UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI ANDISHI UTANZU: USHAIRI KITABU: MALENGA WAPYA MSHAIRI: TAKILUKI WAHAKIKI:KIDATO CHA NNE
UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI ANDISHI
UTANZU: USHAIRI
KITABU: MALENGA WAPYA
MSHAIRI: TAKILUKI
WAHAKIKI:KIDATO CHA NNE
UTANGULIZI:
MALENGA
WAPYA ni diwani mojawapo kati ya diwani
tatu zinazotumika kuwatahini wanfunzi wa kidato cha tatu na nne katika somo la
fasihi andishi. Kama alivyandika Mwalimu Mmanga katika utangulizi wake, diwani
hii hakika imesheheni mashairi mengi yenye ukwasi wa fani na maudhui
yanayojadili maswala kadhaa ya kijamii, kisiasa na kiuchumi na hivyo kuamsha
hisia za wanajamii.
FANI YA
MALENGA WAPYA:
FANI ni
ufundi au ujuzi ambao msanii wa kazi ya kifasihi anautumia katika kujenga na
kuwasilisha kazi yake. Malenga hawa wamefanikiwa kuijenga vizuri tu kazi yao
wakitumia kifundi vipengele kadhaa vya kifani na hivyo kuifanya kazi yao iwe na
mvuto.
A. MUUNDO:
Hii ni sura,
msuko, umbo au uwiano wa vipengele vyote vinavyojenga ushairi. Kuna vipengele
kadhaa vinavyotumika kama sehemu ya muundo navyo ni;
v Idadi ya mishororo:
·
Tathlitha
Huu ni ushairi wenye
mishororo mitatu kwa kila ubeti. Ushairi huu pia huitwa UTATU. Katika kazi hii
ya MALENGA WAPYA yapo mashairi kadhaa yaliyosukwa namna hii, nayo ni kama vile
PAYUKA, TUNZO, KUUNGE, UA na HALI HALISI.
PAYUKA
1. Nasikia makelele,
Ya ngoma ile ya lele,
Kuimba na kupayuka.
·
Tarbia
Ni ushairi uliosukwa kwa
mishororo minne kwa kila ubeti. Tarbia pia hufahamika kama UNNE. Kidesturi
shairi la huwa na mishororo
iliyogawanyika katika vipande
viwili. Malenga wapya nao
wameweza kuisuka kazi yao kwa kutumia muundo
huu, mashairi yanayodhihirisha
hilo ni pamoja na MAISHA NI KAMA NJIA, ULIMI,SISUMBUKIE KICHAA, NIPATIENI DAWA,
NIPATE WAPI MWINGINE na SAMAKI MTONGONI.
ULIMI
1. Ulimi ninakuasa, nisemayo usikie,
Mwenzio sijenitosa, nafasi sijutie,
Ninachokuomba hasa, unifanye nivutie,
Ewe ulimi sikia!
·
Takhmisa:
Ni ushairi wenye
mishororo mitano katika kila ubeti. Ushairi huu huitwa pia UTANO au takhmisi.
Kuna baadhi ya takhmisa hazina mgawo wa vipande viwili kama ilivyozoeleweka.
Katika kazi hii malenga hawa wametumia muundo huu pia kama inavyojidhihirisha
katika ISRAFU, SIHARAKIE MAISHA.
ISRAFU
1. Ali ulojichumia,
Ni yako nakubalia,
Lakini kiangalia,
Vipi unaitumia,
Mwenzangu nakuusia, israfu haifai.
·
Tasdisa:
Ni utungo wenye mishororo
sita katika kila ubeti. Pia huitwa USITA, TARDISA au TASHLITA. Ingawa tungo
hizi si maarufu sana lakini inaonekana katika diwani hii kama
inavyojidhihirisha kwa shairi la PUNDA.
Toka ulipozaliwa, maishayo ni kizogo,
Hujapata kuenziwa, waishi tirigivyogo,
Nawe hujajielewa, u kiumbe hu kigogo,
Kama ungefadhiliwa, usingebeba mizigo,
Hakika ulionewa, hustahili kipigo,
Haki umeitambua, idadi japo japo kidogo.
·
Sabilia:
Ni muundo ambao kazi ya
kishairi hujengwa kwa mishororo saba au zaidi kwa ubeti. Kama ilivyo kwa
tasdisa mashairi ya namna hii ni machache sana. Katika kazi ya MALENGA WAPYA
kuna mfano wa shairi la muundo huu ambalo ni PASUA UWAPE UKWELI.
