MALENGA WAPYA WAANDISHI: TAKILUKI WACHAPISHAJI: O.U.P MWAKA : 1997
MALENGA
WAPYA
WAANDISHI:
TAKILUKI
WACHAPISHAJI:
O.U.P
MWAKA : 1997
UTANGULIZI
MALENGA WAPYA ni diwani yenye
mkusanyiko wa mashairi yapatayo thelathini na saba (37) yaliyoandikwa na
washairi wapya(malenga wapya). Washairi hawa ni wanafunzi wa Taasisi ya
Kiswahili na Lugha za Kigeni huko Zanzibar.
Katika
diwani hii ,washairi wamejadili masuala mbalimbali yanayotokea katika jamii.
Baadhi yake ni masuala ya kisiasa, kiuchumi, kijamii n.k.Washairi hawa
wamejadili masuala ya msingi katika kujenga jamii mpya na kama yatazingatiwa
mabadiliko chanya yatatokea kwenye jamii.
MAUDHUI YA MALENGA WAPYA:
Maudhui ni mawazo
yanayozungumzwa na msanii wa kazi ya kifasihi pamoja mtazamo wa mwandishi au
msanii juu ya mawazo hayo.
A). DHAMIRA:
Ni wazo kuu lililomo katika
kazi ya kisanaa.Huu ni msukumo alionao mwandishi hata akaandika kazi Fulani ya
kifasihi.Mshairi anaweza kuwa na lengo la kuonesha mambo mbali mbali- mienendo
mizuri na mibaya- yatokeayo katika jamii.Katika diwani hii washairi hawa
wameyachora mambo kadhaa yatendwayo na jamii, nayo ni kama;
1.
UONGOZI MBAYA
Washairi
wa diwani hii wamezungumzia suala la uongozi mbaya kama ndicho chanzo cha
kudorora kwa maendeleo ya jamii katika Nyanja mbalimbali.Mwandishi ameonesha
kuwa viongozi wengi hawatekelezi wajibu wao na pia hawapati muda wa kusikiliza
shida za wananchi,viongozi hupuuza kuchukua hatua hata kwa mambo yanayotaka
ufumbuzi wa haraka.Kama shairi la PUUZO msanii anasema;
Unapokuwa
na shida, wao wanakupuuza,
Wanajitia
kidata, na kuifanya ajiza,
Wajifanya hawajali.
Ofisini ukifika, wanakuweka
baoni,
Wakati
uliofika, wao hawauthamini,
Wanakuambia
subiri.
Hali kadhalika viongozi wengi
wadhulumaji kwani huwalazimisha wananchi wanunue hata huduma ambazo kimsingi ni
stahiki yao.Katika shairi la BAHARI . Msanii ameonesha dhahiri namna viongozi
wanavyotumia nafasi zao kuwakandamiza wananchi.Mshairi anasema
Mdai
ni haki yao, mola amewajalia
Kuwadhulumu
wenzao, wao wanafurahia,
Nao
kwa unyonge wao,wadogo wateketea,
Bahari
ni hatari,wala usichezee,
Katika shairi la MPAKA LINI? Mshairi
anelezea kuwa viongozi wana kawaida ya kuwanyanyasa wananchi wanaosema ukweli
na kuwakumbatia wale wanafiki na wafitini,kama ubeti huu usemavyo
Msema
kweli, kwenu nyinyi ni chagizo,
Mtaka
hali, havuki mbele ya vikwazo,
Mwongo
sana, kwenu nyinyi ni kigezo,
Mpaka
lini mtatuchezea?
Pia mwandishi amebainisha jinsi
viongozi wasivyo tekeleza ahadi zao na kubaki wanapayuka (kuhutubia majukwaani)
mfano katika shairi la PAYUKA (uk
50).
Kupayuka
kwenu huko,
Mbona
tu kokoriko,
Sioni
linalokuwa
2.
