CUF yatangaza kuigomea polisi

Naibu Katibu Mkuu wa  CUF,Madgalena Sakaya.
Dar es Salaam. Chama cha Wananchi (CUF) kimesema uamuzi wa Jeshi la Polisi kuzuia misafara ya wagombea urais wakati wa kuchukua na kurejesha fomu batili, kinyume na Katiba ya nchi na sheria ya vyama vya siasa, na unalenga “kuionea huruma CCM” baada ya kufunikwa na vyama vinavyounda Ukawa.
Polisi imepiga marufuku misafara hiyo kwa maelezo kuwa imesababisha usumbufu kwa wakazi na kusimamisha shughuli nyingine za kila siku.
Naibu Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, Abdulrahman Kaniki alitangaza uamuzi huo juzi baada ya watu wengi kujitokeza kumsindikiza mgombea urais wa CCM, Dk John Pombe Magufuli na baadaye wengi zaidi kujitokeza wakati mgombea wa Chadema, Edward Lowassa alipokuwa akienda kuchukua fomu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Jana naibu katibu mkuu wa CUF, Magdalena Sakaya alisema chama hicho kitaendelea kufanya maandamano na mikutano ya hadhara kama kawaida.
Alidai kauli ya polisi ni agizo la CCM baada ya kuona Watanzania wanajitokeza kwa wingi kwenye shughuli za kisiasa zinazofanywa na kwa pamoja na vyama vinavyounda Ukawa ambavyo ni Chadema, NCCR-Mageuzi, NLD na CUF.
“Tumesikitishwa na kauli ya polisi. Nadhani wanacheza na amani na utulivu wa nchi yetu. Maandamano ni haki ya kikatiba ya kila Mtanzania na imeelezwa katika ibara ya 18(a) na 20 ya Katiba ya Jamhuri ya muungano,” alisema Sakaya.
Alisema hata sheria ya vyama vya siasa, ibara ya 11 imefafanua kuhusu maandamano na kusisitiza kuwa kampeni haziwezi kufanywa kimyakimya.
“Huwezi kuzuia maandamano na mikusanyiko katika shughuli za kisiasa,” alisema.
“Kwa sasa vyama vya upinzani vina wapenzi, mashabiki na wanachama wengi. Hizi ni njama za CCM kuzuia maandamano maana… katika mikutano yao watu ni wachache mno. Sisi (Ukawa) mikutano na maandamano yetu ina utulivu mkubwa. Polisi wasiwe na wasiwasi,” alisema. Alisema Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 watu walipoteza maisha kutokana na kauli kama hizo za kuzuia maandamano na mikusanyiko.
“Hii ni ishara kuwa polisi watatumia nguvu nyingi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. Wanataka kulazimisha bao la mkono. Wanatakiwa kulinda usalama wa wananchi katika mikutano na si kuizuia. Wasome katiba na sheria kwanza, si kuzuia tu kila jambo,” alisema.
Alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu msimamo wa CUF, kaimu mkuu huyo wa polisi alitaka atafutwe msemaji wa jeshi hilo, Advera Bulimba ambaye alisisitiza kuwa amri hiyo inalenga kuimarisha usalama wa nchi na wananchi.
“Mambo yaliyojitokeza katika maandamano si sawa maana mwananchi walishindwa kufika katika shughuli zao. Tunaangalia usalama wa nchi kwanza. Tutafanya mkutano na kuwashirikisha wanasiasa ili kutafuta namna bora ya kufanya mambo yao bila kuathiri shughuli nyingine,” alisema.
“Hatutangazi ugomvi wala malumbano na vyama, tunataka siasa kufanyika wakati huohuo watu wengine wasiathirike. Amani ya nchi haitaki ushabiki na inamhusu kila mmoja wetu.”
Wakati polisi inazungumzia maandamano kuwa yalisumbua wananchi wengine, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, walipongeza msafara wa Lowassa kwenda kuchukua fomu NEC, wakisema kama wataendelea hivyo, Uchaguzi Mkuu utafanyika kwa amani.
-
Powered by Blogger.