SITIARI KATIKA KAZI ZA FASIHI
Wataalamu na wachambuzi wa fasihi wanakipa umuhimu mkubwa kipengele cha sitiari (uhamishaji wa sifa kutoka kitu kimoja kwenda chengine) miongoni mwa tamathali za semi katika fasihi. Kuna ambao wanafikia umbali wa kuhoji kuwa ni kipengele hiki pekee ambacho kinaweza kuipa uhai kazi ya fasihi na kuifanya isimame kwenye maana halisi. Sikiliza hapa mhadhara wa Profesa Kulikoyela Kahigi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mbele ya Kongamano la 29 la Kiswahili la Bayreuth, kusini mwa Ujerumani.
VITA BAINA YA UKALE NA USASA KWENYE 'KITUMBUA KIMEINGIA MCHANGA'
Kitumbua Kimeingia Mchanga ni tamthilia ya kimageuzi iliyoandikwa na Said Ahmed Mohamed na kuchapishwa na Oxford University Press East Africa Ltd inayojaribu kuonesha mgongano uliopo kati ya ukale na usasa katika jamii, ambapo mpishano wa kimawazo na kimtazamo baina ya wazee na vijana unayaumba na kuyaumbua mahusiano yao ya siku kwa siku tangu kwenye mambo makubwa na hadi kwenye madogo. Wazee wanachorwa kuwa wahafidhina wanaong'ang'ania ukale wao na vijana kama alama ya mabadiliko na mageuzi, ambao wanapigania kuishi maisha ya usasa. Kwenye gamba la nyuma la kitabu, kumeandikwa hivi:
"Fikirini hakubali kuchaguliwa mke na babaake, Bw. Mambo, na nyanyaake, Bi Haija. Wazee wake wanaona kuwa jambo la kumchagulia mke ni jukumu lao."
Hapa ndipo penye kiini cha mgogoro wote unaowasilishwa kwenye tamthilia hii, mgogoro ambao kwa hakika unawakilisha hali halisi ya jamii zilivyo katika nchi zetu hizi zinazojipapatuwa sasa kutoka maisha ya kijadi na kuingia katika maisha ya kisasa. Mtazamo wa vijana ni kuwa wanastahiki huwa huru katika maamuzi yanayohusu mustakabali wao, lakini wazee wanaamini kuwa ile dhima ya kuwa kwao wazazi inawapa haki na mamlaka yasiyo ukomo kwa watoto wao katika hali yoyote waliyo na hata kwenye umri wowote walio nao. Kwao wao "Mwana hakuwi kwa mvyelewe!"
Tamthilia inatuonesha kuwa ingawa imani ya wazee kwenye hili inakosolewa na vijana, haimaanishi kuwa wanakuwa na dhamira mbaya kwa watoto wao. Uamuzi wa wazazi, kwa mfano katika kumuamulia kijana wao mke au mume wa kuwa naye kwenye ndoa, si lazima umaanishe kuwa wazazi hao hawajali hisia za kimapenzi za mtoto wao, bali huenda unatokana na mapenzi yao kwake kuwa makubwa kuliko hisia za kijana huyo. Wazee wanaamini kuwa "Kuishi kwingi kujuwa mengi", na hivyo uzoefu wao kwenye maisha huwafanya kuwapa madaraka ya kudhania wanaijuwa ghaibu ya watoto wao.
