UTANZU WA HADITHI FUPI

Cover Image

1. UTANZU WA HADITHI FUPI

Sura ya Kwanza
TUKIO linaweza kuelezwa katika tanzu mbalimbali za kifasihi. Aidha, kila utanzu wa kifasihi una kanuni ama misingi ya usanii inayozingatiwa. Kama zilivyo tanzu nyingine za kifasihi, hadithi nazo zina mismgi yake inayozingatiwa katika kuzisanii. Katika utanzu wa hadithi, tuna makundi mbalimbali yanayoweza kuainishwa, lakini kwa ujumla tunaweza kusema kuwa kuna hadithi ndefu na fupi. Lengo letu katika kitabu hiki ni kuupambanua utanzu muhimu wa kifasihi wa hadithi fupi.
Katika kuupambanua utanzu wa hadithi fupi, tutazingatia mambo matatu: Kwanza tutaeleza maana ya hadithi kwa ufupi na kwa ujumla kama inavyofahamika kifasihi. Pili, tutaipambanua hadithi ndefu kwa kifupi. Na mwisho tutajadili utanzu wa hadithi fupi katika fasihi ya Kiswahili kwa undani kwa kuangalia nadharia mbalimbali zilizokwisha tolewa na wataalamu mbalimbali wa fasihi.
Kabla ya kuhitimisha mjadala wetu, tutaangalia tofauti zilizoko kati ya tanzu hizo za hadithi. Hatimaye, tutamaliza mjadala wetu kwa kuangalia yale yaliyokwisha jadiliwa katika vipengele vile vitatu vilivyotajwa hapo awali.
Maana ya Hadithi
Hadithi m kazi ya sanaa inayotumia lugha. Kwa hiyo, hadithi, yaweza kuwa masimulizi ya kubuni ama ya kweli yaliyo katika nathari. Sanaa hiyo ya hadithi ni kazi ya mtu yenye mwigo wa uyakinifu uliofungamana na wakati, mazingira na mfumo wa jamii. Kwa sababu hii, utanzu huu unaweza kupatikana katika fasihi zote zilizopo katika jamii: fasihi simulizi na fasihi andishi.
Katika ujenzi wa hadithi, binadamu hutumia akili kuiga maisha kisanaa. Mwigo katika hadithi hizo buzingatia kanuni na taratibu za uzuri, upendezaji, uozo na ubaya, na kwa hiyo huathiri hadhira katika kuvuta ama kuchukiza nulango ya fahamu ya mwanadamu. Kama kazi ya sanaa, fasihi husawiri maisha ya jamii inayohusika. Kwa sababu ya kusawiri huko, hadithi inalazimika kueleza tukio, mahali na wakati ambapo tukio hilo hutendeka, watenzi wa tukio (wahusika) na hatimaye mbinu za kulieleza tukio hilo, n.k. Masimulizi yanayokuwa katika hadithi yanaweza kumhusu mtu mmoja ama yanaweza kuwahusu watu wengi. Masimulizi hayo yanahusu juu ya mambo yaliyotokea, au mambo yanayoweza kutokea katika jamii.
Uwezo wa kiakili anaokuwa nao binadamu, ni ule wa kuiga maisha, ambao kimsingi mtu anazaliwa nao. Tofauti yake na wanyama ambao nao kwa kiasi fulani wana uwezo wa kuiga maisha ni kuwa bmadamu uwezo anao mkubwa zaidi wa kuiga kuliko viumbe wengine. Kutokana na mambo ya awali ya kielimu, hasa lugha; ambayo hatimaye huitumia katika shughuli mbalimbali za maisha yake, ikiwa ni pamoja na uandishi; mwanadamu huwa juu ya viumbe wengine hai.
Hadithi hutofautiana kutokana na uwezo wa msanii na lengo ama mazingira ambayo hadithi hiyo Husimulia au kuandikwa. Katika msingi huo, uwezo wa fanani ama mwandishi ni nyenzo muhimu sana katika ujenzi wa fani na maudhui ya hadithi. Hadithi hizo huzingatia kanuni ama taratibu maalumu za kisanaa. Hali hiyo huifanya hadithi iwe tofauti na kazi nyingine za kisanaa ama zisizo za kisanaa zinazotumia lugha.
Hadithi kama kazi ya kisanaa hutumia lugha yenye semi, tamathali za usemi, nahau na kadhalika, ili kuwasilisha matendo na mawazo ya wahusika. Tamathali na semi husaidia kuitofautisha hadithi kama kazi ya sanaa na kazi nyingine zitumiazo lugha ambazo si za kisanaa na zimeandikwa kwa ujazo. Tamathali hufanya hadithi isiwe mazungumzo ya kawaida, bali huifanya kazi ya sanaa inayosawiri maisha na inayozingatia kanuni na taratibu maalum kama tulivyodokeza awali.
