DIWANI YA WASAKATONGE. Mwandishi: Mohamed Sef Khatibu Mchapishaji : Oxford University Press. MWAKA :2003

DIWANI YA WASAKATONGE.
Mwandishi: Mohamed Sef Khatibu
Mchapishaji : Oxford University Press.
                          MWAKA :2003
UTANGULIZI
WASAKATONGE ni diwani yenye mashsiri yanayotetea wavuja jasho wanaonyanyswa,kuonewa,kudharauliwa na kunyonywa na wenye navyo (tabaka la juu).Diwani hii ni chachu ya kuuamsha umma unaonyonywa ili uweze kudai haki dhidi ya wanasiasa wanaotumia nafasi zao kuonea wengine.
Diwani hii inaonyesha njia mbalimbali ambazo wanyonge wanaweza kuzitumia ili kupata ukombozi wa kweli. Moja ya njia hizi ni kupiga vita uongozi mbaya wa kidikteta,uongozi unaozifanya nchi nyingi barani Afrika kuendelea kuwa tegemezi.
MAUDHUI;
 DHAMIRA KUU ; UKOMBOZI
Ukombozi ni harakati za jamii yeyote zenye lengo la kuitoa jamii hiyo kwa nguvu  (kwa silaha) au kwa mazungumzo kutoka katika makucha ya utumwa kisiasa,kiuchumi,kimawazo na kiutamaduni.Katika diwani hii dhamira ya ukombozi imetazamwa katika nyanja mbalimbali
Ø Ukombozi wa kisiasa
Mshairi ameonyesha uhuni ni njia mojawapo ya kujitoa katika ukoloni. Mshairi ameonesha umuhimu wan chi za afrika kuwa huru ili kujiletea maendeleo, shairi la AFRIKA linavyoeleza
                   Lini?
                   Afika utakuwa,
                   Bustani ya amani,
                   Ukabila kuuzika,
Udini kuufyeka,
Ni lini?
Ø Ukombozi wa kiutamaduni
Msanii amezungumzia juu ya ukombozi wa mwanamke. Msanii anataka wanawake wajigomboe kutoka kwenye mila na desturi zinazowakandamiza. Njia moja wapo ya ukombozi wa mwanamke ni elimu ambayo itafanya atambue haki zake kama shairi la WANAWAKE WA AFRIKA lisemavyo.
                   Jifunzeni taaluma,
                   Mhitimu na kusoma,
                   Kila fani,
                   Iwe ndani,
                   Ndio ukombozi wenu,
                   Wa kisomi!
Hali kadhalika ukombozi wa kiutamaduni unaongelewa katika shairi la TOHARA ambapo imeonyesha kuwa mwanamke anakandamizwa kupitia mila na desturi ambazo zimepitwa na wakati.
Ø Ukombozi wa kiuchumi
Mwandishi anaonesha umuhimu wa wana jamii kujishughulisha na kazi mbalimbali ili kuinua uchumi wa nchi. Mshairi ametumia shairi la MVUJA JASHO kuonesha namna baadhi ya watu wanavyofanya kazi ili kuinua vipato vyao kama ubeti huu usemavyo:-
                   Wakulima shambani,
                   Majembe mikononi,
                   Wao wa kilimoni,
                   Asubuhi na jioni,
                   Mazao kila fani,
                   Vuno kuwa sokoni,
                   Lakini pato duni,
Ø Ukombozi kifikra
Mwandishi anatumia shairi la WANAWAKE WA AFRIKA kuwaelezea wanawake kuwa na mchango mkubwa sana kwa taifa hivyo ni jukumu lao kujikomboa na kujua haki zao za msingi badala ya kukaa kusengenyana,kuchukiana,kusutana n.k. Kama ubeti huu usemavyo
              Acheni kusengenyana,
              Waama kununiana,
              Kugombana,
Mwandishi anaona kuwa ni vyema suala la ukombozi katika jamii litazamwe kwa jicho pevu kwani ili jamii iendelee inapaswa kujikomboa katika Nyanja zote yaani kiuchumi,kisiasa,kifikra na kitamaduni.

