MAANA YA NADHARIA
MAANA YA NADHARIA
(Williady, 2013), Nadharia ni
maelezo yakinifu kuhusu kitu, tajiriba, mahalifa au upumbavu na
mafanikio au maangamizi yanayochomoza katika jamii. Hivyo nadharia
hufungamana na mambo mbalimbali ya jamii kama vile mbinu, maarifa,
tasinifu, mikabala na mienendo mbalimbali ya jamii.
1. NADHARIA YA UPOKEZI (MWITIKO WA MSOMAJI)
Nadharia ya Upokezi (mwitiko wa
msomaji) ambayo husisitiza nguvu ya msomaji. Nadharia ya Upokezi
(Reception Theory) iliasisiwa na wahakiki wa waasisi wa Kijerumani
mwishoni mwa miaka ya 1960.Miongoni mwa waasisi wa nadharia hii ni
Robert C. Holub,Hans Robert Jauss na Wolfagang Isser.Katika kitabu
chake Reception Theory (1984), Holub anaelezea nadharia ya Upokezi kuwa
ni Mabadiko ya jumla ya umakinikiaji kutoka kwa mwandishi na kazi yake
kwenda kwa matini na msomaji”
Nadharia ya upokezi inaakisi
mabadiliko ya mbinu katika historia ya fasihi na ilizingatiwa kama jibu
kwa jamii,wanazuoni na maendeleo ya fasihi huko Uerumani
Magharibi mwishoni mwa miaka ya 1960.Kwa mujibu wa Holub, nadharia ya
Upokezi ulikuwa ni njia ya Kimapnduzi kwa wahakiki wa kisasa.
Waitifaki wa nadharia hii
wanashiilia msimamo kuwa kazi ya fasihi hupata maana baada ya matini na
msomaji kuadhiriana.Msomaji au mpokeaji ndiye huipa maana kazi ya fasih.
Kwani huiona na kuilinganisha
na uzoefu wake wa maisha. Kielelezo hiki kipya cha uhakiki hutilia
maanani dhima ya msomaji.Hans Robert Jauss katika makala yake “The change in the Paradigm of Literary Scholarship” (1926)
ambaye anachukuliwa kama mmoja wa mihimili ya nadharia hii ya Upokezi
anaelezea umuhimu wa kuielezea kazi ya Fasihi.Isser anaiona kazi ya
Fasihi kama kitu au tukio lililo nje ya muktadha na historia.
Anasema kuwa ili kazi ya fasihi
ieleweke ni lazima ushiriki wa msomaji uoane au upatane na maana
inayojitokeza katika kazi ya Fasihi.
Kwa hiyo basi , nadharia ya
Upokezi hufasili Fasihi kama mchakato wa namna msomaji na
wanavyoathiriana.Uzoefu wa maisha wa msomaji unaweza kutoa tafsiri
tofauti kwa kazi ya fasihi kutoka msomaji mmoja na mwingine.
2.NADHARIA YA ONTOLOJIA YA KIBANTU.
Nadharia
ya Ontolojia ya Kibantu. Kuna wataalamu mbalimbali waliozungumzia
nadharia hii. Kwa jumla, wataalamu hawa wameeleza maana ya Ontolojia
kuwa ni mtazamo unaohusu kuwepo kwa kitu katika dunia na kuangalia vitu
katika uhasilia wake (Nicholaus 2011).
Ontolojia
inaweza kutazamwa kwa namna tatu: kama taaluma, kama falsafa na kama
nadharia. Hivyo kwa kuwa utafiti huu ulichunguza “Mabadiliko ya
kiuandishi kutoka kanuni za Ki-Aristotle kwenda kanuni za jadi ya
Ki-Afrika”, kipengele cha Ontolojia ya Kibantu kinachoweza kutumika
katika kazi za fasihi, tuliona ni vyema kutumia Ontolojia kama nadharia
katika utafiti huu, kwani imewezesha utafiti huu kufikia malengo yake,
pia ilihusiana na mada iliyoshugulikiwa.
Kimsingi
kuna mitazamo minne kuhusu Ontolojia ya Kibantu. Mitazamo hiyo ni, ule
wa falsafa ya kisiasa (Itikadi ya kisiasa), mtazamo au falsafa ya
Kihikimati (Sagacty), wanafalsafa waliojikita katika kurekodi imani
katika utamaduni wa mwafrika (Ethnofilosofia), na falsafa ya Kiuweledi.
Wanaitikadi
wa kisiasa walichunguza masuala ya undugu wa kifamilia, ujamaa na
kujitegemea ndani ya Afrika. Wanasiasa hao ni Julius Nyerere, Leopold
Senghor na Kwame Nkurumah. Lengo lao lilikuwa ni kutaka kutafuta uhuru
wa kweli kwa waafrika ili kurudisha heshima kwa mwafrika kama
ingewezekana.
