UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI ANDISHI UTANZU: USHAIRI KITABU: WASAKATONGE MSHAIRI: MOHAMED S. KHATIB WAHAKIKI: KIDATO CHA NNE – 2013
UTANZU: USHAIRI
KITABU: WASAKATONGE
MSHAIRI: MOHAMED S.
KHATIB
WAHAKIKI: KIDATO CHA NNE – 2013
UTANGULIZI:
WASAKATONGE
ni moja wapo ya vitabu vinavyotumika kuwatahini watahiniwa wa kidato cha nne
kwa upande wa somo la fasihi. Mshairi wa kazi hii amefanikiwa kwa kiasi kikubwa
mno kuifunua jamii yake kwa kuanika UOZO
uliomea vilivyo ndani ya jamii aliyoiandikia. Hakika amegusa mambo kadhaa
yanayomzunguka mwanajamii; yapo yenye kutia moyo na yenye kukera.
FANI YA
WASAKATONGE:
Fani ni
ufundi au ujuzi ambao msanii wa kazi ya kifashi anautumia katika kujenga na
kuwasilisha kazi yake. Mshairi huyu amefanikiwa kuijenga vilivyo kazi yake
akitumia kifundi zaidi vipengele vya kifani hata kuifanya kazi yake iwe ya
kipekee mno.
A: MUUNDO
Ni sura,
mjengo au namna ambavyo kazi fulani ya kishairi ilivyojengwa. Kuna vipengele
kadhaa vinavyotumika kama sehemu ya muundo navyo ni idadi ya mishororo, vipande,beti na vituo.
Kwa
kipengele cha idadi ya mishororo, mshairi ameijenga kazi yake kwa idadi tofauti
tofauti ya mishororo kama ifuatavyo:
Ø Tathlitha:
Katika kazi hii yapo mashairi kadhaa yaliyojengwa kwa mishororo mitatu
maarufu kama muundo wa tathlitha nayo ni kama vile; KANSA, HATUNA KAULI,
TUTABAKIA WAWILI na NILINDE.
Mfano;
NILINDE
Nilinde sichukuliwe,
hata kwa moja shubiri,
Tubaki mimi na wewe,
pendo letu linawiri,
Tuwazidishe kiwewe, wasotutakia
heri,
Ø Tarbia:
Ni muundo mwingine katika kipengele cha idadi ya mishororo ambapo
mashairi hujengwa kwa mishororo minne kwa kila ubeti. Mshairi pia ametumia
muundo huu katika kazi yake hii ya kishairi. Muundo huu unajidhihirisha vizuri
katika MAHABA, TOHARA, TONGE LA UGALI, WAFADHILIWA.
Mfano:
PEPO BILA KIFO
Nataka nifikie pepo,
Nipate raha zilizopo,
Na kila kizuri kilichopo,
Nifaidike.
Ø Takhmisa:
Ni muundo ambao kazi ya kishairi inajengwa kwa mishororo mitano kwa kila
ubeti. Mjengo huu unajidhihirisha wazi katika tungo kama vile; UNYAMA, KOSA,
WASAKATONGE, TWENDA WAPI?
Mfano:
UNYAMA
Unyama wa binadamu,
Haukadiriki
Haufukiriki
Hausaidiki,
Ni mnyama wa wanyama.
Ø Tasdisa:
Ni muundo ambao kazi ya kishairi huundwa kwa mishororo sita kwa kila
ubeti. Mashairi ya namna hiyo yanapatikana katika kazi hii nayo ni kama; TIBA
ISIYOTIBU, SI WEWE,AFRIKA, ASALI ILPOTOJA.
Mfano:
AFRIKA
Lini?
Afrika utakuwa,
Bustani ya amani,
Ukabila kuuzika,
Ukabila kuufyeka,
Ni lini?
Ø Sabilia:
Ni muundo ambao kazi ya kishairi hujengwa kwa mishororo saba au zaidi kwa
kila ubeti. Katika Diwani hii yapo mashairi kadhaa yaliyojengwa kwa:
·
Mishororo
7 ----- MVUJA JASHO, NILIKESHA,
HATUKUBALI
·
Mishororo
8 ------ BUNDI, SIKULIWA SIKUZAMA,
VINYONGA
·
Mishororo
10 ------ MADIKTETA, UASI
·
Mishororo 13 -----
MARUFUKU
B. MTINDO:
Ni tabia ya
kiutunzi au uandishi na huhitilafiana kati ya mtunzi na mtunzi mabayo hutegemea
ufundi, hisia na ufanisi wa mtunzi.
