MADA 2 : MAENDELEO YA FASIHI SIMULIZI UWASILISHAJI NA UENEZAJI WA KAZI ZA FASIHI SIMULIZI
MADA
2 : MAENDELEO YA FASIHI SIMULIZI
UWASILISHAJI NA UENEZAJI WA KAZI ZA FASIHI SIMULIZI
Ni aina ya fasihi ambayo hutumia mdomo katika kuumbwa,
kuwasilishwa na kusambazwa kwa wasikilizaji wake.
AU
Ni sanaaa ambayo hutumia mazungumzo na matendo katika
kuwasilisha ujumbe uliokusudiwa kwa watazamaji au wasikilizaji.
Mazungumzo hayo huwa katika mfumo wa masimulizi kwa kuumbwa,
kutambwa, kuganwa au kutongolewa.Fasihi simulizi hueleza jamii kiutamaduni,
kiuchumi na kisiasa. Fasihi huzungumzia juu ya yale mambo ambayo huzunguka
jamii husika na huathiriwa sambamba na
mabadiliko ya jamii na kwa hiyo nayo hubadilika kimaudhui na kifani kufuatia
mabadiliko ya mifumo ya kisiasa, kiuchumi, na kijamii.Fasihi simulizi ni utanzu
wa Sanaa ambao hukua na kubadilika kutokana na mabadiliko ya wakati na mifumo
ya jamii.
VIPENGELE MUHIMU VYA FASIHI SIMULIZI
(a) Msimulizi (fanani),Huyu huwa ni mtu
ambaye anaitamba hadithi, kuimba wimbo, kusimulia au kutoa vitendawili au
methali.
(b) Wasikilizaji au watazamaji (Hadhira),Hawa
ni washiriki katika kutazama au kusikiliza fani ya fasihi simulizi na mara
nyingine huwa wanatumiwa na fanani kama wahusika katika kazi yake
(c)
Mandhari,
Hili ni jukwaa au mahali ambapo tukio la kifasihi (fasihi simulizi)
litatendeka.Pahali au mahali hapo yaweza kuwa nyumbani, uwanjani, kuzunguka
moto, baharini n.k.
(d)
Tukio/Dhana
inayotendeka,Hili huwa ni tendo linalotendeka katika jukwaa la fasihi
simulizi. Tendo hili laweza kuwa ni usimulizi wa hadithi, kutega vitendawili,
kuimba nyimbo au wimbo au kutoa methali.
SIFA ZA FASIHI SIMULIZI.
Ø
Fasihi simulizi hushirikisha fanani na hadhira katika
utendaji kwa wakati mmoja.Hii humfanya fanani aweze uonyesha baadhi ya
matendo katika usimulizi wake kama vile kutumia viungo vya mwili kwa kuchezesha
midomo, kukunja uso, kubinya macho, kuchezesha mabega n.k.
Ø
Fasihi simulizi ina sifa ya kuwepo kwa
fanani ambaye huweza kusimulia kwa kuimba, kusoma kwa sauti au
kubadilisha mtindo wa usimuliaji wake,fanani huweza kufanya yote hayo kama
akiona hadhira yake imechoka kusikiliza.Pia ana uwezo wa kuona kama ujumbe wake
umeeleweka au la!
Ø
Fasihi simulizi zina sifa ya kwenda na
wakati na mazingira, tabia hii inatokana na jinsi fasihi simulizi
inavyoenea wasikilizaji huwa wengi na hata kama baadhi tanzu za fasihi simulizi
zilipitwa na wakati zinaweza kubadilishwa na fanani ili zisadifu mazingira
maalumu ya wakati huo.
Ø
Fasihi simulizi huzaliwa, hukua, huishi hata
kufa hii inasababishwa na mabadiliko
ya mazingira ambayo hufuata mfumo wa kihistoria wa jamii, mfano kutokana na
maendeleo ya sayansi na teknolojia ya kuhifadhi fasihi simulizi katika
maandishi ya fasihi simulizi huonekana chapwa kwa sababu ya mambo kama vile
miondoko au ngoa, vinakuwa havimo.
Ø
Fasihi simulizi ina uwanja
maalumu wa kutendea, Fasihi simulizi huwa na sehemu inayochaguliwa kwa
ajili ya aina fulani ya fasihi simulizi itakayofanywa na wahusika. mfano
tambiko huwa na sehemu maalumu ya kutambikia kama vile sehemu yenye
pango,kwenye mti mkubwa kama vile mbuyu, njia panda, makaburini n.k.Hivyo ni
wazi kwamba fasihi simulizi inahitaji uwanja wa kutendea yenye kuhusisha
vitendo.
Ø
Fasihi simulizi ni mali ya jamii nzima.Tanzu
zake zote zikishatendwa humilikiwa na jamii kwa pamoja na hii ndiyo inayopatiwa
uwezo wa kurithishwa kizazi kimoja hadi kingine.Hivyo huwafikia watu wengi hata
wale wasiojua kusoma na kuandika.
MCHANGO WA FASIHI SIMULIZI KATIKA
FASIHI ANDISHI
Fasihi simulizi ina mchango mkubwa sana katika fasihi Andishi
kifani n kimaudhui
A.Kimaudhui,Dhamira nyingi ambazo ndicho kiini cha maandishi
mengi katika Fasihi Andishi
zilikwishajadiliwa katika fasihi
simulizi.Dhamira hizo ni kama vile
Mapenzi,Siasa,Matabaka,Uhuru,Ukombozi,Usawa,Unyonge wa mwanamke,Uchawi na
Ushirikina n.k Fasihi simulizi haijavumbua dhamira mpya kabisa bali
maudhui/dhamira zote za kale.
