Unachopaswa kufanya siku ya uchaguzi
Jaji Damian Lubuva, Mwenyekiti NEC
Dar es Salaam. Tanzania inaelekea kwenye
Uchaguzi Mkuu, Oktoba 25, mwaka huu. Baadhi ya wananchi hasa vijana
waliofikisha miaka 18 hivi karibuni hawajawahi kushiriki kwenye uchaguzi
wowote na uchaguzi huu ni wa kwanza kwao.
Vijana hawa
na watu wengine, wanahitaji kujifunza au kukumbushwa juu ya mambo ya
kufanya siku ya uchaguzi ili kufanya zoezi la upigaji kura kuwa lenye
mafanikio na kuepusha uvunjifu wa sheria unaoweza kumweka mtu matatani.
Kwa
bahati mbaya, elimu kwa mpigakura haitolewi mara kwa mara kwa wananchi
mpaka nyakati za uchaguzi. Hata wakati huo ukifika, baadhi ya watu hasa
wale wa hali ya chini, hawafikiwi na elimu hiyo.
Elimu
kwa mpiga kura bado inahitajika ili kila mwananchi afahamu haki na
wajibu wake katika mchakato mzima wa uchaguzi. Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(Nec) ndiyo yenye jukumu la kutoa elimu hiyo kwa kushirikiana na wadau
wengine.
Hata hivyo, zoezi hili linakabiliwa na
changamoto ya uhaba wa rasilimali za kufanikisha utoaji wa elimu kwa
wapigakura. Vilevile, hakuna chombo maalumu cha kuratibu na kusimamia
utoaji wa elimu ya uraia.
Mwenyekiti wa Nec, Jaji
Damian Lubuva anasema changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ni pamoja na
uhaba wa Asasi za kiraia zinazotoa elimu kwa wapigakura na kuwafikia
wananchi wote nchi nzima.
Jaji Lubuva anasema Tume
imejipanga vizuri kuhakikisha kwamba elimu inawafikia wapigakura nchi
nzima. Anasema watatumia vyombo vya habari vikiwamo vinavyomilikiwa na
taasisi za dini ili kuwafikia wananchi haraka zaidi.
Zingatia haya siku ya uchaguzi
Mkurugenzi
wa uchaguzi – Nec, Kailima Kombwey anafafanua mambo muhimu ambayo
mpigakura anatakiwa kufanya siku ya uchaguzi bila kuathiri masharti ya
sheria za uchaguzi na kanuni zake.
Wahi kituoni
Anasema
jambo la kwanzana la msingi ni kuwahi asubuhi katika kituo cha kupigia
kura. Kombey anasema wananchi wanatakiwa kufika vituoni kuanzia saa
moja asubuhi wakiwa na vitambulisho vyao vya kupigia kura.
Anasema
kila mpigakura anatakiwa kujua kituo atakachopigia kura na kuhakiki
kama jina lake lipo kwenye orodha ya wapigakura kwenye kituo husika.
Panga foleni
Kombey
anabainisha kuwa watu watapanga foleni kuingia chumba cha kupigia kura
na vituo vitafungwa kuanzia saa 10 jioni. Anasema watakaokuwa kwenye
mstari baada ya muda huo wataruhusiwa kuendelea kupiga kura mpaka
watakapomaliza.
“Tunasisitiza wananchi wajitokeze kwa
wingi ili wawachague viongozi wao. Kupiga kura ni jambo la muhimu kwa
maendeleo ya Taifa letu. Wasipojitokeza basi wasilaumu kiongozi
atakayechaguliwa na wengine,” alisema Kombwey.
Mkurugenzi
huyo anasema katika uchaguzi wa mwaka 2010, waliandikisha watu milioni
20 lakini waliojitokeza kupiga kura walikuwa chini ya milioni 10. Kwa
hiyo, anasisitiza zaidi kujitokeza kupiga kura siku hiyo.
Usivae sare za chama
Jambo
la pili, mpigakura asivae nguo yenye nembo au alama yoyote ya chama cha
siasa kwenye kituo cha kupigia kura. Kufanya hivyo ni kukiuka taratibu
za uchaguzi na mtuhumiwa anaweza kushitakiwa kwa kuhujumu mchakato wa
upigaji kura.