Mtazamo
wa Kihikimati umejikita katika masuala ya uhuru, hekima na desturi za
watu. Waanzilishi wa mtazamo huu wameshawishika kwamba falsafa ya
kiafrika haiangalii vitu vyote vinavyohusu kazi. Lengo lao walitaka
kuonesha kwamba ujinga sio hali ya kifalsafa na ujinga upo kwa kila
jamii, ujinga wa mwenzako waweza kuwa uhuru kwake. Waanzilishi wa
falsafa hii ni Odera H. Oruka na Marcel Griaule’s.Marcel Griaule’s
alifanya mazungumzo na Oyotemmeli kiongozi wa kabila la Wadogoni na
matokeo yake walipata falsafa ya kidini ya wadogoni.
Ethnofilosofia
hujishughulisha na ukusanyaji wa mitazamo ya kiulimwengu kutoka katika
tamaduni mbalimbali za waafrika. Hii imejikita katika masuala ya imani,
masimulizi na misemo ya watu. Muunganiko huo umeunganishwa na Paulin
Hountondji. Wengine waliojihusisha na falsafa ya kiafrika katika
mtazamo huu ni Placid Tempels, Leopald Senghor, John Mbiti na Alex
Kagame. Hivyo, mtazamo huu umejikita zaidi katika masuala ya mila,
desturi na imani za jamii.
Falsafa
ya Kiuweledi imejikita katika uchambuzi na ufafanuzi wa ukweli. Zaidi
inajihusisha na uhakiki, na hoja ndizo sifa za msingi kwao. Waanzilishi
wa falsafa hii ni Paulina Hountondji, Kwasi Waredu, Odera Oruka na Peter
Bodunrin. Wanasema kuwa falsafa ya kibantu kwa sasa inaitwa
Metafilosofia, na imejikita katika kuangalia maudhui ya msingi. Wao
wanahoji kwamba falsafa ya Afrika ni ipi?
Roberto
(1996) anasema Ontolojiani nadharia inayohusu kuwapo, yaani ni nadharia
inayoangalia yaliyokuwepo na yale ambayo hayakuwepo, halisi na yasiyo
halisi, tegemezi na vinavyojitegemea.
Parrinder
(1969) anasema kuwa nadharia ya kibantu inahusisha mwafrika na imani
yake. Hujumuisha maisha, mazingira pamoja na fikra zake. Pia anasema
kuwa mawazo ya mwafrika hujengwa katika misingi ya nguvu mbalimbali
ambazoni Mungu, binadamu, wanyama, mimea na kadhalika.
Wataalamu
wengine waliozungumzia nadharia ya Ontolojioa ni: Husserl (1913),
Tugendhat (1928), Wolff (1928), Gruber’s (1993), Bolzano (1996),
Guariono (1998), Wamitila (2008) na Cocchiarella (2007).
Kwa
jumla, wataalamu hawa wameeleza mengi juu ya nadharia hii, jambo
lililosisitizwa sanana wataalamu wengi waliojadili nadharia hii ni
kuhusu uchaguzi wa Ontolojia nzuri na namna ya kutumia nadharia hii.
Wanasema Ontolojia nzuri ni ile inayohusisha njia za Kisayansi na
kutupatia njia chache na rahisi ambazo zitaelezea mambo mbalimbali
katika ulimwengu. Pia nadharia hii inatukuza sana Ubantu na kumuona
mwafrika kama kiumbe bora mwenye uwezo wa kubuni na kusimamia mambo yake
kwa usahihi. Mbali na kutumia Ubantu (U-Afrika), nadharia hii inaeleza
mambo kadhaa ambayo ni sehemu ya ufahari kwa waafrika, mambo hayo ni
pamoja na dhana ya familia pana, kuamini uzazi kuwa ndio njia ya uzima
wa milele, yenye kuhashiria umuhimu wa binadamu, na Ugumba ni laana na
utupu kwa binadamu, kuabudu katika Mungu na miungu na kuheshimu Wahenga.
Pia huhusisha na imani kuhusu uchawi, na sihiri, na ndani yake kuna
masuala ya uganga. Pia umri kwa waafrika una nafasi kubwa sana katika
jamii na unabeba hekima za mtu.
3.UJUMI (AESTHETICS)
Ujumi ni nini?
Ujumi ni tawi la falsafa linaloshughulika na uzuri, ubaya, ladha, n.k.
AU
Ujumi ni elimu ya sheria na kanuni za sanaa.
Neno
ujumi kwa kiingereza linajulikana kama “Aesthetics”. Neno hili
limetoholewa kutoka katika lugha ya kigiriki “Ais - thesis”, likiwa na
maana ya “Hisia” (Feelings), hasa hisia za akilini (Mental perception).
Alexander
Gottlieb Baumgarten (mjerumani) ni miongoni mwa wanafalsafa
yalioshungulikia kwa kina juu ya falsafa hii ya Ujumi. Baumgarten
alidokoa baadhi ya mawazo fasaha kutoka kwa Leibniz. Leibniz
alizungumzia mambo makubwa mawili amabayo ni LOGOS na ETHOS.
LOGOS, ni
mantiki itokanayo na neno la maharifa au sababu ipelekeayo uwelewa mpya
au kuyachekecha mawazo makuukuu na kupata neno lenye kuchukua mkondo
mpya.
