakati wa ukoloni wa kidachi,Kurwa na Doto (1969) ni
riwaya yenye kuhifadhi japo kwa kejeli,mila,desturi na itikadi za jadi za
waunguja,Riwaya ya Bwana Mnyombokero na Bibi Bugonoka;Ntuhanalwo na
Buliwali iliyoandikwa na Anicet
Kitereza imehifadhi mila,Imani,mtindo wa maisha,ufundi na taaluma mbalimbali za
jadi za wakerewe mengi yaliyoeleza humo siku hizi hayapatikani popote isipokuwa
katika riwaya hiyo, vile vile Mzishi wa Baba ana Radhi (1967)
kinaeleza mila na desturi za wapangwa.
Watunzi hasa nyimbo na visasili
hukoleza pia shughuli za kijadi za kiutamaduni kwa mfano
Ibada,matambiko,sherehe,katika shughuli za aina hiyo nyimbo licha ya kuwa
kiburudisho hubeba ujumbe wenye kuhusiana na tukio hilo.
4.Kudumisha na kuendeleza lugha,Kwa kadri lugha inavyotumiwa na
kufinyangwa na watunzi ndivyo inavyokuwa na kupevuka.Maneno mengi yatumiwayo
leo katika lugha mbalimbali yalibuniwa na kuenezwa na watunzi wa
mashairi,riwaya,nyimbo na tamthiliya katika Kiswahili.Mifano mizuri ni maneno
mengi yahusuyo Sanaa ya ushairi(vina, mizani, beti, mishororo, miwala,
tathlitha, takhimisa, tarbia n.k)
Katika jadi ya ushairi wa kiswahili inadaiwa kuwa
ushairi ulikua ni ghala ya maneno.Washairi walitumia maneno magumu au
yasiyokuwa ya kawaida makusudi ili kuyahifadhi ysipote.katika tamaduni nyingine
kazi hiyo hufanywa na kamusi pamoja na vitabu viitwavyo Hazina ya maneno kwa kuwa
waswahili hawakuwa na kamusi kazi ya kuhifadhi maneno ilifanywa na ushairi.
DHIMA ZA MHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI
Uhakiki ni kazi au kitendo cha kuchambua au kufafanua kazi
ya fasihi, kuweza kupata maadili na ujumbe uliomo katika maandishi ya mwandishi asilia.
AU ni sayansi maalumu ya
kuchambua na kuona ubora wa kazi hizo kwa kutumia vipengele mbalimbali vya fani
na maudhui na kuangalia uwiano na uhusiano ama kuathiriana kwake. Uhakiki ni
elimu na ujuzi wa kuipembua kazi ya sanaa inayohusika kimaudhui na kifani.
Uhakiki ni daraja ya juu ya maelezo ya kisanii yenye
kuwalenga watu wa aina tatu:- wasomaji wa
kawaida walio nyumbani na shuleni, waandishi asilia wa kazi za sanaa na
wahakiki.Msomaji hupata mwongozo wa namna bora zaidi ya kumwezesha
kuifahamu kazi ya sanaa kutokana na viwango tofauti vya uhakiki juu ya kazi za
sanaa.
Mhakiki ni nani?
Mhakiki ni mchambuzi na mfafanuzi wa maandishi ya kisanaa
hasa yale ya kifasihi. Ni jicho la jamii kwa vile anagundua mazuri yaliyomo
katika kazi ya fasihi na pia ndiye anayeona hatari ya maandishi hayo kwa jamii.
Mhakiki ni bingwa wa kusoma na kuchambua maudhui, maadili na ujumbe uliomo
katika maandishi ya fasihi.
Ni mtu mhakiki anajihusisha na maandishi ya waandishi asilia na hungalia kwa jinsi
gani mwandishi anawakilisha hali halisi ya jumuiya ya watu. Kwa upande
mwingine, mhakiki anashughulikia uwanja wa fasihi andishi pamoja na ule wa
fasihi simulizi.
Sifa za mhakiki
·
Mhakiki
anatakiwa ajue historia na mazingira yaliyomkuza mwandishi.Mhakiki ili
aweze kuifanya kazi yake vizuri anapaswa
aelewe vema historia ya mwandishi na jamii yake inayohusika. Aelewe asili ya
mwandishi, historia yake na utamadumi wake kwa ujumla. Kutokana na hali hii,
mhakiki anaweza kuelewa kama mwandishi amefanikiwa kueleza ukweli wa maisha ya
watu, yaani jamii inayohusika.
·
Mhakiki
anatakiwa kuelewa historia na siasa ya jamii inayohusika.Hii itamwezesha
kuyaelewa matatizo ya jamii hiyo. Mhakiki lazima aifahamu barabara jamii ambayo
mwandishi aliandikia juu yake ili aweze kuandika uhakiki imara, ama sivyo
atakwama na kuandika uhakiki dhaifu. Mhakiki anapaswa kuelewa historia ya watu
ambao maandishi hayo yanawahusu, bila kuifahamu historia yao, itakuwa vigumu
kwake kueleza bayana baadhi ya mambo ambayo mwandishi aliandika na kwa nini
aliandika hivyo. Uhakiki wake ukisomwa na watu wanaoishi katika jamii hiyo si
ajabu kusema yeye si mhakiki. Mhakiki huangalia jinsi gani mwandishi
alivyoiwakilisha hali halisi ya jumuiya na historia ya watu hao.
·
Mhakiki awe amesoma kazi mbali mbali za fasihi na
siyo ile tu anayoifanyia uhakiki. Hii itamsaidia kuwa na ujuzi zaidi katika
uwanja wa uhakiki.
·
Mhakiki anatakiwa asome tahakiki za wahakiki
wengine katika uwanja wa fasihi na hata nje ya jamii yake ili kupata upanuzi
zaidi katika kazi ya uhakiki. Hii itamsaidia kutoa uhakiki bora zaidi, kwani
atakuwa amejifunza yale yaliyo mazuri na kuepuka makosa waliofanya wengine.
·
Mhakiki lazima awe na akili pevu sana ili aweze
kung’amua mambo na akishayang’amua ayaandike kwa lugha rahisi ili mawazo yake
yasomeke na kila mtu kwa urahisi, yaani atumie lugha ambayo itawatumikia
wasomaji wake.
·
Mhakiki lazima ajiendeleze katika taaluma mbali
mbali ili aweze kuwa na mawazo mengi ambayo yatamsaidia kuhakiki maandishi
mbali mbali. Mhakiki hodari huichonga jamii yake kimawazo. Huiimarisha
isitetereshwe au kupofushwa na waandishi wapotoshaji.
·
Mhakiki anapaswa kuwa na uwezo wa kuchambua
mambo kisayansi bila kuonyesha hisia za wasomaji. Asiwe na majivuno na awaheshimu anaowahakiki
na anaotaka wasome uhakiki wake. Asichukie au kusifia tu kazi za
waandishi kwa sababu zake binafsi bila kueleza ukweli wa kazi hiyo. Mhakiki ni
rafiki wa mwandishi na wasomaji . Kwa hiyo, mhakiki ni lazima awe fundi katika
kutoa hoja zake na lazima ziwe zinagonga, zenye kuibua udadisi na kuathiri.
·
Mhakiki anapaswa asiwe mtu wa kuyumbishwa na
maandishi au maneno ya wahakiki au watu wengine. Tunatarajia aseme kweli kuhusu
kazi hiyo. Uhusiano baina ya mhakiki na mwandishi usiathiri uhakiki wake.
TAHAKIKI
NI NINI?
Ni kitabu kinachotolewa na mhakiki kinachambua vitabu mbali
mbali vya maandishi asilia. Tahakiki hutoa uchambuzi na uhakiki wa vitabu vya
hadithi/tamthiliya/ushairi kwa kuzingatia vipengele vya fani na maudhui. Mfano
wa tahakiki ni kama vile:- Senkoro(1988).
Ushairi: Nadharia na Tahakiki. DSM: DUP,Kiango, Msokile na Sengo (1987),
Uhakiki wa vitabu vya Fasihi Sekondari na vyuo. NPA, n.k.
Dhima
ya mhakiki
·
Kuchambua na kuweka wazi mafunzo yanayotolewa na kazi
za fasihi:Hapa
mhakiki anatoa ufafanuzi wa kimaudhui wa kazi ya fasihi. Mhakiki husoma kwa
uangalifu kazi ya fasihi.Baada ya kusoma kwa makini, hutafakari na kuchunguza
maudhui, maadili na ujumbe ambao mwandishi amekusudia kuwafikishia wasomaji
wake na jamii inayohusika.
·
Kuchambua na kufafanua picha za kisanii zilizotumika
katika kazi ya fasihi:Mhakiki huwasaidia wasomaji ili wasishindwe
kuyaelewa maudhui barabar kutokana na kukanyagwa na usanii. Matumizi, mathalani
ya ishara ni baadhi ya mbinu ambazo zinaweza kumkanyaga msomaji ambaye hajapata
utaalamu mkubwa wa kuchambua. Mhakiki wa kufichua ishara fulani ina maana kuwa
amemsaidia msomaji kupata ujumbe kikamilifu.
Kuhusu
matumizi ya picha, kwa kawaida, lugha ya picha ina mguso sana na huibua hisia
aina na hata kuchekesha au kuwafanya watu walie machozi. Mhakiki sharti
awaambie kwamba, matumizi ya picha ni mbinu mojawapo inayosaidia maudhui
kuwaganda wasomaji. Picha inayochekesha, kufurahisha, kukejeli, n.k. Haikomei
pale tu, kwani baada ya kucheka, n.k. msomaji huathiriwa sana kinafsi na
aghalabu huachiwa mafunzo fulani. Hivyo mhakiki lazima achambue na kuyaweka
wazi mafunzo yanayotolewa na picha hiyo.
·
Mhakiki ana dhima ya kumshauri mwandishi ili afanye
kazi bora zaidi:Mhakiki
anamfundisha mwandishi juu ya yale anayoyasema yanavyoweza kupokelewa na jamii.
Humwonyesha msanii uzuri na udhaifu wa kazi aliyoisaini. Kitendo hiki humfanya
msanii ajifunze mambo yapi ni mazuri na yapi ni mabaya kama anavyoelekezwa na
mhakiki, na hivyo humfanya awe na nafasi nzuri ya kuirekebisha kazi hiyo
atakapoishughulikia kazi nyingine. Kwa msingi huo, mhakiki anaweza kulaumu au
kusifu/kumpongeza mwandishi wa kazi yoyote ya kisanaa.
·
Mhakiki ana dhima ya kumwelekeza msomaji ili apate
faida zaidi kuliko ile ambayo angeweza kuipata bila dira ya mhakiki:Mhakiki huifunza
jamii namna ya kupokea na kuifurahia kazi ya sanaa. Vilevile mhakiki huwasaidia
wasomaji kuyabaini maandishi yaliyo sumu kwa jamii. Mhakiki lazima ayafichue
maandishi hayo ili yasieneze sumu kwa jamii. Mhakiki lazima ayafichue maandishi
hayo ili yasieneze sumu kwa jamii inayohusika.
·
Mhakiki ana dhima ya kukuza kiwango cha utunzi na
usomaji wa kazi ya fasihi:Kutokana na ushauri anaopata mwandishi
kutoka kwa mhakiki, humfanya awe makini zaidi wakati wa kushughulikia kazi
nyingine.Vilevile wasomaji wanakuza kiwango chao cha usomaji kwa kufuata
mawaidha ya mhakiki.
·
Mhakiki ana dhima ya kusema wazi kuhusu kiwango cha
maandishi anayohakikiwa:Akisema wazi kwamba, maandishi hayo yako
katika kiwango cha chini, mara mwandishi huyo asilia atakapoamua kutunga tena,
atashawishika kuandika maandishi yaliyo kwenye kiwango cha juu zaidi. Na
waandishi wengine watapatiwa msukumo wa kuandika maandishi yaliyo kwenye
kiwango cha juu zaidi. Na waandishi wengine watapatiwa msukumo wa kuandika
maandishi yaliyo kwenye kiwango cha juu pia. Na hivi ndivyo mhakiki
anavyosaidia kukuza na kuendeleza maandishi ya taifa lake.
·
Mhakiki anatakiwa kuheshimu na kuthamini kazi za
waandishi na kuzifanyia haki:Jamo la msingi (lazima) kuzingatia na
kuwa, mhakiki afanyapo kazi yake huwa vitani. Mhakiki anapaswa kujua namna ya
kuwanasa wasomaji bila wao kujitambua na kuwa na uwezo au kuchambua kisayansi
mambo bila kutoonyesha hisia za wasomaji. Anatakiwa asiwe na majivuno na
aheshimu anaowahakiki na anaowataka wasome uhakiki wake. Awachukue hatua kwa
hatua kifalsafa hata waone vigumu, na kwamba haiwezekani kupigana naye.
MISINGI YA UHAKIKI WA KAZI
ZA KIFASIHI
Uhakiki
wa kazi za kifasihi hufanywa kwa kuzingatia vipengele vya fani na maudhui. Fani
na maudhui ni kama masanduku makubwa ambayo mhakiki huyafungua na kuanza
kuchunguza vilivyomo ndani yake. Kila moja lina vipengele vidogovidogo ndani
yake.
(a)Fani
Fani
ni mbinu au ufundi anaobuni na kutumia mtunzi wa kazi ya kifasihi ili kufikisha
ujumbe kwa hadhira yake iliyokusudia.
Fani ina vipengele mbalimbali. Vipengele hivyo ni pamoja na wahusika, mandhari,
lugha, muundo na mtindo.
1)Wahusika
Wahusika
wa kazi ya kifasihi ni viumbehai au wasio hai; halisi au wa kubuni, ambao
wanatenda matendo mbalimbali ndani ya kazi ya kifasihi. Wahusika wanaweza kuwa
ni binadamu, mawe, miti, malaika, miungu na mizimwi. Kwa kawaida, wahusika
katika kazi ya kifasihi hutumika kuwakilisha au kubainisha maisha halisi ya
wanadamu.
