Lugha Kama Kitambulisho: Changamoto ya Sheng Nchini Kenya
Nordic Journal of African Studies 16(3): 320–332 (2007) Lugha Kama Kitambulisho: Changamoto ya Sheng Nchini Kenya KITULA KING’EI Kenyatta University, Kenya1 Na JOHN KOBIA Western University, Kenya2 ABSTRACT The paper takes a critical look at the fast developing and spreading Kenyan street slang, popularly known as “Sheng”, which basically is a youth code that makes use of coined or borrowed words from Kiswahili, English and other local languages. Sheng adopts the structure of Kiswahili syntax. After tracing the historical origins of the urban youth code which now has speakers in the country side and as far afield as Dar es Salaam, Tanzania, the discussion shifts to the assessment of the negative impacts of sheng on the learning and teaching of standard Kiswahili and especially, English in Kenya. It concludes by raising crucial questions and issues that need to be considered in an attempt to contain usage of sheng and mitigate its negative effects on the national and official languages which are the medium of formal education and business. 1. UTANGULIZI Mnamo mwaka wa 2001, msomaji mmoja alimwandikia mhariri wa gazeti fulani la kila siku nchini Kenya barua akilalamikia kushuka kwa kiwango cha ufasaha katika matumizi ya lugha ya Kiswahili. Alishangaa kwa nini lugha hii ambayo ndiyo lugha ya taifa na pia Kiingereza, lugha rasmi zimedharauliwa na kupuuzwa na Wakenya wengi kiasi cha kuzungumzwa kiholela. Alilalama kwamba ijapokuwa tumeirithi lugha ya kupendeza ya Kiswahili kutoka kwa wahenga na tunawajibika kuikuza na kuilinda badala ya kuibananga, kile ambacho tutawarithisha wanetu ni kinyume cha kile tulichokirithi, kwani tutawapa lugha duni iliyoyumbishwa kwa matumizi yasiyostahili. Alizidi kusema kuwa ingawa ni kweli Kiingereza kinazikalia lugha nyingine zote duniani ikiwemo Kiswahili, pana haja kuu ya kuchunguza hadhi na mahali pa Kiswahili, lugha ambayo ina heshima ya kipekee barani Afrika. Sote tunawajibika kuijenga lugha hii kwani ni muhali na ajabu kuu kwamba 1 Profesa Kitula King’ei ni profesa wa Kiswahili katika Idara ya Kiswahili na Lugha za Kiafrika katika Chuo Kikuu cha Kenyatta, Kenya. 2 John Kobia ni mhadhiri wa Kiswahili katika Idara ya Idara Elimu ya Lugha na Fasihi, katika Chuo Kikuu cha Magharibi, Kenya. Lugha Kama Kitambulisho: Changamoto ya Sheng Nchini Kenya 321 tunaionea haya lugha hii yetu ya kitaifa na kimataifa kiasi tunachelea kuitumia. Baadhi ya watu huogopa kudunishwa waizungumzapo ilhali wengine wanaichukia tu moja kwa moja. Kiini cha barua ya msomaji huyo kilikuwa kwamba hali anayoisimulia hapo juu imepelekea kuzuka kwa msimbo wa mawasiliano ambao ni kama “lugha” ngeni iitwayo Sheng. Jina hili limepewa msimbo huo ambao ni kama lugha mseto inayojumuisha Kiswahili na Kiingereza na hata msamiati kutoka lugha zinginezo za Kenya. Sheng ni kifupisho cha “Swahili-English”. Mwandishi wa barua hiyo anatoa mwito wa kubadilishwa kwa mielekeo kuhusu lugha ya Kiswahili pamoja na lugha nyinginezo akisisitiza kwamba kila mmoja anao wajibu wa kutekeleza katika juhudi hiyo. Hata hivyo, anafafanua kuwa siyo lazima tuyaue matumizi ya Kiingereza ama lugha zingine ili kukuza lugha ya Kiswahili (Rono 2001: 7). Hivi karibuni, kumezuka mjadala kuhusu iwapo vitabu vichapishwe kwa Sheng au la. Kwa upande mmoja kuna wale kundi linalodai kuwa Sheng ni kitambulisho cha vijana na hivyo vitabu vinahitajika kuchapishwa