Mtindo huifanya kazi ya kifasihi kuvutia machoni na masikioni mwa hadhira.
Malenga huyu
ametumia mitindo tofauti katika kazi yake kama ifuatavyo;
I.
Pindu:
Ni mbinu ambayo sehemu ya neno au neno zima la mwisho katika mshororo au
kipande huanzisha mshororo au kipande kingine. Mbinu hii inaonekana vizuri
katika mashairi ya NAHODHA na KANSA.
KANSA
Jamii
imeoza, imeoza yanuka
Uchafu
wachomoza, wachomoza wafoka,
Inatoa
mafunza, mafunza yamwagika.
ii.
kikufu:
tabia kiutunzi ambapo neno la
mwisho au kipande cha mwisho katika kituo cha ubeti
uliotangulia linakuwa neno la kwanza au
linaanzisha mshororo wa kwanza wa ubeti
unaofuatia. M. S. Khatib ameutumia
mtindo huu katika shairi la USIKU WA KIZA na
MCHEZA HAWI KIWETE
Usiku wa
kiza, nimejiinamia
Sana
nakuwaza, nakufikiria
Wakunipumbaza, meniondokeya,
Meniondekeya,
wangu mahabuba,
Nilikuzoweya,
kwa yako mahaba,
Nnajikondeya,
sili nikashiba.
iii. Kidato:
ni mbinu ambayo mshororo mmoja
aghalabu wa mwisho hufupishwa kwa sababu maalum.
Mbinu hii imetumika vizuri katika NALITOTE,
TOHARA.
NALITOTE
Nalitote, mbao tugawane,
Kwa
vyovyote,isiwezekane,
Iwe pute,
mali tugawane.
Nalitote.
iv.
maswali:
ni mtindo ambao mshairi huandika shairi huandika katika namna ya kuhoji
jambo. Mtindo
huu unaonekana vizuri kupitia mashairi ya AFRIKA, WASO DHAMBI
AFRIKA
Lini?
Afrika utakuwa,
Bustani ya amani,
Ukabila kuuzika,
Udini kuufyeka,
Ni lini?
v.
Kiitikio:
Katika mbinu hii mshairi hutumia kibwagizo, Mohamed Seif Khatib ametumia
kibwagizo
katika mashairi yake kadhaa, mfano wa mashiri hayo ni; MAMA NTILIYE,
SILI NIKASHIBA,
TUTABAKIA WAWILI.
BANDARINI
3. utwesi ukenda kombo, zikaingia kikiri,
Mrama kikenda
chombo, nikaliona kaburi,
Mawimbi kupiga
kumbo, hamkani si shuwari.
Kiitikio
Sitopanda
majahazi, vingalawa na vihori,
Adha yake
siiwezi, ya kuleweshwa chakari,
Sisafiri kwa
nyambizi, wala kubwa manuwari.
vi.
Takriri: ( Kikwamba )
Mbinu ya kurudia rudia neno katika
nafasi maalum katika mshororo katika ubeti. Takriri hii
inaonekana katika mashairi kama
KWA HERI, HATUKUBALI, NILINDE.
KWA HERI
Ingawa umenuna,
vishavu vyako kutuna,
Kunapambazuka,
jua linatoka,
Bado
kunakucha,
Kwa heri.
Ingawa
mekasirika, na uso kusawijika,
Zinavuma
pepo, hata kama hupo,
Kusi
matlai,
Kwa heri
vii. Ukaraguni:
Ni mbinu ambayo vina vya mwanzo na mwisho vinatofautiana katika
beti katika shairi zima.
Mtindo huu unajitokeza vilivyo katika shairi la KANSA.
Jamii imeoza,
imeoza yanuka,
Uchafu
wachomoza, wachomoza wafoka,
Inatoa
mafunza, mafunza yamwagika.
Imetunga
usaha, usaha usokwisha,
Yazidisha
karaha, karaha yatapisha
Yahatarisha
siha, siha inadhohofisha.
viii. Ukara:
mbinu ambayo vina vya kipande kimoja
vinabadilika wakati vina wakati vina vya kipande
kingine vinakaririwa ubeti mmoja hadi mwingine katika shairi. Mbinu hii,
mshairi huyu
ameitumia katika mashiri kadhaa kama
vile; NILINDE, JIWE SI MCHI, MAMA
NTILIYE,
SIKUJUA.
