Simba kuanika silaha zake leo

Dar es Salaam. Kocha wa Simba, Dylan Kerr ataitumia siku ya klabu hiyo kuonyesha wapinzani wake matokeo ya mazoezi ya Lushoto na Zanzibar, ingawa kikubwa zaidi ni kuonyesha wachezaji ambao klabu hiyo itawatumia msimu ujao.
Hata hivyo, hiyo itakuwa nafasi ya wapinzani wake, hasa Yanga na Azam kuisoma timu hiyo pamoja na usajili wake itakaposhuka uwanjani kuikabili SC Villa ya Uganda kwenye mchezo wa kimataifa wa Kirafiki.
Timu hiyo imetumia takribani wiki tatu kujiandaa na leo itatambulisha silaha zake mpya mbele ya mashabiki kama sehemu ya maadhimisho ya wiki ya klabu hiyo.
Tayari, timu hiyo imefanya marekebisho makubwa kwenye kipindi hiki cha usajili, ikiwa imebadili benchi la ufundi kwa kumleta nchini kocha Kerr kutoka Uingereza, mtaalamu wa viungo, Dusan Momcilovic, sanjari na kocha wa makipa, Abdul Salim kutoka Kenya.
Wachezaji wapya wa timu hiyo ambao leo watakanyaga nyasi za Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakiwa na uzi mwekundu kwa mara ya kwanza ni, Mussa Hassan ‘Mgosi’, Vincent Angban, Danny Lyanga, Emery Nibomana, Hamis Kiiza, Peter Mwalyanzi, Mohamed Fakhi, Nuhu Haji, Mwinyi Kazimoto na Justice Majabvi.
Pambano la leo linatarajia kukata kiu za mashabiki wa Simba kuiona timu yao iliyoweka rekodi ya kutopoteza mchezo wa kirafiki ilipokuwa Zanzibar kwa kambi ya wiki moja. Ikiwa visiwani, Simba ilicheza na Kombaini ya Zanzibar, Kikosi Maalum cha Kupambana na Magendo (KMKM) na Jang’ombe Boys, ikiibuka na ushindi kwenye mechi hizo zote.
SC Villa au Jogoo imekuja nchini kwa mara ya pili ndani ya kipindi cha miezi miwili kucheza mechi ya kirafiki baaa ya awali kufanya hivyo mwanzoni mwa mwezi uliopita ilipocheza na Yanga na kutoka sare ya 0-0. Timu hiyo iliyoshika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu nchini Uganda msimu uliopita, imechukua nafasi ya AFC Leopards ya Kenya ambayo awali ndiyo iliyotajwa kuwa ingekuja nchini kwa ajili ya kuipima Simba.
Mechi hiyo itampa nafasi kocha Kerr kujua kikosi chake cha kwanza baada ya mazoezi ya muda mrefu wilayani Lushoto, Tanga pamoja na visiwani Zanzibar.
Pia, Kerr atatumia mchezo huo kutoa hatima ya wachezaji walio kwenye majaribio ya kujiunga na klabu hiyo kwani bado kikosi hicho hakijakamilika kama ambavyo kocha huyo alivyolithibitishia gazeti hili.
“Nahitaji kikosi cha wachezaji 22, bado sijakipata, bado tunahitaji kukamilisha usajili wetu,” alisema.
Aliongeza, “Sitaki kuwa na wachezaji 11 wazuri na wengine wabaki kuwa wa kawaida, nataka kuwa na timu mbili zinazoweza kunipa matokeo mazuri,” alisema.
Chanzo;Mwananchi
Powered by Blogger.