Kwa upande mwingine, hadithi huweza kupambanuliwa na kazi nyingine za sanaa zitumiazo lugha kama vile ushairi na tamthiliya. Utanzu wa ushairi kwa mfano, una umbo tofauti na umbo la hadithi. Utanzu wa tamthiliya pia unatofautiana na hadithi kwa misingi kuwa tamthiliya katika uandishi wake huzingatia sana kipengele cha utendaji jukwaani, lakini hadithi lengo lake mara nyingi huwa ni kusomwa tu. Tena, wakati shairi haliwezi kuingiza kitu katika muundo wa usimulizi wake, hadithi na tamthiliya zinaweza kuingiza mashairi na nyimbo katika kuimarisha fani na maudhui yake. Vipengele hivyo ndivyo hufanya hadithi iwe tofauti na tanzu nyingine k'ama vile ushairi na tamthiliya kwa misingi kuwa inao uwezo wa kutumia tanzu nyingine zote za kifasihi.
Ufafanuzi huu ni wa jumla, lakini unatuelewesha waziwazi hadithi ina umbo gani. Sasa hatua itakayofuata ni kufafanua matawi mbalimbali ya hadithi ili tuweze kujua nafasi ya hadithi fupi.
Hadithi Ndefu na Fupi
Katika fasihi simulizi ziko hadithi ndefu zinazosimuliwa na kufahamika sana. Lakini pia kuna hadithi ndefu katika fasihi andishi zenye kuwa na athari nyingi za dhamira zilizokuwa zikijitokeza katika fasihi simulizi.1 Hadithi nyingi ndefu za simulizi mara nyingi zilikuwa katika umbo la tenzi kama vile tenzi za Nanga.2 Hadithi hizo ndefu katika baadhi yajamii, zilikuwa zikisimuliwa toka asubuhi hadi jioni, na zilikuwa zikihifadhiwa kichwani tu. Makabila kama ya Wahehe yanasemekana yalikuwa na aina hizi za hadithi zilizoweza kusimuliwa kwa muda mrefu.3 Kwa sasa usimulizi wa aina hii hauwezekani tena kutokana na mambo mengi yaliyokumbwa na mfumo wa kijamii na wa kihistoria.
Kwa upande wa hadithi ndefu katika fasihi andishi, hizi zinajipambanua zaidi. Utanzu huu ambao huwa katika maandishi tu ulianza kustawi wakati wa mageuzi ya viwanda na utamaduni huko Ulaya. Utanzu huu ulizuka baadaye sana ukilinganisha na tanzu nyingine za kifasihi, kama vile ushairi na nyimbo. F.E.M.K. Senkoro anasema utanzu huu ulizuka katika wakati maalumu wa historia ya jamii. Wakati huo, "jamii ilikwisha kuwa kubwa yenye makao maalumu, na lugha ya jamii hiyo ilikwishapevuka kiasi cha kuweza kueleza dhana, imani na amali mbalimbali za jamii kwa wasanii wa kinathari: (prose fiction)".4 Ukoloni na uvumbuzi ulileta hali ambazo zilihitaji kuelezwa kwa hadhira pana zaidi ya ile ambayo ilikuwa ikisimuliwa kwa ngano na hadithi kwa ufupi. Hata hivyo, bado ni muhimu kuieleza maana ya riwayajapokuwa m kwa ufupi tu, ili tuweze kutumia maelezo hayo wakati wa kuipambanua hadithi fupi.
E. Mphahlele, akitoa maana ya riwaya kwa ujumla, vilevile anakadiria jumla ya maneno yanayotumiwa katika hadithi kuwa ni mojawapo ya kipimo chake cha riwaya. Anasema, "... kati ya maneno 35000 na 50000 tunapata riwaya fupi. Biwaya ndefu ama riwaya kamili ni ile ya maneno 75000..."Lakmi anakiri pia kuwa si lazima kila mara iwe hivyo. Kwa upande mwingine, ufafanuzi huu kimsingi hauzingatii ukweli uliopo wa riwaya za Kiswahili ambazo nyingi zma maneno chini ya idadi anayoisema Mphahlele.
Kwa mujibu wa Penina Muhando na Ndyanao Balisidya, hadithi ndefu ni "fani (utanzu) yenye umbo maalumu. Umbo hili, pamoja na kujengwa katika vipengele vingi ndani yake, lina usanifu unaoifanya hadithi ... isiwe maongezi tu au maandishi ya kawaida."6 Kauli hii ikichambuliwa inaonyesha kuna mambo mengi yanayoiunda riwaya.
Senkoro anasema kuwa riwaya "ni kisa ambacho ni kirefu vya kutosha, chenye zaidi ya tukio moja ndani yake. Ni kisa mchangamano ambacho huweza kuchambuliwa na kupimwa kwa uzito na undani wake kwa mambo mbalimbali kimaudhui na kifani ... kisa ambacho urefu wake unakiruhusu kitambe na kutambaa vizingiti vingi kama apendavyo mwandishi wake."Ufafanuzi huu kimsingi hautofautiani na ule uliotolewa na Penina Muhando na Ndyanao Balisidya.
Sifa ya uchangamano inaonyesha kuwa ni muhimu katika kuielezea hadithi. Aidha, tatizo linalojitokeza katika dondoo hili la Senkoro linahusu utata unaotokana na matumizi ya maneno "kisa kirefu" na "hadithi ndefu" pamoja. Tatizo kubwa ni kutambua tofauti ya msingi baina ya kisa kirefu na hadithi ndefu. Je, pengine tunazungumzia dhana moja, ambayo imekuwa ikitumia maneno hayo katika nyakati mbalimbali? Na kwa upande mwingine, ikiwa tutakubaliana na ufafanuzi wa Muhando na Balisidya, au Senkoro, tuna hakika kuwa hadithi fupi za Kiswahili zitakuwa na sifa zilizo tofauti, au zilizo kinyume na hizo za riwaya. Japokuwa kauli hii ina ukweli fulani, hapa kuna haja ya kuipambanua zaidi hadithi fupi.