NILINDE
Nilinde sichukuliwe, hata
kwa moja shubiri,
Tubaki mimi na wewe, pendo
letu linawiri,
Tuwazidishe kiwewe, wasotutakia heri.
Nilinde unifutike, wala
sione usiri,
Mikononi nisitoke, hata
ikizuka shari,
Kwa huba unigubike, niwe
katika suduri.
C. MATUMIZI YA LUGHA
Diwani ya
WASAKATONGE imetumia lugha fasaha ya Kiswhili ambapo msamiati katika mishororo
umepangiliwa katika namna inayovuta udadisi, hisia na matumizi kadhaa vipengele
vya hisi kama picha, sauti na uchaguzi wa maneno ili hadhira agundue mchomo
ambao malenga huyu aliupata naqzo (hisia ) zaweza kuleta jazba.
§ Matumizi ya tamathali za semi
Tamathali za semi ni viwakilisho au vifananisho vya dhana nyingine
tofauti au zinazofanana. Nazo zaweza kupanua, kupuuza ama kubadilisha maana za
wazi ili kuleta maana maalum katika ushairi.
Diwani hii ina utajiri wa tamathali za semi kama ifuatavyo:
a. Tashbiha:
Ni tamathali
inayofananisha vitu kwa kutumia maneno ya ufananisho. Tashbiha imeonekana
vizuri katika NILINDE, NILICHELEWA
KUPENDWA, KANSA, MWANAMKE.
MWANAMKE
Namwona kitandani,
Yu uchi maungoni,
Ni mrembo,
Kama chombo,
Chenye ushawishi,
Mzima utashi.
b. Sitiari:
Ni ufananisho wa moja kwa
moja bila kutumia maneno ya ufananisho. Sitiari inajidhihirisha katika mashairi
kama TIBA ISOTIBU, MTEMEA MATE MBINGU, MAHABA, JIWE SI MCHI, WEWE JIKO LA
SHAMBA.
WEWE JIKO LA SHAMBA
Wewe ni jiko
la shamba, si kuka
si seredani,
Mezoea kumba kumba, kila aina ya
kuni,
Kwangu huwezi kutamba, nimekutoa
thamani.
c. Msisitizo bayani
Ni tamathali ambayo
hutumika kusisitiza jambo kwa kutumia kinyume. Tamathali hii yaonekana kwa
urahisi katika mashairi kama BUZI LISILOCHUNIKA, NILICHELEWA KUPENDWA, MCHEZA
HAWI KIWETE, BANDARINI.
MCHEZA HAWI
KIWETE
Si unyago si
sindimba, na wewe
kadhalika,
Hata kukiwa na rumba, machezo
hayatatoka,
Mkilema hata tamba, ngoma yake
kunogeka,
Mcheza hawi kiwete, ngoma yataka
matao.
d. Tashhisi: hali ya kuvipa vitu sifa za
binadamu na kuonekana kutenda kama binadamu. Tamatahali hii imeonkana pia kwa
urahisi katika mashairi kadhaa, baadhi ni kama vile AFRIKA, NILICHELEWA
KUPENDWA, PENDO TAMU.
PENDO TAMU
Pendo lenye tabasamu, za dhati si za uheke,
Na nyoyo za ukarimu, uchoyo ni
sumu yake,
Haliishi yake hamu, hupendi
imalizike.
e. Mubaalagha/ udamisi/ chuku: hali
yakutia chumvi sana mambo yanayoonekana kuwa ni ya kawaida. Yanatiwa chumvi kwa
makusudi ya kuleta athari maalum iliyokusudidwa
na mwandishi. Nayo yaonekana katika mashairir kama KANSA, AFRIKA na
PENDO TAMU.
KANSA
Jamii imeoza, imeoza yanuka,
Uchafu wachomoza , wachomoza
wafoka,
Inatoa mafunza, mafunza
yamwagika.
f.
Taashira: ni tamathali hutamka sehemu ya kitu
kinachohusiana na kingine kikubwa ili kuwakilisha kitu kamili. Tamathali hii
yaweza kuonekana kwa uzuri katika shairi la WASO DHAMBI.
Wavilemba!
Wavilemba, na
majoho safi roho, tasbihi,
Wajigamba,
safi roho, ni kebehi,
Wanotenda
Unafiki.
§ Taswira:
Ni mkusanyiko wa picha zinazoundwa na maelezo ya jumla ya msanii katika
kazi yake ya kifasihi.