kwa msimbo huu (Mugubi 2006; Orodho katika Ngare 2006). Kwa upande mwingine kuna wanaodai kuwa hakuna haja ya kuchapisha vitabu kwa kutumia msimbo huu wakiteta kuwa Sheng ni lugha ya manamba na wahuni na kufanya hivyo ni kuupa msimbo huu hadhi ambao haustahili (Ramani, 2006). Maoni ya Rono (2001) na mjadala wa sasa ni dhihirisho la hali ya kutatanisha ya lugha nchini Kenya kwa sasa. Kwanza kabisa, kwa upande mmoja kuna haja ya kuielewa lugha kuwa sio tu kielelezo cha utamaduni bali ni njia mahsusi ya kuelezea na kusambazia utamaduni wenyewe. Katika maana hii, Kiswahili kimepewa umuhimu mkubwa sana kama nyenzo maalum ya kuelezea utamaduni asilia wa Mwafrika. Makala hii inajadili suala la lugha na utambulishaji wa utamaduni kwa kurejelea msimbo wa Sheng. Makala inatoa kauli kwamba iwapo lugha itahesabiwa kama kielelezo na nyenzo ya utamaduni wa kitaifa, basi, katika muktadha wa Kenya ya sasa, kielezo hicho kinatetereka kutokana na hali ya kutatanisha ya lugha nchini humu. Utata huu unadhihirishwa na kuzuka kwa msimbo wa vijana uitwao Sheng ambao, kama itakavyoonyeshwa baadaye, ni ishara ya kutoridhika kitamaduni ambako vijana wanahisi katika jamii ya kisasa. Makala inamalizia kwa kueleza haja kuu iliyopo ya kuunda upya sera ya kitaifa ya lugha itakayofafanua hadhi na majukumu ya lugha za kigeni kama Kiingereza kwa upande mmoja na Kiswahili na lugha zingine za kiasili kwa upande mwingine.
. UHUSIANO KATI YA LUGHA NA UTAMADUNI Utamaduni unaweza kuelezwa kwa kijumla kama jumla ya mfumo wa asasi, amali, mielekeo, fikira na desturi zinazoitambulisha jamii fulani katika kipindi fulani cha historia. Dhana hii ya utamaduni pia hutumiwa kuelezea jamii ya Nordic Journal of African Studies 322 watu iliyostaarabika, kuelimika au kuendelea katika vipengele fulani vya maisha. Jamii au kikundi hicho husika sharti kiwe kinatambuliwa na kinajitambulisha kama jamii moja. Mfumo wa imani na fikira unaotokana na utaratibu wa elimu, mafunzo na mila au desturi unaopelekea kukomaa kwa watu wa jamii fulani pia unaweza kuitwa utamaduni. Mwanachuoni maarufu Lo Liyong (1972: xi) amefafanua utamaduni kama, “jumla ya shughuli, kumbukumbu, matumaini, mipango ya baadaye ya jamii fulani pamoja na ndoto na maono yao”. Ni jambo dhahiri kwamba lugha, ambayo inaweza kuelezwa kama mfumo wa sauti tamkwa zenye maana zinazounganishwa kuambatana na sheria za matumizi na ambazo hutambuliwa na jamii husika, pia ni mfumo unaotumika na kutambuliwa na jamii yenye utamaduni maalum. Hii ina maana kuwa lugha inafungamana sana na ina uhusiano wa karibu na mfumo wa utamaduni wa jamii husika. Kwa ufupi, kauli inaweza kutolewa kwamba utamaduni hugubika asasi zote za kijamii ikiwemo lugha. Hata hivyo, uhusiano kati ya lugha na utamaduni ni jambo lenye utata mkubwa kwani ingawa lugha ni kipengele kimojawapo cha utamaduni, pia ni njia maalum ya kuelezea, kuutetea na kuuhifadhi utamaduni wenyewe. Lugha hueleza utamaduni wa jamii husika katika viwango vyote kama vile tabia, raslimali, mfumo wa ishara na imani. Kwa hivyo, tunaweza kujiuliza, je, ni kwa njia gani ambapo vipengele vya utamaduni kama vile lugha, matabaka na tabia huhusiana katika hali hii ya utata? Kulingana na Fowler (1985: 65), lugha sio tu njia ya kujielezea bali pia ni chombo kinachoashiria tabaka na hadhi ya mtu katika jamii. Kwa hivyo, kutokana na matumizi ya lugha, dini, jinsia, tabaka, umri na maelezo mengine ya mzungumzaji yanaweza kudhihirika. Ni kwa maana