Ngano: Hadithi Fupi za Fasihi Simulizi
Kwanza tutaanza na kuziangalia hadithi fupi katika fasihi simulizi. Katika aina hii ya fasihi, hadithi fupi ambazo hujulikana rasmi kwa istilahi ya "ngano," ni nyingi na zimekuwa zikihifadhiwa kwa kichwa na kutolewa kimasimulizi kutoka kizazi hadi kizazi. Baada ya kugunduliwa kwa maandishi, hadithi hizo zilihifadhiwa kimaandishi, hata katika lugha ya Kiswahili tunayo mifano mingi. Tutazmgatia ngano hizo andishi hasa na kuona uhusiano wake na hadithi fupi za kisasa. Tunapofanya hivi tunaamini kuwa kuna kuchukuliana tabia na kuathiriana ama kufanana kwingi kimaudhui na kifani kati ya ngano na hadithi fupi za kisasa za Kiswahili. Baada ya kusoma sehemu inayohusu ngano na ile inayohusu hadithi fupi, tutaona tofauti kati ya tanzu hizi mbili za hadithi. Hapa tuanze na kuielezea maana ya hadithi fupi ya kimapokeo, yaani, ngano, kama inavyofafanuliwa na wanataaluma na wanafasihi mbalimbali.
Wataalamu wengi, akiwemo J. Berg Esenwein, wamepata kutoa maana ya ngano kwa ujumla. Esenwein anasema kuwa:
...ngano ni masimulizi yaliyorahisishwa (Simple narrative), kwa kawaida masimulizi hayo ni mafupi yasiyo na muundo kama wa hadithi za kawaida. Masimulizi hayo tena hutumia wahusika bapa na hutegemea matakwa ya fanani katika kujenga vitendo mbalimbali kuliko muundo katika kuwajenga wahusika.8

Halafu Esenwein anajaribu kuzigawa ngano katika mafungu kadhaa. Mafungu hayo ni ya ngano-adilishi, ngano-furahishi, na kundi la mwisho linajumuisha aina mbili za ngano zilizotajwa awali. Mgawanyo huu umefanywa kwa kuzingatia dhamira zinazotumiwa na ngano hizo. Kwa mujibu wa Esenwein, mgawanyo huu ni wa jumla mno na ngano hizi zikiangaliwa kwa undani bila kujali mgawanyo huu uliosemwa zitaonekana bado zina muundo rahisi.
Aidha, mwanafasihi na mhakiki Ruth Finnegan9 anazigawanya ngano katika makundi ya jumla mawili kufuatana na wahusika wanaotumika. Kundi la kwanza ni la ngano zitumiazo wahusika-watu na la pili ni la wahusika-wanyama. Finnegan anasema kijumla na kifupi tu kuwa ngano za wahusika-wanyama ni fupi, zinasisimua na zinakejeli. Ngano zinazotumia wahusika-watu nazo ni nyingi na huwa kwa kawaida ni ndefu kidogo kuliko zile za wahusika-wanyama. Hata hivyo, mgawanyo huu pia nao ni wa jumla. Migawanyo midogo midogo ya aina hii si muhimu kwa sasa. Tutazingatia mgawanyo wa msingi ulio mpana.
Ngano hazina mshikamano kama ule wa hadithi fupi za kisasa za Kiswahili katika ujenzi wa vipengele vyake mbalimbali. Ngano huonekana kama kitukio (Episode) wakati mwingine kilichochukuliwa kutoka tukio moja kubwa ili kukidhi haja fulani ya kiadili katika jamii.
