KISWAHILI, MOFOLOJIA,Swali



JINA LA KOZI: MOFOLOJIA
MSIMBO WA KOZI: KI 209          



SWALI LA 8;
a.) Kwa kutumia mifano toa maana ya mofimu ya utendeka.
b.) Taja alomofu zinazojitokeza
c.) Unda kanuni ya utokeaji wa alomofu hizo
  



Kazi hii imegawanyika katika sehemu kuu tatu yaani utangulizi, kiini na hitimisho. katika utangulizi tutajadili dhana ya mofimu, dhana ya alomofu na dhana ya mofimu ya utendeka kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali; baada ya hapo tutatoa fasili kwa ujumla kulingana na istilahi hizo. Pia katika kiini tutajadili kuhusu alomofu za mofimu ya utendeka na mazingira mbalimbali ya utokeaji wa alomofu hizo, halafu tutaonesha kanuni mbalimbali za utokeaji wa alomofu hizo katika vitenzi vya Kiswahili. Kisha tutatoa hitimisho pamoja na marejeo.
Kwa kuanza na maana ya mofimu, wataalamu mbalimbali wanatueleza kama ifuatavyo:
               Matinde (2012:101), anasema kwamba mofimu ni maana inayowakilishwa na mofu. Anaendelea kusema kuwa mofimu ni dhana ambayo ni sehemu ya umilisi kwa watumiaji wa lugha husika.
Pia Mgullu (1999:129), anaeleza kuwa mofimu ni dhana ya kidhahania ambayo ni maana inayowakilishwa au kusitiriwa katika mofu.
Kutokana na fasili za wataalamu hawa tunaweza kufasili kuwa, mofimu ni dhana dhahania ambayo ipo akilini mwa mtu, ambayo ni sehemu ya umilisi ya mtumiaji wa lugha husika na inawakilishwa katika mofu. Kwa mfano neno  anapika.
                        a – na – pik – a
Neno anapika lina mofu nne;
a – ni mofu inayowakilisha mofimu ya nafsi ya tatu umoja.
-na-  ni mofu inayowakilisha njeo ya wakati uliopo.
-pik- ni mofu inayowakilisha mofimu ya mzizi wa neno.
-a  ni mofu inayowakilisha mofimu ya kiambishi tamati maana.
Baada ya kueleza maana ya mofimu tuangalie maana ya alomofu kulingana na wataalamu mbalimbali.
Mgullu (1999:129) akimrejelea Richard na wenzake (1985) anasema kuwa, alomofu ni umbo mojawapo kati ya maumbo kadhaa tofauti tofauti yanayowakilisha mofimu moja. Pia Matinde (2012:100) anadai alomofu ni maumbo mawili au zaidi yanayowakilisha mofimu moja. Anaendelea kueleza kuwa alomofu hutokea katika mazingira maalumu.
               Baada ya kuona fasili za wataalamu hawa tunaweza kueleza dhana ya alomofu kuwa, ni maumbo tofauti tofauti yanayowakilisha mofimu moja na ambayo huwa na mazingira maalumu ya utokeaji. Kwa mfano katika data ifuatayo;
            Oga                     og – e – a                ogea
andika                 andik – i – a            andikia
imba                    imb – i – a               imbia                           
ruka                      ruk – i – a                rukia
lia                         li – li – a                   lilia
toa                        to – le – a                 tolea
Katika mifano hapo juu viambishi vilivyopigiwa msitari ni alomofu za mofimu ya utendea. Baada ya kuangalia maana ya mofimu na alomofu, ifuatayo ni maana ya mofimu ya utendeka kama inavyofasiliwa na wataalamu mbalimbali.
               Mgullu (1999:205), anafasili mofimu ya utendeka kuwa ni mofimu ambayo hueleza jambo ambalo limetendeka, anaendelea kusema kuwa kwa kawaida watu waliotenda jambo hili huwa hawatiliwi maanani kitu ambacho hutiliwa maanani ni kule kutendeka kwa jambo fulani. Anaendelea kufafanua kuwa mofimu ya utendeka huwakilishwa na mofu (- ik-) pamoja na alomofu zake ambazo ni (-ik-), (-ek-) na (-lik-).
Matinde (2012:194), anaeleza kuwa mofimu ya utendeka ni mofimu ambayo hutumiwa kudhihirisha mambo mawili kuwa (i) kitendo kimetendeka au kukamilka bila kuonesha aliyekitenda au kifaa kilichohusika katika utendaji wake. Kwa mfano
Mlango umefunguka               u – me – fung – u – k – a.