MATABAKA
Mwandishi
ameonesha katika jamii kuna matabaka mawili tabaka la chini (tabaka tawaliwa)
na tabaka tawala linavyogandamiza na kulinyonya tabalka la chini (
linavyotumikiswa na kulinganishwa na punda) mfano katika shairi la PUNDA
msanii anasema;
“Toka
tulipozaliwa, maishayo ni kigozo,kizogo,
Hatujapata
kuenziwa, waishi tingivyogo,
Nawe
hujajielewa, u kiumbe u kigogo,
Kama
ungefadhiliwa, usingebeba mzigo,
Hakika
ulionewa, hustahili kupigwa kipigo,
Haki
umeitambua, idadi japo kidogo”
Vile vile suala la matabaka
limejadiliwa na mwandishi mfano mshairi wa SAMAKI
MTUNGONI (UK 19) shairi hili linaonyesha tabaka la juu yaani tabaka tawala
(viongozi) ambao ni wavuvi na tabaka la chini yaani tabaka tawaliwa ni samaki,
tabaka hili linanyonywa na kugandamizwa.
Katika
Shairi la NINI WANANGU (UK 24)
msanii ameonesha maisha ya chini ya tabaka la chini. Tabaka hli lina hali mbaya
ya maisha ukilinganisha na tabaka la juu.
Pia
katika Shairi la MKULIMA (uk 3) wasomi wanaonesha tabaka la chini (wakulima ) lisivyothaminiwa
na tabaka la juu hali hii inasababisha kunyimwa kwa huduma muhimu wanazotakiwa
kupewa raia.
3.
ATHARI ZA UKOLONI MAMBOLEO
Ukoloni
mamboleo ni hali ya nchi moja kutawala nchi nyingine kiuchumi.Ukoloni mamboleo
unaathiri uchumi wanchi zinazoendelea. Katika Shairi NIPATIENI DAWA, mwandishi
anaonesha kuwa baada ya ukoloni kuondoka nchini ukoloni huo ulirudi kwa umbo
(sura) nyingine ukiendeleza taratibu za kikoloni za kunyonya uchumi wanchi
masikini .
“Palepale
penye donda, ndipo apajanibana,
Nikawa
sasa nakonda, pumzi nikawa sina,
Nikabaki
kama ng’onda, la kufanya sikuona,
Nipatieni
dawa, nipate kutononoka,
Kila
nikifurukuta, donde apata toa,
Najitia
kwenye tata, shida kujizidishia,
Dawa
nimeshatafuta, ili niptate kuoa,
Nipatieni
dawa, nipate kutononoka.”
Mwandishi anaonesha jinsi ukoloni
mamboleo ulivozifanya nchi masikini na kunyonya uchumi wake hivyo basi ili
kuondokana nao ni lazima atafute dawa.
4.
NAFASI YA
MWANAMKE KATIKA JAMII
Mshairi
wa diwani hii amemjadili au amemchora mwanamke katika sura au nafasi
tofautitofauti kama ifuatavyo:-
Ø
Mwanamke ni
msaliti
Katika shairi la UTANIKUMBUKA mwanamke anaonekana ni
mtu asiye mwaminifu katika mapenzi na ndoa yake kwa sababu anashiriki ngono na
wanaume wenye pesa na mali nyingi huku akimuacha mume wake ambayeni msikini.
Mshairi anasema
“Umeona
bora kitu, ukasahau ya nyuma,
Umetupa
mbali utu, na zote zangu huruma,
Kwako
kutokaa katu, iko siku utakwama,
Utaumeza
uwatu, iwe ni yako hatima”.
Ø
Mwanamke ni mtu
mwenye tamaa mbaya
Katika shairi la UTANIKUMBUKA,mwanamke anaonekana ni
mtu mwenye tamaa ya kutaka vitu kutoka kwa wanaume sio kuangalia penzi la mtu.
Mwanamke anaonekana kuwa ni mlafi wa mali na mwenye kutamani mali.