Jambo la msingi linalojitokeza hapa ni kuwa ngano ni hadithi za simulizi za mapokeo, si za kubuniwa wala hazichukui mandhari na mazingira ya kiuhalisia. Kauli hii ya kubuni inahitaji ufafanuzi zaidi. Tunaposhikilia suala la kubuni hapa tunasema kuwa katika hadithi za kingano mtunzi ama msanii si lazima ajulikane kwa hadhira, bali la msingi ni yale maadili ambayo kila mwanajamii anayo haki ya kuyaeneza katikajamii na kutoka kizazi hadi kizazi. Japokuwa inawezekana kabisa hadithi hizo za kingano kwanza zilibuniwa, lakini kwa vile hazijabuniwa upya bali zimesimuliwa upya katika mazingira mapya, kwa sasa tunasema kuwa ngano hazibuniwi lakini hadithi fupi za kisasa zinabuniwa na kujikita katika mazingira ya kihalisia. Kwa upande mwingine, japokuwa ngano ni za mapokeo; fanani anao uwezo wa kuingiza vitu vya kubuni ambavyo kwa asili yake havikuwa katika masimulizi ya awali. Na haditbi fupi za kisasa nazo zinaweza kutumia vipengele vingi vya kifasihi-simulizi. Kwa sababu hii, Esenwein anakiri katika ufafanuzi wake wa hadithi fupi kuwa:
... lazima ifahamike kuwa kuna magazeti siku hizi (wakati huo wa 1909) yanayochapisha ngano nzuri sana ambazo zinaweza kuwa na kipengele kimoja, viwili ama vitatu na zaidi ambavyo vinapatikana katika hadithi fupi. Kadiri vipengele hivyo vinavyozidi kuweko katika ngano, ngano huelemea zaidi kwenye hadithi fupi na hivyo huwa vigumu wakati mwingine kuzitenganisha tanzu hizi.10

Suala la muda nalo ni muhimu katika usimulizi wa ngano. Ngano, kwa kiasi kikubwa hutumia muda ambao ni wa wakati uliopita usio na mpaka (Infinite past). Ndiyo maana tunapata hadithi zenye mianzo kama "Hapo zamani za kale..." Kale hii ni ipi? Upi ni mpaka wa ukale na usasa? Au utasikia, "Zamani zile za mababu..." Mababu wepi? Ni zama zipi hizi za mababu, na ni wapi huko? Kwa hakika kuna matatizo makubwa kama tunataka kuuainisha muda wa ngano.
Kwa sababu ya kutumia muda uliopita usio na mpaka, ni vigumu kujua mandhari ya hadithi hizo kwa ufasaha kabisa. Katika hali halisi, tunashindwa kuhusisha historia yajamii na hadithi hizo kikamilifu.
Tukimwacha Esenwein, ufafanuzi mwingine wa maana ya ngano umetolewa na Penina Muhando na Ndyanao Balisidya. Kulingana na ufafanuzi wao, ngano ni aina "maalumu ya hadithi ipatikanayo katika fasihi asilia ya jamii yetu, fasihi ambayo ilitumia zaidi akili na ubongo wa binadamu kwa kuhifadhiwa kwake."11 Halafu wanafasihi hao wanaeleza pia muundo wa ngano na maudhui yake. Wanasisitiza kuwa:
Ngano nyingi aghalabu ni fupi na kutokana na ufupi huo, hizi si hadithi zinazoinglia mambo kwa undani sana. Hadithi hizo huingia moja kwa moja katika kulitoa wazo kuu, na kila kipengele kiijengacho ngano: wahusika, vielelezo na mizungu mingineyo huelemea katika wazo hilo.

Tabia ya ufupi iliyotajwa hapo awali inapatikana katika hadithi fupi za kisasa pia.
Tumeona kuwa baada ya kufika kwa maandishi, baadhi ya hadithi hizo za kingano zimepata kuandikwa. Ngano andishi zinatofautiana na ngano simulizi hasa katika kutoa athari ya maana ama mjengo wa sanaa. Kutokana na kuandikwa, mambo kama vitendo, nyimbo na sauti zake, ming'ong'oso na vidoko n.k., haviwekwi katika ngano kwa sababu si rahisi kufanya hivyo. Katika usimulizi wake, ngano simulizi zinapewa uzito wa kisanaa kwa sauti na matendo. Vitu kama nyimbo na mashairi kadha wa kadha huingizwa pia, vitendawili na methali ama mafumbo mengine, n.k.
Tumekwisha ona kwamba wanyama, mimea, wadudu, miti n.k. ndio wanaokuwa wahusika katika ngano. Kadiri siku zilivyoendelea matumizi ya wahusika binadamu yaliingizwa. Hata hivyo hawa wahusika wa ngano walichanganywa na wahusika wanyama ama miungu, n.k. Wahusika wa ngano, kama wanavyosisitiza Robert Scholes na Robert Kellogg, "ni bapa na mara nyingi hawabadiliki kama vile kukua, kuugua ama kufa katika mkondo mzima wa hadithi. Wakati mwingine wahusika wanakuwa wawakilishi wa makundi mengine ya watu katika jamii."13Wahusika wa namna hii hutumika kama vielelezo na ni wachache mno ukiwalinganisha na wale wa hadithi fupi. Vilevile, wahusika wa ngano mara nyingi hawapewi majina; bali hutokea kama, "Mtu na mkewe ..." au ''Zamani za Mfalme..." au "Paliondokea mtu mmoja..." Mhusika mkuu wa ngano ni muhimu sana. Yeye ndiye anayekuwa kiungo na ndiye anayebeba ujumbe wa hadithi nzima. Wakati mwingine, wahusika wa ngano sio lazima wawe wa kuaminika. Hii ni kwa sababu ngano mara nyingi hazijengwi katika ulimwengu ama mazingira halisi, zinaweza kujengwa katika ulimwengu wa majini, mizimu, miungu, n.k. Tukilinganisha na hadithi fupi katika kipengele hiki, tunaona kuwa hawa wa hadithi fupi za kisasa wanaumbwa kwa mapana kidogo kuliko wale wa ngano, tena ni wa kuaminika. Wasanii wa hadithi fupi za kisasa wanatumia mbinu za kidrama katika usanii wao. Jambo hili ni tofauti na mbinu za kingano.