Katika kazi ya fasihi , taswira hujengwa kutokanan na matumizi ya
tamathali za semi, hasa SITIARI na tashbiha na ishara mbali mbali zenye kuhusu
mawazo, dhana, vitu na umbile na kadhalika. Ujenzi wa taswira humfanya msomaji
apate aina mbali mbali za hisi kama za kunusa , kuona , kugusa na kusikia.
Katika diwani hii, mshairi
ametumia tswaira mbali mbali kama vile “ tonge la ugali” katika shairi la TONGE LA UGALI kuashiria madaraka. Kwahivi
katika shairi hili mshairi anaweka wazi tatizo la kugombea madaraka.
Wanapigana,
Wanaumizana,
Wanauana,
Kwa tonge la ugali!
Pia kuna matumizi ya picha ya “ nahodha “ kuashiria kiongozi wa jamii, “
jahazi “ kumaanisha nchi au jamii. Katika shairi hili mshairi anaweka wazi
tatizo la kung’ang’ania madaraka. Hili ni shairi la NAHODHA.
Nahodha,
Wang’ang’ania sukani
Na
jahazi lenda mramamrama,
Mrama,
na kupasuka mataruma,
Mataruma, mkuku umeachama,
Meachama, tanga limo kudatama,
Kudatama, foromali yainama,
Yainama , chombo sasa kitazama,
Nahodha tosa nanga!
Kama vile haitoshi mshairi huyu ametumia taswira ya “jiko la shamba”
katika shairi la WEWE JIKO LA SHAMBA kuashiria
mwanamke asiyejiheshimu ( Malaya ) anayeshiriki tendo la ndoa na kila mwanaume.
Wewe
jiko la shamba, si kuka si seredani,
Mezoea kumbakumba, kila aina ya
kuni,
Kwangu
huwezi kutamba, nimekutoa thamani.
Vile vile, malenga huyu ametumia picha ya “vinyonga” katika shairi la
VINYONGA kumaanisha viongozi vigeugeu au wasaliti.
Jukwaa
Meingiliwa,
Wanasiasa
vinyonga,
Maisha
ya ufahari,
Kauli
zao nzuri,
Vitendo
vyao hatari,
Ni
kinyume na maadili,
Ni
usaliti.
Taswira nyingine inayoonekana katika kazi hii ni ya “fahari la
dunia”,katika shairi la FAHALI LA DUNIA, malenga anamaanisha mataifa ya
kibeberu/ makubwa. Mataifa haya yanaonea mataifa madogo kisiasa, kiuchumi, hata
kitamaduni.
Fahali la dunia,
Lisilo na
huruma, linatesa,
Linapiga vindama,
Na
wengine wanyama,
Tena
bila ya huruma,
Laoneya.
Tena, “bundi” ni taswira nyingine iliyotumika kazi hii, nayo yapatikana
katika shairi la BUNDI, picha hii imetumika kuashiria ukoloni mamboleo. Ukoloni
mamboleo bado upo na hautoki. Mataifa ya
magharibi yanaendelea kutawala mataifa madogo kwa mbinu nyinginne.
Bundi hataki kubanduka,
Yu
paani amejipachika,
Lalialia kila dakika,
Mambo si salama,
Hakuna uzima,
Ila
ni nakama
Sote
twayoyoma,
Hakujacha.
§ Misemo:
Hizi ni kauli zinazozuka ghafla
katika jamii kufuatana na matukio maalum katika jamii nayo husadifu ukweli.
Misemo kadhaa imetumika katika kazi hii; nayo hubeba maana iliyokusudiwa.
ü Sakubimbi jendaheka:
Msemo huu unaonekana
katika shairi la MAMA NTILIYE
Wameshindwa wenye nyusi,
na kope kukamilika,
Hawakunipa mkosi, ndio
kwanza nachanika,
Seuze ukaragosi, sakubimbi jendaheka.
ü Kumbakumba:
Msemo huu unapatikana
katika shairi la WEWE JIKO LA SHAMBA
Wewe ni jiko la shamba,
si kuka si seredani
Mezoea kumbakumba, kila
aina ya kuni,
Kwangu huwezi kutamba, nimekutoa
thamani.
§ Methali:
hizi ni tungo zenye mpangilio maalum wa maneno yenye hekima, busara,
mafunzo na maadili kwa jamii. Ubora wa hekima hiyo hutegemea muktadha au mahali
ambapo methali hiyo hutumika.
