KISWAHILI IV-NADHARIA YA USHAIRI
Ushairi ni sanaa inayojipambanua kwa mpangilio maalum wa
maneno fasaha na yenye muwala, kwa lugha ya mkato, picha au sitiari au ishara
katika usemi maandishi au mahadhi ili kueleza jambo,wazo au tukio au hisi
fulani kuhusu maisha, mazingira ya binadamu kwa namna inayogusa moyo.
Ushairi ni utanzu / fani mojawapo ya fasihi ambao umbo lake
hutofautiana na tanzu nyingine za fasihi, mathalani tamthiliya na riwaya na
riwaya.
Utanzu huu una historia ndefu iliyojikita katika fasihi
simulizi za jamii zilizohusika. Kutokana na historia yake ndefu ni jambo la
kukubalika kuwa hapana budi kuwepo na mabadiliko ambayo yamechimbuka kutoka
kipindi kimoja kwenda kingine.
Baadhi ya mabadiliko yaliyochimbuka katika ushairi ni hali
ya kuwa na MASHAIRI HURU/ MASIVINA/ YA KISASA amabayo hayafuati kanuni za
kimsingi ambazo washairi wa awali WANAJADI/ WANAMAPOKEO wananazizingatia.
Ushairi wa Kimapokeo na Masivina:
Kuna tofauti
kubwa kati ya utenzi, shairi la kimapokeo na masivina. Nazo zaweza kuwa hivi;
Utenzi
|
Shairi
la kimapokeo
|
Masivina
|
Utenzi hugawanyika katika beti zenye
idadi sawa ya mistari.
|
Hugawanyika kama utenzi katika beti
mbalimbali na katika idadi sawa ya mistari.
|
Kuna beti mbalimbali lakini idadi ya
mistari inatofautiana mara nyingi kutoka kifungu hadi kifungu.
|
Kwa kawaida utenzi unagawanyika ama
kuundwa na mistari minne katika ubeti.
|
Laweza kuwa na mistari miwili, mitatu
na kuendelea katika ubeti kufuatana na matakwa ya msanii.
|
Si rahisi kutaja idadi ya mistari
katika ubeti mmoja wa shairi kwani hutofautiana mara kwa mara.
|
Mistari hugawanyika katika mizani
ambayo huwa kati ya 8 na 12.
|
Mistaari hugawika katika mizani na
maranyingi huwa 16 lakini si chini ya mizani 11.
|
Mizani uwepo lakini hutofautiana
kutoka mstari hadi mstari.
|
Utenzi una vina vya mwisho
vinavyofanana.
|
Lina vina vya kati vinavyofanana na
vya mwisho vinavyofanana. Navyo vyaweza kufanana kwa shairi zima au la.
|
Urari wa vina haujipambabui sana kama
ilivyo katika shairi la kimapokeo.
|
Beti zake hazijitoshelezi, mawazo yake
yanaendelezana kutoka ubeti hadi ubeti.
|
Ubeti mmoja hujitosheleza hivyo waweza
kuwa na shairi la ubeti mmoja tu.
|
Maana ya shairi hupatikana baada ya
kulisoma shairi lote.
|
Kimsingi utenzi huwa mrefu kuliko
shairi la kawaida nao mara nyingi huelezea tukio moja kwa kirefu sana.
|
Mara nyingi haliwi refu sana na
linaweza kuwa na ubeti mmoja.
|
Mara nyingi huwa na urefu wa wastani.
Yanafanana na mashairi ya kimapokeo.
|
Utenzi katika usimulizi wake mara
nyingi huanza na dua au kumaliza na dua
|
Si jambo la muhimu sana ingawa baadhi
ya wasanii hufanya hivyo
|
Dua halijitokezi katika masivina.
|
Sanaaa hii ya ushairi yaweza kujipambanua katika;
·
Tenzi
·
Nyimbo
·
Mashairi
·
Ngonjera.