Kombey anafananisha jambo hilo na
akufanya kampeni siku ya kupiga kura, jambo ni kinyume na kanuni. Kwa
hiyo, fulana, kofia, bendera au kanga au nguo yoyote inayovaliwa na
chama chochote haitakiwi kwenye eneo la kupigia kura.
“Tunatoa
muda wa kampeni ili wanasiasa na vyama vyao wajinadi kadri wanavyotaka
lakini siku ya uchaguzi siyo siku ya kufanya kampeni, ni kinyume cha
kanuni za uchaguzi,” anasema mkurugenzi huyo.
Anaendelea
kubainisha kuwa Tume kupitia kifungu cha 124 (a) cha sheria ya taifa ya
uchaguzi ya mwaka 1985 ilianda maadili ya uchaguzi ambayo yamefanyiwa
mabadiliko madogo mwaka huu na kukubaliwa na vyama vyote.
Wahusika
wakuu katika maadili haya ni Tume ya Uchaguzi, Serikali, wagombea na
wanachama wote wa vyama vya siasa. Kombwey anasema wadau hawa kwa pamoja
wana wajibu wa kufanya uchaguzi huru na wa haki.
Usilete ushabiki
Jambo
la tatu, wapigakura wasilete ushabiki kwenye vituo vya kupigia kura.
Mambo ya ushabiki ni pamoja na kuongelea matokeo ya uchaguzi kabla
hayajatangazwa na mamlaka husika zilizokasimiwa jukumu hilo.
Mkurugenzi
huyo anafafanua kwamba jambo hilo linajenga hisia tofauti miongoni mwa
wapiga kura na linaweza kusababisha vurugu endapo matokeo yatakuwa
kinyume chake. Anabainisha kuwa kura ni siri ya mpigakura mwenyewe.
“Sitarajii
kuona watu wakitengeneza makundi ya kujadili mwenendo wa uchaguzi
kwenye vituo. Hiyo ni sawa na kampeni siku ya uchaguzi, hatutaacha
ufanyike kwa sababu utaharibu mchakato wa uchaguzi,” anasema.
Ukipiga kura nenda nyumbani
Jambo
la nne, mwananchi akimaliza kupiga kura aende nyumbani kusubiri matokeo
kutangazwa. Kuendelea kukaa kwenye vituo vya kupigia kura kunasababisha
msongamano usio wa lazima.
Kombwey anasema hakuna haja
ya kukaa kwenye vituo vya kupigia kura kwa ajili ya kulinda kura kwa
sababu tayari mawakala wa vyama vya siasa wapo kwa ajili ya kuangalia
mwenendo mzima wa uchaguzi.
“Ile dhana ya kutaka
kulinda kura zisiibiwe ndiyo inayosababisha vurugu kwenye vituo. Hizo ni
hisia tu, hakuna wa kuiba kura kwa sababu kuna mawakala wanaowakilisha
vyama vyao,” anasema.
Tume ina jukumu la kutangaza matokeo
Anasema
jukumu la kutangaza matokeo ya urais ni la Tume ya uchaguzi. Tume pia
imekasimisha jukumu la kutangaza matokeo ngazi ya kata kwa msimamizi
msaidizi wa kata na ngazi ya jimbo kwa msimamizi wa halmashauri.
Kombwey
anasema kuna baadhi ya watu wanatishia kutangaza matokeo endapo Tume
itachelewa kufanya hivyo. Anasisitiza kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha
utaratibu kwa sababu hakuna mtu mwenye jukumu hilo zaidi ya Nec.
Anasema
Nec imejipanga kutangaza matokeo ya urais ndani ya siku tatu kwa
sababu watatumia Mfumo wa Kusimamia Matokeo (RMS) ambao utawawezesha
kupokea, kujumlisha na kutangaza matokeo.
Licha ya
kutakiwa kisheria kutangaza matokeo hayo ndani ya siku saba, Nec
imebainisha kwamba mfumo huo utasaidia kuongeza kasi ya ukusanyaji wa
matokeo kutoka sehemu mbalimbli nchini.
Mabadiliko ya sheria
Jaji
Lubuva anasema mabadiliko makubwa ya sheria ya uchaguzi yalifanyika
mwaka 2010, mwaka huu sheria hiyo haijafanyiwa marekebisho isipokuwa
kanuni za uchaguzi zimerekebishwa ili kuleta ufanisi katika uchaguzi
ujao.