Ø
Mwanaume kama
chombo cha starehe(muhuni/Malaya)
Katiaka shairi la “KITENDAWILI” mwanamke anaonekana ni
chombo cha starehe (mtu Malaya) yaani mtu asiyetulia kwa mwanamme wake (ndoa
yake) huku akishiriki mapenzi na wanaume wengine kiasi cha kuogopwa na wengi kwa
matendo yake. Mshairi anasema
“Jogoo
lina mafamba, linatamba kiamboni,
Kwa
kiburi lajigamba, hadi kiambo jirani,
Hili
jogoo la shamba, sasa lawika mjini,
Kitendawili
natega, mteguzi ategue”.
Aidha katika shairi la KUUNGE, mwanamke amechorwa
kama chombo cha starehe (mtu Malaya) yaani anashiriki tendo la ngono na wanaume
wengi ili kukidhi haja ya matamananio ya wanaume. Umalaya husababisha mwanamke
kupata magonjwa mbalimbali ikiwemo UKIMWI na hivyo kuwaambukiza wanaume wengi.
Mshairi anasema
“Nawambia
silipandi, hii pingu naiweka,
Naogopa
sina kundi, nikifa la kunizika,
Nawapenda
kina bundi, na kila anayeruka,
Silipandi
kataani”.
Ø
Mwanamke ni mtu
mwenye mapenzi ya kweli
Katika shairila “NIPATE WAPI MWINGINE” mwanamke
anaonekana ni mtu mwaminifu katika mapenzi, mtiifu, na mtu mwenye tabia njema.
Ndio maana baada ya kufa,mume wake (mshairi) alimlilia sana. Mshairi anasema:
“Njiwa
ali maridadi, kwa tabia hana shaka,
Na
hakuwa mkaidi, umwitapo kakufika,
Mafanowe
Kama radi, chini inapoanguka,
Njiwa
ameshanitoka, nipate wapi mwingine”.
Ø
Mwanamke ni
kiumbe dhaifu/duni
Katika shairi la “KIFUNGO”, mwanamke anaonekana ni
kiumbe dhaifu kisichoweza kufanya chochote cha maendeleo kwani humtegemea
mumewe kwa kila kitu na kunyimwa haki yake ya msingi ya kutafuta riziki.Mwanamke
hufungiwa ndani ya nyumba pasipo kutoka nje akifanya kazi ya kupika na kulea
watoto tu. Mshairi anasema
“Kwa
kuwa ni mwanamke, ndani munanifutika,
Lazima
nje nitoke, kupata ninayotaka,
Nimechoshwa
na upweke, sitaki kudhalilika,
Kifungo
kimenichosha, minyororo nafungua”.
5.
UMUHIMU WA KUINUA UCHUMI
Ili
Kujenga taifa linalojitegemea ni lazima kujenga uchumi unaoweza kuleta
maendeleo.Mwandishi anaonyesha umuhimu wa kilimo ili kuepukana na adui njaa. Katika
Shairi la ADUI msanii anasema;
“Tulime
jama tulime, tushinde adui njaa,
Hapa
kwetu ituhame, kwengine kutokomea,
Wala
sisi tusikome, chakula kujilimia,
Tutie
jembe mpini, tuteremke shambani,
Chakula
kujilimia, ziada kujipatia,
Tuache
kutegemea, vya nje kuagizia,
Siku
watajigomea, nani tutamlilia?
Tutie
jembe mpini, tuteremke shambani”.
Kwa
upande wa kilimo mwandishi ameonesha kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa taifa
letu,katika shairi la MKULIMA mwandishi ameonesha kuwa mkulima ni mtu wa kumthamini kwani yeye ndiyo
kila kitu kama beti hizi mbili zinazothibitisha;
“Wakaazi wa mjini, na wafanya kazi pia,
Na viongozi nchini, huduma awapatia,
Sijui kakosa nini?, thamani kutomtia,
Mkulima naye mtu, yafaa kuthaminiwa”
“Upungufu wa chakula, utokeapo nchini,
Hukumbana na suala, shambani wafanya nini?,
Kazi yako unalala, watia njaa nchini,
Mkulima naye mtu, yafaa kuthaminiwa”.
Mwandishi anaonesha kuwa jamii inapaswa
kumdhamini mkulima kwani anamchango mkubwa katika maendeleo ya taifa.