Aina za wahusika
Wanafasihi
mbalimbali wamewagawa wahusika katika makundi tofauti. Hata hivyo, sisi
tutawagawa katika makundi makuu mawili, yaani wahusika wakuu na wahusika
wadogo.
·
Wahusika
wakuu
Mhusika
mkuu ni mhimili wa kazi ya kifasihi na huonekana kuanzia mwanzo hadi mwisho wa
kazi ya kifasihi. Mhusika mkuu ndiye wa muhimu kabisa kuliko wote. Huyu ndiye
anayehusiana zaidi na dhamira kuu ya kazi inayohusika.
·
Wahusika
wadogo
Hawa
ni wahusika wanaomsaidia mhusika mkuu kufikisha ujumbe wa mtunzi kwa hadhira.
Kwa kawaida, wahusika wadogo huchomoza hapa na pale kwenye kazi ya kifasihi,
kisha huweza kutoweka kwa muda au kutoweka kabisa. Kwa mfano, mhusika mdogo
masikini anaweza kupambanishwa na mhusika mkuu ili kubainisha ukarimu au uchoyo
wa mhusika mkuu, kisha huyo mhusika mdogo hatumwoni tena. Wahusika, wawe
wakubwa au wadogo, wanaweza kuwa duara, bapa au shinda:
§ Wahusika
duara
Wahusika
duara (au mviringo) ni wahusika wenye sifa halisi za ubinadamu, yaani
wanaonekana ni binadamu halisi. Hii ni kwa sababu wanabainisha katika maisha
yao uzuri na ubaya – wema na uovu, ujasiri na woga, ushindi na kushindwa. Pia,
wanabadilika kiakili, kimtazamo na kimaadili kadiri wanavyokutana na changamoto
za kimaisha kama ilivyo kwa binadamu halisi.
§ Wahusika
bapa
Hawa
ni wahusika ambao hutokea wakiwa na tabia ya aina moja kuanzia mwanzo hadi
mwisho.Wao hawakui au kubadilika,bali hubakia na msimamo au mtazamo ule ule walioanza
nao. Kama ni mchoyo, anakuwa ni mchoyo kuanzia mwanzo hadi mwisho.
§ Wahusika
shinda
Hawa
ni wahusika ambao wako katikati ya wahusika duara na bapa. Wahusika hawa
wanaweza kubadilika, lakini si kutokana na misimamo yao, bali ni kwa sababu ya
kuyumbiswa na wahusika wengine. Ni wahusika ambao hawajitegemei kimawazo.
Tunaweza
kuonyesha aina za wahusika kwenye mchoro kama ifuatavyo:
Wahusika
|
Wadogo
|
Wakuu
|
Duara
|
Bapa
|
Shinda
|
Duara
|
Bapa
|
Shinda
|
2. Mandhari
Mandhari
ni mahali ambako matukio ya kwenye kazi ya kifasihi yanatokea.Mandhari yanaweza
kuwa halisi au ya kubuni tu. Kwa mfano, mtunzi anaweza akawaweka wahusika wake
kwenye Jiji la Dar es Salaam. Haya ni mandhari halisi. Vilevile, anaweza
kuwaweka wahusika kwenye nchi iliyoko chini ya bahari au kwenye jua. Hayo
yanakuwa si mandhari halisi bali ni ya kufikirika au ya kubuni tu.Kwa hiyo, mandhari yanaweza
yakawa mjini au kijijini, msituni au baharini, chini ya ardhi au angani.
3
.Lugha
Lugha
ndiyo malighafi kuu inayotumiwa na mtunzi kuzalisha kazi ya kifasihi. Lugha ya
kifasihi ni lugha yenye mvuto kwa vile husheheni maneno ambayo yameshibishwa
taswira au picha, yaani ni lugha ya picha.Lugha ya kifasihi ni ya picha kwa
kuwa ina mambo yafuatayo:
(a) Nahau
Haya ni maneno, aghalabu mawili au
zaidi, ambayo maana yake ya jumla ni tofauti na maana ya neno mojamoja ndani ya
nahau hiyo. Kwa mfano, kuvunjika kwa moyo si kitendo cha moyo ulio ndani ya
mwili kukatika vipande, bali ni kukata
tama.Nahau hunogesha na kunakshi lugha, hivyo huongeza mvuto na kuupa uzito
ujumbe uliokusudiwa.
(b)Methali
Huu
ni usemi mfupi wa hekima ambao kwa kawaida huwa umerithiwa kutoka vizazi vya
nyuma, na ambao umebeba maana pana iliyojificha. Kwa mfano, kidole kimoja hakivunji chawa.
(c)Tamathali za semi
Hii
ni misemo ambayo hutumiwa kutoa maana tofauti na maana ya maneno yake. Zipo
aina mbalimbali za tamathali za semi. Zifuatazo ni baadhi yake:
Ø Tashibiha
Huu
ni ulinganishaji wa vitu au hali mbili tofauti kwa kutumia maneno: kama, mithili ya, sawa na, utadhani na,
mfano wa.Kwa mfano:
·
Ametulia kama gogo la mnazi.
·
Tumbo limetangulia mithili ya ngoma ya gwaride.
·
Ana macho makali utadhani matone ya gongo.
Ø Sitiari
Huu
ni ulinganishaji wa vitu au hali mbili moja kwa moja bila kutumia maneno: kama,
mithili ya, utadhani na mfano wa.
Kwa mfano:
·
Kichwa chake ni benki ya majina ya shule
nzima.
·
Maji ya kifuu ni bahari ya chungu.
·
Huyu mtoto atakuwa kiboko ya wote.
Ø Mubalagha
Huu
ni uelezaji wa jambo kwa kutia chumvi
kuliko hali halisi ilivyo.
Kwa mfano:
·
Yaani Yule ana tumbo kama gunia.
·
Huyu dada anaweza kuongea hadi simu
ikaishiwa chaji.
·
Kwa njaa niliyo nayo, naweza kumaliza
hata mbuzi wawili.
Ø Tashihisi
Hii
ni njia ya kuvipa vitu visivyo binadamu sifa za ubinadamu, kwa mfano sifa za
kuongea, kufikiri, kucheka na kutoa hoja.
Kwa mfano:
·
Jua lilitudokolea jicho lake kali na
kututemea moto wake hadi tukaenda kujificha chini ya dari.
·
Homa ile ilimng’ang’ania kwa makucha
yake huku ikimvutia gizani,lakini alipambana nayo hadi ikatimua mbio.
·
Mlango ule ulitukaribisha kwenye tumbo
la nyumba ile huku madirisha yakitukodolea macho kwa mshangao.
Ø Taashira
Hii
ni njia ya kutaja kitu fulani kwa lengo
la kuwakilisha kitu au jambo jingine.
Kwa mfano:
·
Mwanafunzi Yule si kama wengine. Yeye
ameweka kitabu mbele.(Kitabu
kinawakilisha masomo.)
·
Ni vema kwa kuwa ameamua kuishi maisha
ya jembe.
(Jembe
linamaanisha kilimo.)
Ø Taniaba
Hii
ni njia ya kutumia jina fulani kwa namna ya ulinganisho ili kumaanisha kitu
kingine. Hivyo viwili vinakuwa na tabia fulani linganifu.
Kwa mfano:
·
Kiongozi Yule amekuwa ni Iddi Amini wanchi
ile.
·
Sisi tunafuga mbuzi tu. Hawa ndio
ng’ombe wetu.
Ø Majazi
Hii
ni aina ya tamathali ambayo hutaja sehemu tu ya kitu kwa lengo la kumaanisha
kitu kizima.
Kwa mfano:
·
Masomo haya yanahitaji vichwa kwelikweli. (kichwa = mtu mwenye
akili)
·
Ajali ile imepoteza roho saba. (roho =
mtu kamili)
Ø Dhihaka
Haya
ni maneno yenye maana kinyume na vile yanavyosema, ambayo hutolewa kwa lengo la
kudunisha au kushusha hadhi.
Kwa mfano:
·
Kijana huyu asione chakula; macho
humtoka na miguu humwasha. Domo hujaa mate tele kama fisi aliyeona nyama.
·
Bosi wetu alikaa kwenye kiti chake,
utadhani kakumbatia tungi la pombe ya kienyeji. Ama kwa hakika bosi kajaliwa
tumbo. Tumbo hilo ni shimo refu ambamo zinaishia fedha za kampuni na jasho
letu.
Ø Tasfida
Haya
ni maneno ya heshima yanayotumika ili kupunguza ukali wa jambo linalosemwa,
ambalo aghalabu, huwa aibu kulitamka mbele ya watu.
Kwa mfano:
·
Sehemu za siri
·
Amechafua hewa
·
Yuko uani
Ø Shtihizai,
Hii
pia huitwa kejeli. Haya ni maneno ambayo yamekusudiwa kuleta maana kinyume na
maana ya kawaida ya maneno hayo. Kwa mfano, kumwita mtu mweusi tii mzungu au cheupe; au mtu mwembamba sana kumwita bonge ni shtihizai au kejeli.
(i)
Ritifaa
Katika
tamathali hii, mtu huzungumza na mtu au kitu ambacho hakipo pamoja naye kama
kwamba yuko nacho.
Kwa mfano:
·
“Nyerere na Karume, mlitupenda wanenu;
mkatuwekea misingi ya upendo na amani. Ona sasa wameingia mbweha na fisi
ulingoni. Ninajua kabisa hamngekuwa radhi nao hata kwa dakika moja!”
Mbinu nyingine
Kuna
mbinu nyingine za kifasihi ambazo msanii anaweza kuzitumia, ambazo si tamathali
za semi. Mbinu hizo ni pamoja na:
v Takiriri
Hii
ni mbinu ya kurudiarudia manenokwa lengo la kusisitiza jambo.
Kwa mfano:
·
Wewe utafungwa, utafungwa utafungwa tu!
·
Ukifika pale ni kula, dansi; kula,
dansi!
·
Rudi mwanangu; mwanangu rudi; rudi tu mwanangu;
nitakupokea.
Takriri,
pia inaweza kuwa ni kurudia sauti ileile katika neno zaidi ya moja ambayo yanafuatana
karibu karibu.
Kwa mfano:
·
Matata alitamka maneno matano matamu.
(sauti ma)
·
Sili wali ilhali ukali wa pilipili uko
mbali. (sauti li)
·
Alipanda kwenye kitanda akajitanda shuka
lake. (sauti nda)
v Tanakali
sauti
Hii
ni mbinu ya kuiga sauti fulani. Pia, hujulikana kama onomatopea.
Kwa mfano:
·
Kakachakakacha
za kutembea kwao ziliniamsha usingizini.
·
Mara tulisikia ngo, ngo, ngo, mlangoni.
·
Kabla hatujakaa sawa, gari lile lilipita
kama mshale, fyaaaa!
v Tashtiti
Katika
mbinu hii, msanii huuliza swali ambalo jibu lake liko wazi.
Kwa mfano:
·
Kaka alipofika pale, alimwona rafiki
yake akiondoka. “Unaenda kweli?” aliuliza kwa kutoamini.
·
“Ya nini kujisumbua? Ah! Acha nikalale
zangu,” alijisemea Mawazo.
·
“Mara hii umesharudi?” Nilimuuliza kwa
mshangao.
v Mdokezo
Hii
ni mbinu ya kuanzisha mazungumzo au wazo,kisha unaishia njiani bila
kulimalizia. Hii ni kwa sababu,kwa namna fulani, sehemu ambayo haikumaliziwa
inaeleweka kutokana na muktadha wa mazungumzo au maelezo yenyewe.
Kwa
mfano:
Mama: Yaani Doto, umevunja tena kikombe?
Njoo
hapa! Leo nitaku……..!
Doto: Mama nisamehe. Bahati mbaya.
v Mjalizo
Hii
ni mbinu ya kupanga maneno katika mlolongo bila kuweka viunganishi kati yake.
Kwa
mfano:
·
Wewe lia, cheka, imba, lakini hutoki
hapa!
·
Yule bwana alikaa chini, alisisimama,
alijilaza chini, lakini maumivu yalibaki palepale.
·
Sisi tulifanya kila njia. Tuliita, wapi!
Tukatafuta, wapi! Tukapiga simu, wapi! Mwishowe tukasema, liwalo na liwe!
v Taswira
Utengenezaji
wa taswira katika kazi za kifasihi ni mbinu inayojitegemea,bali huambatana na
mbinu nyingine, kwa mfano, tamadhali za semi. Taswira ni picha zinazoumbika
akilini ambazo tunazipokea kana kwamba ni kupitia kwenye milango ya fahamu.
Kwa mfano:
·
UKIMWI unabugia watu katika domo lake na
kuwatafuna bila huruma.
Ifuatayo
ni mifano ya taswira mbalimbali:
Taswira za kuona
Kwa mfano:
·
Ana tumbo kubwa kama mtungi.
·
Uso wake umetokeza mbele utadhani wa
tumbiri.
·
Nyumba ile ilikuwa kama kilima kikubwa
chenye mapango ndani yake.
Taswira za kusikia
Kwa mfano:
·
Kicheko chake ni kama radi
·
Kelele za watu ukumbini zilikuwa kama
maporomoko ya maji mengi.
·
Njaa husababisha tumbo langu kunguruma
kama pikipiki.
·
Taswira za mguso
Kwa mfano:
·
Mikono ilikuwa inaparua kama msasa.
·
Alikuwa na ngozi nyororo kama kikombe cha udongo.
·
Maneno yake yanachoma kama misumari ya
moto.
Taswira za kunusa
Kwa mfano:
·
Ungemhurumia kwa vile ambavyo mguu ule
ulitoa harufu kama mzoga wa paka.
·
Huyo bwana usimkaribie aongeapo ni kama
unachungulia kwenye debe la pombe ya mnazi.
Taswira ya kuonja
Kwa mfano:
·
Mwonekano wake ulileta uchachu ndani ya
akili yangu.
·
Ana maneno makali kama pilipili.