ETHOS, ni desturi ama mguso, tabia ama kaida Fulani ndani ya jamii ambazo hufanya matakwa yahusuyo jamii Fulani tu.
Baumgarten, alikiendeleza kipengele cha mguso na hisia na neno “Aesthetics” likaanzishwa.
Kabla falsafa mpya ya Aesthetics haijachukua kasi yake, hapo awali
masuala ya hisia yaliwekwa chini ya nadharia ya hisia za akili (mental
perception). Dhana ya ujumi ilitoka kwenye nadharia ya hisia za akili katika
karne ya 18 na kuitwa “Falsafa ya uzuri” au “Falsafa ya sanaa” au yote
mawili kwa pamoja. Baadaye ujumi uliachana na falsafa na kuwa tawi
linalojitegemea la elimu.
Kabla ya Baumgarten, ushairi na sanaa kwa ujumla ilijadiliwa kitaalamu
katika kapumoja. Hii inamaana kwamba ushairi haukutofautishwa na muziki
au uchoraji ama ususi, vyote vilielezwa kwa pamoja.
Baumgarten akaigawa dhana hii katika maeneo mawili ambayo ni uzuri na sanaa.
1. UZURI (The good or the truth).
Uzuri ni ukamilifu wa hisia za akili unaoleta kulitazama jambo au mambo
Fulani katika mtazamo chanya, haijalishi, kwani mwingine anaweza
kulichukulia jambo hilo kimtazamo hasi lakini mtazamo wake hauondoi
uzuri wa chanya kwa atazamaye chanya.
2. SANAA
Sanaa ni ufundi wa kuunda jambo. Twaweza kuueleza uzuri kupitia sanaa.
Sanaa yaweza kuupambanua uzuri kwa viwango vya juu zaidi kuliko jambo
lolote lile.
Tafadhali wasiliana na mwl. Majumbeni kwa,
4. NADHARIA YA UFEMINISTI ( Mtazamo wa kike)
(Williady,
2015) Nadharia hii inahistoria ndefu duniani, ikimaanisha ni moja ya
nadharia zilizopata kutokea miongo mingi iliyopita. chanzo cha kuibuka
kwa nadharia hii ni vuguvugu la kutaka kufuta kabisa uonevu wa mwanaume
kwa mwanamk. nadharia hii inadai kuwa chimbuko lauonevu na
ukandamizaji unaofanywa na wanaume kwa wanawake ni uroho wa mwanaume
katika kumtawala mwanamke. Kwaufupi, ajaenda kuu ya ufeministi na
mafeministi ni kumaliza kabisa utawala wa mwanaume kwa mwanamke.
moja
ya wadau waliochangia sana kuendelea kwa nadharia hii kwa kasi ni Adrew
Dworkin. Mwaka 1976, akiwa katika mji mkuu wa Uingereza, London, alitoa
mapendekezo makali katika kukomesha utawala wa mwanaume kwa mwanamke,
Dworkin anasema: Ili kufanikisha, tunahitaji kubomoa kabisa muundo wa
mihimili ya utamaduni wa jamii kama vile sanaa, kanisa, sheria, kaya
zinazodhibitiwa na baba, jamii na taswira zote za asasi, mila,
desturi ambazo zinamwona mwanamke kuwa mtu ovyo.
WATAALAMU MBALIMBALI WALIVYOZUNGUMZIA MAANA YA UFEMINISTI
Nadharia ya Ufeministi imefasiliwa na wataalamu mbalimbali kama vile:
Wamitila
(2003:253), hii ni nadharia ambayo imewekewa msingi na msukumo mkubwa
pamoja na nia ya kupigania ukombozi wa mwanamke kutokana na pingu za
kiutamaduni, kidini, kijamii, kisiasa na kiuchumi. Hii ni nadharia
ambayo inasaili na kudadisi itikadi ya kiume ambayo imekuwepo katika
jamii kwa kipindi kirefu. Kudadisi pia fasiri za kiume za fasihi pamoja
na mikabala ya kiubabedume.
Ntarangwi (2004:45), ni nadharia ambayo inajaribu kukiuka mitazamo ya kiume ambayo yaelekea inatumiwa sana katika jamii.
Mukobwa
M. nadharia ya ufeministi imetokana na mkondo na harakati za kutetea
haki za wanawake ulimwenguni na imejikita katika imani ya usawa wa
kijinsia, kijamii, kisiasa na kiuchumi.
(Williady,
2015) Ninadharia iliyojaribu kuvunja mwiko wa mfumo dume hapa dunia kwa
kuanzisha mapambano ya usawa wa kijinsia, bilashaka majaribio haya bado
hayajafanikiwa.
Kwa
jumla, nadharia ya ufeministi ni nadharia iliyojikita katika kupinga
ukandamizaji wa mwanamke katika jamii hususan katika nyanja za kisiasa,
kiuchumi, na kiutamaduni.
