MAENDELEO YA KISWAHILI



Katika karne ya kumi na tisa Afrika Mashariki iliingia kwenye mahusiano na mataifa mengine kama vile Marekani, Ujerumani na Uingereza. Mahusiano haya ni baada ya watu wa pwani kuwa na uhusiano wa muda mrefu wa kibiashara na Waaarabu, hawa waliweka athari kubwa katika kukua na kuenea kwa lugha ya Kiswahili. Wageni kutoka Ulaya walipoingia Afrika Mashariki walifanya biashara, shughuli za kidini (mishenari), elimu na utawala. Kama ilivyokuwa katika kipindi cha Waarabu, uwepo wao pia ulikuwa na athari katika maendeleo ya lugha ya Kiswahili Afrika Mashariki na kwingineko.
Ukuaji wa Kiswahili Kimsamiati nchini Tanzania katika Enzi ya Waarabu
Elezea ukuaji wa Kiswahili kimsamiati nchini Tanzania katika enzi ya Waarabu
Waarabu hasa katika pwani ya Afrika Mashariki walifanya biashara ikiwemo biashara ya watumwa. Ilikuwepo misafara mbalimbali ya biashara kutoka pwani hadi bara. Katika misafara hiyo Kiswahili ndio ilikuwa lugha ya mawasiliano hivyo Kiswahili kikaenea pia katika sehemu za bara.
Kuna mambo kadhaa waliyofanya waarabu ambayo yalichangia kukua kwa lugha ya Kiswahili. Waarabu walichangia kukua kwa lugha ya Kiswahili kama ifuatavyo:
Biashara
Waarabu walifanya biashara kati ya pwani na sehemu za bara, katika biashara yao walichangia kwa kiasi kikubwa uenezaji wa lugha ya Kiswahili. Lugha kuu ya mawasiliano na ya kibiashara iliyotumiwa na wafanya biashara wa kiarabu ilikuwa ni Kiswahili, kwa hiyo kwa njia hii waliweza kueneza Kiswahili kuanzia pwani hadi maeneo ya bara kama vile Tabora, Kigoma hadi mashariki mwa Kongo.
Dini
Dini pia ni jambo ambalo liliweza kuchangia ueneaji wa lugha ya Kiswahili enzi za waarabu. Waarabu walipokuja walitaka kueneza dini yao kwa undani kabisa. Kwa hivyo iliwabidi kuanzisha madarasa ambayo walitumia kufundishia, lugha iliyokuwa ikitumiwa ni lugha ya Kiswahili. Na hivyo hii ikasaidia kuenea kwa lugha ya Kiswahili.
Maandishi ya kiarabu
Waarabu pia walileta hati zao zilizotumiwa katika maandishi ya lugha ya Kiswahili. Kwa hiyo kupitia hati za kiarabu maandishi mbalimbali ya lugha ya Kiswahili yaliweza kuhifadhiwa, hivyo Kiswahili kiliweza kukua kwa vile kingeweza kuhifadhiwa katika maandishi na kusomwa wakati wowote.
Kuoana
Pia vilevile Waarabu waliofika pwani waliweza kuoana na wabantu, hii ilisababisha kizazi kipya kutokea. Na kwa sababu hiyo watoto walichukua maneno mengi kutoka kwa baba na mama yao na hivyo kuongeza msamiati katika lugha Kiswahili.
Ueneaji wa Kiswahili nchini Tanzania katika Enzi ya Waarabu
Elezea ueneaji wa Kiswahili nchini Tanzania katika enzi ya Waarabu
Waarabu walieneza Kiswahili nchini Tanzania kupitia biashara, kuoana na wabantu au wenyeji wa pwani, kupitia dini na maandishi ya hati za kiarabu ambayo yalitumika kuhifadhi maandishi mbalimbali ya lugha ya Kiswahili.
Powered by Blogger.