Yanga bwana, we acha tu

Beki Mpya wa Yanga, Vincent Bossou akiwasili kwenye uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam jana akitokea Togo
Dar es Salaam.Wakati Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likisogeza mbele dirisha la usajili, beki mpya wa Yanga, Vincent Bossou, raia wa Togo ametangaza hali ya hatari kwa washambuliaji wa timu pinzani.
Akizungumza baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dra es Salaam jana, Bossou alisema hakuja nchini kujifunza soka, bali kufanya kazi ambayo kila mmoja ndani ya klabu hiyo ataifurahia.
Beki huyo na kiungo Mzimbabwe, Thabani Kamusoko wamefuzu vipimo vya afya na leo wanatarajia kusaini mikataba ya kuichezea klabu hiyo.
Bossou alisema ingawa anakuja kwenye mazingira mapya, hilo halimpi shida kwani mchezaji ni kama askari anayetakiwa kuwa tayari muda wowote na wakati wowote kuishi katika kila aina ya mazingira anayokutana nayo.
Alisema kuwa hakuna sehemu ambako kunakosekana washambuliaji wasumbufu na yeye amejiandaa kikamilifu kukabiliana nao na ndio utakuwa mwisho wa washambuliaji nchini kutamba wakikutana na Yanga.
“Mimi siyo mtu wa maneno mengi, bali nimekuja hapa kufanya kazi ya kupambana na hao (washambuliaji) ambao nimeambiwa kuwa wanasumbua.
“Nawapa angalizo kuwa mimi siyo mtu mzuri kwao na pia ni katili uwanjani, hasa kwa washambuliaji wa aina hiyo ambao ni wasumbufu,” alisema.
Aliongeza kuwa atatumia muda mfupi kuelewana na mabeki wenzake ndani ya timu hiyo (Yanga) na anataka kuhakikisha inatwaa mataji kwa kila mashindano ambayo itakuwa inashiriki.
Wakati huohuo; TFF imesogeza mbele dirisha la usajili wa wachezaji kwa Ligi Kuu Bara, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili hadi Agosti 20, bila kuweka wazi sababu ya kufanya hivyo.
Awali, dirisha la usajili lilitarajiwa kufungwa jana saa 6.00 usiku, lakini ghafla TFF iliongeza siku na sasa litafungwa Agosti 20 na kati ya Agosti 21- 28, kitakuwa kipindi cha pingamizi. Kati ya Agosti 29-30, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji itapitia na kupitisha usajili wakati uhamisho wa wachezaji wa Kimataifa (Fifa –TMS) utafungwa Septemba 6.
Kusogezwa mbele kwa dirisha hilo huenda kutainufaisha Yanga iliyokuwa jana ikikamilisha usajili wao wa wachezaji kutoka nje ya nchi ili kukiongezea nguvu kikosi chake kwa msimu ujao wa ligi.
Yanga imeachana na mshambuliaji Kpah Sherman aliyeuzwa Afrika Kusini, kiungo Andrey Coutinho na beki Joseph Zuttah walioachwa na tayari imewaleta kundini wachezaji wawili, beki wa kati na kiungo mkabaji ili kuziba nafasi hizo, huku nafasi moja ikidaiwa inaweza kujazwa na mshambuliaji Laudit Mavugo kutoka Burundi.
Kumekuwa na habari kuwa Yanga imeanza mazungumzo na Mavugo ambaye awali alitakiwa na Simba, lakini wameshindana kutokana na dau la Sh200 milioni na hivyo uongozi wa klabu hiyo ya Mitaa ya Twiga na Jangwani umeamua kumvalia njuga ili kuhakikisha anaungana na Amissi Tambwe, pia kutoka Burundi kuvaa jezi za njano na kijani msimu ujao.
Habari ambazo gazeti hili imepata zinaeleza kuwa, tayari Yanga imetega rada zake kwa Mavugo, anayesemekana kuwa ni mshambuliaji tishio na kama ikifanikiwa kumpata, basi Yanga itakuwa imelamba dume na kuwa na safu hatari ya ushambuliaji ikiwa nao, Donald Ngoma, Tambwe, Simon Msuva na Malimi Busungu.
-POSTED FRIDAY, AUGUST 7, 2015 | BY- CHARLES ABEL NA OLIVER ALBERT


Powered by Blogger.