KUIBUKA KWA UFEMINISTI NA HARAKATI ZA KUIENDELEZA NADHARIA HII
Uhakiki
wa kifeministi ulishika kasi miaka ya 1960 na kuendelea kukua na
kuishia kuwa muhimu katika miaka ya hivi karibuni. Zipo kazi kadhaa
zilizoandikwa kabla na kulimulika suala hili kwa namna moja ama
nyingine. Kazi kuu mbili zinazorejelewa hapa ni A Room of One’s Own ya Virginia Woolf na A virdiction of the Right of women ya Mery Wollsto Necraft.
Hata
hivyo, kazi iliyoishia kuwa na mchango mkubwa katika kuuweka msingi wa
uhakiki wa ufeministi ni kazi maarufu ya mwandishi wa Kifaransa, Simone
de Beauvoir iitwayo, The Second sex, 1952 katika kitabu hiki,
mwandishi huyu anachukuwa mkabala wa kiharakati kwa kushambulia na
kukosoa baadhi ya asasi zinazochangia katika kumdhalilisha au kumdunisha
mwanamke. Asasi kuu anazozishambulia ni ndoa, dini na utamaduni.
Nadharia
ya ufeministi ilichimbuka huko Marekani katika harakati za kukomesha
biashara ya utumwa mwaka 1830. Wanawake wakaanzisha harakati za
kupigania haki za mwanamke.
Wamitila (2006:160-161) na Ntarangwi (2004:52-56) wamebainisha malengo mbalimbali ya ufeministi.
Ni
kweli kwamba kuna baadhi ya malengo ya ufeministi yanakinzana na maisha
halisi ya mwanamke wa Kiafrika lakini baadhi ya malengo hayo yanasawiri
maisha halisi ya mwanamke wa kiafrika kama ifuatavyo:
Kubainisha
umuhimu wa mwanamke, kutokana na mwanamke kukulia katika jamii zenye
mfumodume. Umuhimu wake haukuonekana, ndiyo maana ikaanzishwa nadharia
ya ufeministi ambayo yenyewe iligundua umuhimu wa mwanamke katika jamii.
Umuhimu wake upo katika Nyanja zote za kiuchumi, kijamii, kisiasa na
kiutamaduni. Mfano, katika nyanja ya kisiasa mwanamke anaweza kuwa
kiongozi bora na mwenye ushauri. Hili linajidhihirisha katika riwaya ya Barua Ndefu Kama Hii iliyoandikwa na Mariama Bâ (1994). Mwandishi anathibitisha hili anaposema:
“Tunayo
karibu miaka ishirini ya uhuru! Lini tutampata mwanamke wa kwanza awe
waziri atakaye husishwa na maamuzi yatakayoongoza nchi yetu huko
tuendako? Kumbe nguvu walizonazo wakina mama, uwezo wao wa kupambana, na
kujihusisha kwao bila kutegemea kupata faida yoyote ni mambo ambayo
hayahitaji tena kuthibitishwa. Wanawake wamewainua wanaume wengi kwenye
ngazi za juu.” (uk.82)
Katika
nyanja ya kijamii, mwanamke ni mlezi wa familia. Mfano, Ramatulayi
anailea familia yake kwani ameweza kulipa bili ya maji, umeme bila hata
kumtegemea mwanaume. Mfano, mwandishi anasema:
“Licha
ya mzigo niliokuwa nao tangu zamani, nikaubeba na ule uliokuwa wa Modu.
Ununuzi wa vyakula muhimu ulinishughulisha kila mwisho wa mwezi.
Nilihakikisha kwamba sikuwa na upungufu wa nyanya au mafuta, viazi
mviringo na vitunguu wakati ambapo vyakula hivi viliadimika sokoni…
Nilikuwa mwangalifu kuzilipa bili za maji na umeme pindi zilipofika.” (uk.69)
Lengo
hili la ufeministi linakinzana na maisha halisi ya mwanamke wa
Kiafrika, kwa kuwa mwanamke wa Kiafrika anaonekana hana umuhimu katika
jamii, pia anaonekana kuwa dhaifu ambaye hawezi kuiendesha familia yake
bila msaada wa mwanaume hii ni kutokana na jamii nyingi kuendeshwa na
mfumodume.
Kuorodhesha
kuwa kihistoria wanawake wamekuwa ni tegemezi na wasaidizi wa wanaume,
ni kweli kihistoria wanawake wamekuwa wategemezi na wasaidizi wa
wanaume. Mfano katika tamthiliya ya Nguzo Mama iliyoandikwa na
Penina Muhando (2007) tunaona mhusika BI MOJA alivyokuwa akimtegemea
mume wake na kutaka anunuliwe kanga. Mwandishi anasema:
“BI MOJA: (kwa
Shaabani): Kama ulijua kufika sasa hivi nipe hela ya kanga bwana meli
meli hii hainikosi leo utanipa hela hizo kanga nikakate. Mwezi wa tatu
huu kanga sizijui.
Shaabani: Nimekuambia mimi hela sina. Sasa unataka nikaibe?”(uk.31-32)
Ni
kweli kwamba mwanamke wa kiafrika amekuwa tegemezi katika jamii, kwani
humtegemea mwanaume katika mambo mbalimbali ya kifamilia. Kwa mfano
kutafuta au kununua mahitaji ya nyumbani kama vile chakula, mavazi yake
na watoto wake au kulea watoto wake.