B. Kifani,Vipengele mbalimbali vya fani ya fasihi simulizi
katika kufikisha ujumbe kwa jamii zao.Vipengele hivyo ni;
1. Muundo,Fasihi
simulizi muundo wake ni wa moja kwa moja pia kuna baadhi ya waandishi wa Fasihi
Andishi ambao wametumia muundo wa moja kwa moja.Mfano Riwaya ya Kuli
(1979) ya Shafi A. Shafi Ametumia muundo wa moja kwa moja.
2. Mtindo,Fasihi
simulizi hutumia mtindo wa masimulizi pia kuna baadhi ya waandishi wa Fasihi
Andishi hutumia mtindo wa masimulizi.Mfano Riwaya ya Shida (1975) ya Balisdya
3. Wahusika,Waandishi wa Fasihi andishi hutumia wahusika wasio
binadamu katika kazi zao ambao kwa kawaida hupatikana katika fasihi simulizi
tu.Mfano Mashetani (1971),Pambo (1975),Adili na Nduguze (1952) Kusadikika (1951)
na Kufikirika (1967) wametumia wahusika mashetani ambao hupatikana katika fasihi
simulizi tu. Wahusika kama wanyama,majini,mazimwi hupatikana katika fasihi
simulizi tu.
4. Matumizi ya hadithi ndani ya
hadithi,hapa wahusika husimulia hadithi mbali mbali katika fasihi
andishi .Hawa husimuliana hadithi za kimapokeo ambapo hadithi ni kipera cha
fasihi simulizi.Mfano Njozi iliyopotea (1980),Lina Ubani (1984),
Mashetani (1971)
5 . Matumizi ya mtambaji hasa katika tamthiliya,Waandishi wengi
wa tamthiliya wametumia mbinu ya utambaji ambapo wanakuwa na mtambaji
anayetamba hadithi fulani.Mfano, Lina
Ubani (1984),Nguzo mama (1980),Pambo (1975)
6.Matumizi ya mianzo ya hadithi za Fasihi simulizi,Mfano
tamthiliya ya Jogoo kijijini na ngao ya jadi(1970) Kilio Chetu (1995) ,Kivuli
kinaishi (1990),Riwaya hizi
zimetumia mianzo maalum ya fasihi simulizi mfano paukwa……,pakawa.
7. Matumizi ya Semi mbali mbali,Fasihi andishi hutumia semi mbalimbali ambazo ni ni
tanzu za fasihi simulizi.Semi ambazo hutumiwa sana ni
misemo,nahau,methali,tamathali ,vitendawili na tanzu nyingine
8. Matumizi ya Ushauri na nyimbo,Waandishi wengi hutumia sana
nyimbo katika kazi zao ili kuzipa mvuto,mfano Riwaya ya Njozi iliyopotea
(1980),tamthiliya ya Kilio chetu wametumia sana nyimbo
katika kufikisha ujumbe kwa jamii husika.
MADA NDOGO-1; UWASILISHAJI NA UENEZAJI WA KAZI ZA FASIHI
SIMULIZI
(a) UWASILISHAJI WA FASIHI SIMULIZI
Uwasilishaji
hutumiwa kuelezea njia au mtindo unaotumiwa kufanya kazi ya kifasihi iwafikie
walengwa .Mfano uwasilishaji wa maigizo ni kutendwa kwake jukwaani mbali ya
hadhira ya watazamaji.Tangu zamani, uzalishaji wa tanzu za mbalimbali za fasihi
simulizi huwasilishwa kwa masimulizi ya mdomo na matendo.
Fasihi
simulizi hubuni hadithi, nyimbo, methali n.k. zinazobaini hisia zao mbalimbali
kuhusu maisha na mazingira yao.Fasihi simulizi pia inaweza kuzungumzia historia
ya watu wa jumuiya Fulani itikadi zao na mambo mengine mengi wanayoyathamini katika
kuishi kwa pamoja.
Kwa
kuwa fasihi simulizi haiandikwi kuhifadhiwa kwake kunategemea kurithishana kwa
mdomo kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia hii kizazi kimoja kinaweza
kurithisha kizazi kingine yale mambo muhimu ambayo kinataka yaendelee katika
jamii hiyo mambo ambayo yamefungamana na mazingira yao maisha yao utamaduni wao
na itikadi zao.
(b)UENEZAJI WA KAZI ZA
FASIHI SIMULIZI
UENEZAJI:
Hutumiwa kueleza
uhusianokati ya hadithi na jamii mbali mbali.Nadharia hii huonyesha kuwa inawezekana kuwa jamii
zinazohusika ziliingiliana kihistoria au kutokana na ukaribu wao wa kijiografia
n zilihusiana kihistoria. kuingiliana huku kunaweza kuwa msingi wa kuwako kwa
hadithi zinazosimuliwa ambazo zinafanana katika jamii mbalimbali.
Mfano;utenzi wa Fumo Liyongo unapatikana
katika jamii kadhaa za pwani ya Kenya kama waswahili, wapokomo, wabajuni n.k.