hii ndipo inaweza kudaiwa kwamba, msimbo wa Sheng unaashiria kitambulisho cha aina fulani kuhusu kiwango cha hadhi na mahali pa mhusika katika jamii yake. 3. SHENG KAMA TUKIO LA KIJAMII Imeelezwa hapo juu kuwa Sheng ni namna ya msimbo au kilahaja cha kundi fulani miongoni mwa vijana. Mfumo huu wa mawasiliano umesanifiwa na vijana hasa wale wanaoishi katika sehemu za mijini. Mfumo wenyewe hufuata muundo wa kisarufi wa Kiswahili na lugha nyinginezo za Kibantu ila hutumia maneno mengi mapya ya kubuniwa na ya mkopo kutokana na lugha mbalimbali kikiwemo Kiingereza na lugha nyinginezo za Kiafrika kama vile Kikamba, Kiluo, Kikuyu, Kiluyia na Ekegusii. Maelezo haya ya kijumla kuhusu maana ya Sheng yametolewa na wasomi kadha kama vile Mkangi (1984: 17), ambaye ameueleza msimbo huu kama lugha mseto au lugha “kiunzi” ya kizazi kipya cha vijana wa mijini. Pia Ogechi (2002: 3) and Shitemi (2001) wanakubaliana na maoni hayo kwamba Sheng ni msimbo wa kijamii unaotumiwa hasa na vijana wa mijini na mashambani nchini Kenya. Maelezo haya yanatoa baadhi ya sifa za kimsingi zinazoutambulisha msimbo huu. Kwa mfano, hutumiwa sana na vijana Lugha Kama Kitambulisho: Changamoto ya Sheng Nchini Kenya 323 ili kujitambulisha kama kundi la kijamii. Maoni haya pia yameungwa mkono na Shitemi. Wachunguzi wengi wanakubaliana kuwa Sheng ilizuka katika miaka ya katikati ya sitini na sabini katika sehemu za makazi za Mashariki mwa jiji la Nairobi kama vile mitaa ya: Kaloleni, Mbotela, Kimathi, Pumwani, Majengo, Bahati, Buruburu, Barma, Umoja, Dandora, Huruma, Mathare, Eastleigh na viunga vyake (Mbaabu na Nzunga, 2003). Kufikia miaka ya awali ya 1970, Sheng ilikuwa imepamba moto sio tu Nairobi bali pia katika miji mingine kote nchini Kenya. Kufikia sasa, Sheng imekuwa kitambulisho cha takriban vijana wote nchini, mijini na mashambani wawe wa shule au la. Kwa mujibu wa Mukhebi (1986: 11), Sheng ni tukio la kitamaduni ambalo linafungamana sana na mawazo au fikira, hisia na matakwa ya watumiaji wake. Anaeleza kuwa wazungumzaji asilia wa Sheng waligundua kuwa kutokana na hali na mazingira yao ya kifukara katika mitaa ya jamii yenye mapato ya chini, hawangeweza kupata elimu yao na kuwasiliana kupitia Kiingereza bali walihitaji mfumo wao wenyewe. Anaongezea kuwa kutokana na ufahamu wao duni wa Kiingereza, iliwawia vigumu vijana hao kuweza kujifunza masomo mseto kwa Kiingereza kama vile Historia, Jiografia, Fasihi na maisha ya kijamii ya Waingereza, masomo yaliyokuwa ya kimsingi katika mitala ya shule za msingi wakati huo. Je, msimbo huu wa Sheng uliibuka kutokana na nini? Kuna nadharia mbalimbali zinazojaribu kueleza asili na chimbuko la Sheng. Hata hivyo, nadharia kuu ni mbili; nadharia ya uhuni na nadharia ya msimbo wa vijana. Kwa mujibu wa nadharia ya uhuni, msimbo wa Sheng ulibuniwa na kuibuka kutokana na wahuni au wakora jijini Nairobi (Kobia, 2006). Waliunda baadhi ya maneno kutoka nyuma kuelekea mbele badala ya muundo wa kawaida wa neno. Kwa mfano, neno kama ‘nyama’ lilibuniwa na kuwa ‘manya’. Nadharia inahusisha kubuniwa kwa Sheng na haja ya wahuni kuwasiliana kwa ‘lugha’ ambayo watu wengine hawangeweza kuifahamu. Mazrui (1995) anadai kwamba Sheng iliibuka miaka ya thelathini jijini Nairobi kama lugha ya wahuni. Ilikuwa ‘lugha’ ya wahuni ya kujitambulisha hasa wale wanaonyakua mali za watu na kutoroka. Nadharia ya msimbo wa vijana kwa upande mwingine hudai kuwa Sheng iliibuka katika mitaa ya mashariki mwa