Ambaye tumekuridhi, asili yetu ni moja,
Sukani tumekukabidhi, oka zama za mababu,
Cheleza lete jahazi, uwapashe wapashike,
Pasi kuwa na woga, viduhushi wachchezi,
Uyakabili mawimbi, midomo yao wafyate,
Na hizo zake tufani, virago vyao wafunge,
Zipoze bila muhali, wawafate bwana zao,
Kwa kupasua ukweli, visiwa vishuwarike,
Kutugawa kwa mafungu, neema iengezeke,
Hilo kwetu ni muhali, tufurahie maisha,
Si dini wala si rangi, au la hata kabila.
v Idadi ya vipande:
Hiki ni kigezo kingine cha kuainisha muundo wa kazi za kishairi, kwa
kigezo hiki shairi laweza kuwa na
·
Vipande
viwili ( manthawi )
Katika muundo huu
mshororo wa ubeti hugawika katika sehemu mbili; sehemu ya kwanza na ya pili.
Mashairi kadhaa katika diwani hii yamesukwa katika muundo huu, nayo ni pamoja
na ADUI, KIFUNGO, KITENDAWILI, CHARUKA,
NIPATE WAPI MWINGINE.
CHARUKA
1. Charuka chacharukaka, mambo
kuyakimbilia,
Charuka kirukaruka,
mipango kufikiria,
Charuka kikurupuka, mbali
uweze fikia,
Kabla hujapotea, charuka
chacharukaka.
·
Vipande
vitatu ( ukawafi )
Kwa muundo huu mshororo
wa ubeti wa shairi hugawika katika sehemu tatu; yaani sehemu ya kwanza, ya pili
na ya tatu. Diwani ya MALENGA WAPYA imetumia pia muundo huu kupitia mashairi
kadhaa kama vile KWA NINI?, TUNZO na HAKI.
HAKI
1. Haki watutisha, tusikuandame, kwa
matendo yetu,
Watukorofisha,
tusikuandame, kila penye kitu,
Mbona watugwisha, miba
ituchome, kwenye huu mwitu,
Tutokwe na utu!
·
Kipande
kimoja ( utenzi )
Katika muundo huu mizani
ya mishororo huwa michache kati ya 4 hadi 12 nao husimulia habari fulani au
tukio fulani. Katika diwani hii msuko huu unajidhihirisha kupitia PAYUKA.
1. Nasikia makelele,
Ya ngoma ile ya lele,
Kuimba na kupayuka.
2. Kupayuka kwenu huko,
Mbona tu kokoriko,
Sioni linalokuwa.
v Mbali ya idadi ya mishororo na
vipande pia kituo hutumika kuainisha muundo wa kazi husika. Katika hili kazi ya
MALENGA WAPYA imetumia vituo tofauti kama vile;
·
Bahari:
Kituo cha namna hii
maneno ya mshororo wa mwisho yanakaririwa kutoka ubeti mmoja hadi mwingine.
Msuko huu unajidhihirisha katika HINA INAPAPATUKA, BAHARI na HALI HALISI.
·
Nusu
Bahari:
Kituo cha namna hii
maneno ya kipande kimoja hukariririwa ubeti mmoja hadi mwingine wakati ya
kipande cha pili hubadilikabadilika. Muundo huu umejitokeza katika shairi la
CHARUKA.
·
Kimalizio:
Katika kituo cha namna hii mshororo
wa mwisho hubadilikabadilika kutoka ubeti mmoja hadi mwingine. Muundo huu
umetumika vilivyo katika diwani hii hasa katika mashairi ya NINI WANANGU?, UTANIKUMBUKA, SOKOMOKO
BAHARINI.
B: MTINDO:
Ni tabia ya
kiutunzi au mbinu za kifasihi za kiutunzi ambazo huhitilafiana kati ya mtunzi
na mtunzi.Katika kazi hii ya MALENGA WAPYA washairi hawa wametumia mitindo
tofauti ambayo imekuwa ni kivutio kwa kazi hii mbele ya macho ya wasomaji na
hivyo kurahisisha ufikishwaji wa maudhui. Mitindo hiyo ni pamoja na;
·
Kikufu:
Ni tabia ya kiutunzi
ambapo neno la mwisho au kipande cha mwisho katika kituo cha ubeti uliotangulia
linakuwa neno la kwanza au linaanzisha mshororo wa ubeti unaofuatia. Mtindo huu
unajidhihirisha katika shairi la SAMAKI MTUNGONI, MAJONZI. Angalia kikufu kinavyojitokeza katika SAMAKI MTUNGONI
1. Kaburi tunaliacha, nyuma twaligeukia,
Mwenzetu tumeshamuacha,
na dongo kumfukia,
Hakuna aliyejacha, sote
tukajiukia,
Huzuni imetukumba, mwenzetu katangulia.