Inawezekana kuwa kupatikana huku ni tokeo la ueneaji hasa kwa kuwa hizi ni
jamii zinazokaribiana kijiografia za zilizohusiana kihistoriau
SABABU ZA KUENEA KWA FASIHI SIMULIZI.
a) Kuanzishwa kwa vikundi vya
Sanaa na muziki,Vikundi mbalimbali vya Sanaa
na muziki vilianzishwa ambavyo kazi yake ni kuendeleza tanzu mbalimbali za
fasihi simulizi hapa nchini.Vikundi vya Sanaa za maonyesho, Vikundi vya taarabu
na muziki mfano, Ottu Jazz Band,Kilimanjro orchestra,Kilwa Band n.k vinafanya
kazi kubwa ya kueneza na kuendeleza fasihi simulizi hapa nchini.
b) Muingiliano na fasihi
andishi,Kuenea
kwa kazi ya fasihi simulizi kwa asili ni kwa mdomo na masikio yaani usimulizi,
hata hivyo maendeleo ya watu yamefanya baadhi ya kazi za fasihi simulizi zienee
kwa maandishi.Maandishi ni jitihada za kuhifadhi kazi ya fasihi simulizi na
kuifikisha mahali ili ikatambuliwe au isimuliwe.Hadithi mbalimbali kama vile Hekaya
za Abunuasi (1915),Hadithi za Esopo (1890),Fasihi simulizi ya mtanzania.Hadithi
(1977) .Hizi zote zimehifadhiwa na kuenezwa kwa maandishi.
Fasihi andishi inatumia vipengele mbalimbali vya fasihi
simulizi katika uandishi wake na hivyo kuviendeleza. vipengele hivyo kama vile
,Matumizi ya semi mbalimbali,Matumizi ya nyimbo,Matumizi ya hadithi ndani ya
hadithi,Matumizi ya mianzo na mishilizo ya hadithi za fasihi simulizi,Matumizi
ya majigambo, utani n.k.
Kwa sasa methali, vitendawili, nahau, vimewekwa katika
maandishi kwa ajili ya kumbukumbu za baadaye na hivyo vinaenezwa kwa njia ya
maandishi.
c)
Ufundishaji shuleni na vyuoni,mfumo wa Elimu nchini nao
umesaidia kueneza fasihi simulizi kwa kiasi kikubwa hapa nchini kwa sasa fasihi
simulizi ni somo linalofundishwa toka darasa la kwanza hadi ngazi za juu (chuo
kikuu)
Vile vile kuna vyuo hapa nchini vinavyofundisha baadhi ya
tanzu mbalimbali za fasihi simulizi kama vile Sanaa za maonyesho na muziki.
Mfano chuo cha Bagamoyo, Butimba, Nyegezi na chuo kikuu cha Dar-es-salaam.
d) Mabadiliko ya kiteknolojia.
Kutokana na maendeleo ya Sayansi na Teknolojia kwa sasa
fasihi simulizi inaenezwa kwa vyombo vya habari kama vile kaseti, redio, video,
luninga, mitandao ya kijamii n.k.Mfano Redio Tanzania (TBC) kupitia kipindi
chake cha “Mama na Mwana” “Watoto Wetu” vimesaidia sana kueneza fasihi
simulizi hapa nchini Tanzania. Luninga nazo zimesaidia sana kueneza fasihi
simulizi nchini kupitia vipindi mbalimbali vya michezo ya kuigiza.Hivyo
mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia hayawezi kuwa fasihi simulizi
E)Mwingiliano wa mataifa mengine.Katika mwingiliano muziki
umesaidia sana kukuza fasihi simulizi.Hali hii imesaidia kuleta muziki wa
kizazi kipya (muziki wa kufoka foka) pamoja na Rege vijana wa kizazi kipya wamechota miundo na
mitindo ya muziki kutoka nje na kuendeleza muziki wao ingawa madhui bado
wanajadili yale yale yaliyojadiliwa na wanamuziki wa zamani.Matumizi ya fasihi
simulizi katika Sayansi na Teknolojia yamesaidia sana kuenea kwa fasihi
simulizi kwani fasihi simulizi inapata hadhira kubwa kwa wakati mmoja lakini
hadhira hiyo haionani ana kwa ana na fanani wao kwa kutumia vyombo hivyo vya
Sayansi na Teknolojia.
ATHARI ZA SAYANSI NA TEKNOLOJIA KATIKA UWASILISHAJI NA
UENEZAJI WA KAZI ZA FASIHI SIMULIZI
Mwanzo
fasihi simulizi iliwasilishwa na kuenezwa kwa njia ya masimulizi ya mdomo hivyo
fanani na hadhira walionana ana kwa ana wakati wa uwasilishaji lakini zama hizi
za Sayansi na Teknolojia, uwasilishaji na uenezaji unatumia vyombo vya habari
kama vile redio, video, televisheni, kanda kunasia sauti, mtandao na hata
kompyuta, mara nyingi hasa hadhira haiwi ana kwa ana na fanani hutokea hadhira
ikawa inaangalia luninga au sinema au tamthiliya jukwaani kwenye mazingira kama
hayo si rahisi hadhira kushiriki kikamilifu katika utendaji.Kutokana na maendeleo
ya Sayansi na Teknolojia fasihi inaathiriwa katika vipengele vifuatavyo:-
1. Uwasilishaji. Mwanzoni fasihi simulizi iliwasilishwa kwa njia ya
masimulizi ya mdomo hivyo fanani na hadhira walikuwa wanaonana ana kwa ana
wakati wa uwasilishaji lakini katika kipindi hiki cha sayansi na teknolojia,
uwasilishaji wa fasihi simulizi unatumia
vyombo kama, vile redio, luninga, video, kanda, mtandao na hata kompyuta na sio
lazima msanii awepo.