1.    UONGOZI MBAYA
Mwandishi ameonesha namna uongozi mbaya ulivyo kikwazo cha maendeleo katika jamii.Suala la uongozi mbaya linaonekana kuwa sugu hasa katika nchi nyingi za kiafrika na kama tiba haitafutwi ni dhahiri kuwa machafuko ya kisiasa yataendelea kila kukicha kama shairi la MADIKTETA linavyosema:
                     Madikteta,
                   Katika dunia hii ya tatu,
                   Na hasa afrika yetu,
                   Itele “Mungu watu”,
                   Bokasa, Idi, Mobutu,
                   Mizinga nayo mitutu,
                   Haitoi risasi,
                   Hutoa maraisi,
                   Walio madikteta.
Mashairi mengine yanayoelezea uongozi mbaya ni NAHODHA,shairi hili  linakemea tabia mbaya ya kung’ang’ania madaraka (kuongoza) hata kama kiongozi mwenyewe aliye madarakani hawezi kuongoza, msanii/mwandishi anashauri kuwa viongozi wa namna hii ni bora wang’atuke.
Pia katika Shairi la MARUFUKU linalozungumzia viongozi madikteta wasiotaka kuuliza maoni ya wananchi (watawaliwa) viongozi wa namna hii hutaka kila wasemalo liwe,wanasahau kuwa wananchi hao wanatambua maovu wanayotendewa na dhuluma wanazofanyiwa na viongozi hao,wao husema marufuku, kama msanii  asemavyo:
                   Sitaki uone,
                   Ingawa una macho,
                   Sitaki useme,
                   Ingawa una mdomo,
                   Sitaki usikie,
                   Ingawa una masikio,
                   Sitaki ufikirie,
                   Ingawa una akili,
                   Sababu utazinduka,
                   Utakomboka,
                   Uwe mtu,
                   Hilo sitaki,
                   Marufuku.
Shairi la UNYAMA linaonyesha namna viongozi wanavyotumia vyombo vya dola kwa manufaa yao mfano,wapo wanaotumia jeshi la polisi na vyombo vingine kulinda maslahi yao kama ubeti huu usemavyo:
                   Binadamu ana vyombo,
                   Amejenga mahakama,
                   Polisi chungu nzima,
Kuadhibu “wakaidi”.
2.    UKOLONI MAMBOLEO
Ukoloni mamboleo ni hali ya nchi kuwa na uhuru wa bendera lakini maamuzi yote yanafanywa na nchi nyingine.Dhamira hii  inaonekana kuota mizizi  katika nchi nyingi hasa.Ukoloni mamboleo ni kikwazo kikubwa cha maendeleo  kwani unaathiri jamii nzima katika suala la maendeleo kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni. katika shairi la HATUNA KAULI  msanii anasema;
                   Hatuna sisi kauli,
                   Ni kwa yetu maduhuli,
                   Si umma si serikali,
Ubeti huu unaonyesha namna nchi zinazoendelea zinavyokosa msimamo kwa kuwa watoa maamuzi ni wale wanaozitawala/ mataifa ya makubwa ya ulaya.
Pia Katika shairi la TIBA ISIYOTIBU  msanii anaelezea madhara ya nchi maskini (Afrika) kutegemea nchi nyingine (Ulaya). Hali ya utegemezi huzifanya nchi hizo ziendelee kuwa chini ya utawala wa kikoloni kwa sababu ya kutegemea misaada.
Nchi nyingi barani Afrika zinazokabiliwa na matatizo kama umaskini, ujinga, maradhi, kwa hiyo misaada inayotakiwa ni ile ya kuzikomboa nchi hizo si vinginevyo.Hivyo jamii inapaswa kupiga vita ukoloni mamboleo na kujenga uchumi usiotegemezi ili kulet maendeleo.
3.    MATABAKA
Matabaka ni hali ya watu kuishi kulingana na kipato.Haya ni matokeo ya mgawanyo mbaya wa rasilimali kati ya tabaka tawala na tabaka tawaliwa.Katika  shairi la WASAKATONGE msanii anasema;
                   Wao ni wengi ulimwenguni,
                   Siku zote wako matesoni,
                   Ziada ya pato hawaoni,
                   Lakini watakomboa nini?
Katika ubeti huo msanii ameonesha kuwa masikini (wasionacho) ni wengi hivyo nguvu za ziada hutakiwa ili kuwakomboa.Aidha mshairi ameonesha namna watu hawa wanavyojituma katika kazi kwa matarajio ya kuinua kipato chao lakini tabaka tawala linawanyonya.
