Agizo la JK Buguruni ‘kizungumkuti’

Rais Jakaya Kikwete akitazama kazi ya utoaji maji ya mafuriko ya mvua eneo la Buguruni kwa Mnyamani Dar es Salaam Machi 24, mwaka huu.  Picha na Maktaba.
Dar es Salaam. Zikiwa zimefikia siku 130 tangu Rais Jakaya Kikwete alipotembelea waathirika wa mafuriko eneo la Buguruni kwa Mnyamani ambako aliagiza kuvunjwa kwa nyumba zilizojengwa juu ya karavati lililoziba na kusababisha maji kujaa kwenye nyumba za wakazi wa maeneo hayo, agizo hilo bado halijatekelezwa ipasavyo.
Zaidi ya wakazi 1,163 wa eneo la Buguruni kwa Mnyamani walikosa mahali pa kuishi baada ya nyumba zao 517 kuzingirwa na mafuriko ya maji ya mvua.
Rais Kikwete alitembelea eneo hilo Machi 24, mwaka huu na kuagiza nyumba hizo zibomolewe pamoja na karavati lililopo eneo hilo lijengwe ili kuruhusu maji mengi zaidi kupita huku akiagiza mamlaka husika kuwalipa fidia wakazi wa eneo hilo. Alisema Serikali itazungumza na wahandisi ili kuhakikisha karavati hilo linajengwa katika viwango ambavyo havitasababisha tatizo jingine kama hilo na aliwatahadharisha wakazi wa eneo hilo kuepuka kuharibu miundombinu na kusababisisha kutokea kwa matatizo mengine zaidi.
Serikali imetekeleza azma yake na imewalipa fidia wakazi wa eneo hilo ambao walijenga juu ya karavati hilo na wameshahama ili kupisha ujenzi wa karavati hilo.
Hata hivyo, hali imekuwa ni tofauti licha ya Rais Kikwete kuagiza ujenzi wa karavati hilo uharakishwe lakini ujenzi huo umekuwa ukisuasua na kusababisha hofu kwa wakazi wa eneo hilo kama mvua kubwa itanyesha kwa mara nyingine.
Mwandishi wa gazeti hili alifika eneo hilo ili kumtafuta mkandarasi wa Kampuni ya Luseko Enterprises anayejenga karavati hilo, lakini hakupatikana.
Jitihada zilifanyika na kupatikana kwa msimamizi mkuu wa ujenzi huo aliyetambulika kwa jina moja la Victor.
Hata hivyo, alipopigiwa simu na kuulizwa kama yeye ni Victor, alijibu: “Yes, ndiyo mimi Victor.” Baada ya hapo Mwandishi alipohitaji maelezo ya ziada kuhusu ujenzi huo, alibadili kauli yake na kusema: “Hilo siyo jina langu nafikiri umekosea namba.”
Wakazi walonga
Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Isaya Abraham anasimulia kuwa mkandarasi huyo amechimba mfereji eneo la barabara na kuacha upande mwingine hali inayotishia iwapo mvua itaanza kunyesha maji yatatuama kwa wingi katika eneo hilo na kusababisha madhara kwa watu na mali zao.
“Hatumuelewi huyu mkandarasi, tangu apewe hii tenda ya kujenga karavati imepita miezi mitatu na mvua inakaribia kunyesha tatizo litakuwapo palepale maji yatasimama kwenye mfereji huu na kusababisha barabara kubomoka matokeo yake mafuriko yanatokea.
“Tulikuwa tunaona vijiko vilivyokuwa hapa eneo linalojengwa karavati lakini sasa vimeshatolewa na hakuna kazi yoyote inayoendelea,” alisema Abraham.
Mkazi mwingine, Hilda Massawe alisema Serikali itafute mkandarasi mwingine aliyepo anafanya kazi anapojisikia yeye na anaweza akaonekana kwa wiki mara moja.
Alipotafutwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Buguruni kwa Mnyamani, Abdallah Mng’ae alisema tatizo lipo kwa mkandarasi anayefanya kazi hiyo pale anapojisikia.
Mng’ae alisema mkandarasi huyo ameanza kumwaga zege upande mmoja na anachofanya sasa ni kubomoa kidogo kidogo na kuziba maji ili yasichanganyike na simenti inayojengewa kwenye karavati hilo.
“Wakazi waliojenga juu ya karavati hilo wameshalipwa fidia na wameshahama hivyo ujenzi unaendelea lakini huyu mkandarasi anajenga taratibu sana, inatutia shaka mvua zitakapoanza kunyesha kuna uwezekano wa kukumbwa na mafuriko tena,” alisema Mng’ae.
-
Powered by Blogger.