4. Muundo
Ni mpangilio na
mtiririko wa kazi hiyo kwa upande wa visa na matukio. Hapa tunachunguza jinsi
msanii wa kazi ya fasihi alivyofuma, alivyounda na alivyounganisha tukio moja
na jingine, kitendo kimoja na kingine, wazo na wazo, sura moja na nyingine,
ubeti na ubeti, hata mstari wa ubeti na mwingine.
Aina za miundo
(a)
Muundo wa msago,huu ni muundo wa
moja kwa moja ambao tunafatilia matukio mbalimbali tangu la kwanza hadi la
mwisho kwa mbinu ya utelezi. Kwa mfano, mhusika huzaliwa, hukua, huchumbia au
kuchumbiwa, huoa au kuolewa, huzaa watoto, huzeeka, hufa. Riwaya ya kuli (1978)
imetumia muundo huu. Katika riwaya hii tunamwona Rashidi akizaliwa, akikua,
anaanza kazi, anaoa, anaanza harakati za kudai haki za makuli na mwisho
anafungwa.
(b)
Muundo wa kioo,huu ni muundo wa
kimchangamano utumiayo mbinu ambayo huweza ama kumrudisha nyuma msomaji wa kazi
aya fasihi katika mpangilio wa matukio yake au kuipeleka mbele hadhira ya kazi
hiyo. Riwaya ya Zaka la Damu
(1976) imetumia muundo huu.
(c)
Muundo wa rukia,huu ni muundo
ambao visa hupandana. Katika muundo huu kunakuwa na visa viwili ambavyo
hupandana katika kusimuliwa kwake, na mwisho visa hivi huungana na kujenga kisa
kimoja. Mfano ni riwaya ya Njama
(1981).
Katika ushairi muundo
tunaangalia idadi ya mistari katika kila ubeti wa shairi. Kuna miundo ya aina
mbalimbali:
(i)
Muundo wa
Tathnia – kila ubeti wa shairi unakuwa na mistari miwili.
(ii)
Muundo wa
Tathlitha – kila ubeti unakuwa na mistari mitatu.
(iii)
Muundo wa Tarbia
– kila ubeti unakuwa mistari minne.
(iv)
Muundo wa
Takhimisa – kila ubeti unakuwa na mistari mitano.
(v)
Muundo wa
Sabilia
– kila ubeti unakuwa na mistari sita na kuendelea.
5.
Mtindo,ni ile namna ambayo msanii hutunga kazi
hiyo na kuipa sura ambayo kifani na maudhui huainisha kanuni au kaida
zilizofuatwa kama ni zilizopo au ni za kipekee.Mtindo ni upangaji wa fani na
maudhui katika kazi ya fasihi kwa njia ambayo hatimaye hutokeza au huonyesha
nafsi na labda upekee wa mtungaji wa kazi hiyo.
Dhima ya mtindo
-
Humwezesha
msomaji kujua hisia za msanii kuhusu analiandika.
-
Humsaidia
msomaji kutafiti thamani ya maudhui na namna ya kuyapima au kuyathamini.
-
Hudokeza
kiasi cha hisia na mwamko wa wahusika katika hadithi, na vilevile kuonyesha
maendeleo yake.
-
Ni
kiungo muhimu cha mtiririko wa matukio.
-
Huiumbua
dunia ulimwengu wake ambapo yale maono ni ya msanii, lakini mtindo ndiyo
unaojitokeza kwa watu wengi ili wajue msanii anaandika kitu gani.
Katika mtindo
kinachotazamwa ni:Matumizi ya lugha,Nafsi alizotumia msanii,Matumizi ya
monolojia (maelezo), masimulizi na dialojia (mahojiano)
(b)
Maudhui
Maudhui katika kazi ya fasihi ni jumla
ya mawazo yanayozungumzwa pamoja na mtazamo wa mwandishi juu ya mawazo hayo.
Maudhui hujumuisha mawazo pamoja na mafunzo mbalimbali yaliyomsukuma msanii
hadi akatunga na kusaka kazi fulani ya fasihi.
Vipengele
vya maudhui
·
Dhamira,Hii ni wazo kuu au mawazo mbalimbali
yanayojitokeza katika kazi ya fasihi. Dhamira hutokana na jamii. Kwa kawaida
dhamira huweza kuwa za kisiasa, kiutamaduni au kiuchumi. Katika dhamira, kuna
dhamira na dhamira ndogondogo.
·
Mtazamo,ni hali ya kuyaona mambo katika maisha
kwa kuzingatia mazingira aliyonayo msanii mwenyewe. Wasanii wana mitazamo ya
aina mbili:
-
Mtazamo
kiyakinifu
– Huutazama ulimwengu au mazingira yanayomzunguka binadamu na mfumo wa
kihistoria. Mtazamo huu humfanya msanii kuutazama ulimwengu kama kitu dhahiri
katika uhalisi wake.
-
Mtazamo wa
kidhanifu
– Huu huchukulia ulimwengu kama kitu kinachobadilika kulingana na matakwa ya
Mungu. Msanii mwenye mtazamo huu, atawasilisha hivyo katika kazi yake.
·
Msimamo,hii ni hali ya mwandishi kuamua kufuata
na kushikilia jambo fulani.Jambo hili linaweza kuwa halikubaliki na wengi,lakini
yeye atalishikilia tu. Msimamo wa msanii ndiyo unaosababisha kazi ya sanaa iwe
na mwelekeo maalumu na hata kutofautiana na kazi za wasanii wengine.
·
Falsafa,huu ni mwelekeo wa imani ya msanii.
Msanii anaweza kuamini, kuwa mfano, mwanamke si chombo duni kama wengine
wanavyoamini. Au, kwa wale wapinga usawa, wanaweza kuwa na falsafa ya kumwona
mwanamke kuwa kiumbe duni.
Kwa hiyo,
falsafa ya kazi ya fasihi inatakiwa ichambuliwe kwa kuzingatia jinsi kazi hiyo
ilivyoutazama ulimwengu na kuueleza ukweli juu ya mambo mbalimbali. Ukweli huo
lazima uhusishwe na binadamu.
·
Ujumbe na maadili
Ujumbe katika
kazi ya fasihi ni mafunzo mbalimbali ambayo hupatikana baada ya kusoma kazi ya
fasihi.
·
Migogoro
Migogoro ni
mivutano na misuguano mbalimbali katika kazi ya fasihi. Katika migogoro kuna
migogoro kati ya wahusika ama vikundi vya wahusika, familia zao, matabaka yao,
n.k. Na migogoro hii mara nyingi hujikita katika uhusiano wa kijamii. Migogoro
yaweza kuwa ya:Kuichumi,Kiutamaduni,Kisiasa,Kinafsia
MADA NDOGO-2; MAENDELEO
YA FASIHI
CHIMBUKO
LA FASIHI NA SANAA.
Kuna mitizamo mikuu minne ya kiulimwengu inavyotokeza katika suala la
chimbuko la fasihi .Mitazamo hiyo ni
kama ifuatayo;
1.
Mtazamo wa kidhanifu.
Mtazamo wa kidhanifu wa misingi yake katika kudhani tu kwa
hiyo kufuatana na mtazamo huu inaaminika kuwa fasihi na Sanaa kwa ujumla kutoka
kwa Mungu kwa hiyo mwanasanaa huipokea ikiwa imekwishapikwa na kuivishwa na
Mungu huyo.
Mtazamo wa namna hii ulijitokeza tangu zamani sana wakati wanafalsafa
wa mwanzo wa kigiriki na kinenzi kama vile Socrates Plato na Anstotle,walipoanza
kuingia katika ulimwengu wa nadharia ya Sanaa. katika uwanja wa nadharia ya
fasihi/Sanaa ya Kiswahili kuna mifano mingi ya wahakiki wa mwanzo waliokuwa na
mitazamo sawa naya wanafalsafa hao mfano F.Nkwera (1970), insha yake ya fasihi inadhihirisha uaminifu
wake wa mawazo ya kidhanifu kwa kudai “fasihi ni Sanaa ambayo huanzia kwa muumba
humfikia mtu katika vipengele mbalimbali -ni hekima ambayo mtu ameshirikishwa
apate kumtambua muumba wake”.Nkwera
ameungwa mkono na wahakiki wengine ambao wanasisitiza mtazamo huu kwa kusema “Mtengenezo
ya Sanaa huonekana kuwa ni shughuli ya kiungu yenyekumwiga Mungu ambaye ndiye
msanii wa kwanza”
John Ramadhani pia katika makala yake ya fasihi ya Kiswahili
anasisitiza kuwa.“Zaidi ya kwamba fasihi ni hisia vile vile kitengo cha mtu cha kubaini
kazi ya Sanaa ni uigaji wa Mungu ambaye ndiye mfalme wa Sanaa zote”.Mawazo
haya ya akina Nkwera,John Ramadhani na wengine yamejaa mwangwi tu wa mawazo yaliyochakaa ambayo
yalikwisha kutajwa na kushughulikiwa na
wahakiki wa zamani tuliowataja kwa msimamo huu wa kidhanifu,Sanaa au fasihi
havijifinyangwi kwa jitihada za akili za mikono ya mtu bali
hupokelewa kutoka katika mikono mbayo mtu hana uwezo wa kuiona.
Udhaifu, mtazamo huu umepotosha maana halisi kwa kuchanganya Imani
na taaluma,pia unajaribu kumtenganisha msanii na jamii yake kwani unatoa
nadharia inayomwinua msanii na kufanya aonekane kuwa mtu wa ajabu aliyekaribu na Mungu kuliko watu
wengine wa kawaida.
2. Mtazamo
wa kiyakinifu
Kulingana na mtazamo huu Chanzo cha fasihi ni sawa na chanzo cha binadamu wenyewe yaani Binadamu
na mazingira yake ndio Alfa na Omega ya fasihi.Iwe kwa kuumbwa au mabadiliko
kuanzia chembe hai ambayo imepitia maendeleo kadha ya makuzi hata kufikia mtu
binadamu alioanishwa na kazi ili kuyabadili mazingira yake.Katika harakati zake
za kujiendeleza kiuchumi kila mara alijaribu hiki na kile alichokiona kinafaa
alikiendeleza Zaidi na kukidumisha katika hali hii hadithi(ngano),methali,vitendawili,nyimbo,tenzi(mashairi)
n.k vyote hivyo vilitungwa na kusimuliwa kwa madhumuni ya kufunza,kukosoa,kuadhibu,kuchokoza fikra
na kuliwaza jamii baada ya kazi.
Sanaa hii ilirithishwa toka kizazi hadi kizazi kwa njia ya
masimulizi na binadamu alivyozidi kujiendeleza kisayansi na kiteknolojia
akahifadhi taaluma hii katika maandishi.Ndiyo sababu tunasema chanzo cha fasihi
ni sawa na chanzo cha binadamu mwenyewe na jinsi binadamu alivyozidi na
atakavyozidi ndiyo taaluma hii ilivyokuwa na kuendelea.
3.
Fasihi inatokana na sihiri,Istilahi
Sihiri’ ina maana ya Uwezo au nguvu ya kimiujiza inayotumiwa na watu
kusababisha matokeo fulani.Watalaam hawa
wanadai kuwa chimbuko la fasihi ni haja
ya mwanadamu kukabiliana na kujaribu
kuyathibiti mazingira yake. Haja hiyo haikutimilika ipasavyo katika hatua zake
za mwanzo za maendeleo ya mwanadamu
kwani uwezo wa kisayansi na kiteknolojia wa mwanadamu wa wakati huo bado
ulikuwa kiwango cha chini sana.Hivyo Imani au miujiza ilichukua nafasi ya
sayansi na ugunduzi.Fasihi ilichimbuka kama chombo cha sihiri hivyo katika kujaribu kuyashinda
mazingira,Mfano Wawindaji walichora picha ya mnyama waliyetaka kumuwinda kabla
ya kwenda kuwinda,kisha walichoma mkuki au mshale kwa kuamini kuwa kitendo
hicho kitatokea kuwa kweli watakapo kwenda kuwinda. Nyimbo walizoimba wakati wa
kufanya sihiri hiyo ndiyo fasihi ya mwanzo.
Udhaifu wa nadharia hii ni kwamba inachangnya dhima na chimbuko
kwani kutumika kwa nyimbo au ushairi katika sihiri hakuthibitishi kuwa sihiri
ndiyo chimbuko lake.Sihiri ni amali moja tu kati ya amali nyingi za wanadamu wa
mwanzo zilizotumia ushairi.
4.
Nadharia ya Mwigo,Wataalam wa
nadharia wanadai kuwa Fasihi imetokana na mwigo(Uigaji),Katika nadharia hii
inaeleza kuwa mwanadamu alianza kuwa mbunifu kwa kuiga maumbile
yaliyomzunguka.Hivyo sanaa za mwanzo mara nyingi zilijaribu kusawiri vitu
vilivyomo katika mazingira ,mfano wanyama,ndege,miti,watu.Nadharia hii ni
kale,ilianzisha na wataalamu wa kiyunani
na walioieneza zaidi ni Plato
(Republic) na Aristotle (Poetics) Plato anahusisha mwigo na dhana ya
uungu.Anaeleza kuwa Maumbile na vilivyomo ni mwigo tu wa sanaa ya kiungu.Sanaa
ya Mwanadamu (Hususani ushairi) ambayo huiga tu mambo hayo yaliyomo katika maumbile haiwezi kuwa na ukweli au uhalisi wa kuwa inaiga maumbile ambayo na
yenyewe yanaiga kazi ya Mungu.Hivyo
alishauri aina fulani za ushairi zipigwe marufuku kwa sababu zinapotosha ukweli.
Udhaifu
wa nadharia hii ni kwamba
inasisitiza mno uigaji na kusahau suala la ubunifu katika sanaa na fasihi.Kama
wasanii wangeig maisha na mazingira tu,sanaa yao ingepwaya sana na haingekuwa
tofauti na picha ya fotografia au maelezo ya matendo ya mazingira na matendo ya
kila siku ya mwanadamu.