Methali imetumika katika shairi la SADDAM HUSSEIN, nayo ni “ulopanda
utavuna!”
Nakuafiki, Saddam,
si kwa Uislamu wako,
Ni wako muumba,
Ingawa Raisi,
Ajua yako ila,
Saddam, ulopanda utavuna!
MAUDHUI YA
WASAKATONGE:
Maudhui ni
jumla ya mambo yanayoelezwa ama kujitokeza katika kazi ya kifasihi. Maudhui ya
kazi ya kifasihi hujumuisha dhamira , ujumbe, maadili, migogogoro na falsafa.
Diwani ya
Wasakatonge imesheheni maudhui yanayogusa mmbo kadhaa yanayoizunguka jamii
inayoandikiwa. Malenga huyu anatanabaisha matatizo yanayoikumba jamii
kinagaubaga ambayo hasa ndiyo chanzo cha ugumu na uduni wa maisha ya jamii
inayoandikiwa.
Katika diwani
hii dhamira mbali mbali zimejadiliwa.
A. Dhamira:
Ni lengo , kusudio au msukumo alionao msanii katika kuumba kazi yake ya
kifasihi. Msanii anawezakuwa na lengo la kuonesha mambo mbali mbali yatukiayo
ndani ya jamii yake anayoiandikia.
Kazi ya malenga huyu yaweza kugawanywa katika maeneo matatu kidhamira,
nayo ni kama ifuatavyo;
1. Kisiasa:
Malenga huyu anaonekana
kusumbuliwa mno na mienendo yetu kisiasa ambayo hakika ndiyo inayochangia jamii kusonga mbele au
kurudi nyuma kimaendeleo. Kisiasa anaichora jamii hivi.
a. Ung’ang’aniaji wa madaraka:
Mshairi anasikika akilia
kwa uchungu juu ya jambo hili lililokuwa kero kubwa ndani ya jamii. Walio
madarakani wamekuwa wagumu mno kuachia madaraka wakati unapotimu. Mshairi
anasikika vizuri katika mashairi ya TONGE LA UGALI na NAHODHA.
NAHODHA
Nahodha,
Wang’ang’ania sukani,
Mechafuka, bahari si
shwari,
Si shwari, pepo
zinatuathiri,
Zatuathiri, na mawimbi ni
hatari,
Ni hatari, tufani
meshamiri,
Meshamiri, na mvua
zitiriri,
Zitiriri,radi nazo si
kadiri,
Nahodha tosa nanga.
b. Unyanyasaji na ukandamizaji wa raia:
Malenga huyu ametoa kilio
chake pia katika suala hili la dola kuinyanyasa jamii yake. Dola imekuwa
ikitumia mamlaka yake vibaya kuwaonea raia wanyonge. Kilio hiki kinasikika
vizuri katika mashairi ya UNYAMA, MIAMBA
na MARUFUKU. Sikia kilio cha msanii katika shairi la MARUFUKU.
Sitaki uone,
Ingawa una macho,
Sitaki useme,
Ingawa una mdomo,
Sitaki usikie,
Ingawa una masikio,
Sitaki ufikiri,
Ingawa una akili,
Sababu utazinduka,
Utakomboka,
Uwe mtu,
Hilo sitaki
Marufuku.
c. Kukosekana kwa uelekeo au itikadi:
Jambo lingine
lililomfanya Malenga huyu kutoa machozi ni hilo. Jamii yoyote ile inapokosa
itikadi inakuwa sawa na ndege isiyo na rubani. Mshairi wetu anatoa kilio cha
kite kuhusu jambo hilo katika mashairi ya NALITOTE na TWENDA WAPI?
Katika shairi la TWENDA
WAPI? Mshairi anasema uchungu.
Twenda wapi?
Mashariki “siko”!
Magharibi “siko”!
Wapi tuendako?
Tunatapatapa!
d. Ukoloni mamboleo:
Mshairi anasema kuwa
pamoja na jamii yake kujipatia uhuru mapema miaka ya 1960 bado jamii hii
imezongwa na inaishi chini ya ukoloni mamboleo. Jamii imechorwa ikishindwa
kufanya maamuzi bila kuingiliwa na mataifa makubwa ya Ulaya. Malenga huyu
analisema hili kupitia HATUNA KAULI, KLABU, HATUKUBALI, TIBA ISOTIBU,
WAFADHILIWA.
