KIJALIZO.
KIJALIZO.
Kijalizo ni kipashio kinachokamilisha/kinachojaliza kipashio kingine katika tungo.
Massamba (2004:33), anaeleza kijalizo huwa ni kiambajengo muhimu cha sentensi au kishazi
ambacho katika sarufi za kimapokeo kimechukuliwa kuwa na kazi ya kukamilisha maelezo
yaelekezwayo na kitenzi kwa mfano: Jamila amepika ugali. Ugali ni kijalizo kwa sababu
inakamilisha kitenzi ‘pika’.
Kijalizo ni istilahi inayotumiwa kurejelea uamilifu wa kisarufi jinsi ambavyo kiima
kinadhihirisha uamilifu fulani wa kisarufi. Kijalizo ni neno au fungu la maneno lenye
kuunganishwa moja kwa moja na kichwa cha kirai (dada ya kichwa cha kirai). Hupanua
kichwa cha kirai hadi kiwango tofauti.TY . Radford (2004:329)
Kila kiarifu huwa na kitenzi. Hata hivyo baadhi ya viarifu huhitaji zaidi ya kitenzi
kukamilisha sentensi. Baadhi ya maneno ambayo huhitajika kukamilisha sentensi yaliitwa
yambwa kimapokeo lakini katika Umilikifu na Masharti yakaitwa kijalizo. Yambwa kwa
hivyo pia hufanya kazi ya kijalizo. Yaani kukamilisha kitenzi. Kwa mfano:
Sara alimwandikia Yurabibarua.
Kuna aina tofauti za kijalizo kama vile kijalizo cha kiima, kijalizo cha kivumishi, kijalizo cha
yambwa, kijalizo cha kihusishi, kijalizo cha nomino na kijalizo cha kitenzi.
Aina hizi za kijalizo zitafafanuliwa baadaye katika sura ya tatu.
HITIMISHO
Katika sura hii, tumeweka wazi dhana ambazo tutatumia katika utafiti wetu. Tumefafanua
dhana ya sintaksia, virai kama vile: kirai nomino, kirai tenzi, kirai vumishi, kirai elezi na kirai
husishi. Tulipambanua pia miundo tofauti ya virai. Tulifafanua vishazi na aina zake tofauti
kama vile vishazi huru na vishazi tegemezi.Tulieleza kategoria amilifu za maneno kama vile:
kijalizo, yambwa, chagizo, kiarifa na kiima.
MIUNDO NA AINA ZA VIJALIZO.
UTANGULIZI.
Katika sura ya pili, tulijadili dhana tofauti ambazo tutatumia katika utafiti wetu. Tumefafanua
dhana ya sintaksia kwamba ni mojawapo ya ngazi za isimu iliyo kati ya mofolojia na
semantiki na huchunguza muundo wa sentensi ya lugha na viambajengo vyake kama vile
mofu, maneno, virai na vishazi. Dhana zingine tulizojadili ni pamoja na: virai, vishazi na
kategoria amilifu za maneno kama vile kiima, kiarifu, chagizo, na kijalizo. Katika sura hii,
tutafafanua miundo tofauti ya kijalizo na aina zake tofauti kwa mujibu wa nadharia ya X-baa.
Kijalizo ni kipashio kinachokamilisha kipashio kingine katika tungo. Mitazamo tofauti ya
kijalizo yako katika 1.4. Kijalizo hutokea katika miundo tofauti. Kinaweza kutokea kama
neno, kirai au kishazi. Kinaweza kuwa nomino au kirai nomino, kitenzi au kirai tenzi,
kihusishi au kirai husishi, kivumishi au kirai vumishi, kielezi au kirai elezi.
Katika Kiswahili, vichwa vya virai hutangulia vijalizo vyake. Kwa sababu hii, Kiswahili ni
lugha ya kichwa – kwanza. Radford (2004:15) Lugha kama vile Kikorea haitangulizi kichwa
bali kijalizo hutangulia kisha kichwa lakini lugha ya Kiingereza inafanana na ya Kiswahili
(kichwa kwanza kisha kijalizo baadaye). Kwa mfano:
Kiswahili: Funga huo mlango.
Kiingereza: Close that door.
Kikorea: Muneul dadara.
Door close
Radford (2004:15)
49
Maneno yaliyokolezwa rangi ni vijalizo.