Katika Onesho la Nne panapotokezea majibizano baina ya Fikirini na wazazi wake, Bw. Mambo na Bi Sikitu, tunayashuhudia haya:
Bw. Mambo: Unakiri na kukubali hayo? (kwamba mimi ni baba'ko na huyu ni mama'ko) Fikirini: Ninakiri Baba. Bw. Mambo: Ikiwa hivyo ndivyo, basi kwa nini sisi kukuchagulia dhahabu, wewe unaokota shaba? (Fikirini kimya, macho chini) Kwa nini…kwa nini basi hujali desturi na heshima ya ukoo huu? Bi Sikitu: Baba, mwanangu Fikirini, wazee wana sehemu ya kukutafutia wewe wema. Unaona mabaya sasa hivi tu, lakini baadaye utakuja kujua kuwa hatukutakii maovu.(Uk. 31-2)
Hivi ndivyo wazee wanavyoamini. Lakini kwa upande mwengine, vijana wanadhani kuwa wazee hawana haki ya kuwaingilia kwenye mambo yao kiasi hicho, hata kama kweli wanastahiki kupewa heshima kubwa. Wanadhani kuwa wanapowaingilia kwenye mambo yao, hawafanyi kwa sababu ya mapenzi yao tu kwao, bali pia kwa khofu na woga wa kuona nguvu na madaraka yao yanahatarishwa. Pia kwa kuwa wazee wana tabia ya kuyatilia wasiwasi kila yale yaliyo mageni kwao. Faki, rafikiye Fikirini, anamueleza sahibu yake huyo kwenye mazungumzo yao ya ufukweni:
"Wewe una homa ya uhuru wako kwamba utakuokowa na kukupeleka unakotaka. Wao wana homa ya kuudhibiti uhuru wako, kwa kuwa hawana hakika kwamba uhuru wako hwenda ukakandamiza uhuru wao. Yaani uhuru wako u dhidi ya uhuru wao." (Uk. 36)
Katika tamthilia hii, mgogoro huu unamalizika kwa ushindi kwa vijana - ushindi wa usasa dhidi ya ukale. Hatimaye, Fikirini anakubaliwa kumuoa amtakaye, Hidaya. Lakini hilo halikuja bure bure. Ni baada ya shindikizo kubwa kutoka kwake na mama yake. Roho ya mama kila siku inaonekana kulainika mbele ya mwanawe kuliko ya baba. Ni ajabu kuwa baada ya maelezo haya kwenye Ukurasa wa 27, Bi Sikitu alikuja kupata upumzi wa kuyameza maneno yake na kulikubali pendo la mwanawe liwe ndoa:
"Si mara moja wala mbili, nimeshamuona katiwa kati na wanaume; huku watano na huku sita, kakumbatiwa kitikiti njiani wanapita wakiyumba na kupepesuka na kucheka….na ubaya zaidi, nimepata habari za kuaminika kwamba kwa Hidaya kitumbua….kime'ngia mchanga!"
Harusi ya Fikirini na Hidaya ilibainisha kuwa khofu za wazazi wake hazikuwa za ukweli. Kitumbua hakikuwa kimeingia mchanga kwa Hidaya, bali ni kwa Zubeda, binti aliyeolewa na Badi, mdogo wake Fikirini, na ambaye alikuwa amechaguliwa na wazazi wake. Huko ndiko mambo yalikokuwa yameharibika.
Dhamira za Familia, Utamaduni na Malezi
Mbali na dhamira ya mageuzi, tathmilia hii inaibua pia dhamira nyengine nyingi yakiwemo masuala ya familia, mila unafiki na utamaduni. Kwa mfano, jinsi mkasa mzima wa kitumbua kilichoingia mchanga ulivyowasilishwa kutoka Onesha la Kwanza hadi Onesha la Tatu, unasema mengi kuhusu familia zetu za Mwambao wa Afrika ya Mashariki - nafasi ya mabibi katika nyumba zetu, mapishi yetu, mjengeko wa familia zetu na ukarimu na njia zetu za kufundishana.
Katika tukio moja, Bi Haja anatengeneza vitumbua na kuwapelekea wanawe, lakini kwa makusudi kabisa anavitia mchanga ili waupate ujumbe anaotaka kuwafikishia, bila ya kuwaambia neno. Na kabla hajaondoka, anawalezea namna ilivyokuwa shida kukitayarisha kitumbua kilicho kitumbua hasa, na namna inavyotia uchungu kuwa baada ya matayarisho yote hayo, anatokea mtu anakutilia kitumbua chako mchanga. (Uk. 5-6).