WAFADHILIWA
Wafadhiliwa
kufurahishwa,
Ni sera zao kupitishwa,
Rais anaamrishwa,
Tekeleza!
2. Kiuchumi:
Mshairi pia amejadili
matatizo ya kiuchumi yanayoizonga jamii yake. Baadhi ya aliyoyaweka qazi ni
pamoja na;
a. Uwepo wa matabaka kati ya wanajamii.
Mshairi analia juu ya
msuguano wa kitabaka uliomo ndani ya jamii yake. Mshairi analia mno na hali
hiyo inayowatenganisha wanajamii katika makundi mawili ya walionacho na
wasionacho. Mashairi ya ASALI LIPOTOJA, MUMIANI, WASAKATONGE, na MVUJAJASHO.
ASALI LIPOTOJA
Asali lipotoja,
Wengine walikuja,
Na mirefu mirija,
Kwao kawa tafrija,
Wakapata faraja,
Sisi tukatengwa.
Kairamba asali,
Kafakamia kweli,
Nao hawatujali,
Wakatutenga mbali,
Kwa fujo na kejeli,
Wakatoneya.
b. Kutokuwajibika kwa wanajamii:
Mshairi anaiona jamii
yake kama jamii isiyotaka au isiyopenda kufanya kazi na hivi kutegemea misaada
na huruma za nchi tajiri. Jambo hili linamkera mno na kumuumiza hata kulisemea.
Mshairi ananung’unikia hali hiyo katika KLABU na WANAWAKE WA AFRIKA. Angalia
kilio cha mshairi katika KLABU.
Tusiwe tegemezi,
Ila tuchape kazi,
Tutumiye ujuzi,
Tuvijenge viwanda,
Na kilimo kutanda,
Ufugaji kushinda.
c. Njaa na ukame:
Mshairi anaguswa pia na
hali ya ukame na njaa inayoikumba jamii yake.
Jamii imejadiliwa
ikizongwa na ukame usiokwisha unaosababisha njaa. Mshairi anailalamikia hali
hiyo katika shairi la AFRIKA.
Lini?
Afrika utakuwa,
Kitalu chenye shibe,
Na njaa isikabe,
Pia watu washibe,
Ni lini?
Lini?
Afrika utakuwa,
Adui wa ukame,
Kwa vyovyote uhame,
Na usikuandame,
Ni lini?
d. Ugumu wa maisha:
Mshairi tena anaumizwa na
ugumu wa maisha unaowazonga wanajamii wake ingawa wanajitahidi kupambana kwa
kila hali. Mshairi analiweka hilo bayana kupitia mashairi ya AFRIKA, MVUJA
JASHO, TWENDA WAPI? Angalia kilio chake katika MVUJA JASHO
Kila mvuja jasho,
Maishaye ya kesho,
Si ya utajirisho,
Achumacho ni posho,
Mbaya wake mwisho,
Lazima suluhisho,
Lakini kwa vitisho.
3. Kijamii:
Kijamii pia mshairi
amesumbuliwa na masuala kadhaa katika jamii yake kama alivyosumbuliwa na
masuala ya kisiasa na kiuchumi. Masuala hayo ya kijamii ni kama;
a. Usaliti na unafiki wa viongozi wa
dini:
Ndani ya jamii
anayoiandikia, mshairi analalamikia viongozi wa dini kwa kutokuwa wakweli na
wawazi kwa wale wanaowaongoza. Mshairi anaumia dhidi ya mitindo yao ya maisha
ambayo imeshindwa kuwa mfano mzuri kwa jamii. Mshairi anayaonesha hayo katika
mashairi ya UASI na WASO DHAMBI. Sikiliza sauti yake katika UASI
Uasi,
Katika dini,
Masheikh na masharifu,
Mapadri na maaskofu,
Kauli zao nadhifu,
Hujigamba waongofu,
Wengi wao ni wachafu,
Wenye vitendo dhaifu,
Dini wanazikashifu,
Wanafiki.
b. Ukabila na udini:
Mshairi analia tena juu
ya tabia hii iliyoota mizizi miongoni mwa jamii nyingi za kiafrika ya
kuendekeza undugu, ukabila na udini ambayo ni chanzo cha uvunjifu wa amani
ndani ya jamii yake. Mshairi anayasema hayo katika AFRIKA na SADDAM HUSSEIN.
AFRIKA
Lini?
