KISWAHILI -2- MADA 2 : MAENDELEO YA FASIHI SIMULIZI
MADA 2 : MAENDELEO YA FASIHI SIMULIZI
UWASILISHAJI NA UENEZAJI WA KAZI ZA
FASIHI SIMULIZI
Ni aina ya
fasihi ambayo hutumia mdomo katika kuumbwa, kuwasilishwa na kusambazwa kwa
wasikilizaji wake.
AU
Ni sanaaa
ambayo hutumia mazungumzo na matendo katika kuwasilisha ujumbe uliokusudiwa kwa
watazamaji au wasikilizaji.
Mazungumzo
hayo huwa katika mfumo wa masimulizi kwa kuumbwa, kutambwa, kuganwa au kutongolewa.Fasihi
simulizi hueleza jamii kiutamaduni, kiuchumi na kisiasa. Fasihi huzungumzia juu
ya yale mambo ambayo huzunguka jamii husika na huathiriwa sambamba na mabadiliko ya jamii na
kwa hiyo nayo hubadilika kimaudhui na kifani kufuatia mabadiliko ya mifumo ya
kisiasa, kiuchumi, na kijamii.Fasihi simulizi ni utanzu wa Sanaa ambao hukua na
kubadilika kutokana na mabadiliko ya wakati na mifumo ya jamii.
VIPENGELE MUHIMU VYA
FASIHI SIMULIZI
(a)
Msimulizi (fanani),Huyu huwa ni mtu ambaye anaitamba
hadithi, kuimba wimbo, kusimulia au kutoa vitendawili au methali.
(b)
Wasikilizaji au watazamaji (Hadhira),Hawa ni washiriki katika kutazama au
kusikiliza fani ya fasihi simulizi na mara nyingine huwa wanatumiwa na fanani
kama wahusika katika kazi yake
(c) Mandhari, Hili
ni jukwaa au mahali ambapo tukio la kifasihi (fasihi simulizi)
litatendeka.Pahali au mahali hapo yaweza kuwa nyumbani, uwanjani, kuzunguka
moto, baharini n.k.
(d) Tukio/Dhana inayotendeka,Hili huwa ni tendo linalotendeka katika jukwaa la fasihi
simulizi. Tendo hili laweza kuwa ni usimulizi wa hadithi, kutega vitendawili,
kuimba nyimbo au wimbo au kutoa methali.
SIFA ZA FASIHI
SIMULIZI.
Ø Fasihi simulizi hushirikisha fanani na hadhira katika
utendaji kwa wakati mmoja.Hii humfanya fanani aweze uonyesha baadhi ya
matendo katika usimulizi wake kama vile kutumia viungo vya mwili kwa kuchezesha
midomo, kukunja uso, kubinya macho, kuchezesha mabega n.k.
Ø Fasihi simulizi ina sifa ya kuwepo
kwa fanani ambaye huweza kusimulia kwa kuimba, kusoma kwa sauti au kubadilisha mtindo wa usimuliaji
wake,fanani huweza kufanya yote hayo kama akiona hadhira yake imechoka
kusikiliza.Pia ana uwezo wa kuona kama ujumbe wake umeeleweka au la!
Ø Fasihi simulizi zina sifa ya kwenda
na wakati na mazingira, tabia hii inatokana na jinsi fasihi simulizi inavyoenea wasikilizaji
huwa wengi na hata kama baadhi tanzu za fasihi simulizi zilipitwa na wakati
zinaweza kubadilishwa na fanani ili zisadifu mazingira maalumu ya wakati huo.
Ø Fasihi simulizi huzaliwa, hukua,
huishi hata kufa hii inasababishwa na mabadiliko ya mazingira
ambayo hufuata mfumo wa kihistoria wa jamii, mfano kutokana na maendeleo ya
sayansi na teknolojia ya kuhifadhi fasihi simulizi katika maandishi ya fasihi
simulizi huonekana chapwa kwa sababu ya mambo kama vile miondoko au ngoa,
vinakuwa havimo.
Ø Fasihi simulizi ina uwanja maalumu wa kutendea, Fasihi simulizi huwa na sehemu inayochaguliwa kwa ajili ya
aina fulani ya fasihi simulizi itakayofanywa na wahusika. mfano tambiko huwa na
sehemu maalumu ya kutambikia kama vile sehemu yenye pango,kwenye mti mkubwa kama
vile mbuyu, njia panda, makaburini n.k.Hivyo ni wazi kwamba fasihi simulizi
inahitaji uwanja wa kutendea yenye kuhusisha vitendo.
Ø Fasihi simulizi ni mali ya jamii
nzima.Tanzu zake
zote zikishatendwa humilikiwa na jamii kwa pamoja na hii ndiyo inayopatiwa
uwezo wa kurithishwa kizazi kimoja hadi kingine.Hivyo huwafikia watu wengi hata
wale wasiojua kusoma na kuandika.
MCHANGO WA FASIHI
SIMULIZI KATIKA FASIHI ANDISHI
Fasihi simulizi ina mchango mkubwa sana
katika fasihi Andishi kifani n kimaudhui
A.Kimaudhui,Dhamira nyingi ambazo ndicho kiini
cha maandishi mengi katika Fasihi
Andishi zilikwishajadiliwa katika fasihi
simulizi.Dhamira hizo ni kama vile
Mapenzi,Siasa,Matabaka,Uhuru,Ukombozi,Usawa,Unyonge wa mwanamke,Uchawi na
Ushirikina n.k Fasihi simulizi haijavumbua dhamira mpya kabisa bali
maudhui/dhamira zote za kale.
B. Kifani,Vipengele mbalimbali vya fani ya
fasihi simulizi katika kufikisha ujumbe kwa jamii zao.Vipengele hivyo ni;
1. Muundo,Fasihi simulizi muundo wake ni wa
moja kwa moja pia kuna baadhi ya waandishi wa Fasihi Andishi ambao wametumia
muundo wa moja kwa moja.Mfano Riwaya ya Kuli (1979) ya Shafi A. Shafi Ametumia
muundo wa moja kwa moja.
2. Mtindo,Fasihi simulizi hutumia
mtindo wa masimulizi pia kuna baadhi ya waandishi wa Fasihi Andishi hutumia
mtindo wa masimulizi.Mfano Riwaya ya Shida (1975) ya Balisdya
3. Wahusika,Waandishi wa Fasihi andishi hutumia
wahusika wasio binadamu katika kazi zao ambao kwa kawaida hupatikana katika
fasihi simulizi tu.Mfano Mashetani (1971),Pambo (1975),Adili na
Nduguze (1952) Kusadikika (1951) na Kufikirika (1967) wametumia
wahusika mashetani ambao
hupatikana katika fasihi simulizi tu. Wahusika kama wanyama,majini,mazimwi
hupatikana katika fasihi simulizi tu.
4. Matumizi ya hadithi ndani ya hadithi,hapa wahusika husimulia hadithi mbali
mbali katika fasihi andishi .Hawa husimuliana hadithi za kimapokeo ambapo
hadithi ni kipera cha fasihi simulizi.Mfano Njozi iliyopotea (1980),Lina
Ubani (1984), Mashetani (1971)
5 . Matumizi ya
mtambaji hasa katika tamthiliya,Waandishi wengi wa tamthiliya wametumia mbinu ya utambaji
ambapo wanakuwa na mtambaji anayetamba hadithi fulani.Mfano, Lina Ubani (1984),Nguzo mama (1980),Pambo
(1975)
6.Matumizi ya mianzo ya
hadithi za Fasihi simulizi,Mfano tamthiliya ya Jogoo kijijini na ngao ya jadi(1970) Kilio
Chetu (1995) ,Kivuli kinaishi (1990),Riwaya hizi zimetumia mianzo maalum ya fasihi simulizi mfano
paukwa……,pakawa.