Pia, ule ukweli kwamba kumbe yule aliyedhaniwa kuwa kitumbua chake kiko safi hakijatiwa mchanga, yaani Zubeda, na akawa ndiye chaguo la wazazi wa akina Fikirini na akaolewa na mtoto wao, Baddi, ndiye ambaye chake kilishatiwa mchanga, unaonesha kiwango cha unafiki kilichomo kwenye jamii zetu. Pengine tukio lenyewe halioneshi kuwa wazazi wameshindwa kulea, lakini linaoenesha namna mwana alivyoshinda kuleleka.
Hilo halitoshi. Bw. Mambo, ambaye ni mhafidhina mkubwa anayepigania kulinda heshima ya familia yake kwa kumkataa katakata Hidaya asiwe mkwewe, kumbe naye ana yake. Anaonekana mwisho wa tamthilia hii akikamatwa na polisi kwa kujihusisha na biashara haramu ya madawa ya kulevya, kitu ambacho hakikuwa kikifanana kabisa na taswira yake. Kumbe alikuwa na sura nyengine aliyokuwa akiificha kwa mkewe na wanawe.
Ni hapo pia inapodhihirka kuwa kumbe siku zote hizo alikuwa na nyumba nyengine ya Bi Mosi, mke aliyemuoa tangu miezi sita iliyopita, huku mkewe wa kwanza, Bi Sikitu, akiwa hana taarifa nayo kabisa.
Yanapombainika mawili hayo, Bi Sikitu anazimia (Uk. 66).
'BABU ALIPOFUFUKA', RIWAYA INAYOAKISI UHALISIA
Riwaya ya 'Babu Alipofufuka' imeandikwa na mwandishi maarufu wa kazi za fasihi na mtaalamu wa lugha ya Kiswahili, Profesa Said Ahmed Mohammed, na kuchapishwa na Jomo Kenyatta Foundation mwaka 2001. Katika gamba lake la mbele, pameandikwa: "pengine ni riwaya ya ujasiri mno kupita zote Said A. Mohammed alizowaji kuandika." Na hivyo hasa ndivyo ilivyo - hii ni riwaya ya kijasiri, ya kimapinduzi. Hii ni riwaya iliyoandikwa kwa mtindo wa kejeli, lakini yenye mchomo mkali kwa wale wanaoelekezewa kejeli hiyo - yaani watawala waovu - na pia inayoibua hisia nzito kwa wale wanaoathirika na uovu wa watawala - yaani raia wa kawaida. Uovu wenyewe unadhihirishwa katika riwaya hii kwa namna ya tashnina na inda, lakini katika hali inayowiana sana na ukweli halisi uliomo katika maisha ya kila siku kwenye mataifa yetu ya dunia inayoambiwa inaendelea. Hadithi nzima inasimuliwa kupitia mazingira yasiyo ya kawaida. Huyo Babu mwenyewe Aliyefufuka anatujia kwa umbo la ajabuajabu kupitia kichwani mwa mjukuu wake, K, ambaye ndiye muhusika mkuu. K mwenyewe ni sehemu ya hao watawala ambao kwao kijembe cha riwaya nzima kinaelekezwa. Kwa ustadi wa hali ya juu, mwandishi anampa Babu nguvu za kuziunganisha dunia zetu mbili - baina ya ile tuionayo kwa macho ya nje na ile ionekanayo kwa jicho la ndani tu. Baina ya dunia hizi mbili, ndipo msomaji anapopewa taswira halisi ya tafauti za waziwazi na za kificho walizonazo wanaoishi ndani yao. Upande mmoja ni maisha ya starehe na anasa za watawala, kule kujilabu na kujitapa kwao, ule uroho na tamaa zao zisizokwisha. Upande wa pili ni maisha magumu ya watawaliwa, kule kutumai na kutamauka kwako, kule kuinuka na kuanguka kwao, na kule kupambana na kujipapatuwa kwao kutoka makucha ya "wenye dunia yao". Katika ukurasa wa 14 hadi 15, kwa mfano, tunakutaka na