6.
UMUHIMU WA KUTENDA MEMA
Ili
jamii iishi kwa utulivu na amani,watu wote hawana budi kutenda mema.Katika shairi
la USIHARAKIE
MAISHA,waandishi wanataka wanafunzi wanaosoma wasiharakie maisha kwa
kutamani vitu vya kesho wakati wao wanaishi leo. Pia katika Shairi la MAISHA
NI KAMA NJIA mwandishi anataka jamii itende mema bila kuwatendea
wengine uovu hivyo kiburi na ubabe haufai katika jamii (maisha).
Pia katika Shairi la ULIMI mwandishi amezitaka
ndimi ziseme mambo mazuri tu kama ubeti ufuatao unavyosema;
“Usiropoke kwa wenzio, kwanza sema,
Usipachike pachike, maneno yasiyo mema,
Useme wanufaike kwa kauli yako njema,
Ewe ulimi sikia”
Mwandishi anaitaka jamii itende mema
nyakati zote ili jamii nzima iishi vyema.
7.
UMUHIMU WA KUTUMIA PESA VIZURI
Mali
bila daftari hupotea bila habari. Hivyo amini inaaswa uwe na matumizi mazuri ya
pesa, mfano shairi la ISRAFU,msanii anasema;
“Mali uliyojichumia,
Ni yako nakubalia,
Lakini kiangalia,
Vipi unaitumia’
Mwenzangu nakuusia,
Israfu haifai”.
Hivyo matumizi mabaya ya pesa
husababisha umasikini ambao husababisha mhusika kukimbiwa na watu hata rafiki
zake.
8.
MAPENZI NA
NDOA
Mapenzi
na ndoa ni kitu cha muhimu katika jamii.Mfano shairi la UA mwandishi anasema mtu
afikapo umri wa kuoa au kuolewa basi na afanye hivyo shairi la NIPATE
WAPI MWINGINE,wasani wanauliza walimwengu wapate wapi wenzi wao baada
ya yule wa kwanza kuwatoka.Vilevile wanasema mapenzi ya siku hizi hayafai kwani
hutegemea zaidi fedha.Ni mapenzi yenye kusababisha umalaya, yamejaa udanganyifu
kati ya mwanamke ana mwanaume mfano shairi la KWA NINI?. Wasanii
wanakemea tabia ya baadhi ya wanaume wanaowaacha wake zao na kufanya uzinzi na
wanawake wengine wa na kupoteza pesa zao.
“Mke wake, atamwacha, singizini,
Atoroke, parakacha, migombani,
Kumbe kake, anakocha, mwa jirani,
Kwa nini?”.
Mwandishi anaitaka jamii kuwa na
mapenzi ya dhati ili kuepusha maumivu kwa anayeachwa na jamii kwa ujumla.
B).
UJUMBE
Waandishi
wa diwani hii ya MALENGA WAPYA wanatoa ujumbe ufuatao;
Ø
Kuinua uchumi ni
jambo la muhimu sana kwani kutapunguza utegemezi wa misaada kutoka nchi
zilizoendelea.Ujmbe huu unapatikana katika shairi la “MKULIMA”, “PUUZO”, “ADUI” na
‘TUYAZINGATIE HAYA”.
Ø
Ukombozi wa
mwanamke ni muhimu kwaajili yake na jamii nzima. Ujumbe huu unapatikana katika
shairi la “KIFUNGO”,“HINA INAPAPATUKA”, na “PUNDA”.
Ø
Hamadi kibindoni
silaha iliyo mkononi.Hii ina maana kwamba ni vema kujiwekea akiba kwa
kuzingatia matumizi mazuri ya mali, ikiwemo pesa, kwaajili ya maisha mazuri ya
kesho. Ujumbe huu unapatikana katika shairi la “ISRAFU”.
Ø
Ili kuinua uchumi
wa nchi ni lazima kusisitiza kilimo na kumthamini mkulima. Ujumbe huu
unapatikana katika shairi la “MKULIMA”.