Nyumba imebomoka                i – me – bom – k – a.
Mofu {-k-} hapo juu iliyopigiwa msitari huonesha kuwa kitendo kimetendeka au kukamilika (ii) uwezekano wa mtu au kitu fulani kupatwa na tukio fulani katika hali ya uyakinishi. Kwa mfano katika data ifuatayo;
Maembe haya yanalika                       ya – na – l - ik – a
Somo linafundishika                          li – na – fund-ish – ik – a
Mpira unachezeka                             u – na – chez - ek – a
Motto analeleka                                a – na – le – lek – a
Kiti kinakalika                                   ki – na – ka – lik – a
Mofu (-ik-), (-ek-), (-lek-) na (-lik-) zilizopigiwa mstari hapo juu huonyesha juu ya jambo fulani kuwa na uwezekano wa kutendeka au kufanyika.
Hivyo kutokana na fasili za wataalamu hawa tunaweza kusema kuwa mofimu ya utendeka ni mofimu ambayo huonesha kuwa kitendo fulani kimetendeka au kukamilika, pia huonyesha uwezekano wa kitendo au jambo fulani, kufanyika, vilevile huonesha uzuri au ubora wa kitu au jambo fulani. Kwa mfano;
Fungua                       fung – u – k – a          funguka
Umba                        umb– ik – a                  pitika
Jenga                          jeng– ek – a               tosheka
Twaa                          twa – lik – a               twalika
Ng’oa                        ng’o – lek – a            ng’oleka
Katika mifano hapo juu ni vitenzi vya kauli vya utendeka vinavyowakilishwa na alomofu mbalimbali za utendeka zilizopigiwa mstari ambazo ni {-ik-},{-ek-},{-k-},{-lik-},{-lek-}. Baada ya kuangalia utangulizi  ambao umeelezea dhana ya mofimu, alomofu na mofimu ya utendeka .Sasa tuangalie alomofu zinazowakilisha mofimu ya utendeka. Alomofu hizo ni      {-k-}, {-ik-}, {-ek-}, {-lik-} na {-lek-}.
Tukianza na alomofu {-k-}, Matinde (2012:191) anasema alomofu hii ya mofimu ya utendeka hutokea iwapo mzizi wa kitenzi ukiwa na irabu aidha (a, i, u au o) na mzizi huo kuishia na irabu na huonyesha kukamilika kwa jambo au kitu fulani. Kwa mfano;
Pasua                                       pasu – k – a          pasuka       
Bomoa                                     bomo – k – a        bomoka
Tumia                                    tumi – k – a          tumika
Katika mifano hapo juu tunaona vitenzi pasua, bomoa na tumia katika mizizi yake ina irabu (a,,u na o) na kuishia na irabu.
 Alomofu nyingine inayjitokeza katika mofimu ya utendeka ni alomofu {-ik-}Mgullu(1999:205) anaeleza kuwa alomofu {-ik-} ya mofimu ya utendeka hutokea iwapo mzizi wa kitenzi ukiwa na irabu (a, i na  u) na mzizi huo kuishia na konsonanti, ambayo huonyesha ubora wa jambo fulani au uwezekano wa  kitu fulani kufanyika. Kwa mfano;
Imba               imb – ik – a         imbika (uwezekano wa jambo kufanyika).     
Umba             umb – ik – a         umbika (ubora au uzuri)
Fanya             fany – ik – a        fanyika  (uwezekano wa jambo kufanyika)
katika mifano hapo juu tunaona vitenzi imba, umba na fanya ni vitenzi ambavyo katika mizizi yake huundwa  na irabu (a, i na u) na  mzizi huo kuishia na konsonanti.
Alomofu nyingine inayojitokeza katika mofimu ya utendeka ni alomofu {-ek-}. Habwe na Karanja (2007:110) wanasema alomofu hii hutokea iwapo mzizi wa kitenzi ndani yake una irabu (e au o) na mzizi huo kuishia na konsonanti.na huonyesha aidha  ubora wa kitu au jambo au uwezekano wa jambo fulani kufanyika Kwa mfano;
jenga                 jeng – ek – a                jengeka
Ponya                 pony – ek – a               ponyeka
Choma               chom – ek – a              chomeka
Katika mifano hapo juu kitenzi jenga, ponya, na choma  katikati ya mzizi wake hubeba irabu  (o au e) na mwisho wa mzizi wake kuishia na konsonanti.