7. Matumizi ya Semi
mbali mbali,Fasihi andishi hutumia semi mbalimbali ambazo ni ni
tanzu za fasihi simulizi.Semi ambazo hutumiwa sana ni
misemo,nahau,methali,tamathali ,vitendawili na tanzu nyingine
8. Matumizi ya Ushauri
na nyimbo,Waandishi
wengi hutumia sana nyimbo katika kazi zao ili kuzipa mvuto,mfano Riwaya ya Njozi
iliyopotea (1980),tamthiliya ya Kilio chetu wametumia sana nyimbo
katika kufikisha ujumbe kwa jamii husika.
MADA NDOGO-1; UWASILISHAJI NA UENEZAJI WA KAZI ZA FASIHI
SIMULIZI
(a) UWASILISHAJI WA FASIHI SIMULIZI
Uwasilishaji hutumiwa
kuelezea njia au mtindo unaotumiwa kufanya kazi ya kifasihi iwafikie walengwa
.Mfano uwasilishaji wa maigizo ni kutendwa kwake jukwaani mbali ya hadhira ya
watazamaji.Tangu zamani, uzalishaji wa tanzu za mbalimbali za fasihi simulizi
huwasilishwa kwa masimulizi ya mdomo na matendo.Fasihi simulizi hubuni hadithi,
nyimbo, methali n.k. zinazobaini hisia zao mbalimbali kuhusu maisha na
mazingira yao.Fasihi simulizi pia inaweza kuzungumzia historia ya watu wa
jumuiya Fulani itikadi zao na mambo mengine mengi wanayoyathamini katika kuishi
kwa pamoja.
Kwa kuwa
fasihi simulizi haiandikwi kuhifadhiwa kwake kunategemea kurithishana kwa mdomo
kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia hii kizazi kimoja kinaweza
kurithisha kizazi kingine yale mambo muhimu ambayo kinataka yaendelee katika
jamii hiyo mambo ambayo yamefungamana na mazingira yao maisha yao utamaduni wao
na itikadi zao.
(b)UENEZAJI WA KAZI ZA
FASIHI SIMULIZI
UENEZAJI:
Hutumiwa kueleza
uhusianokati ya hadithi na jamii mbali mbali.Nadharia hii huonyesha kuwa inawezekana kuwa jamii
zinazohusika ziliingiliana kihistoria au kutokana na ukaribu wao wa kijiografia
n zilihusiana kihistoria. kuingiliana huku kunaweza kuwa msingi wa kuwako kwa hadithi
zinazosimuliwa ambazo zinafanana katika jamii mbalimbali.
Mfano;utenzi wa Fumo Liyongo unapatikana
katika jamii kadhaa za pwani ya Kenya kama waswahili, wapokomo, wabajuni n.k.
Inawezekana kuwa kupatikana huku ni tokeo la ueneaji hasa kwa kuwa hizi ni
jamii zinazokaribiana kijiografia za zilizohusiana kihistoriau
SABABU ZA KUENEA KWA
FASIHI SIMULIZI.
a) Kuanzishwa kwa vikundi vya Sanaa na
muziki,Vikundi mbalimbali vya Sanaa na muziki vilianzishwa
ambavyo kazi yake ni kuendeleza tanzu mbalimbali za fasihi simulizi hapa
nchini.Vikundi vya Sanaa za maonyesho, Vikundi vya taarabu na muziki mfano,
Ottu Jazz Band,Kilimanjro orchestra,Kilwa Band n.k vinafanya kazi kubwa ya
kueneza na kuendeleza fasihi simulizi hapa nchini.
b) Muingiliano na fasihi andishi,Kuenea kwa kazi ya fasihi simulizi
kwa asili ni kwa mdomo na masikio yaani usimulizi, hata hivyo maendeleo ya watu
yamefanya baadhi ya kazi za fasihi simulizi zienee kwa maandishi.Maandishi ni
jitihada za kuhifadhi kazi ya fasihi simulizi na kuifikisha mahali ili
ikatambuliwe au isimuliwe.Hadithi mbalimbali kama vile Hekaya za Abunuasi (1915),Hadithi
za Esopo (1890),Fasihi simulizi ya mtanzania.Hadithi (1977) ,Hizi zote
zimehifadhiwa na kuenezwa kwa maandishi.
Fasihi andishi inatumia vipengele mbalimbali vya fasihi simulizi katika
uandishi wake na hivyo kuviendeleza. vipengele hivyo kama vile ,Matumizi ya
semi mbalimbali,Matumizi ya nyimbo,Matumizi ya hadithi ndani ya hadithi,Matumizi
ya mianzo na mishilizo ya hadithi za fasihi simulizi,Matumizi ya majigambo, utani
n.k.
Kwa sasa methali, vitendawili, nahau, vimewekwa katika maandishi kwa
ajili ya kumbukumbu za baadaye na hivyo vinaenezwa kwa njia ya maandishi.
c)
Ufundishaji shuleni na vyuoni,mfumo wa Elimu nchini nao umesaidia kueneza fasihi simulizi
kwa kiasi kikubwa hapa nchini kwa sasa fasihi simulizi ni somo linalofundishwa
toka darasa la kwanza hadi ngazi za juu (chuo kikuu).Vile vile kuna vyuo hapa
nchini vinavyofundisha baadhi ya tanzu mbalimbali za fasihi simulizi kama vile
Sanaa za maonyesho na muziki. Mfano chuo cha Bagamoyo, Butimba, Nyegezi na chuo
kikuu cha Dar-es-salaam.
d) Mabadiliko ya kiteknolojia,Kutokana na
maendeleo ya Sayansi na Teknolojia kwa sasa fasihi simulizi inaenezwa kwa
vyombo vya habari kama vile kaseti, redio, video, luninga, mitandao ya kijamii
n.k.Mfano Redio Tanzania (TBC) kupitia kipindi chake cha “Mama na Mwana” “Watoto Wetu”
vimesaidia sana kueneza fasihi simulizi hapa nchini Tanzania. Luninga nazo
zimesaidia sana kueneza fasihi simulizi nchini kupitia vipindi mbalimbali vya
michezo ya kuigiza.Hivyo mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia hayawezi kuwa
fasihi simulizi
E)Mwingiliano wa mataifa mengine.Katika mwingiliano muziki umesaidia
sana kukuza fasihi simulizi.Hali hii imesaidia kuleta muziki wa kizazi kipya
(muziki wa kufoka foka) pamoja na Rege
vijana wa kizazi kipya wamechota miundo na mitindo ya muziki kutoka nje
na kuendeleza muziki wao ingawa madhui bado wanajadili yale yale yaliyojadiliwa
na wanamuziki wa zamani.Matumizi ya fasihi simulizi katika Sayansi na
Teknolojia yamesaidia sana kuenea kwa fasihi simulizi kwani fasihi simulizi
inapata hadhira kubwa kwa wakati mmoja lakini hadhira hiyo haionani ana kwa ana
na fanani wao kwa kutumia vyombo hivyo vya Sayansi na Teknolojia.