Pia,katika shairi la MVUJA JASHO na WALALA HOI, mshairi ameonesha namna maskini wanavyokandamizwa na kunyonywa. Amewataja kuwa ni makuli wa bandarini, mayaya, wabeba zege, wasukuma mkokoteni, wafanya kazi, wakulima, wachimba migodini, watu hawa hufanya kazi zisizolingana na pata walipatalo.
4.    UNAFIKI NA USALITI
Mshairi ameonesha namna unafiki na usaliti hasa kwa viongozi wa jamii ambapo, viongozi kujifanya waongofu kumbe vitendo vyao ni nadhaifu (viovu) kama shairi la WASODHAMBI linavyodhihirisha.
          Katika shairi la UASI mshairi amesema baadhi ya viongozi wadini kama mashehe (masharifu, mapadri, maaskofu) ni wachafu ( watenda dhambi) hivyo ni ngumu kwa kukemea maovu ya uami.
                   Uasi,
                   Katika dini,
                   Mashehe na masharifu,
                   Mapadri na maaskofu,
                   Kauli zao nadhifu,
                   Hujingamba waongofu,
                   Wengi wao ni wachafu.
                   Wenye vitendo dhaifu,
                   Wanafiki.
5.     MMOMONYOKO WA MAADILI
Sula la mmonyonyoko wa maadili linajidhihirisha katika diwani hii ambapo katika shairi la WEWE JIKO LA SHAMBA msanii anakemea tabia zinazooneshwa na baadhi ya wanawake yaani umalaya (kutembea na kila mwanaume pasipo kujali kaida zao).
Katika shairi la JIWE SI MCHI usagaji na ulawiti umekemewa ambapo mshairi ameonesha kuwa kuna watu wanahusiana kimapenzi kinyume na taratibu mathalani mahusiano ya jinsia moja,msanii anasema tabia hiyo iachwe,kama msanii asemavyo;
Achana na msagio, walao uongokewe,
Utafutwe mtwangio, jiwe halisagi jiwe,
Unga usiopanga chungio, utapikwaje uliwe,
Pia Katika shairi la UNYAMA mwandishi anaonesha kukerwa na tabia za baadhi ya watu kama vile ubakaji, ulawiti, na unajisi,kama msanii usemavyo;
                   Binadamu hana aibu,
                   Ni kawaida kubaka,
                   Wasichana kunajisi,
                   Wavulana kulawiti,
                   Mufilisi wa maadili.
Mwandishi ameonesha namna  maadili yalivyomomonyoka katika jamii hivyo anaiasa jamii kujaribu kujirekebisha au kufuata maadili ya jamii ya tangu mwanzo.  
6.    NAFASI YA MWANAMKE
Mwandisi wa diwani hii amemchora manamke katika nafasi (majukumu) mbalimbali kama ifuatavyo;.
Ø Mwanamke kama chombo cha starehe
Mwanamke anaonekana ni mtu asiye mwadilifu na Malaya,ambaye hufanya ngono na wanaume wengi pasipo kuangali madhara yake, ikiwemo kupata magonjwa ya zinaa kama vile UKIMWI.Msanii anathibitisha hili katika shairi la WEWE JIKO LA SHAMBA.
Ø Mwanamke kama msaliti
Mwanamke anaonekana ni mtu dhaifu katika ndoa yake kwa kufanya ngono na wanaume wengine nje ya ndoa, sio mwaminifu katika mapenzi, ni msaliti wa mapenzi hili limeelezwa katika shairi la USIKU WA KIZA.
Ø Mwanamke kama kiumbe dhaifu
Mwanamke anaonekana ni kiumbe dhaifu asiyeweza kujitetea dhidi ya mila potofu zinazomkandamiza na kumuumiza kama vile ukeketaji, msanii anadhihrisha katika shairi la TOHARA.
Ø Mwanamke kama mlezi wa familia
Mwanamke ndiye mwenye jukumu la kulea watoto na kuhakikisha kuwa watoto wanakula na kuenenda katika maadili mema, msanii ameeleza katika shairi la MWANAMKE.