Tumedokeza hapo awali kwamba ngano ni fupi kuliko hadithi fupi ya Kiswahili ya kisasa. Hii ni kwa sababu hadithi hizo za ngano hueleza mambo yake kimkato mno ukilinganisha na hadithi fupi za kisasa. Ngano pia husisitiza masimulizi yale yenye lengo la kutoa uzito mkubwa kwa maadili ambayo fanani anapenda yafike kwa hadhira iliyokusudiwa. Kwa mfano, kama fanani analeta dhamira ya choyo, basi ngano nzima itaelekezwa kimasimulizi kwenye ubaya wa uchoyo. Na hivyo ndivyo huwa tabia ya ngano karibu zote.
Inasemekana kwamba ngano zilikuwa za kwanza kuzuka katika jamii baada ya wimbo wa kazi na ushairi. Ngano nyingi zilihusu mazmgira yaliyomzunguka binadamu kwa ujumla. Kwa upande wa maudhui, F.E.M.K.Senkoro14 anasisitiza kuwa ngano za mwanzo zilihusu mazingira na visa-viini. Masimulizi mengi kama vile ya kichawichawi yalizidi. Ngano hizi, kwa kutumia imani mbalimbali za kidini na kichawi zilisimuliwa nyakati za jioni (tena pengine wakati wa kufanya kazi isiyo nzito). Ngano hizo pia zilihusu chanzo cha mtu na chanzo cha dunia. Kulikuwa pia na ngano kuhusu matambiko, uzazi, jando na unyago na nguvu za miungu mbalimbali, vifo n.k. Ngano hizi zilishamiri sana. Umuhimu wa ngano uliwekwa katika maadili ziliyotoa. Kwa sababu hii, kama tulivyokwisha kudokeza hapo awali, suala la watunzi wake halikutiliwa mkazo sana. Hapakuwa na ulazima mkubwa sana kwa mtunzi wa ngano kujulikana, lakini maadili yake yalipaswa kujulikana kwa jamii na kutumiwa vilivyo. Sasa tuangalie utanzu wa hadithi fupi za Kiswahili.
Hadithi Fupi za Kisasa
Baadhi ya wananadharia na wanafasihi, hasa wale wenye mapokeo ya hadithi fupi andishi za huko Ulaya na Marekani wamezipambanua hadithi fupi za kisasa kwa kuzilinganisha na utanzu wa hadithi ndefu, ama riwaya. Kufanya kwao hivyo kunatokana na madai na mtazamo wao kwamba tanzu hizi mbili zinahusiana na kufanana katika baadhi ya mizungu yake ama katika baadhi ya mbinu zake za uandishi na hata kuwasilisha maudhui yake katika jamii.
Japokuwa kuna ukweli katika kauli hii, hadithi fupi andishi katika mapokeo ya fasihi andishi ya Kiswahili zina sifa na misingi muhimu inayozipambanua na kuzifanya zionekane tofauti na tanzu nyingine kama vile riwaya. Viko vigezo vingine vya msingi vinavyozipambanua hizi hadithi fupi ambavyo hutumiwa na wanataaluma mbalimbali katika kuelezea maana ya hadithi fupi kwa ujumla. Tutavijadili vipengele hivyo hapa chini.
Hadithi fupi za kisasa zinabeba uzito wake mkubwa sana katka kipengele cha kubuniwa na kinachosemwa na kuandikwa mara nyingi huelemea kwenye matendo yale ya kihalisia. Pamoja na kubuniwa huko, bado wakati mwingine kuna athari za kifasihi simulizi. Patricia Mbughuni anakiri jambo hili kwa kusema kuwa:
...fasihi ya Kiswahili ya sasa ina athari ya fasihi simulizi kisanaa na kimandhni. Mambo kama dhamira, mtindo na muundo ama ujenzi wa wahusika pamoja na falsafa zilizokuwa ziaajitokeza katika fasihi simulizi zinajitokeza pia katika fasihileo ya Kiswahili japo kama kuna mambo kadhaa yamebadilika.15

Bila shaka mabadiliko hayo yanatokana na mfumo wa historia katika jamii ambao hubadilika kufuatana na wakati.
Kwa mujibu wa Rajmund Ohly,16 athari mbalimbali zilizoko katika fasihileo ya Kiswahili zinatokana na hali ya mazingira. Kwanza, athari hizo zimetokana na mapokeo ya mifumo mbalimbali katika utamaduni, uchumi na siasa. Athari hizo zinaambatana na mtindo wa kutoa maadili ya kidini. Kuna kundi la pili la athari ambalo linatokana na ujio wa wageni katika sehemu hii ya Afrika Mashariki. Athari hizi zinatokana na mataifa ya Asia, Oman na Shiraz, pamoja na zile za mataifa ya Magharibi. Athari ya tatu inayojipambanua katika hadithi za fasihi za kisasa ni ile inayotokana na nafsi-jenzi ya waandishi wenyewe. Hapa ina maana kwamba kama mwandishi ni mwanamke, maandishi yake yatakuwa na athari kadhaa za msingi ambazo ni za kike, na kama mwandishi ni mwanaume, athari kadhaa za msingi zitakuwa zile za kiume. Kwa hiyo tunategemea kuona dhana kama vile madai ya ukombozi wa mwanamke, athari ya mitazamo ya vijana kuhusu maisha na pia mitazamo ya wazee ama watu wa makamo. Tunategemea pia kuona athari za kielimu katika baadhi ya kazi za kifasihi zitakazotolewa na watu wa jamii ya sasa.