FASIHI NI SANAA.
Sanaa ni uzuri unajitokeza katika umbo lililosanifiwa umbo
ambalo mtu hulitumia kuelezea hisia zinazomgusa kwa kutoa kielelezo au
vielelezo vyenye maana maalumu.
Aina za Sanaa
Ø Sanaa
za Uonyeshi,ni sanaa ambazo uzuri wake hujitokeza katika umbo la
kudumu, umbo ambalo linaweza kuhifadhiwa na uzuri wake kuonyeshwa wakati
wowote. mfano uchoraji, uchongaji, kutarizi, ufinyanzi, n.k. Sanaa ambazo
hututolea vitu kama vile picha, vinyago, nguo zilizotarizwa, vyungu n.k.
Ø
Sanaa za Ghibu,ni sanaa ambazo uzuri
wake haujitokezi kwenye umbo linaloonekana kwa macho au kushikika bali katika umbo linalogusa hisia mfano ushairi,
uimbaji, upgaji muziki, n.k. Uzuri wa sanaa hizi umo katika kuzisikia.
Ø
Sanaa za Vitendo,ni sanaa ambazo
uzuri wake umo katika umbo la vitendo. Uzuri wa sanaa hizi umo katika umbo la vitendo, na ili
kuupata uzuri huu yampasa mtu kutazama vitendo vikifanyika. Umbo hili
linalazimisha kuwepo kwa mwanasanaa (mtendaji) na mtazamaji(Hadhira) wa sanaa
mahali pamoja kwa wakati mmoja, ama sivyo sanaa haikamiliki. Hali hii ndiyo
inayosababisha sanaa hizi za vitendo kuita sanaa za maonyesho kwa sababu
lazima wakati zinapototendeka awepo mtu wa kuonyeshwa, maana uzuri wake umo
katika vitendo vyenyewe.
SIFA ZA SANAA ZA
MAONESHO
-
Dhana ya kutendeka (tendo)
-
Mtendaji (fanani)
-
Uwanja wa kutendea/jukwaa maalumu
-
Watazamaji (hadhira).
Hivyo sanaa za maonyesho ni dhana zilizo kwenye umbo
linalotendeka na ili dhana hii itendeke
inahitaji mtu wa kuitenda (mtendaji). Mtendaji huhitaji uwanja wa kutendea hiyo
dhana, na wakati akiitenda hiyo dhana wanakuwepo watazamaji.
Tanzu za Sanaa za Maonyesho
1)Tambiko, ni sadaka
inayotolewa kwa miungu au mahoka, mizimu, pepo, n.k. wakati wa kusalia miungu.Matambiko yalikuwa
na umuhimu mkubwa katika jamii za babu zetu kuliko siku hizi. Jamii ya asili
ilipokabiliwa na matatizo yaliyowashinda kama vile magonjwa, ukame, au kukosa
mtoto, n.k. walifanya tambiko na kusali ili miungu yao iwasaidie. Wakati fulani
walifanya matambiko kwa ajili ya kuomba radhi au kutoa heshima na shukrani.
Mara nyingi matambiko haya huandamana na kafara kama sadaka
inayotolewa na jamii kwa wahenga wao. Kafara inaweza kuwa ya kuku, kondoo,
ng’ombe, mbuzi au chakula. Katika jamii nyingi za Kiafrika kabla ya ukoloni
walitoa kafara ya binadamu.
Fani katika tambiko
Ø
Sanaa
Katika tambiko sanaa inayotendeka ni ule ufundi wa kutenda
vitendo kwa ukamilifu kwa kutambika kwa kutumia ufundi wa aina fulani.
Ø
Wahusika
Wahusika wa tambiko ni wale wazee maarufu walioteuliwa na
jamii kuendesha shughuli hizi za matambiko. Si watu wote katika jamii huhusika.
Ø
Mazingira (Mahali)
Tambiko linaweza kufanyika porini, makaburini, njia panda,
kwenye mti mkubwa au mahali popote kutegemeana na aina ya tambiko lenyewe.
Umuhimu wa Tambiko
ü
Hujenga imani kama chombo cha kutatulia matatizo
ya jamii. Jamii ya asili ilipokabiliwa na matatizo ilifanya tambiko na kusali
ili miungu iwasaidie kuondokana na tatizo hilo.
ü
Tambiko husaidia kuendeleza mila na desturi za
jamii.
ü
Tambiko hujenga na kuimarisha mahusiano miongoni
mwa wanajamii.
ü
Matambiko huiongoza jamii katika mapambano dhidi
ya matatizo mbalimbali yanayowakabili.
Hasara za Tambiko
ü
Hujenga dhana potofu katika jamii kwani watu
huamini nguvu fulani bila kuwa na uhakika au uthibitisho wa kisayansi.
ü
Huleta hasara kubwa kwa jamii kwani kafara ya
tambiko inahitaji mnyama au chakula, ambapo watu hutumia hela nyingi kuvipata
vitu hivyo.
2) Mivigha,ni sherehe
zinazofanywa na jamii katika kipindi maalumu cha mwaka. Mivigha hufanywa kwa lengo la kufundisha jambo fulani maalumu
kwa maisha ya jamii. Sanaa za maonyesho katika kundi hili zinahusu kuingizwa
kwa mwanajamii kwenye kundi la watu wa aina fulani kutoka kundi la watu wa aina
nyingine. Mfano jando na unyago, harusi, kutawazwa chifu, n.k.Katika jando na
unyago mtu hutoka kundi la watoto kuingia kundi la watu wazima, mtu aliyeoa
anatoka kundi la makapera kwenda kundi la waliooa au kutawazwa chifu, mtu
anatoka kundi la raia na kuingia kundi la watawala n.k.
Kutoka kundi moja kuingia kundi jingine ni hatua iliyopewa
umuhimu mkubwa katika jamii ya asili. Umuhimu huu uliambatana na madaraka mapya
yaliyo mkabili mwanajamii kuingia katika kundi jipya. Kila kundi la watu
lilikuwa na madaraka fulani mbayo kutekelezwa kwake ndiko kulikoleta maendeleo ya
jamii .
Fani katika Mivigha
Ø
Sanaa
Sanaa katika mivigha ni ule ufundi wa kutenda kikamlifu na
kiufundi katika kudhihirisha yale yanayotendeka.
Ø
Wahusika,Katika mivigha wahusika ni
wa aina tatu:
a)Mtendaji/watendaji,ni wale wote wanaoshiriki kutenda ile
dhana ya kuwatoa watu kutoka kundi moja na kuwaingiza katika kundi lingine.
Vitendo hivyo huambatana na nyimbo, michezo mbalimbali n.k.
b)Watazamaji ,ni wale wanaoingia kutoka kundi moja na kwenda
kundi lingine. Hawa ndio watazamaji, kwa sababu maneno, nyimbo, vitendo, ngoma,
n.k. vyote vinafanyika ili wao wavione na wajifunze na baadae watekeleze yale
waliyojifunza.
c)Waangaliaji, ni wale wanaoangalia mambo yanayotendeka bila
wao kushiriki katika kucheza au kuimba au kutoa mafunzo, wanaangalia tu. Hawa
kwa upande wa sanaa za maonyesho sio watazamaji kwa sababu yale yafanywayo
hayawasilishwi kwao. Wakiwepo au wasiwepo bado vitendo vinatendeka tu bila
maana yake kupotea. Hawa wanaitwa “waangaliaji”
d)Mahali /Mandhari,kwa upande wa mivigha uwanja wa kutendea ni
mahali sherehe zinapofanyika. Inaweza ikawa ndani ya nyumba, au porini, kwenye
uwanja wa nje ya nyumba,milimani au mapanngoni, n.k.
Umuhimu wa mivigha
ü
Mivigha hufundisha umuhimu wa kazi kama vile
kilimo, uwindaji, uhunzi, ufinyanzi, ushonaji, n.k.
ü
Mivigha huhimiza umuhimu wa ujasiri katika
maisha.
ü
Mivigha
hufundisha suala zima la unyumba na malezi kwa ujumla mfano umuhimu wa uzazi na malezi bora.
ü
Mivigha husisitiza umuhimu wa umoja na
ushirikiano katika jamii.
Hasara
za Mivigha
ü
Hugharimu pesa nyingi sana ambapo huwaacha wenye
sherehe kwenye madeni makubwa.
ü
Sherehe huweza kusababisha ugomvi, chuki,
dharau, tamaa, n.k.
ü
Huleta ushindani na matokeo yake husababisha
baadhi ya watu wasio na uwezo hujiingiza katika wizi, utapeli, ujambazi, n.k.
3. Majigambo
Ni masimulizi ya kujigamba kwa mtu kuhusu mambo ya kishujaa
aliyopata kuyatenda maishani mwake. Majigambo hayo husimuliwa katika lugha ya
kishairi na masimulizi yake huambatanishwa na vitendo vya mjigambaji mwenyewe.
Mtambaji anapotamba katika sanaa hii, kwa kawaida huwa na
tabia ya kujivuna au kujitapa kuwa yeye ni bora kuliko wengine wote.Wakati wa
utambaji mazingira humtawala fanani. Pengine fanani alikuwa akitamba kuonyesha
utukufu wake kwa mfalme wao. Au alikuwa akitamba wakati wa kujiandaa kwenda
vitani.
Fani katika Majigambo
Ø
Sanaa
Sanaa katika majigambo ni ule ufundi anaoutenda mjigambaji,
kwa kujigamba kwa ufundi huku akionyesha vitendo waziwazi alivyopata kuvitenda
maishani mwake.
Ø
Wahusika
Hapa kuna mtendaji na watazamaji
·
Mtendaji ,ni yule anayejigamba mbele
ya wenzake, yaani Yule anayejigamba kuhusu mambo yake ya kishujaa aliyoyatenda
maishani mwake.
·
Watazamaji,ni wale wanaotazama vitendo vinavyotendwa na mtendaji.
Ø
Mahali/Jukwaa maalum
Uwanja wa kutendea ni mahali popote ambapo majigambo yanaweza kufanyikia.
Hapa inaweza kuwa kwenye uwanja mkubwa ambapo sherehe hizo zinafanyikia au
kwenye ukumbi.
Ø
Matumizi ya Ngoma katika Majigambo
Majigambo vile vile yaliambatana na ngoma, wakati mwingine
ngoma zilichezwa na katikati ya ngoma mjigambaji mmoja alijitokeza na kuanza
kujigamba, alipomaliza alirudi kucheza ngoma na mwingine alijitokeza tena
Umuhimu
wa Majigambo
ü
Hudumisha utu wa mwanaume katika jamii.
ü
Hudumisha ari ya kuwa wakakamavu, shujaa na
jasiri katika jamii.
ü
Huburudisha jamii yaani mtendaji na
wasikilizaji.
Hasara za Majigambo
ü
Hukuza na kuendeleza ubinafsi kwani fanani
huonekana ni bora zaidi kuliko watu wengine.
ü
Mkusanyiko wa hadhira hutumia pesa au vyakula
kwa wingi, hivyo husababisha umasikini .
ü
Majigambo husababisha unafiki kwa sababu fanani
huonyesha mafanikio yake tu na sehemu alizoshindwa hagusii kabisa, kitu ambacho
si cha kweli katika maisha ya mwanadamu.
4.Michezo ya Watoto
Ni mchezo mbalimbali inayochezwa na watoto, na michezo hiyo
hufungamana na hali ya utamaduni, uchumi na siasa ya jamii inayohusika. Mchezo
hii husaidia watoto waweze kujifunza mambo mbalimbali yanayotokea katika jamii
yao. Kwa njia hii watoto hujifunza shughuli mbalimbali za uzalishaji kama vile
kilimo, kupika chakula, kuwinda, n.k. Vile vile hucheza mchezo wa baba na mama.
Hapa mtoto mmoja anakuwa mama, mwingine baba na wengine watoto. Mchezo huu
huakisi mambo halisi ya nyumbani.
Fani
katika Michezo ya Watoto
Ø
Sanaa
Sanaa katika michezo ya watoto wadogo ni ule ufundi wa
kutenda vitendo kikamilifu na kuonyesha ujuzi mkubwa katika utendaji huo
Ø
Wahusika
Kuna watendaji na watazamaji. Watendaji ni watoto wenyewe
wanaocheza michezo hiyo, yaani wavulana na wasichana. Idadi ya watendaji
inategemea aina ya mchezo wenyewe.Watazamaji ni wale wanaotazama mchezo huo.
Hapa wanaweza wakawa watoto wenyewe
ambao hawachezi au jamii inayowazunguka watoto hao.
Ø
Mahali
Uwanja wa kutendea michezo ya watoto ni sehemu yoyote
itakayochaguliwa na watoto wenyewe kulingana na michezo unaohusika. Kwa mfano,
wanaweza kucheza uwanjani, chini ya mti, barabarani, chumbani, sebuleni, kando
ya nyumba, n.k.
Umuhimu wa Michezo ya Watoto
·
Huwasaidia watoto wadogo kujifunza mambo
mbalimbali yanayotokea katika jamii yao. Kwa njia hii watoto hujifunza shughuli
mbalimbali za uzalishaji mali, utamaduni na siasa ya jamii yao.
·
Huwasaidia watoto kujifunza kuwa na ujasiri,
ushujaa, udadisi wa mbinu mbalimbali za kupambana na matatizo yanayojitokeza
katika jamii.
·
Hurithisha amali za jamii toka kizazi kimoja
hadi kizazi kingine. Michezo hii hurithisha mila na desturi za jamii fulani kwa
kucheza michezo hiyo.
·
Michezo hiyo huburudisha watoto. Katika kucheza
michezo hiyo, watoto huburudika na kustarehe.
·
Huwasaidia watoto huimarisha viungo vya mwili
kwa watoto wanaocheza michezo hiyo.
Hasara za Michezo ya Watoto Wadogo
·
Watoto huweza kuumizana kutokana na michezo hii.