2. Uhifadhi, kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia sasa fasihi
simulizi inaweza kuhifadhiwa vizuri Zaidi kuliko inavyofikiriwa na
wanamapokeo kwani leo hii fasihi
simulizi inaweza kuwekwa katika mkanda wa kompyuta (flash disc) CD, DVD,
Maandishi n.k na ikaendelea kuwepo kwa miaka mingi sawa sawa na fasihi andishi
hata zaidi.Kwa upande wa video na DVD, uhifadhi wake huendelea kuonyesha
vitendo na sauti huweza kudumu hata zaidi ya maandishi.
3. Wakati na mahali, zamani fasihi simulizi ilifanyika sana saa za jioni,
kando ya moto au barazani. Aidha kwa vile fasihi simulizi hutolewa redioni
inaweza kusimuliwa wakati wowote na mahali popote ambapo kipindi kinasikika na
kwa saa na wakati huo. Majumbani, mijini watoto hawazunguki moto tena, bali
husubiri wakati kipindi kinaporushwa kwa siku maalumu na wanaizunguka luninga
au redio.
4. Hadhira au ushirikishwaji wa hadhira, zamani hadhira ya fasihi
simulizi ilikuwa inaonana ana kwa ana na fanani wake wakati wa uwasilishaji
wake. Hadhira iliweza kuchangia kazi ya fasihi hiyo na hata kuathiri uumbwaji
wake, ikaitwa hadhira tende. Lakini katika muktadha wa maendeleo ya sayansi si lazima fanani na hadhira waonane ana
kwa ana .
MADA NDOGO-2 ;UHIFADHI
WA KAZI ZA FASIHI SIMULIZI
Kwa sasa fasihi simulizi inaweza kukusanywa na kuhifadhiwa
kwa njia zifuatazo:-
a)
Kichwa,uhifadhi wa fasihi simulizi
ni katika vichwa vya watu kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Jambo hili
limekuwa likifanyika kwa muda mrefu sana.Hivyo kutokana na kuhifadhiwa katika
vichwa ndio maana fasihi simulizi imekuwa ikirithishwa kutoka kizazi kimoja
hadi kizazi kingine.
b)
Maandishi, Tangu maandishi
yagunduliwe baadhi ya kazi za fasihi simulizi zimekuwa zikihifadhiwa kwenye
maandishi kwa ajili ya kumbukumbu ya baadaye. Kazi za fasihi simulizi
zikihifadhiwa katika maandishi inaweza kufanya watu wasijue ni simulizi au
andishi. Hata hivyo vidokezo kadhaa husaidiakujua kazi za fasihi simulizi kama vile kuwa na
mianzo maalum,mfano “Paukwaa! Pakawa! Au hadithi…….hadithi njoo” n.k.
Aghalabu fasihi simulizi huwa na mtiririko(muundo) wa moja kwa moja usio na
urejeshi.
c)
Kanda za kunasia sauti (tepu rekoda),Hii
ni njia moja wapo inayotumika kuhifadhi tanzu mbali mbali za fasihi simulizi.
Kanda hizo hushika sauti pamoja na vidokezo vyake, kwa hiyo wasikilizaji ili
wapate wanachokitaka lazima wanunue kanda hizo.
d)
Kanda za video, luninga na filamu z
sinema CD, DVD na Kompyuta/Tanakilishi.Mtandao, picha za video hurekodi sura na
sauti,Picha hizo hutembea na kuonyeshwa kwenye skirini ya video na
lunnga. Picha za sinema hupigwa kwa aina maalumu za kamera ambazo hupiga picha
za mfululizo katika utepe maalumu. Picha hizo huonyeshwa kwa mashine na
huonekana zinatembea, kamera nyingi za
sinema za siku hizi zina mitambo ya kurekodi sauti pia. Hivyo kwa kutumia
filamu za sinema na video tunaweza kuhifadhi na kuonyesha kazi za fasihi
simulizi.
ATHARI ZA MBINU MBALI MBALI ZA
UHIFADHI WA FASIHI SIMULIZI
KICHWANI
Uhifadhi wa kazi za fasihi simulizi
kichwani una matatizo yafuatayo:-
i)
Kumbukumbu za akili zinaweza kupungua au kufifia
au fanani kufa kabisa. Hali hii ikitokea fasihi simulizi hupotea.
ii)
Mtu anayehifadhi kichwani anaweza kubadilisha
mambo muhimu katika simulizi na hivyo kugeuza kiini cha masimulizi hayo.
iii)
Kutokana na mazingira pamoja na mabadiliko kuna
tatizo la kupata watu wanaoweza kuhifadhi kazi hiyo.
MAANDISHI
Uhifadhi
kwa kutumia maandishi una matatizo yafuatayo:-
Ø
Baadhi ya
mambo hayawezi kuhifadhiwa katika
maandishi. Mambo hayo ni yale yanayohusiana na utendaji, sauti, vitendo,
toni, kuimba, muziki n.k. Matokeo ya kukosekana kwa vitu hivi ni kwamba
ladha au athari ya kazi inayowasilishwa hupungua.