Nairobi mnamo miaka ya sabini (Osinde, 1986; Shitemi 2001). Kufuatia kupatikana kwa uhuru hapo mwaka wa 1963, idadi ya wakazi wa jiji la Nairobi ilipanda kwa haraka sana kutokana na kumiminika kwa watu kutoka mashambani wakitafuta nafasi za kazi katika mitaa ya viwanda humo jijini. Wananchi hao maskini waliishia kuishi katika mitaa ya makazi duni ya viwandani mashariki mwa Nairobi ambapo ndio kitovu cha maendeleo ya viwanda. Ijapokuwa wafanyikazi hawa pamoja na jamii zao walilazimika kutumia Kiswahili kwa mawasiliano baina yao, wengi walikichukia Kiswahili kwa vile kilikuwa kimedunishwa sana na sera ya ukoloni kama lugha ya mashambani, lugha ya vibarua au “maboi” wa kuwatumikia Wazungu. Hata hivyo, watoto wa wafanyikazi hao hawakupendelea kuendelea kukitumia Kiswahili kama wazazi wao kwa sababu kadha. Kwanza kabisa, Nordic Journal of African Studies 324 kinyume na wazazi wao, watoto wale walilazimika kuishi katika hali ya jamii ya utatu-lugha: lugha za kinyumbani, Kiswahili na Kiingereza. Pia, walitambua kuwa ingawa walibidika kutumia lugha nyingi, ni Kiingereza pekee ambacho kilipewa hadhi ya juu kama lugha ya utawala, mamlaka, heshima na uwezo wa kiuchumi. Ili kuepuka matatizo ya kimawasiliano na kama njia ya kusuluhisha utata wa hali hiyo iliyowakabili, vijana hao waligundua msimbo wa mawasiliano kati yao ambao, ingawa ulifuata sarufi ya Kiswahili, uliazima msamiati kutokana na lugha za kiasili na kuunda baadhi ya maneno yake. Msimbo huo ndio uliotokea kuwa Sheng hapo baadaye. 4. SHENG KAMA KITAMBULISHO MIONGONI MWA VIJANA Makala hii inachunguza athari, ambazo Sheng imekuwa nazo katika hali ya lugha nchini Kenya, na pia juu ya jinsi vijana wanavyojielewa ama wanavyojitambulisha. Tumeeleza hapo juu jinsi Sheng ilivyochipuka kutokana na azma ya vijana wa mitaa fulani jijini Nairobi kwa kujaribu kusuluhisha hali ngumu ya lugha na kijamii walimojikuta. Hata hivyo, ni kweli kwamba msimbo wa Sheng umeanza kuashiria uhalisia mkubwa wa maisha ya kisasa zaidi katika jamii ya Wakenya. Kwa mfano, wasanii wengi wa muziki, hasa vijana, hutumia lugha ya Sheng kuwasilisha maudhui katika nyimbo mbalimbali, kwa sababu ndio “lugha” inayoweza kuwafikia vijana wengi kwa mvuto wa hali ya juu. Baadhi ya wasanii chipukizi, ambao nyimbo zao zimetumia Sheng, ni pamoja na Nonini, Eric Wainaina, Kalamashaka, Nameless, Wahu, marehemu E-Sir na wengineo. Njia mojawapo inayotumiwa kusambaza maneno ya Sheng ni kupitia muziki, ambao huchezwa kwenye vituo vya redio na runinga mbalimbali. Sheng inaweza kuhesabiwa kuwa kama suluhisho la vijana wa kisasa, ambao wamechukizwa na jamii yao iliyogawika matabaka na hali ya lugha yenye ubaguzi dhidi ya matabaka fulani (Mkangi 1984). Hali hii ya kutatanisha iliibuka kutokana na mfumo ulioanzishwa na wakoloni katika miaka ya mwisho ya karne ya 19, ambao ulikusudiwa kuanzisha kuendesha na kudumisha jamii yenye matabaka ya kiuchumi. Kielelezo cha matabaka hayo ni kuwepo kwa mitaa ya maskini Mashariki mwa jiji na ile ya matajiri Magharibi mwake vilevile. Ili kuhakikisha mpangilio huo ulipata mashiko, viwanda vyote ambamo maskini na vibarua waliajiriwa, vilipangwa kuwepo katika mitaa ya Mashariki, walikoishi wachochole. Mitaa hii ilikuwa na uhaba wa huduma muhimu kama vile shule na hospitali. Vijana hujitambulisha na Sheng kwa sababu ya mahitaji na kutokana na usanii uliomo kwenye msimbo huu. Sheng ni msimbo unaotumia maneno yake kisanii hivi kwamba huwavutia watu