·
Ikiwa wazazi wa watoto hawa wana tabia chafu
kama ile ya kugombana, kutukanana ovyo, vivyo hivyo watoto hawa watarithi tabia
chafu kutoka kwa wazazi wao na wanaweza kuwaambukiza wenzao.
5.
Utani, Ni hali ya kufanyiana mizaha
pasipo kuogopa na kushtakiana au utani ni uhusiano wa kutaniana au kufanyiana
masihara ambao ni tofauti na desturi za kutokuheshimiana. Madhumuni yake
makubwa ni kupunguza na kuondoa kabisa uhasama na chuki iliyokuwepo baina ya
makundi fulani ya watu.
Fani katika Utani
Ø
Sanaa
Sanaa katika utani ni ule ufundi
na uwezo wa kutaniana baina ya wahusika wanaohusika na utani huo.
Ø
Wahusika
Katika utani, washiriki wanaweza
kuwa mtu na mtu, familia na familia, kabila na kabila, ukoo na ukoo au nchi na
nchi.
Ø
Mahali
Uwanja wa
kutendea inaweza kuwa mahali popote ambapo utani unaweza kufanyika. Inaweza
ikawa kwenye harusi, msibani, kwenye pombe wakati watu wanakunywa, n.k.
Umuhimu wa Utani
·
Kutoa
maadili na mafunzo fulani kwa jamii.
·
Kuimarisha
umoja na ushirikiano miongoni mwa wanajamii (kujenga undugu)
·
Kuhimiza
ujasiri na juhudi katika maisha.
·
Kuhimiza
upendo katika maisha.
·
Hukuza
na kuimarisha mila na desturi za jamii.
Hasara za Utani
·
Husababisha
ugomvi katika jamii.
·
Huleta
hasara za kuchukuliana vitu bila malipo.
·
Huvunja
au kuvunjiana heshima miongoni mwa wahusika.
Muziki
|
Ufumaji
|
Utarizi
|
Uchoraji
|
SANAA
|
Fasihi
|
Ufinyanzi
|
Uchongaji
|
Maonyesho
|
Ususi
|
Kila
kipengele cha Sanaa kinatofautiana na
kingine kwa umbo na matumizi. Fasihi ni kipengele cha Sanaa kinachotumia maneno
kuumba huo uzuri wa kisanaa.
TOFAUTI KATI YA FASIHI
NA TANZU NYINGINE ZA SANAA
1.
Lugha ,
kazi zote za kifasihi zinaundwa kisanaa kwa kutumia lugha inayotumika au
kuandikika. Lugha hiyo hubeba maana Fulani (ujumbe) kwa jamii Fulani.Hivyo
lugha ndiyo inayotufautisha fasihi na Sanaa nyingine. Kwa mfano, uchoraji
kipengele chake muhimu kalamu, rangi na kipande cha nguo au karatasi. Ufinyanzi
lugha yake ni udongo , uchongaji wa vinyago lugha yake ni gogo la mti n.k.
Fasihi si maelezo ya kawaida kawaida kama vile matangazo, taarifa ya habari au
barua, fasihi ni maelezo yenye mguso kisanaa. Kazi za kifasihi, huumbwa
kimafumbo hutumia nahau au misemo , methali, tamathali za semi, taswira na
ishara mbali mbali. Kazi za fasihi hufikirisha mtu huweza kutumia akili ili
aweze kugundua kazi ya kifasihi aliyosoma au kuisikia kuwa ina maana gani.
2.
Wahusika,kazi
yeyote ya fasihi inakuwa na wahusika wake ambao matukio mbali mbali yanayohusu
jamii huwazungukia wahusika ni watu ama viumbe, waliokusudiwa wawakilishe tabia
za watu katika kazi za fasihi. Kwa upande mwingine wahusika ni muhimu sana
katika kutoa na kufikisha dhamira kwa hadira iliyokusudiwa na mwandishi.
3.
Mandhari,
kazi ya fasihi inakuwa na mandhri ambayo huonyesha tukio linaponyika. Mandhari
hiyo inaweza kuwa ya kubuni au ya kweli.Mandhari husaidia kujenga hisia
inayokusudiwa na mwandishi.
4
.
Utendaji, utendaji hasa katika fasihi simulizi hushirikisha fanani na
hadhira kwa wakati mmoja. Vile vile utendaji humfanya fanani aweze kuonyesha
baadhi yamatendo katika usimulizi wake.
5
Fani na maudhui,kazi za fasihi zina sehemu mbili yaani fani na maudhui
na sehemu hizi zinafungamana. Maudhui ni kile kinachosemwa na fani ni namna
kinavyosemwa. Kazi nyingine za Sanaa vile vile zinafanikisha ujumbe kwa hadhira
lakini mbinu na vifaa vinavyotumika ni sehemu ya fasihi. Kwa ujumla kazi za
kifasihi, fani na maudhui yake ni ya hali ya juu sana ukilinganisha na Sanaa nyinginezo.
KWA VIPI FASIHI NI
SANAA ?
Usanaa wa fasihi hujitokeza katikavipengele mbali mbali kama
ifuatavyo:-
1. Mtindo, Sanaa katika fasihi hujidhihirisha
katika namna kueleza jamii (mtindo) katika kueleza jambo kunakuwa na aina
fulani ya kiufundi ambao mwanafasihi huutumia katika kufikisha ujumbe kwa jamii
yake. Taarifa inayotolewa inaweza kufichwa katika fumbo, shairi, kitendawili,
tamthiliya au hadithi.
2. Muundo (mpangilio maalumu wa matukio),katika kazi ya fasihi, matukio
yanapangwa kiufundi ili yaweze kuwasilishwa vizuri kwa jamii husika. Matukio
hayapangwi ovyo ovyo tu bali yanakuwa na mpangilio maalumu.
3. Utenzi mzuri wa lugha iliyojaa nahau,
misemo, methali, tamathali za semi,taswira na ishara mbali mbali unaonyesha wazi usanaa wa
fasihi. Lugha itumikayo katika fasihi ni ya kisanaa. Ni lugha iliyopambwa na
inayokusudiwa kuibua hisia za namna Fulani kwa hadhira yake. Lugha hiyo inaweza
kuchekesha, kukejeli, kubeza, kuchokoza, kutia hamasa au kushawishi. Matumizi
ya lugha yako ya aina tofauti, kuna tamathali za semi, misemo, nahau, methali.
Lugha ya wahusika hasa lahaja zao, uchaguzi wa msamiati,ufundi wa kutoa maelezo
hasa ya wahusika ya mandhari na matukio, uteuzi wa lugha yenyewe itumiwayo.
4. Uundaji wa wahusika, wahusika huwa na tabia
zinazotofautiana kati yao. Wanaundwa kiufundi sana na msanii anaweza kuamua
anataka wahusika wanaowakilisha tabia na matendo fulani tu katika jamii na kwa
hiyo atawaumba wahusika hao ili kukamilisha nia na lengo lake.Katika kutofautisha
tabia na hali za wahusika, mwandishi analazimika kutumia mbinu ya kuwapa majina
wahusika wake. Wahusika wanaweza kuumbwa kinafsi au kiakili na kimwili.
Kutokana na ujenzi wa aina hii mhusika huonyesha wasifu wake wa ndani na nje au
anaweza kuonyesha mabadiliko yake kila anapokutana na mazingira tofauti.
5. Ujengaji mzuri wa Mandhari, fasihi hujengwa katika mazingira
maalum. Mandhari husaidia sana kujenga hisia inayokusudiwa na mwandishi.
Mandhari yanajengwa kiufundi na mwandishi ili yasaidie katika kujenga kazi
nzima ya fasihi.
FASIHI KAMA CHOMBO CHA
UKOMBOZI
Ukombozi ni
harakati za jamii yoyote zenye lengo la kuitoa jamii hiyo kwa nguvu (kwa
silaha) au kwa mazungumzo kutoka katika makucha ya watumwa
kisiasa,kiuchumi,kimawazo na kiutamaduni.Jamii inaweza kuwa ni ya kitumwa
kisiasa ikiwa haitakuwa na fursa ya kushika hatamu ya uongozi wao na badala
yake ikategemea uongozi kutoka kwa jamii nyingine jamii itaitwa ya kitumwa ,kiuchumi,ikiwa
haitakuwa na haki ya kuendesha njia mbalimbali za uzalishaji mali.Pia jamii
isiyoweza kufikiri na kuamua wala kutokuthamini mawazo yake yenyewe na badala
yake ikawa katika mgawanyiko wa ibada na itikadi za kigeni ni jamii isiyo huru
kimawazo vile vile jamii haitakuwa huru kiutamaduni ikiwa itakosa kuthamini uaminifu,uumbaji
na ugunduzi wake yenyewe badala yake ikasujudu amali zilizo na chimbuko kutoka
nje.Nyanja za ukombozi wa jinsi fasihi ya Kiswahili ilivyozitazama mpaka leo
(a)Kisiasa
Ukombozi
wa kisiasa unapatikanaje?
Unapatikana
tu baada ya kupigania uhuru wa bendera kuwa ndio wa kwanza kupatikana kwa nchi
ambayo iko katika harakati za kujikomboa.Katika maandishi ya mengi fasihi
ukweli huu unajitokeza kwa mfano katika utenzi wa uhuru wa kenya
msanii anatuonyesha juu ya vita vya
kumng’oa mkoloni kutoka katika kiti cha uongozi kwanza baada ya mwafrika
kupandisha bendera yake mambo mengine yafuate vilevile katika utenzi wa uhuru
wa Tanganyika na utenzi wa jamhuri ya
Tanzania “mwandishi anasisitiza uhuru wa bendera ukielezwa kuwa kabla ya
ukombozi wa aina nyingine kufuata.
Kwa hiyo
ukombozi huu wa mwanzo (uhuru wa bendera) husababisha uhuru wa kisiasa wanchi
kisha uhuru wa kisiasa huwa ni jukwaa la ukombozi wa uchumi na mambo
mengine,vitabu vingine vinavyozungumzia ukombozi wa kisiasa ni mzalendo,F.E.MK
Senkero) Ubeberu Utashindwa(J.K Kiimbila),Tone la Mwisho(E.Mbogo),Kinjikitile
na Mashetani(E.Hussein),Nuru mpya(R.Rufeshobya)
(b)Kiuchumi
Uhuru wa
bendera ni sehemu ya mwanzo tu wa ukombozi wa jamii nchi zinaweza kujidai ni
huru kumbe uchumi wake bado ungali mikononi mwa nchi nyingine.Nchi nyingi
zinazoendelea bado ziko katika harakati hii ya kutaka kujikomboa
kiuchumi.Waandishi wengi wa fasihi ya Kiswahili
wamezungumzia sana suala la uchumi katika mfano ‘’Mashairi ya Azimio la
Arusha’’ mwandishi anaonyesha na kushambulia unyonyaji ambao ni adui wa
uhuru wetu.
Vilevile
waandishi wanasisitiza kufanya kazi kama njia ya kuimarisha uchumi.Pia
wameeleza kuwa unyonyaji unaweza kukomeshwa kwa kutaifisha njia zote za
uzalishaji mali na kuwa mikononi mwa umma. Pia Katika tamthiliya ya “Bwana
Mkubwa”
(J.P Mbonde) mwandishi ameonesha kuwa kwa sasa shabaha yetu sisi ni kupigana
na ukoloni mambo leo ili kupata uhuru kamili.Ukoloni mambo leo ni kikwazo cha
ukombozi wa kiuchumi. Kwa sababu ya ulegevu wa uhuru wa kisiasa nchi inaweza
kuwa na mali lakini ikizembea kufanya
kweli ipasavyo yaweza kufanyiwa njama na ukoloni ndio maana upo umuhimu wa
bidii katika kazi na uzalishaji wa mali kisha linafuata swala la ulinzi wa mali
hiyo.
Kuzikomboa
njia za uzalishaji mali hakutoshi kwani kila hila zao zisizoisha wakoloni
wanaweza wakatupora mali hiyo tunapaswa kuwa macho.Katika utenzi wa “Zindiko
la ujamaa” mwandishi anaeleza utaifishaji wa njia kuu za uchumi na
uhalali wa utaifishaji huo. Mwandishi anaonyesha kuwa utaifishaji huo ulifanywa
si kwa kuwaona wakoloni kuwa wanadhuluma bali kama njia moja wapo ambayo
itaongeza kwenye ukombozi wa kiuchumi katika jamii. Lengo moja ni kufuta
ubinafsi ambao unapelekea tofauti za kitabaka na badala yake manufaa ya umma
kwa ujumla.
Ukombozi wa
kiuchumi si utaifishaji wa njia za uzalishaji mali tu na wala si kukomesha
ukabaila na ubepari bali ni kuongeza juhudi katika kazi mbali mbali ili
kuongeza kiasi cha pato la kitaifa. Waandishi wengine wanazungumzia ukombozi wa
kiuchumi ni kama vile, “Nuru mpya” (G. R. Ruteshubya) “Mashetani”
(E. Hussein) “Sauti ya dhiki” (A. Abdallah) “Kasri ya mwinyi fuad” (Shafi Adam
Shoji) Zetu bora mkulima na wasifu wa sili binti saad(S. Robert).
C) Kimawazo
Ukombozi
wa kimawazo ni uhuru wa mtu katika upeo wa fikra pasipo kutegemea mtu mwingine.
Hapa mtu aliye huru awe anajiamini mwenyewe na awe mtu kama watu wengine. Awe
mwenye uwezo wa kuwaza, kuamua na kutenda, kuchanganua na kupanga kama watu
wengine. Mtu aliye mtumwa wa kimawazo anaweza kufananishwa na mnyama wa
kufugwa. Mnyama wa kufugwa daima ni mtumwa na bwana wake wakati wote huongojea
amri kutoka kwa bwana wake.