Ø Mwanamke ni mchapakazi
Mwanamke ndiye mfanya shughuli zote za shambani na nyumbani.Katika jamii nyingi za kiafrika.Mwanamke hulima mazao,hupika,hufua,hufua nguo,huosha vyombo,hufagia na pia kazi za ofisini na viwandani. Msanii aneleza haya katika shairi la MWANAMKE.
Ø Mwanamke ni mtu muongo na mchonganishi
Mwanamke anaonekana ni mtu mwenye fitina asiyependa maendeleo bali  hutumia muda wake mwingi katika kuchonganisha watu kwa kupika na kusambaza uongo. Msanii anaelezea hili katika shairi la MAMA NTILIYE
                   “Majungu na makaango, jinsi unavyoyapika,
                   Wakazanisha na shingo, moto uzidi kuwaka,
                   Kwa uzushi na uongo, kumbe kwako umefika”.
Kwa ufupi ni kwamba wanawake ni watendaji na wazalishaji katika jamii ingawa mchango wao hauonwi na jamii. Mshairi katika shairi la MWANAMKE WA AFRIKA anawashauri wanawake waungane ili wadai haki zao kwani kuungana ndio njia rahisi ya wao kupata ukombozi wa kweli.Na cha zaidi wakubali kupata elimu katika fani mbalimbaliMwandishi anaonyesha kuwa mwanamke anapaswa kupambana ili kupinga mbinu mbali mbali za ukandamizaji na unyonyaji  ili kuleta haki na usawa katika jamii.

7.    MAPENZI
Kwa upande wa damiraya mapenzi,mwandishi ameonesha kuwa kuna aina mbili za mapenzi,ambazo ni mapenzi ya dhati (kweli), na mapenzi ya ulaghai (uongo).Katika shairi la MAHABA mshairi ameonesha kuwa mtu awapo na mapenzi ya kweli huwa tayari kufanya jambo lolote hata kama ni la hatari,mfano mtu kuwa tayari kupigwa,kutukanwa n.k ilimradi tu ampate ampendaye, kama ubeti huu usemavyo:
                   Kama mapenzi mzigo,nitikwe usinitue,
                   Lau ni pande la gogo, liache lisipasuliwe,
                   Kama mapenzi kipigo,ni radhi kinisumbuwe,
                   Unipe japo kidogo,mwenzio nijilimbue.
Katika shairi la NILICHELEWA KUPENDWA, msanii ameeleza umuhimu wa kuvuta subira kwenye mahusiano kwani papara humfanya mtu awe na mtu asiye stahiki na hivyo kuharibu penzi.
Pia katika shairi la WEWE WAJUA,msanii amehimiza mshikamano kwa wawili wapendanao na hivyo kuawataka wawe pamoja katika nyakati zote,msanii anasema;-
                   Nakupenda,
                       nawe wajua,
                   Tusitupane,
                   Tupendane,
                   Kwa salama.
Katika shairi la SI WEWE?,Mshairi anaonesha madhara ya tamaa kwenye mapenzi, msanii anawaasa watu wasiendekeze tamaa ya mali au vitu bali wawe na upendo wa kweli.
Katika shairi la PENDO TAMU msanii anaeleza kuwa penye mapenzi ya kweli maudhi hujitenga na kwamba ni jambo la muhimu kwa wapendanao kuepuka mambo yanayoweza kuliharibu pendo hilo,msanii anasema
                   Pendo lilojaa raha, ya aina peke yake,
                   Lilosheheni furaha, cheko na bashasha zake,
                   Halizuki la karaha, huo ndio mwiko wake,
                   Pendo tamu kama letu, duniani “hulikuti”.
Halikadhalika mshairi anaeleza kuwa mapenzi yasiyo ya kweli husababisha maumivu makali hasa kwa yule anayesalitiwa. Katika shairi la MACHOZI YA DHIKI msanii anasema;
                   Machozi ya dhiki yanibubujika,
                   Huku na hiliki, sana nateseka,
                   Wangu muashiki, umeadimika,
                   Wala sidhihaki, nnadhulumika.
Hivyo msanii/Mwandishi anaitaka jamii kuwa na mapenzi ya dhati ili kuepusha migogoro, migongano na maumivu kwa anayesalitiwa.