Ø
Jamii izingatie
maadili mema ili kuleta haki, usawa na amani. Ujumbe uu unapatikana katika
shairi la “HAKI” na “SIHARAKIE MAISHA”.
Ø
Matabaka ni
kikwazo kikubwa cha maendeleo ya jamii.Ujumbe huu unapatikana katika shairi la
“SAMAKI
MTUNGONI’, “MKULIMA”.
Ø
Maisha ni kama
njia.Hapa duniani si makazi ya kudumu,isipokuwa mbinguni.Hivyo tutende mema na
tumwombe Mungu ili tuje kuishi maisha ya raha baada ya kifo.Ujumbe huu
unapatikana katika shairi la “MAISHA NI KAMA NJIA”.
Ø
Uongozi mbaya
hurudisha nyuma maendeleo ya jamii.Ujumbe huu unapaikana katika shairi la “PUUZO”
na “BAHARI”.
Ø
Subira yavuta
heri hivyo kila avumiliaye ipo siku atapata.Ujumbe huu unapatikana katika
shairi la “SIHARAKIE MAISHA”.
B: MAADILI
Haya ni
mafunzo, nasaha au ushauri unaopatikana mara baada yakuiptia kazi ya kifasihi.Ni
maelekezo ambayo huelekezwa kwa hadhira ili iweze kutoka katika hali iliyomo na
kuelekea kwenye jamii mpya yenye Maendeleo na utengemano. Katika hili washairi
hawa wameitaka;
· Jamii
kuachana na tabia ya uvivu na utegezi na
kuwa wachapakazi ili kuunua uchumi wa nchi na maisha ya jamii kwa ujumla. Hili
limesisitizwa vizuri kupitia mashairi ya TUYAZINGATIE
HAYA, CHARUKA na ADUI. Hebu chunguza ubeti huu wa shairi la ADUI.
Haya shime tuitane,sote
tushirikiane,
Wala tusitegeane,kwa pamoja tushikane,
Aliye mwoga anene, kabisa tusigombane,
Tutie jembe mpini, tuteremke shambani.
· Pia wanaume walio katika ndoa kuachana na tabia ya
uasaliti wa ndoa zao kwani kwaweza kusababisha maafa makubwa kwa wanafamilia.
Washairi wanashauri hili kupitia shairi la KWA NINI? Wanapohoji sababu hasa
wanaume kuchepuka.
Utamwona, mwanaume, kashaini,
Anong’ona, na Selume, chochoroni,
Ndio laana, ajipime, japatani?
Kwa nini?
· Hali kadhalika malenga hawa wameielekeza jamii yao
hasa viongozi kuacha kukandamiza na kuonea raia. Washairi wanashauri hili
kupitia mashairi ya HAKI, MPAKA LINI?na SAMAKI MTUNGONI.
Angalia ubeti huu katika MPAKA LINI?
Mpaka lini, dhiki hii itafishwa?
Hadi lini,
mnyonge atadunishwa?
Jambo hili,
halina budi kukomeshwa,
Mpaka lini tutasemewa?
· Vile vile
washairi hawa wameelekeza wanajamii waache majungu, umbeya na kusengenyana
kwani hakuna faida yoyote kwa kufanyiana hayo ispokuwa kujenga uadui na chuki
miongoni mwa wanajamii. Wanashauri hilo kupitia shairi la ULIMI
Usiropokeropoke, kwa wenzio kwanza sema,
Usipachikepachike, maneno yasio mema,
Useme wanufaike, kwa kauli yako njema,
Ewe ulimi sikia!
· Isitoshe washairi hawa wamewashauri wanajamii wawe na
misimamo hivyo waachane na tabia ya kuiga matendo ya watu wengine na ambayo hayana maana yoyote wala msaada kwao
kwani yaweza kusabababisha maafa makubwa kwao.Ushauri huu unasomeka vizuri
katika mashairi ya SIHARAKIE MAISHA na USIWE BENDERA. Angalia ubeti huu katika shairi la
USIWE BENDERA.
Usione haya, baya kukataa,
Ingawaje baya, ukajibobea,
Ukaambiwa haya, ukajifanyia,
Usiwe bendera, kufata upepo.