Tulisema pale awali kuwa hadithi fupi za kisasa zinatakiwa ziwe za kubuni, na kwamba kipengele hiki ni muhimu. Aidha, yako mambo mengine ya msingi ambayo kusema kweli yanaifafanua zaidi hadithi fupi ya kisasa. Katika ufafanuzi wake, Esenwein kwa mfano, anaanza kwanza na kusema kile anachokiona kuwa si hadithi fupi. Anasema: "...hadithi fupi si kifupisho cha riwaya."17 Baadhi ya wasomaji na waandishi, hasa wale wachanga, wanashindwa kutofautisha na kuelewa hadithi fupi ni nini hasa. Kwa sababu hii, wanadhani kuwa hata riwaya ikifupishwa inaweza kuchukuliwa kama haditbi fupi. Kimsingi, tofauti katika tanzu hizi mbili zimo kaiika aina na wala sio katika urefu. Urefu ni kigezo kinachoweza kutumika katika kuziainisha tanzu hizi mbili, lakini kigezo hiki lazima kishirikishwe na vingine.
Jambo la pili analoona mtaalamu buyo kuwa si hadithi fupi ni maelezo kuhusu tukio ama masimulizi kuhusu jambo fulani linalotakiwa kukamilishwa kwa kusimuliwa ama kuungwa na jingine. Wala hadithi fupi sio sura moja ya riwaya ndefu. Hadithi fupi ni utanzu mkamilifu unaojitegemea.
Esenwein anaendelea kukanusha kwamba hadithi fupi siyo madondoo yaliy-otayarishwa kwa ajili ya kuandika kazi ya sanaa fulani, hususan hwaya au tamthiliya. Wala hadithi fupi si masimulizi yaliyofupishwa juu ya maisha ya mtu kutoka utotoni hadi uzeeni. Hadithi fupi ni kazi inayojitegemea na ni yenye sifa zake maalumu zinazoifanya iwe fupi.
Wakati mwingine, wako baadhi ya watu wanaoipa ngano uzito na hadhi ya kuwa sawa na hadithi fupi ya kisasa. Esenwein anasisitiza kuwa kila aina hapa ina misingi maalumu, japo kuna kufanana kwa kiasi fulani katika vipengele kadhaa. Mtazamo wake kuhusu hadithi fupi ni upi basi?
Esenwein, kwa kutumia sifa-hasi zilizotolewa hapo juu katika kuipambanua hadithi fupi, analeta sifa-chanya ambazo hatimaye zinaupambanua utanzu wa hadithi fupi. Esenwein18 anatoa sifa zifuatazo za hadithi fupi:
1. Pawepo na tukio moja lililopewa uzito kuliko jingine lolote. Kwa sababu ya kupewa uzito, mawazo na mbinu zote kuhusu tukio hilo, zitaelekezwa kwenye tukio hilo, na ujenzi wa kila kitu huelekezwa kwake.
2. Awepo mhusika mkuu mmoja anayejitokeza sana kuliko wengine wote katika hadithi hiyo. Wahusika wengine wasielezwe kwa mapana.
3. Lazima hadithi hiyo iwe na sifa ya kubuniwa. Sifa hii ikikosekana, tayari kuna dosari katika kuuainisha utanzu huu wa hadithi fupi. Kubuni sio maana yake kusema uwongo, hadithi ya kubuni ina ukweli fulani wa maisha.
4. Hadithi fupi inapaswa iwe na msuko. Pawepo na upangaji mzuri wa maelezo yanayotiririka kutoka mwanzo wa tukio kutendeka hadi mwisho wa kutendeka kadhia hiyo.
5. Maelezo na masimulizi katika hadithi fupi yatumie mawanda yasiyo mapana. Maelezo hayo yatumie muda mfupi, yatolewe kimkatomkato na kwa kifupi.
6. Pawepo na umoja na mshikamano wa maelezo katika mtiririko na msuko wa hadithi nzima. Mshikamano huo lazima ulete mantiki kwa msomaji wa kazi hiyo.
7. Masimulizi yaonyeshe umoja wa hadithi yote.

Tukiyaangalia maelezo hayo kiundani, yote yana ukweli fulani. Japokuwa kuna ukweli huo, tuna wasiwasi juu ya maelezo hayo kwa sababu ya shabaha ya uainisho wake. Esenwein hakufikiria hadithi za Kiswahili katika uainisho wake. Na kusema hivyo haina maana kuwa sifa hizi zilizotajwa hapo juu juu ya uainisho wa hadithi fupi, hazifai. Zinaweza kuwa sahihi kabisa. Tunachbhitaji kufanya sasa ni kuthibitisha kama kweli sifa hizo zipo katika hadithi fupi za Kiswahili kama zilivyo katika mapokeo ya hadithi fupi andishi za Kiswahili.
Pamoja na upambanuzi alioufanya Esenwein ambao pia tunaukubali kwa kiasi kikubwa, ziko nadharia nyingine walizozitumia wataalamu mbalimbali katika kuelezea maana ya hadithi fupi.