Kuondoa
ukandamizaji wa mwanamke kutokana na pingu za kiutamaduni, kijamii,
kidini, kisiasa na kiuchumi. Jamii nyingi za Kiafrika zimejengeka katika
mfumodume, hivyo basi jamii zinamkandamiza mwanamke kutokana na pingu
hizo. Katika kulithibitisha hili waandishi wa kazi za fasihi nao
hawakuwa nyuma kulizungumzia katika kazi zao na lengo ni kuondoa
mfumodume uliojengeka muda mrefu katika jamii.
Kwa
upande wa kiutamaduni mwanamke ameonekana kukandamizwa kwa kuonekana
hana mamlaka hata ya kurithi mali za mumewe au zake mwenyewe, badala
yake hata akifiwa na mumuwe anapigwa, anafukuzwa na kudhalilishwa.
Penina Muhando anayathibitisha haya katika tamthiliya yake ya Nguzo Mama kwa kumtumia BI SABA pale anaposema:
“Akalia Bi Saba tena akalia
Hana wa kumsaidia
Mumewe kafa nduguze wakaja juu
Pesa wamechukua senti tano haikubaki
Vyombo na nguo zote wakagawana
Roho ilimpasuka Bi Saba kuwaona hao ndugu
Walivyogombania mali wasiyoichuma…
Sasa juu ya yote haya wamerudi kufagia
Hata ufagio wamebeba
Na lawama kumtupia eti pesa kazificha.” (uk.39)
Pia
mwanamke anaonekana anajishughulisha na kazi mbalimbali za kujiletea
maendeleo yake binafsi lakini anarudishwa nyuma kwa kukandamizwa na
mwanaume. Penina Muhando anayathibitisha haya kwa kumtumia BI PILI
ambaye alikuwa anapika pombe ili kujikwamua katika hali ngumu ya maisha
lakini mumewe SUDI alizichukua hela zote alizokuwa alizozipata. Kwa
mfano, mwandishi anasema:
“BI MSIMULIZI: Upishi wa pombe balaa ulimzushia
Visa na mikasa Bi pili havikumuishia
Pesa alizipata kutokana na hiyo pombe
Lakini visa vya pombe hiyo pesa hazikufidia”
SUDI: (kwa Bi Pili) Nani kalewa? Umeninywesha wewe?
Wee!hawara zako ndiyo wamekutia jeuri unaninyima pesa.
Toa pesa sasa hivi (Anampiga) Bi Pili anakimbia huku akilia.” (uk.16)
Vilevile,
mwanamke alikuwa anakandamizwa kwa kulazimishwa kurithiwa na kaka au
ndugu wa mume pindi anapofiwa na mumewe. Mwandishi analithibitisha hili
katika riwaya ya Barua Ndefu Kama Hii pale anaposema:
“Tamsiri, zitapike hizo ndoto zako za kutaka kuniposa.
Umeshakaa nazo kwa siku arobaini. Kamwe sitokuwa mkeo.”(uk.81)
Kwa
upande wa kisiasa, mwanamke amekuwa akikandamizwa kwa kuonekana hawezi
kuwa kiongozi bora wa kuiongoza nchi ndio maana hata nafasi za wanawake
zilikuwa chache huko bungeni. Katika riwaya ya Barua Ndefu Kama Hii iliyoandikwa
na Mariama Bâ mwandishi anayadhihirisha haya kwa kumtumia Ramatoulayi
ambaye akilalamika kuhusu ukandamizwaji wa wanawake huko bungeni pale
anaposema:
“Wanawake
wanne, Dauda, wanne miongoni mwa wabunge mia moja uwiano gani huu wa
kimzaha! Wala hakuna uwakilishaji wa kimkoa” (uk.81)
Kwa
upande wa kijamii, mwanamke amekuwa akikandamizwa kwa kupigwa na mumewe
bila sababu zozote za msingi. Hili linajidhihirisha katika riwaya ya Rosa Mistika iliyoandikwa
na Euphrase Kezilahabi (1988) kwa kumtumia mhusika Zakaria ambaye
alikuwa anampiga mkewe bila sababu. Mwandishi anasema:
“Regina
tangu aolewe hakuwa na raha! Alikuwa akisumbuliwa na kuteswa na mumewe
kwa kosa lisilokuwa lake. Katika kijiji chote cha Namagondo hapakuwa na
mwanamke aliyekuwa akipigwa karibu kila juma kama Regina. Wanawake wengi
kijijini walijiuliza kwa nini hakutaka kumuacha bwana wake. wengine
walimuonea huruma, wengi lakini walimuona mjinga.” (uk.3)
Pi,
mwanamke alikuwa anakandamizwa kwa kuonekana kuwa yeye ndiye mwenye
majukumu ya malezi, kwa hiyo hata watoto wakiharibika anayelaumiwa ni
mwanamke. Euphrase Kezilahabi analithibitisha hilo pale anaposema:
“Lete
hiyo barua iko wapi? Pamoja na shilingi ulizopewa unafikiri sisi hapa
maskini. Rosa alipigwa tena na tena. Makofi yalikwenda mfululizo hata
damu zikamtoka puani na mdomoni. Baba nihurumie sitarudia tena… Zakaria
hakujali alichukua fimbo na kuongozana na bintiye mpaka chumba cha
watoto hali akinguluma lazima unioneshe barua hiyo unataka kuniletea
umalaya wa mama yako hapa.” (Uk.7)
Vilevile,
mtoto wa kike alikuwa anaonekana hana thamani katika jamii, na watoto
wa kiume ndio waliopewa kipaumbele. Euphrase Kezilahabi anathibitisha
haya katika riwaya ya Rosa Mistika kwa kumtumia Zakaria ambaye
kabla ya kumpata mtoto wa kiume alikuwa anamnyanyasa sana mke wake
lakini baada ya kujifungua mtoto wa kiume manyanyaso yaliisha na
alimpenda sana mkewe. Mwandishi anasema:
“Zakaria
alirudi nyumbani siku hiyo. Alikuwa amekwisha pata habari hizo njiani.
