Vihunzi nane kwa Rais John Magufuli
“Mvutano
ulioko Zanzibar hauna budi upatiwe ufumbuzi na Rais Jakaya Kikwete na
endapo atakuwa hajamaliza Dk Magufuli atalazimika kubeba kijiti hicho,”
Dk Benson Bana
-
Rais mteule wa Serikali ya Awamu ya Tano, Dk John Pombe
Magufuli anakabiliwa na changamoto nane kubwa ikiwamo ya namna ya
kutatua kwa amani mgogoro wa urais wa Zanzibar ambao umeibuka, baada ya
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kusitisha mchakato wa kumtangaza
mshindi.
Wasomi na wachambuzi wa masuala ya kisiasa
wanasema mbali na changamoto hiyo inayotishia kuwaingiza wakazi wa
visiwa vya Pemba na Unguja katika uhasama wa kisiasa na kijamii, Dk
Magufuli ambaye ataapishwa keshokutwa, atakabiliwa na changamoto ya
ongezelo la Deni la Taifa, matarajio makubwa kupita kiasi kwake, Katiba
Mpya, upinzani wa kisiasa uliokomaa, ‘unafiki’ ndani ya chama tawala,
kufumua mfumo wa utendaji serikalini na kurejesha umoja.
Katika
mahojiano na gazeti hili jana, baadhi ya wasomi wametoa wito Rais
Jakaya Kikwete amalize utata huo wa Zanzibar kabla ya kuondoka ikulu
badala ya kumwachia Dk Magufuli kwani itakuwa changamoto kubwa kwake.
Urais Zanzibar
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Des Salaam, Dk Benson Bana amesema ikiwa Rais Kikwete
hatashughulikia utata huo, Dk Magufuli atakabiliwa na changamoto kubwa
kwani suala hilo linagusa Muungano.
“Mvutano ulioko
Zanzibar hauna budi upatiwe ufumbuzi na Rais Jakaya Kikwete na endapo
atakuwa hajamaliza Dk Magufuli atalazimika kubeba kijiti hicho,” alisema
Bana.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT)
Hamad Salim alisema, “Kile kinachoendelea Zanzibar bado suluhu
haijapatikana, kwa hiyo atakapoingia madarakani ana wajibu wa
kuhakikisha anamaliza tatizo hilo ili kulinda Muungano bila kuacha
dosari yoyote.”
Mgogoro wa Zanzibar umeibuka baada ya
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kuamua
kufuta matokeo yote ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25 kwa madai
zimegundulika kasoro kadhaa katika baadhi ya vituo na majimbo ya Pemba.
Jumuiya
ya Kimataifa; Ubalozi wa Marekani, Umoja wa nchi za Ulaya (EU),
waangalizi wa kimataifa, na wanasiasa nchini wameitaka ZEC kuendelea
kutangaza matokeo ya uchaguzi huo ili mshindi atangazwe. Jecha, ambaye
hakumshirikisha kamishna yeyote wakati akitoa tangazo hilo, ameshikilia
uchaguzi wote urudiwe badala ya maeneo yenye dosari.
Katiba Mpya
Changamoto
nyingine inayomkabili Dk Magufuli ni Katiba mpya. Katika kipindi chote
cha kampeni Dk Magufuli pamoja na mgombea mwenza wake ambaye ni makamu
wa rais mteule, Samia Hassan Suluhu walikwepa kuzungumzia Katiba Mpya.
Profesa
wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Gaudence Mpangala alisema suala la Katiba Mpya
halikwepeki na kwamba akitaka kutekeleza mambo aliyoahidi kwa
Watanzania hana budi kuhakikisha Katiba Mpya inapatikana.
“Ni
lazima aachane na Katiba Inayopendekezwa, arejee kwenye Rasimu ya Jaji
Warioba (Joseph, Mwanyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba) wananchi
waipigie kura upya kwa sababu huko ndipo kulikokuwa na mapendekezo
yao,”alisema Profesa Mpangala.
Alisema mapendekezo
yaliyopo kwenye rasimu hiyo ndiyo yanayoendana na hali ilivyo sasa, hata
miiko ya uongozi itafuatwa ikiwa hilo litafanyika.
Katika
hilo, Dk Magufuli atakabiliwa na changamoto ya kumaliza mchakato wa
Katiba Mpya ambayo imegawanya makundi mawili; kundi linaloiunga mkono
(CCM) na lile linaloipinga. “Je, ataamua kuendelea na Katiba iliyoligawa
Taifa katika makundi mawili au ataanza upya ili kuleta umoja wa
Watanzani?”alihoji Profesa Mpangala.
