Msafara wa Lowassa wapigwa mabomu
Mgombea
urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa akizungumza na polisi
kwenye Daraja la Nduruma mjini Arusha, baada ya kufunga Barabara ya
Sabasaba wakati akitokea kwenye Uwanja wa Tindigani. Polisi walimkubalia
kupita barabara hiyo na kuzuia msafara wake. Picha na Mussa Juma
Ukawa walaani kupigwa mabomu
-
Arusha. Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema
na Ukawa, Edward Lowassa jana kwa mara ya kwanza alikumbana na joto la
upinzani baada ya msafara wake kushambuliwa na mabomu ya polisi.
Tukio
hilo, ambalo lilifanyika mbele ya msafara wa Lowassa, lilitokea jana
eneo la Daraja la Nduruma katika Jiji la Arusha na kusababisha umati wa
watu kutawanyika na wengine kutelekeza magari yao.
Wakati
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akimkaribisha kwenye chama hicho
wakati wa mkutano mkuu alimwambia; “Mzee huku inabidi uwe unafanya
mazoezi kidogo, kuna mabomu huku.”
Lowassa alikumbwa na
kadhia hiyo, akiwa njiani na mgombea mwenza, Juma Duni Haji na viongozi
wengine wa Ukawa, wakitokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro
(KIA), huku wakiwa wamesindikizwa na umati wa watu na magari.
Tamko la polisi
Kamanda
wa polisi mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema kuwa polisi
walilazimika kupiga mabomu ya machozi ili kutawanya watu waliokuwa
wakiwarushia mawe polisi na wengine kufunga barabara.
“Kwa
hali ile, tungefanya nini? Wanatupa mawe kwa polisi na wamefunga
barabara na kuzuia magari mengine yasipite…ikumbukwe kulikuwa hakuna
kibali cha maandamano na hata kingekuja, matamko ya kuzuia maandamano
yameshatolewa,” alisema Sabas.
Katika tukio hilo, idadi
kubwa ya polisi walikuwa kwenye magari na silaha mbalimbali ambao
baadaye walianza kurusha mabomu kutawanya watu na magari kwa eneo la
daraja hilo.
Hata hivyo, katika tukio hilo, lililotokea
saa nane mchana hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa na kutokana na nguvu
hiyo ya polisi watu walitawanyika, na barabara hiyo ya Arusha- Moshi
ilifunguka baada ya kutopitika kwa saa tano kuanzia saa nne asubuhi.
Ukawa walaani kupigwa mabomu
Akizungumza
katika mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa Tindigani, Mbunge wa jimbo
la Arusha, Godbless Lema alisema wamesikitishwa na kitendo cha polisi
kumpiga mabomu Lowassa na msafara wake.
“Tunajua polisi
wamepata maelekezo na sasa wanataka kuwatisha wananchi, lakini tunasema
leo ndiyo mwisho hatutakubali tena kunyanyaswa,” alisema Lema.
Kuwasili Lowassa
Lowassa aliwasili KIA saa 3:20 asubuhi akiwa ameongozana
na viongozi wa Ukawa, Mbowe, Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia
na Mwenyekiti wa NLD, Emmanuel Makaidi, Kaimu Mwenyekiti wa CUF taifa,
Twaha Taslima na viongozi wengine.
Kwenye Uwanja wa
KIA, shughuli mbali mbali zilisimama katika eneo la kushuka viongozi
mashuhuri (VIP), ambapo mawaziri kadhaa walikuwa katika eneo hilo.
Baadhi
ya viongozi hao ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG), Profesa Mussa Juma Hassadi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Dk Mary
Nagu, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tzeba.
Baada
ya Lowassa kutua KIA, alikwenda moja kwa moja kwenye Hoteli ya KIA
Lodge na mgombea mwenza wake, Juma Duni Haji kwa mapumziko mafupi.
Baada
ya kupumzika saa 5:30 msafara ulianza kuelekea uwanja wa Tindigani
Kimandolu na ulifika saa tisa na kukutana uwanja ukiwa tayari umefurika
maelfu ya watu.
Akihutubia mkutano huo Lowassa
alitahadharisha viongozi wa polisi, kuacha kutumia nguvu kupita kiasi,
kwani anaweza kuwafikisha Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) iliyopo
The Hague nchini Uholanzi.
Lowassa alisema alikuwa akiiamini polisi, lakini alichokiona jana cha kupigwa mabomu ni jambo baya.
Kuhusu
suala la Babu Seya aliyefungwa kifungo cha maisha gerezani alisema
atafuatiliwa kwa kutumia suala la utawala bora kwa kuangalia vyombo vya
sheria na hatua zingine zitafuatwa.
Mwenyekiti wa
Chadema, Freeman Mbowe alisema wanachama wanaojiunga sasa wana haki sawa
na mwasisi wa chama hiki Edwin Mtei mwenye kadi namba moja.
Alisema
mara baada ya wanachama wapya kujiunga, kwa kipindi cha wiki moja
nilipokea matusi mengi kuliko niliyowahi kutukanwa baada ya kupokea
wanachama wapya.
Kaimu Mwenyekiti wa CUF, Taslima
alisema kuna watu ambao wamejenga desturi ya kuwabeza watu wanapohama
vyama kwa hiari kwa kuwaita oili chafu au makapi anavunja Katiba.
Alisema
Ibara ya 20 ya Katiba ya mwaka 1977 inasema kila mtu yeyote ambaye ni
Mtanzania, yuko huru kujiunga na mtu yeyote, chombo chochote, taasisi
yoyote atakayopenda na hatazuiliwa.
Mwenyekiti wa
NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema; “Mabomu yamepigwa katika mkutano wa
Chadema, watu wakafa Arusha, Arusha tunayoitegemea kwa uchumi leo hii
zaidi ya asilimia 19 ya pato ya taifa linatokana na utalii, lakini leo
(jana) tunaingia Arusha alipozaliwa Lowassa tunapigwa mabomu, ukweli
utatuweka huru.