wa umri tofauti. Kwa mfano, kutokana na mtindo wa usanii wa hali ya juu wa Sheng, ukumbi wa “Head on Corrishon” katika Sunday Nation kila wiki, ni maarufu sana miongoni mwa vijana na wazee. Lugha Kama Kitambulisho: Changamoto ya Sheng Nchini Kenya 325 Pengine tunaweza kujiuliza, iwapo vijana hao wahusika walihitaji lugha ya kuwaunganisha, kwa nini hawangeweza kutumia Kiswahili? Jibu ni kwamba ingawa vijana hao hawakukichukia Kiswahili, walikiona cha lugha duni kutokana athari ya kutwezwa kwa lugha hiyo na wakoloni katika jamii na hasa katika mfumo wa elimu. 5. SHENG KAMA KIFAA CHA KIJAMII Msimbo wa sheng umejitanzua kutoka hali ya kuwa msimbo wa maongezi pekee na sasa inatumiwa katika baadhi ya vitabu, vyombo vya habari kama redio, runinga, magazeti na hata matangazo ya kibiashara. Kwa mfano, katika gazeti la Taifa Leo, kuna ukumbi wa “Risto za Mateneez” yaani “Stori za Vijana” ambao huandikwa kwa Sheng. Makala yanayopatikana katika ukumbi huu yanatumia ‘lugha’ hii ya Sheng kwa sababu ndio msimbo ambao huwatambulisha vijana. Wanaomiliki vyombo vya habari na sekta nyingine za biashara wamegundua kuwa matumizi ya Sheng ndiyo njia mwafaka zaidi ya kulifikia soko kubwa la vijana kwa ajili ya kueneza matangazo ya bidhaa na huduma za kibiashara. Kwa hivyo, Sheng imekuwa daraja la kuwafikia na kuwavutia vijana ambao ni zaidi ya asilimia 60% ya idadi ya Wakenya. Msimbo wa Sheng kama tukio la kijamii umeenea sana nchini Kenya hivi kwamba hata waandishi wa vitabu wameanza kuutumia katika uandishi wao (Rinkanya, 2005: 43). Miongoni mwa waandishi ambao wameanza kutumia msimbo wa Sheng katika uandishi wao ni David Maillu hasa katika kitabu chake, Without Kiinua Mgongo (1989). Hata hivyo, kwa upande mwingine matumizi ya msimbo wa Sheng yamelaumiwa na walimu wengi katika shule za msingi na zile za upili kuwa ni sababu mojawapo kuu ya kushuka kwa kiwango cha ujuzi wa lugha ya Kiswahili na Kiingereza miongoni mwa wanafunzi. Sheng imelaumiwa kwamba inasababisha wanafunzi kutozingatia mafunzo ya kanuni za sarufi na tahajia au maendelezo. Kwa hakika ni msimbo ambao hauzingatii sheria za sarufi na tahajia kwa sababu zisizofahamika, kwani ingawa muundo wake wa kisarufi ni ule wa Kiswahili, Sheng hupuuza sarufi ya Kiswahili katika matumizi yake. Kwa maoni ya baadhi ya wataalamu wa lugha, msimbo wa Sheng ni kama vile juhudi za aina hiyo zinazofanywa na baadhi ya watumiaji wa lugha ya Kiingereza ambao wamekuwa wakijaribu kuifanya lugha hiyo kuwa kama ya “Kiafrika”. Mifano ya matumizi kama hayo ya Kiingereza yametolewa na Nnamonu (1995), ambaye amedai kuwa mengi ya matumizi kama hayo huwa ni makosa yasiyokusudiwa na yanayotokana na athari za lugha za kiasili za Kiafrika. Bila shaka, Sheng imekuwa ikilaumiwa na waalimu kuwa ndicho chanzo kikuu cha kuzorota kwa Kiingereza na Kiswahili sanifu nchini Kenya. Katika mifano hii, watumiaji hutamka dhana za Kiingereza kwa wingi ambazo kwa hakika hazina wingi: Mifano, Nordic Journal of African Studies 326 Kiingereza Kiswahili accommodation(s) malazi ammunition(s) risasi behaviour(s) tabia / desturi cutler(y|ies) vyombo vya kulia fun(s) mambo ya kuchekesha equipment(s) vifaa elite(s) wasomi advice(s) ushauri au nasaha furniture(s) samani luggage(s) mizigo machine(s) mitambo au mashine taff(s) wafanyikazi stationer(y|ies) makabrasha beard(s) ndevu off-spring(s) chenye kuzaliwa damage(s) uharibifu au hasara gossip(s) masengenyo Vilevile, maneno ya majina