ATHARI ZA SAYANSI NA TEKNOLOJIA KATIKA UWASILISHAJI NA
UENEZAJI WA KAZI ZA FASIHI SIMULIZI
Mwanzo
fasihi simulizi iliwasilishwa na kuenezwa kwa njia ya masimulizi ya mdomo hivyo
fanani na hadhira walionana ana kwa ana wakati wa uwasilishaji lakini zama hizi
za Sayansi na Teknolojia, uwasilishaji na uenezaji unatumia vyombo vya habari
kama vile redio, video, televisheni, kanda kunasia sauti, mtandao na hata
kompyuta, mara nyingi hasa hadhira haiwi ana kwa ana na fanani hutokea hadhira
ikawa inaangalia luninga au sinema au tamthiliya jukwaani kwenye mazingira kama
hayo si rahisi hadhira kushiriki kikamilifu katika utendaji.Kutokana na
maendeleo ya Sayansi na Teknolojia fasihi inaathiriwa katika vipengele
vifuatavyo:-
·
Uwasilishaji. Mwanzoni fasihi simulizi iliwasilishwa
kwa njia ya masimulizi ya mdomo hivyo fanani na hadhira walikuwa wanaonana ana
kwa ana wakati wa uwasilishaji lakini katika kipindi hiki cha sayansi na
teknolojia, uwasilishaji wa fasihi
simulizi unatumia vyombo kama, vile redio, luninga, video, kanda, mtandao
na hata kompyuta na sio lazima msanii awepo.
·
Uhifadhi, kutokana na maendeleo ya sayansi na
teknolojia sasa fasihi simulizi inaweza kuhifadhiwa vizuri Zaidi kuliko
inavyofikiriwa na wanamapokeo kwani leo
hii fasihi simulizi inaweza kuwekwa katika mkanda wa kompyuta (flash disc) CD,
DVD, Maandishi n.k na ikaendelea kuwepo kwa miaka mingi sawa sawa na fasihi
andishi hata zaidi.Kwa upande wa video na DVD, uhifadhi wake huendelea
kuonyesha vitendo na sauti huweza kudumu hata zaidi ya maandishi.
·
Wakati na mahali, zamani fasihi simulizi ilifanyika
sana saa za jioni, kando ya moto au barazani. Aidha kwa vile fasihi simulizi
hutolewa redioni inaweza kusimuliwa wakati wowote na mahali popote ambapo
kipindi kinasikika na kwa saa na wakati huo. Majumbani, mijini watoto
hawazunguki moto tena, bali husubiri wakati kipindi kinaporushwa kwa siku
maalumu na wanaizunguka luninga au redio.
·
Hadhira au ushirikishwaji wa hadhira, zamani hadhira ya fasihi simulizi
ilikuwa inaonana ana kwa ana na fanani wake wakati wa uwasilishaji wake. Hadhira
iliweza kuchangia kazi ya fasihi hiyo na hata kuathiri uumbwaji wake, ikaitwa
hadhira tende. Lakini katika muktadha wa maendeleo ya sayansi si lazima fanani na hadhira waonane ana
kwa ana .
MADA NDOGO-2 ;UHIFADHI
WA KAZI ZA FASIHI SIMULIZI
Kwa sasa
fasihi simulizi inaweza kukusanywa na kuhifadhiwa kwa njia zifuatazo:-
Ø Kichwa,uhifadhi wa fasihi simulizi ni
katika vichwa vya watu kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Jambo hili limekuwa likifanyika
kwa muda mrefu sana.Hivyo kutokana na kuhifadhiwa katika vichwa ndio maana
fasihi simulizi imekuwa ikirithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kizazi kingine.
Ø Maandishi, Tangu maandishi yagunduliwe baadhi
ya kazi za fasihi simulizi zimekuwa zikihifadhiwa kwenye maandishi kwa ajili ya
kumbukumbu ya baadaye. Kazi za fasihi simulizi zikihifadhiwa katika maandishi
inaweza kufanya watu wasijue ni simulizi au andishi. Hata hivyo vidokezo kadhaa
husaidiakujua kazi za fasihi simulizi kama
vile kuwa na mianzo maalum,mfano “Paukwaa!
Pakawa! Au hadithi…….hadithi njoo” n.k.
Aghalabu fasihi simulizi huwa na mtiririko(muundo) wa moja kwa moja usio na
urejeshi.
Ø Kanda za kunasia sauti (tepu rekoda),Hii ni njia moja wapo inayotumika
kuhifadhi tanzu mbali mbali za fasihi simulizi. Kanda hizo hushika sauti pamoja
na vidokezo vyake, kwa hiyo wasikilizaji ili wapate wanachokitaka lazima
wanunue kanda hizo.
Ø Kanda za video, luninga na filamu z sinema CD, DVD
na Kompyuta/Tanakilishi.Mtandao, picha za video hurekodi sura na
sauti,Picha hizo hutembea na kuonyeshwa kwenye skirini ya video na
lunnga. Picha za sinema hupigwa kwa aina maalumu za kamera ambazo hupiga picha
za mfululizo katika utepe maalumu. Picha hizo huonyeshwa kwa mashine na
huonekana zinatembea, kamera nyingi za
sinema za siku hizi zina mitambo ya kurekodi sauti pia. Hivyo kwa kutumia
filamu za sinema na video tunaweza kuhifadhi na kuonyesha kazi za fasihi
simulizi.
ATHARI ZA MBINU MBALI MBALI ZA
UHIFADHI WA FASIHI SIMULIZI
KICHWANI
Uhifadhi wa kazi za fasihi simulizi kichwani una matatizo yafuatayo:-
·
Kumbukumbu
za akili zinaweza kupungua au kufifia au fanani kufa kabisa. Hali hii ikitokea
fasihi simulizi hupotea.
·
Mtu
anayehifadhi kichwani anaweza kubadilisha mambo muhimu katika simulizi na hivyo
kugeuza kiini cha masimulizi hayo.
·
Kutokana
na mazingira pamoja na mabadiliko kuna tatizo la kupata watu wanaoweza
kuhifadhi kazi hiyo.
MAANDISHI
Uhifadhi kwa kutumia maandishi
una matatizo yafuatayo:-
Ø Baadhi ya mambo hayawezi kuhifadhiwa katika maandishi. Mambo
hayo ni yale yanayohusiana na utendaji, sauti, vitendo, toni, kuimba,
muziki n.k. Matokeo ya kukosekana kwa vitu hivi ni kwamba ladha au
athari ya kazi inayowasilishwa hupungua.
Ø Kukosa sauti kwa hiyo msomaji anapaswa atie sauti na
mahadhi yake mwenyewe.Shughuli hii inaweza kuharibu au kufanya kazi ya fasihi ipungue ubora
wake.
Ø Hakuna ushirikishwaji kati ya fanani
na hadhira, kwa
hiyo hadhira inashiriki kwa kuona maandishi.
Ø Haibadiliki kulingana na wakati na
mazingira. Hivyo
huweza kudumu katika hali ile ile kwa muda mrefu kama ilivyo fasihi andishi.
Ø Inakuwa ya ubaguzi au watu wachache yaani wale wanaojua kusoma na
kuandika. Wale wasiojua kusoma na kuandika itawawia vigumu kuelewa fasihi hiyo
iliyoko katika maandishi.
Ø Ni gharama kubwa,kuhifadhi masimulizi katika
maandishi, hii ni kwasababu uandishi hutumia kalamu na karatasi. Hivyo hapa
zinahitajika pesa za kununulia kalamu na karatasi na gharama za uchapaji.
KANDA ZA KUNASIA SAUTI
Uhifadhi kwa kutumia maandishi una
matatizo yafuatayo:-
Ø Kanda za kunasia sauti husikika sauti
tu, Matendo hayawezi kushikwa na hii kuathiri tena uhifadhi na utoaji wa kazi
za fasihi simulizi.