Ø
Kukosa sauti kwa hiyo msomaji anapaswa atie sauti na
mahadhi yake mwenyewe.Shughuli hii inaweza kuharibu au kufanya kazi ya
fasihi ipungue ubora wake.
Ø
Hakuna ushirikishwaji kati ya fanani na
hadhira, kwa hiyo hadhira inashiriki kwa kuona maandishi.
Ø
Haibadiliki kulingana na wakati na mazingira.
Hivyo huweza kudumu katika hali ile ile kwa muda mrefu kama ilivyo fasihi
andishi.
Ø
Inakuwa ya ubaguzi au watu wachache
yaani wale wanaojua kusoma na kuandika. Wale wasiojua kusoma na kuandika
itawawia vigumu kuelewa fasihi hiyo iliyoko katika maandishi.
Ø
Ni gharama kubwa,kuhifadhi
masimulizi katika maandishi, hii ni kwasababu uandishi hutumia kalamu na
karatasi. Hivyo hapa zinahitajika pesa za kununulia kalamu na karatasi na
gharama za uchapaji.
KANDA ZA KUNASIA SAUTI
Uhifadhi kwa kutumia
maandishi una matatizo yafuatayo:-
Ø
Kanda za kunasia sauti husikika sauti tu,
Matendo hayawezi kushikwa na hii kuathiri tena uhifadhi na utoaji wa kazi
za fasihi simulizi.
Ø
Hakuna ushirikishwaji wa hadhira
kwani fanani na hadhira hawaonani ana kwa ana kwa hiyo hadhira inashiriki kwa
kusikiliza kanda tu, sikio huathirika lakini jicho halioni.
Ø
Ni gharama, kuhifadhi fasihi
simulizi kwa njia hii kwani kununua tepurekoda pamoja na kanda zenyewe, betri,
spea hupatikana kwa shida na kwa bei ghali licha ya hiyo si wote wenye uwezo wa
kununua tepurekoda hivyo ni watu wachache sana wenye uwezo wa kuhifadhi fasih
simulizi kwa kutumia chombo hiki.
Ø
Haitabadilika kulingana na wakati au
mahitaji ya hadhira, Huweza kudumu katika hali ile ile kwa muda mrefu
kama ilivyo fasihi andishi.
KANDA ZA VIDEO, LUNINGA, FILAMU ZA SINEMA, CD, DVD, VCD NA
KOMPYUTA
Njia hii ina matatizo yafuatayo:-
v
Upungufu wa ushirikishwaji wa hadhira,Hadhira
haiwezi kushiriki ila inasaidia kufanya fasihi simulizi kupata hadhira kubwa
ingawa hadhira hiyo haionani ana kwa ana na fanani wao.Kanda hizo huwa
zinatazamwa na watu wengi hivyo kupata hadhira wengi kwa wakati mmoja ambao hawawasiliani
na fanani wao.
v
Ni gharama,kwani vitu hivyo
vinahitaji pesa nyingi za kununulia vifaa hivyo ambapo ni watu wachache wenye uwezo wa kununua vifaa
hivyo.
v
Haibadiliki kulingana na mahitaji ya jamii
au hadhira au wakati,Huweza kudumu katika hali ile ile kwa muda mrefu
kama ilivyo fasihi andishi
v
Vifaa hivyo vinahitaji mahali pazuri ambapo
panaweza kutunza vyombo hivyo kwa muda mrefu, endapo havitahifadhiwa hivyo kuna hatari ya kupoteza kilichohifadhiwa
katika vyombo hivi.
MADA NDOGO-3; KUHAKIKI KAZI ZA
FASIHI SIMULIZI.
Kazi za fasihi simulizi zinaweza kupimwa na kuonekana kama
zinafaa au hazifai. Kazi hizi hupimwa kwa kuzingatia uhusiano wake na hali
halisi ya jamii.Katika upimaji vipengele
vya fasihi simulizi huangaliwa jinsi
vilivyotumika.Upimaji wa ubora wa kazi ya fasihi simulizi hujumuisha umuhimu wa
mambo yaliyosemwa katika jamii inayohusika au namna mambo hayo yanayosemwa
Hivyo mhakiki atajiuliza maswali kama:-
Ø
Ujumbe utolewao hapa ni wa kweli na una manufaa
au la!
Ø
Je maadili yatolewayo hapa yanalingana na wakati
tulionao?
Ø
Je nahau, misemo, methali na tamathali za semi
zinalingana na jambo linalosemwa au la!
Ø
Je mtiririko wa matukio unasaidia msikilizaji
kuelewa kisa au unamchanganya?
Maswali ya namna hiyo yanamsaidia mhakiki kuelewa ubora wa
kazi ya fasihi simulizi.Pia yaweza kutumiwa na mtunzi wa kazi ya fasihi
simulizi ili kurekebisha kazi yake na kuifanya iwe bora Zaidi.
FANI KATIKA FASIHI SIMULIZI
FANI
Ni ule ufundi wa
kisanaa anaotumia msanii katika kazi yake
AU
Fani ni ustadi au ubingwa au mbinu ambazo msanii wa kazi ya
fasihi hutumia katika kuwasilisha ujumbe wake kwa hadhira yake.