yafuatayo hutumika kimakosa kwa kutangulizia kibainishi a, kwa mfano: an advice ushauri au nasaha a help msaada a harm madhara a permission ruhusa a treatment matibabu Isitoshe, watumiaji wengi wa Sheng hutatizika kwa kutenganisha dhana za majina ya kidhahania na kufanya yawe kwa uchache badala ya wingi. Kwa mfano: Lugha Kama Kitambulisho: Changamoto ya Sheng Nchini Kenya 327 Sheng Kiswahili Sanifu hitaji mahitaji oni maoni sumbuko masumbuko jaribu majaribu lezi malezi ingiliano maingiliano zoea mazoea teso mateso takwa matakwa 6. MUUNDO WA SHENG (a) Uundaji wa Nomino Kama anavyosisitiza Ogechi (2005), uundaji wa maneno katika Sheng ni utaratibu changamano unaohusisha mbinu tofauti na kufuata hatua kadha. Akitumia mifano ya uundaji wa majina au nomino, vitenzi na vivumishi, Ogechi anaonyesha kuwa leksia za Sheng hutokana na vianzo maalum katika Kiswahili, Kiingereza na lugha zingine za Kenya. Uundaji wa maneno katika msimbo wa Sheng hutumia njia mbalimbali. Kuna matumizi ya ukopaji wa maneno kutoka lugha ya Kiswahili, Kiingereza na lugha nyingine za Kiafrika. Kuna pia kubuni kinasibu kwa maneno ya Sheng. Zifuatazo ni baadhi ya nomino zinazopatikana katika msimbo wa Sheng: gichagi sehemu za mashambani moti gari chapaa pesa manyakee wasichana budaa, mbuyu baba kingoso Kiingereza dem msichana Ili kuyapa maneno yanayohusu majina sifa za Sheng, watumiaji wake huunda majina halisi ya mahali na watu kwa kutumia viambishi tamati -sh. Kwa mfano: Nordic Journal of African Studies 328 Odhiambo Odhish Matumbo Matush Mutunga Mutush Kilonzo Kilosh Kamau Kamash Makokha Makosh Nyalgunga Nyalgush Nairobi Nairosh Namanga Namash (b) Uundaji wa Vitenzi Baadhi ya vitenzi huundwa kwa kuunganisha mwanzo kiambishi ku- na mzizi kwa kitenzi mkopo kutokana na lugha nyingine za Kenya au vitenzi vipya vya kubuniwa vilivyopewa kiambishi cha mwisho cha Kiswahili. Mifano: ku-bonga kuzungumza ku-ush kuondoka, kwenda au kutoweka ku-waka kulewa ku-noki kukasirika (Kiingereza: “knock”) ku-duu kufanya jambo (Kiingereza: “do”) ku-sare kupeana bila malipo (Kiingereza: “surrender”) ku-jienjoy kujifurahisha, kustarehe (Kiingereza: “enjoy”) ku-sosi kula ku-dim kumaliza ku-wea kuvaa (Kiingereza: “wear”) Lugha Kama Kitambulisho: Changamoto ya Sheng Nchini Kenya 329 (C) UFUPISHAJI WA MANENO Katika msimbo wa Sheng, baadhi ya maneno ya Kiingereza yanayokopwa hufupishwa ili kuunda maneno mafupi. Maneno haya hujitokeza kama dokezo la neno kamili. Baadhi ya mifano ni kama vile: tao mji (Kiingereza: “town”) mat matatu hao nyumba (Kiingereza: “house”) Swa Kiswahili, Swahili cole chuo (Kiingereza: “college”) pero mzazi (Kiingereza: “parent”) hasii bwana wa (Kiingereza: “husband”) (d) Matumizi ya Jazanda na Tasifida Msimbo wa Sheng huunda baadhi ya maneno yake kwa kuzingatia mbinu ya jazanda na tasifida. Kwa mfano: boli mja mzito mahewa muziki kuro kahaba pupuu kwenda haja kubwa susuu kwenda haja ndogo (e) Muundo Wa Sentensi Kama ilivyodokezwa hapo juu, sentensi katika msimbo wa Sheng hufuata sarufi ya lugha za Kibantu na hasa Kiswahili. Kwa mfano: amedinda (amekataa). Hapa a ni kiima, me ni hali timilifu, dinda ni kitenzi. Kwa hivyo, ni dhahiri kwamba Sheng ni jitihada za kuunda msimbo wa mawasiliano ambao ni kama lugha mseto kati ya Kiswahili na Kiingereza. Kwa hakika, Sheng inafuata sarufi ya Kiswahili na kutumia maneno ya Kiingereza na lugha nyinginezo za Kikenya. Kwa maoni ya baadhi ya wataalamu, muundo wa Sheng hutinga