Ø Hakuna ushirikishwaji wa hadhira kwani fanani na hadhira hawaonani
ana kwa ana kwa hiyo hadhira inashiriki kwa kusikiliza kanda tu, sikio
huathirika lakini jicho halioni.
Ø Ni gharama, kuhifadhi fasihi simulizi kwa njia
hii kwani kununua tepurekoda pamoja na kanda zenyewe, betri, spea hupatikana
kwa shida na kwa bei ghali licha ya hiyo si wote wenye uwezo wa kununua
tepurekoda hivyo ni watu wachache sana wenye uwezo wa kuhifadhi fasih simulizi
kwa kutumia chombo hiki.
Ø Haitabadilika kulingana na wakati au
mahitaji ya hadhira, Huweza kudumu katika hali ile ile kwa muda mrefu kama ilivyo fasihi
andishi.
KANDA ZA VIDEO, LUNINGA, FILAMU ZA SINEMA, CD, DVD, VCD NA
KOMPYUTA
Njia hii ina matatizo yafuatayo:-
v Upungufu wa ushirikishwaji wa hadhira,Hadhira haiwezi kushiriki ila
inasaidia kufanya fasihi simulizi kupata hadhira kubwa ingawa hadhira hiyo
haionani ana kwa ana na fanani wao.Kanda hizo huwa zinatazamwa na watu wengi
hivyo kupata hadhira wengi kwa wakati mmoja ambao hawawasiliani na fanani wao.
v Ni gharama,kwani vitu hivyo vinahitaji pesa
nyingi za kununulia vifaa hivyo ambapo ni watu wachache wenye uwezo wa kununua vifaa
hivyo.
v Haibadiliki kulingana na mahitaji ya
jamii au hadhira au wakati,Huweza kudumu katika hali ile ile kwa muda mrefu kama ilivyo
fasihi andishi
v Vifaa hivyo vinahitaji mahali pazuri
ambapo panaweza kutunza vyombo hivyo kwa muda mrefu, endapo havitahifadhiwa hivyo kuna hatari ya kupoteza kilichohifadhiwa
katika vyombo hivi.
MADA NDOGO-3; KUHAKIKI KAZI ZA FASIHI
SIMULIZI.
Kazi za
fasihi simulizi zinaweza kupimwa na kuonekana kama zinafaa au hazifai. Kazi
hizi hupimwa kwa kuzingatia uhusiano wake na hali halisi ya jamii.Katika
upimaji vipengele vya fasihi simulizi
huangaliwa jinsi vilivyotumika.Upimaji
wa ubora wa kazi ya fasihi simulizi hujumuisha umuhimu wa mambo yaliyosemwa
katika jamii inayohusika au namna mambo hayo yanayosemwa Hivyo mhakiki
atajiuliza maswali kama:-
Ø Ujumbe utolewao hapa ni wa kweli na
una manufaa au la!
Ø Je maadili yatolewayo hapa
yanalingana na wakati tulionao?
Ø Je nahau, misemo, methali na
tamathali za semi zinalingana na jambo linalosemwa au la!
Ø Je mtiririko wa matukio unasaidia
msikilizaji kuelewa kisa au unamchanganya?
Maswali ya
namna hiyo yanamsaidia mhakiki kuelewa ubora wa kazi ya fasihi simulizi.Pia
yaweza kutumiwa na mtunzi wa kazi ya fasihi simulizi ili kurekebisha kazi yake
na kuifanya iwe bora Zaidi.
FANI KATIKA FASIHI SIMULIZI
FANI
Fani ni ustadi au ubingwa au mbinu
ambazo msanii wa kazi ya fasihi hutumia katika kuwasilisha ujumbe wake kwa
hadhira yake.
AU
Fani ni Sanaa na jumla ya vipengele vya lugha
vilivyowekwa katika mpangilio mahususi ili kutoa maana fulani kwa hadhira.
VIPENGELE
VYA FANI
1.Tukio,Katika tanzu za fasihi simulizi mara nyingi
ni lazima pawe na jambo au tukio ambalo huchukuliwa kama kiini au chanzo cha
utanzu utakaohusishwa fani au utanzu unaotumiwa na msanii hauibuki tu hivi
hivi.Tukio huwa ndio kishawishi cha fanani wa fasihi simulizi .Mfano: Nyimbo za
unyago huibuka katika mazingira yake, methali za kutuliza zaweza kutumiwa pale
ambapo pana majonzi ya aina fulani, kwa hiyo ni lazima pawe na tukio ambalo litachukua
chemichemi ya utanzu utakaotumiwa na fanani kuwasilisha ujumbe wake kwa
hadhira.
2.Mazingira/mandhari, Mazingira ni pale ambapo matukio ya
fasihi simulizi yaliibuka ama yalitokea.Ufundi wa kuchora mazingira unatoa
picha halisi, picha inayoonekana waziwazi juu ya mazingira yaliyohusika.Fasihi
simulizi hutegemea sana muktadha au mazingira maalumu hivyo tungo za fasihi
simulizi huwa zimejikita katika utamaduni wa jamii zinamoibukia vifaa ambavyo
vinatumika katika fasihi simulizi vinategemea mazingira yanayohusika, mfano
msanii anapodhaminia kutoa picha ya kuogofya anatumia mazingira ambayo
yanaogofya kama vile mazingira ya misituni na wahusika kama majitu ili kuleta
dhana ya hofu katika mazingira yake.
3.Muundo,Katika fasihi simulizi muundo ni
mpangilio na mtiririko wa kazi ya fasihi simulizi kwa upande wa visa na
matukio.Katika muundo kinachozingatiwa ni jinsi fanani alivyofuma na kuunda hata alivyounganisha
tukio moja na lingine kimoja na kingine, wazo na wazo, ubeti na ubeti na mstari
wa beti na mwingine.Kuna miundo mbalimali katika tanzu mbalimbali za fasihi simulizi, kama vile muundo
wa moja kwa moja na kuna muundo changamano,pia upande wa ushairi
Katika
mashairi kuna miundo mbalimbali ambayo hutumiwa kuainisha mashairi kwa kufuata
idadi ya mistari katika kila ubeti, miundo hii ndiyo hutupa mashairi ya tarbia,
tathilitha, takhmisa na n.k.Katika hadithi na hata katika tamthiliya waweza
kuwa na muundo ambao fanani ameanza kutoka mwanzo akaenda katikati na baadae kumalizia
kisa chake aina hii ya muundo unaitwa mtiririko shanga.Mtirirko wa namna
hii hujengwa kwa kutumia visa au vitukio mbalimbali na vinaweza kuongezwa na
kupunguzwa bila kupoteza maana ya hadithi au tamthiliya.
1. Mtindo,Katika kazi ya fasihi mtindo ni ile
namna ambayo msanii hutunga kazi yake na kuipa sura ambayo kifani na kimaudhui
huainisha kanuni au kaida zilizofuatwa kama zilizopo ni za kipekee. Mtindo ni upangaji wa fani na
maudhui katika kazi ya fasihi kwa njia ambayo hatimaye huonyesha nafsi na labda
upekee wa mtunzi wa kazi hiyo.
Katika tamthiliya na riwaya katika mtindo kinachotazamwa ni matumizi ya
nafsi,matumizi ya monolojia,masimulizi na dayalojia,matumizi ya hadithi ndani
ya hadithi,matumizi ya barua n.k
Upande wa mashairi kuna mitindo mbalimbali
kama vile Mtindo wa Pindu,mtindo wa kuhoji,mtindo wa beti kubadilishana
vina,mtindo wa kidato n.k na shairi linaweza kuwa la vina na mizani au
la kisasa ambalo halifuati kanuni za urari wa vina na mizani.