2. Mwenzetu katangulia, Mola atamjalia,
Pema atajikalia, dua
tunamuombea,
Nasi tutafuatia, njia
aliyokwendea,
Huzuni imetukumba,
mwenzetu katangulia
·
Kikwamba
( Takriri ):
Ni tabia ya kurudiarudia
neno/ maneno katika nafasi maalum katika mshororo katika ubeti. Mtindo huu
unaonekana katika shairi la CHARUKA.
3. Charuka ndugu usome, uijue na dunia,
Charuka kaka kiume, mambo
usijekosea,
Charuka dada kwa shime,
vitabu kuvipekua,
Safari yaendelea, charuka
chacharukaka.
·
Kidato:
Ni mbinu ambayo mshororo
mmoja aghalabu wa mwisho hufupishwa kwa sababu maalum. Mashairi ya ULIMWENGU,
MPAKA LINI? na KWA NINI? yametumia mtindo huu na hivyo kuonesha upekee wa kazi
hii. Chunguza ubeti huu wa MPAKA LINI?
1. Jamani mambo gani haya,
mnayotufanyia?
Tena bila ya huruma,
mnaturembea,
Tumebaki twalalama, shida
twajionea,
Mpaka lini mtatukemea?
·
Maswali:
Ni mtindo ambao mshairi
huandika shairi katika hali ya kuhoji jambo Fulani. Mbinu hii imejitokeza na kutumika
katika mashairi kama KWA NINI?, NIPATE WAPI MWINGINE? Hebu pitia ubeti huu wa
KWA NINI?
1. Wanaume, nauliza, mwafanyani?
Paka shume, jigeuza, ni
kwa nini?
Mungurume, chezacheza,
majiani,
Kwa nini?
·
Taabili:
Ni mbinu ya uandishi ambao
shairi huandikwa katika namna ya kumlilia mtu au kuomboleza aliyefariki.
Uandishi unajitokeza katika shairi la NIPATE WAPI MWINGINE?, MAJONZI. Chunguza
ubeti huu wa shairi hili la MAJONZI.
1. Asubuhi na mapema,habari nimepokea,
Halikuwa jambo jema, nililolitarajia,
Ujumbe uliosema, Fulani
amejifia,
Huzuni imetukumba,
mwenzetu katangulia.
·
Tabdili:
Huu ni mtindo ambao
mshororo mmoja unakuwa mrefu kuliko mishororo mingine katika beti zote.
Mashairi ya ISRAFU na SIHARAKIE MAISHA. Angalia ubeti huu wa shairi la
SIHARAKIE MAISHA.
1. Nakuona waduwaa,
Maisha kuyashangaa,
Husuda zinakujaa,
Kuhusudu walojaa,
Siharakie maisha, nawe
una fungu lako.
·
Mtirirriko:
Ni mtindo ambao vina vya
mwanzo na vya mwisho vinakaririwa kutoka ubeti mmoja mpaka mwisho wa shairi,
vinakaririwa katika shairi lote. Mfano wa mashairi ya mtiririko ni MAISHA NI
KAMA NJIA, SISUMBUKIE KICHAA, NINI WANANGU? Hebu angalia vina vya kati na
mwisho katika beti hizi mbili za SISUMBUKIE KICHAA
1. Kichaa kusumbukia, sumbuko usisumbuke,
Jambo hilo zingatia,
maoni yangu ushike,
Kichaa ana udhia, utajuta
mwisho wake,
Sumbuko usisumbuke,
kusumbukia kichaa.
2. Kichaa hana sheria, katika maisha
yake,
Kila litomzukia, hilo
ndilo sawa kwake,
Hata kama akasema, jukumu
limuepuke,
Sumbuko usisumbuke,
kusumbukia kichaa
·
Ukara:
Ni tabia ambayo vina vya
kipande kimoja vinabadilikabadilika wakati vya kipande kingine vinakaririwa
ubeti mmoja hadi mwingine katika shairi zima. Mashairi kama NIPATE WAPI
MWINGINE?, UA, KUUNGE. Chunguza kwa makini
vina vya kai na mwisho vya beti hizi mbili za shairi la KUUNGE.
1. Sing’ang’anii kuunge, nikaja
nikaanguka,
Japo kutoa varange, katu
sitababaika,
Nakataa kuwa pange, name
naweza tumika.