Alimbeba mtoto. Alimpa pongezi mke wake. Regina sasa mji huu umekuwa
wako. Asante Regina alijibu akitabasamu, alijiona anauwezo wa
kuzungumza.” (uk.24)
Lengo
hili linakinzana na maisha halisi ya mwanamke wa Kiafrika, kwani
mwanamke hatakiwi kurithi mali yoyote pindi wazazi wake wanapofariki au
mumewe anapofariki. Pia mwanamke kushindwa kupewa nafasi ya kutoa
maamuzi yoyote katika masuala ya kiukoo. Kwa upande wa dini mwanamke
anakandamizwa na kuonekana dhaifu hivyo kutokuwa na nafasi ya kuongoza
waamini. Mfano, dini ya Kiislamu na baadhi ya madhehebu ya Kikristo.
Lengo
lingine ni kuzitambua na kuzibainisha dhamira kuu katika kazi
zilizoandikwa na wanawake. Dhamira kuu ni dhamira inayomsukuma mwandishi
katika kuandika kazi ya fasihi. Baadhi ya waandishi wanawake wameonesha
dhamira kuu katika kazi zao kama ifuatavyo:
Nguzo Mama iliyoandikwa
na Penina Muhando (2007) imebeba dhamira kuu ambayo ni ukombozi wa
mwanamke. Ukombozi huo upo katika nyanja mbalimbali kama vile kijamii,
kiutamaduni, kiuchumi na kisiasa. Mfano, mwandishi ameonesha wanawake
wanavyojishughulisha katika kuinua uchumi wao, kwani walikuwa wakiuza
vitambaa na kupika pombe. Mwandishi anathibitisha haya kwa kusema:
“BI
TANO: Yaani mnasema mimi mvivu siyo nimezunguka mji mzima na zigo hilo
halafu mnaniambia mimi mvivu. Nawaambia watu hawataki kununua au mnataka
niwagawie bure.”
BI NANE: Lakini kwa nini wakatae kununua hivi, mbona vile vya mwanzo walivinunua? (uk.16).
Vilevile, Katika riwaya ya Barua Ndefu Kama Hii iliyoandikwa
na Mariama Bâ (1994) suala la ukombozi wa mwanamke limejitokeza kama
dhamira kuu. Ukombozi huu umejikita katika nyanja za kisiasa,
kiutamaduni, kijamii na kiuchumi.
Mfano, katika nyanja ya kijamii, mwandishi ameonesha jinsi ya kumkomboa mwanamke kielimu, pale anaposema:
“…Shangazi
Nabu anampeleka Nabu mdogo katika shule ya Kifaransa huko. Huko Nabu
alijifunza aina mbalimbali za mapishi, matumizi ya pasi na zana za
kutumia na kumenyea...” (uk.39)
Lengo
hili linakinzana na maisha halisi ya mwanamke wa Kiafrika, kwa kuwa
tangu mwanzo wanawake walikuwa hawaruhusiwi kuwa viongozi, badala yake
wanaume ndio waliochukuwa jukumu hilo la uongozi katika jamii. Pia,
wanawake hawakuruhusiwa kupata elimu wakitegemezwa katika majukumu ya
nyumbani na kuandaliwa kwenda kuolewa na kuja kuwa walezi wa familia.
Kuichunguza
historia ya kifasihi ya jadi ya kike na kuwamulika waandishi wa kike
waliotambua hali za wanawake na ambao wanaweza kuchukuliwa kama
vielelezo kwa wasomaji wao. Hapo awali kazi mbalimbali za kifasihi za
jadi za kike zilielezwa na waandishi wa kiume. Lakini nadharia hii
imemulika waandishi wa kike wanaotambua hali mbalimbali na wameamua
kuandika kazi mbalimbali ambazo zinaelezea matatizo ya wanawake. Mfano,
katika tamthiliya ya Nguzo Mama mwandishi anaelezea jinsi
wanawake wanavyonyanyaswa na kuachiwa majukumu ya kulea familia,
kuchukuliwa mali zilizoachwa na waume zao baada ya kufariki. Mfano,
mwandishi anasema:
“…Haa! Shemeji mmerudi kuchukua hata kitanda! Hata sufuria! Nitalala wapi na nitapikia wapi jamani!” (uk.39)
SUDI: Haya nipe pesa ulizokwisha kupata.
