Ushindi wa Bashe kupingwa mahakamani
Hussein Bashe
-
Nzega. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya
Nzega mkoani Tabora, kimetangaza kwenda mahakamani kupinga
matokeo yaliyompa ushindi mgombea ubunge wa CCM, Hussein Bashe.
Msimamizi
wa Uchaguzi wa Jimbo la Nzega Mjini, Hawa Mniga alimtangaza Bashe kuwa
mshindi baada ya kupata kura 18,774 dhidi ya 9,658 za Charles Mabula wa
Chadema.
Akihutubia mkutano wa hadhara ulioandaliwa
kuwashukuru wananchi kwa kukipigia kura chama hicho juzi, Mwenyekiti wa
Chadema Jimbo la Nzega Mjini ambaye pia alikuwa mgombea, Mabula alisema
uchaguzi huo haukuwa huru na haki kutokana na kasoro nyingi
zilizojitokeza, ikiwamo baadhi ya vituo kuwa na zaidi ya karatasi tatu
za matokeo.
Mabula alisema rushwa ilitawala siku ya
kupiga kura pamoja na vurugu, mambo ambayo waliyaripoti kwa mamlaka
zinazohusika lakini hazikuchukua hatua zozote.
Alisema
hivi sasa wanasheria wao wanaendelea na mikakati ya kuandaa kesi na muda
wowote itafunguliwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, lengo likiwa
haki itendeke na kila mgombea apate kura halali alizopigiwa na wananchi.
Mwenyekiti
wa Chadema Wilaya ya Nzega, Omary Omary ambaye pia ni Diwani wa Kata ya
Bukene aliwataka wananchi kuwa watulivu wakati chama hicho kinaendelea
na mchakato wa kupinga matokeo hayo mahakamani.
Omary
alisema uchaguzi huo ulighubikwa na kasoro nyingi ambazo zitaweza
kutatuliwa na mahakama na kuongeza kuwa, wananchi wanapaswa kuendelea na
shughuli zao, ikiwamo kudumisha amani na utulivu.
Msimamizi
wa uchaguzi huo alisema ulikuwa huru na haki kwa kuwa kila chama
kiliwakilishwa na mawakala na kwamba, kama kuna mgombea hakutendewa haki
afuate utaratibu wa kuipata.