2. Matumizi ya lugha.
Ni kipengele
muhimu cha fani ya fasihi, lugha ndiyo malighafi ya fasihi.Lugha inayotumika
katika kazi ya fasihi ni lugha ya kisanaa inayopambwa na inayokusudiwa kuibua
hisia fulani kwa hadhira yake.Inaweza kuathiri moyo ya hadhira na kulingana na
jinsi inavyotumiwa kwa lengo la kuchekesha, kukejeli, kubeza, kuchokoza, kutia
hamasa au kushawishi
‘’ Fani lazima iwe na utanashati na
ulimbwende wa kipekee wenye mvuto na mnato wa kuteka na kusisimua hisi za
wasikilizaji wasomaji au watazamaji’’(khatibu 1981:16)
Matumizi ya
lugha fasaha, uteuzi wa misamiati na matumizi ya misemo na methali zinazosadifu
mazingira ya jaini inayohusika kufanya kazi hiyo ya fasihi simulizi kuwa sumaku
ya kuvutia msomaji, msikilizaji au mtazamaji.Tamathali za semi za aina
mbalimbali hutumika kujenga picha mfano ya tamathali za semi ni kama vile sitiari,
tashihisi, kejeli, kijembe, tabaini, tuniaba, tashibiha n.k.Taswira
ni lugha ambayo huchora picha za watu, vitu au mahali kwa kutumia ishara katika
taswira unaweza kubainisha maelezo ambayo jinsi yanavypangwa na msanii huweza
kufanya hadhira zipate aina mbalimbali za hisi za kunusa, kusikia, kuona na
kugusa.Mara nyingi hutumiwa na wasanii ili kunasa hisia zao kwa hadhira.Hivyo
wasanii hutumia maneno ambayo huumba picha kamili ya kitu, hali, wazo, dhana au
uzoefu fulani wa jamii inayohusika.Mara nyingi matumizi ya picha huenda
sambamba na ishara mbalimbali ili kuwakilisha vitu, dhana au mawazo mengine.
3. Upeo
Katika fasihi simulizi upeo ni kama
kilele cha kazi yenyewe, kuna upeo wa
aina mbili
Upeo wa juu ,ni zile sehemu za kazi hiyo ambazo
hutosheleza haja za wasikilizaji au watazamaji. Katika sehemu hii hadhira
hupata majibu muhimu ambayo kazi hiyo imechelewesha kwa kutumia taharuki mbinu
rejeshi, mtindo wa kiutelezi n.k.Mara nyingi watunzi wa kazi za fasihi
huweka kipeo cha juu mwishoni mwa kazi zao ingawa si lazima kuwa na kipeo kimoja tu wakati mwingine
waweza kupata kazi ya fasihi simulizi ambayo haina kipeo kabisa Katika kazi
mbalimbali za fasihi wasanii hujenga mgogoro ambao hujtokeza na kukua, jinsi
kazi hizo zinavyokua, kipeo cha juu hutokea pale ambapo msanii hujaribu kutoa
suluhisho kwa mgogoro uliojengwa katika kazi yake.
Upeo wa chini ,ni sehemu ambayo matatizo yaliyounda
kazi ya fasihi yanatatuliwa.Upeo wa chini ni pale ambapo haja na mataajio ya
hadhira hayakukidhiwa, katika baadhi ya kazi za fasihi vipeo vya chini hudhihirisha
udhaifu wa kazi hiyo lakini katika kazi nyingine upeo wa chini huwa umekusudiwa
hivyo na mtunzi.Hali hii ya pili hujitokeza hasa katika kazi ya fasihi ambayo
upeo wa chini hutumiwa kwa lengo la kushangaza hadhira.
4.
UCHESHI KATIKA KAZI ZA FASIHI
Ucheshi ni kipengele muhimu cha kifani katika kazi ya fasihi
hasa fasihi simulizi.Ucheshi ni mbinu ya kifani ambayo watunzi hutumia katika
kazi zao za fasihi kwa lengo la kuchekesha na kuburudisha hadhira na kuondolea
uchovu.
Wasanii mbalimbali hutumia mbinu tofautitofauti kuleta
vichekesho katika kazi zao.Baadhi yao hutumia vitendawili ili kujenga,
kejeli, dhihaka, n.k. vichekesho pia huweza kutumiwa ili kujenga
maudhui.
5.
WAHUSIKA.
Ni viumbe ambavyo hutumiwa na wasanii katika mtiririko wa
matukio kuelezea visa vyake.Wahusika wanaweza kuwa watu, miti, wadudu, mizimu, misitu
na wanyama.Wahusika huwa ni viumbe ambavyo vinatenda na kutendewa wanatumwa na
msanii kusimamia hali mbalimbali za binadamu katika jamii wanamoishi.
Hawa ndio uti wa mgongo wa fani ya fasihi simulizi, Bila wahusika
mtiririko wa matukio au visa hukosa pahali pa kujishikiilia.Wahusika si viumbe
maalumu wa mtunzi kwa vile ndiyo wanaotumia kutoa picha au kuwasilisha mawazo
na fikra zake kwa jamii inayowakilishwa na wahusika hao.Katika Fasihi
simulizi wahusika wanaweza kuwa binadamu
,wanyama,au vitu fulani vilivyopewa fursa ya mandhari na kauli kama binadamu.
VIPENGELE VYA MAUDHUI KATIKA FASIHI SIMULIZI
Ø MAUDHUI
Ni jumla ya
mambo yote yanayosemwa na msimuliaji au mwandishi katika kazi yake.Vipengele
vya maudhui au umbo la ndani la kazi ya fasihi ni kama vile
Ø Dhamira, Ni
kusudio la mtunzi wa kazi ya fasihi.Kazi ya fasihi inaweza kuwa na dhamira kuu pamoja na dhamira
ndogo ndogo.Ubainishaji wa dhamira hufanywa na hadhira,hivyo dhamira hufahamika
kutokana na fasili za wasikilizaji au wsomi wa kazi ya fasihi.
Ø Ujumbe: Ili
dhamira ya mtunzi itimie, msanii hutoa taarifa fulani fulani kwa hadhira
yake.Taarifa hizo huitwa ujumbe.
Ujumbe unaweza kutamkwa wazi au kwa uficho. Kwa mfano methali ya “Asiyesikia la mkuu huvunjika guu” ina ujumbe huu ukidharau maonyo ya wakubwa utapatamatatizo,Siku za mwizi ni arobaini ujumbe wa methali hii chenye mwanzo kina mwisho kwa kawaida
kazi moja ya fasihi inaweza kuwa na taarifa Zaidi ya moja.
Ø Mafunzo: Ni
mafundisho au nasaha za mtunzi katika kazi ya fasihi.Mafunzo pia huwa na maana
kulingana na fasili ya hadhira. Mafunzo humfikirisha msikilizaji au msomaji kwa
njia ya ujumbe.Mfano katika ujumbe huu akaiba akafungwa hapa funzo ni tusiibe wakati mwingine kazi za fasihi
inaweza kutoa mafunzo mabaya (maadili) mtunzi anaweza kukusudia hivyo au
kutokusudia hivyo.