8.    MATUMIZI YA ELIMU
Mwandishi ameonesha matumizi mbalimbali ya elimu,  ameonesha kuwa kuna watu hutumia elimu kuwakandamiza wengine, pia wapo wanaotumia elimu kulipa visasi na kujinufaisha wenyewe na kuna wanaotumia elimu kuleta maendeleo kwao binafsi, jamii na hata Taifa kwa ujumla. Watu wa namna hii ndio huhitajika kwenye jamii (shairi “WASOMI”).
 UJUMBE
Mwandishi ametoa ujumbe kwamba;
Ø Matabaka ni kikwazo katika ujenzi wa jamii mpya. Ujumbe huu unapatikana katika shairi la “MVUJA JASHO”,”WALALA HOI” na “WASAKATONGE”.
Ø Unafiki na unasaliti ni chanzo cha migogoro katika jamii,ujumbe huu unapatikana katika shairi la “WASO DHAMBI”, “UASI” na “VINYONGA”.
Ø Udikteta ni kikwazo kikubwa cha maendeleo hivyo jamii hainabudi kung’oa utawala wa kidikteta. Ujumbe huu unaatikana katka shairi la “MADIKTETA”, “MARUFUKU”, “NAHODHA”, na “SADDAM HUSEIN”
Ø Kumkomboa mwanamke ni kuikomboa jamii nzima. Msanii anaitaka jamii imkomboe mwanamke dhidi ya unyanyasaji, dhuluma, unyonge na mila potofu.Ujumbe huu unaatikana katika shairi la “MWANAMKE”, “WANAWAKE WA AFRIKA”, na “TOHARA”.
Ø Heshima kwa jinsia zote ni muhimu kuzingatiwa ili kuleta usawa  wa kijinsia katika jamii, kama inavyoelezwa katika shairi la MWANAMKE.
Ø Mtaka cha uvunguni sharti ainame,ujumbe unapatikana katika shairi la “MVUJA JASHO”, na ‘PEPO BILA KIFO”.
Ø Umoja ni nguvu utengano ni udhaifu, ujumbe huu unapatikana katika shairi la ‘WANAWAKE WA AFRIKA”
Ø Uongozi mbaya hurudisha nyuma maendeeo ya jamii.Ujumbe huu unapatikana katika shairi la MARUFUKU’, “NAHODHA” na “MADIKTETA”.


 MAADILI:
Haya ni mafunzo, nasaha au ushauri unaopatikana mara baada ya kusoma kazi ya kifasihi. Malenga huyu anatoa ushauri kwa jamii yake kulingana na mazingira  waliyomo.
ü Malenga huyu anaitaka jamii yake iachane na utamaduni wa kumkkeketa mwanamke kwani hakusaidii lolote. Anasema hilo kupitia shairi la TOHARA
ü Mshairi anaishauri jamii yake kuachana na tabia ya kung’ang’ania madaraka kwani haina faida yyoyote. Hili linajidhihirisha kupitia TONGE LA UGALI na NAHODHA.
ü Vile vile mshairi anaitaka jamii yake ipige vita tabia kushiriki tendo la ndoa kinyume na maumbile na ufuska kupitia JIWE SI MCHI na WEWE JIKO LA SHAMBA.
ü Mshairi anaitaka jamii yake ifanye kazi kwa bidii na kuachana na tabia ya utegemezi kupitia shairi  KLABU.
ü Mshairi tena anaitaka jamii yake kujifunza kuwa na upendo wa kweli hasa kwa wanandoa ili kuimarisha ndoa zao kupitia mashairi ya YEYE NA MIMI, PENDO TAMU na WEWE WAJUA.
Ø FALSAFA
Mwandishi anaamini kwamba jamii yote haiwezi kuendelea kama hakuna usawa na kwamba viongozi ndio wanatakiwa kuwa mstari wa mbele katika kutetea usawa huo.Matatizo aliyoyabainisha mwandishi chanzo kikubwa ni viongozi wenyewe hivyo uongozi mbaya upigwe vita.

FANI
Ø MUUNDO
Mwandishi ametumia miundo ya aina mbalimbali kama vile;
TARBIA:Huu ni muundo wa  mistari minne kwa kila ubeti. Katika diwani hii mashairi ya mistari minne ni MCHEZA HAWI KIWETE na PENDO TAMU.
TATHILITHA: Huu ni muundo unaohusu mistari ya mitatu kila ubeti.mfano HATUNA KAULI, SIKUJUA, JAWABU LA NAHODHA.
