NYANZA: Mwenyekiti wa Bawacha adaiwa kutekwa na kujeruhiwa
Geita. Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la
Chadema (Bawacha) mkoani Geita, Husna Amri (34) ameokotwa na wafyatua
matofali wa Mtaa wa Pakacha Wilaya ya Kondoa, Mkoa wa Dodoma, akiwa
amepigwa na kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake.
Amri
ambaye inadaiwa kuwa alitekwa na watu wanne wasiofahamika Agosti 16,
akiwa njiani akitokea wilayani Nyang’hwale Mkoa wa Geita kwenye mkutano
wa uchaguzi wa madiwani wa viti maalumu akielekea mjini Kakola kupanda
gari kurejea nyumbani kwake Buseresere wilayani Chato.
Baada ya kuvamiwa na watu hao, walimpeleka kusikojulikana. Hali hiyo ilizua hofu kwa wanachama wenzake, ndugu na jamaa.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo alisema taarifa za kutekwa kwa
mwenyekiti huyo walizipata kutoka kwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa
Geita, Alphonce Mawazo baada ya kupigiwa simu na mwenyekiti huyo usiku
wa kuamkia Jumatatu akilalamika kuwa ametekwa anahitaji msaada.
“Tuliamua
kufuatilia baada ya kupokea taarifa hizo hadi jana (juzi) saa 2:00
usiku, tulipata taarifa kutoka Kituo cha Polisi Kondoa kuwa kuna
mwanamke ameokotwa akiwa anakimbizwa na watu wanaodaiwa ndiyo
waliomteka,” alisema Konyo.
Kamanda Konyo alisema polisi walipomuuliza Amri ili
awapatie taarifa sahihi, alidai kuwa wakati anatoka Nyang’hwale
alivamiwa na watu wanne wakiwa kwenye pikipiki ambao walimchukua hadi
Kakola wilayani Kahama na kumpeleka mahala kusikojulikana.
“Wakati
anajaribu kujiokoa watu hao walishtuka na kuanza kumkimbiza, lakini
wakati wanakaribia kumkamata alikuwa tayari amefika eneo ambalo kuna
watu hivyo alipiga kelele kuomba msaada, watekaji walipoona watu
walikimbia na kuacha mfuko ukiwa na panga jipya na sindano mbili za
kushonea nguo.”
Alisema tayari watu wawili
wanashikiliwa akiwamo mwendesha pikipiki aliyembeba mwenyekiti huyo
kutoka Nyang’hwale na mwanachama mwenzake, ambaye anaelezwa alipanda
naye kwenye pikipiki moja na alishuka njiani.
Awali,
Diwani wa Kata ya Buseresere, Chrispian Kagoma (Chadema) akielezea mkasa
huo alidai kuwa kabla hajatekwa akiwa Nyang’hwale, wanachama wenzanke
walimtaka alale lakini alikataa kwa madai kulikuwa na watu wanamtafuta
ambao ni wafuasi wa chama kimoja cha siasa kwa sababu aliwahi
kukorofishana nao kwenye mambo ya siasa, hivyo alihofia usalama wake.
Mwenyekiti
wa Chadema Mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo alikiri kutekwa kwa Amri na
kwamba, hali hiyo inawapa hofu wapinzani, kwani hilo siyo tukio la
kwanza kuna mwenyekiti wa Chadema Kata ya Kalangalala alitekwa na watu
wasiojulikana Aprili na hadi sasa hajapatikana.