Ø Migogoro: Hii
huelekeza kisa lakini hujizatiti juu ya migogoro ya maisha anayosimulia
fanani.Baadhi ya kazi za fasihi huonyesha ukinzano uliopo baina ya makundi ya
watu au hali ya aina moja dhidi ya hali nyingine kuna aina nyingi za migogoro
lakini Zaidi ni ile ya kisiasa, kiuchumi na kitamaduni au ile ya kibinafsi
mfano: matatizo yanayosababishwa na uzembe dhidi ya watetezi wa kazi (viongozi)
dhidi ya usasa katika mila na desturi husababisha mgongano wa kiutamaduni.
Ø
Falsafa: Ni mafunzo makuu ya msanii (mtunzi)
kuhusu maisha. Mawazo haya hutokana na uchanganuzi wa kimantiki na huwa ndio
hekima na busara za msanii (mtunzi) huyo.Ni Imani ya mwandishi au fanani katika
maisha juu ya utatuzi wa matatizo katika jamii.
UMUHIMU NA UHUSIANO WA FANI NA MAUDHUI KATIKA FASIHI SIMULIZI.
Fani ni
jumla ya mambo mengi yanayoijenga kazi ya fasihi.Mambo haya ni kama vile
muundo, mtindo, mandhari,wahusika na matumizi ya lugha na maudhui ni jumla ya
mawazo au dhamira, msimamo, mtazamo, falsafa na ujumbe katika kazi ya fasihi.
Kwa ujumla
fani na maudhui ni vitu vya muhimu sana katika fasihi simulizi kwa sababu
mtunzi hutumia vipengele hivi katika kujenga kazi yake anayotaka kuwasilisha
kwa jamii husika.Maudhui ni kila kina kinachosemwa na fani ni namna
kinavyosemwa.
Fani na
maudhui ni vitu vinavyohusiana,
vinaathiriana,vinategemeana na kukamilishana katika kujenga kazi ya fasihi
simulizi na kila kipengele kimo ndani ya kingine
Mudhui
hujumuisha viungo mbalimbali vya kazi ya fasihi simulizi na fani ni mbinu za
kisanaa zinazotumiwa na msanii ili kuvifanya viungo hivyo viyasawili maisha kwa
njia ivutiayo hadhira.kila kigezo (fani na maudhui) kimo ndani ya kingine huku
vikishirikiana na kuathiriana katika kujenga au kubomoa kazi ya fasihi
simulizi.
MADA NDOGO-4 ; KUTUNGA
KAZI ZA FASIHI SIMULIZI
Utungaji ni
uundaji wa mawazo na kuyapanga maneno yakuwasilisha ama kwa njia ya mdomo au
kwa njia ya maandishi.Utungaji unweza kutolewa kawa njia mdomo aqu kwa njia ya
maandishi.
Mambo ya kuzingatia katika kutunga
kazi ya fasihi simulizi.
·
Kuwa na jambo lakuelezea (tukio).Mtunzi anapaswa kuwa na jambo ambalo anaona kuwa
linasababisha mivutano katika jamii.Jambohilo lazima litoke katika jamii
inayohusika na isiwe nje ya jamii hiyo.
·
Kuteua utanzu atakaotumia.Mtunzi ni vyema kujua
ni utanzu upi atakaotumia katika kuwasilisha jambo hilo kwa jamii.Kwa kawaida
fasihi simulizi ina tanzu nne ambazo ni hadithi, ushauri, semi na Sanaa za maonyesho
(maigizo).
·
Kuteua vipengele vya maudhui, mtunzi anapaswa aangalie nini dhamira yake, kuna ujumbe gani
kwa hadhira, hadhira itapata maadili gani na je migogoro ipi na iwasilishwe
vipi ili isipotoshe lengo zima la kazi yake.
·
Kuteua kipera kitakachotumika katika uwasilishaji wa kazi yake kwa
hadhira, mfano
kama mtunzi ameamua kutumia utanzu wa hadithi; hanabudi kuchagua kipera kimoja
wapo kati ya ngano, soga, vigano, visasili au tarihi (visakale)
·
Uteuzi wa vipengele vya fani. Baada ya kubaini vipengele vya maudhui, msanii anapaswa
aangalie namna atakavyowasilisha maudhui hayo kwa jamii.Hapa atatumia au atashughulika
na vipengele vya fani ambavyo atavitumia katika kuwasilisha ujumbe
wake.Vipengele hivyo ni muundo, mtindo, wahusika, matumizi ya lugha na
mandhari.Sehemu hii ndiyo ambayo mtunzi anatakiwa kutumia ufundi na ubunifu wa
hali ya juu ili kazi yake ieleweke, ielimishe na kusisimua hadhira.
Utungaji wa hadithi za fasihi simulizi
Katika
kutunga hadithi yoyote, vipengele vifuatavyo vinastahili kuzingatiwa;
Ø Maudhui
Haya ni masuala yanayowasilishwa na hadithi kwa ujumla wake.Katika
utungaji wa kipengele cha maudhui tutazingatia mambo yafuatayo:-
a)Dhamira – Hili ni
lengo kuu analowasilisha mtunzi kwa hadhira. Dhamira lazima zitokane na jamii
inayohusika. Katika dhamira, kuna dhamira kuu na dhamira ndogo ndogo
zinazojenga dhamira kuu. Mtunzi wa hadithi ni lazima azingatie kipengele hiki.
b) Ujumbe
na maadili – Hadithi lazima iwe na ujumbe fulani kwa hadhira yake.
Mtunzi lazima azingatie hilo. Vile vile hadithi lazima itoe maadili fulani kwa
jamii na maadili yanayotakiwa kutolewa lazima yaendane na jamii husika pamoja na
wakati.
Ø Fani
Fani ni jumla ya mambo yote yanayofanywa
katika kazi za sanaa ili kufanikisha uwasilishaji wa ujumbe. Katika utungaji wa hadithi mtunzi
anatakiwa azingatie vipengele vifuatavyo kifani:-
·
Ploti ,ni mtiririko wa matukio ya hadithi
kuanzia mwanzo hadi mwisho. Kila hadithi ina mwanzo – kati – mwisho. Aghalabu
hadithi zina ploti moja nyepesi ya moja kwa moja. Mtunzi katika kipengele hiki
cha ploti, lazima azingatie hadithi yake itakayokuwa na mwanzo – kati – mwisho.
·
Wahusika ,Hivi ni viumbe vinavyoshiriki katika
hadithi. Hadithi huwa na mhusika mmoja mkuu anayehusishwa na matukio makuu
katika hadithi nzima. Wahusika ni wachache na huwa bapa (wasiobadilika) .
Mtunzi wa hadithi katika kipengele hiki cha wahusika lazima azingatie ubapa wa
wahusika wake katika kuwajenga wahusika wake.
·
Mazingira –
Katika kipengele hiki, mtunzi anapaswa kuangalia muktadha kijiografia na
kuonyesha:-Mazingira ya kijamii yanayojadiliwa,Majukumu ya mhusika mkuu
anayoyatekeleza katika jamii/ familia, n.k,Mahali tukio linapotokea (mahali pa
kazi pa mhusika – msikitini, kanisani, ofisini, nyumbani, kijijini, mjini,
n.k)Mandhari yakichorwa vizuri husaidia kulisukuma gurudumu la wakati na
kwapambanua wahusika.
a) Kilele –
Kilele cha hadithi huwa pale suluhisho la maswali ambayo msikilizaji amefanywa
ajiulize hupatikana.
b) Mtindo wa usimulizi – Hadithi nyingi hutumia nafsi ya kwanza au ya tatu. Zingine hutumia
chuku maelezo na kutumia takiriri – mambo ambayo mtunzi anatakiwa kuyazingatia
wakati wa utunzi wake.