Rais Kikwete
alianzisha mchakato wa kupata Katiba mpya, lakini uliibuka mgawanyiko
baada ya Bunge Maalumu la Katiba lililokuwa chini ya Mwenyekiti Samuel
Sitta na Makamu wake, Samia kutupa mapendekezo mengi ya wananchi.
Malumbano hayo yalisababisha Katiba Pendekezwa kushindwa kupigiwa kura.
Ahadi
Changamoto
nyingine inayomkabili Dk Magufuli ni kutekeleza ahadi zake. Kwa mujibu
wa Dk Bana ili aweze kuendesha shughuli za Serikali itabidi afanye kazi
ya kuwashawishi Watanzania kuwa na utamaduni wa kulipa kodi.
“…Ameahidi
mambo mengi ambayo hayataweza kutekelezeka kama wananchi hawatalipa
kodi ambazo zitamsaidia kuendesha shughuli mbalimbali katika Serikali
yake,”alisema Dk Bana.
Profesa Damian Gabagambi wa Chuo
Kikuu cha Sokoine (SUA), alisema itabidi Dk Magufuli akabiliane na
changamoto ya ajira kwa vijana wanaohitimua elimu ngazi mbalimbali,
wakulima na ardhi. “Badala ya kujenga viwanda vikubwa, Serikali hiyo
mpya inatakiwa ijenge viwanda vidogo vitakavyokamilika mapema ili kutoa
fursa ya ajira,” alisema Profesa Gabagambi.
“Michezo pia inatakiwa kupewa kipaumbele kwani ni moja ya sekta inayotoa ajira kwa vijana,’’alisema.
Kuhusu
ardhi alisema kama walivyohidi wakati wa kampeni, wanatakiwa kufanya
hivyo ili kulinda ardhi ambayo ina rutuba kwa ajili ya kilimo kama
hifadhi za Taifa zinavyolindwa.“Wakulima wamekuwa wakiteseka kwa muda
mrefu ikifika kwenye suala ya bei ya mazao. Ni vyema kukawa na tume
itakayosimamia hilo ili kuhakikisha wakulima wananufaika na bei ya mazao
yao na siyo kuwanufaisha wafanyabiashara tu,”alisema.
Katika
kipindi chote cha kampeni, Dk Magufuli aliwapa Watanzania matarajio
makubwa kwamba atafanya mabadiliko makubwa na ya kweli. Alitoa ahadi
hizo wakati ahadi nyingi za Rais Kikwete hazijatekelezwa.
Hayo yakitekelezwa Serikali ya Awamu ya Tano itaweza
kutekeleza ahadi ya kuongeza ajira kwa vijana, kuimarisha usafirishaji,
kusambaza kwa uhakika na kwa kasi huduma za jamii hasa maji, kuanzisha
mahakama maalumu ambayo itashughulika na mafisadi, na kutoa huduma nzuri
za afya, elimu, barabara, pamoja na kuvipatia vijiji Sh50 milioni.
Deni la Taifa
Changamoto
kubwa ya pili inayomkabili Dk Magufuli ni namna ya kulikabili deni
kubwa la taifa linalokadiriwa kufikia Sh30.6 trilioni. Rais Jakaya
Kikwete alipokabidhiwa nchi deni la taifa lilikuwa Sh9.3 trilioni lakini
katika kipindi cha miaka 10 limeongezeka hadi kufikia kiasi hicho.
Chini
ya Mwalimu Nyerere uchumi ulikuwa umestawi hadi ulipoharibiwa na vita
dhidi ya nduli Iddi Amini Dada mwaka 1978/9. Baada ya vita kumalizika
Mwalimu Nyerere aliwataka Watanzania kufunga mikanda kwa miezi 18,
baadaye akasema miaka mitatu, lakini hali haikubadilika.
Nyerere
alikataa masharti ya kurekebisha uchumi yaliyotolewa na Shirika la
Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia, badala yake kazi hiyo
ilifanywa na mrithi wake Alhaji Ali Hassan Mwinyi na Tanzania ikawekwa
chini ya Mpango wa Nchi Maskini zenye Madeni Makubwa (HIPC) uliowezesha
kufutiwa kiasi kikubwa cha madeni.
Rais Benjamin Mkapa
alipoingia madarakani na kutekeleza kwa kasi masharti ya wahisani kwa
kubinafsisha taasisi za fedha, viwanda na mashirika ya umma, Tanzania
ilifutiwa madeni ya mabilioni ya shilingi, na aliondoka madarakani
akiacha Hazina ikiwa na fedha za kutosha na deni la taifa likiwa
limedhibitiwa.