juhudi za kufunza lahaja rasmi yaani Kiswahili na Kiingereza sanifu (Asiba 1985; Kiama 1990; Ochieng 1990). Ili walimu waweze kuwarekebisha wanafunzi wao ipasavyo kuhusiana na matatizo ya Sheng, hawana budi kujifahamisha na kuelewa muundo wa maneno na sentensi katika msimbo wa Sheng. Nordic Journal of African Studies 330 7. HITIMISHO Makala hii imedhamiria kufafanua kwa ufupi asili na sababu za kuzuka kwa msimbo wa Sheng kama kifaa cha kutosheleza mahitaji fulani ya lugha na kijamii ya vijana wa sehemu za mijini katika miaka ya sitini na sabini. Msimbo huu umeonyesha ishara ya kuambaa uzingatiaji wa lugha sanifu ya Kiswahili na Kiingereza. Pia Sheng inaweza kuhesabika kuwa juhudi ya vijana wa kizazi kipya ya kuua “ukabila” kwa kushirikisha maneno ya lugha tofauti pamoja na kuunda msamiati wa kipekee katika msimbo wa Sheng. Jambo muhimu kabisa ni kwamba Sheng imeonyeshwa kama njia ya mawasiliano na kitambulisho cha kijamii kwa vijana wa matabaka ya chini katika mitaa maskini ya Mashariki mwa Nairobi, ambayo ilikua na kuenea hadi kugubika sehemu zote za Jamhuri ya Kenya kutoka mijini hadi mashambani. Makala imejaribu kuonyesha jinsi vipengele vya lugha na utamaduni vinavyochangiana na kuathiriana kwa kutumia mfano wa kuzuka na kusambaa kwa Sheng nchini Kenya. Kama vile Mazrui na Mazrui (1995) wanavyodokeza, mabadiliko ya lugha ni ushahidi wa mabadiliko mapana zaidi katika mfumo wa utamaduni unaohusika. Kuzuka kwa Sheng katika miaka ya sitini na sabini kumeonyeshwa kama kulitokana na kutoridhika kwa vijana walioishi katika mitaa ya matabaka ya chini na hali ya lugha pamoja na sera yake. Hali ya kutatanisha ya lugha iliyowakabili vijana hawa ni ile iliyosababishwa na sera ya lugha ya kikoloni iliyorithishwa Wakenya na Waingereza. Katika sera hii, lugha za kwanza hazikutumiwa katika shule za sehemu za mijini, ambapo Kiingereza kilitumika huku Kiswahili kikiwa kama lugha ya tabaka la chini na ikinyimwa nafasi katika mfumo wa elimu. Kwa vile vijana waliohusika walizaliwa mijini au mashambani, wengi wao walichukia kufunzwa kwa Kiingereza, lugha ambayo hawakuitumia nyumbani au katika maisha yao ya kila siku. Hii inamaanisha wangeridhika zaidi kama wangelifunzwa kwa lugha zao za kwanza au kwa Kiswahili. Kwa hivyo, walitunga “lugha” yao ya Sheng, ambayo waliitumia ili kujitofautisha na vijana wa matabaka ya juu waliobobea katika lugha na utamaduni wa Kiingereza na ambao walichukia Kiswahili na lugha za kiasili. Hali inayodhihirika katika makala hii ni kuwa Sheng ipo na msimbo huu utaendelea kuwepo kwa miaka mingi ijayo. Labda changamoto kuu ni kutafakari ni kwa njia gani washikadau wanaweza kukabiliana na athari zinazotokana na msimbo huu hasa katika mfumo wa elimu kuhusiana na suala la sera ya lugha. Ingawa Kiswahili kimeanza kutumiwa kufunzia shule za mijini na kufanywa somo la lazima katika mfumo wa elimu ya msingi na upili, bado ushindani na mvutano upo baina ya lugha hizi. Pengine njia ya pekee ya kulitatua tatizo hili ni kuikweza lugha ya Kiswahili na kuwa na taifa lenye lugha mbili rasmi, Kiswahili na Kiingereza. Hatua kama hii ingesaidia kuondoa mtafaruku wa lugha katika viwango vya kijamii, kielimu, kisiasa, kiuchumi na kibiashara na ungeipa lugha ya Kiswahili hadhi inayostahiki kama lugha ya kitaifa. Kwa kumalizia, tunapaswa kujiuliza maswali yafuatayo: Lugha Kama Kitambulisho: Changamoto ya Sheng Nchini Kenya 331 (i) Je, kwa vile Sheng imeenea sana miongoni mwa vijana wa