Kama vile haitoshi, malenga
hawa wamewaelekeza viongozi kuto lewa madaraka na kusababisha kushindwa
kutimiza majukumu yao na kusababisha jamii kuendelea kuwa duni. Maelekezo hayo
yanaonekana vizuri katika shairi la SUKARI.
Utaumbuka ujue, sukari kiizoea,
Hukufunga utambue, utamu ukikukaa,
Lazima usijijue, ukishailafukia,
Haifai kubugia, sukari uiogope.
· Wanajamii pia wanapaswa kuwa makini na matumizi ya
mali na pesa wanazojichumia ili ziweze kuwafaa siku za mbeleni badala ya
kuzitumia ovyo bila sababu maalum. Maelekezo haya yanapatikana vizuri katika
shairi la ISRAFU.
Israfu ikimea,
Mali inayoyomea,
Watu watakuzomea,
Ukikosa egemea,
Mwenzangu nakuusia, israfu haifai.
· Pia wanajamii wanaelekezwa kuwathamini wakulima wakikumbuka
mchango wao mkubwa wanaotoa kwa jamii wa kuhakikisha jamii inapata chakula na
pesa nyingi tu za kigeni na hivyo kusukuma maendeleo ya jamii, badala ya
kuwatenga na kuwaona kama watu duni wasiostahili lolote. Haya yanaonekana kati
ka shairi la MKULIMA.
Dharau wakielewa, kuna hatari mbeleni,
Mkulima ang’amuwa, naye akae mjini,
Hapo ndipo tutajua, mkulima naye nani,
Mkulima naye mtu, yafaa kuthaminiwa.
Ø
FALSAFA
Mwandishi wa diwani hii anaamini kuwa umoja ,amani,na utulivu vitakuwepo
endapo haki na usawa miongoni mwa wanajamii vitazingatiwa.Vile vile anaamini kuwa jamii ikitilia mkazo suala la
kilimo uchumi wan chi utaimarika sana.
Ø
MSIMAMO/ MTAZAMO
Waandishi wanamtazamo wa kimapinduzi kwani wamejadili
kwa kina matatizo yanayozikabili jamii kama vile matabaka,uongozi
mbaya,unyonyaji,ukoloni mamboleo n.k na amependekeza suluhisho la matatizo hayo.
Ø
FANI
Fani
ni umbo la nje ya kazi za fasihi.Katika ushairi vipengele vya fani
vinavyochunguzwa ni:-
A.
MUUNDO:
Hii ni sura, msuko,umbo au
uwiano wa vipengele vyote vinavyojenga ushairi. Kuna vipengele kadhaa
vinavyotumika kama sehemu ya muundo navyo ni;
v Idadi ya mishororo:
· Tathlitha
Huu ni ushairi wenye mishororo mitatu kwa
kila ubeti.Ushairi huu pia huitwa UTATU.Katika kazi hii ya MALENGA
WAPYA yapo mashairi kadhaa yaliyosukwa namna hii, nayo ni kama vile PAYUKA,
TUNZO, KUUNGE, UA na HALI HALISI.
PAYUKA
1.
Nasikia makelele,
Ya
ngoma ile ya lele,
Kuimba
na kupayuka.
· Tarbia
Ni ushairi uliosukwa
kwa mishororo minne kwa kila ubeti.Tarbia pia hufahamika kama UNNE.Kidesturi
shairi la huwa na mishororo
iliyogawanyika katika vipande viwili. Malenga wapya nao wameweza kuisuka kazi
yao kwa kutumia muundo huu, mashairi yanayodhihirisha hilo ni pamoja na MAISHA
NI KAMA NJIA, ULIMI,SISUMBUKIE KICHAA, NIPATIENI DAWA, NIPATE WAPI MWINGINE na
SAMAKI MTONGONI.
ULIMI
1.
Ulimi ninakuasa, nisemayo usikie,
Mwenzio sijenitosa, nafasi sijutie,
Ninachokuomba hasa, unifanye nivutie,
Ewe ulimi sikia!