AU
Fani ni Sanaa na
jumla ya vipengele vya lugha vilivyowekwa katika mpangilio mahususi ili
kutoa maana fulani kwa hadhira.
AU
Fani ni umbo lililosanifiwa ili kueleza hisia za fanani.
VIPENGELE
VYA FANI
1.Tukio,Katika tanzu za fasihi simulizi mara nyingi ni
lazima pawe na jambo au tukio ambalo huchukuliwa kama kiini au chanzo cha
utanzu utakaohusishwa fani au utanzu unaotumiwa na msanii hauibuki tu hivi
hivi.Tukio huwa ndio kishawishi cha fanani wa fasihi simulizi .Mfano: Nyimbo za
unyago huibuka katika mazingira yake, methali za kutuliza zaweza kutumiwa pale
ambapo pana majonzi ya aina fulani, kwa hiyo ni lazima pawe na tukio ambalo litachukua
chemichemi ya utanzu utakaotumiwa na fanani kuwasilisha ujumbe wake kwa
hadhira.
2.Mazingira/mandhari, Mazingira ni pale ambapo matukio ya
fasihi simulizi yaliibuka ama yalitokea.Ufundi wa kuchora mazingira unatoa
picha halisi, picha inayoonekana waziwazi juu ya mazingira yaliyohusika.Fasihi
simulizi hutegemea sana muktadha au mazingira maalumu hivyo tungo za fasihi
simulizi huwa zimejikita katika utamaduni wa jamii zinamoibukia vifaa ambavyo
vinatumika katika fasihi simulizi vinategemea mazingira yanayohusika, mfano
msanii anapodhaminia kutoa picha ya kuogofya anatumia mazingira ambayo
yanaogofya kama vile mazingira ya misituni na wahusika kama majitu ili kuleta
dhana ya hofu katika mazingira yake.
3.Muundo,Katika fasihi simulizi
muundo ni mpangilio na mtiririko wa kazi ya fasihi simulizi kwa upande wa visa
na matukio.Katika muundo kinachozingatiwa ni jinsi fanani alivyofuma na kuunda hata alivyounganisha
tukio moja na lingine kimoja na kingine, wazo na wazo, ubeti na ubeti na mstari
wa beti na mwingine.Kuna miundo mbalimali katika tanzu mbalimbali za fasihi simulizi, kama vile muundo
wa moja kwa moja na kuna muundo changamano,pia upande wa ushairi
Katika
mashairi kuna miundo mbalimbali ambayo hutumiwa kuainisha mashairi kwa kufuata
idadi ya mistari katika kila ubeti, miundo hii ndiyo hutupa mashairi ya tarbia,
tathilitha, takhmisa na n.k.Katika hadithi na hata katika tamthiliya waweza
kuwa na muundo ambao fanani ameanza kutoka mwanzo akaenda katikati na baadae
kumalizia kisa chake aina hii ya muundo unaitwa mtiririko shanga.Mtirirko
wa namna hii hujengwa kwa kutumia visa au vitukio mbalimbali na vinaweza
kuongezwa na kupunguzwa bila kupoteza maana ya hadithi au tamthiliya.
1. Mtindo,Katika
kazi ya fasihi mtindo ni ile namna ambayo msanii hutunga kazi yake na kuipa
sura ambayo kifani na kimaudhui huainisha kanuni au kaida zilizofuatwa kama
zilizopo ni za kipekee. Mtindo ni
upangaji wa fani na maudhui katika kazi ya fasihi kwa njia ambayo hatimaye
huonyesha nafsi na labda upekee wa mtunzi wa kazi hiyo.
Katika tamthiliya na
riwaya katika mtindo kinachotazamwa ni
matumizi ya nafsi,matumizi ya monolojia,masimulizi na dayalojia,matumizi ya
hadithi ndani ya hadithi,matumizi ya barua n.k
Upande wa mashairi
kuna mitindo mbalimbali kama vile Mtindo wa Pindu,mtindo wa kuhoji,mtindo wa
beti kubadilishana vina,mtindo wa kidato n.k na shairi linaweza kuwa la
vina na mizani au la kisasa ambalo halifuati kanuni za urari wa vina na mizani.
2.
Matumizi ya lugha.
Ni kipengele muhimu cha fani ya fasihi, lugha ndiyo
malighafi ya fasihi.Lugha inayotumika katika kazi ya fasihi ni lugha ya kisanaa
inayopambwa na inayokusudiwa kuibua hisia fulani kwa hadhira yake.Inaweza
kuathiri moyo ya hadhira na kulingana na jinsi inavyotumiwa kwa lengo la
kuchekesha, kukejeli, kubeza, kuchokoza, kutia hamasa au kushawishi
‘’
Fani lazima iwe na utanashati na ulimbwende wa kipekee wenye mvuto na mnato wa
kuteka na kusisimua hisi za wasikilizaji wasomaji au watazamaji’’(khatibu
1981:16)
Matumizi ya lugha fasaha, uteuzi wa misamiati na matumizi ya
misemo na methali zinazosadifu mazingira ya jaini inayohusika kufanya kazi hiyo
ya fasihi simulizi kuwa sumaku ya kuvutia msomaji, msikilizaji au
mtazamaji.Tamathali za semi za aina mbalimbali hutumika kujenga picha mfano ya
tamathali za semi ni kama vile sitiari, tashihisi, kejeli, kijembe,
tabaini,
tuniaba, tashibiha n.k.Taswira ni lugha ambayo huchora picha za watu,
vitu au mahali kwa kutumia ishara katika taswira unaweza kubainisha maelezo
ambayo jinsi yanavypangwa na msanii huweza kufanya hadhira zipate aina
mbalimbali za hisi za kunusa, kusikia, kuona na kugusa.Mara nyingi hutumiwa na
wasanii ili kunasa hisia zao kwa hadhira.