BI PILI: Hee! Kwa nini nikupe?
SUDI: Leta pesa upesi kabla sijakukong’ota.” (uk.13)
Mariama
Bâ naye ni kielelezo kwani ameelezea matatizo mbalimbali yanayowakumba
wanawake na namna wanavyokabiliana na matatizo hayo. Mfano mwandishi
anasema:
“… Ramatulayi, Acha nisikilize mimi zaidi; Redio ya Kankan ilinifahamisha kwamba ulikataa kuolewa na Tamsiri. Ni kweli? Ndio.” (uk.87)
Mwandishi
anaonesha jinsi mhusika Ramatulayi alivyojitambua na kukataa kurithiwa
na Tamsiri, pia anamkataa Dauda ambaye alitaka kumrithi baada ya kufiwa
na mume wake.
Kupitia
lengo hili tunaona wanaufeministi wameongelea kuhusu wanawake tu ambao
ni vielelezo katika kazi za fasihi, lakini wapo wanaume ambao
wamezungumzia masuala mbalimbali yanayowahusu wanawake. Mfano, Shaaban
Robert aliyeandika Wasifu wa Siti Binti Saad.
Kudhihirisha
kuwa kuna sifa fulani za kike na uzoefu fulani wa kike katika uwazaji,
hisia, kutathmini, kujiangalia na kuuangalia ulimwengu wao wa nje.
Uzoefu fulani wa kike unajitokeza katika uwazaji na jinsi wanavyousawiri
uhalisi. Kazi ambazo zinamsawiri mwanamke kwa njia chanya, mfano ni
riwaya ya Kiwasifu ya Shaaban Robert Wasifu wa Siti Binti Saad. Kuna
mashairi kadhaa aliyoyatunga mwandishi ambayo yanaendeleza suala hili
la uchanya wa wanawake katika jamii. Mfano wa usawiri wa wahusika
linathibitishwa pale mwandishi anaposema:
“Siti binti Saad,
Ulikuwa mtu lini,
Ulitoka shamba,
Na kaniki mbili chini,
Kama si sauti,
Ungekula nini?” (uk.22)
Hisia: mfano, katika riwaya ya Barua Ndefu Kama Hii kupitia mhusika Daba alivyomwambia mama yake kuhusu Benetuu. Mwandishi anasema:
“Hasira
ya Daba iliongezeka zaidi jinsi alivyozidi kuichambua hali ilivyokuwa.
“Mama! Vunja ndoa yako! Achana naye mtu huyu hajatuheshimu, si wewe wala
si mimi… sitaki kukuona unagombania mwanaume na mwanamke mwenye umri
sawa na mimi.” (uk.52)
Lengo
hili la wanaufeministi, linaendana na hali halisi ya wanawake wa
Kiafrika, kwa kuwa mawazo ya mwanamke jinsi anavyojiwazia yeye mwenyewe
au kuwawazia wanawake wenzake hutofautiana . vilevile, hisia za mwanamke
zinaweza kudhihirika katika maandishi na kuonesha jinsi wanavyowaza
katika hali ya kawaida.
HITIMISHO
Lengo
la nadharia ya ufeministi lilikuwa ni kuondoa unyanyasaji wa kijinsia
hasa kwa mwanamke. Hivyo basi, malengo ya ufeministi yalijikita katika
kumnasua mwanamke kutoka katika pingu za kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni
na kijamii. Malengo haya ndiyo yanayoleta ukinzani wa maisha halisi ya
mwanamke wa Kiafrika. Hali hii imeleta mabadiliko katika maisha ya
wanawake wa kiafrika, kama vile kutaka haki ya elimu, kumiliki mali,
kurithi mali, kutaka nafasi za uongozi, pia kuwa na maamuzi ya kifamilia
au kiukoo, katika kupingana na pingu za maisha.
Nadharia ya Uhemenitiki
Uhemenitiki
ni taaluma inayohusiana na uelewaji na kutafsiri matini. Chimbuko la
nadharia hii ni katika uchambuzi wa falsafa katika matini za kidini,
hususani dini ya Kikristo. Waasisi wanaohusishwa na chimbuko la nadharia
hii ni kama vile Friedrich Schleiermacher (1768-1834),Wilhem Dilthey
(1833-1911) na Martin Heidegger (1889-1976).
Msingi
mkubwa wa nadharia ya Uhemenitiki ni imani ya kwamba matendo ya
binadamu yanaathiriwa kwa njia mbalimbali na asasi tofauti zilizoko
katika mazingira yake. Msingi huo unatupeleka katika dhana ya kuibua
umuhimu wa kuelewa njia au mbinu za uelewaji wa maana za matini. Madai
ya msingi ya nadharia ya Uhemenitiki yanahusisha dhana mbalimbali kama
vile duara la kihemenitiki, utukuzaji pamoja na ile ya ufufuaji wa kisarufi, kisaikolojia na kimuktadha (Senkoro, 1987; Wamitila, 2002 katika Ponera, 2010).