· Takhmisa:
Ni ushairi wenye mishororo mitano katika
kila ubeti.Ushairi huu huitwa pia UTANO au takhmisa. Kuna baadhi ya
takhimisa hazina mgawo wa vipande viwili kama ilivyozoeleweka.Katika kazi hii
malenga hawa wametumia muundo huu pia kama inavyojidhihirisha katika shairi la ISRAFU,
SIHARAKIE MAISHA.
ISRAFU
1. Ali ulojichumia,
Ni yako nakubalia,
Lakini kiangalia,
Vipi unaitumia,
Mwenzangu nakuusia, israfu haifai.
· Tasdisa:
Ni utungo wenye mishororo sita katika kila
ubeti. Pia huitwa USITA, TARDISA au TASHLITA. Ingawa tungo hizi si maarufu sana
lakini inaonekana katika diwani hii kama inavyojidhihirisha katika shairi la PUNDA
msanii anasema;
Toka ulipozaliwa, maishayo ni kizogo,
Hujapata kuenziwa, waishi tirigivyogo,
Nawe hujajielewa, u kiumbe hu kigogo,
Kama ungefadhiliwa, usingebeba mizigo,
Hakika ulionewa, hustahili kipigo,
Haki umeitambua, idadi japo japo kidogo.
· Sabilia:
Ni muundo ambao kazi ya kishairi hujengwa
kwa mishororo saba au zaidi kwa ubeti. Kama ilivyo kwa tasdisa mashairi ya
namna hii ni machache sana.Katika kazi ya MALENGA WAPYA kuna mfano wa shairi la
muundo huu ambalo ni PASUA UWAPE UKWELI.Katika shairi
hili msanii anasema;
Ambaye
tumekuridhi, asili yetu ni moja,
Sukani tumekukabidhi, toka zama za mababu,
Cheleza lete jahazi, uwapashe wapashike,
Pasi kuwa na woga, viduhushi wachochezi,
Uyakabili mawimbi, midomo yao wafyate,
Na hizo zake tufani, virago vyao wafunge,
Zipoze bila muhali, wawafate bwana zao,
Kwa kupasua ukweli, visiwa vishuwarike,
Kutugawa kwa mafungu, neema iengezeke,
Hilo kwetu ni muhali, tufurahie maisha,
Si dini wala si rangi, au la hata kabila.
v Idadi ya vipande:
Hiki ni
kigezo kingine cha kuainisha muundo wa kazi za kishairi,kwa kigezo hiki shairi
laweza kuwa na
· Vipande viwili ( manthawi )
Katika muundo huu mshororo wa ubeti
hugawika katika sehemu mbili; sehemu ya kwanza na ya pili.Mashairi kadhaa
katika diwani hii yamesukwa katika muundo huu, nayo ni pamoja na ADUI, KIFUNGO, KITENDAWILI, CHARUKA, NIPATE WAPI
MWINGINE.
CHARUKA
Charuka chacharukaka, mambo kuyakimbilia,
Charuka kirukaruka,mipango kufikiria,
Charuka kikurupuka,mbali uweze fikia,
Kabla hujapotea,charuka chacharukaka.
· Vipande vitatu ( ukawafi )
Kwa muundo huu mshororo wa ubeti wa shairi hugawika
katika sehemu tatu; yaani sehemu ya kwanza, ya pili na ya tatu. Diwani ya
MALENGA WAPYA imetumia pia muundo huu kupitia mashairi kadhaa kama vile KWA
NINI?, TUNZO na HAKI.
HAKI
Haki watutisha, tusikuandame, kwa matendo yetu,
Watukorofisha, tusikuandame, kila penye
kitu,
Mbona watutwisha, miba ituchome, kwenye
huu mwitu,
Tutokwe na utu!
· Kipande kimoja ( utenzi )
Katika muundo huu mizani ya mishororo huwa
michache kati ya 4 hadi 12 nao husimulia habari fulani au tukio fulani. Katika
diwani hii msuko huu unajidhihirisha kupitia shairi la PAYUKA.