Hivyo wasanii hutumia maneno ambayo huumba picha kamili ya
kitu, hali, wazo, dhana au uzoefu fulani wa jamii inayohusika.Mara nyingi
matumizi ya picha huenda sambamba na ishara mbalimbali ili kuwakilisha vitu,
dhana au mawazo mengine.
3.
Upeo
Katika
fasihi simulizi upeo ni kama kilele cha kazi yenyewe, kuna upeo wa aina mbili
Upeo wa juu ,ni
zile sehemu za kazi hiyo ambazo hutosheleza haja za wasikilizaji au watazamaji.
Katika sehemu hii hadhira hupata majibu muhimu ambayo kazi hiyo imechelewesha
kwa kutumia taharuki mbinu rejeshi, mtindo wa kiutelezi n.k.Mara
nyingi watunzi wa kazi za fasihi huweka kipeo cha juu mwishoni mwa kazi zao ingawa si lazima kuwa na kipeo kimoja tu
wakati mwingine waweza kupata kazi ya fasihi simulizi ambayo haina kipeo kabisa
Katika kazi mbalimbali za fasihi wasanii hujenga mgogoro
ambao hujtokeza na kukua, jinsi kazi hizo zinavyokua, kipeo cha juu hutokea pale
ambapo msanii hujaribu kutoa suluhisho kwa mgogoro uliojengwa katika kazi yake.
Upeo wa chini ,ni
sehemu ambayo matatizo yaliyounda kazi ya fasihi yanatatuliwa.Upeo wa chini ni
pale ambapo haja na mataajio ya hadhira hayakukidhiwa, katika baadhi ya kazi za
fasihi vipeo vya chini hudhihirisha udhaifu wa kazi hiyo lakini katika kazi
nyingine upeo wa chini huwa umekusudiwa hivyo na mtunzi.Hali hii ya pili hujitokeza
hasa katika kazi ya fasihi ambayo upeo wa chini hutumiwa kwa lengo la
kushangaza hadhira.
4.
UCHESHI KATIKA KAZI ZA FASIHI
Ucheshi ni kipengele muhimu cha kifani katika kazi ya fasihi
hasa fasihi simulizi.Ucheshi ni mbinu ya kifani ambayo watunzi hutumia katika
kazi zao za fasihi kwa lengo la kuchekesha na kuburudisha hadhira na kuondolea
uchovu.
Wasanii mbalimbali hutumia mbinu tofautitofauti kuleta
vichekesho katika kazi zao.Baadhi yao hutumia vitendawili ili kujenga,
kejeli, dhihaka, n.k. vichekesho pia huweza kutumiwa ili kujenga
maudhui.
5.
WAHUSIKA.
Ni viumbe ambavyo hutumiwa na wasanii katika mtiririko wa
matukio kuelezea visa vyake.Wahusika wanaweza kuwa watu, miti, wadudu, mizimu, misitu
na wanyama.Wahusika huwa ni viumbe ambavyo vinatenda na kutendewa wanatumwa na
msanii kusimamia hali mbalimbali za binadamu katika jamii wanamoishi.
Hawa ndio uti wa mgongo wa fani ya fasihi simulizi, Bila wahusika
mtiririko wa matukio au visa hukosa pahali pa kujishikiilia.Wahusika si viumbe
maalumu wa mtunzi kwa vile ndiyo wanaotumia kutoa picha au kuwasilisha mawazo
na fikra zake kwa jamii inayowakilishwa na wahusika hao.Katika Fasihi
simulizi wahusika wanaweza kuwa binadamu
,wanyama,au vitu fulani vilivyopewa fursa ya mandhari na kauli kama binadamu.
VIPENGELE VYA MAUDHUI KATIKA FASIHI SIMULIZI
Ø MAUDHUI
Ni jumla ya mambo yote yanayosemwa na msimuliaji au
mwandishi katika kazi yake.Vipengele vya maudhui au umbo la ndani la kazi ya
fasihi ni kama vile
Ø
Dhamira,
Ni kusudio la mtunzi wa kazi ya fasihi.Kazi ya fasihi inaweza kuwa na dhamira kuu pamoja na dhamira
ndogo ndogo.Ubainishaji wa dhamira hufanywa na hadhira,hivyo dhamira hufahamika
kutokana na fasili za wasikilizaji au wsomi wa kazi ya fasihi.
Ø
Ujumbe: Ili
dhamira ya mtunzi itimie, msanii hutoa taarifa fulani fulani kwa hadhira
yake.Taarifa hizo huitwa ujumbe.
Ujumbe unaweza kutamkwa wazi au kwa uficho. Kwa mfano methali ya “Asiyesikia la mkuu huvunjika guu” ina ujumbe huu ukidharau maonyo ya wakubwa utapatamatatizo,Siku za mwizi ni arobaini ujumbe wa methali hii chenye mwanzo kina mwisho kwa kawaida
kazi moja ya fasihi inaweza kuwa na taarifa Zaidi ya moja.
