Wamtaka Magufuli atimize ahadi zake
Rais mteule Dk John Magufuli
Geita. Mchungaji wa Kanisa la AIC
Kalangalala la Geita Mjini mkoani hapa, limeitaka Serikali mpya
inayoingia madarakani itimize ahadi zote walizozitoa kwa wananachi.
Imeelezwa
kuwa, baadhi ya viongozi na Serikali katika chaguzi zilizopita, walitoa
ahadi za maendeleo ambazo zingine hazijatekelezwa hadi sasa.
Akizungumza
kwenye Ibada maalumu ya kumshukuru Mungu kwa kumaliza Uchaguzi Mkuu
uliofanyika Oktoba 25 salama, Mchungaji Masanyiwa alisema Watanzania
wana tabia ya kumshukuru Mungu kwa mambo yanayowapendeza na kuacha yale
yanayowakwaza.
“Tunaambiwa tushukuru kwa kila jambo, linalotukera pia tunapaswa kupiga magoti na kumshukuru Mungu kwa hilo,” alisema Masanyiwa.
Alisema
Serikali inayoingia madarakani ina kazi kubwa ya kurudisha imani ya
Watanzania ambayo imetoweka, kutokana na hali ngumu ya maisha
inayowakabili.
Alisema inatakiwa ionyeshe utofauti wake kwa matendo siyo kwa maneno.
Mchungaji
Masanyiwa alisema maendeleo hayaletwi na Serikali pekee, bali kwa
ushirikiano na wananchi wanaojituma kwa kufanya kazi.
Akizungumzia
wagombea walioshindwa katika kinyang’anyiro hicho, aliwataka kumuunga
mkono mgombea aliyechaguliwa ili kuijenga Tanzania mpya.
Akizungumza
baada ya ibada, muumini Boniface Waika alisema kipindi cha ushindani
kimemalizika viongozi wamepatikana kilichobakia ni kwa Watanzania
kuendelea na mshikamano pamoja na kufanya kazi kwa bidii.
“Viongozi
na Watanzania kwa ujumla, tunapaswa kutambua kuwa uchaguzi umemalizika
tuendelee na maisha yetu na kwa wanasiasa nao wanatakiwa wajipange kwa
uchaguzi mkuu mwingine wa 2020, kwa sasa tufanye kazi zaidi tuweke sisa
kando,” alisema Waika .