Maandishi
ya fasihi yanazungumziakwa upana swala hili la uhuru wa mawazo . Katika riwaya
ya “Njozi za usiku” dhana hii ya utumwa wa kimawazo ipo ndani ya watu wengi
ambao wanashikilia hasa baada ya maajilio ya elimu iliyokuja pamoja na ukoloni
na ikatumika kwa upotofu. Katika riwaya hii msanii anaonyesha kuwa wale
waliosoma walidharau kazi zote za mikono, walifikiri kuwa kazi za mikono
zinafaa kwa wale ambao hawakusoma. Wao wanafikiri kuwa kazi ya mtu aliyesoma ni
kushika kalamu na kuandika tu au kuwasimamia ambao hawakusoma.Tangu uhuru wa
Tanzania kumekuwa na harakati za kufutilia mbal ukanganyifu wa namna hii katika
mawazo ya watu. Mawazo ya namna hii ndio yamekuwa yakiwafanya watu wengi wa
hali ya chini waamini kuwa uchumi walionao wamepewa na Mungu.
Vile vile
kimawazo watu waliamini kwamba kila jambo lilitokana na watawala wa kizungu
lilikuwa ni bora kabisa. Kwa mfano hata majina yliletwa toka Ulaya nay a kwetu ya asili kuachwa. Haya
yanajadiliwa wazi katika tamthiliya ya “Bwana mkubwa” (J. P. Mbonde)
Katika
ukombozi wa kimawazo kuna swala la ukombozi wa mwanamke na swala la dini.Katika
suala la ukombozi wa mwanamke watu wengi wanalitazama kirahisi jambo hili.
Wengi wanadhani kuwa mwanamke hana haki ya kujibagua kutoka kwa wanaume na
kujipigania haki yake. Watu hawa hawaelewi ni mapinduzi gani ambayo hawa
wanapigania.Katika fasihi ya Kiswahili Shaban Robert amewatetea wanawake katika
kazi zake mbali mbali ikiemo Diwani ya”Wasifu wa siti binti saad” na siku ya watenzi
wote. Shaban Robert amemtazama mwanamke kama mtu anayestahili utu kama watu wengine wowote wale.
Katika
kitabu cha “Wasifu wa Siti binti Saad” msanii au mwandishi anaeleza wazi jinsi
jamii ilivyomfanya mwanamke kama chombo cha kutunzwa utawani ili kiwe kizuri
kipate kuwavutia wanaokitafuta na baada ya kutoka utawani kikawa mikononi mwa
mwanaume kikamtegemea kwa hiyo mwanamke alikuwa ni mtu aliyechukuliwa kama hana
wajibu wowote wa maana Zaidi ya kuwa mtegemeaji. Lakini Shabn Robert aliona
kuwa ( uk 23) “Ukimdumisha mtu leo utamuona juu ya kilele cha utukufu kesho.
Mawazo ya mwandishi
ni kwamba wanawake ni vyema watazamwe katika hali zao za maisha katika ubaya na
uzuri kama wanaume. Kuhusu suala la dini linajitokeza katika riwaya ya “Kichwa
maji” ambapo mwandishi anaona dini imeanzishwa na waoga ambao
hutawaliwa na milango yao ya fahamu badalaya kutawaliwa na akili au bongo zao.
Jambo muhimu
katika kumkomboa mtu kimawazo ni kwamba ikiwa dini itaendelea kuwepo isiwe na
mtazamo duni na finyu na athari zake ambazo alikuja nazo mkoloni akidai kuwa
tamaduni zetu ni za kishenzi. Sharti elimu ndiyo iwe ya kutafakari na kugeuza
mfumo wa maisha ya jamii.
Katika dini
pia kuna madhehebu mbali mbali ambayo kati yao kuna uhasama mkubwa, muislamu
anadai kuwa yeye ni bora Zaidi kuliko mkristo na mkristo anajiona yeye ni bora
kuliko muislamu. Madhehebu yote haya yamechimbuka huko mashariki ya
kati…….katika kitabu cha “Bwana mkubwa” (uk 18-19”)……kwanini basi
mlitutenganisha katika vikundi vidogo vya madhehebu tofauti kati ya wakristo na
waislamu iwapo Mungu ni yule yule mmoja leo mnatueleza tuombe kuungana,
utengano alianzisha nani? na kwa faida ya nani?........mbona babu zetu
walimwabudu Mungu wao toka zamani kabla ya ujio wa wazungu.
Kwa ujumla
dini imechangia kwa kiasi kikubwa sana katika kudumisha mtu kimawazo na
kumfanya atumie fahamu tu kwa hiyo katika kumkomboa mtu kimawazo sharti suala
la dini litupiwe jicho kali fasihi inazidi kuona jicho lake.
(d)Kiutamaduni.
Kwa ujumla
utamaduni wanchi zilizotawaliwa na ukoloni umeathiriwa sana na ukoloni huo watu
wa nchi hizo wanazipoteza kidogo kidogo thamani za utamaduni zao.Katika fasihi
ya Kiswahili ukweli huu wa mambo yameoneshwa katika kitabu cha “Njozi za Usiku” mwandishi
wa riwaya hii ameelezea namna vijana wote hasa waliosoma hawataki kabisa kusikia
kuhusu mila na desturi zao (uk 51).Hadi leo vijana wengi wakiwa kwao (vijijini)
na ikatokea kwamba kuna ngoma za kienyeji zinachezwa wao husimama mbali au
kando wakitazama kwa dharau mambo yanayotendeka mbele yao.Wanaamini kabisa kuwa
ngoma hizo ni za kishenzi ngoma ambazo zinafaa kuchezwa na watu wasiosoma watu
wasio staarabika.
Katika
riwaya ya “Kichwa maji” mwandishi ameonesha jinsi isivyo kawaida kwa msomi au watu wenye cheo
serikalini kucheza ngoma za kienyeji lakini vijana hao hao mwanzoni wasomi
wenye mwazo ya kisiasa wakisikia sehemu fulani kuna mziki au disko watajitahidi
sana ili wasikose kufika huko.Kwa sasa kuna mtindo mwingine wa kupaka madawa ya
kujichubua ngozi waonekane weupe na wengine huvaa nywele za bandia au maiti ili
kuficha nywele zao za kipilipili.Huu wote ni utumwa wa kimawazo kwa upande
fulani watu hawa wanaamini kuwa uzungu ndilo shina la maarifa, watu hawa
hawajui kwamba kuna wazungu wengine ni maskini zaidi hata kuliko sisi wenyewe.Hivyo
ili tujikomboe katika nyanja hizi ni lazima tuondoe ubinafsi, uroho wa madaraka
na ulevi wa madaraka hapa nchini.
KAZI ZA FASIHI KATIKA
MIFUMO MBALIMBALI
Kwa kuwa
mwanadamu ni alfa na Omega wa Fasihi ni dhahiri kuwa maendeleo yake yanahusiana
na maendeleo ya fasihi.Hata hivyo sio kila maendeleo huwa na mafanikio mazuri
na hivyo si kila fasihi inatoa mawazo mema.Fasihi kama zao la jamii huenda
sambamba na maendeleo ya jamii
yanayotokana na kazi na fasihi
hujitokeza katika Nyanja zote za kimaendeleo ziwe za kisiasa,kiuchumi,na
kiutamaduni.Safari ndefu ya kimaendeleo imo katika mifumo mitano (5) ya
uzalishaji mali.Mifumo hiyo ni kama ifuatayo:
Fasihi katika mfumo wa Ujima
Huu ni mfumo wa mwanzo kabisa wa maisha ya
binadamu.Fasihi ya kipindi hiki ilikuwa fasihi ya uzalishaji mali.Mfumo wa
ujima haukuwa na matabaka ya watu hivyo fasihi ya wakati huo ilijishughulisha
na manufaa na maslahi ya watu wote Katika jamii.Katika mfumo huu fasihi na
sanaa ni vitu vilivyokuwa vimefungamana na mahitaji ya kukidhi haja ya lazima
ya watu. Fasihi katika kipindi hiki ililea amali za jamii ambazo zilikuwa ni KAZI na USAWA yaani Fasihi ililinganishwa
na kazi.Hata hivyo kutokana na uduni wa uvumbuzi wa kisayansi na
kiteknolojia,Fasihi ya wakati huo iliilea jamii katika jamii katika kutawaliwa
na nguvu za jamii na mazingira.Katika kipindi hiki fasihi haikuwa kitu cha
anasa.Mazingira ya wakati huo yalikuwa ya kiuhasama sana,hayakuruhusu kuwepo na
anasa ya aina yeyote ile.Kutokana na mazingira hayo Fasihi ilizuka kuwa silaha
mojawapo ya mapambano hayo.
Fasihi katika mfumo wa Utumwa,
Mfumo
huu ulitawaliwa na utabaka ambapo kulikuwa na mabwana na watumwa wao.Mfumo huu
uliruhusu baadhi ya watu kuishi kwa jasho la wengine.Watu hao waliishi maisha
ya anasa kutokana na ziada ya mali iliyozalishwa na watumwa wao.Katika mfumo
huu uzalishaji mali umewekwa migongoni mwa watu wa tabaka la chini la
watwana.Katika shughuli za kisanaa,mfano upande wa ushairi ,watu wa matabaka ya
mabwana waliwekewa watwana na
kuwaburudisha kwa kuwaimbia nyimbo na
mashairi.Fasihi nyingi zilikuwa zaile za kuwatukuza mabwana;zinazotukuza
utumwa.Fasihi nyingi za wakati huu zilitumiwa ili kuendeleza itikadi za
kibwana.
Pia kulikuwa na fasihi inayopinga mfumo huu wa
kinyonyaji.Watumwa wanaotumiwa kuwa vyombo vya kuzalisha mali,wanatunga
visa,hadithi,mashairi na nyimbo za kupinga mfumo wa kitumwa.Mara nyingi mabwana wenye watumwa iliwabidi wawasake na
kuwatenganisha watumwa wenye historian a lugha moja iliyowaruhusu kutunga
fasihi ya pamoja iliyelea hoja na hisi zao za kupinga unyonywaji huo.
Kugunduliwa
kwa maandishi kulileta sura mpya kwa upande wa fasihi ya wakati huo.Uandishi
ulikuwa kwa watu wa tabaka la mabwana tu;nao ulielekezwa katika kutoa kazi za
fasihi zinazotetea maslahi ya tabaka hilo.Kutokana na ugunduzi wa maandishi
watunzi walianza mfano kukaa na kupanga juu ya vina na mizani katika
ushairi.Kalam na karatasi zilitumika keneza mitazamo na itikadi za
kibwana.Falsafa na mitazamo ya kiulimwengu wakati huo ilielekezwa huko katika
kuulinda na kuuhalalisha mfumo wa kitumwa.Kwa mfano,mwanafalsafa
Aristotle,katika falsafa zake,alisisitiza na kuhalalisha utumwa kwa kueleza
kuwa kuwa ilikuwa amri ya MUNGU kwamba watu wengine wawe watumwa na wengine
wawe mabwana.
Hatimaye
mfumo huu wa kitumwa ulianza kutetereka kwa mikinzano mbalimbali.Biashara
ambayo hustawi sana katika hatua za mwanzo za mfumo huu zilianza kufilisika
.Wakati huo huo watumwa hujizatiti na kupinga vikali sana utumwa wao.Watu ambao
hapo awali walikuwa na mali zao chache kama vile mashamba na ambazo
walinyang’anywa na mabwana wenye watumwa,nao waliungana pamoja na watumwa
katika harakati za kuupinga utumwa.
Katika
hatua hii ya kukata roho kwa mfumo huu wa kitumwa ,ulitumika kama chombo
kimojawapo cha kiitikadi cha kupinga mfumo huo.Tanzu mbali mbali za fasihi kama
vile hadithi,ushairi,nyimbo n.k zilielekezwa katika harakati hizo.
Fasihi katika mfumo wa kikabaila (Kimwinyi)
Ni
mfumo ambao uhusiano wa kitabaka unakuwa
kiwango cha juu kabisa.Tabaka tawala la makabaila linamiliki njia zote za
uzalishaji mali yaani kiuchumi na kiutamaduni.Njia za kiuchumi hutawaliwa kwa mbinu mbalimbali za kukodisha mashamba.Mfano aliyekodishwa
anapangiwa kutoa fungu kuba sana kwa mwenye shamba wakati wa mavuno.Mtwana wa
wakati huu hutofautiani sana na mtumwa wa kipindi cha mfumo utumwa.Fasihi ya wakati
huu anatawaliwa na falsafa zinazojaribu kuhalalisha uhusiano huo wa wenye
mashamba na njia nyingine za uzalishaji mali na wale wasio na chochote
isipokuwa jasho lao.Fasihi ya kipindi cha ukabaila iliweka msisitizo kuusu
mapambo yasiyo na maana;msisitizo ambao unaathiri kazi ya fasihi pia.Mfano
katika utenzi wa Al-Inkishafi(1810) mwandishi anasema;
37. Nyumba zao mbake zikinawiri,
Kwa taa za kowa na za sufuri,
Masiku yakele kama nahari,
Haiba na jaha iwazingiye.
38. Wapambiye sini ya kuteuwa,
Na kula kikombe kinakishiwa,
Kati watiziye kuzi za kowa,
Katika mapambo yanawirije.
Katika utenzi huu,Sayyid Abdallah
A.Nassir anatuusia kuhusu maisha na ametumia lugha ya picha ya maisha ya uozo
wa wafalme wa Pate kama kielelezo cha uzuri usio na kifani wa maisha ya hapa
duniani.Halafu anaonyesha jinsi ambavyo maisha haya anayoyaona kuwa uzuri
mwingi yanamalizikia katika kaburi ambako miili ya hao wafalme inakuwa chakula
kikubwa cha funza.Uozo wa maisha ya mamwinyi wa pate umeibua Fani na Maudhui ya Al-inkishafi
(1810)
Pia katika Utendi wa mwanakupona (1962) mwandishi anamuusia binti yake kuwa
ajikubali kuwa pambo mbele ya mume wake.Anasema;
38. Na kowa na kuisinga,
Na nyee zako kufunga,
Na asmini kutunga,
Na firashini kutia
39 Nawe ipambe libasi
Ukae kama arusi,
Maguu tia kugesi,
N mikononi makoa.