ISTILAHI ZA KISHAIRI
Istilahi ni
maneno yanayotumika katika uwanja fulani maalum. Sanaa ya ushairi ina istilahi
zake, nazo ni kama vile;
v Utoshelezi:
Katika arudhi ya
kimapokezi, kila ubeti unahitajika kuwa na maana kamili inayojitosheleza au
inayojisimamamia bila kutegemea ubeti unaofuata au unaotangulia na vile vile
kuwa na mtiririko mzuri wa habari zinazoelezwa.
v Muwala:
Ni mtiririko wa mawazo na
fani na mantiki katika shairi. Muwala unaweza kuwa wa namna mbili. Mosi,
inapasa mawazo katika kila ubeti yawe yanafuatana kwa ufasaha kutoka mstari wa
kwanza hadi wa mwisho.
Pili shairi liwe na
mtiririko mzuri wa mawazo kutoka ubeti hadi ubeti katika shairi.
v Ubeti:
Ni mgawo wa vifungu
katika shairi, utenzi, wimbo au ngonjera unaojitosheleza kimaana. Huu ni ubeti
wa shairi:
1. Hicho ni kitu nasema, maarufu
duniani,
Si kikubwa chake kima, si
kidogo wastani,
Tena ni kitu cha nyama,
kina ladha mdomoni,
Nyama nje ngozi ndani, ni
kitu gani wajuzi?
v Mshororo:
Ni mstari katika ubeti wa
shairi, tenzi au ngonjera. Katika mashairi ya arudhi inapasa mishororo iwe na
idadi ya mizani iliyo sawa.
Ubeti ulioainishwa hapo
juu una mishororo minne.
v Kipande:
Ni sehemu za mshororo wa
ubeti wa shairi ambazo hutenganishwa na
alama ya mkato. Mwishoni mwa kila kipande katika mshororo huwa kuna kina. Mashairi
mengi huwa na vipande viwili katika kila mshororo.
v Mizani:
Ni silabi ambazo zimo
katika kila mshororo wa kila ubeti. Mfano:
Hi-cho
-ni- ki-tu- na-se-ma, ma-a-ru-fu du-ni-a-ni
v Vina:
Hizi ni silabi
zinazofanana ambazo hujitokeza mwishoni mwa kila kipande katika kila mshororo
wa ubeti.
v Kituo:
Huu ni mshororo wa mwisho
katika ubeti wa utungo wa shairi. Maneno ya kituo yaweza kuwa yanayokaririwa
kutoka ubeti hadi ubeti ambayo huitwa BAHARI, yanayobadilikabadilika kutoka
ubeti hadi ubeti ambayo huitwa KIMALIZIO au yanayobadilika kwa kipande kimoja
kutoka ubeti hadi ubeti ambayo hitwa NUSU BAHARI.
DHIMA YA USHAIRI
Ushairi una umuhimu
mkubwa sana katika jamii. Kwanza ulikuwa unatongolewa kama fasihi simulizi
katika jamii nyingi za kiafrika. Baada ya mabadiliko ya kihihstoria, kiuchumi
na kisayansi ulianza kuandikwa kama fasihi andishi.
Ushiri hutegemea mapigo
au mahadhi yanayotumika kuweza kuibua hisi mbalimbali ambazo humfanya msomaji/
msikilizaji aone furaha au huzuni. Kwa muhtasari tu dhima za ushairi ni:
ü Kuibua hisia na kuburudisha au
kuhuzunisha
ü Kuadhibu
ü Kuweka kumbukumbu/ kuhifadhi amali za
jamii
ü Kukuza na kuhifadhi lugha
ü Kunoa fikra
ü Kuelimisha
ü Kuhamasisha
MAMBO
YANAYOJENGA USHAIRI WA KIMAPOKEO ( KI-ARUDHI)
FANI
A. MUUNDO
Ni msuko, umbo au uwiano wa vipengele vyote vinavyojenga ushairi. Ushairi
waweza kuainishwa kimuundo kwa kuzingatia.