2. Silipandi asilani, gogo lililokauka,
Naraduwa kuwa chini, japo
nitahangaika,
Munaosema semeni, kisha
mutapumzika.
·
Ukaraguni:
Ni mtindo ambao vina vya
mwanzo na vya mwisho vinatofautiana katika beti katika shairi zima. Ukaraguni
unajitokeza sana katika kazi hii kupitia mashairi haya; NIPATIENI DAWA, TUYAZINGATIENI
HAYA, SAMAKI MTUNGONI, ADUI, KITENDAWILI. Hebu chunguza tena beti hizi mbili za
shairi la KITENDAWILI.
1. Jogoo lina mafamba, linatamba
kiamboni,
Kwakiburi lajigamba, hadi
kiambo jirani,
Hili jogoo la shamba,
sasa lawika mjini,
Kitendawili na tega, mteguzi
ategue.
2. Mbawa linavyozipiga, wengine
hawasogei,
Shuti nejawa na woga,
wote wamekuwa hoi,
Kama wenyewe mwafuga,
kitoweo halifai,
Kitendawili na tega, mteguzi ategue.
C: MATUMIZI
YA LUGHA
Lugha ndiyo
malighafi kuu ya fasihi na ushairi,utamu na ubora wa ushairi hutegemea mtunzi
anavyomudu kuchagua na kupanga maneno yake ili yalete matokeo ambayo
ameyakusudia kwa hadhira yake. Kwa jinsi hii ni lazima mshairi awe na msamiati
wa kutosha.
Ø Uteuzi wa msamiati/ maneno:
Katika eneo hili washairi wamejitahidi kuteua na kutumia maneno katika
jinsi ambayo kazi nzima inaleta mvuto katika macho na masikio ya hadhira yake
kwani wametumia Kiswahili fasaha kinachoeleweka miongoni mwa wasomaji ingawa
imejengwa kisanaa.
Ø Mpangilio wa maneno:
Hata katika mpangilio wa maneno washairi hawa wamejitahidi kuzingatia
taratibu za kishairi ambapo maneno hupangwa ili kuleta maana fulani
iliyokusudiwa, urari Fulani wa mizani.
PAYUKA
Kupayuka kwenu huko,
Mbona tu kokoriko,
Sioni linalokuwa.
Ø Tamathali za semi:
Ni umithilishaji wa jambo kwa kulinganisha au kufanianisha na lingine. Ni
viwakilisho kwa dhana nyingine au zinazofanana. Maranyingi tamathali zinaweza
kupanua, kupuuza ama kubadilisha maana za wazi ili kuleta maana maalum katika
ushairi.
Pia hutumika kuipa mvuto kazi ya kishairi.
Katika kazi hii tamathali zifuatazo zimetumika kwa malengo hay ohayo;
·
Tashbiha:
Hii uhusisha mfananisho
au mlinganisho wa vitu viwili au zaidi kwa kuzingatia sura,sifa au tabia kwa
kutumia maneno ya ulinganisho. Matumizi ya tashbiha yanajidhihirisha katika
NIPATE WAPI MWINGINE, NINI WANANGU,BAHARI, ADUI.
NIPATE WAPI MWINGINE
4. Njiwa ali maridadi, kwa tabia hana shaka,
Na hakuwa mkaidi, umwitapo kakufika,
Mfanowe kama radi,
chini inapoanguka,
Njiwa ameshanitoka, nipate wapi mwingine.
·
Sitiari:
Hii ni tamathali ambayo
athari zake hutegemea uhamishaji wa maana na hisikutoka kitu kimoja au dhana
moja hadi nyingine.Kwa kawaida vitu hivyo vinavyohusishwa havina uhusiano wa
moja kwa moja. Sitiari ni picha ingawa picha si lazima picha iwe sitiari.
Kazi ya MALENGA WAPYA imetumia vilivyo
tamathali hii ya emi kama inavyojidhihirisha katika KITENDAWILI, ULIMWENGU,
MAISHA NI KAMA NJIA, PUNDA, SAMAKI MTUNGONI.
ULIMWENGU.
4. Umbile vile lilivyo,ni umbo la mitihani,
Usilendeshe vilivyo, litakupa hamkani,
Ambaa hebu rudivyo, ulimwengu ni shetani,
Ulimwengu.
