Kuepusha balaa, ZEC itangaze matokeo ya Uchaguzi Zanzibar
Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwamo Zanzibar ilifanya
Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, 2015. Kwa upande wa Visiwani, Wazanzibari
walipiga kura kumchagua diwani, mwakilishi, Rais wa Zanzibar, mbunge wa
Jamhuri ya Muungano na Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa kutumia Daftari
la Wapigakura la ZEC.
Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC)
imetumia matokeo ya kura za Rais katika majimbo ya Zanzibar kujumlisha
na matokeo ya majimbo ya Bara na hatimaye kumtangaza Dk John Magufuli
kuwa mshindi wa kiti cha Rais katika Uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano. Kwa uamuzi huo wa kuchukua matokeo ya majimbo ya Zanzibar
yaliyotumia Daftari la Wapigakura la ZEC na kupiga kura kwenye vituo
vilivyoandaliwa na ZEC, Tume ya Uchaguzi ya Taifa inatambua kuwa
uchaguzi uliofanyika Zanzibar chini ya usimamizi wa ZEC ni halali na
matokeo yake ni halali.
Oktoba 28, siku tatu baada ya
uchaguzi, Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha alitangaza kuwa uchaguzi
wa Zanzibar umefutwa. Alipokuwa anatangaza alikuwa peke yake. Makamu
Mwenyekiti hakuwepo. Mkurugenzi wa ZEC hakuwepo. Wajumbe wengine wa Tume
hawakuwepo. Wajumbe wa ZEC walikuwa Bwawani wakimsubiri Mwenyekiti wao.
Walijaribu kuendelea na kazi ya kuhakiki matokeo chini ya uongozi wa
Makamu Mwenyekiti. Hawakuweza kuendelea na kazi hiyo baada ya Makamu
Mwenyekiti kuondolewa na vyombo vya dola.
Sababu ambazo
Mwenyekiti ametoa za kufuta uchaguzi ni pamoja na eti makamishna wa
uchaguzi katika Tume hiyo walidundana kutokana na tofauti zao.
Makamishna walikuwa wanapendelea vyama vyao. Katika vituo vingine, hasa
Pemba, kura zilizopigwa zilikuwa zaidi ya zilizosajiliwa. Masanduku ya
kupigia kura hayakupewa ulinzi wa kutosha na mawakala pamoja na maofisa
wa uchaguzi. Mawakala wa vyama walifukuzwa katika vituo kadhaa. Vijana
walivamia vituo vya kupigia kura wakiwa na lengo la kuzua ghasia na
kadhalika.
Sababu za Mwenyekiti hazina mashiko.
Malalamiko haya yalipaswa kutolewa na mawakala wa vyama mapema. Vituo
vya kupigia kura vilikuwa na ulinzi wa kutosha wa vyombo vya dola.
Watazamaji wa ndani na nje walisifia namna upigaji wa kura Zanzibar
ulivyokuwa wa amani na utulivu.
Jecha alieleza kwamba,
“Kwa kuzingatia hayo na mengine mengi ambayo sijayaeleza, Mimi
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, nimeridhika kwamba uchaguzi
huu haukuwa wa haki na kuna ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu za
uchaguzi. Hivyo kwa uwezo nilionao natangaza rasmi uchaguzi huu na
matokeo yake yote yamefutwa na kwamba kuna haja ya kurudia uchaguzi
huu.” Mwenyekiti Jecha hakuvitaja vifungu vya Katiba na sheria
vinavyompa mamlaka ya kufuta uchaguzi.
Sura ya tisa ya
Katiba ya Zanzibar inaelezea pamoja na mambo mengine uundwaji, mamlaka
na taratibu za uamuzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar. Hakuna kifungu
chochote cha Katiba kinachoipa tume au mwenyekiti wake maamlaka ya
kufuta uchaguzi. Katiba inaeleza bayana kuwa uamuzi wa masuala yote
unafanywa na tume kwa pamoja. Kifungu cha 119(10) kinaeleza kuwa
“Kiwango cha mikutano ya Tume ya Uchaguzi ni Mwenyekiti au Makamu
Mwenyekiti na wajumbe wanne na kila uamuzi wa tume ni lazima uungwe
mkono na wajumbe walio wengi.” Mwenyekiti Jecha hakueleza kikao gani cha
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kilichokaa na kufikia uamuzi aliotangaza.
Ukweli ni kwamba Jecha amevunja Katiba ya Zanzibar kwa kutoa uamuzi
mzito bila kufuata taratibu zilizowekwa na Katiba ya Zanzibar. Uamuzi
wake ni batili na hauna nguvu ya kisheria. Katiba na sheria ya Zanzibar
hazijampa mamlaka mwenyekiti na hata tume yote kufuta uchaguzi. Kufanya
hivyo ni kuvunja Katiba ya Zanzibar.
Inaelekea
mwenyekiti amepewa shinikizo na ndiyo maana hakuwashirikisha wajumbe
wengine wa ZEC. Bila shaka waliomshinikiza Mwenyekiti wa ZEC kuvunja
Katiba watawashinikiza wajumbe wengine wa ZEC kuunga mkono uvunjaji wa
Katiba uliofanywa na mwenyekiti wao.
Athari za kufuta
uchaguzi ni kuleta vurugu za kisiasa na maafa Zanzibar na Tanzania kwa
ujumla. Kwa kuwa matokeo ya kura za Zanzibar kwa uchaguzi wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano hayaathiri ushindi wa mgombea wa CCM, matokeo hayo
yamekubaliwa. Matokeo ya kura za uchaguzi wa Rais wa Zanzibar
uliofanyika katika mazingira yaleyale na kutumia Daftari la Wapigakura
la ZEC yanakataliwa kwa sababu mgombea wa CCM ameshindwa. Mwenyekiti wa
ZEC ameshinikizwa kufuta uchaguzi wote wa Zanzibar.