Nasikia makelele,
Ya ngoma ile ya lele,
Kuimba na kupayuka.
Kupayuka kwenu huko,
Mbona tu kokoriko,
Sioni linalokuwa.
v Mbali ya idadi ya mishororo na
vipande pia kituo hutumika kuainisha muundo wa kazi husika. Katika diwani hii
ya MALENGA
WAPYA msanii imetumia vituo tofauti kama vile;
· Bahari:
Kituo cha namna hii maneno ya mshororo wa
mwisho yanakaririwa kutoka ubeti mmoja hadi mwingine.Msuko huu unajidhihirisha
katika HINA INAPAPATUKA, BAHARI na HALI HALISI.
· Nusu Bahari:
Kituo cha namna hii maneno ya kipande
kimoja hukariririwa ubeti mmoja hadi mwingine wakati ya kipande cha pili hubadilikabadilika.
Muundo huu umejitokeza katika shairi la CHARUKA.
· Kimalizio:
Katika kituo cha namna hii mshororo wa mwisho
hubadilikabadilika kutoka ubeti mmoja hadi mwingine.Muundo huu umetumika
vilivyo katika diwani hii hasa katika mashairi ya NINI WANANGU?, UTANIKUMBUKA,
SOKOMOKO BAHARINI
MATUMIZI YA LUGHA
Katika ushairi kipengele cha lugha
huhisisha taswira, tamathali za semi, methali, nahau,misemo na mkato wa maneno.
Taswira (picha/jazanda) hiki ni
kipengele cha lugha ambacho huchora au huwasilisha wazo kwa kutumia picha au
taswira mbalimbali,mfano katika shairi la SAMAKI MTUNGONI kuna taswira ya
samaki ikiwakilisha watu wa tabaka la chini (watawaliwa), taswira ya mvuvi ni
watu wa tabaka la juu (viongozi) na taswira ya mtungo ni sheria,kanuni au
taratibu zinazotumiwa kuwabana watu wa tabaka la chini.
Ø Njiwa mpenzi
shairi la NIPATE WAPI MWINGINE?
Ø Punda- tabaka linalokandamizwa (shairi la PUNDA)
Ø Ua – mwanamke/ msichana (shairi la UA)
METHALI
Kuna methali mbalimbali zimetumiwa
katika diwani hii; mfano
Ø Subira yavuta heri (shairi la SIHARAKIE MAISHA)
Ø Aisifie mvua kaloa mwilini mwake (shairi la SISUMBUKIE
KICHAA)
Ø Fahari – wapiganapo nyasi ndizo huonewa (SOKOMOKO
BAHARINI)
MISEMO
Ø Siharakie maisha (SIHARIKIE MAISHA)
Ø Sisumbukie kichaa (SISUMBUKIE KICHAA)
Ø Sokomoko baharini (SOKOMOKO BAHARINI)
TAMATHALI
ZA SEMI
TASHIBIHA
Ø Ubaguzi umezama kama nguzo (shairi la TUNZO)
Ø Maisha ni kama njia (shairi la MAISHA NI KAMA NJIA)
Ø Yametolewa na kombe mithili ya gome la mti (shairi
la BAHARI)
TASHIHISI
Ø Samaki wakasirika (shairi la SAMAKI MTUNGONI)
Ø Njaa imetuvamia (shairi la ADUI)
Ø Ua limejituliza (shairi la UA)
Ø Ulimi ninakuasa (shairi la ULIMI)
TASHITITI
Ø Katika shairi la MWABAJA MWASEMA NINI?
Ø Nasikia mwatunga,mwatungani washairi
TANAKALI
SAUTI
Ø Parakacha mlio wa majani makvu (shairi la KWA NINI?)
Ø Kokoriko – shairi la MKULIMA
TAKRIRI
Ø Kuna takriri kituo cha mfano shairi la KWA NINI?
MKATO WA MANENO
Ø
Kuna maneno
yamekatwa ili kuepuka urari wa vina na mizani mfano “anong’ona (shairi
la KWA NINI?).