·
Idadi
ya mishororo:
Ø Tathnia:
Ni ushairi wenye beti
zenye mishororo miwili kwa kila ubeti. Shiri la tathnia huwa na urari wa vina
na mizani.
Mfano:
Ingawa ni nchi yangu, mie siipendi
sana,
Ina tando na ukungu, kadha mawimbi
mapana,
Ø Tathlitha:
Ni ushairi wenye
mishororo mitatu kwa kila ubeti. Tathlitha pia huitwa UTATU.
Mfano:
Nakupa waswia, moyo shika mno,
Niloyakimbiya, henda penye sono,
Yangalikujiya, usinene neno.
Ø Tarbia:
Ni ushiri ulio na
mishororo minne kwa kila ubeti. Tarbia pia hufahamika kama UNNE. Kidesturi
shairi la tarbia huwa na mishororo iliyogawanyika katika vipande viwili.
Wakati mwingine mshororo
wa mwisho wa tarbia huwa na utaratibu wa kuteua vina vinavyotofautiana na vina
vya mishororo mitatu inayotangulia.
Ushairi huu ndiyo kwasi
na maarufu kuliko aina/ miundo yote katika utanzu wa ushairi kiasi kwamba
unahatarisha uhai wa miundo mingine ya kishairi.
Ø Takhmisa:
Ni ushairi wenye
mishororo mitano katika kila ubeti. Ushairi huu pia huitwa UTANO au TAKHMISI.
Zipo takhmisa ambazo
zilitungwa zikiwa hazina mgawo wa vipande viwili kama ilivyozoeleka sasa na
zikiwa na mizani kufikia 15.
Mfano:
Moyo siwe pite kama jua mwendawazimu
Kwanda tafakari umbo lako ulifahamu
Ni tone la mayi lalokaa likawa damu
Tei Tabaraka lahu kaliumba Mola
Karimu
Katia mifupa na mishipa ngozi na
nyama.
Ø Tasdisa:
Ni utungo wenye mishororo
sita katika kila ubeti. Huitwa pia USITA, TARDISA, TASHLITA.
Utungo huu si maarufu
sana katika ushairi wa Kiswahili. Tungo hizi kama vile tungo za mistarisaba,
nane,tisa, kumi au kumi na mbili hazina mifano mingi.
Mfano:
Ikinipasa kungoja, mpaka nijue
vema,
Pasivumbuke mmoja, kwa makosa
kunisema,
Daima hautakuja, tukawa hivi daima,
Sitatenda neno moja, kwa kuchelea lawama,
Na
jambo hili lafuja, hata kidogo si jema,
Mtenzi
hahofu hoja, wala lawama ya nyuma.
Kigezo
kingine cha kuainisha muundo wa kazi ya kishairi ni;
·
Idadi
ya vipande:
Ø Mashairi ya vipande viwili ( manthawi ):
Mara nyingi mashairi huwa
na vipande viwili; kipande cha kwanza na cha pili.
Mfano;
Ewe la azizi, uloniepuka,
Kama mkimbizi, anavyotoroka,
Rejea mpenzi, bado nakutaka.
Ø Mashairi ya vipande vitatu ( ukawafi
)
Yapo mashairi mengine
yamejengwa kwa vipande vitatu.
Mfano:
Mja hana haya, haya hazimo, mwake
usoni
Mja ni mbaya, hutimba shimo, ungiye
ndani
Na ukishangiya, azome zomo, furaha
gani
Mmoja kwa miya, ndiye hayumo, baya
kundini.
Ø Ushairi wa kipande kimoja ( utenzi )
Mizani ya mishororo huwa michache
toka 4 hadi 12. Kwa kawaida utungo huu una vina vya mwisho bila vya kati.
Utenzi husimulia habari ndefu tena nzito. Pengine huwa juu ya tukio Fulani,
maelezo ya mtu mashuhuri, historia au visa.
Mfano:
Mali ukishika,
Ukitoa sadaka,
Budi takukuka,
Kwa Mola jalia.