Ø
Mafunzo: Ni
mafundisho au nasaha za mtunzi katika kazi ya fasihi.Mafunzo pia huwa na maana
kulingana na fasili ya hadhira. Mafunzo humfikirisha msikilizaji au msomaji kwa
njia ya ujumbe.Mfano katika ujumbe huu akaiba akafungwa hapa funzo ni tusiibe wakati mwingine kazi za fasihi
inaweza kutoa mafunzo mabaya (maadili) mtunzi anaweza kukusudia hivyo au
kutokusudia hivyo.
Ø
Migogoro:
Hii huelekeza kisa lakini hujizatiti juu ya migogoro ya maisha anayosimulia
fanani.Baadhi ya kazi za fasihi huonyesha ukinzano uliopo baina ya makundi ya
watu au hali ya aina moja dhidi ya hali nyingine kuna aina nyingi za migogoro
lakini Zaidi ni ile ya kisiasa, kiuchumi na kitamaduni au ile ya kibinafsi
mfano: matatizo yanayosababishwa na uzembe dhidi ya watetezi wa kazi (viongozi)
dhidi ya usasa katika mila na desturi husababisha mgongano wa kiutamaduni.
Ø
Falsafa: Ni
mafunzo makuu ya msanii (mtunzi) kuhusu maisha. Mawazo haya hutokana na
uchanganuzi wa kimantiki na huwa ndio hekima na busara za msanii (mtunzi)
huyo.Ni Imani ya mwandishi au fanani katika maisha juu ya utatuzi wa matatizo
katika jamii.
UMUHIMU NA UHUSIANO WA FANI NA MAUDHUI KATIKA FASIHI SIMULIZI.
Fani ni jumla ya mambo mengi yanayoijenga kazi ya
fasihi.Mambo haya ni kama vile muundo, mtindo, mandhari,wahusika na matumizi ya
lugha na maudhui ni jumla ya mawazo au dhamira, msimamo, mtazamo, falsafa na
ujumbe katika kazi ya fasihi.
Kwa ujumla fani na maudhui ni vitu vya muhimu sana katika
fasihi simulizi kwa sababu mtunzi hutumia vipengele hivi katika kujenga kazi
yake anayotaka kuwasilisha kwa jamii husika.Maudhui ni kila kina kinachosemwa
na fani ni namna kinavyosemwa.
Fani na maudhui ni vitu vinavyohusiana, vinaathiriana,vinategemeana na
kukamilishana katika kujenga kazi ya fasihi simulizi na kila kipengele kimo
ndani ya kingine
Mudhui hujumuisha viungo mbalimbali vya kazi ya fasihi
simulizi na fani ni mbinu za kisanaa zinazotumiwa na msanii ili kuvifanya
viungo hivyo viyasawili maisha kwa njia ivutiayo hadhira.kila kigezo (fani na
maudhui) kimo ndani ya kingine huku vikishirikiana na kuathiriana katika
kujenga au kubomoa kazi ya fasihi simulizi.
MADA NDOGO-4 ; KUTUNGA KAZI ZA FASIHI SIMULIZI
Utungaji ni uundaji wa mawazo na kuyapanga maneno
yakuwasilisha ama kwa njia ya mdomo au kwa njia ya maandishi.Utungaji unweza
kutolewa kawa njia mdomo aqu kwa njia ya maandishi.
Mambo ya kuzingatia
katika kutunga kazi ya fasihi simulizi.
i)
Kuwa na jambo lakuelezea (tukio).Mtunzi
anapaswa kuwa na jambo ambalo anaona kuwa linasababisha mivutano katika
jamii.Jambohilo lazima litoke katika jamii inayohusika na isiwe nje ya jamii
hiyo.
ii)
Kuteua utanzu atakaotumia.Mtunzi ni vyema kujua ni utanzu upi atakaotumia
katika kuwasilisha jambo hilo kwa jamii.Kwa kawaida fasihi simulizi ina tanzu
nne ambazo ni hadithi, ushauri, semi na Sanaa za maonyesho (maigizo).
iii) Kuteua
vipengele vya maudhui, mtunzi anapaswa aangalie nini dhamira yake, kuna
ujumbe gani kwa hadhira, hadhira itapata maadili gani na je migogoro ipi na iwasilishwe
vipi ili isipotoshe lengo zima la kazi yake.
iv) Kuteua
kipera kitakachotumika katika uwasilishaji wa kazi yake kwa hadhira,
mfano kama mtunzi ameamua kutumia utanzu wa hadithi; hanabudi kuchagua kipera
kimoja wapo kati ya ngano, soga, vigano, visasili au tarihi (visakale)
v) Uteuzi
wa vipengele vya fani. Baada ya kubaini vipengele vya maudhui, msanii
anapaswa aangalie namna atakavyowasilisha maudhui hayo kwa jamii.Hapa atatumia
au atashughulika na vipengele vya fani ambavyo atavitumia katika kuwasilisha
ujumbe wake.Vipengele hivyo ni muundo, mtindo, wahusika, matumizi ya lugha na
mandhari.Sehemu hii ndiyo ambayo mtunzi anatakiwa kutumia ufundi na ubunifu wa
hali ya juu ili kazi yake ieleweke, ielimishe na kusisimua hadhira.