Lakini sasa, Rais Kikwete anaondoka
akiacha deni kubwa, uchumi unaokua kwa asilimia 7 huku utawala wake
ukigubikwa na kashfa za ufisadi kama wa Epa, Richmond na Tegeta Escrow.
Ufisadi wa Tegeta Escrow ndiyo ulisababisha Bodi ya Wakurugenzi ya
Maendeleo ya Milenia (MCC) kusitisha msaada kwa Tanzania wa Sh992.8
bilioni.
Serikali
Changamoto
nyingine ni kufumua mfumo wa uendeshaji wa Serikali. “Hayo waliyoahidi
hata hayati Mwalimu Julius Nyerere aliahidi, Tanzania kuwa nchi ya
viwanda, yote yaliahidiwa tangu zamani. Suala ni kubadili mfumo wa
uchumi na siasa ili Tanzania iwe nchi ya kujitegemea, iwe na vyanzo
imara vya kuingiza mapato bila utegemezi kutoka nje,” alisema Profesa
Mpangala.
Wakati wa kampeni, Dk Magufuli alisema mbali
ya mawaziri wake kuapa watatia saini ili wathibitishe kuwa hawatakuwa
watendaji mizigo, wazembe, wasiowajibika pamoja na kugeuza ofisa za
Serikali kuwa vijiwe vya ‘kupiga dili.’
Katika awamu ya
kwanza ya utawala chini ya Mwalimu Nyerere kulikuwa na uwajibikaji wa
kizalendo, utiifu na hofu ya matumizi mabaya ya madaraka. Katika awamu
ya pili chini ya Alhaji Ali Hassan Mwinyi wafanyabiashara walithaminiwa
zaidi kuliko wafanyakazi, na hapo ndipo udokozi wa mali ya umma na
upigaji dili ulikithiri.
Mkapa alifumua vijiwe vingi na
ofisi nyingi za mfukoni, lakini hali ya uzembe, upigaji dili vilirejea
awamu ya nne jambo ambalo Dk Magufuli amelalamikia kipindi chote cha
kampeni.
CCM
Kipindi
cha kampeni na baada ya kushinda urais, Dk Magufuli amekuwa
akisikitishwa na usaliti wa baadhi ya wanachama. Kauli zake zinaonyesha
atapambana na aliowaita “wana CCM wanafiki” ili kukijenga chama katika
mwelekeo mpya.
Mhadhiri wa UDSM, Richard Mbunda amesema
kazi kubwa aliyonayo Dk Magufuli ni kubadilisha mfumo wa chama
hicho.“Kama CCM inataka kuendelea kubaki madarakani na isipate ushindi
mwembamba kama ilivyopata katika uchaguzi wa mwaka huu, lazima wafanye
mabadiliko…chama kimetekwa na baadhi ya makada jambo ambalo siyo
zuri,”alisema Mbunda.
Pia alisema utekelezaji wa ahadi nyingi alizotoa ni jambo la msingi bila hivyo Watanzania watamhukumu baada ya miaka mitano.
Upinzani
Tofauti
na watangulizi wake, Dk Magufuli atakakabiliwa na upinzani uliokomaa
dhidi ya Serikali ya CCM. Mwaka 1992 upinzani uliporuhusiwa rasmi
kisheria ilikadiriwa kwamba kulikuwa na asilimia 20 hivi na ulijionyesha
katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi 1995.
Upinzani
umeendelea kukua mwaka hadi mwaka na mwaka huu ulikuwa na ushindani wa
nguvu baada ya mawaziri wakuu wawili wastaafu Frederick Sumaye na Edward
Lowassa kujiondoa CCM na kujiunga na upinzani. Katika kampeni Lowassa
ambaye alikuwa mgombea urais wa Chadema na Sumaye akiwa mpambe, walitoa
upinzani mkali majimboni.
Dk Magufuli atapaswa kuwa
makini katika utekelezaji wa ahadi lukuki alizotoa vinginevyo wana CCM
wengi zaidi wanaweza kuwa wamefunguliwa minyororo na kujiunga na vyama
vya upinzani ili kutekeleza haki yao kidemokrasia.
Umoja
Kwa
mujibu wa Dk Bana, changamoto nyingine ya Dk Magufuli ni kuziba nyufa
zilizojitokeza wakati wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu. Alisema wakati wa
mchakato huo kulikuwa na makundi mengi yaliyowagawanya Watanzania
kikanda hivyo ana jukumu la kuziba nyufa hizo ili kurejesha umoja ikiwa
ni pamoja na kuendeleza mambo mazuri ambayo Rais Kikwete aliyaanza
katika kipindi cha uongozi wake.