maelezo kuhusu K ambayo yanawasilisha hisia zake za kuutaka na kuupenda ufakhari kama ilivyo kawaida ya watawala wa aina yake: "Mbali na gari, kulikuwa pia na kasri la kuonewa fahari. Na fahari ndiyo madhumuni yenyewe. Na kasri lake K linamstahiki kwa kila hali, kwa kile cheo cha kiungo. Kama chumvi na chakula alikuwa. Bila ya yeye, mengi ya wakubwa na wadogo hayachapuki... Mjengo wa kasri lake ni wa aina ya zile husuni za tasnifa tunazoziona kwenye snema za filamu za sayansi ya kubuni." Wakati akina K wakiishi maisha hayo ya ukwasi na kujitanua, akina Kali ndio muhanga wa anasa hizo za watawala. Kwao maisha ni msegemnege na hali zao ni ngumu kupindukia. Huko ndiko kwenye 'maitikwenenda' kama wanavyoitwa na mwandishi na walivyowahi kuitwa na Sembene Ousmane kwenye God's Bits of Wood au Ayi Kwei Armah kwenye The Beautiful Ones Are Not Yet Born. Katika ukurasa wa 115 hadi 116, kwa mfano, tunasimuliwa maisha ya watu kula togonya na mboga ya kikwayakwaya sio kwa kupenda, bali kwa kuwa hawana namna nyengine. Huku ndiko ambako mtu anakwenda hospitalini kusaka matibabu, lakini anaondoka akiwa ameongezwa maradhi mengine zaidi kwa kuwa serikali imezitelekeza zahanati zake: "Walipofika zahanati, mlango ulikuwa wazi, lakini mwuguzi aliyekuwa zamuni hayupo. Ilichukuwa saa nzima mpaka alipopatikana. Alikuwa kenda kumpiga mtu sindano kwa pesa. Alipofika alimkagua Kali, alisema anahitajia wembe wa kumnyoa nywele. Kisha uzi wa kushonea anao lakini anahitajia sindano au shazia ambayo hanayo. Alisema japo ya kushonea nguo inafaa. Zaidi ya hayo hana vidonge vya kuondolea maumivu. Plasta pia hakuna... Kali akanyolewa bila maji, akashonwa bila ya sindano ya ganzi, akatiwa plasta na kupewa vidonge viwili vya asprini kubwia.... alipoondoka, juso na jichwa lake zima lilikuwa limemvimba." (Uk. 121-22) Huko kunaitwa Kataa na K anaamini kisa cha kuitwa hivyo ni kwa kuwa watu wa huko ni wakaidi na hawakubaliani hata kidogo na watawala wao. Ndiko hasa alikotokea K, lakini ambako mwenyewe amekutupa na kukusahau kwa miaka yote hiyo. Kwa ujumla, hali ya maisha ya watu wa huko ni duni sana, nyumba zao ni dhaifu na hawana pesa za kununulia hata mahitaji ya lazima: "Mbele zaidi waliposonga wakipasua kiini cha miti na mimea iliyokuwa mali kubwa hapo zamani, maisha na uhali yalianza kujiliza. Vibanda viwili vilivyolalia yombo. Kitambo,,, vibanda vyengine vitano vikirukuu. Hatua... vibanda vyengine vikisujudu.... ghafla walitokeza mahala ambapo ungeweza kupapagaza jina la sokoni. Watu walionekana... wamesogelea chanja zilizowekwa biashara... wote wametumbua macho, bila ya kuweza kununua chochote. Wengine wanavitumbulia macho vidaka vya nazi. Wengine vichungwa, vilimau, viembe na vipapai... kwenye soko la samaki, mafungu ya dangaauronga na dagaaupapa yakishindana kutumbuliana macho na watu..." (Uk. 95) Kwa hivyo, riwaya ya Babu Alipofufuka ni kielelezo cha usimulizi unaoakisi uhalisia wa dunia mbili