41. Pete sikose za ndani,
Hina sikome nyaani,
Wanda sitoe matoni,
Na inshini kuitia
Katika
utendi huu mwandishi anamuasa mwanamke aweke na kuelekeza akili yote kwenye
kujipamba ambapo kwa kufanya hivi kumemfanya mwanamke abaki katik nafasi duni
sana katika jamii;nafasi ya chini ya kuonekana,kujiona na kujikubali kuwa pambo
la kuufurahisha moyo na jicho pamoja na uchu wa mwanamume.
Pia mfumo huu unamdanganya akubali kumtumikia
na kumtii mume wake bila kumbishia wala kumjibu kwa lolote lile
atakalosema.Mwanamke anaaswa kwamba amtii na amuogope mume wake;
28. Keti naye kwa adabu,
Usimtie ghadhabu,
Akinena simjibu,
Itahidi kunyamaa,
36. Mpumbaze apumbae,
Amriye sikatae,
Maovu kieta yeye,
Mungu atakulipa.
Katika ubeti wa 36 wa utenzi huu inaonyesha
wazi kuwa dini ilitumika kama taasisi kubwa ya kudumisha na kuhalalisha unyonyaji
na mgawanyiko wa jamii katika matabaka ya watu.Katika utenzi huu,binti anausiwa
kuwa afuate yote anayoambiwa na anayoamriwa
na mume wake kwani yote ni amri ya MUNGU.Hapa tunagundua athari za
kitabaka zilizojikita katika dini na mafundisho yake.Athari hizo zinazidi
kumdidimiza na kumkandamiza zaidi na
kumfanya mtu duni sana.
Katika mfumo huu maisha huwa ya kibiashara
na yaliyozingwa na imani kubwa juu ya pesa.Pesa
zinaanza kuabudiwa katika mfumo huu,nazo hujitokeza katika nyuso mbalimbali za rundo la utajiri
wa makabaila.Katika utenzi wa sundiata jambo hili linajitokeza waziwazi mwandishi
anaelezea kuhusu utajiri wa wafalme kama vile Mansa Mussa.Mfumo huu wa
kikabaila haukuendelea kuwapo muda wote. Mikinzano ambayo daima huwapo baina ya
wanyonyaji na wanyonywaji ,pamoja na nguvu za vibwanyenye uchwara ambao
walikwishaumbika katika harakati za kitabaka.Upande mmoja wa harakati hizo walikuwepa wakulima wanyonywaji pamoja na vibwanyenye ambao daima wamekuwa
wakijitahidi kuangusha mfumo huu wa kikabaila ili badala yake wakite mizizi ya
kibepari.Nguvu zote hizi za kiuchumi na kisiasa
hatimaye kuuangusha mfumo wa kikabaila.
Katika kipindi hiki pia fasihi ilikuwa chombo
kilichosaidia kuendeleza harakati za kuuangusha mfumo wa kikabaila wakati
makabaila waliitumia fasihi kueneza na kuendeleza itikati zao za
kikabaila,papohapo wanyonywaji nao pia walitunga fasihi yao inayoeleza hisia
zao,taabu zao na umuhimu wa kujikomboa.Kwa wakulima fasihi yao ilikuwa ndiyo
silaha ya kifasihi na kwa vibepari uchwara piawalikuwa na fasihi yao ya kupinga
ukabaila na kutetea umuhimu wa kuwa na mfumo mpya wa maisha yaani mfumo wa
kibepari.Mfano wa fasihi ya Kiswahili ya wakati huo ni kama vile; Utenzi wa fumo liyongo (1913) ambap
awali utenzi huu ulielezwa kwa njia yam domo tu.Kwa watu wa tabaka la chini
waliosimulia kisa hiki cha liyongo kilionekana kuwa cha kusifu ushujaa wa mtu
huyo lakini papo hapo liyongo alikuwa mtetezi na mpenda watu wanyonge.
Fasihi katika mfumo wa kibepari
Fasihi
ni zao la jamii na hufungamana na mfumo wa maisha ya jamii na pia ulifungamana
n mapambano ya kudumu dhidi ya mazingira ,yaani kiuchumi,kisiasa na
kiutamaduni.Katika mapambano hayo dhidi ya mazingira kulikuwa na mitazamo
tofauti ya fasihi.Pia fasihi ilionekana kuwa ni silaha mojawapo kati ya silaha
nyingi zilizotumiwa na tabaka moja kutetea maslahi yake kwenye mapambano ya
kudumu ya kitabaka katika jamii
Katika
ubepari kuna matabaka mawili ya watu yaani wenye mali wanaoshikilia rasilimali
zote na wanyonge wasio na kitu.Fasihi ya kibepari ilielezea uzuri wa fedha kwa
sababu pesa iliabudiwa sana katika mfumo huu.Waanii wa kipindi hiki ni wale
walionuia kupata pesa,wasanii hawa walivaa uso wa udanganyifu huku tegemeo lao
kubwa ni gunia la fedha,unyang’anyi na umalaya.Mfumo hu umefanikiwa kuwatenga
waandishi na jamii zao.Wengi wametunga kazi zao za fasihi ambazo maudhui
yake,dhamira na lengo lake pamoja na fani
kama vile Mzimu wa watu wa kale (1958),Kisima cha giningi (1958),Siri ya sufuri
(1974),Duniani kuna watu (1973),Mwana wa Yungi hulewa (1976), na Kosa la Bwana
Msa (1984) zaidi wasanii hawa walishighulikia suala la kusisimua
msomaji na kumpumbaza kwa visa vya upelelezi.Fasihi ya kibepari iliifumba macho
jamii isiione machungu yanayoisakama
jamii.Fasihi hii huwafumba macho watu (jamii) ili wasione udanganyifu
ulioshamiri katika jamii hiyo.Huwaficha wagandamizaji na kuwapa nguvu za
kumiliki jamii kisiasa ,kiuchumi,na kiutamaduni ili kuendeleza matabaka yanayo
wanufaisha wachache.
Fasihi ya kibepari haikomboi watu kimawazo ili
waweze kuchambua na kutambua jamii yao kwa jicho pevu.Haiwachochei
wanaogandamizwa kukataa machungu yanayosababisha na wagandamizaji
wachache.Katika mfumo huu fani huwa kubwa kuliko maudhui yaliyopatikana
humo.Kazi a fasihi iliyo nzuri ni ile ambayo fani na maudhui huwa katika uwiano
ulio sawa.Fani isaidie kuyaweka maudhui katika hali nzuri ya kueleweka kwa
jamii.
Fasihi katika mfumo wa kijamaa
Mfumo
huu huu ulibuniwa na Marx na Angels ambao walidai kuwa mfumo huu utatetea na
kuleta kheri kwa umma.Fasihi ya mfumo huu itakuwa ya kunufaisha umma na kulinda
amali na hali ya jamii.Matunda ya kazi huwa kwa faida ya wote.Usawa,utu na
kuheshimiwa ndiyo msingi wa fasihi ya kijamaa.Fasihi ya kijamaa ni ya jamii
nzima ambapo huiangalia jamii kisiasa,kiuchumi na kiutamaduni.Huyamulika
matatizo ya jamii.Ni chombo cha kuunganisha,kuadibu,kuhimiza,kuongoza na
kushauri jamii katika lake la kufuta unyonge na uchafu unaoikabili jamii.
Fani na maudhui katika fasihi ya kijamaa ni
vitu ambavyo hufungamana kwa mtazamo wa jumla.Fasihi lazima iwe wazi ili watu
wa ngazi zote waweze kuelewa na kuzichukua fikra nzuri zilizomo.Uhuru wa
kuikosoa na kuichambua jamii ni wazi kwa fasihi hii,tofauti na fasihi ya
kibwenyenye ambayo uhuru huu haupo.Hivyo basi, fasihi iliyo ya kweli ni ile inayoelewesha
umma katika mapambano yake dhidi ya mazingira,kuikosoa jamii,na kuielekeza
jamii katika ukombozi wa kweli.Fasihi ya dhati ni sharti iendeleze shabaha
zilizofikiwa na umma yaani wakulima na wafanyakazi.
MADA NDOGO-3; UHURU WA MWANDISHI/MTUNZI WA KAZI ZA KIFASIHI
Dhana ya
uhuru wa mwandishi ni pana sana na inatazamwa kwa kuangalia vipengele kadhaa
kama ifuatavyo:
Mosi,uhuru wa mwandishi uko katika utashi,Bila utashi mwandishi atakuwa mwoga
na mwepesi wa kukata tamaa.Atayumbishwa haraka kutoka kwenye msingi wa falsafa
yake na Imani aliyo nayo juu ya mabadiliko yatokeayo katika jamii.Makombora ya
wahakiki na wanasiasa huweza kumyumbisha, lakini kwa mwandishi mwenye utashi
makombora hayo humkomaza.
Baadhi ya
waandishi walioonyesha utashi wao katika Afrika ni ‘Ole Soyinka na Ngugi wa Thiongo
waandishi hawa wameshambuliwa sana na wahakiki, lakini misimamo yao ni ile ile,
pia wamewahi kufungwa na walipotoka kifungoni hawakubadili misimamo yao na
wamekuwa hivyo kwa sababu ya utashi wa falsafa zao katika fasihi ya kiswahili,
waandishi wenye utashi wapo na msingi wa kuwepo kwao ni kutoyumbishwa na
matamshi ya jukwaani na wahakiki ambao hawajapevuka.
Pili,uhuru wa mwandishi
umo katika kuwa na falsafa moja inayoeleweka, Falsafa ifanyayo maandishi ya mwandishi moja yawe na kitu
kijulikanacho kama lengo.Waandishi waliotajwa hapo juu yaani Ole
Sanyika na Ngugi wa Thiongo ndio wanaongoza kuwa na falsafa zao
zinazojulikana. Katika fasihi ya Kiswahili tunaona waandishi wachache wenye
falsafa zao inayojulikana wengi tulio nao wanaandika kufuatana na jambo fulani
au tukio la wakati huo bila kulinganisha leo ataandika juu ya mapenzi, kesho juu
ya upelelezi na kesho kutwa mapinduzi mwishowe anakuwa na orodha ndefu ya
vitabu visivyokuwa na lengo.Waandishi wachache tulio nao ambao wameelekea kuwa
na falsafa inayoongoza maandishi yao ni kama Shaban Robert, G.Kezilahabi na
Mohamedi Suleiman.Bila kuwa na falsafa maalumu ni rahisi sana mwandishi kuyumbishwa.
Tatu,uhuru wa mwandishi umo katika kuitawala vema Sanaa yake,kama unaandika riwaya na hujui
misingi ya Sanaa ya aina hiyo atajikuta katika kikwazo,utajikuta uhuru wa
kisanaa unaweza kujaribu, lakini kazi utakayoitoa itakuwa hafifu.Kazi nzuri ya
kisanaa ni ile inayounganisha vema ubunifu na uhalisia.Mwandishi akielemea sana
katika ubunifu anazua matatizo mengine kazi ngumu aliyonayo mwandishi ni katika
kupata barabara msitari huo.Mwandishi mwenye vitabu vingi anaweza kuwa na
kitabu kimoja tu kilichoupatia vema mstari huo. Katika fasihi ya Kiswahili
waandishi walioupatia msitari huo tunao ni kama vile Ebraim Hussein,Penina
Mhando,Mohamed Suleiman, C.G Mng’ong’o na J.A.Safari.Msanii anayeweza
kuitawala vema Sanaa yake anaunganisha
vizuri Sanaa na maudhui yake.
Mwisho, uhuru wa mwandishi
umo katika lugha anayotumia,ili msanii atawale vema Sanaa yake nilazima ajue
lugha anayotumia.Lugha
ndicho kiungo maalumu kati ya Sanaa na kazi ya kifasihi mwandishi kama hajui
vema lugha anayotumia atajikuta hana uhuru wa kukisema anachotaka kwa hiyo
lugha ndiyo nguzo ya nne katika uhuru wa mwandishi, waandishi wa Kiswahili waliokwisha kutajwa wanakitawala Kiswahili
sanifu,Kiswahili sanifu ndiyo msingi wa fasihi ya Kiswahili.
Ni
kweli kuna uhuru wa mwandishi?
Uhuru
wa mwandishi ni nini?
Ni
ile hali ya mwandishi wa fasihi kuwa huru na wazi katika kutoa mawazo au hisia
zake kwa jamii.Ni uhuru wa kuandika na kulikosoa tabaka lolote katika jamii
bila kupata matatizo yoyote.
Mwandisihi ni nani?
Ni mtu
yoyote atumiaye muda wake mwingi
kuandika na kuzungumzia jamii yake kwa njia ya maandishi.
Je kuna uhuru wa
mwandishi?
Kwa ujumla
uhuru wa mwandishi ni uhuru ikiwa hakufaulu kudhuru tabaka tawala hii ni kwa
sababu suala la uhuru wa mwandishi ni la kitabaka na lilianza pale jamii
ilipogawanyika katika matabaka kwa maana hii uhuru wa mwandishi unaamuliwa na
tabaka tawala
Kuanzia enzi
za utumwa, maandishi ya liyovumbuliwa katika fasihi andishi ya mwanzo ilikuwa ya wateule wachache
tu na wenye vyeo vyao.Hao mabwana, wamwinyi na mabepari walihakikisha kila
mbinu inatumika ikiwemo ya udhibiti wa maandishi ili kuendeleza na kulinda
utawala wao.