Nadharia ya kwanza ni ile inayohusu muda. Nadharia hii imepata kutumiwa na baadhi ya wanataaluma kuelezea maana ya hadithi fupi, hasa katika mapokeo ya fasihi andishi ya huko Ulaya na Marekani. Nadharia hii inasisitiza kuwa hadithi fupi iwe ni kitu (maandishi) kinachoweza kusomwa kwa muda mfupi. Hadithi fupi inatakiwa isomwe katika kikao kimoja. Allan Poe19ndiye aliyekuwa miongoni mwa watu walioiendeleza sana nadharia hh. Lakini waanzilishi wa nadharia hii ni Plato na Aristotle (300 K.M.).20 Wanataaluma hao walidai kuwa kazi ya sanaa ya kitanzia lazima iwe fupi ili iweze kusomwa kwa muda mfupi na kukaa akilini mwa watu na kukumbukwa kirahisi. Hii, waliona wataalamu hao, itawafanya watu waweze kukumbuka maudhui na falsafa zilizomo kwenye kazi ya aina hii ya kisanaa bila matatizo makubwa.
Wanataaluma hao pia walisisitiza juu ya mpangilio mzuri wa maneno wakati wa kuandika kazi ya sanaa ili isomeke kwa urahisi na haraka.
Kwa miyibu wa Aristotle, kazi zote za tanzia, kwa kuwa zilikuwa ngumu, zilihitajika, pamoja na mengineyo, kuwa na msuko mzuri (safi) wa visa, fikra kuu au wazo kuu moja na sahihi ili wasomaji wake wasipate shida. Inawezekana mtazamo huu umechangia katika kuikuza nadharia hii inayohusu muda katika kuelezea maana ya hadithi fupi.
Aidha, katika hali halisi, kigezo hiki cha muda kina matatizo yake. Kwanza kabisa, baadhi ya wasomaji wa hadithi fupi wanaweza kutumia saa nyingi mno kuliko labda inavyotakiwa kuisoma hadithi moja fupi kwa sababu hawasomi harakaharaka. Ama wengine nao wanaweza kutumia muda mchache mno kuliko labda inavyokadiriwa iwe katika kuisoma hadithi fupi hiyo kwa sababu wanaweza kusoma haraka. Tatizo kubwa hapa ni kuuainisha muda huu unaosemwa kuwa m mfupi, na kuangalia misingi inayozingatiwa katika kuisoma kazi inayohusika. Ni kipimo kipi hasa kichukuliwe kama ni muda mfupi utakaotumika katika kuisoma hiyo hadithi fupi?
Kwa upande mwingine ziko kazi za kisanaa ambazo zinaweza kusomwa katika kikao kimoja na kumalizika kwa muda mfupi. Kwa mfano, riwaya iliyofupishwa inaweza kusomwa yote kwa muda mfupi. Lakini hii haina maana kuwa riwaya hiyo iliyofupishwa itakuwa ni hadithi fupi. Jambo la muhimu kusisitiza ni kuwa pamoja na kutumia muda mfupi, lazima pawe na vigezo vingine vitakavyosaidia kuipambanua hiyo hadithi fupi. Kwa msingi huo, nadharia hii ya muda ni yajumla mno katika kutoa ufafanuzi wa hadithi fupi ya Kiswahili.
Nadharia nyingine mayotumika katika kuelezea maana ya hadithi fupi ni ile inayozingatia idadi ya maneno. William Saroyan21 anapendekeza na kuona kuwa hadithi fupi inapaswa iwe na maneno kati ya elfu mbili mia tano na chini ya elfu kumi. Ikiwa hadithi itakuwa na maneno chini ya elfu mbili mia tano, basi itakuwa imechukuliwa kuwa ni hadithi fupi iliyo fupi sana.
Akizungumzia nadharia hiyohiyo ya wingi wa maneno, Walter Blair na wenzake anasema kuwa hadithi fupi mara nyingi, "huwa chini ya maneno elfu kumi, lakini mara chache huwa na maneno zaidi ya elfu thelathini na tano."22 Halafu anaendelea kwa kusisitiza kuwa "hadithi fupi hukamilika inapokuwa yenye umoja na mshikamano na uhusiano katika vipengele vyake vyote. Hadithi fupi si kifupisho cha riwaya ama hadithi ndefu ya aina yoyote ile..."23 Mawazo hayo yanaelekea kukubaliwa na kuungwa mkono na wataalamu wengine kama vile Ezekiel Mphahlele na Penina Muhando na Ndyanao Balisidya. Katika kusisitiza hoja yao, kwa mfano, Muhando na Balisidya wanasema kuwa "visa (hadithi fupi) ni hadithi zenye fani inayoachana na ile ya ngano kwa undani na uhuru wake... Aidha, zina urefu ulio pungufu ya ule wa riwaya..."24 Hawatoi idadi ya maneno.
Tukifuatilia kwa makini hoja hizo zinazotolewa, tunaona kuwa katika mapokeo ya fasihi andishi ya Kiswahili, nadharia ya maneno inatofautiana kimtazamo na ilivyoelezwa hapo awali kama kipimo cha hadithi fupi. Hii inatokana na hoja kuwa dhana ya "neno" katika lugha za Kibantu, si sawa na dhana ya neno katika lugha kama vile Kiingereza. Katika lugha za Kibantu, neno linaweza kuwa na maana ya sentensi kamili.