Mbali ya
idadi ya mistari, vipande pia KITUO ni kigezo kingine cha kuainisha muundo wa
kazi za kishairi.
·
Kituo:
Hutumiwa kumaanisha
mshororo wa mwisho katika ubeti wa utungo wa ushairi. Aina za kituo hutegemea
maneno yanavyotumika katika mshororo huo.
Kama maneno ya kituo
yanakuwa yaleyale yanayokaririwa kutoka ubeti hadi ubeti huitwa BAHARI au
kibwagizo.
Tena kama
yanabadilikabadilika kutoka ubeti mmoja hadi mwingine huitwa KIMALIZIO.
Wakati mwingine maneno ya kipande
kimoja hubadilika na kipande cha pili hubaki vivyo hivyo kutoka ubeti mmoja
hadi mwingine. Kiyuo hiki huitwa NUSU BAHARI.
B. MTINDO:
Ni tabia ya utunzi au uandishi na huhitilafiana kati ya mtunzi na mtunzi
ambayo hutegemea ufundi, hisia na ufanisi wa mtunzi.
Katika mtindo mhakiki huangalia yafuatayo;
v Pindu:
Ni mbinu amabayo sehemu
ya neno la mwisho au neno la mwisho katika mshororo au kipande huanzisha mshoro
au kipande kingine.
Mfano:
Nyayo, kanyagio umekanyaga mwiba,
Mwiba, ni mwiba hasa si kijiba,
Si kijiba, na wala siyo mbigili,
Siyo mbigili, bali mchongoma,
Kuutoa ndio ngoma!
v Kikufu:
Ni tabia ya kiutunzi
ambapo neno la mwisho au kipande cha mwisho katika kituo cha ubeti uliotangulia
linakuwaneno la kwanza au linaanzisha mshororo wa ubeti unaofuatia.
Mfano:
Mcheza hawi kiwete, kilema
kilomshika,
Lau mchezo wa kete, angezila pasi
shaka,
Au kama kibafute, ushindi
angeushika,
Mcheza hawi kiwete, ngoma yataka
matao.
Ngoma yataka matao, huchezwa kwa kudemka,
Kwa
maringo na pumbao, mwili wote kunyumbuka,
Haichezwi kama bao, komwe zako kupangika,
Ngoma yataka matao, mcheza hawi
kiwete.
v Kidato:
Ni mbinu ambayo mshororo
mmoja aghalabu wa mwisho hufupishwa kwa sababu maalum.
Mfano:
Dhuluma isipoondoka, kwa amani,
Na haki zetu kukoseka, kuwa shani,
Lazima twalazimika, tuamuweni,
Turudi mwituni, tuwe vitani,
tuwasakeni,
Damu tumwaeni.
v Malumbano:
Ni mbinu ya kiutunzi amabyo
mshairi anatoa maoni au anashiriki katika mjadala fulani wa kishairi. Mbinu hii
huonekana zaidi katika magazeti.
Mfano:
Wa ubani Bawaziri, na Kandoro
kadhalika,
Lumbano la kishairi, gazetini
kuliweka,
Nami nimejikusuri, maoni kuyatamka,
Ua si ruwaza njema,tunzo ya mtu
kupewa.
v Maswali:
Ni mtindo ambao mshairi
huandika shairikatika namna ya kuhoji jambo.
v Majibizano:
Ni mtindo unaojitokeza
zaidi kwenye kipera cha ngonjera ambapo wahusika wawili au zaidi hujibizana.
Mfano:
KAKA
Kusoma nilikosoma, nambiwa sipati
kazi,
Yapata mwaka mzima, nategemea
shangazi,
Wasioujua husema, sababu sina
ujuzi,
Huo uhaba wa kazi, mesababishwa ni
wake.
DADA
Mbona watuingilia, kaka acha
ubaguzi,
Likukeralo twambia, tulijuwe
waziwazi,
Au unalochukia, ni wake kufanya
kazi?