·
Matumizi ya lugha,Katika kutunga kazi za mtunzi
anapaswa kutumia lugha yenye mvuto iliyojaa Taharuki,Tamathali za semi kama vile tashihisi, tashibiha, sitiari, n.k
UTUNGAJI WA MASHAIRI/TENZI/NGONJERA WA
FASIHI SIMULIZI
Kabla ya kuanza kutunga shairi lolote,
mtungaji anawajibika kuvifahamu kwanza vipengele vinavyojenga shairi,
vinginevyo utungaji wake utapwaya sana.Vipengele muhimu vinavyojenga shairi ni
vya aina mbili: vya kifani na, vya kimaudhui.
Fani
Shairi lolote lile ni muungano wa fani,
maudhui na muktadha.Kwa kawaida, mashairi
hutunga ili kueleza maudhui fulani kutokana na, au kwa ajili ya muktadha
fulani. Shabaha hiyo ya mshairi hutimizwa kwa kutumia fani na hudhihirika
kifani. Ingawa maudhui hutawala fani kwa maana ya kuwa mtunzi huanza na wazo
ambalo hulitafutia fani ya kulielezea, lakini fani vilevile huathiri maudhui
hayo, maana maudhui yamo ndani ya fani na hudhihirika kifani. Hivyo tukitaka
kutunga shairi sharti kwanza tuviainishe na kuvielewa vipengele vya kifani
vitakavyotumika. Vipengele muhimu vya kifani ni lugha, muundo, wahusika na
mtindo.
(a)Lugha,ushairi hutumia lugha yenye mpangilio na maneno maalumu
yaliyoteuliwa ili kuwasilisha ujumbe wake. Kwa hiyo, vipengele vya kuzingatia
upande wa lugha ni ;Utenzi wa maneno na
semi,Mpangilio wa maneno katika sentensi,Matumizi ya picha (Jazanda) na
tamathali: Picha (taswira) ni uwakilishaji wa jambo kutumia kauli maneno
yanayosawiri picha au hali ya jambo hilo na kuibua hisia au vionjo kuhusu jambo
hilo katika akili ya msomaji/msikilizaji. Picha huweza kumfanya msomaji au
msikilizaji, katika mawazo yake, aone, asikie aonje, anuse, apende au achukie
kile kinachosawiriwa.
Tamathali ni aina ya picha. Ni ufananisho wa vitu kisanii kwa kusudi
maalumu. Baadhi ya tamathali zinazotumika sana ni tashibiha, sitiari, tashihisi, metonomia (kutumia sehemu ya kitu
kuwakilisha kitu kamili, au kutumia kitu kidogo kuwakilisha kitu kikubwa
kinachohusiana nacho), mubalagha na kejeli.
Picha na tamathali hutumiwa sana na
washairi ili kuyasawiri mawazo yao. Baadhi ya picha na tamathali hizo huwa na
viwango mbalimbali vya maana na kuhitaji akili pevu na uzoefu kuzifumbua.
(b)Muundo,mashairi ya
Kiswahili yana miundo mingi. Baadhi ya vipengele vya kimuundo vinavyotumika
zaidi ni mistari,beti,mizani na vina. Urefu wa wa mistari hutofautiana
kutegemea mizani ya shairi linalohusika, au kutegemea mtiririko wa wazo/hisia
kama ni shairi huria. Urefu wa beti hutegemea idadi ya mistari katika kila
ubeti: zipo tungo za utatu(tathlitha),unne(tarbia), utano (takhimisa), n.k.
Kwa kweli miundo inayotokana na
mpangilio wa vina na mizani haina idadi, inategemea matakwa na ubunifu wa
washairi wanaohusika.
(c)Wahusika,mashairi ya
kawaida hayategemei sana wahusika ili kuwasilisha ujumbe wake. Hata hivyo,yapo
mashairi ya masimulizi,kwa mfano, tendi, ambayo hutumia wahusika kujenga
maudhui yake. Utungaji wa mashairi ya aina hiyo lazima uzingatie pia dhima na
taswira ya wahusika hao katika ujenzi wa matukio na maudhui ya utenzi huo.
(d)Mtindo,mtindo ni tabia
ya utungaji ambayo humpambanua mtunzi mmoja na mwingine. Mtindo hubainika
katika namna mtunzi anavyotumia maneno yake (Kama anaendelea kutumia maneno magumu
au rahisi, kuchanganya lugha, kutumia methali, n.k.) Jinsi anavyozipanga semi
zake (kama anatumia sentensi fupifupi au ndefu, takiriri (vibwagizo, n.k.), na
namna anavyoumba tungo zake. Mtindo wa mtunzi humwezesha msomaji kubainisha
upekee na uasilia wa mtunzi huyo,na pia athari za watunzi wengine kwenye usanii
wake.
Mambo
muhimu ya kuzingatia katika utungaji wa ushairi wa kimapokeo
Hapa yanaingia mashairi ya tenzi za
kijadi zenye kufuata kanuni za urari wa mizani na mpangilio wa vina vya mwisho
au kati. Katika ushairi wa kimapokeo,kuna mambo ya msingi yanayosemekana kuwa
ni uti wa mgongo wa ushairi wa Kiswahili. Kwa mujibu wa wanamapokeo, shairi la
Kiswahili lazima liwe na vina, mizani, mstari, ubeti na kituo. Katika utenzi
(aina pia ya ushairi wa kimapokeo) kunakuwa na bahari katika mstari wake wa
mwisho. Hapa tutaelezea kwa ufupi juu ya vipengele hivyo.
·
Vina, ni silabi za namna moja zinazotokea
baada ya kila mizani kadhaa katika mstari wa shairi. Mashairi ya mistari minne
ya mizani 16 huwa na vina katika silabi ya 8 na ya 16 katika mistari mitatu ya
kwanza. Kwa kawaida, vina vya silabi 16 huwa vya namna moja katika beti zote za
shairi zima, na vina vya silabi 8, kwa desturi inayotumika sana, huwa tofauti
ubeti na ubeti. Kwa kawaida tuna vina vya kati na mwisho. Mfano:
Kuna utesi uzushi, nchi ina maongezi,
Pembeni
twaona moshi, moshi haujitokezi,
Shairi
kuzinakishi, kugeuza maongezi,
Mashairi
na utenzi, sanaa tusipotoshi.
Katika ubeti
huu,kuna vina vya kati na mwisho ambavyo hufanana.
·
Mizani ,ni jumla ya silabi zilizomo katika
kila mstari wa ubeti.katika ushairi, hizi ndizo ziletazo urari wa mapigo, kwani
kila mstari unatakiwa uwe na mizani sawa na mistari mingine. Kwa kawaida
mashairi ya kimapokeo huwa na mizani 16, sehemu ya kwanza mizani 8 na sehemu ya
pili mizani 8.
Mfano
Ku
na u te si u
zu shi, n chi i na ma o nge zi
8 2 3
4 5
6 7 8 9 10 11 12 13 14 15
16
·
Kituo,Huu ni mstari wa mwisho katika kila
ubeti wa shairi. Kituo huweza kuwa kimalizio au kiini.Kinakuwa ni kimalizio
kinapokuwa kinatumika kama kitu cha kulifunga na kulikamilisha wazo moja katika
kila ubeti. Kinakuwa ni kiini kinapokuwa kikitumiwa na kinajitokeza katika kila
mwisho wa ubeti na kinataja kwa muhtasari jambo muhimu linalozungumzwa.