zinazoishi ndani ya jamii moja kwenye mataifa yetu. Mwandishi anampa Babu nguvu za kumfanya mjukuu wake, muhusika mkuu K, azidurusu dunia hizo ambazo kwa kila hali zimekuwa sehemu yake - moja aliyotokea na akaikimbia na kuitelekeza na nyengine aliyokimbilia, kuipenda na kuitukuza. Babu yake alipofufuka na kumjia kwenye maisha yake ya ndani, ndipo anatoa wasaa kwa msomaji kuyaona yaliyomo kwenye nafsi za madhalimu na madhulumu na zinavyosawirika dunia zao. Baada ya kuziona dunia hizo, mwandishi anamfanya msomaji wake ahitimishe kwa mambo matatu haya: Kwanza, watu wa aina ya K, ambao wameendeleza dhuluma kubwa kwa kutumia vyeo na majina yao, huwa wanaishi na khofu ya milele ya kuporomoka. Matokeo yake, kila siku hutamani na kupigania kwenda juu na juu zaidi kusudi wasifikwe na walio chini, ambao wanadhani kuwa endapo mikono yao itawafikia tu, basi watawashika miguu na shingo zao na kuwaporomosha chini kwa kishindo kikubwa. Kwa hivyo, ishara yoyote ya kuporomoshwa huwatia jaka moyo kubwa na kuwatetemesha hadi machango. Katika ukurasa wa 92, mathalan, mwandishi anatuonesha namna K anavyogwaya akiliogopa anguko lake: "Ghafla alijihisi anachukuliwa na lepe jengine lililomdidimiza katka singizi zito la ajabu. Alitumbukia kwenye singizi huku akienda. Lilikuja tu kwa hakika hilo singizi ama upepo wa ghafla. Lilikuja kumvaa na kumdidimiza kwenye maweko ya chini ya kiini cha dunia. Alihisi anazama kwenye dimbwi refu lisilo ukomo... di, di, di... alididimia mpaka akajihisi ameibuka pahala penye mwangaza wa maisha. Akajihisi kama katupwa hapo. Katupwa kama gunia. Moyo ukaanza kupiga beni alipogundua hivyo. Aa, kubwagwa kila siku yeye alikuwa akikuogopa. Kuanguka alikuchelea. Akihofu kutupwa, hasa namna hiyo." Pili, msomaji anahitimisha kuwa watawala wa aina ya K wanakuwa wanajijuwa hasa kwamba wamewakosea raia. Kwa hivyo, kila wanapokaa huwa wanajitia wasiwasi kuwa wanaandamwa au wanafuatwafuatwa na watu hao wenye hasira na wakati wowote wanaweza kulipiziwa kisasi kwa maovu yao. Hayo ndiyo matokeo ya kuishi kwa dhuluma. Siku zote huwa unakhofu kuwa madhulumu wako watakurudi kwa yale uliyowatenda. Huwa huko huru. Angalia vile wanavyopita barabarani kwenye magari yaliyofungwa vioo vyote, tena vyeusi visivyopenya risasi na bado mbele yao ving'ora mita kadhaa ili wapishwe njia peke yao na bado maaskari kibao na bunduki. Hawa hawafanyi yale kwa kupenda, bali kutokana na khofu waliyonayo kwa umma walioukosea (Uk.24-7). Wakati Babu anamzukia K kwa mara ya kwanza kwenye ndoto-macho zake, alijitambulisha kwa namna hii: "Nikwambie tena, mimi ni babu yako; kisha niongeze kuwa mimi ni dhahiri kwa kisia kikubwa kuliko hata wewe, kwa sababu sina farakano na watu. Wala sina makiwa na utawa kama ulionao wewe. Sina hofu wala siogopi kama uogopavyo wewe. Nakwenda nipendapo. Nakutana na nimpendaye. Ufunguo wa kasi yangu ninao mwenyewe. Hakuna niliyemdhulumu." (Uk. 21-2) Tatu, msomaji anahitimisha