Ukawa wavutana mgombea ubunge Nzega Vijijini
Mgombea Mwenza wa Ukawa kupitia Chadema, Juma Haji Duni akihutubia wananchi .
-
Tabora. Ziara ya Mgombea mwenza urais kwa
tiketi ya Chadema kupitia Ukawa, Juma Duni Haji imeingia dosari baada ya
viongozi na wafuasi wa vyama hivyo ndani ya jimbo la Nzenga Vijijini
kutoridhiana mgombea atakayewakilisha jimbo hilo.
Hivi
karibuni, Ukawa ilipitisha jina la Khamis Katuga(CUF), kuwakilisha jimbo
hilo kwa umoja wa Ukawa lakini mgombea wa Chadema, Joseph Malongo
alikataa uamuzi huo.
Kabla ya kutambulishwa Katuga
mbele ya wafuasi hao, Duni alimwomba apande jukwaani na ndipo kundi la
wafuasi wengi lilianza kupinga utambulisho huo.
Duni aliwataka wafuasi hao wampokee na kumpigia kura ili Kumshinda mgombea kutoka CCM,Dk Khamis Kigwangalla.
Kila
alipojaribu kuwaomba utulivu vijana wengi walikataa na hata
alipowasalimia kwa lugha ya vyama hivyo walipiga kelele za kumtaka
mgombea wa Chadema.
"Naomba mumchague huyu ndiye
aliyepitishwa na vikao vya Ukawa, tunatakiwa umoja wetu na lengo ni
maslahi ya kuiondoa CCM madarakani,"alisema Duni.
Licha ya kutumia muda mwingi kufafanua uamuzi huo, bado haikusaidia hatua iliyomkwaza Duni na kushuka juu ya jukwaa hilo.
Tukio hilo limetokea jana majira ya saa 9:30 jioni katika Uwanja wa taifa,uliopo Kata ya Ndalla, Nzenga vijijini.
Baada ya kushuka Duni, mgombea huyo wa Chadema alipanda jukwaani huku akishangiliwa na wafuasi wengi uwanjani hapo.
Baadhi yao walisema wako tayari Ukawa ivunjike katika jimbo hilo lakini hawatakubali kuunga mkono mgombea wa Cuf.
"Uamuzi
uliopitishwa na viongozi hatuwezi kukubaliana nao, haujatenda haki,
sisi tunamtaka Malongo basi, Ukawa wamchukue mgombea wao
waliyetuletea,"alisema Bernard Samwel ambaye ni mkazi wa jimbo hilo.