·
Tashhisi:
Tamathali ambayo vitu
hupewa sifa zote au baadhi ya sifa za binadamu na kuonekana kutenda kama
binadamu. Tamathali hii pia imetumika katika diwani hii hasa katika mashairi
haya; ULIMI, SAMAKI MTUNGONI,
ULIMI
1. Ulimi ninakuasa,nisemayo usikie,
Mwenzio sije nitosa,
nafasi sijijutie,
Ninachokuomba hasa,
unifanye nivutie,
Ewe ulimi sikia!
·
Takriri:
Ni marudiorudio ya sauti,
neno, silabi au sentensi ili kuweza kuleta athari na maana iliyokusudiwa iliyo
maalum kwa msikilizaji na msomaji. Njia hii huonesha uzito wa hisia, kusisitiza
jambo au dhamira Fulani. Mashairi kama PAYUKA na CHARUKA yanadhihirisha
matumizi ya tamathali hii katika diwani hii.
CHARUKA
1. Charuka chacharukaka, mambo
kuyakimbilia,
Charuka kirukaruka,
mipango kufikiria,
Charuka kikurupuka, mbali
uweze fikia,
Kabla hujapotea, charuka
chacharukaka.
Ø Matumizi ya lugha ya picha/ taswira:
Haya hupambanuliwa na na uteuzi na utumizi mzuri wa maneno, ulinganifu na
udhahiri wa maelezo wenye kuhusisha na kujumuisha dhana mbalimbali tofauti
ndani ya dhana moja ili kuleta taswira na athari maalum katika mawazo ya
msikilizaji.
Taswira huundwa au kujengwa kutokana na matumizi ya tamathali za semi
hasa sitiari na tashbiha na ishara mbalimbali zenye kuhusu mawazo, dhana, vitu
na umbile na kadhalika.
Diwani ya MALENGA WAPYA imetumia taswira kadhaa kwa lengo la kuchochea
hisia za wasomajiza uoga, furaha, kilio hasura hata kukarahishwa. Nazo ni kama
vile;
·
Samaki
: katika shairi la SAMAKI MTUNGONI ambapo washairi wanawazungumzia raia
wanyonge wanokandamizwa na mfumo mbaya uliopo ndani ya jamii yao.
1. Samaki hufurahika, wawapo kwao
ziwani,
Si ziwani patashika, bali
hata baharini,
Wacheza warukaruka,
hufika hadi hewani,
Leo wako mtungoni, huzuni
imewakumba.
·
Punda:
katika shairi la PUNDA ambapo pia malenga hawa wanmzungumzia raia wa hali chini
ambaye amekuwa akiishi maisha duni tangu kuzaliwa kwake akifanya kazi nzito na
ngumu.
1. Toka ulipozaliwa, maishayo ni kizogo,
Hujapata kuenziwa, waishi
tigirivyogo,
Nawe hujajielewa, u
kiumbe hu kigogo,
Kama ungefadhiliwa, usingebeba
mizigo,
Hakika ulionewa,
hustahili kipigo,
Haki umeitambua, idadi
japo kidogo.
·
Ua:
katika shiri la UA ambapo washairi hawa wanazungumzia mwanamke mrembo
aliyetunzwa akatunzika anayevutia macho ya wanaume waloho.
1. Ua limejituliza, mtini laning’nia,
Mwenyewe laniliwaza,
furahani lanitia,
Ua sasa limepea, macho
walikodolea.
·
Mshumaa
na giza: katika shairi la HALI HALISI washairi hawa wanazungumzia hali ya kukua
kwa uchumi na kuongezeka kwa ugumu wa maisha kunakowakabili wananchi.
1. Hali hii yashangaza, nasi imetulemaza,
Imekuwa miujiza, yafaa
kujiuliza,
Mshumaa unawake, giza
mbona linazidi?
·
Sukari:
katika shairi la SUKARI ambalo washairi wanazungumzia utamu wa madaraka kwa
viongozi hata wansahau wajibu wao na kutenda yasiyofaa.
9. Si mapenzi asilani, haifai fikiria,
Utakuwa unabuni, hilo
ukiliwazia,
Bali iko mafichoni, kazi
kwako kufichua,
Kitendawili tegua,
kishindwa tanipa mji.
·
Nahodha:
katika shairi la SOKOMOKO BAHARINI ambalo washairi wanazungumzia kiongozi au
viongozi wanaoyumba kwenye madaraka.
2. Manahodha waminifu, sasa waanza
ghumiwa,
Tena walo watiifu, sukani
kuaminiwa,
Mawimbi yawatlifu, sasa
wachanganyikiwa,
Vipi hali itakuwa, kwetu wenye
vimashua?
