TMA: Mvua za El-Nino zinakuja
Chumba
cha darasa la tatu katika Shule ya Msingi Izia, kikiwa kimeezuliwa paa
kufuatia mvua kubwa iliyonyesha jana ikiambatana na upepo mkali mjini
Sumbawanga mkoani Rukwa. Picha Mussa Mwangoka
Imeandikwa na Fidelis Butahe, Lauden Mwambona na Jesse Mikofu
-
Desktop View
Dar/mikoani. Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini
(TMA), imewatahadharisha wananchi kuwa mvua kubwa za El-Nino
zinatarajiwa kunyesha mwezi huu na Desemba, katika mikoa ya Kanda ya
Ziwa, Kanda ya Magharibi na Nyanda za Juu Kaskazini mashariki.
TMA imesema mvua hizo zinakuja kutokana na mifumo ya hali ya hewa kuzidi kuonyesha hali hiyo.
Mamlaka
hiyo imewataka wakulima, wafugaji, mamlaka za wanyamapori, mamlaka za
maji na afya kufuata ushauri wa wataalamu wa sekta husika ili kutekeleza
mipango isiyoweza kuathiriwa na mwelekeo wa hali ya hewa ya msimu wa
mvua za vuli.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk
Ladislaus Chang’a alisema jana katika taarifa kuwa maeneo yanayopata
mvua mara moja kwa mwaka ya Dodoma, Singinda, Ruvuma, Lindi, Mtwara,
Songea, Mbeya, Iringa, Njombe, Tabora, Kigoma Rukwa na Katavi
zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya pili na ya nne ya mwezi huu.
“Mvua
hizo zimeanza kujiimarisha katika mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi na
zinatarajiwa kusambaa katika maeneo mengine mwezi huu,” alisema.
Kwa
mujibu wa taarifa hiyo, wilaya za Kondoa, Kongwa na maeneo ya Singida
vijijini pamoja na Dodoma yanatarajiwa kupata vipindi vya mvua mwanzoni
mwa mwezi huu.
Alisema mvua za El-Nino zinatokana na
kuendelea kuongezeka kwa joto katika maeneo ya Bahari ya Pacific na
kusababisha mifumo mingine ya hali ya hewa kuvurugika.
Chang’a
alisema mabadiliko hayo yamesababisha mwitikio wa mfumo wa hali ya hewa
katika Bahari ya Hindi kuwa na mchango hasi, kinyume na ilivyotarajiwa
katika mwenendo wa mvua za vuli nchini kwenye kipindi Oktoba na
kusababisha vipindi virefu vya upungufu wa mvua katika mikoa ya
Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.
“Hata hivyo, mifumo
ya hali ya hewa katika Bahari ya Hindi kwenye ukanda wa Afrika Mashariki
na ukanda wa Pwani ya Angola katika Bahari ya Atlantic imeanza na
inaendelea kuimarika,” alisema.
Kaimu mkurugenzi huyo
alivitaka vyombo vya habari kufuatilia, kupata na kusambaza taarifa
sahihi za mienendo ya hali ya hewa kutoka TMA na kutumia wataalamu wa
sekta husika kuandaa na kufikisha taarifa za masuala mtambuka ya hali ya
hewa kwa jamii.
Wakati TMA ikitoa taarifa hiyo, tayari
mvua imeanza kunyesha kwa kasi ikiwa na upepo mkali katika mikoa ya
Mwanza na Mbeya na kukwamisha baadhi ya shughuli za jamii katika sehemu
hizo.
Katika mkoa wa Mbeya, mvua iliyoambatana na upepo mkali
iliyonyesha jijini hapa jana, ilisababisha kuta kubomoka na mabati ya
nyumba nyingi kuezuliwa.
Mvua hiyo ilinyesha kwa dakika
20, lakini ilikuwa na mawe ya theluji, huku ikiambatana na upepo mkali
kutoka Kaskazini kwenda Kusini.
Nyumba zlizoezuliwa mapaa ni pamoja na mabanda ya biashara ya mitaa ya Sokoine, Jakaranda na Mwanjelwa.
Katika Mtaa wa Mwambene, wigo wa nyumba mbili tofauti ulianguka huku mabati ya nyumba nyingi yakinyofolewa.
Kutoka
jijini Mwanza, mvua kubwa iliyonyesha kuanzia alfajiri ilisababisha
kufungwa kwa Uwanja wa Ndege na mwanafunzi mmoja kusombwa na maji.
Kutokana
na mvua hizo, usafiri wa kuingia na kutoka katikati ya jiji hilo
ulikuwa wa shida na kusababisha wafanyakazi wengi kuingia ofisini
kuanzia saa 4:00 asubuhi kutokana na foleni kubwa za magari zilizokuwa
barabarani.
Maeneo ya Mabatini na Kirumba ambayo
hukumbwa na mafuriko mara kwa mara yalijaa maji na kusababisha watu
kulazimika kuyachota ndani na kumwaga nje.
Mkazi wa
Mabatini, Ronaida Mtatina alisema vitu vyake vilivyokuwa kwenye kibanda
cha biashara vilisombwa na maji na vingine kulowana.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo alisema mwanafunzi wa Shule ya
Sekondari ya Nyamanoro, Zainab Shaaban (18) alisombwa na maji eneo la
Nyamanoro wakati akivuka kwenda shuleni, lakini haijathibitika kama
alifariki au la.
Meneja wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza,
Ester Madale alisema kutokana na mvua hiyo ulijaa maji na ilipotimu saa
3:00 asubuhi walilazimika kusitisha huduma za kutua na kuruka kwa ndege
hadi saa 8:00 mchana.