Naye B.Goya (1974-78) anasema kuwa mwandishi hana uhuru
kwa vyovyote vile kwa sababu yeye ni tokeo la jamii Fulani, kila jamii ina
mipaka yake ambayo mtu hatakiwi kukiuka kwa vyovyote vile mwandishi huyu
amebanwa na mipaka hiyo asivuke.Pindi avukapo mipaka hiyo atapambana na jamii
hiyo (tabaka tawala) vitabu vya mwandishi huyo vitapigwa marufuku au vitabu
vikitolewa havitanunuliwa au serikali itavikusanya na kuvifanyia mipango
mwingine. Katika Afrika kuna mifano
mingi ya udhibiti wa waandishi mfano mzuri ni mwandishi maarufu wa Kenya Ngugi
wa Thiongo ambaye kazi zake hasa ya “Ngaahika Ndeenda”(I will marry
when I want)- Nitaolewa Nitakapotaka, ilimgombanisha na vyombo vya dola
hadi akawekwa kizuizini, Ngugi ni mwandishi wa kwanza kufichua siri za mfumo wa
kibepari kwa watu wanyonge aliliuzi tabaka tawala la jamii yake ambalo
halikusita kutumia udhibiti na vyombo vyake vya Mabavu.
Baada ya
uhuru vitabu vingi sana viliandikwa kwa kudhibitisha maandishi mbalimbali
uliojitokeza waziwazi E.Kazilabi aliandika riwaya “Rosa
mistika”(1971),kitabu hiki kilipigwa marufuku kisitumike mashuleni na
wala kisiuzwe waziwazi madukani.Ilidaiwa na waliokipiga marufuku kuwa kilikiuka
maadili ya jamii kwa kueleza mambo ya aibu kwa wazi.Sura ya kumi ndiyo hasa
ilitolewa mfano wa uchafu wa kitabu hiki.Udhibiti huo ulifanywa na Wizara ya
Elimu na ulizusha maswali mengi kwa wasomaji.Wasomaji walianza kujiuliza, Je si
kweli uchafu uelezwao katika “Rosa mistika” umo ndani ya jamii ya
Tanzania? Je upotofu na uongozi mbaya ulifuchuliwa na riwaya hiyo hii si upo
kati yetu? Kwa baadhi ya wasomaji ilielekea kuwa suala la uchafu wa maelezo
yatokeayo kitandani baina ya wakuu wa chuo na wanafunzi wao lilitumika kama
kisingizio tu cha kudhibiti ukweli wa masuala mengine nyeti yaliyowagusa
viongozi yaliyowakilishwa na watu kama vile Bwana Maendeleo Deogratius
anayeshiriki katika kuwaharibu vijana.
Vitabu
vingine ambavyo havieleweki vinasema nini, maudhui, falsafa na ujumbe wa
mwandishi ni mashetani(E.Hussein) “Aliyeonja Pepo”(F.Topan) na “Ayubu” Paukwa
theatre Association.Na hivi viko kwa kukwepa mkono mrefu wa tabaka
tawala.
DHIMA YA UHURU WA MWANDISHI.
·
Mwandishi
atakuwa huru kuikosoa jamii au tabaka
lolote litakaloenda kinyume na utaratibu wa jamii bila matatizo.Mwandishi
atakuwa huru kuonyesha dhuluma, ukatili na ujangili unaofanywa katika jamii na
tabaka lolote bila matatizo yoyote.
·
Kukiwa
na uhuru wa mwandishi, msanii atakuwa na
falsafa inayoeleweka pamoja na utashi wake.Hii itamfanya mwandishi awe na
msimamo unaoeleweka.Msimamo wake utamsaidia
kuifundisha na kuielimisha jamii bila uoga.Ataijiulisha jamii hali yake na
ataonesha jamii njia za kufikia haja na kutatua matatizo ya jamii bila uoga
·
Mwandishi
atakuwa huru kutoa mwongozo katika jamii kwa kuikomboa jamii kutoka katika
fikra mbovu za kugandamizwa,kunyonywa na kuonewa na tabaka tawala ili jamii ipate
haki na heshima bila woga wa kuliondoa tabaka ambalo ndilo lenye mamlaka yote
katika jamii.
·
Uandishi wa kikasuku utapungua, waandishi au wasanii huacha tabia ya kuwa vipaza sauti vya
tabaka fulani katika jamii, wasanii makasuku huandika mambo bila kufikiri na
kurudiarudia mawazo yaliyokwisha semwa
na wanasiasa majukwaani bila fikra mpya kwa hali hii hupotosha jamii.Hivyo
kunapokuwa na uhuru wa mwandishi wa kutosha hali hii haiwezi kutokea kwa sababu
mwandishi ataandika mambo mbalimbali yanayojitokeza katika jamii na hataweza
kujikomba au kujipendekeza kwa tabaka tawala lenye mamlaka yote katika jamii.
·
Kunapokuwa
na uhuru wa mwandishi fasihi inakuwa chombo cha kuikomboa jamii
kiuchumi,kisiasa, kiutamaduni na kifikra (kimawazo). katika jamii ya kitabaka
fasihi ni mali ya tabaka tawala na hutumia fasihi kutetea na kulinda maslahi
yao.Hivyo inapokuwa mali ya jamii nzima inatumiwa na jamii hiyo katika
kuwakomboa wanajamii wote.
·
Kunapokuwa
na uhuru wa mwandishi, mwandishi anakuwa huru kuichokoza na kuisukasuka (kuichochea)
jamii
bila matatizo yeyote. Mwandishi atachokoza jamii ya wakulima na
wafanyakazi kufikiri ili waweze kulichunguza tabaka tawala kwa jicho pevu na
kutoa hadharani uozo uliopo katika kunyonywa, kupuuzwa,kuonewa, kugandamizwa na
kunyanyaswa na tabaka tawala
·
Mwandishi
atakuwa huru kuelimisha na kuishauri jamii katika mambo muhimu yanayojitokeza
katika jamii bila woga.Mwandishi ataishauri jamii kuhusiana na mambo kama vile
afya, elimu na ichague mambo gani yanafaa kuhifadhiwa na yapi hayafai vile vile
msanii anakuwa huru kuirekebisha jamii bila woga kwa kuangalia yapi ni mazuri
na yapi ni mabovu yanayotendeka katika jamii
MADA NDOGO-4;MASUALA YA KIITIKADI NA DHANA YA UDHAMINI
KATIKA KAZI ZA FASIHI
Maana ya Itikadi
Itikadi ni Imani ya watu au jamii
fulani juu ya kitu fulani. Itikadi kisiasa ni mfumo wa mawazo na Imani ambao
umewekwa na tabaka tawala/ tawaliwa au tabaka lolote lenye nguvu katika jamii
inayohusika ikiwa na lengo la kulinda, kutetea na kuendekeza matakwa na maslahi
yake. Utaratibu huo unaambatana na umilikaji wa njia kuu za uchumi na umilikaji
wa mapato ya ziada yatokanayo na jasho la wazalishaji mali hizo, nyenzo za
kitaaluma kama vile elimu ni nyenzo zisaidia kuimarisha itikadi kama vile dini
vinatumika kutetea utaratibu uliowekwa na tabaka tawala.
Kimsingi kuna mitazamo miwili ya kiitikadi:-
i)
Itikadi inayotetea na kulinda maslahi ya watu
wchache tu katika jamii (utumwa, ukabaila na ubepari)
ii)
Itikadi inayotetea na kulinda maslahi na matakwa
ya watu wengi katika jamii (ujima na ukomunisti).
Vile vile tunapojadili juu ya itikadi katika fasihi na usemi kwa ujumla
pia tunaongelea juu ya utabaka uliopo katika jamii inayohusika . Kuna matabaka
ya aina mbili:-
a)
Tabaka tawala
b)
Tabaka tawaliwa
·
Tabaka tawala linamiliki vyombo vya dola na kwa
kutumia vyombo hivyo na kwa kutumia waandishi, tabaka tawala linaunda,
linaendeleza na kutetea maslahi yake.Vile vile tabaka tawala lina nguvu za
kiakili na za kielimu kwa manufaa yao. Mwandishi kwa ujumla hawezi kuepukana na
mfumo huo wa kitabaka. Tabaka fulani huwadhamini waandishi kwa njia mbali
mbali.
UDHAMINI
Ni hali ya watu au shirika fulani kutoa fedha kwa ajili ya
kugharamia kitu fulani . Mdhamini au wadhamini ni kundi la watu wenye shabaha
zinazofanana wenye kusimama kama ufadhili wa mradi fulani. Katika fasihi hawa
ni wale wanaosimamia makundi maalumu kipropaganda na kiitikadi.
AINA ZA UDHAMINI
Kuna udhamini wa aina
mbili:-
i)
Udhamini wa ushawishi
ii)
Udamini wa nguvu
Ø
UDHAMINI WA USHAWISHI
Ni aina ya udhamini ambao mdhamini huwashawishi na kuwanunua
waandishi au wasanii. Matokeo yake ni kwamba msanii anafungwa na matakwa ya
mdhamini.
Ø UDHAMINI WA NGUVU
Huu ni udhamini unaotumia vyombo
vya dola kama vile jeshi, polisi, magereza kumdhamini mtunzi au mwandishi n.k.Hakuna
hiari katika udhamini wa nguvu, kila kitu kinaendeshwa kama vile mashine tu.
Kwa ujumla mwandishi akidhaminiwa kwa nguvu za serikali huwa kama kasuku
aimbaye na kuutukuza mfumo wa maisha uliopo katika jamii hata kama roho na moyo
wake viko mbali sana na mfumo huo. Lakini msanii anapodhaminiwa kutetea umma,
lazima kutakuwa na madhara yake katika jamii yake inayohusika.
Mwandishi wa fasihi katika kila nchi atakuwa na udhamini
unaolingana na mazingira yake kwa mfano katika nchi ya Tanzania, mwandishi
anaweza kuandika kwa udhamini wa jamii yake inayohusika.Mdhamini anaweza kuwa mtu
binafsi mwenye fedha, shirika, chombo cha serikali, chama fulani au kundi la
mataifa kwa ushirikiano. Pia mdhamini ni mwakilishi wa wenye mamlaka juu yake,
kwa mfano katika serikali yaTanzania chuo kikuu ni mwakilishi wa serikali na
serikali ni mwakilishi wa tabaka tawala. Hivyo msanii anayedhaminiwa na chuo
kikuu ambacho ni chombo cha serikali hatimaye anajikuta anafanya kazi ili
kuendeleza maslahi ya tabaka tawala.
SABABU ZA UDHAMINI
Ø
Uhaba wa fedha kwa waandishi za kuendeshea
shughuli zao za uandishi katika uandishi wa kazi za fasihi. Pesa zinahitajika
kwa ajili ya kununulia karatasi, kalamu, uchapaji n.k.
Ø
Kulinda na kutetea maslahi yawadhamini wao. Hii
inatokea zaidi kama mdhamini ni wa tabaka tawala. Kama tabaka linalo tawala ni
la mabepari kazi za fasihi zitatetea tabaka hilo.
Ø
Kujulikana au kuipendekeza. Baadhi ya waandishi
hudhaminiwa kwasababu ya kutakakujulikaa na kwa upande mwingine mdhamini
anawadhamini waandishi kwa lengo hilo.
Ø
Kupata fedha za haraka. Hawa huandika vitabu
vyenye kujaa wahusika wakuu, mafundi wa kufanya mahaba, kutumia madawa ya
kulevya na kufanya mapenzi kwa kutumia mipira ya kiume na kike bila kujali
staha utamaduni wa jamii yake. Mwandishi anachojali hapa ni pesa na sio matakwa
ya jamii yake.
Ø
Kulazimishwa na tabaka tawala. Waandishi hawa wanakubali
udhamini huo kwa kuogopa udhabiti wa kazi zao na tabaka tawala. Waandishi hawa
wakikataa udhamini huo kazi zao zitadhibitiwa na kupigwa marufuku zisisomwe au
kuchapishwa kabisa.
UMUHIMU WA
UDHAMINI
·
Husaidia waandishi chipukizi katika kuchapisha
kazi zao.
·
Husaidia waandishi katika kufanya utafiti wa
mambo mbalimbali yatakiwayo katika Sanaa hiyo ya fasihi.
·
Husaidia jamii kupata kazi mbali mbali za
kifasihi.
·
Husaidia
kuleta ushindani wa ubora wa kazi katika soko la kazi za fasihi.
·
Husaidia
kuinua vipaji hasa vya waandishi chipukizi.
ATHARI ZA UDHAMINI
Ø Mwandishi anayedhaminiwa anatakiwa
kuandika yale tu ambayo mdhamini wake anayataka. Msanii hatakuwa na uhuru wa
kuandika kitu chochote na kwa njia anayotaka.
Ø Mapana ya uandishi wake kidata, kigiografia na kimaudhui huamuliwa na
mdhamini na kutegemea
mahitaji yake na kiwango cha fedha alichonacho mdhamini.
Ø Ufafanuzi wa data na maudhui ya kazi ya fasihi lazima ulingane na mtazamo
wa itikadi ya mdhamini.Hii ina maana kuwa mwandishi wa kazi ya fasihi hawezi kufanya ufafanuzi
wa data na maudhui mwenyewe bila kumshirikisha mdhamini.
Ø Matokeo ya uandishi wa kazi za fasihi mara nyingi ni mali ya mdhamini na
hutumia kuendeleza
maslahi yake mabayo sio lazima yalingane na malengo ya mwandishi.
Ø Wasanii au waandishi wengi kutokana na kudhaminiwa huanza kuandika kazi
zao kwa kupenda pesa
hii huwafanya waandishi kuwa makasuku kwasababu ya kuandika yale tu yasemwayo
na mdhamini wake bila kuyafanyia uchambuzi wa kina.
Ø Udhamini hukuza utabaka katika jamii, hapa tunakuwa na tabaka la wenye nacho (mdhamini) na
tabaka la wasionacho (msanii) mdhamini humnyonya msanii.
Ø Kuzuka kwa fasihi pendwa (riwaya ya pendwa).Hapa waandishi huandika kazi zao kwa
lengo la kupata pesa za haraka, huandika riwaya pendwa ambazo zina soko kubwa
hapa nchini hasa kwa vijana na wakati huo huo riwaya hizo hazifunzi lolote
jamii Zaidi ya kuburudisha.
Ø Huchochea rushwa, hii ni kwa sababu waandishi wengi wanataka udhamini huo na matokeo yake
wale wanapata udhamini huo lazima watoe chochote (rushwa) kwa mdhamini.