MAUDHUI YA
MALENGA WAPYA:
Maudhui ni
mawazo yanayozungumzwa na msanii wa kazi ya kifasihi pamoja mtazamo wa
mwandishi au msanii juu ya mawazo hayo.
A. DHAMIRA:
Ni wazo kuu lililomo katika kazi ya kisanaa. Huu ni msukumo alionao
mwandishi hata akaandika kazi Fulani ya kifasihi. Mshairi anaweza kuwa na lengo
la kuonesha mambo mbali mbali- mienendo mizuri na mibaya- yatokeayo katika
jamii.
Katika diwani hii washairi hawa wameyachora kadhaa yatendwayo na jamii,
nayo ni kama;
Ø Unyanyasaji na uonevu:
Hili ni moja ya mienendo isiyo ya kiutu inayotendwa na wanajamii.
Washairi wamejadili hili kwa kina katika mashairi yao ya PUNDA, HAKI, na SAMAKI
MTUNGONI.
3. Hawajui la kufanya, wabaki
kutazamana,
Mvuvi kawakusanya,
tungoni wanaminyana,
Na nyumbani kuwafanya,
kitoweo cha mchana,
Leo wako mtungoni, huzuni
imewakumba.
Ø Kudharau wakulima:
Jambo lingine ambalo limekuwa ni kero kwa washairi hawa hata wakaamua
kuliandikia ni kuwadharau wakulima ingawa wamekuwa wakifanya kila juhudi
kuliinua taifa kwa kazi zamikono yao. Hili limewekwa wazi kupitia shairi la MKULIMA.
1. Si leo toka zamani, mkulima mtu duni,
Ana tabu maishani, tena
hapewi thamani,
Yafaa tutizameni, kisha
tuyachunguzeni,
Si leo toka zamani ,
mkulima mtu duni.
Ø Usaliti na ulaghai katika ndoa;
Malenga hawa wanaichora jamii hususan akina baba kuwa wamekosa uaminifu
kwa wenzi wao wa ndoa na hivyo kuhatarisha uimara wa ndoa na familia zao.
Malenga wanatoa kilio chao kupitia shairi la UTANIKUMBUKA na KWA NINI?
4. Mke wake, atamwacha, singizini,
Atoroke,parakacha,
migombani,
Kumbe kake, anakocha, mwa
jirani,
Kwa nini?
Ø Matumizi mabaya ya mali;
Jambo hili pia limewakera vilivyo washairi hawa hata kuamua kulipigia
kelele vilivyo; wanajamii wengi wamekuwa wakitumia walichovuna na kupata ovyo
bila kufikiria siku zijazo itakuwaje. Hili wamelisema vilivyo kupitia shairi la
ISRAFU na KWA NINI?.
5. Huu ni wakati wako,
Kuijenga kesho yako,
Kuepuka chokochoko,
Za hao adui zako,
Mwenzabgu nakuusia,
israfu haifai.
Ø Ukosefu wa uwajibikaji:
Hili pia ni jambo liwezalo kuleta madhara makubwa kwa wanjamii hasa
inapotokea viongozi katika ofisi au wenye madaraka kushindwa kubeba majukumu
yao na kuendekeza mambo yasiyo na umuhimu kwa jamii. Washairi wanaliona hili
hasa maofisini ambako watumishi wengi wa ofisi hawatimizi maukumu yao ipasavyo
kama wanavyosema katika shairi la PUUZO, MPAKA LINI? Na PAYUKA. Angalia jinsi
washairi wanvyolia katika PUUZO;
1. Ofisini ukifika, wanajitia pirika,
Haja unayoitaka, mwenyewe
tahangaika,
Wanajifanya hawajali.
Ø Kulewa madaraka:
Ni tabia nyingine ambayo imekuwa kero kwa wanajamii. Tabia ya kulewa
madaraka na majukumu na kusahau kabisa unalopaswa kufanya. Washairi wnawalaumu
viongozi kwa kukaa madarakani kwa muda mrefu hata kujisahau kutimiza majukumu
yao. Washairi wanalisema hili kupitia shairi la SUKARI.
6. Waone wanaokula, vibaya kwa mazoea,
Sasa wameanza lala, kwa
mshangao kuwangia,
Humaliza zao hila, taabu
kuiondoa,
Lishalo kujigandia,
kupapatua ni mambo.
Ø Hali ngumu ya maisha, njaa na
umaskini:
Washairi pia wametoa sauti yao ya maumivu makali kuhusu hali ngumu inayowakabili wanajamii
wanaowandikia, na hivyo kuwataka wanajamii kuamka kupambana na hali hiyo
vinginevyo jamii inatafuta mauti. Washairi wanalia vilivyo kupitia TUYAZINGATIE
HAYA, HALI HALISI na ADUI. Angalia wanachokisema katika shairi la ADUI.