Mambo ya kisiku hizi, watu ni bega
kwa bega.
v Taabili:
Ni mtindo ambao shairi
huandikwa katika namna ya kumlilia mtu au kuomboleza aliyefariki.
Mfano:
Amina umejitenga, kufa umetangulia,
Kama ua umefunga, baada ya
kuchanua,
Nakuombea mwanga, peponi
kukubaliwa,
Mapenzi tuliyofunga, hapana wa
kufungua.
v Kiitikio:
Ni mbinu nyingine ambayo
kazi ya kishairi huwa na kibwagizo. Mbinu hii hujidhihirisha zaidi katika
kipera cha nyimbo.
Mfano:
Rabi utubarikie, la wawili pendo
letu,
Rehemu tuzidishie, zisafike nyoyo
zetu,
Roho zetu zitulie, tusitamani vya
watu.
Kibwagizo:
Nia yangu sigeuzi, kupenda
anipendaye,
Ajue nitamuenzi, milele taishi
naye.
v Takriri( kikwamba ):
Ni tabia ya kurudiarudia
neno/ maneno katika nafasi maalum katika mshororo katika beti.
Mfano:
Duniani, vyakula hawavioni,
mafakiri,
Lakini, vyakula, kwao pomoni,
mabepari,
Abadani, hawa si waja wa Mungu.
Duniani, wanalala majiani,
mafakiri,
Lakini, wanalala ghorofani,
mabepari,
Abadani, hawa si waja wa Mungu.
Duniani, nguo mbovu matakoni,
mafakiri,
Lakini, nguo tele kabatini,
mabepari,
Abadani, hawa si waja wa Mungu.
v Masimulizi:
Ni mbinu ambayo shairi
huandikwa au kuimbwa katika mtindo wa usimulizi.
Mfano:
Hadithi inayokuja, ni ya sungura
sikia,
Hadithi uliyongoja, leo
ninakuletea,
Alitoka siku moja, njaa aliposikia,
Njaa aliposikia, sungura nakuambia.
v Ukara:
Ni mtindo ambao vina vya
kipande kimoja vinabadilika wakti vya kipande kingine vinakaririwa ubeti mmoja
hadi mwingine katika shairi.
Mfano;
Nyuki ni mtanashati, umbo na zake
tabia,
Yeye yu kila wakati, vichafu
kuvikimbia,
Mchana na lailati, hatui kwa
kukosea,
Kuntu Sauti ya Kiza, nyuki hapendi
vichafu.
Nyuki hatui topeni, na zizini
kuingia,
Sijamwoni karoni, mikojo kufakamia,
Haingii na chooni, hata kwenye
mazulia,
Kuntu Sauti ya Kiza, nyuki hapendi
vichafu.
v Mtiririko:
Ni mtindo ambao vina vya
mwanzo na vya mwisho vinakaririwa kutoka ubeti mmoja mpaka mwisho wa shairi,
vinakaririwa katika shairi lote.
Mfano:
Nijapotendwa ubaya, na wabaya kiwajua,
Mwenzio huona haya, ubaya
kuwatendea,
Japo moyo una waya, hufanya
kuuzuia,
Nacheka hali najua, Hila zina
maulaya,
Hila zina maulaya, na
wakinishambulia,
Nyama ilooza mbaya, mbesi huifurahia,
Samba huona vibaya, kula kilojiozea,
Japo zogo la ngamia, Hila zina
maulaya.
v Ukaraguni:
Ni mtindo ambao vina vya
mwanzo na mwisho vinatofautiana katika beti katika shairi zima.
Mfano:
Kitedo kimetendeka, onyesho
limetimiya,
Baruti imelipuka, baki ni moshi na
maya,
Taa sasa zinawaka, mwenye macho
angaliya,
Limeanguka paziya, sasa mwaka
ni dakika.
Kariuki kifo chako, ni jogoo
amewika,
Amesikika tuliko, saa ya
kupambazuka,
Kwa kipofu sikitiko, wenye macho
wanacheka,
Pazia limeanguka, tujitafute
tuliko.