Afrika utakuwa,
Bustani ya amani,
Ukabila kuuzika,
Udini kuufyeka,
Ni lini?
c. Ushoga, usagaji na umalaya:
Mshairi anaisuta pia jamii yake juu
ya tabia ya kujenga uhusiano kinyume na maumbile iliyojengeka ndani ya jamii
yakepia tabia ya ufuska ambazo ni kero kubwa kwa jamii. Mshairi analisema hilo
kupitia mashairi ya WEWE JIKO LA SHAMBA na
JIWE SI MCHI. Angalia shairi la JIWE SI MCHI.
Vinu wenzake ni michi, wala
sibadilishiwe,
Ufundi haujifichi, utwanzi na mizunguwe,
Jiwe la manga si fichi,
haiakidhi hajawe.
d. Unafiki, majungu na umbeya miongoni
mwa akina mama:
Hili ni jambo lingine
ambalo linamuumiza kichwa mshairi huyu. M.S. Khatib analia juu ya tabia ya
akina mama ya kuendekeza fitina, vitimbi na kufanyiana majungu bila sababu ya msingi. Anaitaka jamii hii
iachane kabisa na jambo hilo. Anayaesema hayo kupitia WANAWAKE WA AFRIKA na MAMA NTILIYE.
Msikie mshairi huyu
katika WANAWAKE WA AFRIKA.
Achaneni
kusengenyana,
Waama kununiana,
Kugombana,
Kusutana,
Nguvu zenu zapungua,
Mtashindwa!
Msikie tena katika MAMA
NTILIYE
Majungu na makaango, jinsi
unavyoyapika,
Wakazanisha na shingo,
moto uzidi kuwaka,
Kwa uzushi na uwongo,
kumbe kwako umefika.
e. Mwanamke kuwa chombo cha starehe:
Vilevile mshairi anainyooshea kidole
jamii yake kutokana na mtazamo ilionao kwa mwanamke kuwa kama chombo cha
kuburudisha macho na miili ya wanaume. Hili linaonekana katika shairi la
MWANAMKE.
Namwona kitandani,
Yu uchi maungoni,
Ni mrembo,
Kama chombo,
Chenye ushawishi,
Mzima utashi.
f.
Mwanamke
kufanywa mlezi pekee wa familia:
Hili nalo linamliza
mshairi, mbali ya kufanywa kuwa ndiye msimamizi pekee wa familia bado mama huyu
hathaminiwi na jamii yake. Hili laonekana katika shairi la MWANAMKE.
Namwona yu nyumbani,
Mpishi wa jikoni,
Yaya yeye,
Dobi yeye,
Hakuna malipo,
Likizo haipo.
g. Mapenzi ( uhusiano wa kijinsiakati ya
watu wawili )
Mshairi anautazama
uhusiano huu katika namna mbili. Wapo wanajamii ambao wamekuwa wakijenga
uhusiano wa kilaghai na wenzao labda kwa lengo la kujinufaisha kiuchumi au
kukidhi haja za miili yao. Jambo hili linamuumuza sana mshairi kwani mapenzi ya
namna hii yanazingirwa na:
usaliti kama inavyojitokeza katika USIKU WA
KIZA
usiku wa kiza, nimejiinamia,
sana nakuwaza, nakufikiria,
wakunipumbaza, meniondokeya.
Kukosekana kwa amani
kama ilivyojitokeza ITOE KAULI YAKOna USIKU WA KIZA.
ITOE KAULI YAKO
Kitoe chako kiapo, kama kweli
wanipenda,
Niweze kujizatiti, moyo uondoke
funda,
Nizidi kukudhibiti, sikuache
hata nyanda.
Kukosekana kwa furaha
ndani ya nyumba kama inavyojitokeza katika SI WEWE na USIKU WA KIZA.
USIKU WA KIZA
Meniondokeya, wangu mahabuba,
Nilikuzoweya,kwa yako mahaba,
Nnajikondeya, sili nikashiba.
Pia yapo mapenzi
yaliyosheheni udhati na ukweli, mapenzi ya namna hii yamezingirwa na mambo haya;
Udhati, faraja na raha
kati ya wapendanao. Hili linaoneshwa katika mashairi ya MAHABA na NILINDE.
NILINDE
Nilinde wasinipate, wabaki
kutahayari,
Tubaki chanda na pete, kama
udi na ambari,
Wabaki kumeza mate,
waambulie sifuri.
Amani na utulivu miongoni
mwa wapendanao, hili laonekana katika mashairi ya TUTABAKI WAWILI na WEWE
WAJUA.