2. Tulime jamatulime, tushinde adui
njaa,
Hapa kwetu ituhame,
kwengine kutokomea,
Wala sisi tusikome,
chakula kujilimia,
Tutie jembe
mpini,tuteremke shambani.
Ø Kutotendeana mema:
Nalo ni jambo lingine ambalo lililowashughulisha washairi hawa na kuamua
kulipigia nduru kwani inakera mno kuona wanajamii wakishindwa kusaidiana na
kukirimiana kama inavyotakiwa. Hili linajidhihirisha vilivyo katika shairi la
MAISHA NI KAMA NJIA.
3. Iweze yako saduri, binadamu zingatia,
Kaa ukitafakari, utende
yalo sawia,
Ubabe au kiburi,
havitokusaidia,
Maisha ni kama njia,
tukumbuke akhiria.
Ø Unyanyasaji wa wanawake:
Mwenendo mwingine uliowakera washairi hawa hata kuamua kuiandikia jamii
hili ijitambue ni tabia ya kuwanyanyasa wanawake na kuwanyima fursa za kufanya
vitu vya kimaendeleo kama wafanyavyo wanaume nadni ya jamii. Hili wamelijadili
sana katika mashairi ya HINA INAPAPATUKA na KIFUNGO.
2. Zamani tukikumbuka, watiaji walivia,
Nyumbani katu
kutoka,ndani walijichimbia,
Mabwana walitamka,
marufuku kutembea,
Unyonge inaondoa, hina
inapapatuka.
Ø Ufuska na umalaya:
Washairi pia wanaguswa sana na tabia ya ufuska na umalaya inayofanywa na
akina dada wengi mijini. Tabia hii mbaya huwafanya akina dada kukosa heshima
miongoni mwa jamii kwani inawadhalilisha sana na kuwafanya waonekane si mali
kitu mbele ya macho ya watu. Pitia beti hizi za shairi la KUUNGE
3. Kuunge limeshaoza, lote linatukusika,
Silione limekaza, mizizi
haikushika,
Kilipanda sitoweza,
hadharani natamka.
4. Nayakataa maafa, wenzangu
yalowafikia,
Waliofanya dafafa,
kidhani watatajika,
Hawapo wameshakufa, na
juu hawakufika.
5. Nawambia silipandi, hii pingu
naiweka,
Naogopa sina kundi,
nikifa la kunizika,
Nawapande kina bundi, na
kila anayeruka,
Silipandi kataani.
B: MAADILI:
Haya ni
mafunzo, nasaha au ushauri unaopatikana mara baada yakuiptia kazi ya kifasihi.
Ni maelekezo ambayo huelekezwa kwa hadhira ili iweze kutoka katika hali iliyomo
na kuelekea kwenye jamii mpya yenye Maendeleo na utengemano. Katika hili washairi
hawa wameitaka;
Jamii
kuachana na tabia ya uvivu na utegezi na
kuwa wachapakazi ili kuunua uchumi wa nchi na maisha ya jamii kwa ujumla. Hili
limesisitizwa vizuri kupitia mashairi ya TUYAZINGATIE HAYA, CHARUKA na ADUI.
Hebu chunguza ubeti huu wa shairi la ADUI.
1. Haya shime tuitane, sote
tushirikiane,
Wala tusitegeane, kwa
pamoja tushikane,
Aliye mwoga anene, kabisa
tusigombane,
Tutie jembe mpini, tuteremke
shambani.
Pia wanaume
walio katika ndoa kuachana na tabia ya uasaliti wa ndoa zao kwani kwaweza kusababisha
maafa makubwa kwa wanafamilia. Washairi wanashauri hili kupitia shairi la KWA
NINI? Wanapohoji sababu hasa wanaume kuchepuka.
2. Utamwona, mwanaume, kashaini,
Anong’ona, na Selume,
chochoroni,
Ndio laana, ajipime,
japatani?
Kwa nini?
Hali
kadhalika malenga hawa wameielekeza jamii yao hasa viongozi kuacha kukandamiza
na kuonea raia. Washairi wanashauri hili kupitia mashairi ya HAKI, MPAKA
LINI?na SAMAKI MTUNGONI. Angalia ubeti huu katika MPAKA LINI?
3. Mpaka lini, dhiki hii itafishwa?
Hadi lini, mnyonge
atadunishwa?