C. MATUMIZI YA LUGHA:
Lugha ndiyo malighafi ya
ushairi. Utamu na ubora wa shairi hutegemea mtunzi anavyomudu kuchagua na
kupanga maneno yake ili yalete athari au matokeo aliyokusudia. Hivyo mshairi ni
lazima awe na hazina kubwa ya msamiati.
1. Uteuzi wa msamiati/ maneno:
Uteuzi wa msamiati
huzingatia
a. Kile kinachosemwa.
b. Muktadha wa kisarufi
c. Umbo la shairi.
Kama shairi lina mpangilio wa
vina, maneno yanayoteuliwa kuwa ya mwishoni mwa
mshororo sharti yaishie kwenye
silabi zinazooana na vina vya shairi. Kadhalika maneno
yanyoteuliwa inabidi yaingie katika mfumo wa
urari. Ni vigumu kupunguza, kuongeza au
kubadilisha neno katika shairi zuri bila
kuvuruga muwala wa shairi.
2. Mpangilio wa maneno:
Maneno ya ushairi hupangwa ili kuleta
maana fulani, sauti za aina fulani au urari fulani wa mizani.
Kwa kawaida katika Kiswahili
kivumishi hufuatia nomino lakini kwenye ushairi pengine kivumishi hutangulia
nomino. Mwandishi wa ushairi huweza kubadilisha mpangilio huo kwa sababu
maalum, pengine hufanyika ili kulinganisha vina.
Mfano:
Suu ulimwengu bahari tesi,
Una masaibu na mengi maasi
Mpangilio huu usio wa kawaida huvuta
udadisi kuliko lugha ya kawaida na hutumika kusisistiza vipengele fulani vya
hisi au wazo fulani la msanii ingawa si lazima shairi liwe na m[angilio usio wa
kawaida ili lipendeze kwani vipengele kama taswira vyaweza kuleta athari ya
mguso.
3. Matumizi ya lugha ya picha/ taswira:
Ni matumizi ya lugha yanyopambanuliwa
na uteuzi mzuri wa maneno, ulinganifu na udhahiri wa maelezo wenye kuhusisha na
kujumuisha dhana mbali mbali tofauti ndani ya dhana moja ili kuleta taswira na
athari maalumkatika mawazo ya msikilizaji. Ni mkusanyiko wa picha zinzoundwa
kutokana na maelezo ya msanii katika kazi yake ya kifasihi.
Katika fasihi , taswira kwa kawaida
hujengwa kutokana na matumizi ya tamathali za semi, hasa sitiari na tashbiha na
ishara mbalimbali zenye kuhusu mawazo , dhana, vitu na maumbile.
Mshairi anapotumia taswira huwa na
nia ya kuchochea hisia za msomaji za uoga , furaha, kilio, hasira au kukarahishwa.
4. Tamathali za semi:
Ni umathilishaji wa jambo kwa
kulinganisha au kufnanisha na lingine. Ni viwakilisho au viwakilisho kwa dhana
nyingine au zinavyofanana. Mara nyingi tamathali zinaweza kupanua, kupuuza
amakubadilisha maana za wazi ili kuleta maana maalum katika ushairi.
Tamathali za usemi pia zaweza
kutumika kuipamba kazi ya sanaa ya kifasihi kwa kuongeza utamu wa lugha
iliyotumika. Baadhi ya tamathali hizo ni:
a. Tashbiha:
Ni tamathali ya ufananisho au
mlinganisho wa vitu viwili au zaidi. Hulinganishwa
kwa sura, sifa au tabia kwa kutumia maneno ya ulinganisho.
Mfano.
Kweli ni sawa na radi, inapotoa
kaul…
Kweli kinywani ikawa sawa na mto
Nile…
Kwali kama msumeno, hukereza sawa
kweli.
b. Tashhisi:
Kitu kisichokuwa nauhai hupewa sifa za kitu chenye uhai hasa za kibinadamu.
Kifasihi maelezo ya kitashihisi huwa na upekee unaomwingia mtu akilini haraka.