Alomofu nyingine inayojitokeza katika mofimu ya utendeka ni alomofu {-lik-}. Nkwera (1989:69) anasema alomofu hii hutokea endapo mzizi wa kitenzi ukiwa na  irabu (a, i, au u) na mzizi huo kuishia na irabu. Kwa mfano;
Rarua                        raru – lik – a                          rarulika     
Fungua                     fungu – lik – a                       fungulika
 Kimbia                     kimbi – lik – a                       kimbilika
Katika mfano hapo juu vitenzi rarua, fungua na vaa ni vitenzi ambavyo ndani yake vina irabu (a, i na u ) na mwisho wa mzizi huishia na irabu (a)
Alomofu nyingine inayojitokeza katika mofimu ya utendeka ni alomofu {-lek-}Matinde (2012:hutokea iwapo mzizi wa kitenzi ndani yake kukiwa na irabu e au o na mwisho wa mzizi huishia na irabu. Kwa mfano;    
            Zoa                                   zo – lek – a                      zoleka
Tembea                            tembe– lek – a                 tembeleka
Toa                                  to – lek – a                       toleka
Katika mifano hiyo hapo juu ya vitenzi zoa, toa na oa ni vitenzi ambavyo ndani yake kuna irabu (e na o) na mwisho wake humalizia na irabu.
Baada ya kuangalia alomofu za mofimu ya  utendeka ambazo ni {-k-}, {-ik-}, {-ek-}, {-lik-} na {-lek-}. Zifuatazo ni kanuni mbalimbali za utokeaji wa alomofu hizi..
Alomofu {-k-}
                                i.            /-ik-/                     {-k-}/ MZ (a, i, u, o) – I (utimilifu)
Mofimu ya utendeka {-ik-} inabadilika na kuwa alomofu {-k-} katika mazingira ya katikati ya mzizi wa neneo (kitenzi) kuwa na irabu (a, i, u au o) na mwisho wa mzizi huishia na irabu.
                              ii.            /-ik/                               {-ik-}/ MZ (a, u , o) – k
Mofimu ya utendeka {-ik-} inabadilika na kuwa alomofu {-ik-} katika mazingira ya mzizi wa kitenzi kuwa na irabu (a, u au o) na mwisho wa mzizi kuishia na konsonanti.
                            iii.            /ik/                                  {-ek-}/ MZ (o ,e) – k
Mofimu ya utendeka {-ik-} katika mazingira ya katikati ya mzizi wa kitenzi kuwa na irabu (o au e) na mwisho wa mzizi huo kuishia na konsonanti.
                            iv.            /-ik-/                              {-lik-}/ MZ (a, i, u) – I
Mofimu ya utendeka {-ik}inabadilika na kuwa alomofu {-lik-} katika mazingira ya katikati ya mzizi wa kitenzi kuwa na irabu (a, i au u) na mwisho wa mzizi huo huishia na irabu.
                              v.            /-ik-/                               {-lek-} MZ (e , u) – I
Mofimu ya utendeka {-ik-} inabadilika na kuwa alomofu {-lek-} katika mazingira ya katikati ya mzizi wa kiteenzi kuwa na irabu (e na o) na mwisho wa mzizi huu huishia na irabu.
                  Tunahitimisha kwa kusema kwamba mofimu {-ik-} huchukuliwa  kama  umbo la msingi la kuchangunua alomofu zote za utendeka, kwa sababu inatokea katika vitenzi  vingi vya utendeka kwa mfano imbika, fulika. pigika, chanika,tandika na vinginezo.Pia mofimu hizi za utendeka {-ik-},{-k-},{-ek-},{-lik-} na {-lek-} vikipachikwa katika mzizi wa neno hupanua maana ya msingi ya  neno lakini havibadili kategoria ya neno.




MAREJEO

Habwe, J. na karanja, P. (2007). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix publishers
Matinde, R.S. (2012). Dafina ya Lugha, Isimu na Nadharia. Mwanza: Serengeti Educational Publishers.
Mgullu, R. (1999). Mtaala wa Isimu: Fonetiki, Fonolojia na Mofolojia ya Kiswahili. Nairobi.
Nkwera, F.M.V (1989). Sarufi na Fasihi. Dar es salaam: Tanzania Publishing House.
Powered by Blogger.