·
Muwala (kutosheleza),Muwala ni ile
hali ya utoshelevu katika ubeti hadi katika utungo mzima. Yaani kila ubeti
uweze kujitosheleza katika maana, lakini wakati huo huo ukawa hausigani na beti
nyingine.
·
Ubeti.,Hiki ni kifungu chenye kuleta maana
kamili katika jumla ya vifungu vilivyomo katika utungo.
·
Kipande,Hiki ni kisehemu kimojawapo katika
visehemu viwili au zaidi vya kila mstari kwa tungo zenye kugawanyika katika
sehemu mbili au zaidi katika kila mstari.
HATUA/Mambo ya kuzingatia katika utungaji wa
mashairi
Ø Kuteua maudhui na dhamira
Katika kipengele cha
maudhui, mtunzi wa mashairi anatakiwa kuzingatia vipengele vifuatavyo ili aweze
kufanikisha lengo lake.
·
Kuweka lengo maalumu – Kabla ya kuanza kutunga hairi
lazima ujue nini unataka kueleza. Hapa lazima ujue sababu inayokufanya utake
kueleza hayo uliyonayo. Lengo laweza kuwa kupinga mauaji ya albino, ajira kwa
watoto au unyanyasaji wa wanawake.
·
Kuteuwa wazo kuu la shairi – Hili ndilo wazo utakalolikuza na
kuliendeleza. Wazo kuu linaweza kuwa “ athari za ugonjwa wa UKIMI” katika
jamii. Hivyo mwandishi ataliendeleza wazo hilo kutoka mwanzo hadi mwisho.
·
Kuoanisha dhamira na wakati – Ni muhimu mtunzi wa ushairi
kuhakikisha kwamba anazungumzia mambo ambayo anafikiri jamii inayahitaji katika
wakati huo. Kwa mfano, leo Tanzania imekabiliwa na matatizo kama vile ugonjwa
wa UKIMWI , ajira kwa watoto, mauaji ya albino, madawa ya kulevya, n.k. Haya
ndiyo mambo ambayo mtunzi hupata hadhira kubwa. Kama taongea mambo ambayo yako
nyuma ya wakati, atakuwa haitendei haki jamii yake kwa kujadili mambo ambayo
hayako katika jamii yake kwa wakati uliopo.
·
Kupanga vizuri mawazo yako – Panga mawazo yanayojenga maudhui
kimantiki kutegemea uzito, upya, ugumu na umuhimu wake kwa jamii inayohusika.
Ø Kuteua vipengele vya fani
Maudhui
pekeehayatoshi kulipa shairi mvuto. Mtunzi ni lazima azingatie fani, yaani
mbinu za kisanii anazotumia mtunzi kulipa shairi mvuto. Mbinu hizi ni pamoja
na:-
·
Kutumia mitindo inayofaa – Shairi linaweza kuwa la kimapokeo
au kisasa. Uteuzi wa mtindo untegemea sana dhamira inayokusudiwa pamoja na
lengo alilonalo mtunzi mwenyewe. Kwa mfano, tukio la kihistoria utatumia
“utenzi” badala ya “wimbo”, mawaidha fulani huwezi kutumia “utenzi” bali
utatumia “ushairi” au “wimbo”.
·
Kutumia miundo inayofaa,Kuamua muundo wa shairi kutategemea
idadi ya mistari. Mtunzi anaweza kutumia muundo wa tathnia (mistari miwili),
Tathlitha (mistari mitatu), Tarbia (mistari mine), Tkhimisa (mistari mitano) au
sabilia (mistari sita na kuendelea). Katika kipengele hiki ni muhimu vile vile
mtunzi kuzingatia idadi ya mizani, aina ya vina, vipande, kituo msisitizo,
muwala, ubeti na urari. Vitu hivi ni muhimu sana hasa kwa ushairi wa kimapokeo.
·
Uteuzi wa lugha – Ushairi una lugha yake ya tofauti
na kazi nyingine. Mtunzi hana budi kutumia lugha yenye sifa zifuatazo:- Lugha
ya mkato, -Matumizi ya picha, Matumizi ya tamathali za semi, Matumizi ya
methali, misemo, nahau na mbinu nyingine za kisanaa
UTUNGAJI WA MAIGIZO YA FASIHI
SIMULIZI
Katika
utungaji wa maigizo kuna vipengele mbali mbali ambavyo lazima vifuatwe ili utungaji
ukamilike. Vipengele hivyo ni :-
·
Kuchagua tendo au tukio la kuigiza ,Mtunzi achague matendo yale tu
ambayo lazima yatasaidia kujenga wazo lake. Ni lazima jambo hilo liwe uzito au
athari fulani kwa jamii. Matukio yanayoweza kuwa kiini cha kutungiwa maigizo ni
kama vile ufisadi, malezi ya watoto, unyanyasaji w mwanamke, mauaji ya albino,
ujambazi, madhari ya UKIMWI, n.k
·
Kuchagua mahali pa kutenda jambo ,Mahali pa kutenda panaweza kuwa
ofisini, nyumbani, barabarani kwenye
basi, mjini, kijijini, n.k.
·
Kuteua mtindo wa kuteuwa jambo la
kuigizwa,Hapa mtunzi
anaweza kutumi fumbo, vichekesho, tanzia, ramsa (futuhi), n.k. Ni vizuri mtunzi
achanganye mbinu ili kutdumisha mvuto.
·
Kupanga hoja zinazojenga maudhui ya
igizo,Maudhui
hujikita katika migogoro. Masuluhisho ya migogoro hupatikana pale migogoro
inapofikia kilele. Kwa mfano, mwanamke anapojikomboa kutokana na manyanyaso ya
mwanaume.
·
Kuweka mpangilio wa maonesho,Maonesho ambayo hujumuisha vitendo
na hoja zinazokamilisha sehemu inayobeba
maudhui ni muhimu sana. Maonesho yapangwe kwa utaratibu maalumu ili yaweze
kufikisha ujumbe kirahisi kwa hadhira. Maonesho yakipangwa ovyo, mvuto wa kazi
ya sanaa huwa ovyo pia.
·
Ujengaji wa wahusika- Wahusika wajengwe kutokana na
misukosuko ya migongano. Matendo, maneno na mawazo ya wahusika yapate chanzo
kutokana na misukumo hiyo. Mtunzi anashauriwa kutumia wahusika tofauti tofauti.
Kwa mfano, wazee, vijana, wanawake, wanaume, wanene, wafupi, wembamba, n.k. Ni
muhimu pia kwa mtunzi kuwaumba wahusika wake na kuamua mavazi yao na vifaa
vingine. Uamuzi huu yafaa ufanywe kwa kuzingatia mazingira.
·
Uteuzi wa maneno – Maneno ya kusema wahusika
yanapaswa kuwa yale tu ambao yanajenga tendo. Maneno yanajengwa ili
kudhihirisha tendo liwe wazi zaidi. Kuweka maneno mengi hudhoofisha nguvu ya
matendo, katika kuleta maana inayokusudiwa kwa vile huwa vigumu hupatanisha
maneno hayo na matendo. Kwa hiyo, mtunzi wa maigizo anapaswa kuwapa wahusika
wake maneno machache jinsi iwezekanavyo, na tena yale tu ambayo yanaoana na
vitendo.
·
Baada
ya yote hayo, mtunzi anawezakuandika maigizo na kuhariri – Ni muhimu kutumia lugha ya
kimazungumzo (dayolojia) inayovutia na kuleta taharuki na yenye utamu unaoeleze
maadili kwa mnato.
M W
I S H O