Jambo hili, halina budi
kukomeshwa,
Mpaka lini tutasemewa?
Vile vile
washairi hawa wameelekeza wanajamii waache majungu, umbeya na kusengenyana
kwani hakuna faida yoyote kwa kufanyiana hayo ispokuwa kujenga uadui na chuki miongoni
mwa wanajamii. Wanashauri hilo kupitia shairi la ULIMI
Usiropokeropoke, kwa
wenzio kwanza sema,
Usipachikepachike, maneno
yasio mema,
Useme wanufaike, kwa
kauli yako njema,
Ewe ulimi sikia!
Isitoshe
washairi hawa wamewashauri wanajamii wawe na misimamo hivyo waachane na tabia
ya kuiga matendo ya watu wengine na ambayo hayana maana yoyote wala msaada kwao
kwani yaweza kusabababisha maafa makubwa kwao. Ushauri huu unasomeka vizuri
katika mashairi ya SIHARAKIE MAISHA na USIWE BENDERA. Angalia ubeti huu katika
shairi la USIWE BENDERA.
2. Usione haya, baya kukataa,
Ingawaje baya,
ukajibobea,
Ukambiwa haya,
ukajifanyia,
Usiwe bendera, kufata upepo.
Kama vile
haitoshi, malenga hawa wamewaelekeza viongozi kutolewa madaraka na kusababisha kushindwa
kutimiza majukumu yao na kusababisha jamii kuendelea kuwa duni. Maelekezo hayo
yanaonekana vizuri katika shairi la SUKARI.
3. Utaumbuka ujue, sukari kiizoea,
Hukufunga utambue, utamu
ukikukaa,
Lazima usijijue,
ukishailafukia,
Haifai kubugia, sukari uiogope.
Wanajamii
pia wanapaswa kuwa makini na matumizi ya mali na pesa wanazojichumia ili ziweze
kuwafaa siku za mbeleni badala ya kuzitumia ovyo bila sababu maalum. Maelekezo
haya yanapatikana vizuri katika shairi la ISRAFU.
4. Israfu ikimea,
Mali inayoyomea,
Watu watakuzomea,
Ukikosa egemea,
Mwenzangu nakuusia, israfu haifai.
Pia
wanajamii wanaelekezwa kuwathamini wakulima wakikumbuka mchango wao mkubwa
wanaoutoa kwa jamii wa kuhakikisha jamii inapata chakula na pesa nyingi tu za
kigeni na hivyo kusukuma maendeleo ya jamii badala ya kuwatenga na kuwaona kama
watu duni waiostahili lolote. Haya yanaonekana kati ka shairi la MKULIMA.
5. Dharau wakielewa, kuna hatari
mbeleni,
Mkulima ang’amuwa, naye
akae mjini,
Hapo ndipo tutajua,
mkulima naye nani,
Mkulima naye mtu, yafaa kuthaminiwa.
C: UJUMBE
Ni taarifa
anazotoa msanii kwa hadhira; ujumbe mara nyingi hutokana na dhamira na unaweza
kujitokeza wazi au kwa kujificha.
Katika
diwani ya MALENGA WAPYA mshairi anatoa ujumbe ufuatao;
ü Kutumia mali ovyo ni hatari kwa siku
za usoni. Washairi wanayasema haya kupitia shairi la ISRAFU.
ü Ulevi wa madaraka husababisha
kushindwa kutimiza majukumu ya kuwatumikia wnanchi. Hili linasemwa katika
shairi la SUKARI.
ü Umbeya, majungu na fitina ni chanzo
kikubwa cha mafarakano ndani ya jamii. Hili nalo limesemwa sana kupitia shairi
la ULIMI.
ü Moja ya vyanzo vya migogoro katika
ndoa kutokuwa mwaminifu katika ndoa. Hili limewekwa wazi kupitia shairi la KWA
NINI?
ü Uhumi wa nchi yoyote ile hauwezi
kukua kwa nchi kuwa tegemezi au wananchi
wake kuwa wavivu, haya yanaonekana vizuri katika mashairi ya TUYAZINGATIE HAYA
na ADUI.
ü Kukosa msimamo na kuiga maisha ya
watu wengine kwaweza kusababisha matatizo ndani ya jamii. Washairi wanayasema
haya kupitia mashairi ya SIHARAKIE MAISHA na USIWE BENDERA.
ü Kukandamiza na kuonea raia ni kukua
demokrasia ndani ya jamii. Ujumbe huu unapatikana vizuri kupitia mashairi ya
MPAKA LINI?, HAKI na SAMAKI MTUNGONI.