TUTABAKIA WAWILI
Wenyewe tunajienzi, hakuna
cha kuhofia,
Tunaishi kwa mapenzi, raha
kuziogelea,
Wala hatuna simanzi, roho
zetu maridhia.
Furaha kati yao
wapendanao kama ilivyo katika YEYE NA MIMI na PENDO TAMU.
Angalia PENDO TAMU.
Pendo lisilo maudhi, na wala
upekepeke,
Wawili limeturidhi, ni kubwa
haiba yake,
Kupendana ni faradhi, yeye
wangu mimi wake.
B. Ujumbe:
Ni taarifa anazotoa msanii kwa hadhira,; ujumbe mara nyingi hutokana na
dhamira na unaweza kujitokeza wazi au kwa kujificha.
Katika diwani ya Wasakatonge mshairi anatoa ujumbe ufuatao;
ü Mwannamke ana haki sawa na mwanaume
yeyote kayika jamii kupitia mashairi ya MWANAMKE.
ü Matabaka ni chanzo cha migogoro
katika jamii; hili linaonekana kupitia mashairi kama WASAKATONGE, MVUJASHO na
WALALAHOI.
ü Mapenzi ya dhati hujenga mshikamano
na uaminifu ndani ya jamii kupitia mashairi kama TUTABAKIA WAWILI, PENDO TAMU
na YEYE NA MIMI.
ü Kufanya kazi kwa bidii ni suluhisho
la umaskini; ujumbe huu unaonekana kupitia shairi la WANAWAKE WA WAAFRIKA na KLABU.
ü Uongozi mbaya ni chanzo cha umaskini
na minyukano ndani ya jamii; taarifa hii yapatikana kupitia SADDAM HUSSEIN,
UNYAMA na MIAMBA.
ü Tohara kwa wanawake huweza kuleta
matatizo makubwa kama vifo na magonjwa, anasema hili katika shairi la TOHARA
ü Kung’ang’ania madaraka kunaweza
kukaleta kukosekana kwa raha na amani na
kutokushirikiana miongoni mwa wanajamii. Hili linasemwa kupitia shairi la NAHODHA na TONGE LA UGALI.
C. Maadili:
Haya ni mafunzo, nasaha au ushauri unaopatikana mara baada ya kusoma kazi
ya kifasihi. Malenga huyu anatoa ushauri kwa jamii yake kulingana na
mazingira waliyomo.
ü Malenga huyu anaitaka jamii yake
iachane na utamaduni wa kumkkeketa mwanamke kwani hakusaidii lolote. Anasema
hilo kupitia shairi la TOHARA
ü Mshairi anaishauri jamii yake
kuachana na tabia ya kung’ang’ania madaraka kwani haina faida yyoyote. Hili
linajidhihirisha kupitiaTONGE LA UGALI na NAHODHA.
ü Vile vile mshairi anaitaka jamii yake
ipige vita tabia kushiriki tendo la ndoa kinyume na maumbile na ufuska kupitia
JIWE SI MCHI na WEWE JIKO LA SHAMBA.
ü Mshairi anaitaka jamii yake ifanye
kazi kwa bidii na kuachana na tabia ya utegemezi kupitia KLABU.
ü Mshairi tena anaitaka jamii yake
kujifunza kuwa na upendo wa kweli hasa kwa wanandoa ili kuimarisha ndoa zao
kupitia mashairi ya YEYE NA MIMI, PENDO TAMU na WEWE WAJUA.
KUFANIKIWA AU KUTOFANIKIWA KWA MWANDISHI
KIMAUDHUI
Mwandishi amefaulu kimaudhui kwa kuonesha udhaifu mkubwa
unaomea ndani ya jamii yake anayoiandikia kuanzia kwa viongozi mpaka kwa mtu
mmoja mmoja.
Mshairi huyu amefanikiwa kuwachora viongozi kama ndio chanzo
kikuu cha matatizo yaikumbayo jamii kwa kushindwa kuwajibika vilivyo katika
dhamana walizokabidhiwa na hivyo kuzua mitafaruku mingi ndani ya jamii hii; wao
ndio vyanzo vya kukithiri kwa rushwa ndani ya jamii yetu hasa wanaposhindwa
kukemea au wao wenyewe kuwa washiriki wa tendo hilo kama alivyoliweka wazi hili
katika shairi la KANSA au MVUJA JASHO.