JK, Magufuli warusha kijembe ‘kwa Ukawa’
Rais Jakaya Kikwete akijaribu Trekta alilozawadi na Wadau wa Sekta ya Ujenzi wakati wa sherehe za kumuaga iliyofanyika Dar es Salaam jana.Picha na Said Khamis
Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amesema
anaamini mgombea wa urais kupitia CCM, Dk John Magufuli ndiye
atakayeshinda katika Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu, na kwamba vuguvuru
la kisiasa linaloendelea hivi sasa ni moto wa mabua.
Rais
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM alikuwa akihutubia watendaji wa
Wizara ya Ujenzi na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo katika hafla ya
kumuaga, iliyofanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es
Salaam.
Kauli ya Rais Kikwete inaweza
kutafsiriwa kuwa ni vijembe kwa vyama pinzani, hasa vinavyounda Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa), vinavyoendelea na pilikapilika zake tangu
kumpokea Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa aliyehamia Chadema kutoka
CCM na kuteuliwa kuwania urais, huku nao wakitupia vijembe CCM.
“Sishangai
chama chako kimekuteua kuwa mgombea wa urais wa chama hicho ambacho
ndiyo chama changu na mimi ndiyo mwenyekiti wake, nina imani Mwenyezi
Mungu akijalia, kazi iliyobakia tutaikamilisha kwa salama. Huo mwingine
ni moto wa mabua tu, hauwaki ukadumu,” alisema Rais Kikwete na
kushangiliwa na wahandisi hao.
Jina la Lowassa
lilikatwa pamoja na wagombea wengine 38 wa CCM walioomba kuteuliwa
kuwania urais kupitia chama hicho katika vikao vyake vya Halmashauri Kuu
ya Taifa na Kamati Kuu, vilivyoketi makao makuu yake mjini Dodoma.
“Huwezi
kulazimisha, hata ukilazimisha hayawi,” alisema Rais Kikwete na kuamsha
shangwe nyingine uwanjani hapo huku akiwaambia: “Mtampata mwenzenu,
inshallah;… ombi langu mpeni ushirikiano rais ajaye, kwani kutokana na
kazi yenu nchi imefikia mahali pa kuanza ‘ku-take off.”
Kikwete
aliyewasili uwanjani hapo saa 5:02 asubuhi na kuanza kupokea taarifa za
utekelezaji za atendaji wakuu wa taasisi saba zilizo chini ya Wizara ya
Ujenzi katika miaka 10 inayomalizika, kabla ya Dk Magufuli kumkaribisha
kutokana na utendaji wake, taifa likimpata Dk Magufuli litanufaika
kwani ni kiongozi mzuri.
Rais Kikwete aliyetumia
takriban dakika 47 kutoa hotuba ya kuwaaga wafanyakazi wa wizara hiyo,
alimsifu na kumshukuru Dk Magufuli akimwelezea kuwa ni msikivu
aliyefanya kazi nzuri, iliyomfanya alale usingizi usio na mawaa.
Vile
vile, Rais alitumia muda huo kuwaeleza wananchi kuwa mara atakapotoka
madarakani atakwenda kuishi kijijini kwake Msoga, wilayani Bagamoyo
katika Mkoa wa Pwani na kwamba asingependa watu wamfuate fuate huko.
Alisema
akirejea kijijini kwake atafuga ng’ombe na kulima mananasi kwa kuwa ana
eneo la ekari 1000 lililopo katika jijini cha Kibindu alilopewa wakati
akiwa mbunge wa Chalinze na kwamba akikaa kijiji atakuwa na utulivu wa
kutosha hivyo wasimfuatefuate.
Tangu Lowassa aenguliwe
katika kinyang’anyiro cha kuingia Ikulu kwa tiketi ya CCM na baadaye
kujiunga na Chadema, kumekuwapo na vuguvugu la wanachama wengi wa CCM
kukihama chama hicho na kumfuata.
Akiwahutubia mamia ya
wafuasi wa Ukawa muda mfupi baada ya kuchukua fomu ya kugombea urais
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), makao makuu ya Chadema, Lowassa alisema
rafike yake Kikwete ndiye aliyeharibu uchumi, lakini akasema asingetaka
kutoa mashtaka bila kutoa takwimu.
“Wakati Rais
Benjamini Mkapa anaondoka madarakani, bei ya sukari ilikuwa Sh650, leo
ni Sh2, 300, kutoka 650 hadi 2,300 ameharibu uchumi, hajaharibu?”
aliuliza na kujibiwa, “ameharibuuu.”
Magufuli
Akimkaribisha
Rais Kikwete, Dk Magufuli katika hotuba yake iliyochukua dakika 12 na
sekunde 26, alisema kuwa anashanga kwa nini wataalamu hao wa ujenzi
hawajamwandalia sherehe ya kumwaga kama walivyofanya kwa Rais, lakini
akasema anaamini wana matumaini fulani, hivyo watakuwa wanajiandaa
kumfanyia sherehe ya kumpokea mara baada ya kuingia Ikulu mwishoni mwa
mwaka huu akiwaomba wasimsahau katika ‘ufalme wao’.
“Kama ndiyo hivyo basi Mungu awabariki, tuliombee taifa tupite salama katika uchaguzi” alisema Dk Magufuli.
Dk
Magufuli naye alimtupia kijembe mmoja wa wagombea urais kupitia vyama
vya upinzani aliyesema kuwa akiingia Ikulu anawasaidia waendesha
bodaboda akisema mtu huyo kasahau kujiuliza vyombo hivyo vya usafiri
vililetwa na nani.