kuwa khofu hizi za watawala zina uhalali wake na ni za kweli. Ni kweli kuwa wananchi walioonewa na kudhulumiwa kwa miaka mingi hufika pahala pa kusema "hapana" kwa watawala wao. Miongoni mwao huwa wanasema hivyo kwa maneno, wengine kwa vitendo, wengine wakiwa na akili zao na wengine tayari wameshachanganyikiwa kwa mateso ya muda mrefu. La muhimu ni kuwa wananchi hufika mahala wakasema "liwalo na liwe" lakini hawatakubali tena dhuluma nyengine dhidi yao. Katika ukurasa wa 92, K alimkuta Mussa katika eneo la Kataa akijisemea peke yake njiani: "La, hatutaki, hata ikiwaje hatutali tena.... La, hatutaki, hata iwaje hatutali tena.... La, hatutaki, hata ikawaje, hatutali tena.." Lakini madhulumu wengine huamua kwenda mbali zaidi ya kupita mitaani wakijisemea peke yao tu. Wao huamua kuwarudi madhalimu wao kwa namna yoyote ile wanayoiona inawafalia na wanaimudu. Mno yachosha eti! Na ni hiki ndicho ambacho kinadhihirika mwishoni, pale umma uliokwishachoshwa na udhalimu wa watawala wao, unapoingia barabarani na kuukabili mkono wa utawala. "Nje aliwakuta wale mahasimu zake wamejipanga upande huu na huu wa njia. Sasa walikuwa mamia kwa mamia... Kuna waliochukuwa marungu na wengine mabango yaliyoandikwa maneno mengi...M'MEZIFISIDI NAFSI ZETU.... MMEVUNJA HESHIMA ZETU.... VIJANA WETU WANAPOTEA... VIFO NA NJAA NA MARADHI SABABU SI SISI... HATUNA NAFASI PANAPOSTAHIKI NAFASI ZETU... ARDHI INACHUKULIWA HIVI HIVI TUNAONA.... KESHO YETU IMO KATIKA GIZA...TUNAANGAMIA...TUMESHAKWENDA KAPA...na zaidi na zaidi...Mlio ule wa bunduki K aliusikia ndani apokuwa tayari ameshakua kitini ofisini mwake. Alitetemeka kwa muda. Lakini alipojishika, aligunduwa kwamba hata ofisini mambo yalikuwa yamegeuka pia." (Uk. 154-56) Riwaya inamalizika kwa kumuonesha K akipoteza kila kitu - ulwa, nyumba, gari na, zaidi kuliko yote, hata ile heshima aliyojidhani alikuwa nayo. Na mwisho anakufa kifo cha kidhalilifu kama alivyosababisha maelfu ya wengine kufa katika udhalilifu kwenye zama za madaraka yake. "Alfajiri ya siku ya pili, watu wa kijiji kile waliamshwa na sauti ya jibwa kubwa, Biye aliloliita Doggy. Ilikuwa si kawaida jibwa kubwa kama lile kubweka kwa muda mrefu namna ile hapo kijijini. Walipoufuata mbweko wa jibwa, walimkuta K ananing'inia kwenye kigogo cha mti uliokuwa umeota katikati ya kaburi la Babu. Alikuwa mkavu keshang'ang'anaa." (Uk.165) Naam, hapa ndipo hasira ya umma ilipomfikisha K. Hapa, kwa hakika, ndipo kiuhalisia wafikishwapo watawala madhalimu wa aina yake. Hivyo ndivyo umma unavyomuhukumu mkosaji wake. Umma ukikosewa kiasi kikubwa kama hiki, ni wenyewe ndio ambao hushitaki, na wenyewe ukahukumu. Na hivi ndivyo Babu Alipofufuka na kumtahadharisha mjukuu wake, K: "...Pia unashitakiwa na wakati ulioutumia vibaya...Unashitakiwa vile vile na matendo yako mwenyewe...matendo ya upotofu...Maovu yako mwenyewe....Hakuna uchaguzi. Huna njia. Wakati ukifika, utakwenda tu; utakwenda tu..." (Uk. 137)