Diwani Kata ya Ubungo kizimbani kwa kujeruhi
Kushoto
ni Diwani wa kata ya Ubungo anayemaliza muda wake, Boniface Jacob
akisindikizwa na Afisa usalama wa jeshi la polisi. Picha na Omary
Fungo.
-
Dar es Salaam. Diwani wa kata ya Ubungo
anayemaliza muda wake, Boniface Jacob leo amepandishwa kizimbani katika
Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam akituhumiwa kumpiga na kumjeruhi
mwandishi wa habari wa gazeti la Uhuru, Christopher Lisso.
Mbele
ya hakimu Hellen Liwa, wakili wa serikali Kenneth Setwao alisema
Septemba 11, 2015 katika Wilaya ya Kinondoni mtuhumiwa alitenda makosa
mawili.
Katika kosa la kwanza Setwao alisema mtuhumiwa
alimpiga mwandishi wa habari wa gazeti la Uhuru, Christopher Lisso na
kumsababishia maumivu sehemu mbalimbali za mwili wake.
Alisema
katika shitaka la pili mtuhumiwa anatuhumiwa kuharibu kamera yenye
thamani ya Sh8 milioni, mali ya kampuni ya Uhuru Publications Limited.
Mtuhumiwa
anayetetewa na wakili wa kujitegemea, John Mallya amekana mashtaka yote
mawili na yuko nje kwa dhamana baada ya kutimiza matakwa yaliyowekwa ya
kuwa na mdhamini mmoja aliyesaini bondi yenye thamani ya Sh8 milioni.