Zaidi ya hayo, hadithi fupi za Kiswahili kimsingi hazijawahi kuvuka maneno elfu kumi. Katika Kiswahili, hadithi zilizokuwa na maneno zaidi ya elfu kumi zimekuwa zikichukuliwa kuwa m riwaya. Hapajawa na ugumu aghalabu wa kuainisha riwaya. Mara nyingi imekuwa ni ndefu, fupi au ndogo.
Tukizitazama nadharia zote hizo, sasa tunaweza kusema kuwa hadithi fupi ya Kiswahili m nini. Hadithi fupi ya Kiswahili itakuwa na misingi karibu yote tuliyoyadili hapo awali. Aidha, ili kuikamilisha na kuitambulisha kuwa ni hadithi ya Kiswahili, mazingira yake ya kifani na kimaudhui yanakuwa yale yaliyojikita katika utamaduni wa watu watunriao lugha ya Kiswahili.
Vifuatavyo ni vipengele muhimu ambavyo vinaipambanua hadithi fupi ya Kiswahili:
· Ni masimulizi ya kadhia moja lililowekwa katika mazingira ya utamaduni wa lugha ya Kiswahili.
· Kadhia hiyo ielezwe kwa ufupi na isitumie wahusika wengi, mara nyingi mmoja au wawili.
· Hadithi fupi iwe ni masimulizi ya kubuni. Maana ya kubuni siyo kusema uwongo. Hadithi ya kubnni ni kiwakilishi cha kisanaa kwa kutumia lugha.
· Hadithi fupi ya kubuni sio foto ya maisha halisi, bali ni maisha yaliyosan- ifiwa, yaliyorembwa au kutiwa chumvi kwa shabaha maalumu.
· Hadithi fupi ya Kiswahili inatakiwa iwe na msuko, tofauti na hadithi za kingano. Maelezo na mawazo muhimu yawe yamepangwa vizuri
· Hadithi fupi ya Kiswahili haipaswi kuwa na mawanda mapana kwa namna yoyote ile.
· Hadithi fupi ya Kiswahili haina mchangamano wa masimulizi. Mandhan huwa si mapana.

Ni muhimu kutambua kuwa baadhi ya sifa hizi zinaweza pia kupatikana katika tanzu nyingine za kisanaa kama vile riwaya na tamthiliya.

Kielelezo 1: Fasihi na Tanzu Zake
Maelezo
1. Maoni hayo yalipata kutolewa kwangu na Profesa E. Kezilahabi wakati alipousoma mswada huu kwa mara ya kwanza.
2. Hizi ni tenzi za Bahaya ambazo ni maarufu sana. M M.Mulokozi amefanya uchunguzi mkubwa na mpana kuhusu tenzi hizo za Nanga katika tasnifu yake ya Udaktari (Ph.D.) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
3. Maelezo hayo yalitolewa kwangu na Daktari C. Ndulute ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi katika Idara ya Fasihi ya Kiingereza ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
4. F.E.M.K.Senkoro, Fasihi, Press and Publicity Centre, Dar es Salaam 1984.
5. E. Mphahlele, A Guide to Creative Writing, EALB, Dar es Salaam 1986.
6. P. Muhando na N. Balisidya, Fasihi na Sanaa za Maonyesho, TPH, Dar es Salaam: 1976.
7. F.E.M.K.Senkoro, Riwaya ya Kiswahili na Maendeleo ya Umma, (Tasnifu ya M A. ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam 1978)
8. J. Berg Esenwein, "Writing the Short Story." A Practical Handbook on the Rise, Structure, Writing and Sale of Modern Short Siory, Hinds, Nobe and Eldredge - New York: 1909.
9. R. Finnegan, Oral Literature in Afnca, Oxford University Press: 1970
10. Kama Na 8. 11 Kama Na. 6.
12. Kama Na. 6.
13. R. Scholes and Kellog, R., The Nature of Narrative, Oxford University Press, New York: 1986.
14. Kama Na. 4.
15. P. Mbughuni, From Oral to Written- The Politicization of Kiswahili Literature, Ph.D. Thesis, University of Indiana: 1978.
16. R. Ohly, Aggressive Prose, TUKI, Dar es Salaam: 1981.
17. Kama Na. 8.
18. Kama Na. 8.
19. E.A. Poe, On the Aim and Technique of the Short Story, Thomas Y Crowell & Co., New York: 1902.
20. J.H. Smith na Parks E.W., The Grat Critiques: An Anthology of Literary Criticism, W.W. Norton & Co Inc. Vail Ballow-Press; 1978.
21. W. Saroyan katika Steinberg, S.H. (Ed.) (et al.) Cassell's Encyclopaedia of Literature (In two volumes: Volume 1), Cassell &; Company Ltd, London: 1953.
22. W. Blair (na wenzake), "Introduction to Short Stories, Drama and Poetry," katika Literature, Scott, Foresman and Company, 1959: 1966 338
23. Kama Na. 22
24. Kama Na. 6.
Powered by Blogger.