Mfano:
Kimya hakineni jambo, si kimya
chawatazama
Kimya chajazua jambo, pasiwe
mwenye kusema..
Kimya kipimeni sana, msione
kutosema,
Kimya hakiishi kunena, kitakapo
husimama,
Kimya chaja katakana, kizue
yaliyozama.
c. Mubaalagha au Udamisi:
Aina hii tamathali hutia chumvi sana
mambo yanayoonekana kuwa ya kawaida. Yanatiwa chumvi kwa makusudi ya kuleta
athari maalumu iliyokusudiwa na mwandishi. Angalia sentensi hii.
Nitakuandikia barua za mapenzi
zitakazojaza posta yote ya Jiji.
d. Kejeli:
Ni usemi ambao maana yake ya ndani ni
kinyume na inabeua maana yake halisi. Ni usemi wa kebehi ambao kisemwacho sicho
kikusudiwacho na msemaji.
Mfano:
Huifanya fedha kuwa Mungu wao,
Itazame adha na imani yao!
Na mwenye akili kama hana fedha,
Hatajwi mahali ila kwa rakadha.
Na kuadhieriwa kuwa mtu duni,
Tazama dunia ilivyo na
dini!
e. Sitiari:
Ni tamathali ya semi ambayo athari
zake hutegemea uhamishaji wa maana na hisi kutoka katika kitu au dhana moja
hadi kitu au dhana nyingine tofauti.
Vitu hivyo viwili vyenye kuhusishwa kwa kawaida huwa havina uhusiano wa moja
kwa moja. Sitiari ni picha ingawa picha
si lazima iwe sitiari ila sitiari ni kipengele cha muhimu kabisa katika ushairi
na matumizi yake bora hudhihirisha ubingwa na uwezo wa mshairi.
f.
Takriri:
Ni marudiomarudio ya sauti, silabi,
neno, sentensi au wazo ili kuleta athari na maana maaalum kwa msikilizaji au
msomaji wa shairi hilo. Njia ya kishairi ya kuonesha uzito wa hisia, kusisitiza
wazo au dhamira fulani.
Marudiomarudio haya huvuta hisia na
udadisi na umakini wa msomaji wa shairi ingawa pia kwaweza kumchosha msomaji
kama ufundi hautotumika.
Mfano:
Siku ya panga kufuta,
Mashujaa kwenda kombo,
Siku ya kuja matata,
Na fadhaa na mshindo,
Siku ya watu kuteta,
Kufua moyo mfundo,
Siku ya nchi kutota,
Kwa damu kwenda mkondo…
g. Mjalizo:
Ni mbinu ya kuunda maneno yanayofuatana
bila kuwa na viungo vilivyozoewa kama vile na, kwa, mfano, kama…
Mfano:
Nilikaa, nikashangaa, nikachoka.
Niliimba, nikanuna, nikacheka.
MAUDHUI
Maudhui ni mawazo yanayozungumzwa na msanii wa kazi ya kifasihi
pamoja mtazamo wa mwandishi au msanii juu ya mawazo hayo.
A. DHAMIRA:
Ni wazo kuu
lililomo katika kazi ya kisanaa. Huu ni msukumo alionao mwandishi hata
akaandika kazi fulani ya kifasihi. Msanii anaweza kuwa na lengo la kuonesha
madhara ya ufisadi, matatizo ya ndoa, umaskini, uongozi mbaya au upofu wa
kisiasa.
B. UJUMBE:
Ni taarifa
aipatayo msomaji asomapo shairi au kazi ya kifasihi. Ujumbe unawezwa kutazamwa
kwa njia kuu mbili unaweza kuwa mbaya au wenye mafunzo mabaya au ukawa mzuri.
C. MAADILI:
Haya ni
mafunzo, nasaha au ushauri unaopatikana mara baada ya kupitia kazi Fulani ya
kifasihi.
D. MTAZAMO:
Utetezi
au hali ya kubeza aliyonayo msanii.