Akizungumzia suala la Mviringo au Duara la Kihemenitiki, Senkoro (1989:9) anasema:
“…katika
usomaji kuna mviringo wa kihemenitikiambao humfanya msomaji aende mbele
na nyuma, kushoto na kulia mwa yale yaongelewayo katika kaziya
fasihi.Hadhira huwa wanabashiri na kuhusisha mambowanayoyapitia maishani
mwao”.
Kulingana
na nadharia hii ya Uhemenitiki huwa kuna ugumu wa kuwepo kwa uwiano
kati ya malengo na maana asilia ya mtunzi dhidi ya uelewaji wa maana
aipatayo msomaji. Uelewaji wa maana kwa msomaji huhusisha kuyajua mambo
mbalimbali yaliyomzunguka mtunzi wakati au kabla ya kuitunga kazi
husika. Ni vigumu kuelewa malengo na maana asilia ya mtunzi iwapo
msomaji au mhakiki hatahusisha mambo hayo. Kwa kufanya hivyo, ndipo
msomaji atakuwa amelitalii duara la kihemenitiki. (Ponera, 2010).
Dhana ya Utukuzaji katika
nadharia ya Uhemenitiki inamaanisha jumla ya makisio mbalimbali ambayo
msomaji au mhakiki wa kazi ya fasihi huwa nayo punde aishikapo kazi
yoyote ya kifasihi. Makisio hayo hujengwa akilini mwa msomaji kulingana
na misingi mbalimbali kama vile anwani yake (jina na picha ya kitabu),
kiwango cha usomi, utamaduni, upeo wa uelewa, pamoja na ulinganisho wa
kazi zozote zilizotungwa na watunzi wengine zinazofanana na hiyo
(Wamitila, 2002).
Wamitila (2002:193) anafafanua kuwa dhana ya Ufufuaji, hususani
ule wa kisaikilojia iliasisiwa na Dilthey (1833-1911). Alisisitiza
kuwa kuna umuhimu mkubwa kwa msomaji au mhakiki kufufua muktadha asilia
wa kazi inayohusika na kujaribu kujiweka katika muktadha huo ili aweze
kuipata maana asilia ya matini. Kwa mujibu wa mawazo yake, kazi
mbalimbali za kifasihi zinaweza kuwa na maana mbalimbali kwa wasomaji
mbalimbali. Aidha, dhana ya ufufuaji inasisitiza kuwa ili kuielewa na
kuitafsiri maana ya matini lazima msomaji au mhakiki azame katika
kuuelewa mtindo. Hapa neno ‘mtindo’ limetumika kumaanisha muktadha wote
wa mfumo wa maneno na sentensi zilizotumika katika matini.
Dhana hizi
zinazobeba madai ya msingi ya nadharia ya Uhemenitiki zinahusiana kwa
kiasi kikubwa. Gadamer (1960) ambaye amenukuliwa na Senkoro, (1987:7)
anasema:
“Taaluma ya Uhemenitiki hujihusisha na utafutaji wa maana ya kazi ya fasihi
kwa kuuliza maswali muhimu manne:
i. Ni nini maana ya fasihi?
ii. Je, maana hii inahusianaje na kusudi la mwandishi?
iii. Je, tunaweza kuzielewa kazi za fasihi za tamaduni na historia tofauti na zetu?
iv. Je, ni rahisi kupata uelewaji wa ndani wa kazi ya fasihi au huu hutegemea
mazingira na historia ya hadhira ihusikayo?”.
Kuyajibu maswali haya kulihusisha kwa pamoja dhana za Duara la Kihemenitiki, Ufufuaji na Utukuzaji ambazo
zinaunda madai ya msingi ya nadharia hii. Misingi ya nadharia hii
ilitumika katika kuendesha utafiti uliofanywa unaohusu vipengele vya
msingi vya kiufafanuzi. Misingi hiyo ni ile iliyomo katika dhana tatu
muhimu zilizomo katika nadharia hii ambazo ni Duara la Kihemenitiki,
Ufufuaji na Utukuzaji.
Hivyo,
taswira zinazojitokeza katika ushairi wa Kaluta Amri Abedi
zilichunguzwa kwa kuhusianishwa na vipengele vingine vya kimaisha kama
vile matukio ya kihistoria yaliyojiri kabla au wakati wa utunzi, tabia
na mwenendo halisi wa Sheikh Kaluta Amri Abedi mwenyewe, hali halisi ya
maisha tangu kipindi cha baada ya kazi husika kutungwa hadi sasa, na
jiografia ya alipokuwa mtunzi (duara la Kihemenitiki). Aidha, uchunguzi
ulihusisha fikra binafsi za mtafiti kuhusiana na lugha na taswira
mbalimbali zijitokezazo katika Diwani ya Amri (Utukuzaji).
Vilevile uchambuzi wa data ulizingatia mtindo mahsusi ambao Kaluta Amri
Abedi aliutumia katika utunzi kwa kuulinganisha na matumizi ya lugha ya
wakati huo (Ufufuaji).