SABILIA:Huu ni muundo unaohusu hasa mashairi yenye mistari mitano kila ubeti.mfano KOSA, NILIKESHA, WALALA HOI, NAHODHA, UNYAMA.
Ø MTINDO
Ni mbinu za pekee ambazo hutumiwa na msanii kumtofautisha na msanii mwingine. Msanii wa diwani hii ametumia mitindo mbalimbali kama vile;
 Takriri pindu,mwandishi ametumia mtindo huu katika shairi la NAHODHA, ambapo neno analomalizia mwishoni ndilo analoanzia mstari mwingine, mfano
                        Vikongwe wayayatika,
                        Yayatika, na nanga inatutaka
 Mtindo wa matumizi ya nafsi mbalimbali mfano, katika shairi la NILICHELEWA  KUPENDWA ametumia nafsi ya kwanza umoja (ni-mimi). Pia shairi la SILI NIKASHIBA mshairi ameeleza katika la NAHODHA namna uongozi ulivyo
Mtindo wa kuhoji,katika mashari ya SI WEWE? Na AFRIKA anaanza kwa swali lini? Anamalizia pia na swali lini?
Mtindo wa vidato,katika mtindo huu baadhi ya mistari na maneno yake au silabi zake zina maneno machache au zimefupishwa tofauti na mistari mingine ambayo huwa na silabi aumaneno mengi.mfano shairi la WASODHAMBI.
Kwa ufupi ni kwamba mtindo aliotumia na mshairi huyu ni wa pekee kabisa na hivyo kufanya kazi yake ilete mvuto zaidi.
Ø MATUMIZI YA LUGHA
·       TAMATHALI ZA SEMI
Mwandishi ametumia tamathali semi zifuatazo:
·       TASHBIHA
Ni tamathali ilinganishayo vitu kwa kutumia viunganishi mfano shairi la ‘Yeye na mimi’anasema ‘hubakia kama wang’a, shairi la KANSA anasema lanuka kama ng’onda na katika shairi la NILINDE anasema chanda na pete kama udi na uvumba.
·       TASHIHISI
Ni tamathali ivipavyo uwezo vitu visivyo binadamu kutenda matendo ya kibinadamu mfano katika shairi la TIBA ISOTIBU anasema “inaumwa Afrika”, bara linapewa uwezo wa kuugua kama auguavyo binadamu. Katika shairi la AFRIKA anasema “ radi yenye chereko” na shairi la YEYE NA MIMI anasema “na akili humrusha”.
·       TAKRIRI
Ni tamathali inayorudiarudia maneno mfano katika shairi la KANSA anasema “inatoa mafunza, mafunza yachomoza”,inadhoofisha siha-siha, pia kuna takriri mistari kwa baadhi ya mashairi.
·       SITIARI
Ni tamthali ambazo hulinganisha vitu pasipo viunganishi mfano katika shairi la VINYONGA anasema “wanasiasa vinyonga
·       MKATO WA MANENO
Mkato wa maneno umetumiwa katika mashairi mbalimbali mfano shairi la MVUJA JASHO maishaye” badala ya maisha yake na “ achumacho” badala ya anachochuma.
·       MJALIZO
Mwandishi ametumia kipengele hiki katika shairi la WASODHAMBI anasema
                             Wako wapi, ni wangapi?
                             Chao kipi, haki ipi, nchi zipi?
                                    Nakuwa vipi?

          TASWIRA/JAZANDA
Mwandishi ametumia lugha ya picha katika kazi yake mfano
-Shairi la NAHODHA kuna taswira (picha )ya nahodha inayomaanisha kiongozi, nanga  yenye maana madaraka,
-Shairi la WEWE JIKO LA SHAMBA linamaanisha Malaya,
-Shairi la JIWE SI MCHI taswira ya jiwe na mchi linamaanishausagaji,
-MVUJA JASHO ,WASAKATONGE na WALALA HOI linamaanisha masikini.
         
JINA LA KITABU

Jina linasadifu yaliyomo ndani ya kitabu kwa kuwa hali ya umasikini ndiyo imetawala kazi hii,watu wengi ni masikini ambao kazi zao huwapatia mlo wa siku hawatarajii kuweka akiba benki au kwenye taasisi yoyote ya kifedha.
Powered by Blogger.