Ni
wazi wananchi wengi wa Zanzibar hawawezi kukubali kurudia uchaguzi kwa
sababu wenye vyombo vya dola wameamua lazima CCM ishinde ndiyo matokeo
ya uchaguzi yakubaliwe. CCM inawaeleza Wazanzibari mabadiliko ya
Serikali hayawezi kuletwa na vikaratasi vya kura. Mapinduzi daima maana
yake lazima CCM itawale Wazanzibari wakitaka au wasitake. CCM inawaeleza
Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla kama wanataka mabadiliko aslani
hawatayapata kupitia visanduku vya kura. Watafute njia nyingine. Hili ni
jambo la hatari.
Nilidhani CCM imejifunza tangu matukio ya 2001 baada ya uchaguzi wa 2000, uchaguzi wa majimbo 16 ulifutwa na kurudiwa.
CUF
ilipotoa taarifa ya kufanya maandamano ya amani nchi nzima kudai tume
huru ya uchaguzi, Katiba Mpya yenye misingi ya demokrasia, utawala bora
na kurudiwa kwa uchaguzi wote wa Zanzibar kama ilivyopendekezwa na
watazamaji wa uchaguzi wa ndani na wa nje, mimi binafsi nilikamatwa
nikapigwa na kuvunjwa mkono na kutupwa jela. Dhahama hiyo iliwakuta
wanachama na viongozi wengine wa CUF. Wananchi wa Zanzibar walipojaribu
kuandamana Januari 27, zaidi ya watu 60 waliuawa na kwa mara ya kwanza
Watanzania zaidi ya 2000 walikimbia nchi yao kwenda Kenya kunusuru
maisha yao. Watanzania tusikubali wanaoishinikiza ZEC kuturudisha huko.
Rais
mteule wa Jamhuri ya Muungano, Dk John Magufuli ataapishwa Novemba 5,
2015 na ndiye atakayekuwa Amiri Jeshi Mkuu. Rais Jakaya Kikwete
hatamtendea haki Rais Magufuli kumwachia mgogoro wa Zanzibar ambao
anaweza kuutatua.
Uchaguzi umefanyika Zanzibar na kwa
kuzingatia matokeo kwenye vituo vyote vya wapigakura yaliyotiwa saini na
wasimamizi wa vituo na mawakala wa vyama, mgombea wa urais wa Zanzibar
kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ameshinda uchaguzi huo. Tume
ya Uchaguzi ya Zanzibar ikamilishe uhakiki wa matokeo na kumtangaza
mshindi.
Tangu mwaka 1995 sera ya CUF ni kuunda
serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar. Katiba ya Zanzibar ya 2010
imeingiza serikali ya umoja wa kitaifa kuwa sharti la kikatiba. CCM
watakuwa sehemu ya serikali ya umoja wa kitaifa. Nina uhakika kwa
uzalendo wa Kizanzibari wa Maalim Seif, ataunda Serikali ya Umoja wa
Kitaifa itakayowaunganisha Wazanzibari.
Propaganda
kubwa dhidi ya CUF ni kwamba ikipewa fursa ya kuongoza Zanzibar,
itavunja Muungano. Msimamo rasmi wa CUF ni mfumo wa muungano wa
shirikisho lenye serikali tatu ya Zanzibar, Tanganyika na Muungano kama
uliopendekezwa na Tume ya Jaji Warioba. Huu ndiyo msimamo wa CUF tangu
mwaka 1995 wakati wa uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi. Msimamo huu
ulifanana na mapendekezo ya Tume ya Jaji Nyalali. CUF inaheshimu sheria
mama ya Jamhuri ya Muungano ambayo ni Makubaliano ya Muungano.
Tume
ya Jaji Warioba ilitoa uhuru kwa Watanzania kutoa maoni kuhusu Katiba
wanayoitaka. Mjadala huu ulitoa mapendekezo mengi likiwamo la Muungano
wa mkataba. Baada ya kuchambua mapendekezo yote, Tume ya Jaji Warioba
iliandaa Rasimu ya Katiba yenye mfumo wa Muungano wa serikali tatu.
Chama cha CUF na Katibu Mkuu wake waliunga mkono mapendekezo ya Tume ya
Jaji Warioba na ndiyo sababu ya kuanzisha Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) katika Bunge Maalumu la Katiba. Wazanzibari wengi wanaoishi
Tanzania Bara wanaunga mkono CUF, lakini pia wanaelewa umuhimu na faida
za Muungano. CUF haitavunja muungano bali itauimarisha kwa kutumia njia
za demokrasia na sheria kutatua kero za Muungano.
Kufuta
uchaguzi wa Zanzibar ni kuwanyima Wazanzibari haki ya kuchagua viongozi
wanaowataka. Nikuwaeleza hawawezi kupata mabadiliko kupitia visanduku
vya kura. Watafute njia nyingine. Wanaowanyima Wazanzibari haki ya
kuchagua viongozi wao kwa utaratibu wa kupiga kura ndiyo wanaoandaa
mazingira ya kuvunja Muungano. Rais Kikwete na Rais Ali Mohammed Shein
malizeni tatizo msiliingize taifa kwenye balaa na kumuachia Rais mteule
mgogoro utakaomzuiwa kusimamia ajenda ya maendeleo ya nchi yetu.
Posted Tuesday, November 3, 2015 | by- Ibrahim Haruna Lipumba
Mwandishi wa makala haya, Profesa Ibrahim Lipumba alikuwa Mwenyekiti wa CUF