Kenya, ambao ni asilimia 60 ya Wakenya wote, tunaweza kuujenga na kuuendeleza msimbo huo kuwa “lugha” kamili ya mawasiliano na hata kuitungia vitabu badala ya kuikashifu na kuipinga? Bila shaka, kwa sasa jibu la swali hili ni la. Hatuwezi kwa vile Sheng sio lahaja ya lugha yoyote inayojulikana ila ni msimbo tu miongoni mwa vijana. Lakini, iwapo hilo ni kweli, sharti tujiulize, je, tutafanya nini kuhusu vizazi vingi vya jamii maskini vinavyozaliwa mijini kwenye mitaa au mabanda na ambavyo vinategemea tu Sheng wala havina nafasi ya kujifunza lugha au lahaja wastani? (ii) Mbinu gani za kufunzia lugha zinafaa kutumiwa ili kupunguza makali ya athari za lugha za mitaani za vijana kama vile msimbo wa Sheng juu ya lugha au lahaja wastani ya Kiswahili au Kiingereza? (iii) Kwa vile hali na sera ya lugha nchini Kenya ni kielezo cha hali ilivyo katika mataifa mengi ya Kiafrika na pia katika mataifa yanayostawi, ni kwa njia gani upangaji wa lugha unaweza kushirikisha vipengele vya utamaduni na maisha ya kijamii kwa jumla ili kuyapa masuala ya kitamaduni kipaumbele katika ustawishaji wa lugha? Masuala haya na mengine yanayoambatana nayo yanafaa kufikiriwa katika upangaji wa mikakati ya maendeleo ya lugha na jamii katika mataifa kama Kenya kwani kuyapuuza masuala yenyewe kutapelekea ujenzi wa mifumo chapwa isiyoweza kuridhisha matakwa ya wanajamii wote. MAREJELEO Asiba, A. 1985. Can Sheng Stand the Test of Time?. Sunday Nation, Nairobi, August 30. Fowler, D. 1987. Language and the Social Context, Giglioli, P. (ed.). Middlesex: Penguin. Kiama, B. 1990. Sheng: Monstrosity or Tool for Unity? Kenya Times, Nairobi, November 12. Kobia, J. 2006. Sheng is not a language, but Popular Slang. Sunday Nation, Nairobi, February 2. Lo Liyong, T. 1972. The Popular Culture of East Africa. Nairobi: Longman. Mazrui, A. na Mazrui, A. 1995. Swahili, State and Society. Nairobi: EAEP. Nordic Journal of African Studies 332 Mbaabu, I. na Nzunga, K. 2003. English-Kiswahili Dictionary of Sheng: Deciphering East Africa’s Under-World Language. Dar es Salaam: TUKI Mkangi, K. 1984. Sheng and the Kenyan Culture. The Standard, Nairobi, August 30 (17–18). Mukhebi, L. 1986. Is Language and Culture Inseparable? Kenya Times, Nairobi, May 28 . Ngare, P. 2006. Firms Likely to Start Printing Books in Sheng. Daily Nation, Nairobi, September 26. Nnamonu, J. 1995. Common Errors in English. Essex: Longman. Ochieng, P. 1990. Sheng as a Tool Against Tribalism. Kenya Times, Nairobi, October 8. Ogechi, N.O. 2002. Trilingual Codeswitching in Kenya: Evidence from Ekegusii, Kiswahili, English and Sheng. Unpublished Ph.D Thesis. Hamburg: University of Hamburg. 2005 On Lexicalization in Sheng. Nordic Journal of African Studies, 14(3): 334–335. Osinde, K. 1986. Sheng: An Investigation Into the Social and Structural Aspects of an Evolving Language. Unpublished B.A. Dissertation. Nairobi: University of Nairobi. Ramani, K. 2006. Leave Sheng to Matatu Touts and musicians. The Standard, September 29. Rinkanya, A.N. 2005. Sheng Literature in Kenya: A Revival? Katika H. Indangasi na M. Odari (Wah). The Nairobi Journal of Literature, Number 3. Nairobi: Department of Literature, University of Nairobi. Rono, M. 2001. We should Arise and Save Kiswahili. The People, Nairobi, July. Shitemi, N.L. 2001. Pidginization: Sheng, the Melting Pot of Kenyan Languages and an Anti-Babel Development. Kiswahili Vol. 64. Dar es Salaam: Institute of Kiswahili Research